Rais Kikwete atengua uteuzi wa DC wa Kishapu
Na Julius Sazia, Shinyanga
Source: Mwananchi
RAIS Jakaya Kikwete ametengua uteuzi wa Mkuu mpya wa Wilaya ya Kishapu, Anatory Choya muda mfupi baada ya kumtangaza na badala yake akamteua mwingine, Abdul Suleiman Lutavi.
Habari zilizopatikana zinaeleza kutenguliwa kwa uteuzi wa Choya ambaye ni mbunge wa zamani wa Biharamulo Magharibi mkoani Kagera, kutokana na kukamatwa na Takukuru na kufunguliwa kesi ya kutoa rushwa wakati wa uchaguzi wa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Biharamulo mwaka jana, nafasi ambayo alishinda.
Kesi yake namba 270 ya mwaka 2008 inaendelea katika Mahakama ya Wilaya ya Biharamulo na wiki iliyopita, Aprili 17 mwaka huu ilitajwa na inatarajiwa kutajwa tena Mei 11 mwaka huu.
Jumatatu wiki hii wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Shinyanga, pamoja na wananchi waliohudhuria hafla ya kuapishwa kwake walipigwa na butwaa baada ya kushuhudia akiapishwa Lutavi badala ya Choya.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Brigedia Jenerali Dk Yohana Balele alimwapisha Lutavi na kuwafanya watu kuhoji kimya kimya nini kilichofanya Choya kushindwa kuapishwa na hakuna maelezo yaliyotolewa.
Hata hivyo, taarifa zilizopatikana baadaye zinaeleza kuwa Rais Jakaya Kikwete, alitengua uteuzi wa Choya kutokana na taarifa zilizoifikia ikulu kuwa Choya, anakabiliwa na kesi ya rushwa mahakamani.
Afisa Tawala wa Wilaya ya Kishapu, Jonathan Simkoko alipohojiwa na Mwananchi Jumapili alidai mara baada ya uteuzi huo, ofisi yake ilifanya maandalizi yote ya kumpokea mkuu mpya wa wilaya kwa kumtuma dereva wa halmashauri hiyo kumfuata Choya na familia yake wilayani Biharamulo kwa ajili ya kuapishwa.
Alisema wakati Choya na familia yake wakiwa njiani kuelekea Shinyanga walipofika katika Kijiji cha Tinde mkoani Shinyanga, mkuu huyo alipokea simu kutoka ikulu ikimuarifu asiripoti kwanza kwenye kituo chake kipya na badala yake aende mara moja jijini Dar es salaam ikulu kwa maelekezo zaidi. Simkoko alisema walichokifanya ni kumpeleka moja kwa moja uwanja wa ndege wa Mwanza kwa ajili ya safari ya ghafla ya kuelekea Dar es Salaam.
Alisema waliamua kuitafutia hoteli familia akiwamo mkewe, kaka yake na mtoto wao mmoja mjini Shinyanga kumsubiri hadi atakaporejea kutoka jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Simkoko, Choya aliporejea kutoka Dar es Salaam, alifuatwa na gari la wilaya Uwanja wa Ndege Mwanza na kuwaeleza walioompokea kuwa, 'mambo yameshaharibika'.
Baada ya hapo wakamsafirisha hadi Shinyanga kuungana na familia yake ambayo ilikuwa imeshakaa hotelini kwa siku tatu.
Mwenyekiti huyo wa CCM wilaya ya Biharamulo na familia yake walisafirishwa kwa njia ya barabara kupitia Kahama kurejea wilayani kwake. Mwananchi Jumapili lilipowasiliana na Choya, alikiri kuwa ni kweli alisimamishwa kuripoti kwenye kituo kipya cha kazi lakini akabainisha kuwa hadi jana, alikuwa hajui sababu zilizosababisha mabadiliko hayo ya ghafla.
"Kwa sasa (jana jioni) niko njiani naenda Dar es Salaam ili kujua sababu zilizosababisha hali hiyo," alisema Choya alipokuwa akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu.
Alisema kuwa alipata taarifa hizo akiwa safarini pamoja na familia yake kwenda Kishapu lakini baada ya kueleza, ilibidi airejeshe familia yake nyumbani. Kuhusu kukabiliwa na kesi ya rushwa, Choya alikiri lakini akasema ni vigumu kutoa maelezo juu ya kesi hiyo kwa njia ya simu na isitoshe alikuwa kwenye basi. Baadhi ya wananchi waliohojiwa na gazeti hili, wamesema kuwa wateule wa rais ngazi za wilaya na mkoa wawe wanaziacha familia zao nyumbani hadi pale wanapoapishwa ndipo wanasherehekea kwa vile wakati wowote rais anaweza kutengua uteuzi huo na kuleta tafrani katika familia.
Wakati wa kuapishwa kwa Lutavi, Dk Balele aliahidi kutoa ushirikiano wa karibu kwa mkuu huyo katika kusukuma gurudumu la maendeleo mkoani Shinyanga hasa katika sekta ya elimu, afya, kilimo na mifugo ambazo alidai bado ziko nyuma. Kwa upande wake, DC Lutavi, aliomba ushirikiano wa karibu kati ya viongozi na wananchi katika kufanikisha shughuli za maendeleo katika Wilaya ya Kishapu ambayo inakabiliwa na umaskini licha ya kuwepo mgodi pekee nchini wa almasi wa Mwadui.
Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Celina Kombani aliithibitisha jana kutokea kwa mabadiliko hayo ya uteuzi na kwamba hilo limefanyika kutokana na mamlaka ya Rais ya kuteua na kubatilisha wakati wowote. Hata hivyo, alisema ofisi yake haina taarifa za sababu zilizomfanya rais kutegeua uteuzi wa Choya. Juhudi za kuwasiliana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, hazikuzaa matunda jana kuzungumzia suala hilo.
Machi 27 mwaka huu Rais Jakaya Kikwete alifanya mabadiliko ya wakuu wa wilaya nchini na kuwastaafisha saba, akiwamo Choya, kuwateua wapya 15 na kuwabadilisha vituo vya kazi 54.
Aliyekuwa DC wa Kishapu kabla ya mabadiliko hayo, Khadija Nyembo, alihamishiwa wilaya ya Chato mkoani Kagera.
Choya aliyekuwa mbunge kwa kipindi kimoja (2000-2005) shindwa ubunge katika uchaguzi wa mwaka 2005 na kufungua kesi mahakamani kupinga ushindi wa hayati Phares Kabuye (TLP) na matokeo yake kutenguliwa miezi 20 baada ya uchaguzi huo baada ya mahakama kuridhika kuwa mdaiwa alitumia lugha ya matusi wakati wa kampeni.
Hata hivyo, Kabuye hakuridhika na hukumu hiyo alikata rufaa ambayo hadi juzi alipofariki dunia katika ajali ya Basi mkoani Morogoro, ilikuwa haijasikilizwa.