RIWAYA : KIAPO CHA JASUSI
SEASON 1
SEHEMU YA 4
MTUNZI: PATRICK CK
MAWASILIANO :0764294499
ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
"Dastan ninakuheshimu sana na hata mimi ninamuonea huruma mzee Dr Alfredo lakini kwa watu hawa ambao wameweza hata kulipua simu wakiwa mbali siwezi kujihusisha na lolote linalohusiana na huyu mzee.Sitaki kuingia katika mapambano na hawa jamaa.Nimenusurika kifo leo hivyo kesho asubuhi na mapema nitaondoka na boti linalokwenda mjini nataka nikatulize kwanza akili yangu" akasema Dr William
"Ninakuelewa Dr William lakini ninakuomba ndugu yangu tusimuache mzee huyu.Mimi na wewe ndio pekee tunaofahamu hatari inayomkabili huyu mzee.I need you William" akasema Dastan na Dr William akainamisha kichwa akawaza kwa muda halafu akasema
"Unahitaji nifanye nini Dastan?Nikusaidie kitu gani?
"Wakati ninatafuta namna ya kufanya,nataka uende ukakae na yule mzee na usiondoke hadi nitakapokuambia vile vile usiruhusu mtu yeyote asiye daktari kuingia katika chumba cha mzee Alfredo"akasema Dastan na Dr William akamtazama kwa muda halafu akasema
"Sawa Dastan.Nitafanya hivi kwa heshima yako ila ninarudia tena kukujulisha kuwa kesho asubuhi na mapema nitaondoka kuelekea mjini.Nimepaogopa sana mahala hapa" akasema Dr William
"Usijali Dr William" akasema Dastan na kuelekea nyumbani kwake.Akachukua simu na kumpigia padre Thadei lakini simu yake haikupatikana tena.Akajaribu tena zaidi ya mara mbili lakini simu haikuwa ikipatikana.
ENDELEA………………
OFISI ZA JARIDA BEAUTIFUL TANZANIA - DAR ES SALAAM
Beautiful Tanzania ni jarida la kila mwezi lililojizolea umaarufu mkubwa kutokana na mkusanyiko wa habari nyingi za kuvutia zilizotokea nchini Tanzania kwa muda wa mwezi mzima.Ni jarida lenye kuandikwa kwa lugha ya kiingereza na lenye kusomwa na watu wengi ndani nan je ya nchi
Licha ya kuwa jarida pendwa Tanzania,hakuna aliyefahamu siri iliyokuwepo nyuma ya jarida hili.Jarida hili lilikuwa chini ya umiliki wa kikundi cha 100CHITAS. Wafanyakazi wa jarida hili walikuwa ni watu waliopata mafunzo makubwa ya ujasusi nje ya nchi na walitumia jarida hili kama mwavuli wa kufunika shughuli wanazozifanya kwa kujifanya ni waandishi wa habari.
Katika chumba kidogo cha mikutano kilicho ghorofa ya tatu katika jengo ziliko ofisi za jarida hili watu kumi walikuwa katika kikao cha dharura
"Ndugu zangu tumelazimika kukutana hapa kwa dharura kufuatia taarifa za kustusha zilizotufikia usiku huu" akasema mtu mmoja mwenye mwili uliojengeka vyema,akavua kofia na kuiweka mezani
"Tulipata taarifa kutoka kwa mwenzetu Chita73 kutoka gereza la Markubelo ambaye alitujulisha kwamba mzee Alfredo ambaye tumekuwa tukimchunguza kwa muda mrefu amempa ujumbe fulani katika karatasi mkuu wa gereza kamishan msaidizi Dastan na kumtaka aupeleke sehemu Fulani na ujumbe huo ulisomeka hivi
"I'm dyind.I have few days left.Meet me before I die"
"Hatujafahamu bado ujumbe huo Dastan ameupeleka kwa nani na hivyo tulihitaji kuipata simu yake ambayo aliitumia kuupeleka ujumbe huo lakini kumetokea kitu cha kustusha sana.Tumepoteza wenzetu nane jioni ya leo ambao niliwatuma kwenda kufuatilia suala hili.Kwa mujibu wa taarifa nilizozipata kutoka ndani ya jeshi la polisi ni kwamba wenzetu wanne walimfuata Dastan baharini alikokuwa anavua samaki lakini Dastan akiwa peke yake aliweza kupambana nao na kuwaua wote kwa risasi.Aliporudi nyumbani alikuta Joyce na wengine Chita40,23,na 37 wakimsubiri.Walimtia nguvuni lakini wakatokea askari magereza wenye silaha wakadhani wale ni wavamizi na kuwashambulia kwa risasi wakawaua wote .Hili ni pigo kubwa sana ambalo hatujawahi kulipata" akanyamaza na kuwatazama wenzake halafu akaendelea
"Hii ni mara ya kwanza tunapata pigo kubwa namna hii.Hatujawahi kupoteza watu wetu wengi namna hii kwa mara moja.Kwa sasa taratibu zinaendelea ili tuweze kuipata miili hiyo ya wenzetu na tuisitiri.Ninaendelea kulifuatilia jambo hili kwa karibu sana lakini wakati tukiendelea kulishughulikia suala hili kuna kazi ambayo lazima ifanyike kwa haraka sana.Tunatakiwa kufahamu nani alipewa ujumbe na Dastan? Tutafanikiwa kulifahamu hili kwa kumchunguza Dastan.Kwa sasa baada ya kilichomtokea leo haitakuwa rahisi sana kumpata hivyo tunatakiwa kutafuta namna nyingine ya kumfanya atueleze mahala alikoupeleka ujumbe ule.Njia pekee ya kuweza kupata taarifa kutoka kwake kirahisi ni kwa kuitumia familia yake.Nataka Dastan achunguzwe tumfahamu chimbuko lake.Tujue wazazi wake wako wapi na kama ana watoto wako wapi?Tukimpata mtoto wake hata mmoja tutafanikiwa kupata kile tunachokihitaji.Ingieni kila mahali,dukueni kila taarifa inayomuhusu Dastan na baada ya saa moja nataka niwe nimepata taarifa kuhusiana na huyu mtu halafu nitatoa maelekezo mengine" akasema Noah Mwamba mkurugenzi mkuu wa jarida la Beautiful Tanzania ambaye pia ni kiongozi mkuu wa kikundi hatari cha 100Chitas.Wote wakatoka mle katika kile chumba cha mikutano na Noah akaelekea ofisini kwake alikuwa na mawazo mengi sana
"Hatujawahi kupoteza watu wengi namna hii kwa wakati mmoja.Hili ni pigo kubwa mno tumelipata.Rais anaweza akahoji kulikoni watu wote hawa wakauawa kirahisi namna hii ili hali ni watu wenye mafunzo ya hali ya juu.Jambo hili linaweza kumfanya akakosa Imani nami jambo ambalo sitaki litokee”akatoa sigara akawasha na kuanza kuvuta
"Huyu Dastan ni nani hata akaweza kupambana na watu wanne wenye mafunzo ya hali ya juu akafanikiwa kuwamaliza?Ameweza hata kumuua Sam?Sikuwahi kumtuma Sam kazi yoyote akashindwa kuifanikisha.Imeniumiza sana kwani ni mtu niliyekuwa namtegemea mno katika kazi nyingi na hakuwahi kuniangusha hata mara moja.Huyu Dastan amejipalia makaa kwani maisha yake yatakuwa magumu sana kuanzia sasa na atajuta kuzaliwa.Ngoja nisubiri kwanza taarifa za kumuhusu Dastan ili nifanye kila linalowezekana usiku huu Dastan apatikane na tufahamu ujumbe ule aliopewa na Dr Alfredo ameupeleka wapi? Tukifanikiwa kujua mahala na mtu aliyepewa ujumbe ule inaweza ikasaidia katik akutoa maelezo kwa rais”akaendelea kuwaza Noah Mwamba huku akivuta sigara na kupuliza moshi mwingi
BAADA YA SAA MOJA
Noah Mwamba au Chita01 alikutana tena na watu wake aliowapa kazi ya kumchunguza Dastan baada ya saa moja kupita.
"Nadhani lile zoezi letu limekamilika.Nataka taarifa tafadhali.Teddy Jini tuanzie kwako,niambie umepata nini kuhusu Dastan? Akauliza Noah na kuelekeza macho yake kwa mwadada Teddy ambaye wanamuita Jini kutokana na uwezo wake mkubwa wa udukuaji.Teddy na wenzake wakatazamana.Noah akahisi kitu
"Mr Noah kuna tatizo limejitokeza” akasema Teddy na kunyamaza akamtazama Noah
“Kuna tatizo gani Teddy? Akauliza Noah
“Hakuna taarifa zozote za kumuhusu huyu jamaa Dastan Mwaikambile" akasema Teddy Jini
"Unamaanisha nini Teddy?
"Mkuu nimejaribu kutafuta taarifa za Dastan lakini sijafanikiwa kuzipata.Hakuna taarifa zake zozote seemu yoyote"akasema Teddy
"What? Noa akashangaa
“Hilo haliwezekani kutokea.Huyu ni mtumishi wa umma na lazima taarifa zake zote ziwepo.Huwezi kuajiriwa katika utumishi wa umma bila serikali kuwa na taarfa zako zote.Search again...."akasema Noah
"Mkuu hata mimi pia na wenzangu tumeshangazwa sana na jambo hili na ili kujiridhisha nikarudia tena na tena kukagua lakini hakuna taarifa zozote za kumuhusu Kamishan msaidizi Dastan Mwaikambile katika taarifa za wafanyakazi wa serikali.Jina hilop halipo katika orodha ya watumishi wa umma" akasema Teddy na Noah akavuta pumzi ndefu
"Imewezekanaje? akauliza tena na wote wakabaki kimya.Hakuna aliyekuwa na jibu.Lilikuwa ni jambo la kushangaza sana kuzikosa taarifa za kamishna msaidizi wa magereza Dastan Mwaikambile katika taarifa za watumishi wa umma
"Ni mara ya kwanza Teddy unaniambia kwamba umeshindwa kuzipata taarifa za mtu.Ninajiuliza yawezekana labda Dastan anatumia jina lingine tofauti na hili tunalolifahamu la Dastan Mwaikambile?akauliza Noah
"Hapana mkuu jina lake ni hilo hilo.Kuna sehemu nimeona katika orodha ya viongozi wa taasisi zilizo ndani ya wizara ya mambo ya ndani jina la Dastan Mwaikambile lipo na ameorodheshwa kama mkuu wa gereza la Markubelo na hii inatuthibitishia kwamba wizara ya mambo ya ndanoi inamfahamu na hadi kupewa cheo cha Kamishna lazima wanazo taarifa zake zote.Kinachoshangaza ni kwamba hakuna taarifa zozote zinazoonyesha elimu yake,sehemu alizowahi kufany akazi kabla ya kuwa mkuu wa gereza la Markubelo na vile vile ,hakuna taarifa zozote binafsi"akasema Teddy bingwa wa udukuzi
"Hii inashangaza sana.Ninaanza kufikiria yawezekana mtu huyu akawa ni hewa" akasema Noah
"Hapana mkuu.Dastan si hewa.Ni halisi yupo na ni mtumishi wa umma.Ninaamini kabisa lazima wizara ya mambo ya ndani wanazo taarifa za kuhusu Dastan.Haiwezekani wasiwe na taarifa za mtumishi wao tena anayesimamia gereza kubwa kama Markubelo.Lazima taarifa zake zipo mahala fulani and we have to find them.I think you have to inform president and ask for help.Yeye anaweza akawaamuru wakuu wa wizara hii ya mambo ya ndani wampelekee taarifa za Dastan" akasema Teddy.Noah akatikisa kichwa kukubaliana na wazo la Teddy akachukua simu akampigia rais
"Noah whats going on?Nimesikia kuna mauaji yametokea katika gereza la Markubelo.Unahusika?akauliza Dr Enock rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania
"Mheshimiwa rais ni kweli tunahusika na hicho ulichokisikia kimetokea.Nilituma vijana wangu waende kupata taarifa kutoka kwa mkuu wa gereza Dastan kuhusiana na ule ujumbe aliopewa na Dr Alfredo lakini mambo hayakwenda kama tulivyotarajia na watu wangu wote niliowatuma wakapoteza maisha"
"Hii imetokeaje?Wameauawa vipi? akauliza Dr Enock kwa sauti ya mshangao
"Nilitaarifiwa kwamba Dastan alikuwa baharini akivua na watu wanne wakaamua kumfuata huko huko baharini na hatuelewi nini kilitokea huko lakini watu wangu wote waliuawa.Nina hakika waliuawa na Dastan.Aliporejea nyumbani alikutana na watu wangu wengine waliokuwa wamejificha nyumbani kwake ambao walimuweka mikononi lakini kabla hajasema chochote wakatokea askari magereza na kudhani wale jamaa ni majambazi wakawashambulia kwa risasai wakawaua wote akiwemo Joyce ambaye amekuwa mtu wetu ndani ya gereza la Markubelo na ndiye mahsusi kwa ajili ya kumchunguza mzee Alfredo"akasema Noah
"Dah ! hili ni pigo kubwa sana,haijawahi kutokea watu nane wakauawa kwa pamoja.Chita imejaa vijana wenye uwezo mkubwa sana imekuwaje wakaweza kuuawa kirahisi namna hii?hawakuwa wamechukua tahadhari yoyote?akauliza Dr Enock
"Mheshimiwa rais hata sisi hapa imetushangaza pia kwani watu niliowatuma kule walikuwa ni watu wenye uwezo mkubwa"
"Kwa hiyo mmechukua hatua gani hadi hivi sasa?Nini unafikiria kukifanya?
"Baada ya kupata taarifa za kilichotokea tulipata ushawishi wa kumchunguza kwanza huyu Dastan ni nani na amewezaje kuwaua watu wanne akiwa peke yake?Vile vile tulitaka kumfahamu kiundani ili tuone namna tutakavyofanya ili aweze kutueleza Dr Alfredo alimtuma aupeleke wapi ule ujumbe.Tulianza kwa kutafuta taarifa zake tukiwa na lengo la kuishikilia familia yake lakini kwa bahati mbaya hakuna taarifa zozote za kuhusiana naye"
"Sijakuelewa Noah unamaanisha kitu gani unaposema hakuna taarifa za kuhusiana na Dastan?akauliza rais
"Mheshimiwa rais tumejaribu kuingia katika mitandao ya wizara zote zenye kuhifadhi taarifa za watumishi wa umma lakini hatujafanikiwa kupata taarifa za kumuhusu Dastan Mwaikambile mkuu wa gerezala markubelo ndiyo maana nimekupigia ili kupata msaada wako"
Dr Enock akavuta pumzi ndefu halafu akauliza
"Noah hicho unachokisema si kitu cha kweli.Nimewawezesha muweze kuingia katika mtandao wa serikali na kupata taarifa zozote zile ambazo mnazihitaji na taarifa zote za watumishi wa umma zipo katika kumbu kumbu za wizara ya mambo ya ndani na vile vile katika wizara ya utumishi n ahata hazina nao wana kumbu kumbu zote za watumishi wa umma hivyo si kweli kwamba taarifa zake hazipo.Yawezekana Dastan anatumia jina lingine tofauti"akasema
"Hata sisi tulihisi hivyo lakini baada ya kuchimba Zaidi tukagundua kwamba wizara ya mambo ya ndani wanamtambua Dastan kama mkuu wa gereza la Markubelo lakini cha ajabu hakuna taarifa zozote za kuhusiana naye kama vile uraia,taarifa za elimu ,familia n.k."
"Hii ni habari mpya tena.Inawezekanaje tukawa na mtumishi serikalini tena mwenye cheo kikubwa lakini hatuna taarifa zake? akauliza rais
"Mheshimiwa rais kuna mtu moja ambaye tunadhani anaweza akatupa majibu kuhusiana na Dastan ambaye ni Inspekta jenerali wa magereza.Huyu ndiye aliyemteua Dastan kuwa mkuu wa gereza la Markubelo hivyo naamini lazima anamfahamu vyema hadi akamteua kushika nafasi hiyo"akasema Noah
"Uko sahihi Noah ngoja nimpigie simu na nimtake anipe taarifa zote za Dastan" akasema Dr Enock na kukata simu akazitafuta namba za Inspekta jenerali wa Magereza akapiga.Simu ikaita na kupokelewa haraka
"Hallo mheshimiwa rais" akasema Dr Isaack Mchana
"Afande Isaack,habari za usiku huu?
"Nzuri kabisa mheshimiwa rais" akajibu Isaack
"Afande Isaack ninahitaji msaada wako."
"Ninakusikia mheshimiwa rais"
"Ahsante.Ninahitaji kupata taarifa zinazomuhusu mkuu wa gereza la Markubelo Dastan Mwaikambile"akasema Dr Enock halafu ukapita ukimya mfupi
"Afande Isaack" akaita rais
"Nd..ndiyo mheshimiwa rais.Unahitaji taarifa zipi kuhusiana na huyu jamaa?
"Taarifa zake zote zinazomuhusu.Nataka taarifa zake za elimu,familia n.k.Nitawatuma vijana wangu ndani ya dakika chache zijazo watakuja hapo kupata taarifa hizo" akasema Dr Enock
"Mheshimiwa rais kwa hapa sina taarifa hizo ninaomba unipe muda hadi kesho asubuhi nikakukusanyie taarifa zote za kuhusiana na Dastan"
"Afande Isaack ninahitaji taarifa hizo ndani ya muda mfupi ujao.Ninawatuma vijana wangu sasa hivi wanakuja hapo kuja kuchukua taarifa hizo.Fanya kila uwezavyo niweze kuzipata hizo taarifa ndani ya muda mfupi ujao" akasema Dr Enock na kukata simu halafu akampigia Noah
"Mheshimiwa rais" akasema Noah baada ya kupokea simu
"Nimezungumza na Inspekta jenerali wa magereza na nimemtaka aniandalie taarifa zote za Dastan"
"Ahsante sana kwa hilo mheshimiwa rais"
"Nataka uende nyumbani kwake sasa hivi wewe mwenyewe ukazichukue taarifa hizo kwani nimemwambia nitawatuma vijana wangu kwake usiku huu .Ukizipata zichambue uone kama kuna chochote kinachoweza kukusaidia.Kitu ingine chunguzeni kwa nini taarifa hizi za Dastan hazipo katika kumbu kumbu za serikali?
"Sawa mheshmiwa rais nitafanya hivyo na nitakujulisha kila hatua tunayochukua"
"Noah tafadhali,hili suala la Dr Alfredo si la kufanyia mzaha hata kidogo.Hakikisha usiku huu umefahamu ujumbe ambao Dastan alipewa na Dr Alfredo ameupeleka wapi?Nataka kabla ya kufika asubuhi niwe nimepata jibu kwamba mmemfahamu mtu huyo aliyepewa ujumbe ni nani " akasema Dr Enock
"Mheshimiwa rais tunafanya kila tuwezalo na ninakuhakikishia kwamba kabla ya mapambazuko tutakuwa tayari na taarifa zote za kuhusiana na huyo mtu" akasema Noah na kukata simu akawageukia wenzake
"Rais amewasiliana na Inspekta jenerali wa magereza na kumtaka atupatie taarifa zote za kumuhusu Dastan.Teddy,Jeff na Santana tunakwenda kwa Inspekta jenerali wa magereza kufuatilia taarifa hizo za Dastan.Wengine mtaendelea kudukua sehemu mbali mbali ili tuweze kupata jambo lolote la kumuhusu huyu Dastan" akasema Noah kisha yeye na vijana wake wakajiandaa wakaondoka kuelekea nyumbani kwa Dr Isaack Mchana
Dakika ishirini toka Noah na wenzake waanze safari ya kuelekea kwa Dr Isaack Mchana,simu yake ikaita alikuwa ni rais,Noah akaipokea haraka haraka
"Mheshimiwa rais" akasema Noah na kisha ukapita ukimya mdogo halafu rais akasema
"Noah uko wapi?
“Mheshimiwa rais ninaelekea nyumbani kwa Inspekta jenerali wa magereza kuchukua taarifa za Dastan kama ulivyoelekeza”
“Mmefika wapi? Rais akauliza
"Tumefika hapa katika hospitali ya Dr Tamala" akajibu Noah
"Noah ahhmm !! rais akasita kidogo akanyamaza halafu akavuta pumzi ndefu na kusema
"Nimepokea taarifa muda mfupi uliopita Dr Isaack amefariki dunia"
"Amefariki dunia?!! Noah akapatwa na mstuko
"Ndiyo"
"Amefariki muda gani wakati muda si mrefu umetoka kuzungumza naye?
"Nimetaarifiwa kwamba amejiua kwa kujipiga risasi ya kichwa"
"Dah ! akasema Noah halafu kukawa kimya
"Noah" akaita rais
"Ninataka muwahi hapo nyumbani kwa Dr Isaack mkaichukue simu yake.Naamini kujiua kwake si kwa bahati mbaya.Kuna jambo limepeleka akaamua kujitoa uhai" akasema Dr Enock na kukata simu.
"Kumetokea kituko kingine" akasema Noah
"Nini kimetokea tena?Jeff akauliza
"Mtu tunayemfuata Dr Isaack amejiua muda mfupi uliopita kwa kujipiga risasi"
"oh my God ! akasema Teddy
"Jeff ongeza mwendo tunapaswa kufika hapo nyumbani kwa Dr Isaack haraka kabla polisi hawajafika.Tunaihitaji simu yake" akasema Noah na Jeff aliyekuwa katika usukani akaongeza mwendo.
"Unadhani nini sababu ya Dr Isaack kujiua? akauliza Santana huku akizifunga vizuri nywele zake kwa nyuma.
"I think he's hidding something" akasema Noah
"Amejiua baada ya kuombwa na rais ampe taarifa za Dastan Mwaikambile.Inaonyesha kuna kitu anakifahamu kuhusiana ana Dastan ambacho hataki kijulikane na ndiyo maana akajitoa uhai.Hii inazidi kutupa ushawishi wa kumfahamu zaidi huyu Dastan ni nani.Tukiipata simu ya Dr Isaack tutaweza kufuatilia watu ambao amekuwa akizungumza nao na tutajua ni siri gani iliyojificha.Guys tunaingia katika operesheni nyingine ambayo inaonekana itakuwa kubwa na ngumu.Tujiandae" akasema Noah
USIKOSE SEHEMU IJAYO……………..
SIMULIZI NYINGINE UNAZOWEZA KUZIPATA KUTOKA MASIMULIZI
1)- MISS TANZANIA 1&2
2)- SERENA
3)- BEFORE I DIE
4)- BEYOND PAIN
5)- PENIELA 1-5
6)- QUEEN MONICA 1-8
7)- THE FOOTBALL 1-7
8)- I DIED TO SAVE PRESIDENT 1-7