Analogia Malenga
Platinum Member
- Feb 24, 2012
- 5,292
- 10,842
RISALA YA CHAMA CHA WALIMU TANZANIA KWA MGENI RASMI
MH. MAJALIWA KASIM MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE KONGAMANO LA SIKU YA WALIMU DUNIANI - OKTOBA 05, 2020 KATIKA UKUMBI WA LAPF- MAKOLE
JIJINI DODOMA
MH. MAJALIWA KASIM MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE KONGAMANO LA SIKU YA WALIMU DUNIANI - OKTOBA 05, 2020 KATIKA UKUMBI WA LAPF- MAKOLE
JIJINI DODOMA
Mheshimiwa Majaliwa Kasim Majaliwa (MB), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jenister Mhagama (MB), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge, Sera, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu
Mheshimiwa George H. Mkuchika (MB), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma,
Mheshimiwa Seleman Jafo (MB), Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),
Mheshimiwa Joyce Ndalichako (MB), Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,
Mheshimiwa Anthony P. Mavunde (MB), Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu,
Komred rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA),
Komred Mwl. Leah Ulaya, rais wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT),
Mheshimiwa Dr. Binilith Mahenge, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,
Komredi Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA),
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,
Katibu Mkuu Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu,
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,
Kamishna wa Kazi,
Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi Tanzania,
Katibu Mtendaji Tume ya Utumishi wa Walimu
Waheshimiwa Viongozi wa Serikali mliohudhuria katika kongamano hili,
Makomredi Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi mliohudhuria kutoka ndani na nje ya Tanzania,
Waandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana.
Itifaki imezingatiwa.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, awali ya yote tunapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na hivyo kutuwezesha kuhudhuria Kongamano hili. Aidha tunatumia fursa hii ya kipekee kukushukru wewe binafsi kwa kukubali mwaliko wetu na kuweza kujumuika na walimu wenzako katika ufunguzi wa Kongamano hili. Pia, tunawakaribisha na kuwashukru wote kwa kukubali kuja kushiriki nasi katika Kongamano.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Siku ya walimu duniani husherehekewa duniani kote kila tarehe 05 mwezi wa Oktoba ili kuenzi mchango mkubwa wa Walimu katika kuelimisha dunia lakini pia kujadiliana kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili Walimu na kupanga mikakati ya kukabiliana nazo. Kauli mbiu ya maadhimisho haya kwa mwaka huu 2020 ni “Walimu, huongoza katika mazingira magumu wakifikiria siku zijazo “(teachers: leading in crisis reimagining the future). Kauli mbiu hii inatusaidia kukumbuka kuwa Walimu mahali pengi duniani wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu lakini bado wameendelea kufikiria mustakabali mwema wa nchi zao katika kuhakikisha jamii inapata Elimu iliyo bora.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Chama cha Walimu Tanzania, kimekuwa pia kikiadhimisha siku hii kwa shughuli mbalimbali ambapo kwa mwaka huu kimeandaa kongamano hili kwa lengo la kujadiliana masuala mbalimbali yahusuyo elimu na ualimu. Kauli mbiu ya kongamano hili ni
“ELIMU BORA KWA MAENDELEO YA TAIFA”.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Chama cha Walimu Tanzania, kipekee tunamshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili Walimu. Tangu alipofungua mkutano wetu mkuu wa uchaguzi tarehe 05/06/2020 aliahidi kutatua changamoto hizo na tumeendelea kuona utekelezaji wa maagizo yake. Tumeshuhudia madai ya walimu yakilipwa akiwemo malimbikizo ya mishahara, na mfumo mpya wa malipo ya madai yasiyo ya mishahara kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa. Tunaimani kubwa sana maelekezo ya Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya Walimu waliyokasimiwa kupandishwa vyeo kwa mwaka wa fedha 2019/2020 yatatekelezwa.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Tunaipongeza Serikali kwa kuboresha miundo mbinu na kukarabati shule kongwe pamoja na vyuo vya Ualimu. Pia kwa kuhakikisha samani zinapatikana za kutosha kwenye taasisi hizo. Lakini pia tunatambua jitihada za Serikali kuwapunguzia mzigo wa vipindi walimu wetu kwa kutangaza ajira za walimu 13,000.
Tunatambua nia njema ya serikali katika kuboresha Elimu kwa kufuta Ualimu wa ngazi ya Cheti, lakini tunaiomba serikali kutoa muda wa kutosha kwa Walimu wenye ngazi ya cheti kujiendeleza. CWT kilianza mapema kuwainua wanachama wake kielimu kupitia mradi wake wa diploma ya elimu ya awali unaotekelezwa katika Wilaya za Chemba na Mpwapwa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Huku Serikali ikishirikiana na Chama Cha Walimu Tanzania katika mradi huu ambao umekuwa wa manufaa makubwa kwa Walimu wetu.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Chama cha Walimu Tanzania kinaamini kupitia kongamano hili tutapata fursa ya kujadili kwa upana mafanikio na changamoto zinazoikabili sekta ya elimu nchini na kupendekeza na kushauri namna bora za kukabiliana na changamoto hizo.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Tunaomba utupelekee salamu za upendo wa dhati kwa Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, “Mwambie Walimu wenzake tunampenda sana, na kwa kipindi hiki hatutamuangusha!
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Chama cha Walimu Tanzania kitaendelea kushirikiana na serikali katika Nyanja mbalimbali ili kukuza kiwango cha elimu nchini.
Mwisho, Mheshimiwa mgeni rasmi, tunakushukuru sana kwa kukubali mwaliko wetu wa kuja kutufungulia kongamano letu.
Mungu akubariki sana na akujalie afya njema wewe na familia yako.
MSHIKAMANO DAIMA!
Nawasilisha,
Mwl. Deus G. Seif
KATIBU MKUU CHAMA CHA WALIMU TANZANIA
PIA SOMAKATIBU MKUU CHAMA CHA WALIMU TANZANIA
= > Siku ya Mwalimu Duniani: Janga la CoronaVirus laongeza changamoto zaidi kwenye sekta ya Elimu