REDET: Kikwete aporomoka
na Sauli Giliard
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
UTENDAJI kazi wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kwa kipindi cha miaka mitatu alichokaa madarakani, umeporomoka kutoka asilimia 67 alipoingia madarakani hadi asilimia 39.5.
Takwimu hizo ni kwa mujibu wa utafiti wa Mpango na Elimu ya Demokrasia nchini wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (REDET), uliotolewa jana.
Aidha, utafiti huo, umebainisha kuwa kati ya watu 1,300, waliohojiwa katika wilaya 26 kutoka mikoa yote nchini, asilimia 39.0 walisema wanaridhika na kasi ya utendaji kazi wa Serikali ya Rais Kikwete, huku wengine asilimia 19.3, wakisema hawaridhiki.
Akisoma matokeo hayo ya utafiti wa 15, uliofanyika Novemba mwaka jana, Mtafiti Mkuu wa REDET, Dk. Bernadeta Killian, alisema asilimia 67 ya waliohojiwa, walisema wanaridhika na utendaji wa rais, wakati mwaka 2007, takwimu hizo zilishuka na kufikia asilimia 44, lakini sasa imeshuka zaidi hadi kufikia 39.5.
"Hata hivyo, ukilinganisha na takwimu kutoka utafiti uliofanyika Oktoba mwaka 2006 na 0ktoba 2007, kutathimini utendaji wa Serikali ya Rais Kikwete tangu aingie madarakani, asilimia ya waliohojiwa ambao wanasema wanaridhika na utendaji kazi wake, inaonekana kupungua kutoka asilimia 67, hadi 44 Oktoba 2007 na kufikia asilimia 39.5, Novemba 2008," alisema.
Dk. Killian ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC) ya chuo hicho, aliongeza kuwa, idadi ya wanaoridhika na kasi ya utendaji wa Serikali ya Rais Kikwete, ni asilimia 78.5 ya waliohojiwa, idadi ya wasioridhika, ikiongezeka kutoka asilimia 7.8 mwaka 2006 hadi kufikia asilimia 19.3, mwaka jana.
Akifafanua zaidi, alisema idadi ya wanaoridhika na utendaji kazi wa Rais Kikwete ilishuka kwa tofauti ya asilimia 23 kati ya mwaka 2006 na 2007, huku kasi ya kutoridhika, ikishuka kwa tofauti ya asilimia 4.5.
Mtafiti huyo aliyeambatana na Mwenyekiti Mwenza wa REDET, Dk. Benson Bana, alisema Wilaya ya Karatu, inaongoza kwa kutoridhishwa na utendaji wa Rais Kikwete, kwani kati ya watu 50 waliohojiwa, asilimia 66 walisema hawaridhishwi, ikifuatiwa na Wilaya ya Lindi, yenye asilimia 40.
Kwa upande mwingine, kati ya wilaya zote 26, zinazowakilisha mikoa, asilimia 82 ya wakazi waliohojiwa Wilaya ya Mkoani, walisema wanaridhishwa sana na utendaji wa Serikali ya Kikwete, ikifutiwa na Unguja Kaskazini, yenye asilimia 80.
Akitoa sababu za watu wanaoridhika kiasi na ambao hawajaridhika, Dk. Killian alisema, theluthi moja ya waliohojiwa, sawa na asilimia 31, walisema Rais Kikwete ameshindwa kuboresha hali ya maisha kwa Watanzania, asilimia 24 walisema hajatimiza ahadi na asilimia 12.2, hawajaridhika na utendaji wake, hasa katika kufuatilia utekelezaji.
Licha ya idadi inayoridhika sana na utendaji kazi wa Serikali ya Rais Kikwete kupungua, lakini kiwango cha watu wenye imani na rais huyo ni asilimia 50.3, huku wenye imani kiasi ni 33.9, na kufanya jumla ya wenye imani na Rais Kikwete, kuongezeka hadi asilimia 84.2.
Akielezea matokeo ya utendaji kazi wa serikali na baadhi ya taasisi zake, mtafiti huyo alisema Baraza la Mawaziri na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), zimefanya vibaya kwa kupata asilimia 18 na 13.4.
Watendaji wengine wanaomfuata Rais Kikwete kwa kuwa na imani sana ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (54), Makamu wa Rais, Dk. Ali Shein (48) na mawaziri (23).
Kwa mujibu wa Dk. Killian, tofauti na taasisi nyingine zote, Bunge linaongoza kwa kuwaridhisha wananchi kutokana na utendaji wake kwa kupata asilimia 77.4 na kufutiwa na Serikali za Mitaa, asilimia 75.6. Pia Baraza la Mawaziri (63.8), Polisi (62.5), Mahakama (62.2) huku TAKUKURU ikiwa ya mwisho kwa kuwa na asilimia 39.9.
Kwa mujibu wa utafiti huo, sababu nyingi zilizotolewa na wananchi ambao hawakuridhishwa na utendaji wa serikali na taasisi zake, ni pamoja na serikali kutofuatilia utekelezaji wake, mikataba mibovu ya serikali na wawekezaji juu ya rasilimali zake.
Kuhusu hatua zilizochukuliwa dhidi ya wizi wa fedha katika Akaunti ya Malipo ya Nje (EPA), asilimia 23, hawaridhiki na ushughulikiaji wake, huku asilimia 49.5 wanaridhika kiasi.
Kuhusu Zanzibar, wataalam hao wa REDET katika utafiti wao walibainisha kuwa, asilimia 44 ya Wazanzibar waliohojiwa juu ya utendaji kazi wa Rais Abeid Karume, walisema wanaridhishwa sana, asilimia 28 wakisema wanaridhishwa kiasi huku, asilimia 26 walijibu hawaridhishwi kabisa na utendaji wa rais huyo.
Kama ilivyo kwa Rais Kikwete, ambao hawakuridhishwa na utendaji wa Karume, asilimia 29.2 walisema ameshindwa, huku asilimia 12.8 wakisema hajatimiza ahadi.
Akilizungumzia eneo la utendaji wa vyama vya siasa, Dk. Killian alisema, kwa kufanya ulinganifu wa matokeo ya tafiti za REDET tangu 2006 hadi mwaka jana, idadi ya waliohojiwa waliosema utendaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) umeporomoka kutoka asilimia 60, mwaka 2006, na kufikia asilimia 32, mwaka 2007, huku idadi hiyo ikishuka zaidi na kufikia asilimia 32.3 katika utafiti wa mwaka jana.
Katika suala hilo, vyama vya siasa vimeonekana kuwa na ufanisi mzuri kwani utafiti huo umeonyesha kuwa, utendaji wake umepanda kutoka asilimia 18 hadi 27, huku wanaoridhishwa kiasi ikiongezeka kutoka asilimia 23 mwaka 2006 na kufikia asilimia 27.
Akisoma matokeo ya utafiti huo, alisema asilimia 34.9 walisema kupanda kwa gharama za maisha ndiyo kero kuu, asilimia nyingine 32.1 waliohojiwa walisema huduma mbaya za jamii ikiwemo afya, elimu na afya ndizo kero kuu, rushwa ikiwa ni asilimia 8.7.
Kero nyingine na asilimia zake katika mabano ni viongozi walioko madarakani (6), ufisadi (5.2), ukosefu wa ajira (5), kilimo kutopewa mkazo (2.1) na mikataba mibovu isiyo na maslahi kwa taifa (1.4).
Akizungumza mara baada ya kusoma matokeo ya utafiti huo, Dk. Killian alisema kuwa hali ya kupanda kwa gharama za maisha, hasa kipindi hiki cha mtikisiko wa uchumi duniani, ni changamoto kwa serikali kwa kufuata mifano ya nchi nyingine zilizokwishaandaa mipango kwa ajili ya kuwalinda watu wake.