Katika hotuba yake ya kufunga mwezi wa kumi Rais Kikwete hakuzungumzia vifo vya watoto 19 Tabora, wala ripoti ya Mkuu wa Mkoa wala mpango wa kutekeleza mapendekezo ya ripoti ile ili tukio hilo lisijuridie tena katika mazingira yale yale. Akazungumza mengi isipokuwa watoto 19! Nimedokewa kuwa alisahau!
Katika mjadala wa wabunge wa JMT kwa wiki mbili wakiwa Dodoma, mjadala ulioanza mwishoni mwa mwezi wa kumi sijui ulifunguliwaje lakini hakukuwa na mjadala motomoto kuhusu mazingira yaliyosababisha vifo vya watoto wale na kelele za kutaka wahusika wote wawajibishwe kwa mujibu wa ripoti na hata kuitisha uchunguzu huru zaidi (ambao ungechunguza ofisi ya mkuu wa mkoa na Mkuu wa Polisi). Hawakufanya hivyo; Wakazungumza mengi kweli isipokuwa ya watoto 19 au hata kutaka ile ripoti ijadiliwe Bungeni. nimeambiwa wabunge karibu 320 (wa CCM na wa UPinzani) walisahau vifo vya watoto hao!
Wakati wa hotuba yake ya kuliahirisha Bunge Waziri Mkuu Pinda naye alizungumza kwa kirefu lakini kama wenzake na yeye hakugusia kabisa vifo vya watoto wale 19 na wengine kujeruhiwa katika mazingira ya kizembe, aibu na ya kutokuwajibika kama yale tena siku ya Sikuu kubwa ya Idi El Fitr. Akazungumza mambo mengi ya kusifia shughuli za Bunge na kuuza utendaji kazi wa serikali yake. Lakini na yeye kama wenzake hakugusia vifo vya watoto 19 Tabora. Naambiwa na yeye alipitiwa.
NIkasema labda waandishi wetu wanaweza kukumbuka; na wao vile vile wakasahau hata kuhoji kwenye magazeti kwanini Rais, Bunge, Waziri Mkuu hawakuzungumzia vifo vya watoto 19 Tabora? Nikajiuliza kwanini waandishi wa habari hawakuichambua ripoti hiyo, kuhoji maswali na kupiga kelele watu wawajibishwe. Nikaambiwa na wao wamesahau!
Nikasubiri kwenye mtandao maarufu wa Watanzania kuona kama kuna mtu hata mmoja aliyeona mapungufu hayo kwenye hotuba ya Rais, ya Waziri Mkuu, mjadala wa Bunge na kwenye Magazeti. Hakuna aliyekumbuka vifo vya watoto hawa. Nimeambiwa wote wamesahau.
Nikabakia najiuliza, kwanini ninakumbuka? Nikaenda kutafuta majibu. Nilipoyapata na kujua kilichomo nikajikuta na mimi naletewa vidonge viwili nichague kimoja chekundu kingine cha bluu:
Nikaambiwa kwa maneno ya Morpheus katika Matrix:
You have to see it for yourself. This is your last chance. After this there is no turning back. You take the blue pill, the story ends, you wake up in your bed and believe whatever you want to believe. You take the red pill, you stay in Wonderland, and I show you how deep the rabbit hole goes. Remember, all Im offering is the truth, nothing more
Sasa mimi kama vile ilivyokuwa kwa Rais, Bunge, Waziri Mkuu, Waandishi, na wanachama wa mitandao mbalimbali ya Wabongo na wananchi kwa ujumla natakiwa nami nifanye uamuzi. Uamuzi ambao nitaishi nao. Naamini kuwa kidonge cha bluu kitakomesha hii njozi mbaya. Chekundu hata hivyo kinahitaji ujasiri maana unaweza kujikuta uko peke yako katika tandabui ya njama ya ukimya!