Kuna mambo ambayo nadhani ni muhimu Taifa likaweka mbele katika agenda zake za maendeleo, kuanzia sasa. Kati ya mambo hayo kilimo ndio jambo kuu.
Baada ya mtikisiko wa uchumi duaniani (GFC), nchi nyingi za ulaya na marekani zimetambua kuwa Afrika inaweza kuwa mshiriki mkubwa katika kuweka maslahi yao salama zaidi. Imedhihirika hivyo kwa kuwa, waliokuwa wamewekeza Afrika, pesa zao na vitega uchumi vingine vimekuwa salama zaidi kuliko walikuwa wamewekeza ulaya, Asia na Marekani. Hii inatokana na Afrika kutokuwa na misukosuko mingi au harakati nyingi za kiuchumi kulinganisha na nchi zilizoendelea.
Katika wakati huu, nchi itakayowekeza kwenye kilimo ndio itakayonufaika zaidi. Maana dunia nzima inahitaji chakula kutokana na hali mbaya ya hewa na uchumi wa dunia kutikisika. Tanzania ina nafasi muhimu sana katika hili kwa kuwa ina ardhi nzuri na imezungukwa na maji mengi (maziwa, mito na hata bahari) kila upande. Maji Tanzania yako mengi hata chini ya ardhi.
Wawekezaji wengi watajitokeza na kuitaka serikali iwape nafasi ya kuwekeza kwenye kilimo hapa ila kwa masharti ya kumilikishwa ardhi na si kukodisha kutoka serikalini. Hii inaweza ikabadili sheria za ardhi na kuwa mwenye ardhi anaimiliki moja kwa moja (100%). Wawekezaji hutumia upungufu huu kukwepa kuwekeza nchini, na serikali haitaweza kuacha hali hiyo iendelee kwa muda mrefu. Pressure ni kubwa sana.
Kwa mtazamo wangu, mwekezaji yeyote mwenye nia ya kuwekeza kwenye kilimo hapa nchini ni vyema akapewa nafasi ya kufanya hivyo bila kujali ametoka wapi na soko lake liko wapi. Ili mradi tu analipa kodi zinazotakiwa na uzalishaji wake unaipa nchi tija bila kuvunja uhuru wa mTanzania (bila kutufanya watumwa).
Inabidi waTanzania waanze kuamka sasa na kuona umuhimu wa ardhi. Nakumbuka alipokuwa anawasilisha bajeti ya wizara yake ya mwisho mwaka 2005, Keenja alisisitiza sana hili hasa akijua kuwa wawekezaji wanatamani kuja nchini kuwekeza kwenye kilimo na serikali imeanza kufikiria kuwakaribisha. Wakija wawekezaji hao, watachukua ardhi kubwa sana, hivyo kuna hatari kuwa baadhi ya watu wakakosa ardhi baada ya miaka kadhaa. Inabidi kuwa aggressive sana kujitwalia ardhi mapema.