Deodatus Balile
NIKIWA na matumaini chungu wa tele kuwa mpendwa msomaji wangu hujambo, leo nimeona ni vyema nitupie macho sekta mpya inayoibukia hapo nchini kwetu, ambayo kimsingi ni fursa na ufunguo wa kukuza uchumi wetu.
Sekta hii ni tawi jipya la huduma katika usuluhishi wa migogoro (conflict resolution).
Nikijaribu kuangaza katika mitandao mbalimbali, kwa sasa jina la Tanzania linakuja juu kwa kiwango cha kutisha katika sekta hii ya usuluhishi wa migogoro. Yapo mataifa magwiji kama Uswisi, yenye kuaminika kuwa ni eneo salama kwa mazungumzo na mikataba mizito, na ndiyo maana leo ukiangalia mikutano inayofanyika Geneva, Uswisi, ni mingi kuliko maelezo.
Geneva imekuwa nyumbani kwa mikataba mingi ya kimataifa, kuanzia sekta ya diplomasia, uchumi (ikiwamo Shirika la Biashara la Kimataifa – WTO), biashara na usuluhishi. Kwa bahati mbaya nchi hii haina maliasili kwa kiwango kikubwa. Viongozi wa taifa hili walilifahamu hilo na kuamua kuwekeza katika huduma. Uchumi wa Uswisi unategemea au unajiendesha kutokana na mapato yatokanayo na sekta huduma kwa asilimia 98.
Taifa hili lina benki kubwa na zenye fedha nyingi kuliko mataifa karibu yote duniani na lilijiingiza katika biashara ya usiri wa kumbukumbu za fedha, ambapo viongozi wengi wa dunia hii hupora fedha katika mataifa yao na kuzihifadhi Uswisi. Nieleweke hapa, sisemi kuhifadhi fedha za wahalifu ni mchezo mzuri, lakini nataka kujenga hoja yenye kuonyesha walivyojipanga kuhakikisha sekta ya huduma inakuwa nguzo ya uchumi wao.
Taifa kama Uingereza ambalo ni visiwa vidogo vyenye ukubwa sawa na mkoa kama wa Morogoro vikichanganywa, lina uchumi mkubwa ajabu. Taifa hili la Uingereza limewekeza katika sekta ya huduma. Kama Uswisi, nao mikataba mikubwa mingi hutiwa saini hapa. Leo ukitafuta kampuni kubwa 10 za masuala ya uhasibu, zote zina makao makuu hapa London.
Kati ya kampuni 10 kubwa za masuala ya kisheria duniani, 6 zipo hapa Uingereza, tatu zipo Marekani na moja ina makao makuu ya umiliki wake Uholanzi na Uingereza (kwa wakati mmoja).
Hali ni hivyo katika uhandisi, ugavi, mawasiliano na sekta nyingine nyingi. Waingereza wamejielekeza katika huduma. Kwa Marekani shughuli kama hizo zinazohusu mikutano mbalimbali ya kimataifa na huduma nyingine zikiwamo za kifedha, kisheria na fani nyingine, zinaendesha uchumi wa taifa hilo kwa asilimia 63 sasa.
Mataifa haya sasa yanafunga viwanda na kuvihamishia India na China, huku yenyewe yakibaki kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa.
Nimeyasema haya, yanisaidie kujenga hoja juu ya fursa tuliyonayo Watanzania katika usuluhishi wa migogoro ya kimataifa. Kazi anayoifanya Dk. Salim Ahmed Salim, ya kusuluhisha mgogoro wa Darfur, nchini Sudan, inalitangaza taifa letu kwa kiwango cha ajabu.
Habari nyingi zinazochapishwa zinaitaja Arusha kama kituo cha usuluhishi wa migogoro kilichobobea, ambapo wanarejea mgogoro wa Burundi na Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari iliyopo Arusha. Leo mataifa mbalimbali yameanza kuamini kuwa ikiwa Afrika Kusini, inayoonekana kuwa mshindani mkubwa wa Tanzania katika sekta hii ya usuluhishi ikishindwa kusuluhisha mgogoro wa Zimbabwe, basi ikabidhiwe Tanzania, itauweza.
Imani hii kwa taifa letu, ni nguzo kubwa na chimbuko la maendeleo. Kwa nchi zinazotokea kupata fursa kama hizo, huo ndiyo mwanzo wa kutimua vumbi kuelekea mji wa maendeleo.
Najua yapo mataifa mengi yangependa kupata fursa hii ila kutokana na misingi fasaha aliyoijenga muasisi wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, taifa letu linayo fursa ya ziada; amani, utulivu na utengamano wa kisiasa.
Kimsingi kazi ya usuluhishi wa migogoro ni biashara kubwa. Nasema ni biashara kwa misingi kuwa watu wetu watakaokuwa wanafanya kazi katika mabaraza au mahakama za usuluhishi, ni wazi watakuwa hawajitolei. Hawa watakuwa wanalipwa, kumbi za mikutano na hoteli wanapolala wahusika wakati wa mikutano vinalipiwa, bila kutaja chakula na matumizi ya ziada wanayofanya washiriki wa mikutano hii wanapokuwa hapo nchini.
Hata hivyo, lipo jambo moja linalonitia wasiwasi kwa sasa. Jambo hili ni umahiri wa watu wetu hasa katika fani hii ya usuluhishi wa migogoro.
Kipo kizazi kilichofanya kazi Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa miongo kadhaa na kupitia uzoefu au shule walizopata wakapata utalaamu unaotumika kushawishi na hatimaye kutatua migogoro hii.
Kinachonitia wasiwasi na kunilazimu kumtahadharisha waziri mwenye dhamana ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, kuwa fursa hii tunaweza kuipoteza sioni mipango thabiti ya kuandaa vijana wapya wa kuendeleza taaluma hii ya usuluhishi. Conflict Resolution ni fani maalumu inayokuja juu kwa kasi kubwa duniani na watu wanaisomea kuanzia shahada ya kwanza hadi ya uzamivu, ila sijaona mpango-mkakati wa kuhakikisha Tanzania inakuwa na wataalamu wa kutosha katika nyanja hii.
Kwa kuwa wizara hii iliyopo chini ya Membe inayo dhamana ya usuluhishi wa migogoro, nimsihi aliangalie suala hili na kujaribu kutafuta hata vyanzo mbadala vya mapato, vijana wetu wanaoibukia wenye umri wa miaka 19 hadi 30, wapelekwe shule katika fani hii tuwe na wataalamu wa kutosha.
Napendekeza umri huu kwa sababu hawa wakipata utalaamu kwa umri wao wataweza kulitumikia taifa kwa miaka 30 na zaidi, badala ya kupeleka shule kwa kiwango cha uzamivu mtu mwenye miaka 48, akirejea kutoka masomoni anatumikia miaka minne anastaafu kwa hiari au anaongeza miaka mitano na kulazimika kustaafu kwa mujibu wa sheria.
Itakuwa ni aibu kwa taifa letu kuwa na sifa ya usuluhishi wa migogoro, lakini watendaji wa mabaraza au mahakama husika wanatoka mataifa mengine na hakuna Watanzania wenye kufanya kazi hii.
Chonde chonde Membe lifikirie hili, na ikiwezekana ulitafutie ufumbuzi. Tukisuasua, fursa hii tutaipoteza. Mungu Ibariki Tanzania.
deobalile@yahoo.com – 0007904159144