Ripoti ya ukaguzi BoT isikaliwe-CHADEMA
2007-12-19 08:42:00
Na Godfrey Monyo
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeitaka serikali kutoa ripoti ya uchunguzi juu ya tuhuma za ubadhirifu wa fedha za Benki Kuu (BoT) kwa kuwa ipo tayari.
Aidha, kimesema kuwa kinashangazwa na ukimya unaoendelea kuhusu 'mafisadi' waliotajwa na kambi ya upinzani baada ya kuwatangaza kufanya ubadhirifu wa fedha za umma.
Hayo yalielezwa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Freeman Mbowe, alipokuwa akifungua mkutano wa kawaida wa Baraza Kuu la chama hicho.
Alisema ingekuwa busara kama taarifa hiyo ingetolewa na ijulikane kwa wananchi badala ya kuendelea kuwa siri na kuwafanya wananchi kukosa imani na serikali.
Aliongeza kuwa kitendo cha Mkaguzi Mkuu kutotoa ripoti hiyo wakati ipo tayari kinajenga mazingira ya kupotosha ukweli wa majibu ya uchunguzi.
Bw. Mbowe alisema habari walizonazo ni kwamba uchunguzi umeonyesha kiasi cha fedha `zilizochotwa` ni kikubwa kuliko kiasi kilichotajwa na kambi ya upinzani hapo awali.
``Serikali imepata kigugumizi baada ya kugundua kuwa kiasi cha fedha kilichochukuliwa BoT ni mara dufu ya kile tulichotangaza,`` alisema na kuongeza: "nakumbuka kuwa, awali tulielezwa taarifa hiyo itatolewa kwa wananchi haraka pindi wakaguzi hao watakapokamilisha kazi yao lakini cha ajabu wameendelea kukaa nayo.
Sisi tunadhani wana mpango wa kuibadilisha lakini lazima watambue kuwa fedha zilizofujwa ni jasho la Watanzania wanaolipa kodi na wanaohitaji taarifa za kweli kuhusu matumizi ya kodi zao.``
Mwenyekiti huyo alieleza kuwa mbali ya serikali kupata kigugumizi cha kutoa ripoti hiyo, pia `mafisadi` wameshindwa kutekeleza azimio lao la kwenda mahakamani.
``Mafisadi wameshindwa kutushtaki. Tunataka kufahamu nini mstakabali wa taifa hili, wakati wa kuvumilia utapeli umepitwa,`` alisema.
Serikali ilifikia uamuzi wa kufanya ukaguzi BoT baada ya kutolewa malalamiko ya kuwepo kwa tuhuma za ubadhirifu.
Kwa mara ya kwanza tuhuma za ubadhirifu ziliibuliwa bungeni katika kikao cha bajeti cha Julai na Mbunge wa Karatu, Dk. Wilbrod Slaa, ambaye pia aliwatuhumu baadhi ya vigogo wa serikali kwa ubadhirifu wa mabilioni ya fedha.
Kampuni iliyokuwa ikifanya uchunguzi huo ni Ernst & Young ambayo ilipewa siku 60 kukamilisha kazi hiyo.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Novemba 24, mwaka huu ilieleza kuwa Ernst & Young ilikwishakamilisha kazi yake na kuikabidhi kwa CAG.
Taarifa hiyo ambayo pia iliripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari nchini ilieleza kuwa hivi sasa mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali anaifanyia kazi.
Aidha, Bw. Mbowe alisema amesikitishwa na kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Siasa na Uhusiano wa Jamii, Bw. Kingunge Ngombale Mwiru, aliyesema kuwa mjadala wa katiba umefungwa kwa sasa.
Kwa mujibu wa Mbowe, Bw. Kingunge aliitetea hoja yake kwa kusema kuwa suala la mabadiliko ya katiba haliwezi kujadiliwa hivi sasa kwa kuwa halipo katika ilani ya CCM.
Akizungumzia suala hilo alisema mjadala wa katiba hauwezi kufungwa na ilani za chama chochote na kwamba unawahusu Watanzania wote bila kujali itikadi au dini.
SOURCE: Nipashe
Wakuu, kama kuna mwenye full report tafadhali iwekeni mezani ...