Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, ameipongeza Benki ya NMB kwa kutenga sehemu ya faida wanayopata kurudi kusaidia jamii, ametoa pongezi hizo leo Oktoba 22, 2024 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Halmashauri ya Mbozi mkoani Songwe.
Chongolo amesema hayo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi magodoro 60 kwa ajili ya Wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Songwe, vitanda 40 vya wanafunzi aina ya double, kwenye Shule ya Sekondari Nambizo pamoja na madawati 100 kwa Shule za Msingi Londoni na Sai.
Vifaa hivyo vyote vimetolewa na Benki ya NMB vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 23 ambapo lengo ni kuboresha sekta ya afya na elimu.
Chongolo ameahidi ushirikiano wa karibu na Benki ya NMB na kutoa wito kwa Wananchi na watumishi katika mkoa wa Songwe kutumia huduma za benki hiyo, hususan mikopo yenye gharama nafuu, pia, amewataka kuepuka mikopo isiyo na unafuu inayojulikana kwa jina maarufu kama "Kausha Damu."
Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Ester Mahawe, ameishukuru Benki ya NMB kwa kuendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuinua na kuunga mkono juhudi za serikali katika sekta za afya na elimu kupitia michango yao.
Upande wa Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Willy Mponzi amesisitiza kuwa benki yao ina wajibu wa kushirikiana na serikali, hususan katika kuboresha sekta ya elimu na afya ili kuleta maendeleo endelevu kwa jamii.
Ameongeza kuwa ni jukumu la NMB kuhakikisha jamii inafaidika kutokana na mafanikio ya benki hiyo.