Ripoti kuhusu hali ya haki za binadamu duniani inayotolewa na Marekani kila mwaka inaendelea kupoteza maana

Ripoti kuhusu hali ya haki za binadamu duniani inayotolewa na Marekani kila mwaka inaendelea kupoteza maana

ldleo

JF-Expert Member
Joined
Jan 9, 2010
Posts
1,116
Reaction score
1,121
VCG111369286228.jpg


Ofisi ya habari ya baraza la serikali la China wiki hii imetoa ripoti kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu nchini Marekani kwa mwaka 2021. Ripoti hii kimsingi haina mambo mapya, kwani imeendelea kuonyesha usugu wa tatizo la haki za binadamu nchini Marekani, ambalo baadhi ya zinazojiita kuwa taasisi za haki za binadamu za kimataifa ni kama zinapuuza. Jambo jipya ambalo pia linaonekana kuwa si jipya sana, ni kuongezeka kwa ubaguzi wa rangi dhidi ya wamarekani wenye asili ya Asia.

Ripoti hiyo inayotolewa kila mwaka na ofisi ya habari ya baraza la serikali ya China, imesema hali ya haki za binadamu nchini Marekani kwa mwaka 2021 iliendelea kuwa mbaya. Sababu kubwa iliyofanya hali iwe mbaya zaidi ni upotoshaji mkubwa wa kisiasa, uliofanya vifo kutokana na COVID-19 viwe vingi na kufanya nchi hiyo iwe na rekodi kubwa ya vifo.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bw. Anthony Blinken amesema COVID-19, imetumiwa na nchi zenye tawala za kiimla kama njia ya kuwakandamiza wakosoaji wa serikali na kukandamiza haki za binadamu. Lakini hali halisi na ukweli vimekuwa tofauti sana na anachosema waziri Blinken. Kwani ukiangalia jinsi Marekani ilivyoshughulikia COVID-19 ikilinganishwa na nchi nyingine tunaona kuwa njia ya Marekani ni kama ilipuuza haki na maisha ya watu wasio na uwezo, na matokeo yake ni kuwa Marekani imekuwa na vifo zaidi kuliko nchi nyingine.

Demokrasia ya Marekani ambayo inazingatia haki na uhuru kwa wenye nguvu na matajiri, imeendelea kupuuza haki na uhuru wa wasio na nguvu na hata kuendeleza utekelezaji wa sheria wa kikatili unaofanya haki ya maisha ya wahamiaji na wakimbizi nchini Marekani iwe ngumu. Ripoti hiyo pia imeonesha kuongezeka kwa vitendo vya ubaguzi dhidi ya watu wachache, hasa wenye asili ya Asia kutokana na habari za upotoshaji wa makusudi.

Pamoja na ukweli kwamba hayo yote si mageni kwenye suala la haki za binadamu nchini Marekani, na hata jinsi Marekani inavyozinyooshea vidole nchi nyingine kuhusu maswala ya haki za binadamu, ukweli unazidi kufichua kuwa suala la haki za binadamu ni karata ya kisiasa ya Marekani, sio kama ni kweli ni huruma kwa watu nchi inazozitaja kuwa zinakiuka haki za binadamu.

Waraka mfupi uliotolewa January 24 na idara ya utafiti wa bunge (Congressional research service), umeeleza kuwa mwanzoni serikali ya Marekani haikufurahia ripoti ya haki za binadamu kuzungumzia vibaya hali ya haki za binadamu kwa nchi washirika. Hata nchi washirika wa Marekani zilikuwa zikitaja ripoti hizo kuwa zina upendeleo, kwa hiyo Marekani ililazimika kuongeza ufuatiliaji kwenye nchi zisizo washirika, na hata kuongeza yaliyomo kwenye ripoti hiyo ili kupata maeneo zaidi ya ukosoaji.

Tukiangalia yaliyomo (contents) yanayofuatiliwa na Marekani na kuyafanya kuwa mambo ya haki za binadamu, tunaweza kuona kuwa mambo mengine yasiyohusiana moja kwa moja na haki za binadamu yameingia kwenye ripoti ya Marekani. Baadhi ya mambo hayo ni pamoja na uhuru wa habari, au uhuru wa watu kutumia internet. Kwa nchi nyingi zinazoendelea haki hizi ni za ziada, kuna watu wanaoishi au wanaoweza kuishi bila mambo haya. Na kimsingi haki hizo zinapatikana kwa pesa kulingana na uwezo wa mtu. Hata kwenye nchi zilizoendelea ikiwa ni pamoja na Marekani, si kweli kwamba kila mtu ana haki hiyo.

Kinachoonekana ni kuwa vipengele hivi vimewekwa ili kuzilenga nchi ambazo kwa namna moja au nyingine zitaonekana kufanya vizuri kwenye maeneo mengine ya haki za binadamu, lakini zina dosari kwenye eneo hilo. Na inaonekana kuwa hakuna hatua yoyote inayochukuliwa dhidi ya nchi hizo zaidi tu ya kuzidhalilisha. Kibaya zaidi ni kuwa ni Marekani hiyo hiyo inaonekana kuwa na ukaribu zaidi na baadhi ya nchi inazozitaja kuwa wakiukaji wa haki za binadamu, lakini inazikosa vikali hata kuzinyima msaada nchi nyingine ambazo hali yake ya hali za binadamu si mbaya sana.

Kinachofichuka ni kuwa kwa Marekani haki za binadamu, sio suala la haki za binadamu, bali ni karata ya kisiasa au nyenzo ya kidiplomasia ya kuzidhibiti nchi nyingine na kuingilia mambo yake ya ndani.
 
Back
Top Bottom