ChingaMzalendo
Senior Member
- Nov 9, 2008
- 192
- 3
Na Waandishi Wetu
Habari hii imeandaliwa na Julieth Ngarabali, Kibaha, Lilian Lucas,Morogoro, Paulina David, Mwanza, Brandy Nelson, Mbeya, Joyce Joliga, Songea, Lilian Lugakingira Bukoba, Mwandishi Wetu, Sumbawanga na Ally Sonda,Moshi.*
.KATIKA hali inayoonyesha utaratibu wa kurithishana uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) umeanza kushamiri , watoto wa vigogo kadhaa wa chama hicho akiwemo wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, wamechaguliwa kushika nyadhifa mbalimbali kwenye Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM).
Matokeo ya uchaguzi huo yaliyopatikana jana kutoka mikoa mbalimbali, yameonyesha kuwa mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, Ridhiwan Kikwete ni miongoni mwa viongozi waliochaguliwa kwa kishindo kuwa mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM taifa, akipata kura 274 kati ya 315 zilizopigwa.
Wengine waliochaguliwa na Ridhiwan kuongoza jumuiya hiyo mkoani Pwani na nyadhifa zao kwenye mabano ni Abdalah Ulega (mwenyekiti) na Mkomwa Mtiga (Mjumbe wa Mkutano Mkuu taifa).
Kwa mujibu wa matokeo hayo yaliyotangazwa na Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Said Mwambungu, wengine waliochaguliwa kuongoza jumuya hiyo mkoani Pwani ni Josephat Msonde (Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM mkoa), Hilda Mzengo (Mwakilishi wa UWT) na mwakilishi wa wazazi mkoa, Siza Mjokaba.
Mkoani Morogoro, mtoto wa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii jinsia na Watoto, Lucy Nkya, Jonas Nkya, alichaguliwa kwa kura 290 kuwa Mwenyekiti wa Mkoa UVCCM.
Jonas aliibuka mshindi baada ya kuwashinda wapinzani wake Musa Kingu ambaye ni ndugu wa katibu wa uchumi na fedha wa CCM Taifa, Amos Makala na Adela Ng'atigwa.
Nkya alishinda katika kura za marudio baada ya matokeo ya awali kushindwa kumtoa mshindi aliyepata zaidi ya nusu ya kura zote zilizopigwa.
Hata hivyo, Musa Kingu alibahatika kushinda nafasi ya mjumbe wa Mkutano Mkuu CCM taifa, huku Pili Jabiri akijishindia nafasi ya mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM taifa.
Aliyechaguliwa kuwakilisha vijana UWT mkoani Morogoro ni Sepesina Lugalila, huku Masumbuko Igebya akichaguliwa kuwa mjumbe wa Mkutano Mkuu wa UVCCM mkoa na Antony Muhando akiwawakilisha wazazi.
Amosi Makala ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uchaguzi huo, aliwataka vijana kuwa na mshikamano na kutokubali kugawanywa na viongozi wachache ndani ya chama kwa kuwa vijana ndio nguzo kubwa na tegemeo la chama.
Naye mtoto wa Mbunge wa Jimbo la Kwella, wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa, Chrisant Mzindakaya, Paul Mzindakaya, ameibuka mshindi wa kiti cha mwenyekiti wa umoja wa vijana mkoani humo.
Akitangaza matokeo hayo msimamizi wa uchaguzi huo kutoka Makao makuu ya umoja wa vijana, Thomas Mwang'onda ambaye pia ni Mbunge wa kuteuliwa, alimtangaza Paul Mzindakaya kuwa amewashinda wenzake kwa kupata kura 205.
Katika uchaguzi huo mwandishi wa habari na mtangazaji wa Radio Free Afrika, Kituo cha Rukwa, Sammy Kissika, alishinda nafazi ya ujumbe wa Baraza Kuu la Vijana taifa Mwang'onda alimtangza Bernard Mukasa kuwa ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM taifa.
Mkoani Mwanza, Maghembe Boniphace Koneli amechaguliwa Mwenyekiti wa UVCM katika uchaguzi huo uliofanyika juzi.
Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mwanza, Barnabas Essau aliliwaambia waandishi wa habari jana kwa kura 365 na kuwashinda wagombea wenzake Abel Maiga Kaitila aliyepata kura tisa na John Dea aliyepata kura 184.
Essau alisema kuwa nafasi ya mjumbe wa Baraza Kuu Taifa la chama hicho ilikwenda kwa Barnabas Mathayo, mjumbe wa Mkutano Mkuu CCM Taifa amechaguliwa Barnabas Mathayo, nafasi ya mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa ilikwenda kwa Peter Yona Minga, uwakilishi wazazi ilikwenda kwa Muhoja mwinamila Mapande na uwakilishi wa UWT ilikwenda kwa Rehema Laurent.
Mkoani Mbeya UVCCM ilipata sura mpya baada ya kumchagua Regnand Msomba kuwa Mwenyekiti wake kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Naye Benedict Ngwenye alichaguliwa mwenyekiti mpya wa UVCCM mkoa wa Ruvuma kwa kura 331.
Akitangaza Matokeo hayo jana katika ukumbi wa shule ya wasichana Songea Msimamizi wa uchaguzi huo Livingstone Msinde ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tunduru alisema,wajumbe waliopiga kura ni 391 ambapo kura halali ni 387 na kura nne ziliharibika.
Mkoani Kagera, Deusdedith Katwale kuwa mwenyekiti mpya ya jumuia hiyo Mkoani Kimalinjaro Godliving Mosha ambaye ni mpiga debe alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa mkoa baada ya kumpa kura 259 dhidi ya Antony Malisa kura 127 na Gilbert Temu aliyeambulia kura 102.
Mosha mwenye elimu ya Sekondari, aliwabwaga wasomi wawili Malisa na Temu ambao wana elimu ya chuo kikuu.
Wakizungumza na Mwananchi baada ya matokeo kutangazwa, baadhi ya Wajumbe wa mkutano mkuu walisema wameamua kumchagua Mosha kwa vile anafahamu vema shida na matatizo ya vijana wa mkoa wa Kilimanjaro
Habari hii imeandaliwa na Julieth Ngarabali, Kibaha, Lilian Lucas,Morogoro, Paulina David, Mwanza, Brandy Nelson, Mbeya, Joyce Joliga, Songea, Lilian Lugakingira Bukoba, Mwandishi Wetu, Sumbawanga na Ally Sonda,Moshi.*