Raia wawili wa China wajenga makazi kwa wasichana 29 katika uwanda wa Maasai mara nchini Kenya

Raia wawili wa China wajenga makazi kwa wasichana 29 katika uwanda wa Maasai mara nchini Kenya

ldleo

JF-Expert Member
Joined
Jan 9, 2010
Posts
1,310
Reaction score
1,265
640.png


China na nchi za Afrika zimekuwa na ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara na uchumi, kilimo, afya, ujenzi wa miradi mikubwa ya miundombinu, na elimu. Pia pande hizo mbili zimekuwa na urafiki wa jadi uliodumu kwa miongo kadhaa, ambao bado unaendelea kuimarika kupitia njia za jadi za kidiplomasia lakini pia kwa mawasiliano ya watu na watu.

Karibu kila wikiendi, raia wawili kutoka China, Tang Lin na Yuan Lin wanakwenda kwenye uwanda wa Maasai Mara, gari lao likiwa limesheheni vitu kadhaa ikiwemo viatu, nguo, vitafunwa, na mahitaji ya lazima ya kila siku, na vyote hivyo vinapelekwa kwa wasichana 29 walio chini ya uangalizi wao.

Tang na Yuan wanaotokea manispaa ya Chongqing, kusini magharibi mwa China, kwa mara ya kwanza walikwenda nchini Kenya kutafuta kazi katika sekta ya utalii. Baada ya watalii kutoka China kuongezeka nchini Kenya, biashara yao ilishamiri sana, na mwaka 2019, walichukua hatua ya kununua hoteli ya kiikolojia huko Maasai Mara. Kile kilichoanza kama hatua ya ujasiriamali baada ya muda mfupi kilishamiri na kuwa jukumu lisilotarajiwa la hisani.

Muda mfupi baada ya kufungua hoteli yao, mwanamke mmoja wa huko aitwaye Mary Silantoi alitaka kuongea nao. Akijitolea katika idara ya masuala ya wanawake na watoto katika Kaunti hiyo, Silantoa aliokoa wasichana kadhaa waliokimbia makwao kutokana na ndoa za mapema na ukeketaji. Hivyo alitaka kukutana na raia hao wa China akitaka wampe sehemu ya kufungua duka dogo katika hoteli hiyo kusaidia kuwapatia wasichana hao mahitaji yao. Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na serikali ya huko, wasichana wenye miaka 10 hadi 19 wanachukua karibu asilimia 30 ya wanawake wajawazito kwenye eneo hilo. Wengi wao, ambao na wenyewe bado ni watoto, wameozwa na wazazi wao kwa mahari ya ng’ombe kadhaa.

Tang, mwenye umri wa miaka 48, anasema yeye pia ana mtoto wa kike, na alipoona watoto wanakimbia pekupeku na kujua kuwa wengi wao hawaendi shule, alishindwa kupuuzia jambo hilo, huku Yuan akisema, kwa sababu wakazi wa huko waliwasaidia kuanzisha biashara yao, nao waliamua kufanya jambo la kusaidia jamii hiyo. Wachina hao waliamua sio tu kumsaidia Silantoi kuendesha duka lake, bali pia walisaidia kutengeneza nyumba salama na ya kudumu kwa wasichana hao. Uamuzi huo ulipeleka kufunguliwa kwa Namunyak, shirika la kijamii linalolenga kuwalinda watoto wa kike walio hatarini. Juni, 2023, Tang na Yuan walinunua ekari 15 za ardhi karibu na mji wa Aitong, huko Narok, na kujenga kile ambacho sasa kinajulikana kama Kituo cha Uokoaji cha Namunyak. Ingawa ni kidogo, kituo hicho kimempa Silantoi na wasichana anaowahudumia sehemu ambayo wanaweza kuita ni ya kwao.

Katika miaka miwili iliyopita, Tang na Yuan wamekarabati nyumba hiyo, wameweka umeme na mnara wa maji, wanawalipia ada, na kuajiri walinzi pamoja na wahudumu. Karibu na kituo hicho, kuna darasa jipya lililojengwa, jiko, na vyoo, pamoja na nyumba tatu za nyasi za jadi zinazotumika kama ofisi na makazi ya Silantoi. Mama huyo mwenye umri wa miaka 56, anasema waswichana hao wamepitia mambo magumu katika maisha yao, lakini sasa wanajiamini, wana utashi na matumaini makubwa.

Kati ya wasichana wanaoishi hapo, ni Mitchell Ketere, mwenye umri wa miaka 13, ambaye alijiunga na Namunyak miaka miwili iliyopita baada ya kifo cha baba yake kuiacha familia katika matatizo. Akiwa na tabasamu kubwa, Mitchell anasema anapenda kuwa mpishi katika siku za baadaye, kwani anapenda sana kuwapikia wengine.

Kwa Tang na Yuan, safari yao nchini Kenya ni zaidi ya hisani, kwani wamejenga biashara huko, lakini pia wamejenga familia, na kuongeza kuwa, kila binti, awe nchini Kenya ama China, anaweza kuishi maisha mazuri.

Mwezi Machi, 2024, serikali ya huko ilisajili rasmi Namunyak kama shirika la kijamii, ikitambua mchango wake katika ustawi wa jamii.

Katika uwanda mpana wa Maasai Mara, ambako wanyamapori wanatembea kwa uhuru, wanaume wawili kutoka China wamepanda mbegu ya matumaini, na kwa wasichana 29 wa Namunyak, furaha sio neno tu, bali ni nyumbani.
 
Back
Top Bottom