Mimi binafsi, naona Ripoti hiyo, imemtambulisha Mwakyembe ni nani: Aliyefanikisha fitina za kumzulia kuwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, anahusika na Richmond, mpaka akaamua kuachia ngazi.
Ushahidi wa Mwakyembe kuwa Lowassa anahusika ni habari za "kung'ata sikio" na kudokezwa na baadhi ya watu nje ya kiapo kuwa "jeuri yote inaonyesha kuwa kuna mkubwa fulani" anahusika!
Ushahidi mwingine ni maandishi ya gazeti la Saed Kubenea la MwanaHalisi, ambalo habari zake ni kuwaandama "watu fulani" na siyo kuandika "issues".
Imethibitika kuwa Lowassa hakuhusika, lakini akajiuzulu kwa kuwajibika kisiasa!
Kilichokosewa awali ni kutowajibishwa kwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Ibrahim Msabaha, ambaye ndiye aliyewajibika Wizarani mpaka Kampuni ya Richmond ikapewa zabuni na baadaye ikajitoa kwa kushindwa kazi.
Mwakyembe, pamoja na Spika, waliukataa kata kata na kuutupilia mbali, ushahidi wa Lowassa wa maandishi kuwa alimuandikia Msabaha Septemba 2006, kumtahadharisha kuwa ni vema ajiridhishe uwezo wa Kampuni hiyo, lakini Msabaha alishindwa kujiridhisha na hakuchukuliwa hatua wakati huo, mpaka alipolazimika kujiuzulu baada ya WM kusema anajiuzulu! Mambo haya sasa yanafukuka na ukweli, ambao kwa kawaida huwa haukubali kugubikwa na uongo, unajitokeza!
Miaka mitatu ya Richmond, EPA, Ufisadi, imeigharimu CCM na Serikali yake kusuasua kutekeleza Ilani ya Uchaguzi. Walianza vizuri na Shule (Sekondari za Kata, Chuo Kikuu cha Dodoma), chini ya usimamizi wa Lowassa, lakini wakashindwa kutekeleza Afya (Zahanati kila Kijiji na Kituo cha Afya, Kila Kata).
Serikali ya CCM sasa imekuja na "Kilimo Kwanza", ni mpango mzuri, lakini baada ya kuchelewa sana kutokana na porojo za kisiasa zisizokuwa na tija za Richmond, EPA, Ufisadi n.k. Umaarufu gani kwa Mwakyembe, wakati chama chake cha CCM kinaharibikiwa kwa porojo na fitina za kisiasa zinazochelewesha maendeleo ya nchi hii?
Bwassa