Ripoti iliyotolewa Agosti 9 na jopo la kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi (IPCC), imetoa tahadhari kuwa mabadiliko ya tabia nchi yanayoendelea kutokea duniani yanaweza kuchukua maelfu ya miaka kurudi katika hali ya kawaida. Lakini pia ripoti hiyo hiyo imetoa matumaini kuwa kama juhudi za kupunguza hewa zinazosababisha kuongezeka kwa joto (CO2) zitakuwa endelevu, baadhi ya mambo kama kuongezeka kwa joto na kuwepo kwa hewa chafu, kunaweza kudhibitiwa au kurekebisha kabisa ndani ya miaka 20-30.
Ripoti hii imetolewa wakati hoja za wanaopinga uwepo wa mabadiliko ya tabia nchi zikiendelea kukosa mashiko, na ushahidi wazi wa madhara yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi yakiendelea kuonekana. Kuanzia mjini Zhengzhou China ambako mvua kubwa isiyo ya kawaida ilinyesha na kuleta mafuriko yaliyosababisha vifo vya watu zaidi 300, nchini Ujerumani vifo vya watu zaidi ya 110, na moto wa msituni uliotokea nchini Ugiriki, Uturuki, Algeria na Canada, na baridi isiyo ya kawaida katika maeneo kadhaa barani Afrika
Siku chache kabla ya kutolewa kwa ripoti hiyo kulikuwa na mambo kadhaa ya kutia moyo. Umoja wa Ulaya ulitangaza kuwa unataka kuhakikisha kuwa kabla ya mwisho wa muongo huu, kuwe na walau magari milioni 30 yanayotumia umeme, hili ni ongezeko kubwa sana ikilinganishwa na magari milioni 1.4 ya aina hiyo kwa sasa. Zaidi ya Euro bilioni 750 zimewekezwa ili kufikia lengo hilo.
Nchini Marekani serikali ya Rais Joe Biden pia imetoa msukumo mkubwa kuelekea kwenye matumizi ya magari ya umeme, pale aliposaini amri inayotaka nusu ya magari yote mapya yatakayouzwa nchini Marekani hadi mwaka 2030, yawe ni yale yatakayotumia umeme. Lakini pia kwenye mswada wake wa sheria ya ujenzi wa miundo mbinu, kuna kipengele kinachosema mabasi yote ya wanafunzi yanatakiwa kuwa ya umeme.
Ikumbukwe kuwa serikali iliyopita ya Marekani ilikuwa inakanusha kuwa kuna mabadiliko ya tabia nchi duniani, na kuamua kuiondoa Marekani kwenye Mkataba wa Paris. Uamuzi huu serikali ya Biden ambao unaonekana kuwa ni U-turn umechukuliwa na baadhi ya wachambuzi kuwa ni lengo la Marekani kutotaka kuwa nyuma ya China kwenye sekta ya magari ya umeme. Hata hivyo bila kujali kama lengo lake ni kushindana na China au juhudi za dhati za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, matokeo yake yatakuwa na manufaa kwa dunia.
Lakini hatua zilizotangazwa kuchukuliwa na Marekani na nchi za Ulaya, ni hatua ambazo tayari zilichukuliwa na China katika miaka kadhaa iliyopita. Serikali ya China imetekeleza hatua nyingi za kuhimiza matumizi ya nishati safi kwenye vyombo vya usafiri katika miji yake mikubwa ili kupunguza utoaji wa hewa chafu. Kwa sasa kuna mabasi mengi ya usafiri wa umma yanayotumia betri, gesi na umeme, kuna magari mengi binafsi na taxi zinazotumia betri, hali ambayo imepunguza sana utoaji wa hewa chafu.
Muundo wa matumizi ya nishati wa China imekuwa ni sera ya muda mrefu, ambayo haijajikita kwenye magari peke yake. Kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya nishati ya upepo, nishati ya jua na nishati nyingine zisizo za visukuku (non-fossil fuel) Kwenye mpango wa 13 wa maendeleo ya miaka ya mitano wa China (2016-2020) lengo lililowekwa lilikuwa ni kuhakikisha nishati safi inachukua asimilia 30 – 35 ya uzalishaji wa umeme. Na shirika la nishati duniani IEA limekadiria kuwa, katika miaka mitano ijayo China itachangia kati ya asilimia 36 na 40 ya matumizi ya nishati ya jua na upepo duniani.
Ni jambo la kutia moyo kuona kuwa nchi kubwa duniani, zinafanya maamuzi na kuchukua hatua za kubabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Kinachosubiriwa kwa sasa ni kuona utekelezaji.