Mzee Mwanakijiji,
Kwanza Obama si Kikwete!
Obama hajatuhumiwa na hajatumia fedha chafu kugombea uraisi wa Marekani kama Kikwete na CCM walivyofanya.
Furaha ya watu Weusi, mimi nikiwa mmoja wapo ni kule kuushinda Unyonge uliojengwa ndani yetu, ule wa Nyani wa Ngabu kusema ndivyo tulivyo, unyonge wa kuonekana kuwa hatuna thamani wala uwezo wowote.
Ushindi wa Obama si kwa watu Weusi na Waafrika tuu, bali ni kwa kila mtu ambaye siku zote amelelewa na kukuwa katika mazingira yanayomwambia kuwa yeye ni batili, nusu na hana thamani.
Ushindi wa Obama ni sawa na kuvunja minyororo ya utumwa na ukoloni. Pamoja na kuwa ni kweli kuwa si yeye pekee ambaye ataongoza nchi ya Marekani, lakini kitendo cha yeye kuwashinda wale ambao siku zote wamekuwa wakidharau na kukandamiza binadamu wa rangi, dini, jinsia na aina nyingine kwa kujifanya wao ndio wateule, ni dalili tosha kuwa nyakati zinabadilika na kila tunaloambiwa haliwezekani, linawezekana.
Ushindi wa Obama naupokea kama siku Chadema, CUF, TLP au chama kingine kinaposhinda Ubunge nchini Tanzania au siku mojawapo ya Vyama hivi au kwa umoja vitaing'oa CCM kutoka madaraka ya kututawala Watanzania.
Najua una mtazamo wako wa kulia ambao ni tofauti na ule wa Obama kisera na hata labda kiimani, lakini ukweli unabakia kuwa tulishaambiwa haitawezekana, hamuwezi, sasa milango imefunguka, tumeona na kushuhudia kuwa inawezekana, tunaweza na zaidi tuna haki sawa.
Huu ni mwanzo wa mwisho wa Unyonge. Hata kama hataweza tatua matatizo yote au kuleta Maisha bora kwa kila Binadamu au Mwananchi na mkazi wa Marekani, kuweza kupata ushindi na kuwa mshindi ni tuzo ya pekee na ni tumaini na faraja ya ajabu kwa kila ambaye amedhalilishwa na kufanywa mnyonge.