Riwaya: Bondia

Riwaya: Bondia

Mkuu casuist.... wengine usingizi wetu upo jf! Tafadhali tufanye tulale kwa raha leo. Tuwekee angalau chapter moko tu
 
RIWAYA: BONDIA
MTUNZI: HUSSEIN ISSA TUWA


SEHEMU YA KUMI NA TATU

“Hey, vipi...nimechelewa sana nini?” Kate alisema huku akimtazama Roman akiwa amesimama kando ya ile meza waliyokuwako, macho yake yakahamia kwa Inspekta Fatma, yakarudi kwa Roman na kuyarudisha tena kwa Inspekta Fatma, na mara moja akamtambua.
Wale wanamama walitazamana kwa muda, kisha Kate akamtupia Fatma salamu. Lakini inaelekea Fatma hakuwa na muda wa kusalimiana, na badala yake alimgeukia tena Roman kwa ghadhabu. Lakini kabla hajasema alichotaka kusema, Roman akamgeukia Kate.
“Ah, Kate! Wala hujachelewa. Tena ndio umefika katika muda muafaka haswa, kwani Inspekta Fatma hapa nd’o alikuwa anaaga.” Roman alisema, kisha hapo hapo akamgeukia Inspekta Fatma, “Kwa heri Inspekta, na...usikose kuhudhuria mapambano yangu yajayo, okay?”
Kate akavuta kiti kingine kilichokuwa pale mezani na kuketi. Inspekta Fatma alimtupia Roman jicho la ghadhabu, kisha akainuka huku bado akiwa amemkazia macho Roman.
“Huu mjadala haujaisha Roman!” Alisema kwa hasira, kisha akapachika kofia yake ya kiaskari kichwani, akageuka na kuondoka kikakamavu. Kwa muda Kate na Roman walibaki wakiukodolea macho mgongo wa yule askari wakati akiondoka eneo lile, kisha Kate akamgeukia Roman.
“Inahusu nini hii Roman?”
Roman alibaki akitabasamu huku akiendelea kumtazama Inspekta Fatma akiondoka eneo lile.
“Inahusu askari aliyeshindwa kupata akitakacho kutoka kwangu!” Roman alimjibu huku bado akitabasamu.


***


Siku zilizofuatia mkabala ule baina yaje na Inspekta Fatma zilikuwa za mishughuliko sana kwa Roman na bondia Deus “deadly” Macha. Baada ya waandishi wa habari kuzidi kuandika habari za Roman magazetini, wengi wao wakipewa motisha wa kufanya hivyo na Dan Dihenga, promota wa bingwa wa dunia Deusdelity Macha alimuandalia pambano jingine dhidi ya bondia kutoka Kenya, ambaye alipigwa kwa Knock-out mnamo raundi ya sita. Magazeti yakaandika sana kuhusu ushindi ule wa Deus na kidogo akarudi tena kwenye vyombo vya habari.
Dihenga naye akamuandalia Roman pambano jingine la kimataifa, safari hii akipata mpinzani kutoka Zimbabwe. Ilipofika raundi ya nne kwenda ya tano Mzimbabwe akagoma kurudi ulingoni, kipigo alichokuwa akipokea kutoka kwa Roman kilikuwa kizito sana, na refa akasitisha pambano, Roman akatoka mshindi!
Ushindi wa Roman nao ukaandikwa kwa sana na vyombo vya habari, ukielezewa kuwa ni ushindi wa aina yake katika historia ya ndondi, kwani haijawahi kutokea bondia kugoma kurudi ulingoni akihofia kipigo kutoka kwa mpinzani wake.
Sasa ikawa Deus anapambana, anashinda. Roman naye anapamana, anashinda. Ilikuwa kama kwamba kila mmoja anamtumia ujumbe mwenzake kwa kumpiga mpinzani anayepambana naye. Ikiwa ni pambano la Roman, Deus naye hakosi kwenda ukumbini kushuhudia. Na Roman naye ikawa hivyo hivyo, siku Deus akipambana naye hakosi ukumbini. Hali hii iliendelea hata kwa mapambano yaliyokuwa yakifanyika nje ya nchi, ambapo Roman na Dan walisafiri hadi nje ya nchi kushuhudia mapambano ya Deus.


Kutokana na umahiri wake ulingoni, Roman akapachikwa jina la bondia asiye na mpinzani. Jambo hili lilimkera sana Promota wa Deus kiasi cha kuita mkutano na waandishi wa habari, akisema kuwa anashangaa kuwa mabondia wasio na ubingwa wowote wasemekane kuwa hawana wapinzani wakati mabingwa wapo. Deus pia alikuwapo kwenye mkutano ule wa waandishi wa habari, na alipoulizwa juu ya hilo, alisema kwa dharau na kujiamini.
“Dunia nzima inajua kuwa mimi ndiye bingwa wa dunia...hakuna mwingine katika uzito wangu. Sasa kama kuna mabondia wasio na wapinzani, basi ni wazi hao hawana hadhi ya kuwa mabondia, watafute michezo mingine tu wacheze...kuna netiboli, marede...kuruka kamba, kombolela au mdako...yaani michezo ni mingi tu sio lazima ndondi.”
Sasa ikawa ni uhasama wa wazi baina ya mabondia Deus na Roman. Waandishi wa habari hawakufanya ajizi, walimfuata Roman mazoezini kwake na kumuuliza ana kauli gani juu ya yale maneno ya Deus.
“Mimi huwa sipigani kwa maneno...napigana ngumi ulingoni. Sasa kama kuna mtu anayetaka kujua iwapo mimi nina hadhi ya kuwa bondia au vinginevyo, apande nami ulingoni tu. Hapo ndipo kila kitu kitakuwa wazi, au unaonaje mwandishi?”
Loh, jibu la Roman likaleta mjadala mzito miongoni mwa wapenzi wa michezo, hususan ndondi. Swala kubwa sasa likiwa ni nani mbabe kati ya Deus na Roman.
“Naona sasa mambo yanaenda kama tulivyokuwa tukiyatarajia Roman...wananchi wanataka mpambano baina yako na Deus sasa!” Mark Tonto alimwambia Roman.


“Yeah...na ndicho nilichokuwa nikikitaka...mambo yanaelekea kule tulipotaka yaelekee Mark...muda si mrefu azma itatimia...muda si mrefu!” Roman alijibu huku uso wake ukionesha azma ya wazi.
Mwezi mmoja baadaye Roman akaandaliwa pambano jingine la kirafiki na bondia wa hapa hapa nchini. Pambano lilifanyika ndani ya ukumbi wa hoteli marufu ya Ubungo Plaza, ambapo ulingo wa kisasa uliwekwa maalum kwa pambano lile. Kutokana na ushabiki wa mchezo ule, ukumbi ulifurika kweli kweli siku ya pambano, na kama kawaida yake, Deus na promota wake walifika ukumbini.
Pambano lilikuwa kali sana, na bondia mpinzani alitoa upinzani wa hali ya juu kwa Roman, huku mashabiki wake wakimshagilia kwa nguvu. Mpaka raundi ya sita wote walikuwa nguvu sawa. Kutokea kule ulingoni Roman alimuona Deus akiwa na tabasamu la kejeli, akiona kuwa Roman alikuwa amewekwa katika wakati mgumu na yule bondia asiye na jina hata kidogo. Ghadhabu zilimpanda. Raundi ya saba Roman aliingia kwa nguvu na akitumia mtindo tofauti kabisa wa upiganaji na ule alioanza nao. Yule bondia ambaye tayari alishajiona kuwa ameusoma mchezo wa Roman alichanganyikiwa vibaya sana, na ndipo Roman alipomporomoshea masumbwi mazito na ya mfululizo ambayo hakuweza kuyahimili. Akawa anatupa ngumi ovyo, ngumi ambazo Roman alizipisha kirahisi sana huku akizidi kumtandika ipasavyo. Ndani ya ile raundi ya saba, Roman aliyumba kushoto na kumgusa mpinzani wake kwa ngumi nyepesi ya kulia, jamaa akayumba kushoto kuikwepa, na hapo ndipo Roman aliyejawa ghadhabu sio kwa mpinzani wake bali kwa Deus aliyekuwa akijichekesha kwa dharau nje ya ulingo, alipomvutia ngumi ya kushoto aliyokuwa inaenda kuua.
Nje ya ulingo Mark Tonto aliona kile ambacho Roman alikuwa anataka kukifanya, na aliinuka huku akimpigia bondia wake ukelele, “Roman Noooo!”


Ngumi ya kushoto ya Roman ilikuwa ikimshukia yule mpinzani wake aliyeleweshwa masumbwi, na katika sekunde ya mwisho kabisa, Roman aliirudisha nyuma ngumi ya kushoto, na hapo hapo alimchimbua yule mpinzani kwa upper cut ya mkono wa kulia.
Jamaa alienda chini kama mzigo na kutulia huko huko. Ukumbi ulilipuka kwa hoi hoi na shangwe. Nje ya ukumbi Mark Tonto alishusha pumzi za faraja na kuketi kitini akishuhudia jinsi watu walivyokuwa wakishangilia ushindi mwingine wa Roman. Kule ulingoni Roman wala hakuwa akizisikia zile shangwe, mishipa ilikuwa imemtutumka kwa ghadhabu wakati akienda kutulia kenye kona muafaka, wakati refa akimtangaza mshindi kwa knock-out.
Hoi hoi na vifijo vilirindima huku na huko. Roman alienda hadi ule upande ambao Deus na promota wake walikuwa wameketi na kumnyooshea ngumi Deus, kisha akajiashiria alama ya mkanda wa ubingwa kiunoni mwake na kujipiga-piga kifuani kibabe.
E bwana we!
Deusdelity Macha alichachamaa na kusimama kutoka pale alipokuwa ameketi.


“Nini wewe! Unataka mkanda wangu? Unadhani unaweza kuchukua mkanda wangu wewe?” Alipiga kelele huku akijaribu kuparamia ulingoni, wapambe wake wakimzuia na kumrudisha pale alipokuwa amekaa. Roman alibaki akimtazama huku akimcheka kwa dharau.
“Wewe huna ubavu wa kuchagama na mimi wewe!” Deus alibwata kwa hasira akiwa nje ya ulingo. “Mimi ndio bingwa wa dunia na hakuna anayeweza kunivua ubingwa huu!” Deus alizidi kujigamba kwa jazba. Roman alimcheka sana, kisha akamnyooshea kidole na kumfanyia ishara ya kuonesha kuwa alikuwa akiongea sana.
Ukumbi ulilipuka kwa shangwe na hoi hoi mpya, jina la Roman likirindima kila kona.
Wakati Deus aliondolewa ukumbini kwa kubururwa na wapambe wake, mwenyewe akitaka kupanda ulingoni kukabiliana na Roman, mwenzake aliondoka akiwa amebebwa juu juu na wapambe wake.


Kutokea kwenye kona moja ya ukumbi ule, Inspekta Fatma alikuwa akifuatilia kila kilichokuwa kikitokea pale ukumbini kwa umakini wa hali ya juu, uso wake ukionesha kusikitishwa na kile alichokuwa akikiona.
“Sasa kwa nini pale ulipiga kelele kumwambia Roman No? Yaani hukutaka ashinde... au...? Sikuelewa kabisa pale!” Kate alimuuliza Mark Tonto baadaye usiku ule wakiwa kwenye kambi yao baada ya pambano. Mark alimtupia jicho la wizi Roman, ambaye aligeuza uso wake pembeni.
“Yeah...hata mimi sikukuelewa pale coach...nini ilihusu ile?” Dan Dihenga alisaili. Mark Tonto aliguna kidogo na kukaa kimya kwa muda.
“Unajua pale niliona kabisa kuwa Roman alikuwa akipigana kwa hasira zaidi kuliko busara...ni hatari sana namna ile...na mabondia wengi hupoteza mapambano kwa kuruhusu hasira ziwatawale ulingoni...lakini nashukuru nilipompigia kelele alinielewa na akajirekebisha, na tukashinda pambano!” Hatimaye Mark alifafanua, muda wote alipokuwa akitoa maelezo yale, macho yake yalikuwa yamefungana na yale ya Roman. “Sasa unaona Roman? Jazba itakuja kutuaibisha bwana!” Dan Dihenga alidakia. Roman alimtazama kidogo, kisha bila ya kujibu kitu, alirudisha macho yake kwa Mark na kubaki wakitazamana kwa muda. Baina yao, walijua kuwa ile sio sababu iliyomfanya Mark apige ule ukelele wakati Roman alipokuwa akipigana pale ulingoni usiku ule.


***


Siku mbili baadaye, Dan Dihenga aliitisha mkutano wa waandishi wa habari, na katika mkutano huo, alitangaza rasmi nia ya bondia wake asiye na mpinzani, Roman, kuwania mkanda wa ubingwa wa dunia katika uzito wa Super Middle. Mkanda ambao ulikuwa ukishikiliwa na bondia Deusdelity “deadly” Macha.
Kilichofuatia hapo ni malumbano makali kupitia vyombo vya habari baina ya Deus na Roman, Deus akijitamba kuwa Roman hana uwezo wa kupambana naye hata kidogo, Roman akiendelea kusisitizia kauli yake kuwa yeye ni bondia anayepigana kwa ngumi ulingoni na si kwa maneno redioni na magazetini. Na katika malumbano haya, kila mmoja alijikusanyia mashabiki lukuki, wale waliokuwa wakimshabikia Deus hapo awali, sasa walipata wapinzani waliokuwa wakimshabikia Roman. Sasa na malumbano yakahamia kwa mashabiki, na homa ya mpambano baina ya Roman na Deus ikazidi kupanda. Swala kubwa likiwa ni je itatokea siku wawili hawa wakapambana uso kwa uso ulingoni? Hii ilitokana na ukweli kwamba si Roman pekee aliyekuwa akiuwania ule mkanda wa Deus. Kulikuwa kuna mabondia wengine waliokuwa wakiutaka ule mkanda wa Deus duniani. Ndipo hatimaye, shirikisho la mchezo wa ngumi duniani, lilipopitisha uamuzi wa kumpambanisha Roman na bondia Sergoyev “the hulk” Sucuchev kutoka Serbia, ambaye naye pia alikuwa akiuwania mkanda ule. Mpambano ulipangwa kufanyika katika ukumbi wa hoteli kubwa na maarufu ya The Conrad, kandokando ya mto Nile, ndani ya jiji la Kairo, nchini Misri. Pambano lilipangwa kufanyika miezi miwili baada ya Roman kutangazwa kuwania mkanda wa Deus.
Mshindi katika pambano hili angeondoka na kiasi cha dola za kimarekani zipatazo elfu kumi na saba, na ndiye ambaye angepambana na bingwa wa dunia Deus “deadly” Macha kutoka Tanzania.
***


***ROMAN kuzipiga na THE HULK je atafanikiwa kumwangusha na kisha kupambana na DEUS MACHA???
***NINI KISA CHA KUCHUKIANA…NINI KISA CHA ROMA KUHUKUMIWA NA KISHA KUTUMIKIA KIFUNGO CHA MIAKA MIWILI JELA???


ram BPM Sangomwile Mamamercy jonnie_vincy Khantwe mbalu byb sac mlyn VAN HEIST nrango mangimeza muuza ubuyu Jullie ZIgunga Mojaculbby mugaru
 
Casuist....siondoki hapa mpaka nione pambano kati ya Roman na huyo mserbia
 
Last edited by a moderator:

SEHEMU YA KUMI NA NNE


Ndipo hatimaye, shirikisho la mchezo wa ngumi duniani, lilipopitisha uamuzi wa kumpambanisha Roman na bondia Sergoyev "the hulk" Sucuchev kutoka Serbia, ambaye naye pia alikuwa akiuwania mkanda ule. Mpambano ulipangwa kufanyika katika ukumbi wa hoteli kubwa na maarufu ya The Conrad, kandokando ya mto Nile, ndani ya jiji la Kairo, nchini Misri. Pambano lilipangwa kufanyika miezi miwili baada ya Roman kutangazwa kuwania mkanda wa Deus.
Mshindi katika pambano hili angeondoka na kiasi cha dola za kimarekani zipatazo elfu kumi na saba, na ndiye ambaye angepambana na bingwa wa dunia Deus "deadly" Macha kutoka Tanzania.
***
Sergoyev Sucuchev, kama jinsi ambavyo jina lake la kimichezo "the hulk" lilivyomnadi, alikuwa ni bondia mwenye mwili mkubwa, akimzidi urefu Roman kwa inchi tatu, na alikuwa amejichora tojo, au tatoo, nyingi mwilini. Alikuwa na historia ya mapambano kumi na saba ya kimataifa, kumi kati ya hayo akiwa ameshinda kwa knock-out, manne kwa pointi, mawili suluhu na kupoteza moja.
Siku ya pambano, The Conrad ilifurika mashuhuda kutoka kila pembe ya dunia, na kutoka Tanzania, Dan aliweza kutumia uwezo wake kama promota kupata ufadhili wa makampuni maarufu na makubwa nchini ambayo yalidhamini safari ya watanzania wapatao hamsini kwenda Kairo kushuhudia pambano lile, wakiwemo waandishi wa habari.
Na kwa upande wake, promota mpinzani wa Dan Dihenga,alitumia wadhamini wake kugharamia safari yake na bondia wake Deus kwenda Kairo kushuhudia jinsi ndoto ya Roman ya kumvua ubingwa Deus ikisambaratishwa na bondia yule hatari sana kutoka Serbia.
Kwa Roman lile lilikuwa ni pambano kali kabisa miongoni mwa mapambano aliyowahi kushiriki tangu aingie kwenye ndondi za kulipwa. Sergoyev "the hulk" Sucuchev alikuwa na ngumi kali na nzito, na kwa mara ya kwanza Roman alijikuta akipokea masumbwi yaliyomletea kizunguzungu ulingoni. Tangu raundi ya kwanza ya pambano,mabondia wale hawakuwapa nafasi ya kutulia vitini watazamaji wa pambano lile. Ilikuwa ni piga nikupige, na kufikia raundi ya tano mabondia wote wawili walikuwa wakivujwa damu, lakini si kwa kiasi cha kumlazimisha mwamuzi kusimamaisha pambano.
"Roman vipi...naona sasa ubadili mtindo wa upiganaji...huyu jamaa ni mzuri kweli kweli!" Mark Tonto alimwambia bondia wake wakati wa mapumziko kabla ya raundi ya sita. Roman aliafiki kwa kichwa huku akitweta. Kengele ikagonga, na mabondia wakaingia tena ulingoni kuanza raundi ya sita, lakini Roman hakubadili mtindo wa upiganaji ingawa pambano lilikuwa kali zaidi, mabondia wote wawili wakitupiana makonde mazito. Kengele ilipogonga kumaliza raundi, ilikuwa wazi kuwa raundi ya sita ilikuwa nguvu sawa baina ya mabondia wale wawili.
"What's the matter with you Roman? Nimekwambia ubadili mtindo wa upiganaji! Una nini leo? Huyu Mserbia mjinga sana! Unataka atuadhiri hapa? Sisi tumekuja huku ili…"
"Relax Mark! Hana ubavu wa kuniadhiri yule!"
"Usipobadili huo mtindo wako atatuadhiri…"
"Sibadili mtindo Mark!"
"Why, for God's sakes Roman, why?" Mark alipandwa wahka. Kengele ya kurudi ulingoni kwa raundi ya saba iligonga.
"Kwa sababu sitaki Deus aone mtindo wangu mwingine wa upiganaji Mark!" Roman alimjibu, kisha akainuka na kurudi ulingoni.
Raudi ya saba ilikuwa na msisimko wa aina yake, na ukumbi wa hoteli ile maarufu jijini Kairo ulirindima kwa hoi hoi na vifijo kutoka kwa watazamaji. Sergoyev "the hulk" sasa alikuwa amepandwa jazba, kwani naye alimuona Roman kuwa ni mpinzani tata kwake. Alikuwa akimuendea kwa ngumi kali na za mfululizo, wakati Roman aliendelea kumkwepa na kumtandika ngumi za hapa na pale. Ndipo ilipotokea nafasi ambayo Sergoyev "the hulk" asingeweza kuipoteza hata kidogo, pale alipotupa konde zito lililomsukuma Roman mpaka kwenye kamba, kisha akasukumwa tena ulingoni na zile kamba akionekana kabisa kuwa alikuwa amepoteza uelekeo, mkono wake wa kulia ukiwa chini na ule wa kushoto ukiwa umeinuliwa juu. Na hapo, uso wa Roman ukibaki bila kinga yoyote.
Ni nafasi ambayo bondia yoyote duniani huwa akiiombea, na Sergoyev hakufanya ajizi.
Alikwenda mzima mzima, akimtupia Roman konde la kulia lililokuwa limebeba nguvu zake zote nyuma yake. Ukumbi uliachia mguno wa fadhaa ilhali watazamaji wengine, akiwemo Deusdeadly Macha, wakiinuka vitini kwa midadi huku wakiwa vinywa wazi. Kila mtu alijua kuwa sasa Sergoyev alikuwa anamaliza mchezo.
Roman aliliona konde la m-serbia likimjia wazi wazi usoni, na katika nukta ya mwisho kabisa alijipindua haraka kutokea sehemu ya kiuno kwenda juu akilalia kulia kwake, na kwa namna isiyotegemewa, ngumi nzito ya m-serbia ilimkosa kwa kupita kiasi cha milimeta chache sana mbele ya uso wake.
Sergoyev Sucuchev aliachia mguno wa mshangao na wakati huo huo akageuza uso wake kumtazama Roman bila ya kuamini kuwa ngumi yake ilikuwa imemkosa mtanzania yule, na wakati huo huo akipoteza muelekeo na kupepesuka kama mlevi. Sasa Roman alikuwa akiutazama uso wa m-serbia ukiwa hauna kinga yoyote, na hii ndiyo nafasi ambayo yeye alikuwa akiitarajia.
Mkono wake wa kushoto uliokuwa juu muda wote ulishuka na pigo moja lililotukuka, na kushuka kama nyundo usoni kwa m-serbia. Sergoyev Sucuchev alienda chini kama gogo lililooza.
E Bwana we!
Hakika ile ilikuwa ni sucker punch ya hali ya juu na m-serbia hakuiona kabisa ilipotokea.
Ukumbi ulilipuka kwa hoi hoi.
Haraka sana yule m-serbia, ambaye hakuamini kama kweli alipokea pigo kwa mtindo wa ajabu namna ile, aliinuka tena, lakini miguu ikamkatalia na akaenda tena chini kwa kishindo.
Ukumbi ukaachia ukulele mwingine mkubwa.
Sergoyev bado alijitahidi kuinuka tena huku akishikilia kamba za ulingo na kupiga hatua moja…
Refa akamkibilia huku akiumuashiria kuwa atulie.
M-serbia akapiga hatua ya pili…
Sasa ukumbi ulikuwa kimya kabisa, ukifuatilia kile kilichokuwa kikitokea pale ukumbini.
M-serbia akanyanyua mguu kupiga hatua ya tatu…kisha macho yake yakapinduka na kubaki weupe tu, na akapiga mweleka mwingine mzito sana, akisambaratika chali kwenye sakafu ya ulingo.
Kwisha kazi!
Ukumbi ulirindima kwa mayowe yenye mchanganyiko wa hisia wakati refa alipomtazama Sergoyev na hapo hapo kuamua kuwa hawezi tena kuendelea na pambano. Roman akainuliwa mkono juu na kutangazwa mshindi kwa Knock-Out!
Si mchezo!
Hoi hoi, nderemo na vifijio vilitawala pale ukumbini kutoka kwa watanzania na wananchi wa nchi nyingine waliokuja kushuhudia mpambanao ule wa kukata na shoka. Hoi hoi pia zilikuwa zikirindima sehemu mbali mbali nchini Tanzania kutoka kwa watanzania waliokuwa wakiufuatilia mpambano ule wa kimataifa kupitia kwenye chaneli za Supersport na ESPN kupitia kwente runinga zao. Sergoyev Sucuchev aliyepoteza fahamu alitolewa ulingoni akiwa kwenye machela, wakati Roman alibebwa juu juu huku akiwa ameinua ngumi yake hewani, macho yake yakimtafuta Deusdelity Macha pale ukumbini bila mafanikio.
Waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali vya kimataifa walimzonga Roman kwa maswali kem kem juu ya ushindi wake ule. Aliongea kwa kifupi tu kuwa kwake lile ndilo lilikuwa pambano la kugombea mkanda wa ubingwa wa dunia katika uzito wa Super Middle, na kwa ushindi ule ni kwamba tayari yeye alikuwa ndiye bingwa wa dunia.
"Lakini tunavyofahamu sisi ni kwamba mpaka sasa bingwa wa dunia bado ni mtanzania mwenzako Deusdelity Macha, Roman, sasa una maana gani kwa kauli yako hiyo?" Mwandishi wa shirika la habari la Reuters ya uingereza alimuuliza kwa kimombo.
"Ndio Roman… una maana gani? Kwani tujuavyo ni kwamba sasa unatakiwa upambane na bingwa aliyepo, Deusdeadly Macha, na mshindi wa hapo ndiye atakayekuwa bingwa!" Mwandishi mwingine alidakia.
"Kwangu mimi pambano langu na Deus si la kugombea ubingwa!" Roman alijibu kwa kimombo fasaha, kisha akafafanua; "…Kwangu lile ni pambano la sherehe tu ya kunikabidhi mkanda wangu niliojinyakulia leo hii!"
"Hatujakuelewa Roman…" Mwandishi wa chanel ya televisheni ya Al-Jazeera aliuliza. Roman alitulia kwa muda akiwaangalia waandishi wale, kisha akajibu.
"Namaanisha kwamba Sergoyev Sucuchev…the hulk…ni bondia mzuri mara tano zaidi ya huyo Deus…na nyote mmeona jinsi nilivyomfanya hapa!" Kisha akageuka na kuwaacha waandishi wakitupa maswali zaidi ambayo hakujishughulisha kuyajibu.
Sasa azma yake ilikuwa inaelekea kutimia.
***
Siku mbili tu baada ya pambano la kule Kairo, Deus "deadly" Macha alitupa gazeti kwa hasira huku akiachia tusi zito la nguoni, na kusimama kutoka kwenye kiti alichokuwa amekalia na kubaki akitweta huku amejishika kiuno. Promota wake aliyekuwa naye mle ndani alimtupia jicho la mshangao na kuyarudisha macho yake kwenye lile gazeti lililotupwa kwa ghadhabu na yule bondia wake.
"Nini sasa Deus?"
"Ujinga mtupu! Mimi nimuogope Roman mimi?" Deus alimaka kubisha kile kilichokuwa kimeandikwa gazetini.
"Ah, hayo si magazeti tu? Sioni sababu ya kujijaza upepo kwa habari kama hiyo, hao wanataka kuuza magazeti tu!" Promota alimwambia. Walikuwa sebuleni nyumbani kwa Deus. Deus alibaki akiwa amekunja uso bila ya kujibu kitu. Lile gazeti lilikuwa limeandika kuhusu kauli ya Roman aliyoitoa siku ile aliyomuangusha m-serbia Sergoyev Sucuchev kuwa pambano lake na Deus lilikuwa ni la sherehe za kumkabidhi Roman mkanda wa ubingwa ule. Tangu kauli ile itolewe, Deus hakujibu kitu, na ndio maana gazeti liliandika namna ile.
"Sasa kwani ni kweli kuwa we' unamuogopa Roman Deus...?" Promota alimuuliza kwa mashaka. Deus alimgeukia yule promota na kumtazama kwa hasira, kisha akarudi na kuketi kitini.
"Mi' siwezi kumuogopa Roman hata siku moja...haniwezi!"
"Sasa ya nini kujijaza jazba?"
"Kwa sababu we' hutaki nimjibu kashfa zake gazetini bwana! Mi sipendi namna hii...!"
"Kama nilivyokwambia Deus...sasa maneno basi. Tutapambana naye ulingoni tu, kwisha!" Promota alisisitiza.


**HATIMAYE unangojewa ule mpambano mkali kati ya DEUS NA ROMAN…..nini kitajiri…….labda mpambano huu ndo utatoa jibu kuu la riwaya hii….


ram BPM Sangomwile Mamamercy jonnie_vincy Khantweeeeeeeeeeee mbalu byb sac mlyn VAN HEIST nrango mangimeza muuza ubuyu Jullie ZIgunga Mojaculbby mugaru
 
Huyu bondia wa kichaga Macha atapewa upper cut moja tu,chali!
 
Casuist siku ya pambano la Deus na Roman uniarifu mapema ili na mimi nikashuhudie mauaji...
 
Last edited by a moderator:
Back
Top Bottom