Rais wa Jamhuri ya Botswana, Mokgweetsi Masisi
Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Botswana, Mokgweetsi Masisi anatarajia kuwa na ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Tanzania, kuanzia kesho Juni 10, 2021 kwa mwaliko wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Juni 9, 2021 amesema Rais Masisi atawasili nchini kesho asubuhi na baada ya hapo atakuwa na mazungumzo ya mwenyeji wake Ikulu Jijini Dar es Salaam.
"Viongozi wetu wanatarajia kuzungumzia masuala ya ushirikiano kati ya nchi zetu mbili, uhusiano wa kidiplomasia, matumizi ya lugha ya Kiswahili nchini Botswana, bishara na uchumi pamoja na namna ya kuimarisha zaidi Jumuiya ya maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc)," amesema.
Balozi Mulamula amesema Rais Masisi ataondoka nchini Ijumaa Juni 11, 2021 baada ya kutembelea kituo kimoja wapo cha biashara hapa nchini (ambacho hakukitaja).