MWINDAJI HARAMU
JF-Expert Member
- Dec 21, 2013
- 210
- 295
Naona tumefika tamati, Shukran kwako chief🙏🙏🙏🙏
Follow along with the video below to see how to install our site as a web app on your home screen.
Note: This feature may not be available in some browsers.
RIWAYA: JANGA
MTUNZI: richard MWAMBE
Akawaonesha gari yake na wote wakaingia humo, Amata akafungua droo ya gari hiyo akatoa fulana moja ya Gina akampa Alinda avae maana hakuwa na nguo upande wa juu baada ya marehemu wale kuilarua. Kasha akachukua kiboksi fulani, akafungua na kutoa sindano ambayo ndani yake ilikuwa na dawa tayari, akajidunga kwenye msuli wa mkono, na kutulia kama dakika mbili hivi, akarudiwa na nguvu zake za awali. Akachukua sindano nyingine akamdunga Mustafa, naye dakika hizo hizo akarudiwa na nguvu yake kama awali.
Amata akahakikisha kila kitu kipo sawa, akawasha gari na kuondoka katika msitu ule.
***
SIKU ILIYOFUATA
Simu ya Madam S ikaita, akaichukua na kuitazama namba akaifahamu mara moja.
“Upo sawa Kamanda?”
“Nipo sawa, tutaongea Madam, sasa naelekea Mahakamani,” akamwambia na kukata simu. Madam S hakuamini kama ameongea na kijana wake ambaye usiku uliyopita hakulala usingizi kwa ajili ya kupotea kwake.
Kamanda Amata akaegesha gari yake nje ya jingo hilo la mahakama, akavaa miwani yake vizuri, akachukua kijibegi chake na kuvuta hatua kuingia ndani ya jingo hilo. Hakupata tabu kuipata afisi ambayo Jaji Tulabayo alikuwa tayari akijiandaa kwenda kwenye kesi.
“Mheshimiwa Jaji, nina mazungumzo mafupi na wewe kama utaniruhusu,” Amata akamwambia huku akimwonesha kitambulisho halisi cha kazi yake. Tulabayo akabaki kimya kama kapigwa shoti ya umeme, aliporejewa na fahamu akamjibu.
“Muda umekwisha kijana, tuonane baada ya shughuli hii”.
“Najua hilo, lakini ninachotaka tuzungumze ni juu ya hilo hilo, dakika chache, naomba uketi,” Amata akatumia ukali, na kuufunga mlango kwa ndani. Tulabayo akaketi kitini na Amata upande wa pili.
“Kama nitakuwa nimevunja taratibu za mahakama na ninastahili kushtakiwa hata kufungwa basi niko tayari baada ya kulimaliza hili,” akafungua mkoba wake na kuto faili moja na kuliweka mezani, “Naomba unipe hukumu yako unayoisoma leo,” akamwambia. Jaji Tulabayo akiwa anatetemeka, akampatia faili linguine Amata.
“Sasa sikiliza, najua na tunajua kuwa umepokea rushwa nzito sana kutoka kwa hawa wafanyabiashara na kigogo mmoja wa serikali, hukumu hii umeipindisha na kuwapendelea wao, hatutaki hicho kitokee. Hiyo niliyokupa, ni hukumu iliyoandikwa na Jaji Shekibindu, tunataka isomwe hiyo na si hii,” Amata akamaliza. Akachukua faili la ile hukumu ya Tulabayo akaitia mkobani na kusimama.
“Nakutakia kazi njema, ukifanya vingine tu, nakupoteza leo hii hii,” alipomaliza kusema hayo, akaufungua mlango na kuondoka zake. Akinua mkono wake na kutumia saa yake kupeleka ujumbe kwa Madam S.
“Nimemaliza sehemu yangu, sasa tusikilize hukumu”.
Madam S akakata kile kijimkanda kutoka katika simu yake na kukitia kwenye mfuko wa suruali aliyovaa. Ndani ya ukumbi wa Mahakama, Gina aliingia kama mwandishi wa habari huku wengine wote wakiwa wamebaki kwenye magari yao wakisikiliza kila kitu kupitia kamera maalum ambayo Gina aliiweka mle ndani. Nusu saa ikapita Jaji Tulabayo hakuingia mahakamani. Mpaka dakika hiyo alikuwa akisubiriwa yeye tu, watuhumiwa walikwishafika na kila kitu kilikuwa tayari. Minong’ono ikaanza kusikika miongoni mwa watu waliokuwepo ndani ya ukumbi wa Mahakama.
***
Upande mwingine wa jiji, Mheshimiwa Waziri Kalembo alikuwa akihangaika kupiga simu ya Kebby bila mafanikio, akajaribu kutafuta kila aina ya mawasiliano ikashindikana, mara mlango wa ofisi yake ukafunguliwa, Alinda akajitokeza na kumsalimu kigogo huyo. Badala ya kuitikia Kaman kawaida yake, akajikuta anakodoa macho, haamini anachokiona mbele yake.
Yeye alikuwa tayari amehesabu kuwa Alinda, Mustafa na Amata watakuwa marehemu muda huo. Mtu kweli au mzimu? Akajiuliza, kasha akainuka na kutoka nje ya ofisi, akaingia katika gari yake na kumwamuru dereva ampeleke shambani haraka sana. Toyota V8 ilifungua mapafu yake na kwenda kwa mwendo wa kasi kuelekea Mabwepande. Haikuwachukua muda wakawasili na kuingia katika uga huo wa ardhi anayoimiliki mheshimiwa.
“Weka gari hapa,” akamwambia dereva kasha yeye akatembea kwa mwendo wa harakaharaka kuelekea ndani ya ghala kubwa. Alipofungua tu mlango ule wa chuma, akakutana na harufu kali ya damu iliyoganda.
“Mh!” akaguna.
Akasogea tena taratibu na kuona kitu ambacho hakukielewa. Ni watu au kitu gani? Akajiuliza, alipoona hakielewi sawasawa kutokana na giza ndani ya ghala hilo, akaisogelea swichi iliyokuwa jirani kabisa na ule mlango aliyoingilia, akaishika kile kidubwasha cha kuwashia, akafikiria na kuacha, kasha akaufunga ule mlango na kuondoka.
“Kila kitu kipo sawa?” dereva wake akamwuliza.
“Hapana, nahisi kama kuna vitu vyangu vimeibwa, inabidi nikachukue poisi waje kuchunguza,” akamjibu dereva wake na kuketi tayari kwa safari.
***
“Kooooorrrrrrrrtttttttttt!!!!!!” iliposikika sauti hiyo watu wotw wakasimama na Jaji Tulabayo akaingia ndani ya ukumbi ule wa Mahakama, akapanda kwenye kijukwaa chake na kuketi nyuma ya meza kubwa iliyochongwa kwa mbao safi, na kunakshiwa ka maua maua, mbele ya meza hiyo kulikuwa na picha kitu kama mzani ambacho daima humaanisha usawa wa kisheria. Akaketi na wengine wote wakaketi.
Mwendesha mashitaka akasimama akiwa amependeza ndani ya suti yake nyeusi iliyotanguliwa na shati safi jeupe. Kabla hata hajaaanza kusoma shitaka lile, macho yake yakagongana na Gina, akajihisi anapata ganzi mwilini, hasira zikaanza kumtawala kichwa chake akamkumbuka mwanamke huyu aliyemlaza usingizi kule Hoteli ya Serena na kumwacha uchi kitandani.
The devil is here again! ‘shetani liko hapa kwa mara nyingine’ akawaza.
“Mwendesha mashitaka!” Jaji Tulabayo akamshtua Danstan Majoti kwa maana alikwishajisahahu na akili yake ikahamia kwa Gina. Kijana huyo akasoma mashitaka yote kama ilivyo ada, alipomaliza zikafuata itifaki za kimahakama kasha ikawa nafasi ya Jaji kutoa hukumu na kuimaliza keshi hiyo.
Katika hali isiyo ya kawaida, Jaji tulabayo alikuwa amelowa jasho mwili mzima, akisoma kwa sauti ya kitetemeshi hati ile ya hukumu. Ilmchukua dakika arobaini na tano kukifikia kipengele kile ambacho ndiyo mwisho wa kila kitu.
“… Mahakama imeamuru, vipodozi vyote vilvyo madukani viondolewe mara moja na wamiliki wa maduka hayo walipwe gharama ya hasara watakayopata. Vilevile kontena zote zilizopo bandarini zinazosadikiwa kuwa na vipodozi hivyo ziteketezwe chini ya uangalizi wa jeshi la polisi. Kutokana na uthibitisho wa idara ya viwango ya serikali kuwa si kontena zote zilizoathirika na mahakama imejiridhisha na hilo, inawatia hatiani Bwana Ankhit na Suleiman na kuwahukumu kifungo cha miaka kumi na tano jela au faini ya shilingi Milioni kumi na tano kila mmoja inayotakiwa kulipwa papa hapa…”
Baada ya hukumu hiyo ndefu, Jaji Tulabayo akafunga faili lake, akainama kidogo kushusha pumzi na kasha akasimama na watu wote wakasimama. Akatoka katika ukumbi wa mahakama na kurudi katika kile chumba alichokuwa mwanzo.
“Umefanya nini Mheshimiwa Tulabayo?” Sauti ya Amata ikasikika kutoka katika kochi kubwa ndani ya chumba hicho.
“Ulitaka nifanye nini kijana? Kila mtu ana namna ya kuendesha kesi yake, Shekibindu aliona hivi na mimi nikaona vile,” akajibu kijeuri.
“Asante kwa nuamuzi wako, asante kwa kuwapa uhuru rafiki zako, kumbuka sheria ni msumeno, inakata huku na kule,” Amata akamaliza na kutoka.
“Nenda bwana, usiniumize kichwa saa hii,” Tulabayo akamwambia Amata huku akimwangalia kijana huyo akipotelea koridoni.
Amata akarudi garini na kuondoka taratibu katika viwanja vya mahakama hiyo huku akishuhudia nje ya mahakama hiyo vurugu ya wananchi kuikataa kabisa hukumu hiyo. Vijana wa FFU walikuwa wakihaha kupiga mabomu ya machozi huku na kule kuwatawanya vijana hao waliobeba mabango makubwa yenye picha za watu walioathiriwa na vipodozi vile.
Madam S akainua simu yake na kuwataarifu vijana wake kuwa huko nje hakufai, hakupitiki kutokana na watu hao.
“Nimemwabia kuwa hiki alichokifanya ni kuhatarisha usalama wa taifa,” Amata akajibu ujumbe ule.
Katika Barabara ya Maktaba na ile ya Bibi Titi, kulijawa na watu, akina mama waliokuwa wakilia kwa uchungu, wakigalagala chini huku wengine wakivua nguo zao kuonesha wanatoa laana kwa serikali yao. Vijana wa FFU walijikiuta wakizidiwa nguvu, pande zote ikaonekana bado watu walikuwa wakiandamana kuja eneo hilo huku wakiimba nyimbo za maazishi na kubeba masanduku yenye picha za marehemu.
Kamanda Amata akateremka kwenye gari na kusimama nje ambako ni moshi tu wa mabomu ya machozi na harufu ya baruti.
Pale wanyonge wanapoikosa haki yao… akawaza na kugeuka kuondoka.
“Unaelekea wapi?” Madam akamuuliza kwa kutumia kifaa chake maalumu alichokiweka sikioni.
“Naenda kumwona Jaji Tulabayo, aje ashuhudie hiki kinachoendelea,” akajibu huku akizikwea ngazi na kuingia ndani Mahakama hiyo, katika moja ya vikorido akapishana na kijana mmoja ambaye sura yake haikuwa ngeni sana lakini hakukumbuka kamuona wapi. Wakatazamana na kupishana hakuna aliyemsalimu mwenzake. Amata akawahi na kufika katika mlango wa afisi ya mheshimiwa Yule, akaingia ndani na kumkuta ameketi kana kwamba anaandika jambo fulani.
“Mheshimiwa! Twende ukashuhudie huko nje,” akamwambia lakini Tulabayo hakushtuka akabaki katulia pale pale, akamwendea na kumgusa paji la uso kumwinua, amekufa.
“Shiiiiittttt!” akang’aka na kutoka mle ndani haraka akawahi, akapita kwa mwendo wa haraka haraka, akatoka nje na kuketi ndani ya gari yake.
“Tunaomba wananchi mtulie!” sauti kutoka kwenye kipaaza sauti ikasikika, na moja ya gari iliyokuwa ikipepea bendera ya taifa, ilifunguliwa juu na akajitokeza Waziri Mkuu. Umati ule ukatulia.
“Kilio kimefika, nilikuwa afisini kwangu lakini imenibidi kuja hapa, ninachowaomba ndugu zangu, mama zangu. Kweli haki yenu inapindishwa siku hadi siku, na hili linasababishwa na viongozi walafi, wapenda pesa…”
“NDIYOOOOOO!!” wakaitikia.
“Sasa basi, ili twende sawa, fanyeni hivi, undeni kamati ndogo ya watu watano ambayo itawawakilisha ninyi na kukata rufaa ili kesi hii isikilizwe upya,” Waziri Mkuu alipomaliza kusema hayo umati wote ukalipuka kwa shangwe, watu wakaanza kutawanyika huku wanasheria wakijitokeza kuunda kamati hiyo bila kuchelewa.
***
Mheshimiwa Waziri wa Usafirishaji alituma askari polisi kutoka kituo cha kati kwenda katika shamba lake huko Mabwepande kufanya uchunguzi, wakateremka na kuweka sawa bunduki zao. Wakiwa katika harakati za kuingia ndani ya ghala hiyo, simu ya upepo ya kiongozi wao ikakoroma.
“Krrrroo! Krrroooo! Nyuki, nyuki,” ikaita.
“Unasomeka,” akajibu Yule kiongozi.
“Hakikisha, usishike kitu chochote, hata swichi ya taa, hakikisha mnafanya ukaguzi kwa kutumia tochi za simu zenu, ova!”
“Copy!!”
Ndani ya jingo lile wale askari wakagundua zile maiti tatu, mbili zikiwa pamoja katika sime na mojaikiwa pembeni, wakapiga picha kila kitu na kupita kwenye mavyumba tofauti na kukagua kila kilichomo. Hakukuwa na cha maana zaidi ya zana za kilimo. Baada ya kujiridhisha wakampa taarifa Mkuu wa Kikosi, naye akampa taarifa waziri huyo.
Taarifa ya kuuawa Kebby na Jalal Nabi iliwamaliza nguvu kabisa watatu hawa, yaani Kalembo, Ankhit na Suleiman. Lakini bado waziri huyo akawahakikishi usalama wao kuwa wasiogope kwani yeye anajua nini atafanya kuwakingia kifua.
***
Ndani ya afisi za AGI Investment, TSA walikutana kutathmini hali nzima ya kesi ile. Pembeni yao luninga ilikuwa ikionesha habari mbalimbali. Mara matangazo yakakatika na maandishi makubwa BREAKING NEWS yakajitokeza. Mwanadada mmoja akapeperusha habari ya kifo cha Jaji Tulabayo, wakaonesha picha mbali mbali za uhai wake Jaji huyo.
“Taarifa zinasema bado haijabainika chanzo cha kifo hicho na uchunguzi unaendelea,” ikamaliza taarifa hiyo iliyokuwa ya dakika tano tu.
“Amata!!” Madam akaita, “Amata umeua, kwa vyovyote, wewe mtoto mi nakujua sana, sasa umefanya nini?” akafoka.
“Hapana Madam! Nimemkuta keshakufa,” akaeleza.
“Hapana, tuliache hilo,” Madam akasema, “Kama ni wewe, safari hii utashughulikiwa…”
“Madam mi sio mpumbavu siwezi kuua mtu kama yule kwa wakati ule,” Amata naye akafoka, kikao kile kikakwa katika mtafaruku, Madam S alibadilika kabisa na kuwa mkali, mwisho akaamua kuondoka zake akimtaka TSA 1 kumpa maelezo ya kutosha juu ya hilo.
“Shiiiiit!” akang’aka Amata na kujitupa kitini kwa nguvu huku sura yake ikiwa imejikunjakunja kwa hasira.
***
“Hii nchi yetu bwana, haya yote yamekwisha,” Kalembo alikuwa akiongea kilevi huku akielekea katika ghala yake huko Mabwepande.
Ukimya ulitawala kila upande, akashuka na kwenye gari na kutembea taratibu akiyumbayumba kwa pombe aliyokuwa akinywa, akaufikia mlango.
“Sisi ndiyo wenye nchiiiiiiiiiiii, tutaila na kuitafuna tutakavyo, mtaandamana weeee, haki yenu ng’o! haki inanunuliwa sheria inauzwa, Watanzania wenzangu vipi?” akaendelea kubwabwaja akiwa peke yake eneo lile.
“Na kesho asubuhi yuleeeeeee Nairobi kula bata na wadau wangu, mnachoma kontena moja, nay ale ishirina saba je, pesa bado ipo!” akaongea huku akipapasa funguo ni ipi ya mlango huo. Alipoipata akafungua na kuingia ndani akapapasa kwa shida na kuipata swichi akabofya kuwasha taa.
Sekunde ile ile alipobonyeza ile swichi, mlipuko mkubwa ukatokea, ukafumua ghala yote, ukateketeza kila kitu, Kalembo akajikuta anashindwa kukimbia kutokana na ulevi ule, akaanguka chini, akajitahidi lakini moto ukamfikia na kumteketeza kama mali nyingine zilizokuwa humo.
Jeshi la zimamoto likawasili lakini hawakuwahi kuokoa chochote ndani ya ghala hilo, zaidi walikuta mwili ule uliokakamaa kwa moto na kuungua vibaya.
OFISI ZA GAZETI LA MBALAMWEZI
Mustafa aliketi kwenye kompyuta na habari tatu muhimu za kuuza gazeti siku inayofuata.
MAHAKAMA YATOA HUKUMU TATA akasoma kichwa hicho na kukikata, kwamba hakipendezi.
Sasa niipe kichwa gani? Akajiuliza.
MWISHO WA UBAYA AIBU, akaandika nacho akakata maana hakuridhika nacho.
HUKUMU YA ANKHIT NA SULEIMAN, WANANCHI WAPAZA SAUTI, akakisoma na kukubaliana nacho kasha akaendelea kuandika vichwa vidogodogo chini yake kuisindikiza habari hiyo.
HUKUMU YA ANKHIT NA SULEIMAN, WANANCHI WAPAZA SAUTI
Yaambatana na vifo vyenye utata
Rushwa yadhihirika kuwa ni janga la taifa
Akina mama walaani serikali
Waziri Mkuu aokoa jaazi
Baada kuandika habari hiyo kwa marefu na mapana, akaiwasilisha kwa mhariri naye hakuwa na shaka, akaitumbukiza kiwandani tayari kuchapa gazeti hilo.
* MWISHO *
aASANTENI KWA KUWA NAMI