Pre GE2025 Rais Samia na CCM wametimilisha msemo wa wahenga kwamba kelele za vyura kwenye dimbwi hazimzuii ng'ombe kunywa maji na ushindi ni lazima 2025

Pre GE2025 Rais Samia na CCM wametimilisha msemo wa wahenga kwamba kelele za vyura kwenye dimbwi hazimzuii ng'ombe kunywa maji na ushindi ni lazima 2025

Mijadala ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2025 (Kabla, wakati na baada)

Richard

JF-Expert Member
Joined
Oct 23, 2006
Posts
15,692
Reaction score
23,038
Kabla ya kuanza uchambuzi wangu ningependa kutoa angalizo kuwa mimi siko upande wowote ule. Naandika maoni, uchambuzi au mapendekezo yanotokana na yale tunoyaona, kusikia na pia kuyasoma katika vyombo vya habari au mitandao ya kijamii.

CCM chama tawala Tanzania tangu kuanzishwa kwake kimeshika madaraka ya kuwaongoza watanzania ambao wengi wao bado hawajapata fursa ya kubadili fikra zao.

Kumbadili fikra mwananchi ni lazima umwambie sera, mipango na mikakati ya chama tawala na serikali yake na kisha uonekane watekeleza kwa vitendo masuala hayo. Kama raisi alietoka CCM akisema ntapambana na vitendo vya rushwa na mafisadi kwelikweli na aonekane atenda jambo hilo bila uonevu hilo litakuwa ni jambo la kuungwa mkono na kila mwananchi.

Tanzania kwa bahati tu ya mtende ikapata kiongozi ambae alikuwa tayari kukidhi matarajio ya wapiga kura, akaahidi kutekeleza ilani ya chama cha CCM na akasema itakuwa ni kazi tu. Yote yalotokea tumeyashuhudia na baadhi ya mazuri alotenda kiongozi yule ambae aliitwa John Magufuli yameonekana na yapo.

Hata kama alikuja kuyatekeleza baada ya kuwekwa makabatini kwa miaka nenda rudi miradi kama ule wa umeme wa Mwalimu Julius Nyerere ni mradi ambao ni lazima uwepo nchini ili kuiwezesha nchi kuendelea kiuchumi kwa kuwa na viwanda vitavyotumia umeme huo, wananchi kupata umeme wa bei nafuu na pia kuondoa tatizo la ukosefu wa umeme ambao wababisha kuwepo kwa mgao mara kwa mara.

Tufikirie kwamba wale wanopinga mradi huo khasa wale wa nje wao wana umeme wa masaa 24 ambao haujawahi kukatika hata siku moja. Wale watanzania wenzetu wanoshirikiana nao kupinga mradhi huo wa umeme wao hawana fikra sahihi na ni wapigaji ambao wapo kulinda vikampuni vya kuuza umeme kwa Tanesco.

Sasa tujikite katika lengo halisi ya mada hii ambalo ni kuonyesha kwamba CCM chama tawala Tanzania sasa hivi kimepanga kutawala tena kwa lazima bila kujali kwamba wananchi wamependa wala hawajapenda.

Tangu nchi iondokewe na hayati John Magufuli, ni wazi kuwa CCM na nchi nzima imeyumba kuanzia uchumi kwamba shilingi ya Tanzania kulinganisha na dola au pauni ya Uingereza imeshuka sana. Bei ya fedha yetu ya madafu kwa pauni ya Uingereza ni zaidi ya 3,300 na kwa dola ni 2,600 na kwa Euro ni zaidi ya 2,700.

Katika maeneo mengine muhimu kama Afya, Elimu, Ulinzi, sera ya mambo ya nje, bado hakuna taarifa sahihi na labda mabadiliko yalotokea hivi majuzi yataweza kuweka sawa suala la taarifa za serikali kwa wananchi. Kwenye hili ntavilaumu vyombo vya habari kwa kukubali kubinywa ili viwe vyatoa tu taarifa za kusifu na kupongeza kazi za raisi Samia lakini hapohapo bila kuhoji baadhi ya masuala mapya yanoibuliwa khasa bungeni na wabunge kama Luhaga Mpina.

Lakini jambo kubwa zaidi ya haya yote ni lile la CCM kuamua kuwatumia mkuu wa mkoa wa Arusha Paul Makonda, waziri wa ardhi Jerry Silaa na mkuu wa mkoa wa Dar-es-salaam bwana Albert Chalamila kuwalaghai wananchi ambao ndo wapiga kura ili kuwaghilibu na kuwafanya wasiwe na maamuzi sahihi ifikapo siku ya kupiga kura.

Je, ni nani alipia gharama za matumizi kwa vyombo vya habari na waandishi ambao kutwa kuacha hufuatana na viongozi hawa mikoani, wilayani na katika kata mbalimbali wanozitembelea kutatua kero za wananchi?

Jambo jingine kubwa ni la jana ambapo mheshimiwa raisi Samia alikutana na waandishi wa habari kwa mazungumzo. Nilitegemea kuwa ule utakuwa ni wakati na fursa nzuri kwa waandhishi wa habari kuuliza masuali mazito kwa kiongozi wetu hususan masuali yanohusu uchumi, siasa, jamii na sera yatu ya mambo ya nje.

Lakini ukimsikiliza kwa umakini, mheshimiwa raisi amewakumbusha waandishi kuwa yeye ataka waandishi hao wamuunge mkono. Pia amewakumbusha wajibu wao wa kuandika mazuri juu ya taifa lao na kuhakikisha siri za taifa hazivuji nje.

Siku za hivi karibuni barani Ulaya kumetokea mabadiliko makubwa yalotokana na wananchi kubadili mawazo yao juu ya aina ya tawala wanoziona zikifanya mambo kinyume na matarajio yao. Katika chaguzi hizo za Ulaya katika nchi mbalimbali wananchi wenye misimamo mikali wamepewa nafasi ya kuwaondoa wabunge wao wanowawakilisha katika bunge la Ulaya kupiti sanduku la kura jambo lilopelekea raisi wa Ufaransa kuitisha uchaguzi ambao kwa maoni ya awali yaonyesha kuwa chama chake cha mlengo wa kati hadi sasa chasimama katika nafasi ya tatu nyuma ya chama natinal Rally kinoongozwa na Marine le Pen.

Kilio cha wapinzani wa raisi Macron ni kwamba nchi ina madeni makubwa na wananchi wakiwa na maisha magumu. Raisi Macron yupo akijitahidi kuwaghilibu wananchi ikiwemo kumtumia hata mchezaji mpira wa miguu Kylian Mbappe kuwashawishi wapiga kura.

Hali hii inotokea Ufaransa ndio inoelekea kutokea nchini Uingereza ambapo chama cha Labour hadi sasa chaongoza katika kura ya maoni dhidi ya chama tawala cha wahafidhina. Licha hivyo chama hiki cha wahafidhina wabunge wake wengi ambao ni matajiri wa kutupwa tayari wamejiondoa katika kinyang'anyiro cha kugombea nafasi za ubunge na wengine kutimkia katika chama cha labour na chama cha wahafidhina.

Lakini wapiga kura wengi waingereza tayari wameishafanya maamuzi akilini mwao kwamba safari hii ni lazima chama cha labour kiwe chama tawala kwa kuzingatia kuwa chama cha wahafidhina kimekuwapo madarakani kwa miaka 14 na uchumi wa nchi hiyo umedorora huku matokeo hasi ya kuondoka katika umoja wa Ulaya yakijidhihirisha.

Hali ya maisha ya wananchi wa nchi hiyo imekuwa duni huku vijana wengi wakiwa hawana ajira na uhakika wa maisha yao ya baadae ukiwa haujulikani, migomo ya mara kwa mara kutoka kwa madaktari na watumishi wa sekta ya usafiri na hali hiyo yasemwa ni kutokana na serikali kuondoa fedha nyingi katika mzunguko na pia kutumia fedha nyingi katika mgogoro wa Ukraine.

Matatizo yaliyopo Tanzania ambayo baadhi nimeyataja hapo juu yalikuwa ni mwanzo mzuri wa vyama vya upinzani kuhakikisha vyajipanga kuhakikisha vyaikabili CCM vilivyo na kuwaambia wananchi kuwa vipo tayari kuwa mbadala.

Tofati uliyopo kati ya wapiga kura wa Tanzania na wapiga kura wa Senegal ni kwamba wale wa Senegal wengi ni vijana na ndo wameamua raisi wao awe kijana ambae kwa mtazamo wao waona kuwa atawasikiliza na atawaelewa. Wakati wapiga kura wa Afrika Kusini wao wengi wana maarifa na akili ya kutambua kuwa chama cha ANC chapaswa kupisha chama cha AD au chama cha MK.

Lakini jambo ambalo wapiga kura wa Afrika Kusini wameshindwa kulitambua ni kwamba chama cha ANC kama kilivyo chama cha CCM kina mbinu nyingi za ushindi. Katika uchaguzi ulofanyika juzi Julius Malema alikuwa aenda kupata kura nyingi khasa katika majimbo kama la Kwa Zulu Natal ambako kiongozi wa MK Jacob Zuma ndo atokea. Ikumbukwe kuwa chama cha Jacob Zuma kilianzishwa mwishoni mwa mwaka 2023 na kilianza rasmi kampeni za kisiasa mwezi Disemba na miezi si zaidi ya saba chama hicho kikashiriki uchaguzi na kikashika nafasi ya tatu bungeni kikipata viti 58 bungeni.

Ikumbukwe ANC imeambulia viti 159 na chama cha Julius Malema kikipata viti 39 huku vyama vingine vidogo vya Inkatha Freedom kikiambulia viti 17 , na vingine viti 19.

Hivyo Julius Malema na chama chake cha wapigania uhuru wa kiuchumi EFF ambae aliwahi kuwa mwanachama wa ANC na akafukuzwa kawekwa kando kwa malipoi ya kumrudisha Zuma kupitia chama cha MK ili tu kuondokana na Julius Malema.

Kwahiyo kuapishwa kwa raisi Ramaphosa ni mwendelezo wa kuhakikisha wale wanotawala wakiwemo chama cha AD ambacho pia ni chama cha matajiri waendelea kushikilia rasilimali za nchi hiyo.

Matatizo ya nchi hii yote yajulikana na yaneongelewa kwa marefu, na sasa yote yazidi kudhihirishwa na kero wanokumbana nazo Paul Makonda kule Arusha na waziri wa ardhi Jerry Silaa. Isitoshe mbunge Mpina nae juzi katoa ushahidi wa jinsi viongozi waandamizi wa serikali wanavyoshiriki vitendo cha upigaji.

Kuwaita waandishi au kuwaandalia mkutano wa kuwapanga uzuri kwa ajili ya future yao na future ya wapigaji ni dalili sawia na maandalizi ya CCM kuhakikisha yashinda uchaguzi mkuu wa 2025 kwa lazima na kwa kuchakachua kura.

Kwa maana hiyo ni kwamba hata ziara za RC Makonda, Jerry Silaa na Chalamila ni za kupasha tu moto wa ushindi mkuu wa CCM pale uchaguzi utapofika. Na pia ni onyo kwa Chadema kwamba wapige tu kelele lakini kelele za vyura kwenye dimbwi hazimzuii ng'ombe kunywa maji.
 
Weka namba yako ya simu hapo mwisho. Ni ushauri tu.
 
Kuna nyakati unawaza kuwa kama vile kuzaliwa Tanzania ni laana flani hivi
 
Back
Top Bottom