Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
UZINDUZI WA KITABU: ‘’RAJABU IBRAHIM KIRAMA
JEMADARI WA VITA KUWA JEMADARI WA UISLAM’’
(Kirama Muro, Rajabu Kirama, Rajabu Ibrahim Kirama)
MUSLIM UNIVERSITY OF MOROGORO
(MUM)
Mzungumzaji Mwandishi wa Kitabu
Mohamed Said
8 Januari, 2021
Halikadhalika khitma hii inahudhuriwa na nduguze ambao wao walibakia katika Ukristo baadhi yao wakitokea Old Moshi na sehemu nyingine za Kilimanjaro. Baba yake Mzee Rajabu, Muro Mboyo alitafuta hifadhi na kuishi Old Moshi kwa Chief Rindi Mandara miaka mingi mwishoni mwaka miaka ya 1800. Shughuli hii imekuwa kalenda muhimu katika kijiji cha Nkuu Machame. Kisomo cha kumrehemu Mzee Rajabu na wenzake waja wema kinafanyika kila mwaka katika msikiti ambao Waislam wameupa jina ‘’Msikiti wa Mzee Rajabu.’’
Katika hawli ya mwaka wa 2019 uliposomwa wasifu wa Mzee Rajabu wajukuu zake waliguswa na historia yake kiasi wakajiuliza kwa nini historia hii isihifadhiwe katika maandishi ili isipotee? Historia ya Mzee Rajabu yote ilikuwa mikononi kwa mwanae Salim Rajabu ambae baada ya kifo cha baba yake mwaka wa 1962 yeye alikusanya nyaraka zote za baba yake akazitia ndani ya gunia na kuzihifadhi juu ya dari la nyumba yake. Nyaraka hizi sasa zina umri wa miaka 90 na zilikuwa hapo darini bila kufunguliwa kwa muda wa miaka inayokaribia 60. Nimebahatika kuwa mtafiti wa kwanza kuzipitia nyaraka hizi na hivi ndivyo nikajikuta nimehusika katika kutafiti maisha ya Mzee Rajabu na mwishowe kuandika kitabu cha maisha yake na jinsi alivyosimama kuuingiza Uislam Uchaggani mahali ambapo Uislam haukuwapo kabisa.
Maisha ya Mzee Rajabu na historia yake ya kuuingiza Uislam Uchaggani ni kilele katika historia ndefu ya ukoo wake wa Nkya. Historia ya ukoo huu inakwenda nyuma kiasi cha miaka 200 na zaidi na imehifadhiwa kwenye vichwa kama simulizi ikipokelewa kutoka kizazi kimoja hadi kingine hadi kufikia miaka ya 1800. Historia ya kipindi hiki cha Wamishionari walipoanza kuingia Tanganyika na kufika Uchaggani kulifuatiwa na Tanganyika kuwa koloni la Wajerumani. Historia hii ya ukoloni imeandikwa na wenyewe Wajerumani kwa yale ambayo wao waliona ndiyo muhimu kwao. Mengi katika historia hii yakiwa ni shughuli za Wamishionari, uvumbuzi, kueneza Injili kwa Wachagga na vita vilivyopiganwa baina ya Wajerumani na Wachagga.
Historia inayowahusu Wachagga wenyewe na watawala waliojulikana kama Mangi, historia hii haikupatwa kuandikwa si na Wajerumani au Wachagga wenyewe. Lakini hii haina maana kuwa historia hii haikuwapo. Ilikuwapo historia hii na ukoo wa Nkya wanayo historia ambayo ilihifadhiwa kutoka kizazi hadi kizazi ikihadithiwa ndani yao kizazi kimoja kikirithisha simulizi hii kizazi kingine hadi kuingia kwa karne hii ya 21 na kuandikwa na kuwa kitabu.
Mzee Rajabu hakupata kuwa Mkristo alitokea katika Upagani akaingia Uislam yeye na watoto wake wote. Baada ya kusilimu mwaka wa 1930 alianza taratibu za kujenga msikiti. Mzee Rajabu kama alivyokuja kufahamika aliingia Uislam baada ya kukutana na Shariff Muhsin kutoka Mombasa alipokwenda Moshi na kufika Machame kwa shughuli za tabligh. Wakati huo Mzee Rajabu tayari alikuwa na watoto wanane mkubwa akiwa Salim Rajabu ambae alishirikiananae katika ujenzi wa huu msikiti na shule na kwa kila kila jambo lililohusu Uislam. Paliponyanyuka nyayo ya Mzee Rajabu Salim mwanae alikanyaga ardhi hiyo. Pamoja nao walikuwa Waislam wa mwanzo wa kijiji cha Nkuu Machame na vijiji vingine vya jirani kama Lyamungo, Masama, Mudio, Kibosho, Mkoanju na Uswaa. Msikiti huu sasa unakimbilia umri wa miaka 100 na katika kiwanja cha msikiti huu kuna shule (Muslim School) aliyojenga Rajabu Ibrahim Kirama ambayo hadi leo ipo ingawa sasa iko katika mikono ya serkali.
Salim Rajabu alikuwa mtoto mwema kwa baba yake na kwa Waislam wa Machame akaja kuwa mfanyabiashara mkubwa wa nyama akafahamika kwingi Uchaggani. Mbali na sifa hii Allah alimjaalia Salim nguvu akiweza peke yake kumwangusha ng’ombe chini kuchinjwa kwa ajili ya biashara yake ya nyama. Dua kubwa ambayo baba yake aliyokuwa akimuombea ni kuwa Allah ampungizie Salim zile nguvu zisije zikawaumiza binadamu wenzake. Katika hali kama hii Salim akiwa kijana mdogo akawa nguzo ya baba yake na fedha alizopata katika biashara mkono wake ukawa wazi kwa Waislam na Uislam.
Nilipoanza utafiti nilifahamishwa kuwa historia hii kwa kizazi kilichopo imehifadhiwa na mtoto wa Mzee Rajabu, Bi. Hawa bint Rajabu maarufu kwa jina la Mama Ali, Ali likiwa jina la mwanae. Msingi wa kitabu hiki ni simulizi ambayo nimeipata kutoka kwa Mama Ali ambae anafikia umri wa miaka 85. Mama Ali ni mjukuu wa Mangi Ngamini Ndesaruo Mamkinga kwa kikeni kwake. Mangi Ndeseruo Mamkinga alitawala Machame kutoka mwaka wa 1855 – 1880. Mama Ali kiumeni ni mjukuu wa Muro Mboyo, baba yake Mzee Rajabu aliyekuwa Jemadari wa Vita wa Mangi wa Ndeseruo Mamkinga.
Huu ndiyo uhusiano wa Mama Ali katika koo hizi mbili kubwa zilizotawala Machame kabla ya ukoloni. Mama Ali kwa upande wa kikeni kwake ni ukoo wa Shangali. Chief Abdiel Shangali aliyeshika utawala wakati wa ukoloni wa Waingereza ni kilembwe cha Mangi Ndeseruo Mamkinga. Utawala wa Waingereza baada ya kuondoka Wajerumani Chief Abdiel Shangali alichagulikuwa kama Mwafrika wa kwanza Tanganyika kuwa Mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria (LEGICO) mwaka wa 1945. Abdiel Shangali alitawala Machame hadi uchifu ulipofutwa baada ya uhuru wa Tanganyika mwaka wa 1961. Mama Ali kwa ufupi ni mjukuu wa Mangi Ngamini kikeni kwake akiwa mtoto wa Bi. Ngumbe Ngamini na kiumeni kwake ni mtoto wa Rajabu Ibrahim Kirama. Hii ndiyo silsila ya Mama Ali.
Katika mazungumzo yetu Mama Ali alinieleza mgogoro mkubwa uliotokea kati ya babu yake, Muro Mboyo Jemedari wa Vita na Mangi Ndeseruo Mamkinga. Mgogoro ulihusu urithi wa nafasi ya Mangi kati ya wanae watatu, babu mzaa mama yake, Ngamini na nduguze Ngulelo na Shangali Ndeseruo. Mama Ali anasema mgogoro huu ulisababisha Mangi Ndeseruo Mamkinga kutoa amri ya kuuliwa Ngamini ili asirithi kiti cha baba yake. Mtekelezaji wa amri hii alikuwa babu mzaa baba yake Mkuu wa Vita Muro Mboyo. Muro Mboyo alikataa kutii amri hii na Ngamini alirithi kiti na alikuja kukiachia baada ya vita ya wenyewe kwa wenyewe na kwenda kwenda uhamishoni Old Moshi kwa Mangi Rindi Mandara.
Historia hii huipati popote labda katika ukoo wa Shangali wenyewe. Shangali Mamkinga akatawazwa na kuwa Mangi mwaka wa 1890 na mwaka wa 1901 aliacha nafasi hiyo ikashikwa na Ngulelo. Wajerumani wakawa wamechoshwa na vita hivi vya wenyewe kwa wenyewe wakawakamata Mangi 19 wakawanyonga. Mama Ali anasema kuwa Wajerumani walimpeleka Ngulelo Kismayu, Somalia uhamishoni ili akanyongewe huko lakini hili halikutekelezwa na huko Somalia akaingia Uislam na jina alilochagua ni Selemani. Taarifa nyingine zinasema alipelekwa Lamu. Ngulelo aliporudi uhamishoni akawa ndiye Muislam wa kwanza Machame kutoka ukoo wa Shangali.
Akiwa uhamishoni Muro Mboyo alikutana na kufanya urafiki mkubwa na mmeshionari wa Kijerumani Bruno Gutmann kutoka Leipzig Mission aliyefika Kidea Mission, Old Moshi mwaka wa 1902. Hapa kuna kisa kizuri sana. Mama Ali hakuweza kunipa jina kamili la Gutmann na akilitamka kwa makosa kama ‘’Kutimani.’’ Nilikwenda Kidea Mission Old Moshi kuendelea na utafiti. Kwa mastaajabu makubwa sana nilionyeshwa kaburi la Bruno Gutmann yule Mjerumani rafiki yake Muro Mboyo, babu yake Mama Ali ambae Mama Ali hakuweza kulitamka vyema. Hili lingekuwa kaburi la Gutmann kama angekufa Uchaggani lakini alikufa Ujerumani mwaka wa 1966. Gutmann alifanikiwa kuwatia katika Ukristo wazee wengi mashuhuri Old Moshi isipokuwa Muro Mboyo.
Yeye alibakia katika Upagani. Sijaweza kujua kwa nini Muro Mboyo hakuingia Ukristo wakati kila mtu Uchaggani alikuwa anaupokea. Lakini kwa kukuza urafiki wao Muro Mboyo alimpa ardhi Bruno Gutmann na Gutmann alijenga kanisa ambalo naamini lipo hadi leo ingawa wahusika pale Kidia hawakuweza kunipa taarifa za kutosha. Nyaraka za Mzee Rajabu zina historia ya babu zake walioishi karne ya 19 na nyadhifa mbalimbali walizoshika katika uongozi wa utawala wa Machame chini ya Mangi. Babu yake wa tatu alikuwa Waziri wa Mangi Renguo (1784 – 1837), babu wa pili alikuwa Waziri wa Mangi Mamkinga aliyekuwa Mangi kuanzia mwaka wa 1855 – 1880, na baba yake, Muro Mboyo alikuwa Waziri wa Mangi Ndeseruo Mamkinga.
Baada ya kupata msingi huu wa simulizi kazi yangu sasa ikawa kuingia katika historia ya Wachagga ambayo karibu yote imeandikwa na Wazungu na hapo kutazama taarifa ambazo zipo katika nyaraka za Mzee Rajabu. Nyaraka za Mzee Rajabu zimebeba unaweza kusema historia kubwa ya Uchaggani kwa kuweza kumkutanisha mtafiti na viongozi wa nyakati zile na siasa zilizotamalaki baada ya kundoka Wajerumani na kuja Waingereza. Nyaraka zina taarifa za Gavana George Stewart aliyekuwa Gavana wa tatu wa Tanganyika aliyetawala mwaka wa 1931 hadi 1934. Ndani ya nyaraka hizi kuna barua walizokua wakiandikiana Mzee Rajabu na Chief Abdiel Shangali kuhusu mambo mengi yaliyokuwa yanaikabili Machame hasa kuhusu ugomvi uliozuka baina yao pale Mzee Rajabu aliposilimu na kujenga msikiti. Nyaraka za Rajabu Ibrahim Kirama zina barua nyingi zinazoeleza yote yaliyotokea hadi kufikia kujengwa msikiti mwaka wa 1933 ambao sasa unaitwa Msikiti wa Mzee Rajabu.
Kuna barua baina ya Mzee Rajabu na Mangi Mkuu Chief Thomas Marealle. Kuna taarifa za wanasiasa mahiri wa zama zile Petro Njau na Joseph Merinyo. Hawa wawili walikuwa waandishi wa Mzee Rajabu wakimuandikia barua zake kwenda serikalini na kwengineko barua nyingine zikiandikwa kwa lugha ya Kiingereza. Halikadhalika wamo wanamji watu wa Moshi mjini kama Liwali Minjanga Mussa na mwanae Liwali Mussa Minjanga waliokuwa mahakama ya mwanzo Moshi Bomani wakihukumu kwa mujibu wa sharia, Shariff Muhdhar Hussein, Suleiman Nassor Gurnah, Shariff Jiwa kwa kuwataja wachache, hawa walikuwa viongozi wa East African Muslim Welfare Society (EAMWS)tawi la Moshi. Hawa wote walikuwa watu mashuhuri katika siasa za Uislam Kilimanjaro. Nyaraka hizi zina taarifa za wanazuoni maarufu wa nyakati zile kutoka Zanzibar ambao walisubihiana na Mzee Rajabu, wanazuoni kama Sayyid Omar bin Sumeit, Sayyid Omar Abdallah Mwinyibaraka na Sheikh Abdallah Saleh Farsy.
Inasikitisha kuwa historia ya Wachagga imeandikwa na Wazungu kama Bruno Gutmann, Charles Dundas kwa mtindo wa wao kuelezwa kila kitu na wenyeji kuanzia mila na utamaduni, historia za watawala hadi vita vilivyopiganwa baina yao lakini hakuna mahali popote ambapo watoa taarifa wa historia hii wametajwa. Machifu wanapotajwa wanatajwa kutokana na jicho la Wazungu pale waliposuhubiana na Wachagga katika historia yao ya ukoloni. Kama isingekuwa kwanza kwa kuhifadhiwa historia hii ya ukoo wa Nkya kwa simulizi na kwa kuhifadhi nyaraka historia hii ya Uislam Uchaggani ingepotea. Watafiti walikuwa wametosheka na historia ya jinsi Ukristo ulivyofika Uchaggani nay ale manufaa ambayo wao wanaona waliwaletea Wachagga kama shule, hospitali na mengineyo.
Mangi Shangali Ndeseruo ndiye aliyewapokea Machame Wamishionari wa Leipzig Mission kutoka Ujerumani mwaka wa 1893 na alijenga uhusiano mzuri sana na Wamishionari hawa wa dhehebu la Kilutheri. Kitabu hiki kinaeleza maisha ya Rajabu Ibrahim Kirama ambae ndiye aliyeuingiza Uislam Nkuu Machame kwa kujenga msikiti shule na kuleta walimu kusomesha Qur’an. Hivi ndivyo Mzee Rajabu alivyoweza kuifungua Kilimanjaro kupokea Uislam. Hapa ndipo panapoanza harakati za Uislam Machame Nkuu na kusababisha uhasama mkubwa kati ya ukoo wa Muro Mboyo na ukoo wa Mangi Ndeseruo Mamkinga. Huu ukaja kuwa ugomvi baina ya mjukuu wa Mangi Ndeseruo Mamkinga, Chief Abdiel Shangali na mtoto wa Mkuu wa jeshi lililokuwa la babu yake kabla ya utawala wa Wajerumani, Muro Mboyo, sasa akijulikana kwa jina lake jipya la Kiislam, Rajabu Kirama.
Abdiel Shangali alipochukua utawala kutoka kwa baba yake Mangi Shangali Ndeseruo Ukristo ulikuwa umeshamiri vyema Machame na kote Uchaggani. Mzee Rajabu alipokuja na ombi la kujenga msikiti katika himaya ya Chief Abdiel Shangali, jambo hili lilimghadhibisha sana Chief Shangali. Chief Shangali alifanya kila juhudi aliyoweza ili Uislam usishike mizizi Machame na kwa takriban miaka 20 palikuwa na uhasama mkubwa baina yake na Mzee Rajabu.
Msikiti ulipojengwa Mangi alitoa amri uvunjwe na Waislam wakamatwe. Halikadhalika palitokea jaribio la kumuua Mzee Rajabu. Baadhi ya Waislam walikimbia Machame kwa kuhofia maisha yao. Mzee Rajabu alikwenda hadi Dar es Salaam kutafuta msaada kutoka kwa Al Jameeat Islami Umumia of East Africa (Umoja wa Waislam wa Afrika ya Mashariki). Juhudi za kutaka kujenga msikiti na baadae shule kulimpeleka Mzee Rajabu Mombasa na Dar es Salaam kutafuta vibali kutoka kwa Gavana na ofisi nyingine za serikali. Mzee Rajabu alitumia nafasi hii ya mgogoro kuomba Machame iwe na mafungamano na Al Jameeat Islami Umumia of East Africa ili kujiongezea nguvu. Jumuia hii katika mazingira ya kikoloni ilikuwa ikiongozwa na Wahindi na hili lilipunguza nguvu ya Waislam kwa kiasi kikubwa sana. Mwaka wa 1933 Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika ilipoundwa Dar es Salaam na vijana wanasiasa waliokuwa viongozi wa African Association Mzee Rajabu haraka aliwaunganisha Waislam wa Machame na jumuia hii mpya.
Mwaka wa 1943 Mzee Rajabu alikwenda Dar es Salaam na kumchukua Sheikh Hassan bin Ameir na kujanae Machame. Baada ya safari hii Sheikh Hassan bin Ameir alileta walimu wanne kuja kufundisha dini Machame na Upare - Sheikh Salehe Mwamba, Shariff Alawi, Sheikh Mahmud Mshinda na Sheikh Abdallah Minhaj. Kuanzia hapa taratibu pakawa na mabadiliko makubwa katika mila za Wachagga hasa kuhusu pombe na misikiti ikawa sasa inajengwa kila walipokuwapo Waislam. Kuja kwa Sheikh Abdallah Minhaj Machame na kuanza kusomesha kulileta mafanikio makubwa sana Machame. Uislam ulianza kupata nguvu na Waislam wakajipembua kwa mila na tabia ikawa sasa Waislam wanaweza kutambulikana kwa muonekano wao kabla ya kudhihirika tabia zao. Waislam wakawa jamii inayotambulikana.
Sheikh Abdallah Minhaj aliacha athar kubwa sana Kilimanjaro na ndiye mwalimu aliyemsomesha Mama Ali Qur’an. Wakati tunaagana baada ya mazungumzo yetu nilivutiwa na usomaji wa Qur’an wa Mama Ali wakati alipokuwa anasoma dua. Sikuweza kustahamili nilimuuliza kuhusu hili na yeye akanijibu, ‘’Mimi ni mwanafunzi wa Sheikh Abdallah Minahaj.’’ Mzee Rajabu alipofariki mwaka wa 1962 alipata maziko makubwa sana Waislam kutoka kila pembe ya Uchaggani na Upareni walihudhuria mazishi yake pamoja na Mangi Mkuu Thomas Marealle. Kaburi la Mzee Rajabu lipo katika uwanja wa msikiti alioujenga, uwanja ambao pia ilijengwa Muslim School ya kwanza Uchaggani na hii ndiyo shule aliyosoma Mama Ali na watoto wengi Uchaggani. Wanafunzi wa shule hii walikuja kushika nyadhifa mbalimbali katika serikali ya Tanganyika na Tanzania. Maarufu katika hawa akiwa Prof. Awadh Mawenya aliyekuwa Mtanzania wa kwanza kuwa Mkuu wa Idara ya Uhandisi Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.
Ningependa kuhitimisha kwa kusema kuwa athari ya Uislam Uchaggani ilijitokeza wazi miaka ya 1950 wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika pale TANU ilipopanda mlima kumkabili Mangi baada ya kujiimarisha kupitia Waswahili wa Moshi mjini chama kikiongozwa na wazalendo kama Yusuf Olotu, Juma Ngoma, Melkezedek Simon, Gabrieli Malaika, Bi. Halima Selengia, Bi. Amina Kinabo, Mama bint Maalim, Lucy Lameck kwa kuwataja wachache. Iliwachukua muda kwa machifu kutambua kuwa huu ulikuwa mwamko mpya tofauti na kuingia kwa Uislam Uchaggani ambao ulianza na Mzee Rajabu Kirama Machame Nkuu na kusambaa taratibu. Mwamko huu wa uhuru na kujitoa katika minyororo ya ukoloni uliitikiwa na kila Mchagga kwa wakati mmoja bila ya kujali imani yake. TANU ikaweza kwa kipindi kifupi cha miaka saba ya kupigania uhuru kuvunja nguvu ya Mangi iliyobakia Uchaggani chini ya utawala wa Waingereza.
Tunamuomba Allah alifanye kaburi la Mzee Rajabu Ibrahim Kirama kuwa moja ya mabustani ya peponi.
Amin.