Riwaya: Bondia

Riwaya: Bondia

Casuist siku ya pambano la Deus na Roman uniarifu mapema ili na mimi nikashuhudie mauaji...
Khaa, we ulikosa utamu kule Cairo siku ya pambano la 'the hulk' na Roman ilikuwa ni hatari! Yaani lile konde siku hiyo lilituacha mdomo wazi mikono kiunoni! Kuanzia siku hiyo niliacha kabisa kuhudhuria mpambano wa ndondi kama unamhusisha Roman kwani yule jamaa ni mbayaaaa, unaweza ukashuhudia mtu anauwawa kirahisi kabisa!
 
Khaa, we ulikosa utamu kule Cairo siku ya pambano la 'the hulk' na Roman ilikuwa ni hatari! Yaani lile konde siku hiyo lilituacha mdomo wazi mikono kiunoni! Kuanzia siku hiyo niliacha kabisa kuhudhuria mpambano wa ndondi kama unamhusisha Roman kwani yule jamaa ni mbayaaaa, unaweza ukashuhudia mtu anauwawa kirahisi kabisa!

Umeona eeee!!!
 
RIWAYA: BONDIA
MTUNZI: HUSSEIN TUWA


SEHEMU YA KUMI NA TANO


Siku mbili tu baada ya pambano la kule Kairo, Deus "deadly" Macha alitupa gazeti kwa hasira huku akiachia tusi zito la nguoni, na kusimama kutoka kwenye kiti alichokuwa amekalia na kubaki akitweta huku amejishika kiuno. Promota wake aliyekuwa naye mle ndani alimtupia jicho la mshangao na kuyarudisha macho yake kwenye lile gazeti lililotupwa kwa ghadhabu na yule bondia wake.
"Nini sasa Deus?"
"Ujinga mtupu! Mimi nimuogope Roman mimi?" Deus alimaka kubisha kile kilichokuwa kimeandikwa gazetini.
"Ah, hayo si magazeti tu? Sioni sababu ya kujijaza upepo kwa habari kama hiyo, hao wanataka kuuza magazeti tu!" Promota alimwambia. Walikuwa sebuleni nyumbani kwa Deus. Deus alibaki akiwa amekunja uso bila ya kujibu kitu. Lile gazeti lilikuwa limeandika kuhusu kauli ya Roman aliyoitoa siku ile aliyomuangusha m-serbia Sergoyev Sucuchev kuwa pambano lake na Deus lilikuwa ni la sherehe za kumkabidhi Roman mkanda wa ubingwa ule. Tangu kauli ile itolewe, Deus hakujibu kitu, na ndio maana gazeti liliandika namna ile.
"Sasa kwani ni kweli kuwa we' unamuogopa Roman Deus...?" Promota alimuuliza kwa mashaka. Deus alimgeukia yule promota na kumtazama kwa hasira, kisha akarudi na kuketi kitini.
"Mi' siwezi kumuogopa Roman hata siku moja...haniwezi!"
"Sasa ya nini kujijaza jazba?"
"Kwa sababu we' hutaki nimjibu kashfa zake gazetini bwana! Mi sipendi namna hii...!"
"Kama nilivyokwambia Deus...sasa maneno basi. Tutapambana naye ulingoni tu, kwisha!" Promota alisisitiza.
Dakika kumi baadaye promota alitoka na kumuacha Deus peke yake pale nyumbani kwake. Alikaa kimya kwa muda akiwa amejawa na mawazo mazito, akilini kwake akikumbuka siku alipopambana na Roman miaka kadhaa iliyopita... wakati huo wote wawili wakiwa wanajeshi katika jeshi la wananchi wa Tanzania, wote wakiwa mabondia wa ridhaa katika michezo ya majeshi.... Mwili ulimsisimka.
Alikaa vile kwa muda mrefu, kisha akachukua simu yake ya mkononi na kupiga namba ambayo alikuwa akiijua kwa kichwa.
"Ni mimi..." Alijitambulisha kwa yule mtu aliyepokea ile simu, kisha akaendelea, "...sasa nataka nikupe tena ile kazi uliyoshindwa kuitekeleza wakati ule..." Alisikiliza kwa muda, kisha akaongea tena, "...si tatizo pesa yako utapata, ila nataka safari hii kusiwe na makosa bwana...Roman apatwe na ajali mbaya...!" Alisikiliza kwa muda kisha akasema neno moja tu kabla ya kukata simu.
"Okay!"
Wiki moja baadaye shirikisho la ndondi duniani lilitangaza kuwa pambano kati ya Roman na Deus lingefanyika miezi mitatu baadaye, jijini Dar es Salaam.
****
Maisha ya Roman yalibadilika sana baada ya yale mapambano yake mawili ya kulipwa. Aliweza kununua gari zuri la kutembelea na kiwanja ambacho alipanga kuanza kukijenga taratibu. Dan Dihenga naye kama promota wake na Mark Tonto kama mwalimu na rafiki yake nao walinufaika na mamilioni yale aliyoyakumba baada ya kumuangusha m-serbia kule Kairo. Lakini vyote hivi, bado havikuwa lengo la Roman kuingia kwenye ndondi za kulipwa. Lengo lake kuu bado lilikuwa halijatimia, ingawa sasa lilikuwa limekaribia sana.
Baada ya kurejea kutoka Kairo, Roman alipokelewa kwa shangwe sana uwanja wa ndege na mashabiki wa ndondi.
Ushabiki baina ya kambi ya Roman na Deus ukapamba moto maradufu, mashabiki wakiisubiri kwa hamu siku ambayo mabondia wale wawili wenye upinzani mkali nchini wangekutana ana kwa ana ulingoni.
Bondia Deusdelity Macha alikuwa na mkataba wa udhamini na kampuni moja kubwa ya simu za viganjani nchini, ambayo ilisimamia mapambano yake yote, na kumdhamini kwa namna mbalimbali katika vifaa vya mazoezi, mavazi na hata safari zake za kimataifa. Deus kwa upande wake naye alitokea kwenye matangazo mengi ya biashara ya kampuni ile. Sasa ilijitokeza kampuni nyingine ya simu za viganjani ambayo nayo ilikuwa ikigombea soko la watanzania katika uteja wa huduma zake za simu. Matokeo yake makampuni haya mawili yakawa kwenye ushindani mkali wa kibiashara. Dan Dihenga aliona nafasi ya kuwanufaisha yeye na bondia wake katika hili, na hivyo aliweza kuishawishi ile kampuni ya simu pinzani kumdhamini Roman kama sehemu ya upinzani wake na ile kampuni iliyokuwa ikimdhamini Deus. Hoja yake ilipita bila kupingwa.
Na ndipo bila ya yeye mwenyewe kujua, alipofanikiwa kuyaokoa maisha ya Roman kutokana na ajali ya kupangwa ya kugongwa na gari akiwa mazoezini, pale alipoishawishi ile kampuni kudhamini maandalizi ya Roman kwa pambano lake na Deus kwa kumuweka kambini nje ya nchi, kwenye visiwa vya ushelisheli, kwa siku zote mpaka siku ya pambano lake na Deus.
Siku ilipotangazwa kuwa Roman hatokuwapo nchini kwa muda wote hadi siku ya pambano lake na Deus, bingwa wa dunia Deus "deadly" Macha alipokea simu kutoka kwa mtu wake.
"Sorry boss, naona zoezi halitawezekana tena...Roman anaondoka nchini ndani ya siku mbili, nami sina uhakika wa kumpata akiwa mazoezini barabarani ndani ya siku mbili hizi!" Alimueleza. Deus alifura kwa hasira.
"Si bado yuko nchini ndani ya siku mbili? Mtafute, mfuatilie mpaka umpate! Hakikisha jambo linamtokea kabla hajaondoka bloody fool!" Deus alifoka, kisha akakata simu. Alibaki akiwa amefura kwa hasira.
***
Mark Tonto alingia sebuleni kwa Roman pale kwenye nyumba aliyopangiwa na Dan Dihenga kule bagamoyo, na kushusha pumzi ndefu.
"Wheew! Si joto hilo! Nijaalieni maji ya kunywa tafadhali jamani." Alisema. Roman, aliyekuwa amejilaza kwenye kochi aliachia tabasamu pana wakati, Kate aliyekuwa kwenye kochi lile lile alilokuwa amelalia Roman, alijiinua na kwenda kumletea maji Mark.
"Pole sana mzee...vipi za Dar?" Roman alimuuliza.
"Huko shwari tu..." Mark alijibu huku akipokea gilasi ya maji baridi kutoka kwa Kate. Muda huo ulisikika muungurumo wa gari lililokuwa likiegeshwa nje ya nyumba na muda si muda hodi ikabishwa pale mlangoni. Roman na Mark walitazamana.
"Vipi, unatarajia mgeni nini?" Mark aliuliza. Roman alitikisa kichwa.
"Hapana. Dan hatokuja leo, na zaidi yake na sisi tuliomo humu ndani, hakuna mtu mwingine apajuaye hapa!"
Kate alienda kufungua mlango, na mara alipoufungua tu, Roman na Mark walimsikia akiachia mguno wa mshangao. Walitazamana, kisha wote wakakurupuka kuelekea kule mlangoni...
***
"Vipi Kate...hujawahi kuona askari akibisha hodi mlangoni?" Inspekta Fatma, akiwa ndani ya sare zake za kiaskari, alimuuliza huku akiachia tabasamu la upande mmoja. Kate alibaki akimkodolea macho ya kutoamini. Aliishia kujiona sura yake kwenye miwani myeusi ya jua iliyokuwa usoni kwa yule askari.
Roman na Mark walifika pale mlangoni, nao wakabaki wakishangaa.
"Mark...unaendesha gari kwa kasi sana wewe. Hujui kuwa ni hatari kwa usalama wa barabarani?" Fatma alimwambia Mark, kisha akamgeukia Roman, "...siku nyingine ukimuachia kocha wako hili gari lako jipya hakikisha umelifunga kidhibiti mwendo Roman, ama si hivyo utalikuta mtaroni siku moja!"
Roman alimtazama kwa kutoamini yule dada. Mark alikunja uso.
"Khah! Ina maana..." alianza kusema, lakini Fatma alimkatisha. "Ndio hivyo Mark...nimekufuata kwa gari tangu Dar mpaka hapa...vinginevyo ningepajuaje huku?"
"Na kwa nini umepata taabu yote hiyo afande, kama naruhusiwa kuuliza?" Roman alimuuliza kwa hasira. Fatma alimtazama kwa muda.
"Kwa hiyo sikaribishwi ndani?" Akamuuliza.
Roman alimtazama kwa muda kisha akageuka na kurudi ndani kwake, wengine wote wakimfuata ndani. Roman alisimama katikati ya sebule na kumuuliza.
"Okay Fatma, unataka nini tena kwangu?"
"Nahitaji kuongea nawe Roman."
"Ongea nakusikiliza...!"
"Naomba tuongee peke yetu...mimi na wewe."
"Hilo halitawezekana..." Roman alianza kujibu, lakini hapo hapo Mark Tonto akaingilia.
"Eh, mi' na Kate tutakuwa nje kwa muda..."
Roman na Fatma walibaki peke yao pale sebuleni.
"Hongera kwa ushindi wa Kairo Roman..." Fatma alianza.
"Fatma usinipotezee muda. Hukuja mpaka huku eti kunipongeza. Sema lililo kuleta uende zako!"
Fatma alimtazama kwa huzuni, kisha akatikisha kichwa kwa masikitiko.
"Roman, nadhani bado nina wajibu wa kukuasa juu ya pambano lako na Deus...najua utaondoka ndani ya siku mbili kwenda ushelisheli kwa maandalizi, lakini...bado mi' nilikuwa nadhani kuwa hutakiwi kufanya hivyo Roman...bado una nafasi ya kubadili mawazo!"
"Kwa hiyo unachoniambia ni kwamba niite waandishi wa habari halafu niwaambie kuwa nimeamua kujitoa kwenye pambano langu na Deus? You must be crazy Fatma. Mi' sirudi nyuma!"
"Kuna namna nyingi za kulimaliza hili Roman, sio lazima iwe hivyo...unaweza kujitoa kutokana na sababu za kiafya...achana na..."
"No! Sina tatizo la kiafya Fatma..." Roman alimjia juu, kisha akamwambia, "Lakini Fatma, kwa nini unanifuata fuata mimi tu? Kwa nini usiupeleke ushauri huu kwa mtu ambaye atanufaika nao zaidi?"
"Mtu gani sasa?"
"Deus!" Roman alimjibu mara moja, na kuendelea, "Deus ndiye haswa ambaye ungepaswa umpe ushauri huu Fatma, sio mimi. In fact, sasa naomba nikutume rasmi kwa Deus...kamwambie kuwa mimi niko tayari kusahau yote yaliyopita iwapo atatangaza kujitoa kwenye pambano na kuusalimisha mkanda wake kwangu. Akiweza kufanya hivyo, kila kitu kitakuwa sawa!"
Fatma alibaki akimtazama kwa muda mrefu kabla hajaongea.
"Naona umeamua kutimiza ahadi uliyoitoa miaka miwili iliyopita Roman."
"Khah! Mbona sikuelewi...mi' nimekupa ufumbuzi wa hili tatizo halafu..."
"Unajua kabisa kuwa Deus hawezi kukubali hiyo hoja Roman..."
"Ila kwa kuwa mimi -----, tena ----- mtozeni, ndiye ninayetakiwa nikubaliane na huo upuuzi wako? Toka nyumbani kwangu Fatma. Peleka ujumbe niliokutuma kwa Deus, ama si hivyo sitaki nikuone tena mbele ya uso wangu!" Roman alimjia juu. Fatma alimtazama kwa muda mrefu, kisha aliinuka taratibu na kuelekea mlangoni. Alifungua mlango, lakini kabla ya kutoka, alimgeukia tena.
"Okay, Roman. Mi' nimejitahidi kadiri ya uwezo wangu kuokoa ubinaadamu wako Roman..."
"Nashukuru kwa hilo. Sasa naomba uende!"
"...ila tu nataka uelewe kuwa ni ile kauli yako ya mwisho wakati unapelekwa gerezani, na azma niliyoiona wazi machoni mwako wakati ukitoa kauli ile, ndivyo vilivyonifanya nipate taabu yote hii kwa ajili yako...kwa sababu mi' bado naamini kuwa ndani kabisa ya huo moyo wako uliozongwa na chuki, kuna binadamu mwema na mstaarabu. Nahofia kuwa binaadamu huyo yuko mbioni kupotezwa kabisa na ile kauli yako Roman...usiruhusu hilo litokee!" Fatma alimweleza kwa kirefu. Na baada ya maelezo yale, alibaki akimtazama Roman usoni kwa macho makavu. Roman alifunua kinywa kutaka kumjibu, lakini hakupata neno muafaka la kumwambia. Walibaki wakitazamana tu, kisha Fatma akatoka nje, akiufunga mlango taratibu nyuma yake.
Mark na Kate walirudi mle ndani na kumkuta Roman akiwa ameketi ilhali uso wake ukiwa na mawazo mazito.
"Haya, leo amekuja na lipi tena yule askari?" Kate alimuuliza.
"Yale yale tu ndugu zangu...Inspekta Fatma anadhani nitakuwa binaadamu na mstaarabu zaidi kama nikijitoa kwenye kugombea mkanda wa Deus..."
"Ana wazimu...!" Kate alimaka kwa hasira.
"Tena sana..." Roman aliafikiana na Kate, bado uso wake ukiwa na mawazo mazito. Mark alimtazama kwa mashaka, lakini hakusema kitu.
...ni ile kauli yako ya mwisho wakati unapelekwa gerezani, na azma niliyoiona wazi machoni mwako wakati ukitoa kauli ile, ndivyo vilivyonifanya nipate taabu yote hii kwa ajili yako...
"Sasa mmemalizana vipi?" Kate alihoji zaidi.
"Nimemtuma kwa Deus...akamwambie ajitoe kwenye mpambano na asalimishe mkanda wake kwangu..."
"Wacha bwana!" Mark alimaka.
"Ndiyo...! Na akishindwa kufanya hivyo, basi asirudi tena kwangu na ule upuuzi wake!" Roman alimalizia, lakini bado alionekana kuwa kuna kitu kilikuwa kikimsumbua akilini mwake.
Nahofia kuwa binaadamu huyo yuko mbioni kupotezwa kabisa na ile kauli yako Roman...
"Roman, uko sawa lakini...? Mbona nakuona kama kwamba una kitu kinakusumbua?" Kate alimuuliza kwa wasiwasi. Roman alimtazama kwa muda, kisha akamgeukia Mark, halafu akatazama ukutani kwa muda.
...usiruhusu hilo litokee...
"Aam...nadhani nahitaji kuwa peke yangu kwa muda jamani...samahani..." Hatimaye aliwaambia wenzake, na bila kusubiri kauli yao, aliinuka na kuelekea chumbani kwake. Mark na Kate walibaki wakitazamana.
"Usijali...mpe muda atulie kwanza...bila shaka Inspekta Fatma amemkumbusha mambo mengi mazito, lakini atakuwa sawa tu." Mark alimwambia Kate. Kate aliafiki kwa kichwa bila ya kusema kitu.
Chumbani kwake Roman alivuta droo na kutoa picha ya msichana aliyekuwa amesimama kwenye bustani huku akiwa ameachia tabasamu mororo, furaha iliyokuwa moyoni mwake ilikuwa wazi machoni mwake, na ikanaswa sawasawa na kamera. Alikuwa ni binti mrembo aliyepata umri wa miaka kama kumi na minane hivi wakati picha ile inapigwa.
Aliketi kitandani taratibu huku akiitazama ile picha ilhali uso wake ukiwa na simanzi kali, na hapo kwikwi ya kilio ilimtoka bila kutarajia, tone la chozi likiangukia kwenye ile picha.
"Oh, Rachel mdogo wangu! Nisamehe malkia wangu...nilikuacha mikononi mwa shetani mdogo wangu, na sasa haupo tena duniani..." Alibwabwaja huku akilia kwa uchungu. Alilia kwa muda mrefu, kisha alijitahidi kujifuta machozi, na kuitazama tena ile picha, sasa uso wake ukiwa na ghadhabu zaidi kuliko huzuni.


ITAENDELEA..


ram BPM Sangomwile Mamamercy jonnie_vincy Khantwe mbalu byb sac mlyn VAN HEIST nrango mangimeza muuza ubuyu Jullie ZIgunga Mojaculbby mugaru
 
RIWAYA: BONDIA
MTUNZI: HUSSEIN TUWA



SEHEMU YA KUMI NA SITA


Chumbani kwake Roman alivuta droo na kutoa picha ya msichana aliyekuwa amesimama kwenye bustani huku akiwa ameachia tabasamu mororo, furaha iliyokuwa moyoni mwake ilikuwa wazi machoni mwake, na ikanaswa sawasawa na kamera. Alikuwa ni binti mrembo aliyepata umri wa miaka kama kumi na minane hivi wakati picha ile inapigwa.
Aliketi kitandani taratibu huku akiitazama ile picha ilhali uso wake ukiwa na simanzi kali, na hapo kwikwi ya kilio ilimtoka bila kutarajia, tone la chozi likiangukia kwenye ile picha.
"Oh, Rachel mdogo wangu! Nisamehe malkia wangu...nilikuacha mikononi mwa shetani mdogo wangu, na sasa haupo tena duniani..." Alibwabwaja huku akilia kwa uchungu. Alilia kwa muda mrefu, kisha alijitahidi kujifuta machozi, na kuitazama tena ile picha, sasa uso wake ukiwa na ghadhabu zaidi kuliko huzuni.
"...lakini nakuahidi mdogo wangu...nakuahidi, kama jinsi nilivyokuahidi hapo awali Rachel...nitahakikisha kuwa nalipiza kifo chako, nitalipiza kisasi...na muda si mrefu azma hiyo itatimia Rachel...!" Aliiambia ile picha huku akibubujikwa na machozi.
...kwa sababu mi' bado naamini kuwa ndani kabisa ya huo moyo wako uliozongwa na chuki, kuna binadamu mwema na mstaarabu...
"Inspekta Fatma anadai kuwa nikilipiza kisasi nitapoteza moyo wangu wa ubinaadamu na ustaarabu..." Roman alizidi kuongea na picha ya hayati mdogo wake, akaachia mguno wa dharau, kisha akaendelea, "...kitu ambacho haelewi ni kwamba huo moyo wa ustaarabu na ubinadamu ndio uliosabaisha nikuache mikononi mwa shetani, nikiamini kuwa naye ni binadamu na mstaarabu kama mimi Rachel...shetani aliyekuja kukuangamiza mdogo wangu. Hapana Rachel, ni bora nipoteze ubinaadamu na ustaarabu, kuliko kuacha kifo chako kipite bila kulipizwa! Nitalipiza...nitalipiza...na nitalipiza kwa namna ambayo ninaiweza! Hiyo ni azma yangu!" Roman Kogga aliongea kwa uchungu na ile picha ya hayati mdogo wake, Rachel Kogga. Na ndani ya muda huo, matukio ya miaka kadhaa iliyopita yalimrudia kichwani mwake kama kwamba yalikuwa yametokea jana tu...


*****


MIAKA KADHAA ILIYOPITA...


Roman Kogga alikuwa ni miongoni mwa vijana waliojiunga na jeshi la wananchi wa Tanzania baada ya kumaliza masomo yake ya kidato cha sita. Baba yake, ambaye naye alikuwa ni afisa katika jeshi la wananchi wa Tanzania, ndiye aliyekuwa kishawishi kikubwa cha yeye kujiunga na jeshi. Akiwa jeshini, alijiunga na chuo cha usimamizi wa fedha, akisomea shahada ya uhasibu, chini ya udhamini wa jeshi la wananchi. Na wakati akiwa anakamilisha masomo yake, wazazi wake wote wawili walipata ajali mbaya ya gari na kufariki dunia. Ndipo Roman alipojikuta akikabiliwa na jukumu la kumlea Rachel, mdogo wake wa pekee ambaye muda huo alikuwa kidato cha pili. Lakini kwa kuwa tayari yeye alikuwa ana kazi ya uhasibu katika jeshi la wananchi, na wazazi wao waliwaachia nyumba na mali kadhaa, hawakutetereka kimaisha. Roman alimchukua mdogo wake na kuishi naye kwenye nyumba aliyopewa na jeshi, na ile nyumba waliyoachiwa na wazazi wao wakaipangisha. Hivyo maisha hayakuwa na tatizo.
Tangu akiwa shuleni, Roman alikuwa akipenda sana mchezo wa ngumi, na alikuwa akihudhuria mazoezi ya vikundi mbali mbali vya ngumi. Lakini alipata nafasi ya kujiingiza zaidi kwenye ndondi wakati alipojiunga na jeshi. Na huko ndipo alipokutana na Sajini Meja Makongoro "Mark Tonto" Tondolo, ambaye alikuwa ni mwalimu wa ndondi katika jeshi la wananchi wa Tanzania. Roman aliondokea kuwa bondia mzuri sana katika timu ya jeshi, na katika maandalizi ya michezo ya majeshi, Sajini Meja Mark Tonto alimchagua kwenye timu ya kikosi chake. Na hapa ndipo Roman alipokutana na bondia mwingine aliyekuwa akija juu sana katika mchezo ule jeshini, Desudelity Macha.
Baada ya uteuzi wa timu, Sajini Meja Makongoro TAondolo aliinoa timu yake kwa mazoezi makali, na hapa akajionea uwezo mkubwa wa mabondia Roman Kogga na Deusdelity Macha. Moja kwa moja Mark akajua kuwa wawili wale ndio ambao wangekuwa vinara wa timu yake.
Kwa upande wao, Roman na Deus walijenga urafiki haraka sana. Wote walikuwa wakiupenda mchezo ule, na walikuwa wakikutana kila siku kwenye mazoezi. Na katika siku ambazo hakukuwa na mazoezi ya timu yao, wao wenyewe walikuwa wakikutana na kupeana mazoezi mbali mbali. Lakini nyota ya Roman katika ndondi za ridhaa ilianza kuzimika pale ambapo siku moja, wakiwa katika mazoezi ya maandalizi, alipopanda ulingoni na bondia mwenzake katika timu ya kikosi chao, na katikati ya pambano, Roman alichomoa sumbwi la mkono wa kushoto kwa mtindo wa upper-cut, sumbwi lililotua sawia kidevuni kwa mpinzani wake na kumpeleka chini kama puto lililotobolewa.
Jamaa aliaga dunia pale pale!
Heh!
Lilikuwa ni tukio la kushtua sana, ingawa mwisho wa yote lilionekana kuwa ni ajali tu ya kimichezo. Lakini kuanzia wakati ule kocha Mark Tonto alianza kumtazama Roman kwa makini sana. Siku zilipita, mashindano ya michezo ya majeshi yalikaribia, lile tukio likasahaulika, na Roman akapambanishwa na Deusdelity Macha katika mazoezi. Mark Tonto alikuwa makini sana na pambano lile, kwani wapiganaji wale ndio walikuwa vinara wa timu yake, na pambano lao lilikuwa kali sana. Deusdelity alikuwa mpiganaji mzuri sana aliyetoa upinzani mkali kwa Roman. Pambano lilikuwa linaelekea kuwa nguvu sawa, lakini ilipokuwa imebaki raundi moja pambano liishe, Deus alitupa konde kali sana lililokuwa linaelekea usoni kwa Roman. Roman aliyumba, konde likamkosa, na hapo hapo mkono wake wa kushoto ulichomoka na hook iliyotua kwenye taya la Deus, na hapo hapo aliona macho ya mpinzani wake yakitumbukia ndani huku akienda chini kama mzigo!
E bwana we!
Roman alibaki akimshangaa Deus akiwa chini wakati kocha Mark Tonto na wauguzi wakiwahi ulingoni. Dakika chache baadaye Deus alitolewa ulingoni akiwa kwenye machela akiwa hana fahamu.
Si mchezo!
Deus alipona, lakini hakuweza tena kushiriki mashindano ya majeshi ya mwaka ule, kwani alikaa hospitali wiki mbili akitibiwa taya lililovunjika, na baada ya hapo alitakiwa awe nje ya ulingo kwa miezi sita.
"Roman, nadhani unabidi uwe makini sana na hiyo ngumi yako ya kushoto...ningeshauri utumie zaidi ngumi ya kulia, na utumie mkono wa kushoto kujikingia na kutupa ngumi ndogo ndogo tu...inaonekana ni ngumi hatari sana!" Kocha Mark Tonto alimwambia Roman baada ya tukio lile.
"Ah, coach...sasa ndio n'takuwa bondia gani wa kutumia mkono mmoja tu bwana? Mi' naona hili shoto ndio turufu yangu ulingoni bwana..."
"Hapana Roman, hiyo ngumi ni hatari sana...inaua!"
"Aaw, come on coach...ile ilikuwa bahati mbaya tu bwana..."
"No Roman, hii si maskhara. Ona jinsi ulivyomfanya Deus...bahati ile ngumi imemshukia kwenye taya, ingempata juu kidogo tu kichwa, juu ya sikio, nakuhakikishia naye tungemzika!" Kocha Mark Tonto alimwambia kwa hamasa. Roman alibaki akishangaa.
"Kwa hiyo basi unaniambia kuwa niache ndondi kocha!"
"Hapana...ila nataka nikuulize swali moja Roman...je unajua iwapo utotoni mwako ulipata kuchanjiwa mkono wako wa kushoto?"
Roman alimshangaa zaidi yule mkufunzi wake.
"Kuchanjiwa?"
"Ndio Roman...kuchanjiwa! Nasikia kuna makabila ambayo huwa yanachanjia vitu kama hivi...mtu anakuwa na ngumi nzito yenye uwezo wa kuua...je nawe ulifanyiwa kitu hicho Roman?" Mark alimuuliza. Roman alidhani kuwa mwalimu wake alikuwa akimtania, lakini alipomtazama aliona kuwa hakuwa akitania hata kidogo.
"Hapana coach...sina habari ya kitu kama hicho...kama kipo basi wazazi wangu hawakuniambia..." Roman alimjibu kocha wake. "Basi zingatia ushauri wangu." Mark alimwambia na mjadala ukaishia pale. Roman hakuyatilia maanani kabisa yale mazungumzo, kwani kwake kitu cha mtu kuchanjiwa kuwa na ngumi ya kuua hakikumuingia akilini hata kidogo.
Kwa hiyo timu ya kikosi cha Mark Tonto iliendelea na mashindano yale bila ya Deus. Na katika mashindano yale, ambayo ndio yalikuwa ya kwanza kabisa makubwa kwake kushiriki, Roman aliua mtu mwingine ulingoni kwa sumbwi la mkono wa kushoto!


***


Waraka aliopokea kutoka makao makuu ya jeshi ulikuwa unajitosheleza. Kufuatia matukio mawili ya kuua wapinzani wake ulingoni, na moja la kumjeruhi vibaya mpinzani mwingine katika mchezo wa ndondi, Kapteni Roman Kogga, kuanzia tarehe ya waraka ule, alikuwa amezuiliwa kushiriki katika mchezo wa ndondi popote pale ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania.
Ni amri.
Imezuiliwa.
Ndoto za Roman kuwa bondia bora wa ngumi za ridhaa ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania zilikatikia hapo.


***


Roman Kogga aliachana kabisa na ndondi, na kuendelea na utumishi wake ndani ya jeshi kama mhasibu. Lakini muda wote huo urafiki wake na Deus haukutetereka. Alikuwa akienda kumtembelea hospitali na hata alipotoka na kulazimika kukaa nje ya ulingo kwa miezi sita, Roman na Deus walikuwa wakiendelea na urafiki wao. Baada ya kupona Deus alirudi tena ulingoni na kuwa bondia mzuri sana ndani ya jeshi. Walikuwa wakitembeleana na siku za mwisho wa wiki, walikuwa wakienda kwenye kumbi za starehe na kujifurahisha kwa starehe mbali mbali.
Miezi sita baada ya Deus kupona na kurejea ulingoni ndani ya jeshi,Kepteni Roman Kogga alipata udhamini wa jeshi la wananchi kwenda kusomea shahada ya pili ya uhasibu nchini Uingereza. Ilikuwa ni habari ya furaha sana kwake, lakini pia ilikuwa na wingi wa huzuni, kwani ilimaanisha yeye kuwa mbali na mdogo wa pekee wa kike, Rachel, kwa miaka miwili!
Roman aliongea na rafiki yake mpenzi, Deus juu ya hatima ya Rachel wakati yeye akiwa nje ya nchi. Akamuomba amuangalie mdogo wake wakati yeye yuko nje ya nchi. "Usijali partner...Rachel ni mdogo wetu sote bwana, kwa hiyo hatokuwa peke yake. Mimi nitachukua jukumu la kumuangalia katika muda wote ambao hutakuwepo...nenda ukasome salama rafiki yangu, na mungu akujaalie!" Deus alimwambia.
"Loh, ahsante sana partner...ahsante sana. Nilijua kuwa ninaweza kukutumainia rafiki yangu." Roman alimjibu kwa shukurani.
Kufikia wakati huu Rachel alikuwa ameshamaliza kidato cha nne na alikuwa amefaulu kuendelea na kidato cha tano. Kabla hajaondoka, Roman alihakikisha kuwa dada yake ameshapata nafasi kwenye bweni la shule aliyoteuliwa kujiunga nayo jijini Dar, na hivyo Rachel hakulazimika kuishi peke yake nyumbani kwa Roman. Pia alimfungulia akaunti na kuweka maelekezo maalum ya kukatwa sehemu ya mshahara wake kila mwezi na kuingizwa moja kwa moja kwenye akaunti ya Rachel. Siku ya safari ilipowadia, kaka na dada waliagana kwa huzuni.
"Usiwe na wasiwasi Rachel, tutakuwa tukiwasisliana kwa mtandao mara kwa mara...na kama kuna tatizo lolote litakalokuwa nje ya uwezo wako, muone kaka yako Deusdelity...atakusaidia". Roman alimwambia mdogo wake wakiwa uwanja wa ndege.
"Sawa kaka...uende salama..." Rachel alijibu huku akibubujikwa machozi.
"Come on Rachel...sio kwamba Roman anaenda kuuawa huko bwana...anaenda kuongeza elimu kwa faida yenu nyote. Usilie namna hiyo...tumuombee mungu tu huko aendako arudi salama, au sio?" Deusdelity Macha, aliyekuwa pamoja nao pale uwanja wa ndege alimfariji Rachel.
"Najua kaka Deus...lakini..." Rachel alijitahidi kujibu lakini hakuweza kumalizia, alizidi kulia. Roman alimkumbatia mdogo wake kwa muda mrefu, kabla ya kumtazama usoni kwa muda, machozi yakimlenga-lenga, na kumbusu kwenye paji la uso. Aligeuka na kuingia ndani ya uwanja ule bila kugeuka nyuma. Akiwa ndani ya uwanja, ambapo alijua hawataweza kuona jinsi alivyokuwa akitiririkwa na machozi, aligeuka na kuwapungia mkono. Deus na Rachel walimpungia, naye akapotelea ndani ya eneo la kusubiria ndani ya uwanja ule.
Ndio ilikuwa mara yake ya mwisho kumuona mdogo wake akiwa hai...


***


***RACHEL alikufa katika namna gani???
***kumbe ROMA na DEUS walikuwa marafiki??? NINI KILITOKEA WANACHUKIANA KWA SASA


ram BPM Sangomwile Mamamercy jonnie_vincy Khantwe mbalu byb sac mlyn VAN HEIST nrango mangimeza muuza ubuyu Jullie ZIgunga Mojaculbby mugaru
 
Back
Top Bottom