Ripoti: Tanzania inakabiliwa na ukosefu wa Ajira Bora licha ya Uchumi kukua kwa 5.9%

Ripoti: Tanzania inakabiliwa na ukosefu wa Ajira Bora licha ya Uchumi kukua kwa 5.9%

Waufukweni

JF-Expert Member
Joined
May 16, 2024
Posts
5,383
Reaction score
18,776
Tanzania imerekodi ukuaji wa uchumi wa asilimia 5.9 mwaka 2025, huku ukuaji huo ukitarajiwa kufikia asilimia 6.1 mwaka 2026 na asilimia 6.5 katika kipindi cha muda wa kati, kwa mujibu wa ripoti ya Tanzania Economic Update 2026: Making Jobs Work.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa sekta za huduma, ikiwemo fedha, biashara na usafirishaji, zimechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji huo. Aidha, mfumuko wa bei umeendelea kuwa ndani ya wigo wa asilimia 3 hadi 5 unaolengwa na Benki Kuu ya Tanzania, huku deni la Taifa likiwa asilimia 49 ya Pato la Taifa.

Licha ya ukuaji huo, ripoti imebainisha kuwa Tanzania inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ajira zenye ubora, huku takribani asilimia 69 ya watu walio katika umri wa kufanya kazi wakiwa wameajiriwa lakini wengi wao wakipata kipato kisichokidhi mahitaji yao.

Watanzania wengi wanafanya kazi katika kilimo chenye uzalishaji mdogo au sekta isiyo rasmi, huku ukosefu wa ujuzi, fursa chache za mafunzo na vikwazo vya kiuchumi vikiathiri upatikanaji wa ajira bora. Ripoti pia imeeleza kuwa ni asilimia 12 pekee ya kampuni zilizosajiliwa Tanzania ambazo ni changa, ikilinganishwa na asilimia 38 nchini Rwanda, hali inayoashiria kasi ndogo ya kuanzishwa kwa biashara mpya.

Changamoto zinazokabili uchumi na ajira ​

Ripoti imebainisha kuwa licha ya uchumi kuendelea kukua, sekta ya madini imeathiriwa na uchakavu wa uzalishaji katika baadhi ya migodi iliyokomaa na uwekezaji mdogo katika migodi mipya. Kwa upande mwingine, kilimo kinakabiliwa na changamoto za ufanisi katika upatikanaji na usambazaji wa pembejeo, ikiwemo mbola.

Soma >> Prof. Kitila: Kiwango cha ukosefu wa ajira kimepungua hadi 6.4% mwaka 2024. Tuna uwezo wa kuzalisha ajira angalau kwa 7.8%

Aidha, nakisi ya akaunti ya sasa imeongezeka hadi asilimia 2.5 ya Pato la Taifa mwaka 2026, ikichangiwa kwa kiasi kikubwa na kupanda kwa bei za nishati duniani na gharama za usafirishaji kutokana na migogoro inayoendelea Mashariki ya Kati.

Kuhusu ajira, ripoti inaeleza kuwa Watanzania wengi wanafanya kazi katika kilimo chenye uzalishaji mdogo au shughuli zisizo rasmi, huku ukosefu wa ujuzi wa msingi ukiwazuia kupata ajira zenye tija na kipato bora. Wanawake wanakabiliwa na vikwazo zaidi vinavyohusiana na majukumu ya malezi, upatikanaji mdogo wa mafunzo na mgawanyo wa kazi kulingana na jinsia.

Mapendekezo​

Ili kukabiliana na changamoto hizo, ripoti inapendekeza Serikali kurahisisha usajili wa biashara kupitia mifumo ya kidijitali, kuboresha upatikanaji wa mikopo na kuimarisha mifumo ya kisheria ili kuwezesha biashara kukua na kuongeza ajira.

Pia, imesisitiza umuhimu wa kuongeza uwekezaji katika kilimo na viwanda, kuboresha upatikanaji wa pembejeo na masoko kwa wakulima wadogo, pamoja na kuimarisha mafunzo ya ujuzi kwa wafanyakazi.

Aidha, ripoti inapendekeza kutambua rasmi ujuzi walioupata wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi kupitia uzoefu, huku programu za ajira zikizingatia mahitaji ya wanawake, ikiwemo huduma za malezi ya watoto. Ripoti inahitimisha kuwa ukuaji endelevu wa uchumi unahitaji kuimarisha sekta binafsi na kuwawezesha wananchi kupata ajira zenye tija na kipato bora.
 

Attachments

Back
Top Bottom