Sina utaalamu na masuala ya fedha au kodi ila nimeona suala la kodi watakayolipa Ramadhani Brothers baada ya ushindi wao kule Marekani kwenye mashindano ya America's Got Talent (Fantasy League) likiibua maswali juu ya kodi watakayolipa.
Ningependa kujua kama nitakuwa sahihi kwa huu mchanganuo:
Kwa mapato yoyote ya fedha kuanzia $5,000 nchini Marekani wanakata 24% ambayo inaweza kupanda mpaka 37% kwa kiwango kikubwa cha fedha.
Kwa Ramadhani Brothers mpaka hapo wapo kwenye kundi hilo. Kigezo kingine kwakuwa wapo wawili (filing jointly)
na kiwango cha fedha walichoshinda kipo kati ya $201,051 mpaka $383,900 watalipa $34,337 pamoja na 24% kwa taarifa za kodi kwa mwaka 2023.
Kwahiyo, ukiachana na hiyo $34,337 ukitoa Federal Tax (24%) ni $60,000. Hii ni kwa jimbo la California.
Kwahiyo baada ya kodi kuna uwezekano wakabaki na $190,000.
Nimeona TRA nao wametoa ufafanuzi kuwa "Kwa aliye na sifa za mkazi wa Tanzania analipa kodi ya mapato atakayopata popote duniani. Na kwa kuwa hawa ni watu binafsi watalipa kodi kulingana na kiwango cha mtu binafsi ambacho ni shilingi 1,536,000 kujumlisha 30% ya kiasi kinachozidi milioni 12. Na hiyo ndiyo kodi watakayolipa kila mmoja kulingana na vipato watakavyopata baada ya kutoa gharama. Hakutakuwa na 10% ya nyongeza kwa kuwa hawana repatriated income. Pia wanaweza kupata unafuu wa kodi hapa Tanzania kwa kulingana na kifungu cha 77 cha sheria ya kodi ya mapato ya mwaka 2004."
Kwa maana hiyo kama mapato yao yatakuja kama ya watu binafsi watalipa kodi ya 1,536,000 pamoja na 30% kwa kila mmoja. Sasa kama watagawana ½ ya mapato kila mmoja: $190,000 ÷ 2 x TZS 2550 = TZS 242,250,000
Ukitoa kodi ya 1,536,000 pamoja na 30% kwa mapato ya kila mmoja huenda wakabaki na TZS 168,499,800.
Kwahiyo kwa makadirio pesa yote ile kila mmoja anaweza kubaki na TZS 168,499,800.
Sina uhakika sana na mchanganuo huu kama nilivyosema awali sina utaalamu na masuala ya fedha au kodi, naamini wajuzi watatupa picha kamili.
Ila, kama wanavyosema kodi ni moja ya utapeli uliohalalishwa. Kazi kubwa imefanywa na Ramadhani Brothers lakini % kubwa ya mapato yao yataishia kugawanywa kwa nchi 2.
Nilimsikiliza mtaalamu wa masuala ya fedha akitoa ushauri kuwa mapato yao wayapokee kama taasisi maana kuna uwezekano wa kupata unafuu wa kodi tofauti na mapato hayo wakiyapokea kama watu binafsi. Nina imani watapata ushauri mzuri wa kifedha huko walipo maana ni hatari, haya ndiyo mambo yanayopelekea watu kukwepa ulipaji wa kodi.