Mheshimiwa Spika, mashahidi wengi walioitwa kwa hati hususan kutoka TANESCO, Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Fedha na Wizara ya Katiba na Sheria walionyesha hofu, mashaka na hali ya kutojiamini kwa kutoa majibu yaliyofanana ya kiitifaki-itifaki na yaliyokosa mvuto na ushawishi wa kawaida mithili ya watu walioketishwa pamoja na kukaririshwa hoja za kujibu.
Wataalam wa TANESCO, mathalan, waliikataa Richmond Development Company LLC mara tatu wakati wa kutathmini zabuni ya umeme wa dharura, kwa hoja za kitaalam kuwa haifai kwa vigezo vyote muhimu.
Walipofika mbele ya Kamati Teule, wakawa wapambe nambari moja wa kampuni hiyo, wote wakiimba sifa za kulazimisha za kampuni hiyo!
Aidha, nyaraka nyingi ambazo Kamati Teule ilizipata toka Serikalini na taasisi mbali mbali, zilikuwa nakala zilizokosa mtiririko wa kimasijala. Kamati Teule ilipodai nyaraka halisi kulinganisha na nakala ilizokuwa nazo, ilipewa majalada yaliyoonyesha dalili zote za kukarabatiwa.
Mheshimiwa Spika, hali hii ilijitokeza zaidi kwa TANESCO na Wizara ya Nishati na Madini. Jalada halisi kutoka TANESCO lilichukua siku tatu kuifikia Ofisi Ndogo ya Bunge likiwa na nyaraka zenye namba zilizokosa mtiririko stahili.
Wizara ya Nishati na Madini ndiyo iliyotia fora kwa kumtuma Msaidizi wa Katibu Mkuu, Ndugu Julius Sarota tarehe 18 Disemba 2007 akiwa na maagizo ya kuwafungulia Wajumbe wa Kamati Teule kurasa maalum tu na si nyinginezo hivyo kuinyima Kamati Teule mtiririko halisi wa mawasiliano.
Kamati Teule haikuridhishwa na utaratibu huo, hivyo ilimtaka Msaidizi huyo wa Katibu Mkuu aondoke na majalada yake na kumpelekea hati ya kuitwa Katibu Mkuu, Ndugu Arthur Mwakapugi afike yeye mwenyewe na majalada hayo.