Riwaya: Kibiritingoma

Riwaya: Kibiritingoma

CamScanner 09-06-2026 00.55_1.jpg
SEHEMU YA KUMI NA TATU


Katu usijidharau na wala usiwadharau wengine.
Huenda wewe ni daraja la mafanikio ya mtu mwingine, yupo mahala fulani na mtakutana katika namna ya kushangaza.
Ama neema ya mafanikio yako imebebwa na mtu fulani aliye mbali ama huyuhuyu aliye karibu yako.
Ulimwengu wetu umeumbwa kwa kanuni ya ajabu sana...
Tunaishi kwa kutegemeana.

Karibu kwenye sehemu ya kumi na tatu.




Kila kitu kilikuwa kama mchezo wa sinema. Ndani ya siku moja tu...kila mtu alikuwa amebadilisha historia ya maisha yake.
Sio Bebe, sio J4 na pia sahau kuhusu Chief Didas, kama alivyozoea kuitwa na Bebe.
Kila mtu kwa nafasi yake, aliyapokea mabadiliko japokuwa katika namna tofauti.
Haswaa,
Bwana Didas, alilazimishwa kulivujisha pakacha lake.
Bebe na J4, wakafurahia nafuu hii ya kuwa wachukuzi.


Bwana Didas alikuwa bado haamini kama ameokoka kwenye hatari kama hii. Hatari ya jina lake kupakwa matope mbele ya Watanzania wanaomheshimu. Na zaidi ya yote, wanazipenda bidhaa za kampuni yake.
Akashusha pumzi ndefu kujiweka sawa. Ni kama punguani aliyeiokoa kete yake ya mwisho kwenye mchezo wa kamari ambao alikuwa na kila dalili ya kupoteza. Hofu ya kuaibika bado ilizidi kuutafuna ujasiri wake.
"Hivi huyu jamaa hajapost kweli?!" Ni swali pekee alilozidi kujiuliza akiwa anaendesha gari lake kuelekea nyumbani.
Ameshapiga simu mara kadhaa kwa mkewe, akimuuliza endapo kuna taarifa yoyote ile mpya iliyogonga hodi.

"Mh Baba Junior, umekuwaje mme wangu? Hii ni mara ya nne. Mara ya nne unaniuliza kama kuna jipya. Vipi, kwema huko? Ama kuna msiba?" Sauti bembelezi ya kujali, lakini yenye kujiamini ikahitaji majibu.

"Aaam...hapana laazizi. Nakujulia tu hali mke wangu. Hehehe wala hamna shida." Didas anamjibu huku akijichekesha kwa aibu.
Siku hii anamuita mkewe kwa jina Laazizi , haikuzoeleka hivi.
Hatulii anabadili upepo angani, atapiga simu kwa baadhi ya vigogo na viongozi wakubwa wa serikali anaofahamiana nao. Hawa atawauliza juu ya kile kinachoendelea Ikulu.
Didas atasimamisha gari lake kando kidogo. Anapoongea na watu wenye nyadhifa kama hizi, kelele hazihitajiki.
Badala yake ataiinamia simu yake na kulitega sikio lake kwa adabu zote, kusikia litakalosemwa.
Hataambulia kitu zaidi ya malalamiko ya viongozi hawa juu ya kero za wananchi na ugumu wa majukumu yao.

Ni saa tatu na robo usiku,
Didas Kilonzo Ambrozi anarudi nyumbani baada ya siku ndefu sana.
Ama siku hii gari la faza hausi limerudi nyumbani mapema kuliko siku za nyuma. Tazama, hii ni siku ya tofauti kabisa kwa familia hii tangu asubuhi.
Labda ni siku nzuri kwa mama Junior na wanae, lakini kwa Didas ni ya kipekee.
Anakuja kupokelewa na bintiye mdogo wa kike katika namna ya Baba huyo...anaigiza tabasamu, nalo linamgomea kuigizwa.
Anamkwapua na kumuinua juu kiasi lakini hambebi, anamrejesha upya sakafuni baada ya kugundua kuwa amechafuka!

Suti yake nyeusi nadhifu aliyoandaliwa na mkewe asubuhi ya siku hii, imepakwa rangi mpya ya vumbi.
Tai yenye nembo ya bendera ya taifa, haipo tena shingoni mwake. Ukosi wa shati lake nao ni kama umepata muundo mpya shingoni mwake.
Didas anaiburuza miguu yake na kuingia nyumbani mwake akiwa amechoka mwili na akili.
Hataki usumbufu wala mazozano na mkewe, ambaye anamshushia mvua ya maswali juu ya muonekano wake.
Huyooo Didas anajisogeza bafuni ili akakoge.
Lakini hapigi hatua zaidi ya tano kabla hajahisi kuongezeka kwa gramu kadhaa za uzito wa kichwa ni chake.
Anayumba na kuisalimia ardhi kwa kuanguka chini kama mzigo.
Hii nayo ina maswali ya kumuuliza. Hana majibu...anakoroma tu, anaona giza! Giza linamfumba macho yake.
Kinachofuata ni hekaheka za mama Junior na wanae kumpepea kabla hawajaomba msaada wa wafanyakazi wa nyumba ile.


*******


"Mic check, mic check...one two, one two!" Sauti nzito changamfu iliendelea kurindima ndani ya Studio kubwa.
Ilikuwa sauti ya bwana mmoja mnene wa umbo, aliyeyafunika masikio yake yote mawili kwa kifaa cha kidigitali, maalumu kwa ajili ya kusikiliza muziki, headphones!
Fulana yake pana ya kijivu, imelowa jasho na kuchora mfano wa ramani kwenye kifua na mgongo wake.
Mbele yake ni meza iliyochafuka kwa vifaa lukuki vya kieletroniki. Vifaa vinavyomweka kwa rangi mchanganyiko.
Rangi zinazompa mzuka wa kufanya hiki anachokifanya. Atagusa hapa na pale, atabonyeza kitufe hiki na kile, huku atasugua sugua kisha kile atakizungusha. Ili mradi tu, aukoroge mchanganyiko wa sauti na azalishe mziki bora.
Hii nd'o kazi yake.Yeye ni producer (mzalishaji) wa muziki. Pia ni mkufunzi wa wasanii wa muziki wa kizazi kipya.
Na siku hii alikuwa akimpika kijana mpya pale pale kwenye studio yake.

Kichwa chake kinapanda juu na chini, kikifuatisha miondoko ya mdundo wa muziki anaousikia yeye peke yake.
Kisha anatoa ishara ya kidole gumba kwa kijana nyuma ya kinasa sauti, aliye ndani ya chumba maalumu kilichomtenganisha naye kwa kioo kipana kinachoruhusu waonane.

Kijana yule anaiweka sawa sauti yake, anayafumba macho yake kiasi kwa hisia kali na kuanza kuimba yale anayoyasoma kwenye karatasi mbele yake, japo kwa kuibiaibia.
Hamalizi hata mshororo mmoja wa beti lake,
"Hajwaa! Hajwaaa!" Sauti inapazwa, haisikiki.
"Dogo achaa! Acha nakwambia! Hii mbovu, mbovu sana!" Bwana yule mnene amechachamaa, anasimama kwa hasira na kufoka. Kitambi chake kinatikisika, ndita zimeweka kambi usoni mwake.

"Nimeshakwambia, usiimbie kooni my boy! Sauti itoke kwenye tumbo! Tumboni nimesema! Haya shime..." Anarejea kwenye kiti chake, uso wake mnene bado una ramani za ndita. Ni kama aliyekunywa dawa chungu.
Kijana ndani ya chumba, anajiweka sawa kwa mara nyingine. Naye, anavaa kifaa kilekile masikioni. Safari hii anajitahidi kuimba kama alivyoelekezwa. Anaibia mashairi kwenye karatasi mbele yake, kisha anapepesa macho kumsanifu bwana yule mnene, ambaye bado amemkazia macho kwa hasira.

Mara ghafla, bwana yule mnene anakitoa kifaa kile masikioni. Anasimama kwa pupa, akimtazama kijana yule. Pumzi zinapishana kwa kasi puani mwake, ni kama mbogo mwenye hasira.
"Dogo! Hivi nikueleze mara ngapi? Umekuja kuimba au kunipotezea muda?Mh? Sema!"
Akiwa kwenye mahojiano haya na kijana huyu ambaye anaonekana kuipoteza hali yake ya kujiamini. Mara unafunguliwa mlango wa studio hii na kinaingia kikundi cha wanaume watano, kikiongozwa na kijana mmoja aliyevalia mavazi ya kisasa.
Nyuma yake ni wenzie wawili wanaoonekana kufanana naye kimavazi, pamoja na watu wawili wa miraba minne, waliovimba kwa mazoezi.

Ujio huu unabadilisha hali ya hewa ndani ya studio hii na kusababisha uchangamfu wa ghafla.
"Alaaaa! Kenzy kama Kenzy! Finally, you are here my boy!" Bwana mnene anakurupuka na kumkumbatia kijana huyu.
"Eeeeh BIG kama BIG!" Kijana yule akamchangamkia.
Wanakumbatiana kwa furaha huku kicheko cha ushindi kikikatiza baina yao.

"Aiseee...kitambo sana ticha!" Kenzy akatamka kwa bashasha.
"Haswaa naona umenitupa mwanangu...mara ya mwisho, lini ilikuwa?...show yako ya pale Mbeya! Tangu hapo!" Bwana mnene, aliyetambulishwa kwa jina la BIG akatamka huku anakielekea kiti chake.
"Nimeimiss sana hii studio ticha!" Kenzy anagundua kuwa kuna kijana ndani ya chumba cha mazoezi.
"Nani huyu? Chipukizi eeh?"
"Yeah...niko namchonga kijana. Sema huyu boga sana aisee...doh!" BIG akatamka huku akilipangusa jasho lake kwa kitambaa kipana.
Kenzy akamfanyia ishara kijana yule asogee pale walipokuwa wao.
Kijana anasogea akiwa anatetemeka. Haamini kama ni yeye leo hii anaonana na mwanamuziki mashuhuri nchini uso kwa uso.
Msanii nyota, ambaye anatamani siku moja aje kuwa kama yeye.
"Mambo vipi?!" Kenzy akamuuliza kwa uchangamfu.
"Sa..sa-lama bro! Ke- Kenzy. Shkamoo!" Anajiumauma.

"N'do nakwambia boy! Mimi nimewaandaa wasanii wakubwa! Huyu hapa Kenzy, nimemchonga mimi.
Alikuwa anafuata maelekezo. Anatoa sauti! Kutoka tumboni...haibanii. Wewe sasa!" BIG akatamka kwa kisirani huku akisonya.
Wale wapambe waliokuja na Kenzy wakacheka kwa sauti baada ya kuyasikia maneno ya BIG.
Kijana akatazama chini kwa aibu.

"Unaitwa nani mdogo wangu?" Kenzy amemshika begani kijana huyu, katika namna ya kumfariji.
"Jackson"
"Hili ni jina lako la kisanii?"
"J-la...J-love nd'o jina langu la kisanii"
"Safi sana...haya sasa nenda katuoneshe ulichonacho. Jiamini!" Kenzy anampiga begani, kijana anarejea ndani ya chumba.
Anavaa kifaa kile masikioni, anashusha pumzi kwa nguvu.

BIG anamtazama kwa pembe za macho yake katika namna ya ole wako na hii uharibu.
Unawashwa muziki na kijana anaanza kutembea na mapigo yake akiimba.

Ama!
Ni kama mashetani yake yalikuwa yanasubiri ujio wa Kenzy, ndipo yampande kichwani.
Sauti yake ikapita kwa adabu kwenye vifaa hivi vya kielektroniki. Ikawa sasa, ni kama mapigo ya muziki ule yanamtii yeye na kuifuata sauti yake badala ya yeye kuyafuata mapigo.
Jackson, J-love akamaliza ubeti wake wa mwisho kwa kufumbua macho yake. Akakuta watu wote ndani ya studio hii, vinywa wazi.
Makofi!
Wote wakampigia makofi! Wote isipokuwa BIG.
"Hebuu kwanza!" Bado haamini kama kweli Jackson ameimba namna ile.
"Nipe stanza ya mwisho..." Akamsihi huku akicheza na vifaa vyake.
J-love akaiimba beti ile kwa ubora zaidi ya mara ya kwanza. Aliyepiga makofi safari hii alikuwa ni BIG peke yake.

"Unaishi wapi aisee!" Kenzy akamuuliza akiwa na shauku.
"Msasani bro." Akajibu kwa adabu.
"Unaimba vizuri sana mdogo wangu. Ukiendelea hivi, nitatoa ngoma moja na wewe siku si nyingi!" Kauli hii ikafufua tabasamu usoni mwa Jackson.
"Sauti yako ina kitu mdogo wangu...ina raw energy ambayo wasanii wengi wanaikosa. Usiache, push harder! Na ukiweza kupata mentor kama BIG hapa, usimuachie." Kenzy akaongeza.
Wakabadilishana nambari za mawasiliano na kupiga picha ya pamoja. Hili likawa kama kombe la ushindi kwa Jackson. Achana na kupiga picha na staa, hilo si suala. Suala kubwa ni kumiliki namba zake za mawasiliano.

"Karibuni aisee wanangu! Sie tupo." BIG akarejea kuutambua ugeni wa Kenzy na wenzie. Ni yeye aliyemtengeneza Kenzy tangu alipokuwa chipukizi mpaka hivi sasa alivyo. Nyota wa muziki wa kizazi kipya.

"Naam faza! Nilikuwa nakatiza, nikaona si vyema nipite kwenye mtaa ulionilea halafu nisipite hapa mgodini pasi na kutoa hata salamu!"
"Oooh safi sana...walau hata umelikumbuka hilo. Nyie mkitoka huwa mnatusahau. Tumeshawazoea, na wala sishangai!" Producer BIG anajibu kwa kujiamini bado kitambaa chake kipana cha jasho kipo mkononi mwake, kinafanya kazi yake kwa uaminifu.
"Walaa mimi siwezi kukusahau anko wangu, BIG mzazi! Tena..." Kenzy anasita kisha mkono wake unazama mfukoni na kuibuka na noti nyekundu kadhaa.
"Nadhani hii ya maji itakufaa!" Anampatia BIG kiasi kile.

BIG haonekani kushtuka. Anaipokea na kuisweka kwenye mfuko wa suruali lake bila hata kuihesabu.
"Mafao yetu ya uzeeni haya!" Anatoa kijembe. Wote wanacheka kidogo.
Anamkazia macho Jackson kisha na yeye anazama mfukoni na kumpatia noti ya rangi tofauti na zile alizopewa.
"Haya dogo! Changanya mbaliga zako, kaniletee maji makubwa. Chenji inayobaki chukua!"
Jackson anaipokea noti ile na kuondoka ndani mule kwa bashasha.

"Enhe vipi umefikia wapi na ile project yako mpya? " BIG anamuuliza Kenzy.
"Ipi hiyo?"
"Video ya lile jiwe lako, ME AND YOU!" Anaweka wazi swali lake.
Kenzy anachangamka,
"Aaaah ME AND YOU....naelekea kushoot wiki ijayo mzazi. Kila kitu kipo tayari so far! Na pia kuna surprise hapo!" Kenzy anatulia na kuiacha sentensi yake ielee hewani ili auvute usikivu wa BIG.
"Surprise gani tena?"
"Unajua ni video vixen gani nitakuwa naye?" Akauliza tena kwa bashasha. Lengo lake ni lilelile, amshangaze BIG.
"Ni nani?"
"Queen Frola!" Akatamka kwa kushtukiza, akitabasamu kwa shauku. Na kweli BIG akashangaa.
"Unamaanisha? Huyu huyu mrembo ninayemuona kila siku kwenye matangazo au?"
"Eeh huyu huyo. Na mimi nitakuwa msanii wa kwanza kufanya naye kazi hapa nchini!"
"Duh hongera bwana. Lakini mbona kama ni wa bei ghali sana yule. Utamudu kum-"
"Nitamlipa. Pesa sio tatizo. Uzuri ni kwamba nikifanya naye video moja. Itakimbiza sana mitandaoni, faida itakuja kwa kasi!" Kenzy akajipeperusha.
"Mh sawa! Utakuwa umepiga hatua kubwa sana aisee. Maana industry haicheki na mtu sasa hivi." BIG akatamka bila kumuangalia Kenzy usoni.

"Tena jioni hii nina appoitment naye, tutakutana tuongee." Kenzy akaweka nukta.
Baada ya dakika kadhaa za maongezi mafupi hususani ya kisanaa, Kenzy na jopo lake waliondoka na kuacha ahadi nyingine lukuki za kurejea tena.
Ahadi ambazo masikioni mwa BIG zilikuwa sawa na baba anayemuhaidi peremende mwanae mdogo ma asimletee. Alishawazoea hawa wasanii!
Anawachonga mpaka wanafanikiwa na kupenya kwenye tasnia, wakishapata mafanikio wanamsahau.
Ama kweli, Tenda wema nenda zako!

Anakunywa mafunda makubwa ya maji na kurejea upya katika darasa lake na kijana Jackson J-love.
"Sikiliza, mgema aliwahi kusifiwa sana kuwa anatengeneza pombe aina ya Tembo kwa ustadi wa hali ya juu pengine kupita wagema wote.
Unajua ni nini alifanya baadae?" Akamtupia swali Jackson.
"Alilitia maji!" Akajibu upesi kwa kujiamini.
"Unajibu kwa kuwa umekaririshwa hivyo au unaelewa?"
"Naelewa!" Jackson akamjibu.
"Haya vaa Headphones tuendelee. Kanuni ni ileile, toa sauti tumboni...imba kwa kujiachia. Usibane sauti!
Haya sasa...One! two! three!....twende!"


*******


Kipande cha kitu mfano wa kalamu ya rangi kinapitishwa kwa adabu kwenye papi za midomo yake.
Anaifumba na kuigusanisha katika namna ya kuikausha rangi ile. Lipstick!
Hii ni baada ya uso wake kurembwa kwa vipodozi na kuufanya ung'ae na kumeremeta.
Sijaongelea kope zake ndefu ambazo sio za bandia. Ni kope ambazo zikipepesa tu, zinatamfanya mtu anayetazamana naye aimbe pambio kumsifu Mungu.

Alikuwa na silaha zote za maangamizi.
Kama hatakuua kwa sura yake iliyovimbiwa urembo, basi umbo lake na ngozi yenye nuru havitakuacha salama.
Basi tuseme wewe ni mgumu sana. Utapona kwenye haya, lakini chunga sana masikio yako. Labda yafunike kwa pamba usiisikie sauti yake inayoweza kuwatorosha malaika mbinguni.
Basi tuseme wewe ni kiziwi japo kwa mkopo.
Chunga sana, usimsogelee karibu.
Huyu hapa! Anajipulizia manukato yake ya bei mbaya. Manukato yenye harufu tamu, inayodai kumbato zito la mtu atakayepishana naye karibu.
Eeh unashangaa?!
Inabidi uwe na mkusanyiko wa vilema vitatu mpaka vinne vinavyohusisha milango ya fahamu.
Uwe kipofu, macho yako simuone
Uwe kiziwi, masikio yako yasimsikie
Uwe toinyo, harufu yake ikupite kando.
Na katu, ngozi yako isimguse kumhisi...utapagawishwa na wororo wa ile ya kwake.
Ulimi hauna mfupa! Hii dhambi sitaki kushiriki.

Hamna namna yoyote ile utakayokwepa kukiri kuwa Bebe ni malikia wa uzuri. Hasa jioni hii anayojiandaa kwenda kukutana na Kenzy. Msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania.
Bongo Fleva!
Anasimama mbele ya kioo chake kipana. Anajitazama. Anajigeuza huku na huku, anajibinua kidogo. Kisha anazunguka nyuzi mia tatu sitini kwa madaha.
Anafurahi namna nywele zake zinavyoufuatisha mzunguko ule.
Ni huu urembo wake uliomtajirisha siku mbili zilizopita. Anatabasamu anapolifikiria hilo.

Upesi anaitwaa simu yake, simu janja.
Akachukua picha mbili tatu mbele ya kioo kile.
Anamtazama yule Bebe mwingine wa ndani ya kioo. Ni kama anaweza kuzungumza naye, anampa uhai,
"Enhe una nini sasa? Ulidhani nitakuwa mtumwa daima? Tazama! Mwili wangu unanilipa...tabia ile chafu, uliyokuwa ukinishutumu kwayo, inaeleka kunitajirisha. Upo hapo?!" Anatamka akitazamana na taswira ile.
Safari hii huyu Bebe wa kwenye kioo hamjibu na wala habadiliki katika namna yoyote ile. Bali anafanya kile anachokifanya kwa kuigiza. Akicheka naye anacheka, akiruka anaruka.
Bebe akatoka ndani ya chumba hiki akiwa na pochi yake ndogo.
Anatoka nje akipewa salamu lukuki na vijakazi wake. Anazipokea kishingo upande kana kwamba hazistahili.
Na kweli hazistahili!

Anajua fika kuwa ima fa ima, muda wowote ule atanyang'anywa mji huu. Anaitazama nyumba hii kwa nje, kisha analigeukia gari lake na kulitazama kwa macho ya aibu. Dhamiri yake inamsuta kwa kutumia kisicho chake.
Ilikuwa wazi sasa kuwa ameachana na kampuni ya Bwana Didas.
Anaachana na mawazo haya baada ya kukumbuka kuwa hana muda wa kuwaza yaliyopita. Bado kitambo kidogo, atamiliki majumba makubwa hata kumi ya kifahari.
Wasiwasi wa nini?
Ofa mbalimbali za matangazo bado zimepanga foleni kuhitaji sahihi yake. Hata jioni hii anaenda kuongelea dili linalohusisha pesa.
Ana shida gani sasa?
Na zaidi ya yote, amefahamiana na J4. Ambaye ana madili ya maana zaidi yanayohusisha fedha nyingi chekwachekwa.

Analiondoa gari lake taratibu na kuanza safari ya kuelekea walikopanga kukutana na msanii Kenzy.
"Nipo njiani!"
"Ooh okey, mi nimeshafika mama. Nakungoja wewe tu." Ni sauti ya Kenzy ndani ya simu ya Bebe.
"Santeeee!"
"Take care." Simu inakatwa.
Kabla hajaitua chini, inaingia simu nyingine ambayo inaanza kuzungumza papo hapo bila yeye kuiruhusu.
"Mlimbwende! Hakikisha anajaa kwenye mfumo huyo msanii. Naona ameshaanza kulainika."
Bebe anashtuka. Ni sauti ya J4.
"Wewe ina maana umeidukua simu yangu ama?" Anauliza akiwa na hamaniko.
"Usiwe na hofu bibiye...mimi nimekutafuta tu kwa muda huu, na kwa bahati nikakuta unaongea na nyama mpya. Nilitaka kukusalimia tu."
"Mh kwa nini lakini? Biashara gani hizo unaleta sasa? Masuala ya kudukuana mi staki."
"Alaa basi sawa, nitakutafuta usiku." Simu ile ikakatwa.
Kukatwa kwa simu hii, kukaambatana na Bebe kupokea ujumbe wa kutoka kwa namba hii ngeni.
Ujumbe uliokuwa na ile picha yake nzuri aliyojipiga kwenye kioo chumbani mwake!
Maneno chini yameandikwa,
What a beautiful lady!

Imemfikiaje huyu? Hajui.
Na wala hata hajaitundika mitandaoni.
Bebe akakosa la kufanya, akatabasamu na kuendelea na safari yake.
J4 mdukuaji kwenye ubora wake.


Itaendelea....
 
Now this is too much,umeamua kufanya jambo likamilishe uswahili Swahili hutokifikisha ppt!
 
KIBIRITINGOMA
YA: Godlove Kabati
SEHEMU YA 14

Sikia,
Tafsiri sahihi ya wewe kuwa na umaarufu, ni kujulikana na watu wengi ambao wewe huwajui.
Haijalishi wanakujua kwa mema ama mabaya. Lakini daima tambua kuwa, kwenye wengi kuna mengi.
Zichunge sana nyendo zako ewe supastaa mwenzangu.
Ni kosa moja tu linaweza kuyafuta mema tisini na tisa uliyoyafanya.

Nakuandikia haya katika sehemu hii ya kumi na nne.




Siku zilitembea kwa kasi sana kama mshale hewani. Ndani ya wiki moja baada ya makubaliano ya ana kwa ana baina ya Bebe na msanii Kenzy, hatimaye mtandaoni lilitupwa jiwe jipya lenye mshindo mkuu, ulioyatikisa masikio ya watanzania.

FROLA ATAKUWEPO KWENYE NGOMA MPYA YA KENZY FLAVOUR!

Hii haikuwa taarifa rasmi, bali zilikuwa tetesi tu. Tetesi hizi zikatambaa kwa kasi kama moto mkubwa nyikani. Macho na masikio ya watanzania wote wapenzi wa Bongo fleva vikakaa chonjo kusubiri.

"Acha utani bwana!! Kwamba Frola huyuhuyu, atakuwa video queen kwenye ngoma mpya ya Kenzy?"
"Sa' hapo unabisha nini mzee? Unaambiwa Kenzy flavour amemwaga mpunga wa kutosha kaka. Majuzi tu kamera zimewanasa pale Sheraton wanashoot! We unacheza na media nini?"
Yalikuwa ni maongezi ya vijana wawili wa rika moja, wakipata mlo wa mchana kwenye moja kati ya migahawa, uliokuwa karibu na chuo chao.
Wanakula chakula, vidole vya mikono yao ya kuume vikikamata vijiko kupambana na punje tamu za wali mweupe. Huku vile vya mikono yao ya kushoto vikipapasa vioo vya simu zao. Macho yao yanazidi kupepesa wakikagua kinachojiri kwenye kurasa mbalimbali za mitandao.
"Kama ni kweli, basi hili dude litakuwa na bonge moja la video aisee!"
"Ooh ooh, Bro! Hii Me and you itakuwa ni dunia nyingine."
Wakamaliza kupashana habari na kuendelea kuufaidi uhondo wa kile kilichoko kwenye sahani mbele yao.

Dunia ya muziki, ikaisubiri kwa hamu kubwa ile tarehe ya kuachiwa kwa video ya wimbo huu mpya wa msanii Kenzy Flavour.
Kuhusu ubora wa uimbaji wake, hilo halikuwa suala la kushangaza. Tayari alishafanikiwa kuziteka nyoyo za mashabiki wake wengi tangu walipompa masikio yake. Suala kubwa muda huu lilikuwa ni kuitazama video ya wimbo huu ambao ilisemekana kuwa yule mrembo maarufu nchini Tanzania, yumo ndani.
Mrembo ambaye anajulikana mpaka na watoto wadogo kila wanapoyaona makopo ya icecream yaliyopambwa na sura yake.

Siku ya siku ikawadia.
Lile jiwe la kimondo cha Me and you lililohaidiwa, likatupwa mitandaoni. Safari hii haikuwa tetesi tena na hakuna aliyetaka kusimuliwa.
Mitandao ya kijamii ikafurika. Watu wakateketeza masalio ya vifurushi vyao vya intaneti ili tu kutazama kunani?
Maajabu,
Ndani ya lisaa limoja tu, takribani watu milioni moja na ushee walikuwa wamezipepesa mboni za macho yao kwenye ukurasa wa msanii Kenzy. Rekodi mpya ikaandikwa nchini Tanzania katika mtandao wa Youtube . Msanii wa kwanza Afrika mashariki, kupata watazamaji wengi ndani ya muda mfupi.
Mafanikio!

"Bro siamini macho yangu aisee!" Kenzy flavour alikuwa wima, mikono yake inamtetemeka viganja vyake vinamiliki simu yake. Anachokiona haamini kama ni kweli kinatokea. Amewahi kupandisha video za kutosha, tena zenye mawe ya maana kwelikweli. Lakini hii ilikuwa ni kubwa kuliko.
Haelewi afanye nini. Ni kama anayetaka kupaa na kukimbia kwa wakati mmoja. Anazunguka huku na kule kwenye sebule yake ya kifahari. Mara anaitupa simu ile na kumrukia rafiki yake aliyekuwa karibu kwa shangwe.
Ni furaha tupu! Haya ni mafanikio makubwa kwake katika tasnia hii. Yupo kwenye kilele cha furaha yake.
Upesi anawasiliana na Bebe, na kumshirikisha juu ya hili.

Ni furaha na burudani mara mbili kwa wale wanaosimuliana hadithi za urembo na madaha ya Bebe kwenye video ya wimbo huu. Wimbo wenye mashairi matamu ya mapenzi yenye mchanganyiko wa kiingereza na kiswahili.
Anga la nchi ya Tanzania, likahanikizwa kwa mrindimo wa sauti za wimbo huu.
Umaarufu wake ukatishia kuuweka kwenye daraja moja na wimbo wa taifa.

LE CLUB GRANDE, ukapigwa usiku na mchana. Ukamfikia mpaka Madam Sally na mabinti zake ambao waliufurahia japo kwa matamanio makubwa ya kuipata nafasi kama ile aliyo nayo Bebe.
Mitandao haifichi kitu, wimbo ukapigwa mpaka kwenye vipindi mbalimbali vya runinga. Ukaifikia familia ya Bwana Didas. Watoto wake wakaufurahia, wakajitahidi kuyakariri mashairi yake, mke wake akayatumia mashairi haya kumliwaza mmewe.
Lakini yeye bwana Didas aliutazama wimbo huu kwa uchungu, roho yake imechafuka kwa kisirani, wivu na hasira.


* * * * * *


Jukumu la mashabiki siku zote ni moja tu. Ama ni mawili kwa hakika. Kusifia na kupiga makofi pale panapostahili pongezi vilevile kukosoa na kukemea pale panapohitaji kukosolewa.
Baada ya makofi mengi kupigwa na sifa kedekede kujazwa kwenye kurasa za mitandao ya kijamii kuhusu wimbo huu mpya wa msanii Kenzy Flavour, ghafla likaibuka kundi la wale mashabiki wenye macho ya mwewe yanayotazama na kufanya uchambuzi wa umakini zaidi.

Hawa wakayafuatilia kwa umakini zaidi yale makumbato, ile mipapaso na miguso kwenye video hii...kisha wakarejea na mawazo mapya ambayo abadani hayakutegemewa.
Mawazo haya yaliyobeba hoja mbalimbali, yakaibua mijadala kwenye makundi mbalimbali ya udaku kwenye mitandao ya kijamii.
Wimbi kubwa la wale wanaokesha kujadili maisha ya wasanii, wakaipenda mada iliyosogezwa mezani.
Vikao visivyo rasmi vikaanzishwa.

:Sanaa imeingiliwa!
:Kenzy hakufanya makosa kabisa, alihakikisha hela yake haiendi burebure.
:Alimkamatilia kwelikweli aisee.
😀uh! Kwa namna alivyokuwa anampiga tachi, sidhani kama yule manzi alitoka salama.

Mijadala hii ikaibua hoja ambazo ni kama zilikuwa zinasubiriwa kwa hamu na kiumbe fulani aliyekuwa nyuma ya kioo cha kompyuta yake, ndani ya chumba chake chenye giza la wastani.
Kiumbe huyu akatabasamu kisha kwa utulivu mkubwa, akaendelea kunukuu machache kwenye kitabu chake kidogo chakavu kilichokuwa kando.
Akaendelea kusoma yanayoendelea huko mitandaoni.
:Aaaah wasanii hawa kawaida yao hawa! Tumeshawazoea!
:Kwanza huyo Frola si inasemekana aliwahi kufanya kazi pale LE CLUB GRANDE? Au kumbukumbu zangu haziko sawa?
:Uko sawa mkuu, miaka ya nyuma aliwahi kufanya kazi pale.
:Kwa hio flavour kapita naye? Ila wabongo, hampoi
:Naipenda nchi yangu, kila siku skendo mpya.
:Huenda hii nchi ni chaneli ya vichekesho huko mbinguni.

Maoni haya lukuki yakazidi kuipeleka mada hii kwenye uelekeo ule ule, aliokuwa anautaka.
Kiumbe huyu alikuwa mtandaoni muda huu pia, japo kwa akaunti isiyo rasmi. Kwa maana hiyo, isingekuwa rahisi kujulikana na vyombo vya usalama. Kwa kujiamini akavielekeza vidole vyake juu ya kompyuta ile na kuzicharaza herufi,

:Kwani bado tu hamjaona koneksheni yao?
Akauliza swali lililozua kizaazaa.
Neno koneksheni, kama lilivyotumika mitandaoni kumaanisha video chafu za ngono zinazorekodiwa kwa makusudi ama kimakosa.
Watu waliomuelewa wakamshukia kwa maombi na vingi viulizo, ikiwa ni kweli kitu kama hicho kipo.

:Mnadhani natania? Haya huyu nani?
Akatuma picha, ambayo iliwashangaza wengi. Ni Bebe akiwa na Kenzy, miili yao ikiwa ndani ya mavazi mepesi ya kulalia. Wamekumbatiana na tabasamu zito la huba likitalii nyusoni mwao.
Picha hii inaelezea kila dalili ya wawili hawa kuwa ndani ya chumba kimoja, hotelini.
Baada ya sekunde sitini akaifuta picha hii.
Ilikuwa picha ya kipekee, picha ambayo kila aliyejaribu kuipakua alishindwa. Waliofanikiwa kuiona upesi wakawaka kwa shauku ya kutaka kuiona tena. Lakini isivyo bahati, ilionwa na wachache.
Wakamlalamikia kwa kitendo chake cha kikatili kwa kutundika picha na kuifuta upesi.

:Mnadhani ni nini kiliendelea baada ya hapo?
Akatupa swali jingine.
Watu wakazidi kumshambulia kwa maswali na kudai udhibitisho wa ziada ambao hakuutoa. Wengine wakaifatilia akaunti yake kumchunguza. Mtu huyu ni nani?
Hakuwa wafuasi wengi mtandaoni. Lakini kitendo chake alichokifanya dakika kadhaa nyuma, kikampatia umaarufu wa ghafla.

Naam, jina la ukurasa wake aliouita kwa jina la MUTU MWEUSI ukawa gumzo kwenye mtandao huu.
Mafuriko ya jumbe nyingi kutoka kwa watu mbalimbali yakammiminikia, wakimsihi awatumie picha na video hizo kwenye akaunti zao binafsi, kama ikiwa ni kweli anazo.
Kiumbe huyu, akatabasamu baada ya kuiona fursa.
Namna ambavyo wanadamu wanalalamika kutaka kuziona tupu za wanadamu wenzao wakifanya zinaa.
Wana nini watu hawa?
Tamaa! Tamaa ya ngono.
Macho yao yenye tamaa yanang'aa kwa uchu yakidai shibe kwa kuangalia video hizi chafu zinazojulikana kama koneksheni huko mitandaoni.
Watu hawa wanaabudu fedheha kuliko utu.

Kiumbe huyu, J4 akashusha pumzi na kuchepuka kutoka mtandao ule, akaunti yake feki ikayeyuka na kusinzia ghafla. Akaifunga kompyuta yake na yeye akakisogelea kitanda kuutafuta usingizi wake.
Mtego wake umenasa tayari.
Mwanzo wa usingizi wake mtamu, ukawa ndio kengele ya kuwaamsha wale wanaokesha mitandaoni usiku kucha. Linalotafutwa ni jina moja, ama mawili hakika lakini ya mtu mmoja.
Mtu mwenye koneksheni ya Kenzy na mrembo Frola. Kampuni za mitandao zikapata wateja lukuki mida hii. Wateja wanaomtafuta mtu mmoja tu.
MUTU MWEUSI !!!

*******

Baada ya kazi ngumu ya kurekodi na mahangaiko ya uandaaji wa video ya wimbo huu, kila mtu alikuwa tepetepe kwa uchovu.
Bajeti iliyotengwa kando na Kenzy, ilitosha kabisa kukodi vyumba kadhaa vya hoteli kubwa kwa ajili ya mapumziko ya kundi lote linalohusika na uandaaji wa kazi hii.
Ni katika namna ambayo hakuelewa ilikuwaje, na wala hakukumbuka alifanya nini.
Lakini alijikuta yeye na Bebe, wameamua kupumzika kwenye chumba kimoja. Achana na chumba, hebu tuongeze ukali wa maneno kidogo. Walipumzika kwenye kitanda kimoja.
Yumkini kwa Bebe hili lilikuwa ni pumziko la kawaida. Lakini kwa Kenzy hii ilikuwa ni kama nafasi moja ya kipekee inayojitokeza kila baada ya miaka elfu.
Nafasi ya dhahabu! Nafasi ambayo hakutaka kuipoteza kabisa.
Kulala na mrembo kama huyu kwenye kitanda kimoja? Maajabu!

Pumziko hili likaanza kupata uhai baada ya ngozi za miili yao kugusana. Kila mmoja akalihisi joto la mwenzie. Wakabadilishana joto hili na damu kwenye mishipa yao ikaanza kuchemka. Hisia kali ikasafiri kwenye mishipa hii kwa kasi.
Yule Frola, akabadilika ghafla na kuwa Bebe tuanyemfahamu sisi. Bebe aliyehitimu chuo cha Profesa madam Sally.
Na sasa huyu hapa yuko kazini.
Masomo kwa vitendo bwana!

Ghafla wakachangamkiana.
Wakausahau ule uchovu wa siku nzima uliowafanya wapumzike.
Haoooo, kukurukakara, vuta n'kuvute, wakatapatapa huku na kule.
Dakika thelathini za mahangaiko zikahitimishwa kwa usingizi mzito wa Kenzy Flavour, msanii wa kizazi kipya anayetegemea kuachia ngoma yake hivi karibuni. Huku Bebe akiwa nd'o kwanza amechangamka.
Hii michezo ana uzoefu nayo. Na hapa alikuwa uwanja wa nyumbani.

Mashahidi wa tukio hili walikuwa na ahadi moja tu. Kubaki kimya milele. Japo sio wote ambao wangeitimiza ahadi hii. Wapo waliokataa katakata kubaki kimya. Na ni hawa ambao walimfanya Bebe asipate usingizi.
Binti akasimama baada ya kuhakikisha kuwa Kenzy amelala usingizi wa pono. Akanyata taratibu mpaka kwenye pembe kadhaa za chumba kile na kunasua vipande vidogo vya kamera kwa uangalifu.
Akavitunza mahali salama na kisha akaikota simu yake kufanya mawasiliano na namba ambayo alijua tu kuwa iko hewani kusubiria majibu.
DEAL DONE, akaandika.
BRAVO, akajibiwa.

Akazima simu yake na kurejea kitandani kuubembeleza usingizi. Roho yake ina amani na anauona ushindi mkubwa mbele yake. Mtego umenasa!

Inaendelea....
 
KIBIRITINGOMA
YA: Godlove Kabati

SEHEMU YA KUMI NA TANO

Jenga tabia ya kuukimbia upweke, pale unapokabiliana na changamoto zilizo nje ya uwezo wako.
Toka nje...kaongee na watu wenye busara machoni pako. Zielezee changamoto zako waziwazi.
Wakati mwingine, maongezi ni dawa bora sana ya nafsi.

Nakuandikia haya katika sehemu hii ya kumi na tano.



Yalianza kama majadiliano ya kawaida tu. Majadiliano yaliyozoeleka kutoka kwa mashabiki. Majadiliano ya amani, yanayolenga kusifia ama kukosoa video ya ngoma hii mpya mjini. Ngoma ya msanii Kenzy flavour.
Mara ghafla katika hali ambayo haikutarajiwa, katikati ya majadiliano haya akaibuka mtu ambaye alichafua hali ya hewa. Kwanza akauaminisha umma kuwa ana uhakika juu ya dhambi zilizofanywa na msanii huyu na sio uhakika tu, bali pia anao udhibitisho juu ya dhambi hizo.
Picha na video za ngono kati ya msanii huyu na huyo mrembo.
Baada ya kupingwa, kutukanwa na kumuonwa kama mwendawazimu, akafanya tukio ambalo liliushangaza umma!
Akauonjesha umma thumuni ya dhambi zile kisha akaondoka na kupotea ghafla mtandaoni.
Tukio hili likamzolea umaarufu mkubwa. Macho na umakini wa kila mtu mwenye uwezo wa kuvinjari mitandaoni vikamuelekea yeye.
MUTU MWEUSI!!
Ndivyo alijiita.
Ukurasa wake haukuwa na maudhui yoyote yale zaidi ya picha kubwa ya bendera ya taifa la Tanzania...iliyosindikizwa na maneno- NAIPENDA NCHI YANGU.
Habari juu ya tukio lake ikaanza kuota mbawa. Ikasafiri kwa kasi, zaidi ya habari njema za wokovu. Mtandao ukadhihirisha kuwa una taaluma kubwa ya utarishi. Hatimaye taarifa zikamkuta mhusika akiwa kwenye kilele cha furaha yake.

Hata yeye alikuwa akiperuzi huku na huku katika kurasa kadha wa kadha mitandaoni akiwa amelewa sifa. Na sasa alikuwa tayari kukipoza kilevi hiki kwa kusoma maoni yanayolenga kumkosoa.
KONEKSHENI YA KENZY NA FROLA Akashtuka!
Alipigwa na butwaa mara baada ya kusoma kichwa hiki. Akapangusa tena simu yake katika namna ya kutaka kuusoma ujumbe ule vyema.
Mara akakutana na picha yake akiwa na amemkumbatia Frola wakitabasamu. Ni mavazi mepesi ya kulalia pekee, yamewastiri na mdomo wake umeivamia shingo ya Frola, kutaka kuachia busu mwanana.
Mabadiliko ya kasi ya upumuaji yakaongezeka. Moyo nao ukaanza kushindana na kasi ya pumzi zake.
"Mungu wangu!"
Akamkumbuka Mungu huku maswali lukuki yakiogelea akilini mwake, ni nani, wakati gani, na kivipi picha ile imechukuliwa?
Kabla hajafikiria juu ya jibu lolote lile, simu yake ikanguruma. Alipoitupia jicho akaipokea upesi, baada ya kugundua kuwa ni Bebe amempigia.
"Kenzy..ni nini umefanya?!" Huenda hili lilikuwa swali gumu zaidi kuliko yote aliyowahi kukutana nayo kwenye mitihani yake yote ya maisha.
"Kenzy umepanga kunidhalilisha? Unataka kunichafua eh? Ina...ina maana ulitaka nilale na wewe, halafu unirekodi si ndio?" Bado hajajibu swali la kwanza, wakati anagugumia kujibu swali, anaongezewa swali.
"Wewe ni shetani! Sikujua kama ulipanga kunifanyia hivi..." Bebe ama Frola, analalamika huku sauti yake ikianza kuhama kutoka kwenye jahazi la ujasiri na hasira, sasa inaangukia kwenye bahari ya kilio.
"Fro..Frola. Sikia, mimi sielewi chochote. Ndo naona sa'hivi hapa. Kwani..sikia hebu ngoja! Kata simu huko niongee na Anko hapa kanipigia. Nitakutafuta baadae! Nisaidie kukata simu tafadhali."
Simu ya mjomba wake inaingia, na ile ya Frola anayelia inakatwa kisharishari.
Mjomba naye ana ajenda ileile.
Kenzy amepagawa hajui anajitetea vipi. Anatamani autupe mpira huu wa lawama kwa wahuni ambao huenda wame-edit. Lakini hana uhakika wowote ule, labda ni kweli hata video zake zimeanza kuzagaa kwa watu huko mitandaoni.
Je, hata huyo Kenzy wa kwenye video atakuwa siye yeye?
Alichoka.
Akiwa bado anayasikiliza maswali mazitomazito kutoka kwa mjomba, simu yake inapokea jumbe lukuki kutoka kwa marafiki zake na baadhi ya wasanii anaofahamiana nao.
"Mbona hunijibu?"
Mjomba anadai majibu yake kwa sauti iliyovimbiwa hasira.
Kenzy akaikata simu ile mara moja. Akakipa kichwa chake jukumu la kuibeba mikono yake yote miwili katika namna ya majuto.
Furaha yake ilikuwa imetumbukia nyongo. Tayari amenasa kwenye mtego. Ni kama tahira aliyewekwa ndani ya chumba cha duara na kupewa agizo la kuitafuta pembe ya chumba hiki. Anazunguka tu, bila kuiona.
Akiwa katika hamaniko hili, mara inaingia simu nyingine. Namba mpya kabisa! Hataki kuongea na mtu yeyote kwa sasa.
Anaikata simu yake, lakini haikatiki. Anaipokea kwa hasira akiporomosha matusi mfululizo. Kitu pekee anachoambulia kutoka upande wa pili ni kupewa salamu ya kiungwana na pole kwa yale yaliyomkuta.
"Inaonekana hauko sawa kuzungumza na mimi kwa muda huu. Basi ukiwa tayari, nitakupigia. Najua utanitafuta tu...tutaliongea hili suala liishe."
Sauti ile nzito ilitamka kwa utulivu.
"Who are you eh? We nani? Na ni suala gani hilo unalozungumzia kuwa liishe? "
Kenzy akauliza kwa jazba.
"Sasa hapo nianze kukujibu swali la kwanza ama la pili?"
"Usinipotezee muda aisee..." Anafanya juhudi za kuikata simu hii, lakini anagundua kuwa hawezi kuikata.
"Naitwa Mutu mweusi. Ni matumaini yangu kuwa tayari umelisikia jina hili ndugu yangu!"
Kwa utulivu wa hali ya juu, sauti ile ikajitambulisha.
Kenzy ambaye basi halikuwa haelewi lolote kuhusu jina hili, akatapatapa bila kujua ajibu nini..
"Mtu mweup...mweusi?!"
Hakukuwa na muda wa majadiliano. Simu ile ikajikata ghafla.
Kengele ya hatari ikalia akilini mwa Kenzy. Akajipa dakika chache sana za kuyakumbuka matukio yote aliyoshiriki na Bebe siku ile hotelini. Halmashauri ya kichwa chake, ikaja na jibu la ni wapi ataupata msaada wa haraka. Upesi miguu yake ikambemba kuelekea kwa BIG, mzazi na mlezi wake katika sanaa.

******

Hali ya utulivu aliyoikuta kwenye studio hii baada ya kufungua mlango, iliendelea kumtisha zaidi. Tofauti na siku zote, siku hii studio ilikuwa imepoa sana. Ni kama nayo ilikuwa inamtazama kwa kuibia, baada ya kupata taarifa zake.
Kenzy akanyata, akichelea sauti za hatua zake kusikika. Akaingia kwa namna ya kipekee, tofauti na alivyoingia kwa mbwembwe mara ya mwisho mahali hapa.
Yuko peke yake, leo hana wapambe wala wale walinzi shupavu waliovimba kwa mazoezi. Ni mnyeyekevu na sura yake inatangaza huzuni.
"Tupo aisee, karibu sana!" Sauti kavu kutoka kwenye pembe ya chumba hiki ikamshtua katika namna ya kumkaribisha.
Ilikuwa sauti ya BIG. Yu tumbo wazi, jasho linamtiririka. Ameketi kihasarahasara juu ya kiti, mikono yake inamiliki simu ya mkononi iliyowaka. Hili likamzidishia hofu Kenzy, huenda hata BIG ameshafahamu kinachojiri.
"A-asante! Nimeshakaribia." Akajibu huku akipambana na kigugumizi chake.
Teke jepesi la BIG, likatumika kumsogezea kiti cha plastiki. Kenzy akaketi kwa kusita, ni kama mtu anayekalia kiti chenye misumari.
"Huyo MUTU MWEUSI, unamfahamu?" Katika namna ya kushtukiza lilikuwa swali la kwanza kutoka kwa mwenyeji.
"Mtu mweusi? No simfahamu na pia ninasha-" akakatizwa.
"Una uhakika kuwa huyu binti hajakuchezea mchezo mchafu?" Swali likaongezwa juu ya swali.
"Hapana...sio yeye. Nimetoka kuongea naye muda sio mrefu. Analia, amenikasirikia.." akameza funda zito la mate kwa woga baada ya kutamka maneno haya.
"Sogea karibu." BIG akajiweka sawa na kuinama kidogo. Kenzy akajisogea kwa kuburuta kiti kile.
"Sogea tena..."
Akasogea tena na kumuinamia BIG kwa ukaribu zaidi.
"Usiyaamini machozi ya mwanamke hata siku moja. Huyo msichana amekuingiza kwenye kichaka usichokijua...ama la, kama tunamsingizia. Basi chunguza vizuri uongozi wa ile hoteli mliolala usiku huo. Una maadui wengi sana mdogo wangu!" BIG akamnong'oneza. Maneno yake yamesheheni upole ni kama maneno ya mzazi kwa mwanae.
Akili ya Kenzy ilikuwa imechoka. Alimsikia pasi na kumuelewa.
"Come on BIG, Nifanye nini sasa? Eh? Huyo jamaa mutu mweusi sijui mweupe...amefanya nini? Au nd'o kanirekodi?"
"MUTU MWEUSI...ni jina la akaunti iliyoanzisha hiki kizaazaa huko mtandaoni jana hiyo. Lakini muda huu hayupo tena online." BIG akanong'ona tena kwa upole.
"Nimeongea na mtu leo..amejitambulisha kwa hilo jina..." Kitendo cha kutamka maneno haya kikamkurupua BIG. Kenzy akaendelea,
"Amesema kuwa anataka tuongee ili kusudi hili sakata liishe kwa amani. Pia amesema kuwa-" akakatishwa.
"Haya mpigie sasa hivi...muongee yaishe. Msikilize anachokitaka, kama anataka kiasi cha fedha we mpe tu!" BIG akadakia.
"Lakini hapa..."
"Hakuna cha lakini hapa mdogo wangu...wasanii mnatofautiana na wanasiasa kwa sentimita chache sana. Muda wote skendo zinawaandama ili tu kuwachafua. Nisikilize, mimi nina uzoefu na hii industry najua hilo unalijua. Mara nyingi mikasa ya namna hii huusisha hela tu...wahuni wenye njaa wamekuzidi ujanja wamekuzunguka na kukurekodi. Wanataka uwalipe...hilo tu!" BIG amechachamaa, yupo wima, mikono yake inaelea huku na kule kwa msisitizo kila anapoyatamka maneno yake.
Kenzy akaguna. BIG akaendelea kulikamata dimba,
"Mpigie muda huu...muulize anataka kiasi gani. Hizo video azifute kama ni kweli anazo...na najua anazo. Haya upesi, usipoteze muda." Akaweka nukta.
"Lakini nina uhakika gani kama anazo kweli? Na je kama ikitokea ni kweli nikamlipa, itakuwaje kama asizifute na aendelee kuninyanyasa?" Kenzy akarusha karata yake iliyopambwa kwa maua ya hofu na mashaka.
BIG akashusha pumzi ndefu na kutua juu ya kiti chake kilichobonyea na kunesanesa shauri ya uzito wake.
Akapangusa jasho lake kwa kutumia kipande kipana cha kitambaa, kinachotokana na vazi lililochanika.
"Sikiliza mdogo wangu. Hii ni kamari! Na daima, tunacheza tukitegemea kupata zaidi kuliko kukosa. Ni punguani pekee atakayecheza kamari akitegemea kupoteza. Haya sasa ni juu yako..uwe punguani au uwe-"
"Amepiga!" Kenzy akamkatisha BIG. Mkono wake uko hewani umeikamata simu yake inayoita.
"Eeh ni yeye...ni namba yake hii. Amepiga!" Kenzy akatamka huku macho yake yaking'ara kwa hofu.
"Shhhhh!" Kidole cha shahada kikiwa wima mdomoni, BIG akamuashiria Kenzy akae kimya. Akanyata na kuichukua simu yake na kuzinakiri namba zile zilizopiga. Kisha akamuashiria aipokee simu ile.

"Bado tu hujatambua mimi ni nani...bwana Kenzy Flavour?!"
Sauti kavu ikatupa swali.
"Sikia bro...naomba tuongee. Kwa-kwani we unataka sh'ngapi bro?" Akiwa na hofu, anauliza huku anamtazama BIG.
BIG ambaye yuko bize na simu yake huku akiyafuatilia maongezi yao kwa karibu.
"Mia hamsini!"
Sauti ile ikaunguruma.
"Mia hamsini...yaani laki moja na nusu au?"
"Sifanyi biashara za pipi mzee...hapa naongelea milioni."
Paaaaaa! Moyo wa Kenzy ukapiga kishindo kikubwa. BIG naye akagutuka. "Milioni mia?!! Aaah kaka...milioni mia ni mbali sana kaka. Nisaidie kaka, usiziposti hizo kaka. Nitaaibika mimi." Yuko katikati ya kulalamika na kulia, Kenzy anajitetea.
Kwake neno milioni mia tu...lilimtisha. Achana na hio hamsini nyingine aliyoisahau.
"Kabla ya leo saa nne kamili usiku. Nategemea niwe na hicho kiasi kwenye akaunti yangu ya benki. Ukiipata nitafute, nitakupa maelekezo yote! Shime." Simu ikakatwa.
Sauti yake haina utani hata kidogo. Iko mbali kwa maili nyingi sana na neno kicheko. Kenzy akamtazama BIG usoni.
"Faza umeyasikia haya?!"
"Duh! Nimeyasikia aisee. Mpango wako ni upi?" Akajibu huku cheko jepesi likiangaza u Hili halina mjadala. Kicheko hiki, kikazidi kumkasirisha Kenzy.
"Huyu mwamba anataka kuniangushia jumba bovu huyu. Yaani hundred millions? BIG...mia moja kweli? Hii si bajeti ya kutengeneza albamu kabisa? Tena audio na video?" Kenzy amekunja ndita.
"Hiyo hamsini nyingine unayoiacha, nitakulipia mimi au?" Swali hili baridi likamsindikiza Kenzy mpaka juu ya kiti.
Ameshika tama anahuzunika.
"Nimejaribu kuifatilia hii namba...inaonekana anayeitumia hayupo hapa Bongo. Yuko Thailand! In short hapa unapigana vita na mtaalamu wa TEHAMA. Na sioni kama utashinda mdogo wangu. Sidhani..."
Kenzy akaanza kupumua kwa kasi, hasira, majuto na wasiwasi vyote vinammliki.
"Sidhani kama huu ni wakati wa kutumia hasira. Sikia, ni wiki moja tu tangu utoe hiyo ngoma. Jambo jema ni kwamba, bado hii taarifa haijashika attention za watu wengi."
"Mpaka mjomba wangu, Mwalimu Rama kanipigia...unasema haijashika attention?"
Akalalama.
"Sawa, sikia...ukimya wako mtandaoni unazidi kuwaaminisha watu juu ya hili janga lililokukuta. Fanya hivi...nenda online. Kazikanushe hizi taarifa. Waambie watu kuwa, hicho kilikuwa ni kipande tu kati ya scene za kushoot, ambacho kilihairishwa. Baada ya hapo sasa mrudie tena huyo jamaa yako, muanze sasa kushushana bei."
Wazo lake likasikilizwa. Baada ya mashauriano ya hapa na pale, Kenzy na BIG wakaagana.
Kuagana huku kukaambatana na kitendo cha Kenzy kuingia mtandaoni na kuzikanusha taarifa hizi zinazosambaa kwa kasi.

Akiwa ndani ya gari lake, roho ya kiburi ikamtembelea, akaikaribisha na kuketi nayo siti moja. Akaipa sikio lake, nayo ikamshawishi kuwa asiwe mwepesi kuamini kila kiti cha mtandaoni. Bali awe mgumu ili aone kitakachotokea. Kwani yeye ni wa kwanza?
Kwani ni jambo gani la ajabu ambalo kalifanya na halijawahi kufanywa na watu mashuhuri zaidi yake?
"Yaani kisa nimelala na Frola...kamera zikatunasa ndio nitoe kila senti iliyoko benki nikampe jamaa?! Thubutu.. labda sio mimi Kenzilaba mwana wa Kisaunga." Kenzy akajipeperusha akiyataja majina yake ya ukoo.
"Hivi anadhani mimi ni mjinga mjinga eh? Yaani kapicha kamoja tu, nikanunue kwa milioni mia na hamsini? Kweli? Fokofuu!"
Akasonya na kuendelea kuugeuza usukani wa gari lake.
"Limtu linaona nimeanza kutikisha kwenye mitandao huko...ngoma zangu zinafanya vizuri halafu lije lichukue mirabaha hivihivi. Yaani hivihivi kize-"
Mara kioo cha simu yake kikawaka, na simu yake ikanguruma kuashiria kuwa ujumbe umeingia. Akaipuuza na kuendelea kuendesha gari lake. Lakini moyo wake ukakosa amani, akaamua kuiokota simu ile na kutazama kunani?
Paaa! Puuu! Paaa!
Moyo wake ukaruka mapigo kadhaa. Alichokiona kikazua kizaazaa...ni heri labda asingeiokota simu ile.
Ni heri labda asingekuwa na umaarufu, ni heri labda asingekutana na huyu binti Frola usiku ule.
Ni heri labda, labda....



Inaendelea....
 
CamScanner 09-06-2026 00.55_1.jpg
SEHEMU YA KUMI NA SITA


Alisema, hayati Shaaban Robert gwiji na fundi wa fasihi ya Kiswahili.
Utajiri wa maana zaidi kwa mtu yeyote ni kuwa na jina jema miongoni mwa vinywa vya watu.
Hata leo hii mimi nakuasa kujitahidi sana, kuilinda heshima ya jina lako miongoni mwa watu.
Maisha yetu ni mafupi sana katika dunia hii yenye zaidi ya miaka milioni.
Uchaguzi ni wako...utakapondoka, uwe historia au uache historia.
Nakuandikia haya kwenye sehemu hii ya kumi na sita.

________________________



Nisikilize Kenzilaba,
Nimetoka kutumiwa huu uchafu, hivi punde na huyo wa kujiita MUTU MWEUSI.
Mwanzo aliponitafuta, nilimuona kama punguani. Nikamdharau...
Lakini baada ya macho yangu kukosa pazia na kuiona hii video fupi, uvumilivu umenishinda.
Umenifanya niiamini ile kasumba kuwa wasanii ni wahuni na wadhambi.
Kila kukicha mnajitapa kuwa nyinyi ni vioo vya jamii, haya ni nini hiki ambacho umeakisi? Au jamii yetu inafanya ufuska na kujirekodi ili kujifurahisha?
Umeendekeza kuandaa video zisizo na maadili. Umezungukwa na mabinti lukuki ambao sio kwamba wako nusu uchi tu, bali ni kama wameamua kuziweka wazi sehemu zao nyeti.
Tazama ulichokivuna sasa mwanangu,
Umelala na binti wa watu, ukamlubuni mfanye ngono, halafu ukajirekodi au sio? Unadhani mzee Kisaunga akiuona huu uchafu atakiri kuwa we ni mwanae?
Kenzilaba,
Nilipokupigia simu kukuhoji, uliikata na kunifokea kuwa niachane na maisha yako. Ukadai kuwa unajua unalolifanya.
Mnasema ujana ni maji ya moto eh?Sawa...endelea kuukumbatia huo moto. Utakubabua ngozi yake na kukuacha mtupu.
Unajidanganya sana kutafuta starehe za muda mfupi.Halafu ukikosolewa, unajiona uko kwenye njia sahihi.
Ni sawa mjomba. Nisikilize!
Sitaki unipigie simu wala ufanye chochote kile kabla ya kufuata hiki ninachokuelekeza.
Aliyenitumia huu upumbavu, anadai kuwa mnadaiana kiasi fulani cha fedha.
Ameapa kuwa hatosita kuziweka hadharani kama sio kuzitangaza, mpaka pale utakapomalizana naye.
Bado nina wasiwasi na usanii wako mwanangu!
Sanaa haiendi hivyo! Shauri yako.

Ulikuwa ni ujumbe kutoka kwa Mwalimu Mathias. Mtu ambaye hakumuheshimu tu, bali pia alimuogopa. Ujumbe huu haukutumwa peke yake, uliambatanishwa na kipande cha video fupi.
Kulikoni?

Nukta ya sentensi ya mwisho ya ujumbe huu, ukawa ni kama fungua semi kwa video ile kuchezwa.
Kenzy akapigwa na butwaa kwa kile alichokiona katika video ile. Ni kama aliyeirekodi alikuwa karibu yao na alitumia kamera yenye ubora mkubwa.
Kitu kiko HD!
Mvurugano kati ya utumbo mdogo na ule mpana vikaanza kumsumbua Kenzy flavour. Akasisimka! Bado haamini kama hata mjomba wake aliiangalia video ile na kuimaliza yote.
"Au sio mjomba Mathias huyu?" Akajiuliza.
Akakagua kwa mara nyingine simu yake na kujihakikishia kuwa aliyemtumia ujumbe huu si mwingine bali ni yuleyule mjomba wake. Macho yake hayakumdanganya.
Ile roho ya kiburi iliyokuwa imemtembelea, safari hii ikavua kinyago chake na kugeuka kuwa roho ya hofu. Ikamualika na rafiki yake, roho ya mashaka.
Wote waketi kando ya Kenzy, Kenzilaba.

"Ooho! Habari ishakuwa kubwa!" Akili ikamkaa sawa. Akuthubutu kuendelea na safari yake kabla hajatafuta eneo la kuliegesha gari lake.
"Kama huyu mtu mweusi ameweza kumfikia mjomba wangu, basi si shaka kuwa anaweza kuwafikia ndugu na jamaa wa karibu zaidi." Akatamka na nafsi yake, akiwa na tahadhari kubwa juu ya vitu kama hivi kumfikia mtu yeyote yule.
Dhambi ni salama kwa yule aliyeifanya kama tu ikitendwa gizani ama kwenye maficho. Lakini ni kama moto mkali unaoteketea kama ikiachwa waziwazi ionwe na kila mtu.
Kwa mtu mwenye umaarufu kama yeye, katu hakuwa tayari macho yote ya watanzania wote yashuhudie namna anavyohangaishana na Frola juu kitanda.
Kenzy akabaki na chaguo moja tu ili aulinde wajihi wake, aitafute hii fedha mahali popote pale ilipo na amalizane na huyu MUTU MWEUSI.
Alitaka alitekeleze hili kimyakimya bila kuwahusisha watu wake wa karibu. Ni jina moja tu lilimlomjia akilini kiwa huenda likawa na msaada katika jambo hili.
Akainyanyua simu yake na kulitafuta jina hili lilipo, akalipigia simu.

"Haloo Fro-Frola!"
Kimya!
Anayepigiwa ni kama yuko mtungini.
"Frola! Unanisikia?" Akauliza tena kwa jazba iliyochanganyikana na wasiwasi.
"Kenzy." Sauti nyororo iliyo katika kilio, ikamuitikia katika namna ya kulitaja jina lake.
"Vipi umekuwaje tena?! Mbo-mbona unalia?"
"Amenitumia hizo video Kenzy...anataka tumpe hiyo hela la sivyo atazipeperusha mpaka kwenye vyombo vya habari! Anadai kuwa huo uwezo anao!" Kitu kama kisu kikali kikatua kwenye kifua cha Kenzy baada ya kuyasikia maneno haya.
Bebe alikuwa katumiwa "Hizo video" na wala sio video moja.
Dunia ilikuwa inamtumia ujumbe wa kutisha Kenzy.
"Si-sikia Frola! Usijali. Hili litaisha na nitampa hizo hela zote. Lakini ninapungukiwa na kiasi kidogo tu Frola. Mimi sasa hivi naweza kupata kama milioni themanini za uhakika, na hapo nitakuwa nimeipangusa akiba yangu yote iliyo benki. Vipi kama ukinisaidia kama milio-"
Kabla hajamaliza maneno yake. Bebe akayadakia mazungumzo,
"Themanini? Yaani wewe na wenzio mlipanga kunitega ili mniaibishe halafu mnidhulumu sio? Ndio malengo yenu wasanii eh? Hii nd'o michezo mnawafanyia madada wote kwenye hoteli zenu?! Nijibu Kenzy, nijibu!" Bebe amewaka kwa hasira. Bado sauti yake imelowa machozi lakini matamshi yake yamejaa uhai wenye shari.

"Hapana Frola! Ha-hata mimi sielewi ni nini kimetokea mpenzi. Nime-"
"Koma! Mimi sio mpenzi wako!" Bebe akalipuka.
"Come on Fro...usikasirike mamy. Hili ni jambo kubwa na limetukuta wote. Hizo milioni mia hamsini ni nyingi Frola. Imagine a hundred point five M, girl. Just imagine!" Kenzy akajaribu kuipaka rangi lugha yake kwa lahaja za kizungu na kibantu lengo lake ni lilelile, amlainishe Frola mpaka alainike kisha wote walipe fidia ya dhambi yao.
"Wewe mvulana una matatizo." Kauli hii ikageuka kuwa ngumi ya tumbo kwa Kenzy. Ameitwa mvulana!
"Siku ile uliniita chumbani kwako tena ukaneng'eneka weeee, mpaka ukanishawishi nikupe tunda. Nakumbuka namna ulivyokuwa unajibebisha na kunipapasa, lengo lako lilikuwa ni hili eh?Kenzy we ni shetani! Mdanganyifu na muharibu maisha ya watu.
Unadhani nashindwa kwenda kukuchafua mitandaoni kuwa uliniingilia kwa nguvu na kunibaka?" Sindano nyingine ya moto, ikachomwa kwenye kichwa cha Kenzy kilicho na nywele nyingi katika mtindo wa rasta.
Kenzy akajikuna kichwani kwa nguvu bila kujua ni nini kimemuwasha. Bebe anataka kuongeza viungo kwenye chungu chake cha sifa mbovu, kinachopikwa kule mitandaoni.
"Wewe ni tapeli Kenzy...laghai na mbwa!"
"Basi Frola inatosha..." Anajaribu kuishusha sauti yake ili kuituliza dhoruba hii ya hasira kwenye matamshi ya Bebe.
"Inatosha? Inatosha vipi wakati unataka kuniharibia maisha yangu?" Bado Bebe amechachamaa.
"Yameisha Frola!"
"Hapana Kenzy, siwezi kukuelewa kwenye hili. Au ulitumwa kuichafua sura yangu kwen-" Sauti yake haikusikika ikiendelea kuongea zaidi, Kenzy aliikata simu hii akiwa amevimba. Sio kuvimba mwili. Alivimba kwa hasira.
Kifua chake kilikuwa kimejaa matusi mazitomazito ambayo hakujua ayamwage kwenye masikio ya nani.
Hakuwahi kumtukana mwanamke hata siku moja na hii ndio sababu aliacha kuongea na Bebe mara moja.
"Shenzi kabisa!" Akalipuka huku akiigonga simu yake kwa nguvu juu ya usukani.
Sauti kali ya honi ikalipuka na kumshtua mbwa-koko mzee ambaye alikuwa amejipumzisha kando ya gari lile. Huyoo akakimbia akiwa ameufyata mkia wake.
Ni kama ambaye ameogopa vitu viwili kwa wakati mmoja. Kaiogopa honi lakini zaidi ya yote, aliyoyasikia yamemtisha zaidi, kama tu ni kweli mbwa wanaweza kuelewa yanayozumgumzwa na wanadamu.
Kenzy akamtazama kwa macho ya kisirani. Anatamani amshukie na kumpasua lakini anahofia kuonekana mwendawazimu.
Hata hivyo nd'o kwanza alikuwa anaelekea uwendawazimuni.
Akashusha pumzi ndefu.

Ghafla simu nyingine ikaingia. Sasa akaitazama simu yake kwa jicho la woga. Anaiona kama bomu ambalo litamlipukia muda wowote.
"Mama!" Akalitaja jina hili huku akimeza funda la mate.
Maswali mengi yanafanya riadha kichwani mwake. Na huyu kaambiwa nini?
Mkono unamtetemeka, akaipokea simu kinyonge.
"Shikamoo mama!"
Siku hii akatanguliza salamu. Sio kama siku nyingine ambazo alikuwa anazipokea simu za wazazi wake kwa namna ileile anavyozipokea za mashabiki wake. Supastaa!
"Kenzilaba mwanangu!" Mama akamuita kwa utulivu. Sauti yake imepambwa kwa lafudhi ya kabila la kikwao, japo hii haioneshi hasira wala jazba. Imejaa upendo na amani.
"Naam mama." Akaitika kwa nidhamu.
"Una nini mwanangu?"
Kimya!
"Wamekufanya nini huko?" Mama bado anauliza.
Kenzy hajui ajibu nini. Mkono wake mmoja ukaenda kinywani. Labda mjomba ameshayaharibu huko, hakujua. Ghafla jibu la haraka likamjia,
"Mama nani amekutafuta? Eh? Kwani kuna mtu amekwambia nina shida?" Anapambana kujitoa kwenye hofu, lakini sauti yake bado ina kigugumizi.
"Kuna mtu kanipigia hapa, anasema una matatizo. Mimi nikadhani labda mwanangu umevamiwa. Au labda watu unaumwa. Si unajua tena watu huku kijijini wanavyokuonea tamaa eh?"
Kenzy akashusha pumzi.
"Mimi mzima mama. Wala sina shida yoyote ile. Ni watu tu na roho zao mbaya mama!" Anajitetea.
"Eeh maana hata huyo aliyenipigia, ana sauti kavu huyoo. Kama jambazi!" Mama akaisindikiza sauri yake kwa kicheko. Kicheko hiki cha upendo kikageuka kicheo cha kigaidi kwenye masikio ya Kenzilaba.
"Amejitambulisha jina?"
"Eeh anaitwa, nani vile? Mweusa..sijui mweusi. Kama sikosei ni mtu mweu-" Kenzy akakata simu ile upesi, akaizima na kuitupa kando. Ilikuwa imeanza kuwa ya moto. Labda nd'o bomu lenyewe lililochemka.
MUTU MWEUSI alianza kugusa anga za mbali. Safari hii hakutaka msaada wa mtu yoyote.
Akaliwasha gari lake na kupepea kuelekea popote alikokujua zinapatikana milioni mia hamsini.


**********


"Naam Bebe! Niambie, amesemaje?"
"Duh! Eti anataka nisaidiane naye kulipa huo mpunga wote."
"Aiseee...sasa hapo si tutakuwa tunajitekenya na kucheka sisi wenyewe?"
"Weee thubutu, sijampa nafasi ya kupumua. Nimempiga mabomu hayo, mpaka akaachia kamba yeye mwenyewe."
"Wacha weee!"
"Kweli tena...sa sijui we uyafanyaje auachie huo mzigo fasta!"
"We niachie mimi. Kesho asubuhi, njoo uchukue tembo zako!"
"Utafanya nini sasa, make ujue huo ni mpunga mrefu ujue?"
"Hizi game huwa tunazicheza kwanza nje ya uwanja mrembo. Tukishinda nje, tunakuja uwanjani kukamilisha ratiba tu."
"Mmmh...sawa, mi yangu macho na masikio ety."
"Ongezea na pua na mdomo."
"Hahah kwa nini?"
"Pua itanusa harufu tamu ya vinono na mdomo utavifaidi hivyo vinono."
"Hahahaha ila J4 kwa maneno. Sikuwezi we mkaka."

Simu inakatwa.
Kwenye chumba chake chenye giza jepesi, mtu huyu anaigeukia kompyuta yake ndogo na kupekua mafaili kadha wa kadha.
Amekesha hapa siku nzima akifanya kazi ambayo ni ya muhimu zaidi kwake.
Kazi ya kumchezesha msanii Kenzy ngoma ambayo anaipiga yeye mwenyewe.
Tayari ameidukua nambari ya simu ya mjomba wake na kuitumia kumtumia ujumbe wenye kitisho pamoja na video ya aibu.
Na sasa yu makini juu ya uso wa kompyuta yake. Kuna data anazozitafuta akiamini kuwa endapo akizitumia hizi, mateka wake atanasa kwenye mtego wa kitaalamu zaidi.
"Huyu mshenzi bado hajalewa huyu. Ngoja nimshtue mama yake!"
Ananakiri namba fulani kutoka kwenye kompyuta hii na kuipigia simu.
Anajitambulisha kwa jina la MUTU MWEUSI. Na anatuma ujumbe fulani kwa namna ya usamaria wema.
Anafahamu anachokifanya. Baada ya dakika mbili za mazungumzo, anatulia.
Anaivuta chupa yake ya maji ya matunda na kujiburudisha. Kisha anakisogelea kitanda chake na kujilaza.

Baada ya masaa manne, anashtuliwa na mlio wa kitu kama kengele. Ni ujumbe ambao umeingia kwenye kompyuta yake. Anairudia na kuusoma. Anatabasamu.
Mateka wake amesalimu amri!


*********


Alikuwa kwenye kubahatisha tu kama namba hii itamjibu baada ya kujaribu kuipigia kwa muda mrefu na isipatikane.
Akaandika ujumbe mfupi na kuitumia.
"Sijui atanijibu huyu?" Akajiuliza.
Rasta zake kichwani ziko timtimu, sio nadhifu kama zilivyozoea kuwa.
Uso umeungana na kifua chake kulowana kwa jasho, fulana yake nyepesi pia haikukubali kubaki nyuma kwenye hili.
Yu ndani ya gari lake alilolizima, anahema juujuu.
Macho yake yametulia juu ya kioo cha simu yake. Anageuka na kutazama pembeni yake kama mzigo alionao bado upo salama.
Naam, upo salama na unapumua.
Bado haamini. Anaufungua na kupitisha mkono wake akiukagua, hapa anaridhika.
Anatumia fulana yake ileile aliyoivaa kujipangusa jasho usoni.
Mara simu inaita. Ni namba ngeni ileile, inayosemekana ni ya yule...MUTU MWEUSI.
Anaipokea kwa hofu,

"Enhe...vipi sasa!" Sauti nzito inahoji.
"Mkuu...ninao mzigo tayari. Nasubiria tu maelekezo yako ni wapi tukutane nikupe, tumalizane." Sauti yake imechoka. Anatangaza huruma na unyonge.
"Ooh Okay, safi sana. Nakupatia maelekezo. Uko tayari?" Sauti ile inauliza.
"Nipo tayari! Lakini nina ombi moja tu kaka yangu..."
"Nakusikiliza. Fanya haraka nina mengi ya kufanya."
"Sisi ni wanaume...tunatafuta kwa jasho na njia zetu za utafutaji ni ngumu sana ndugu yangu. Sina uhakika kama-" akakatishwa.
"Sitaki mashairi ndugu msanii. Nenda kwenye point!"
"Sawa..naomba unipunguzie walau milioni thelathini kaka. Maisha yangu ya muzili yanategemea sa-"
"Kwenye ngoma yako ya ME AND YOU, ulisema kuwa pesa kwako sio shida, ila penzi lake tu sivyo?"
"Eeeh...ila ni verse yu kwenye-"
"Leo saa tano usiku tukutane LE CLUB GRANDE. Ukithubutu tu kunifanya uhuni, litakalokukuta sitohusika."
Simu ikakatwa.
Masaa yakasogea, unasubiriwa mshale wa saa tu usomeke muda wa miadi.


Itaendelea, Jumatano ijayo, usiku....
 
KIBIRITINGOMA

SEHEMU YA KUMI NA SABA

Utauziwa bidhaa nyingi sana kwenye huu ulimwengu.
Nyingine utazinunua kwa kupenda na nyingine utazinunua bila kupenda.
Chunga sana, usilitembelee duka la hofu.
Utainunua hofu kwa gharama kubwa, kisha utakaa nayo ndani mwako, ikisubiri muda na wakati sahihi wa kukumaliza.
Hofu ni bomu linaloua na kuzika!
Usiinunue hofu

Nakuandikia haya katika sehemu hii ya 17.




Abarikiwe sana yule mgunduzi wa ala za muziki. Na abarikiwe zaidi, Mungu aliyetuumbia muziki. Akaupa ladha ya ajabu. Ladha inayoweza kuituliza mioyo ya watu, ikaiburudisha, ikawafanya watu wasimame na kuitikisa miili yao katika namna ya kucheza.
Hata jioni hii hapa LE CLUB GRANDE, baadhi ya watu walikuwa wima, mikono yao juu, vitambaa vyeupe vikipepea hewani kufuatisha muziki uliokuwa ukitumbuizwa na bendi.

Nainua mkono mama, kitambaa cheupeeee!
Ishara ya mapenzi mamah, oooh Zimorah!

Watu waliendelea kuvitikisa viuno vyao huku na huko. Ambao hawakusimama kucheza, vichwa vyao viliendelea kunesanesa. Ilikuwa ni burudani!
Burudani kwa wote, isipokuwa kwa huyu mwanaume mmoja aliyejibanza kwenye upenu wa ukumbi huu.
Huyu hakutaka kabisa kuonekana na watu. Kwanza sio kawaida yake kwenda kwenye kumbi za starehe ovyoovyo bila kutoa taarifa kwa wamiliki wa kumbi hizo.
Yeye ni mtu mkubwa sana!
Na hata akizitembelea kumbi hizo, lazima ataomba kinasasauti na kutumbuiza wale waliokuja kujistarehesha maeneo hayo.
Sauti yake ni ya gharama kubwa sana. Lazima ilipiwe!
Kwa maana hiyo kitendo cha yeye kuwepo kwenye ukumbi fulani wa starehe, kilikuwa ni fursa ya kujipatia viingilio kwa wamiliki wa kumbi hizo.
Yaani Kenzy Flavour awe LE CLUB GRANDE, halafu watu waingie bure? Hili lilikuwa ni kama tusi la nguoni kwa Madam Sally.
Lakini leo hii mambo ni tofauti. Leo yupo hapa kwa bahati mbaya. Kwa mtu yeyote ambaye angemuona basi angedhani ni sawa na malaika aliyepotea njia na kujikuta jehanamu. Hakutaka kujulikana kabisa!
Anajitahidi kuuficha wajihi wake kwa kuvaa kofia kubwa na mwili wake kwa koti pana jeusi. Katikati ya miguu yake limetulia briefcase juu ya ardhi na mkono wake wa kulia ambao haueleweki kama unatetemeka kwa baridi au la, umeibeba simu. Anasubiria wito kutoka kwa mtu maalumu wa kujiita MUTU MWEUSI.

"Yaani leo lazima nimjue huyu fala ni nani. Na kama ikiwezekana, namfumua hapahapa!"
Yu katika mazungumzo ya siri na akili yake ambayo inamshauri juu ya mbinu fulanifulani za kumtia mbaroni huyu MUTU MWEUSI.
"Kwanza ni kwa nini isiwezekane? Ni lazima nimfumue." Akajisahihisha.
"Ma'ke hapa, hana pa kuchomolea. Akija yeye namfyeka! Labda amtume mtu! Na huyo mtu akija tu, nambana huyohuyo. Mimi sio mlainilaini kama alivyodhani." Akaendelea kujipa ushauri huku akijipapasa kiunoni mwake.
Bastola yake ilikuwa inapumua kwa uhai.
"Ipo! Sasa ajichanganye tu...ninaye huyu." Akajipeperusha.
Alikuwa amelenga kuua kabisa!

Mawazo yake yakamgeukia yeye, akajikagua moyo wake. Alikuwa anaogopa! Licha ya kumiliki silaha ile, mapema sana alikuwa amesalimu amri tayari kwa kuzitafuta milioni mia na hamsini tena ka hofu kubwa ili amlipe huyu MUTU MWEUSI na aipoteze aibu yake.
Hili tu lilitosha kumsuta kuwa ameshapoteza mchezo akiwa nje ya uwanja.
Ghafla simu yake ikaita na akaipokea upesi bila kusita.
"Nisikilize Kenzy!" Sauti ya mtu yule simuni, ikaunguruma.
"Ni matumaini yangu kuwa, haijapungua hata senti kwenye hilo sanduku lako." Akahoji.
"Nimeleta yote! Mia hamsini, kama tulivyokubaliana." Kenzy akamjibu kwa sauti inayoelea kwenye nusu woga na nusu kujiamini.
"Safi...sasa iko hivi, angalia pembeni yako upande wa kulia hapo uliposimama."
Kenzy akageuza shingo yake na kutazama alikoelekezwa. Macho yake yakapambana na giza jepesi lakini bado hakuelewa MUTU MWEUSI alimaanisha nini.
"Umeona nini?" Likawa swali gumu.
"Mmh...hapa sioni kitu, kwani kuna-kuna nini?" Akauliza.
"Una uhakika huoni chochote?"
"Hamna kitu hapa."
"Kabisa?"
Kenzy akashusha pumzi kwa uchovu.
"Labda kama unamaanisha huu ukuta. Ndio kitu pekee ninachokiona hapa. Zaidi zaidi naona kuna maua yamepandwa halafuuu na, majani hivo tu basi. Kuna jipya?" Akajibu katika namna ya kukereka, ili mradi tu amemjibu.
"Ewaaaa! Kumbe macho yako yanafanya kazi. Sa sikia, hebu hesabu hatua zako vizuri mpaka uufikie huo ukuta. Halafu hilo sanduku ulidondoshe nje ya ukuta."
Akatoa maelekezo.
Mwili wa Kenzy ukasisimka! Akawa sanamu kwa takribani sekunde sita .
"Umenisikia?"
Kenzy akapata kigugumizi cha ghafla kilichomuweka kwenye kundi la bubu wa mkopo.
Mpango wake umepinduliwa katika namna ambayo hakuitemea.
Hajaja MUTU MWEUSI na wala hakuna aliyeagizwa aje kuchukua fedha.
Ila ni ukuta umepewa kazi hii.
Aiseee Kenzy alichoka!
Ameteketeza nguvu na nishati ya kutosha kukipata kiasi hiki cha fedha. Amefagia kila thumuni katika akiba zake na kiasi kingine akakipata baada ya kukumbatia madeni kutoka kwa watu ambao walimkopesha kwa viapo, amri na sheria kali. Halafu muda huu anaambiwa kuwa atupe utajiri huu nje ya uzio!
"Yaani unamaanisha nitupe nje briefcase la milioni mia hamsini?!" Sauti yake imetumbukia kwenye bahari ya jazba.
"Sidhani kama nastahili kupoteza hii dakika moja kulijibu swali lako. Unachotakiwa kufanya muda huu ni kufuata maelekezo Flavour!" Akatulia na kuvuta pumzi.
"Sogea hapo udondoshe briefcase nje!" Akamalizia.
Kishingo upande, Kenzy akaanza kuzihesabu hatua zake taratibu kuelekea ukutani. Ameona waziwazi namna mpango wake unavyoenda kuharibika.
Akaufikia ukuta ule ambao ulimzidi urefu kwa futi chache. Matumaini yake ya kumuona huyu wa kujiita MUTU MWEUSI, yakafifia. Akalirusha brifcase hili nje.
Kwa mbali akasikia mlio ulioashiria kuwa limepokelewa na ardhi. TI!
Akatamani awe na urefu walau wa mti ili amuone aliyeko kule nyuma ya ukuta lakini matamanio hili lilikuwa la dhahania tu. Lisingewezekana asilani.
Akatamani labda angepiga mbio upesi atoke nje ili amfumanie yule atakayeliokota. Lakini hata hili tamanio, likaifanya bastola ile kiunoni imecheke kwa dhaharau.
Huyu mpumbavu ameniweza akatamka kwa sauti ya chini.

"Tayari!" Akatoa mrejesho huku midomo yake ikimtetemeka kwa hasira.
"Ooh safi kabisa...Haya hebu sogea huku kwenye mwanga nikuone vizuri bwana, usijibanze huko gizani ndugu yangu." Sauti ile kavu ikamuamuru afanye mjongeo.
Akasogea kinyonge japo hakufika palipoamriwa.
"Sogea tena basi. Mbona unajibanabana kaka?" Sasa ilianza kuwa sauti nyepesi inayotangaza masihara. Hili likazidi kumkasirisha Kenzy.
Safari hii hakusogea!
"Bro! Nimeshakupa unachokitaka, unanidai nini sa'hivi? Eeh? Niambie bro..."
Amekunja ngumi yake. Yuko tayari kumtwisha makonde mtu yeyote aliye karibu yake. Bastola ile sasa haina msaada.
"Hahaha!"
Sauti ya kicheko ikatetema upande wa pili.
"Usikasirike Kenzilaba...ah samahani, nimekosea. Usikasirike Mr. Kenzy Flavour! Mimi na wewe hakuna tunachodaiana mpaka sasa. Hizi video zenu zimefutwa tayari na mko huru bro, kuweni na amani kabisaaa! Nina imani kuwa hata huyo demu wako amechangia chochote kitu." Akatulia kulisubiri jibu lake.
"Wewe mwenyewe uko wapi?! Njoo tuonane uso kwa uso kama wanaume!" Hakulijibu swali lake, badala yake akatoa madai yake.
"Nipo mtandaoni ndugu yangu. Jina langu ni lilelile, MUTU MWEUSI! Ukitaka kuniona, njoo hukoo nitumie ujumbe tutaonana, uzuri teknolojia inaweza kulifanikisha hili." Akatamba.
Kenzy akapigwa na baridi. Hakujua anajitetea vipi kwa kauli kama hii. Mara ghafla,
Wimbo wa taifa ukalipuka kutoka kwenye spika kubwa za klabu hii!
Sio ule wimbo wa taifa mtukufu unaoliombea bara la Afrika na nchi ya Tanzania kama tujuavyo wewe na mimi. Huu ulikuwa ni ule wimbo maarufu nchini unaovuma wakati huu. Wimbo wa taifa,
Me and you!

Kenzy aligutuka mara baada ya kuusikia wimbo huu. Wimbo wake mpya wenye siku sita tu tangu uwe hewani.
Hakuna mtu yeyote aliyekubali kubaki juu ya kiti.
Watu walisimama, waume kwa wake. Wapenzi walikumbatiana kwa mahaba. Kila mtu alikuwa akiyarudia mashairi ya wimbo huu kwa hisia kali, ndita zikijenga mistari ya kontua kwenye nyuso zao.
Hakika waliupenda sana wimbo huu.
"Unaona sasa...mimi nimekuleta huku ili uone namna ngoma yako inavyopendwa na
Watanzania kaka! Tazama wanavyocheza! Inapendeza eh?" Sauti ile ikarindima huku ikisindikizwa na kicheko.
Kicheko cha dhihaka.
Kenzy akaikata simu ile kwa hasira. Na kutoka nje ya klabu hii kubwa. LE CLUB GRANDE.
Huenda Me and you ulikuwa ni wimbo mtamu wa mapenzi, uliozikonga nyoyo za wale waliousikiliza. Lakini kwake yeye ulikuwa ni wimbo unaomkumbusha usiku wa laana, alioutumia na Bebe kwenye hoteli ile.
Usiku ambao angetamani ufutike kabisa kwenye vitabu vya historia na tarehe yake ifutike kwenye kalenda, isikumbukwe daima.
Hakutaka kujua ni namna gani mambo yanaendelea huko ndani. Akaendesha gari lake na kuondoka mahala hapa.
Kuondoka kwake kukafuatishwa na kijana maridadi kutoka ndani ya ukumbi. Alikuwa mavazi ya kisasa, kapendeza kwelikweli. Mkononi ana kinywaji katika kikombe cha plastiki cha rangi nyekundu. Kichwa chake kinanesanesa kufuatisha mapigo ya mziki yanayofifia kutokea ukumbini.
Akalisindikiza gari lile kwa macho mpaka likapotea kabisa. Kisha akatabasamu na kuitoa simu yake.
"Hey Baby, njoo hapa nje tayari nyama yetu imeshaondoka."
Akatamka kwa bashasha.


*******

Baada ya dakika sekunde thelathini, gari dogo jeupe aina ya IST likatambaa na kumfikia alipokuwa.
Alipoufungua mlango ili aingie ndani akapokelewa na harufu tamu ya manukato, yaliyomfanya atulie kwa sekunde kadhaa kuhakikisha kuwa aliyemo garini sio malaika.
"Karibu my boy, MUTU MWEUSI!" Sauti hii ya kinanda, iliyobebwa na tabasamu angavu linalong'aa gizani kutoka kwa Bebe, vyote vikaungana na harufu tamu ya manukato haya kumkaribisha.
Yeye ni nani mpaka asikaribie?
"Uum Asante." Akajibu na kuzama ndani.
Alipoketi akashusha pumzi ndefu na kumtazama Bebe usoni ambaye naye alikuwa amemtazama tayari.
Kama walioambiana vile, wakacheka kwa pamoja tena nguvu.
"Uwiii, aisee hebu ondoa haka kaIST kako hapa kwanza. Asije akarudi likatutokea la kutokea hapa." Akatamka kwa sauti ya kicheko akiwa analegeza vifungo vya shati lake jepesi.
"Duh ila J4 kweli we kiboko. Kweli wewe hujawahi kusomea upelelezi?" Sauti nyororo ya Bebe ikamjibu huku akiliondoa gari eneo hili.
"Mi nilikwambia! Silaha yetu ya kwanza ni woga wake. Kitendo cha yeye kuogopa tu, tayari tumeshamnyanganya kete."
"Duh! Mwenzio huku nje nilikuwa naogopa jamani. Tena lilivyodondoka sasa, puuh kidogo nikimbie. Alilirusha vibaya jamani. Ulishindwa kumwambia alirushe taratibu?"
Mkono mmoja wa Bebe unaachia usukani na kupepea kuigiza yale anayoyasema.
"Umezihesabu tayari? Zimetimia?"
J4 akabadili upepo wa mazungumzo.
"Zimefika ndio."
"Mia hamsini?"
"Eh kwani ilibidi ziwe ngapi?"
"Anaweza akawa amezidisha yule. Sio kwa jambajamba zile nilizoziona."
"Hahaha! Kwani akizidisha utamrudishia au?" Bebe akahoji akiwa amezama kwenye kicheko.
"Eee sasa kwa nini tumdhulumu mtu? Mimi ni Mwislamu swafi kabisa. Nilifundishwa madrasa kuwa Dhulma ni dhambi, sio hakhi!" Jumanne Maliki, ajulikanaye kwa jina la J4 akajitapa huku mikono yake akiinyanyua juujuu kuonyesha
kuwa hana makosa.
Kicheko kikamchukua Bebe kwa nguvu. Akacheka sana mpaka akauachia usukani. Akaurejea mara moja akingali katika kicheko hiki.
Isivyo bahati, macho ya J4 yakajikuta yakitumia mwanya huu kumkagua kwa haraka. Yakatua juu ya kifua cha Bebe kilichokuwa wazi kulingana na vazi alilokuwa amelivaa. Yakayaona maziwa yake yaliyojaa jinsi yalivyokuwa yakirukaruka kadri anavyocheka. Nayo yanamcheka!
Akatamani kujikaza lakini akashindwa kujizuia akayahamisha mpaka kwenye mapaja yake yaliyonona.
Yakagota hapo. Alishtuka mara baada ya Bebe kurekebisha mkao wake kwa kulivuta gauni lake vyema.
"Duh umeniacha hoi. Kwahiyo madrasa ndio wakakufundisha namna ya kuwa MUTU MWEUSI au sio?" Anauliza swali akiwa bado anaelea kwenye kicheko. J4 naye akajichekesha.
Kisha kwa kutumia pembe za macho yake akausaili mwili wa Bebe kwa mara nyingine tena.
Akaanza kuyaona yale ambayo wanaume wengine huyaona. Shetani wake akaanza kumvuta kwenye ulingo ambao hakutaka kuingia hapo mwanzo.
"Lakini huyu ni changudoa!" Akawaza.
"Ni mzuri, anavutia, amenona sana. Natamani kulala naye. Lakini ni changudoa!" Akajikosoa kwa mara nyingine tena.

"Vipi mbona hivyo?" Bebe akamkurupua kutoka kwenye mawazo yake.
"Haa..hamna kwani vipi?"
"Umekuwa kimya ghafla!"
"Nimependa tu hilo gauni ulilovaa. Ndio mnaitaje? Mini-skirt sio?"
"Hapana bwana...hii sio sketi." Bebe akajibu kwa kudeka.
"Aah ni sawa tu." J4 akawahi kubadilisha mada.
"Muda umeenda. Nilitaka nikuulize kesho tunaenda wapi au unachagua twende hoteli gani tukajipongeze?" J4 akamnong'oneza.
"Aaah we naye, saa sita kasoro hii unasema muda umeenda? Wenzio nd'o kwanza kumekucha!" Bebe akamjibu kwa kushtukiza.
"Mimi nimechelewa tayari. Hii ni mida ya watu kuingia ofisini huko kwenye vichochoro vya mtaani kwangu. Inabidi niwahi." J4 akaweka hoja yake mezani huku akiinamia saa yake ya mkononi.
"Utalala kwangu!!"
Katika namna ya kushtukiza. Bebe akatoa kauli ambayo ilimshtua J4.
"Yaani nikalale kwako?-"
"Eeh utalala kwangu. Vyumba vipo vya kutosha!" Bebe akajazilizia.
"Lakini vipi kuhusu yule mzee Did-"
"Bado anaugulia yule. Anaogopa kunifuata kuchukua mali za kampuni yake. We usiogope, twende tu ukapaone!"
Akamuondoa wasiwasi.
J4 akakosa namna ya kumpinga. Ni kweli kuwa mida hii saa sita kamili usiku, ulikuwa muda hatarishi sana kukatiza kwenye vichochoro vya mitaa aliyokuwa anaishi. Wezi na vibaka walikuwa kazini. Halikuwa jambo la ajabu kukutana na kibaka ambaye hajala tangu asubuhi, akukamue kila mali uliyonayo kisha uende zako. Ama sivyo njaa yake inayohimizwa na hasira za bange, inaweza kukuacha na kilema cha kudumu kisha ukapoteza mali zako. Chagua wewe tu, utoe mali bila ubishi ama upewe ulemavu na mali zako zichukuliwe.
J4 akakubali kupumzisha mwili wake nyumbani kwa Bebe usiku huu.
Pumziko ambalo liliambatana na furaha kando yao kila walipoliona briefcase lililosheheni noti nyekundu.
Matairi ya gari hili yakazunguka upesi mpaka wakafika nyumbani kwa Bebe.
Honi ikapigwa kwa nguvu lakini mngoja mlango hakuitikia wito huu kwa kufungua geti upesi kama siku zote.
Piiiiiiii! Piiiiiii! Wapi.
"Wamekuaje hawa? Au wamelala?!" Bebe akauliza kwa hamaki.
"Ooh ooh, kuna jambazi limefyeka tayari." J4 akafanya mzaha.
Wakiwa bado ndani ya gari mara akatokea kijana mrefu aliyevaa mavazi ya ulinzi. Huyu hakuonekana kuwa na pupa, akafungua geti na kutoka nje kuwalaki bila ya kufungua mlango mkubwa wa gaei kuingilia.
"We Ramso vipi ulikuwa wapi?" Bebe akaanza kugawa malalamiko yake ya siku zote.
Baada ya kunyeshewa mvua ya malalamiko na shutuma kutoka kwa Bebe.
Mara ghafla,
"Samahani Madam!"
"Nini? Kuna shida?" Bebe akauliza kwa dharau.
"Leo walikuja wageni hapa."
"Wageni? Wageni gani?"
"Uum ni viongozi wa kampuni. Walitaka kuzungumza na wewe. Kwa-kwa vile hukuwepo wakasema kesho asubuhi watarudi!" Akajitahidi kunyoosha maelezo yake.
Akili ya Bebe ikaanza kumkaa sawa.
Aliwafahamu wageni hawa na ni nini walitaka kukifanya.
"Sawa asante sana Ramso!" Akapiga hatua kuungana na J4 ambaye alikuwa ametulia tu akiyasikiliza maongezi yao.
Walipotaka tu kuingia ndani ya nyumba wakazuiliwa.
Mlinzi yule akasimama mbele yao kwa ukakamavu.
"Samahani madam wametuambia kuwa hauruhusiwi kuingia humu ndani bila kuonana nao."
"What??!" Bebe mkono uko kiunoni. Haamini kile anachokisikia.
J4 naye mkono wake mmoja uko mfukoni, mwingine umebeba briefcase, amechagua kuwa mtazamaji tu.
"Huruhusiwi kuingia ndani ya nyumba hii bila idhini kutoka kwao Madam. Hili ni agizo kutoka juu!" Mlinzi huyu amesimama kwa kujiamini, anachezea rungu lake kwenye viganja vya mikono yake. Shingo yake imebeba silaha ya moto.
Inahitajika rukhsa kutoka juu, ili Bebe na J4 waingie ndani ya uzio wa nyumba hii!

Itaendelea.....
 
KIBIRITINGOMA
YAKE: GODLOVE KABATI

SEHEMU YA KUMI NA NANE


Wapo watakaokushauri kuwa, kula raha, ponda mali-TUNAISHI MARA MOJA TU.
Lakini mimi nakuambia kuwa, tunaishi kila siku, lakini tutakufa mara moja tu.
Zitumie rasilimali zako kwa uadilifu. Hasa muda, ambao ni rasilimali adimu kuliko zote!
Kifo ni barua ambayo hatujui itatufikia lini.
Nakuandikia haya katika sehemu hii ya 18





"Amri kutoka juu?! Juu kwa nani?" Mkono wa Bebe uliokuwa umebeba mkoba, nao ukahamia kiunoni.
"Sina taarifa ya ziada madam...lakini nadhani ukimtafuta Boss Ambrozi au yule bwanaa-" hakumalizia sentensi yake.
"Didas ndio amewaambia mnizuie?" Bebe akamkatisha akilitaja jina la Bwana Didas kama walio kwenye rika moja, ama anamzidi kiumri.
"Walikuwa wengi Madam! Hata yeye alikuwepo. Walifanya ukaguzi halafu-"
"Kwa nini hukunipigia simu?" Bado Bebe anafoka.
"Hukupatikana hewani Madam!" Akamjibu kwa nidhamu.
Bebe akamgeukia J4, akamtazama kwa uchovu na kukata tamaa. J4 bado ametulia tuli, hana la kutamka.
"Jay, tunafanyeje sasa?"
"Mpigie huyo Didas uone anasema nini. Kwani si una mawasiliano yake?" Kwa mara ya kwanza J4 akatoa mawazo yake.
"No sina...nilishafuta namba zake mimi." Bebe akamjibu akijishughulisha na simu yake. Jibu lake likamshtua mlinzi yule, aliyekuwa bado anaamini kuwa kuna uhusiano wa karibu sana kati ya Bebe na Bwana Didas Ambrozi.

"Basi twende tukapumzike hotelini halafu kesho mapema, mguu wako wa kwanza uwe hapa." J4 akatoa wazo.
Bebe akashusha pumzi kwa nguvu kisha katika namna ya kususa, akapiga hatua zake kuelekea kwenye gari lake.
J4 akamfuata nyuma kwa utulivu.
"Na hili nalo watalichukua kesho." Bebe akatangaza hisia zake kwa masononeko huku akiliwasha gari hili na kuelekea popote pale watakapopata hifadhi.
"Ooh kumbe na haka kaIST ni kao eh?" J4 akauliza kwa mzaha. Analidharau gari la Bebe na kusahau kuwa yeye hajawahi kuwa na umiliki wa walau baiskeli ya miti. Maskini jeuri!
"Supastaa kama wewe sio wa kuendesha magari madogo kama haya. Hili halikufai hata kidogo hili. Inabidi uwe angalau na Range kama mbili mpaka sasa." Akaweka pumziko kuyaacha maneno yake yazame, kisha akaendelea.
"Hata nyumba. Inabidi uwe na bonge moja la apartment. Wewe sio wa kuishi kwenye nyumba za kampuni kama yao." Akatua.
"Jamani Jay inatosha basi, niache nipumue mwenzio. Kwani hayo yote nikiamua hata kesho asubuhi, naweza kuwa nayo. Ni uvivu wangu tu, nimebweteka mpaka muda huu nafukuzwa." Bebe akasonya huku analiendesha gari.
Maneno yake yakamkumbusha J4 kuwa, yeye na Bebe hawako daraja moja. Bebe ana mitego yake kadhaa ya fedha inazomuingizia kipato kila anaposimama nyuma ya kamera na kutabasamu. Halafu yeye J4, ni masikini tu ambaye ana dira ya kuokota utajiri katika namna hii ya utapeli aliyoichagua, utapeli wa kisasa.
Akameza funda jepesi la mate, na kukaa kwa utulivu.
Waliifikia hoteli moja kubwa, ambayo kwa hakika, ingekuwa na vyumba vilivyokuwa wazi ndani yake. Sio kwa vile haikuwa na mvuto kwa wateja, bali ni aina ya wateja ambao hulipia ili kupumzika mule. Hili likajenga ukuta mkubwa wa mawe uliowatenganisha wenye nazo na wale wasiokuwa nazo.
Muda huu Bebe na J4, walikuwa kwenye kundi la wale walionazo.
Wakalipia na kupata vyumba viwili tofauti. Kabla ya yote wakajistarehesha kwa vinywaji laini na katika namna ambayo haikutegemewa, chumba kimoja kilicholipiwa hakikutumika!
Usiku huu tulivu ukaendelea kwa viumbe hawa wawili wanaodai kuwa kwenye mahusiano ya kibiashara, wakiwa kwenye mahusiano mapya yaliyodumu kwa muda mfupi kabla usingizi mzito uliokaribishwa na ulevi haujawachukua.
Mahusiano haya ya muda mfupi, siwezi kuyasimulia. Sikuwa shuhuda wake. Ni kile chumba kilichowameza, kilichoamua kubaki kimya kuitunza siri ya kile kinachoendelea mule ndani.
Elewa neno, siri!


*******

Macho yake yalikuwa mazito sana kufumbuka. Akajitahidi kuyaweka wazi lakini mwangaza mkali wa taa, ukayaumiza macho yake. Kwa kutumia kiganja cha mkono wake wa kulia, akajitahidi kuyafikicha. Akajigeuza ubavu wa kushoto.
Mara mkono wake wa kushoto ukagota baada ya kutambua kuwa kuna unyevunyevu usio wa kawaida kando ya kiuno chake. Akapapasa kwa uangalifu kisha mkono wake ukasafiri mpaka puani, akaikunja sura yake kwa kinyaa baada ya kunusa harufu ya ajabu.
Ni harufu ambayo ni kama aliitambua. "Nimelala na msichana!" Jawabu likamjia kwa herufi kubwa.
Ni msichana gani aliyekuwa naye hivi karibuni zaidi ya Bebe?
Akagutuka na kuketi kitandani, akakikagua chumba hiki huku na huko, hakukuwa na kiumbe hai chochote zaidi yake. J4 akashtuka!
"Ina maana jana sikulala chumbani kwangu au? Kwa hio nimelala na Bebe halafu- Aaargh!" Akajikuna kichwani bila kuwashwa. Akagundua kuwa alilala na Bebe kwenye kitanda kimoja usiku uliopita. Na sio kulala tu, bali alilala akiwa uchi wa mnyama. Hisia zake zikamuarifu kuwa hata Bebe alilala hivyohivyo akiwa mtupu. Na kama dhahania yake ilikuwa kweli, basi ni lazima lipo jambo lililotendeka kati yao.
"Kwani Bebe mwenyewe yuko wapi?" Hakuwa na majibu.
Akakurupuka na kusimama, akitumia shuka kuzisitiri nyeti zake.
Akaangaza huku na huko kuyatafuta mavazi yake akiwa na mang'amung'amu ya usingizi.
"Baby! We Baby! Bebeee." Akajaribu kumuita bila mafanikio.
"Kaenda wapi huyu?! Au anaoga bafuni."
Akavikagua bafu na choo, Bebe hayupo. Akaitazama saa yake, ni saa kumi na mbili na dakika thelathini na saba asubuhi.
Ni kawaida kwa jua la jiji hili la DaresSalaam, kuangaza mapema sana muda huu.
"Au kafuata chai nini?" Akajiuliza J4. Akarejea juu ya kitanda na kuketi. Akapiga mwayo mrefu na kunyoosha mgongo wake. Harufu ya pombe ilikuwa bado imemng'ang'ania kinywani mwake. Hakuzoea kulewa, lakini jana alilewa sana usiku ule wa manane akiwa na Bebe.

Milioni mia hamsini!
Mbiu ikalia kwenye ubongo wake. Labda Bebe amekimbia na utajiri ule waliouchuma jana! Akili ikamkaa sawa, masalia yote ya ulevi yakakimbia.
Mawazo mbalimbali yakapita kwa kasi akilini mwake.
Akasimama wima na kuangaza chumbani mule, alipotupa macho yake kwenye meza ya kioo iliokuwa ndani mule akakutana na kipande cha karatasi kilichoonekana kiwa na ujumbe.
Akakiendea na kukiokota. Kiliandikwa hivi;

Goodmorning Jay,
Najua unashangaa, hata mimi nashangaa hivyohivyo kama wewe.
Naandika ujumbe huu, nikiwa mwingi wa aibu. Hivi ilikuwaje mpaka tukajisahau?
Achana na hayo,
Nimewahi nyumbani kwangu, kufanya makabidhiano kama walivyodai maafisa wa kampuni ya Chief.
Na baada ya hapo kuna wito nimepata mahali fulani. So, usishangae ni kwa nini nimeondoka haraka bila kukuaga.
Ukifungua kabati hilo kubwa upande wa kushoto kwa chini, utalikuta briefcase lenye sehemu ya mgawo wako kama tulivyogawana jana.
Nimeshalipia kila kitu hapo hotelini. Hawatudai kitu.
Kama kuna jipya, ukipata nafasi utanitafuta.
FROLIDA.


J4 akatabasamu akiikunja barua hii fupi baada ya kuisoma.
"Kumbe hii Frola ni kifupisho eh? Aaitwa Frolida!" Akatamka kwa sauti ya chini akipiga hatua kuelekea ilipo kabati.
"Halafu huu mwandiko wake sasa. Lo! Au alikuwa na ndoto za kuwa daktari siku moja? Yaani haumfanani kabisa. Mwandiko mbaya sana aisee. Anaandika kama anakoroga." Akajichekesha kidogo baada ya kuliona briefcase lile kama alivyoelekezwa.
Akalifungua na kuhakiki kiasi kilichokuwemo kwa kuhesabu mabunda kadhaa ya fedha.
Baada ya yote akaingia bafuni na kuuweka sawa mwili wake kwa kuoga. Akajivesha mavazi yake na kujiandaa tayari kwa kuondoka mahali hapa akiwa na tahadhari kubwa akilini mwake.

"Nimeanza kulegea!" Kauli hii ikakatiza akilini mwake.
"Yaani nimefikia hatua ya kufanya mapenzi na huyu kahaba?!" Akiwa kwenye ngazi akasimama ghafla na kurejea nyuma alikotoka. Akakitazama chumba kile alichokuwa amepangiwa yeye kilichokuwa mkabala na kile cha Bebe.
Akakipuuza na kuingia kwenye hiki cha Bebe. Akakikagua tena kwa makini. Akapekua huku na huko kuhakikisha kuwa hakuna mtego wowote uliokuwa humo.
Mganga anaogopa kujiloga kwa sanaa yake yeye mwenyewe!
Hakukuwa na lolote. Aliporidhika, akaondoka na kutoka nje.

"Penzi ni kitovu cha uzembe!" Akajikanya.
"Najiona kabisaaa, naanza kupoteza umakini."
Akalikumbuka umbo la kuvutia aliloliona jana usiku kwenye gari. Akaikumbuka sura yake nzuri na sauti yake ya kubembeleza.
Akatikisa kichwa chake katika namna ya kuyafukuza mawazo haya.
"Ajali kazini bwana! Na mimi ni mwanaume. Hili halitatokea tena!" Akatamka peke yake kwa sauti.
Kisha huyooo akavuka barabara na kujichanganya na watu waliokuwa kwenye hekaheka na mahangaiko ya kila siku. Briefcase limekamatwa imara kwenye mkono wake.
Sindano ya dawa ya Bebe, imeanza kumuingia. Ni kama lilikuwa suala la muda tu, dawa ianze kufanya kazi.


********


Kama wewe ni mgeni kwenye matumizi ya mitandao, unaweza kushangazwa na jambo kuwa huku mtandaoni, kuna habari zinazokuja kwa kishindo kikubwa. Kisha baada ya hapo, zinayeyuka ghafla kana kwamba hazikuwahi kutokea kabisa.
Ndio!
Kwa wewe mgeni ni haki yako kushangaa. Lakini utashtuka baada ya kugundua kuwa, wazoefu wa mitandao wanakushangaa zaidi wewe usiyeifahamu kasumba hii.

Ni siku sita tu pekee, zilizotosha kumsahau Kenzy Flavour na picha zake za uongo na kweli. Hata waliokuwa wakizidai picha na video hizo zilizotajwa kwa uchu mkubwa, wakaridhika baada ya kuzikosa na kubaki na lawama mashavuni mwao.
Jina la MUTU MWEUSI likawekwa kwenye kundi la wale watumiaji wapya wa mitandao, ambao wanachapisha na kuandika lolote lile wanalojisikia bila kujua ni nini kinachozungumzwa huko kwenye mijadala.
"Mbona sasa alipotea ghafla?! Itakuwa aliogopa baada ya kutafutwa sana."
"Aah we, sasa ile picha aliitoa wapi?"
"Bro, siku hizi makanjanja ni wengi hapa hapa town mzee. AI inatengeneza hizo."
"Akaunti yenyewe hata followers mia tano haina. Unaamini akaunti kama hiyo ili iweje kwanza."
MUTU MWEUSI akakataliwa.
Hii ikawa kama kuponea chupuchupu kwa Kenzy flavour. Skendo yake ikatupwa kwenye jalala lilelile la sahau. Maisha yakaendelea.
Na sasa iliibuka habari kubwa zaidi, iliyotikisa mitandaoni na vyombo mbalimbali vya habari. Kuwa kuelekea kipindi cha uchaguzi mkuu mwaka huo, waziri mkuu wa nchi ametoa nia ya kugombea uraisi wa nchi.
Macho na masikio ya watanzania wote, vilikuwa makini kufuatilia vyombo vya habari na mitandao, kufahamu lolote linalojiri na sababu kuu ya waziri huyu, mheshimiwa Brown Kashinde Masanja kugombea nafasi hii kubwa.

Waziri huyu alijulikana sana kwa haiba yake nzuri na ujasiri aliokuwa nao kutimiza shughuli zake za kiuongozi.
Uchapakazi wake na uadilifu kazini, ndivyo vilivyompandisha daraja kutoka kwenye uwaziri mpaka kuwa waziri mkuu.
Umahiri wake katika kujenga hoja na kuitetea katika vikao mbalimbali bungeni, vikampatia jina la utani katika vinywa vya watanzania.
Wakamuita JEMBE!
Tangu zamani, watu wenye macho ya kiroho waliwahi kumtabiria kuwa atakuja kukikalia kiti cha uraisi kama akiendelea kuwa na moto huu.
Moto wake haukuzimika asilani, na sasa alitengaza nia ya kukigombea kiti hicho akiwa tayari kuiongoza nchi hii nzuri yenye neema.

"Mpaka naingia kaburini, nitaendelea kukataa katakata kuwa nchi yangu pendwa ya Tanzania ni nchi masikini.
Tunao utajiri hapahapa kwenye ardhi yetu. Mazao ya kutosha kwenye udongo wetu wenye rutuba! Hatuna njaa sisi! Itazame miamba yetu, inaelemewa kwa wingi wa madini kama dhahabu, almasi na na Tanzanite. madini yote haya tunayakalia tu! Tuna mlima Kilimanjaro, kilele cha Afrika! Wanyama mwitu kwenye mbuga zetu! Tunayo maziwa makubwa matatu yenye samaki watamu! Tumebarikiwa bahari! Kwa nini tusipate maendeleo?!"
Brown Masanja alisikika akihubiri maneno haya mbele ya vinasa sauti vya vyombo mbalimbali vya habari.
Kamera nyingi zinammulika, picha nyingi zikipigwa.
"Nimeshuhudia unyanyasaji mkubwa kwa raia wa nchi yangu. Sio kushuhudia tu, mimi mwenyewe nimeyaishi maisha hayo. Uonevu na ubadhilifu unaofanywa na viongozi kwa raia wao! Ni mambo yanayoumiza sana na kuwafanya watanzania waichukie nchi yao wenyewe.
Na sasa natangaza rasmi nia ya kugombea uraisi kwa mwaka huu wa uchaguzi. Nataka nipanyooshe pale palipopotoka na kusawazisha pale palipovimbishwa kwa ufisadi!"
Mheshimiwa akajinadi.
Waliomfurahia wakapiga makofi kila alipotulia kwa makusudi. Kitendo cha waziri mkuu kutaka kugombea uraisi, kikawasha moto upya mitandaoni na kwenye vyombo vya habari.
Mitandao ikawa ya moto kwa mara nyingine!
Chama chake cha kisiasa kikampitisha baada ya kura za maoni. Na harakati za kampeni zilipowadia akajiweka tayari kwa ajili ya zoezi hilo.
Wasanii mbalimbali wakatafutwa ili kutumbuiza kwenye ziara mbalimbali za kampeni zake katika majimbo yote nchi nzima, kama katiba inavyoelekeza.
Ile kanuni ya usawa kwa vyombo vya habari, katika kutangaza sera za wagombea wa vyama vyote bila ubaguzi ikazingatiwa.
Ni hapa alipotumia mgongo wa chama chake kilichokuwa kimojawapo miongoni mwa vyama vikubwa vyenye ushawishi nchini, kuandaa matangazo yenye ubora katika vipindi mbalimbali kwenye vyombo vya habari.
Ndipo jina moja miongoni mwa majina mengi, likapendekezwa kutumika katika matangazo haya.
Frola!
Hata mheshimiwa alipolisikia, hakutaka majadiliano yawe marefu sana,
"Mna-mnasubiri nini sasa? Mpigieni simu upesi...fedha ipo, atalipwa!" Akawaharakisha.
Simu moja tu ikapigwa. Makubaliano yakafanyika, mikataba ikasainiwa. Bebe akaingia kazini. Safari hii akakubali kuivaa bendera yenye rangi na nembo ya chama na kusimama nyuma ya kamera, kuziomba kura za ndio kwa Mheshimiwa Brown Masanja!
Bebe katika mchezo wa kisiasa!


Itaendelea....
 
CamScanner 09-06-2026 00.55_1.jpg
SEHEMU YA KUMI NA TISA

Sikia,
Utajiri wa kwanza unaotakiwa kuutafuta kwa nguvu zako zote, sio pesa, majumba, mashamba wala migodi ya madini.
Ni watu!!
Tena watu walio sahihi!
Mtu mwenye nguvu kubwa sana ya watu wanaomuunga mkono, ana nguvu ya kufanya lolote hapa duniani!
Tafsiri kadri ya uelewa wako.

Na hii ni sehemu ya 19





CHAGUA BROWN MASANJA!
JEMBE LILIMALO BILA KUCHOKA!

Hizi zilikuwa ni herufi kubwa zilizokozwa kwa rangi ili tu zionekane waziwazi kwa kila jicho la wale wanaojua kusoma.
Hata wale wasiojua kusoma hawakuachwa nyuma, picha kubwa ya mgombea huyu wa urais ilionekana kwenye mabango barabarani, kwenye kuta za nyumba na nguzo za umeme.
Ili mradi tangazo lake linalomnadi linaweza kubandikwa...basi litabandikwa popote pale panapostahili.
Wanawake wakazivaa kanga zilizochapishwa sura yake inayotabasamu sambamba na maneno adhimu yanayomsifia.
Kampeni zake zikawa vuguvugu la kisiasa lililotikisa kila jimbo alilokanyaga, aliwakusanya mamia kwa maelfu ya watu. Akazimwaga sera zake zilizobeba ahadi nyingi za maendeleo atakayoyaleta nchini. Watu wakampa masikio yao, wakamshangilia kila walipohitajika kufanya hivyo.
Bendera za chama chake na zile zilizopambwa kwa picha yake zikapepea hewani.
Kila alipoziona naye akazidi kuongeza munkari wa kunguruma mbele ya kinasasauti.
Akawa ni kama mhubiri anayeihubiri habari njema ya wokovu kwa watu wote waliokata tamaa ya maisha yao.
Akaikunja ngumi ya mkono wake wa kushoto na kujipiga kifua chake kwa simanzi.

"Nataka niongee na nyinyi watanzania wenzangu. Nataka niongee na nyinyi wakazi wa jimbo hili la Mwanza!
Najua mtataka kufahamu ni kwa nini ninajiamini sana juu ya kile ninachokiahidi.
Na mnajiuliza kuwa ati, nitapata wapi hizo fedha za kuendesha na kutimiliza miradi yote hii hapa nchini, ikiwemo kuziondoa adha na shida mnazozipitia nyinyi ndugu zangu.
Najua kuwa mna wasiwasi sana na utajiri wa nchi yetu sio?
Sasa nisikilizeni!
Mimi Masanja Kashinde nimehudumu kwenye serikali yetu tukufu kwa takribani muda wa miaka kumi mpaka sasa.
Nimezishika nyadhifa mbalimbali kama waziri wa wizara tatu tofautitofauti mpaka nilipoaminiwa na kuchaguliwa na baraza la bunge letu tukufu la jamhuri ya muungano kiwa waziri mkuu.
Kwa maana hiyo nimeona mengi na ninajua kuwa kuna ubadhilifu unaotendeka hasa kwenye suala zima la usimamizi wa ruzuku na mgawo wa fedha huku kwenye idara za chini kabisa!
Yapo machujio yasiyohitajika!" Akaweka kituo huku akikitumia kitambaa chake kujifuta jasho.
Ukimya wake ukapokelewa kwa shangwe, nderemo na vifijo kutoka kwa kadamnasi iliyokuwa inamsikiliza.
"Huku chini kuna madudu mengi ambayo yamefumbiwa macho kwa muda mrefu." Akaendelea.
"Haya ni magugu yanayotuzuia tusifaidi matunda ya jasho letu. Na ndio maana mkaniamini, mkanipa hii nafasi ya kukiwania kiti hiki, mimi kama jembe kwa ajili ya kazi moja tu, kuyalima na kuyang'oa haya magugu!" Akajazilizia.
Makofi na vigelegele vikafuata! Baadhi ya wanachi waliopendezwa na maneno yake, wakainama na kurusha vumbi hewani. Wengine wakayavua mashati na kofia zao na kuzipeperusha juu.
Hivi vyote mheshimiwa Brown, aliviona kwenye kila jimbo alilofanya ziara yake kwa ajili ya kampeni. Na hivi vilivyoiwasha cheche ya matumaini ya ushindi kwenye moyo wake.
Akatabasamu!


Anayafumba macho yake, mbele yake analiona jengo kubwa la Ikulu likimeremeta. Tazama rangi yake inavyovutia!
Rangi nyeupe kama theluji!
Mara mlango wa Ikulu unafunguka. Anakiona kiti kikubwa cha Raisi kwa mbali. Kiti hiki kinapaza sauti na kumuita kwa majina yake yote matatu.
Anashangaa!
Akigeuka nyuma anawaona wananchi wa Tanzania wakilipuka kwa shangwe kuliimba jina lake,
"Masanja jembe! Masanja jembe!"
Anazipiga hatua zake kuukaribia mlango wa Ikulu ili akifikie kiti hiki moja kwa moja ili akikalie. Uso wake umefunikwa kwa tabasamu lenye bashasha.
"Asante Mungu! Asante! Nimeshinda uraisi! Nimeshindaaa! Naingia Iku-" Mara ghafla tabasamu lake linayeyuka.

Anakiona kiwiliwili cha mtu mbele yake ambaye amevaa gubigubi kuuficha wajihi wake. Kiwiliwili hiki kinamzuia kusogeza walau hatua moja zaidi mbele. Mara kinampiga kikumbo kwa nguvu na kumtupa pembeni.
Akiwa anajitahidi kujizoa pale sakafuni, anagundua kuwa kiwiliwili hiki cha ajabu kinazidi kumshindilia pale pale chini kwa mateke.
"We-wewe ni nani aisee?" Anauliza huku akijitahidi kuing'amua sura ya mtu huyu.
Mtu huyu anaacha kumpiga na anasogea kando. Anavua kitambaa kilichokuwa kinaufunika uso wake.
"Huwezi kukichukua kiti cha kwa urahisi namna hii mzee Masanja. Inuka tupigane, atakayeshinda ndiye atakikalia kiti hiki! Simama Masanja! Simama ukitetee chama chako!" Sauti nzito ya kiume inatamka. Ni kama mheshimiwa Masanja aliwai kuisikia mahali lakini kumbukumbu zake wakati huu zinampiga chenga.
Mwanaume huyu wa ajabu anampa mkono na kumuinua kutoka pale chini.
Masanja anasimama kwa taabu akitegemea mhimili kutoka kwa mwanaume huyu.
Mara Masanja anamtazama usoni. Lahaula!
"Mheshimiwa Zakaria?!" Anagutuka kwa mshangao. Huyu ni waziri wa wizara ya utamaduni, sanaa na michezo.
Amezoeleka kuwa mtu wa watu, mcheshi na mchangamfu sana hasa katika mijadala mbalimbali ya kijamii na hata kwenye vikao vya bunge. Huenda hizi ni baadhi ya sifa zake, zilizomsogeza kwenye wizara hii. Na sasa huyu hapa amesimama mbele yake anataka wakipiganie kiti cha uraisi. Ametokea wapi? Kwa nini anataka kupigana naye? Je, na yeye anakitaka kiti? Haya yote aliyajua yeye mwenyewe.

"Muda unaenda mheshimiwa. Silaha yako hiyo hapo chini! Pigana nami, mheshimiwa waziri mkuu!" Zakaria akanguruma.
Bado Masanja haelewi ni kitu gani kinaendelea, anageuka pembeni kuitazama silaha aliyoambiwa. Ni jembe!
Jembe lisilo la mpini!
Akiwa bado analistaajabia jembe hili lililotajwa kama silaha. Mara anapigwa na kitu kizito kwenye kifua chake.
Anayumba na kuanguka chini.
Umati wa watu unazidi kumshangilia na kumuhimiza asimame.
Bado haelewi, anajitahidi kusimama tena. Anasimama huku miguu yake inatetemeka, inamnyima ushirikiano.
Anapigwa na kitu kingine chenye uzito kuliko kile cha mara ya kwanza, safari hii kinatua tumboni mwake.
Tumbo linaungana na kifua chake, kuyasikilizia maumivu.
"Anatumia shoka!" Anaing'amua silaha anayoitumia mpinzani wake.
"Shoka lake lina mpini!" Anazidi kustaajabu.
Anaangaza huku na huko kuutafuta mpini wake, anauona. Anatambaa kuuendea lakini anapigwa tena kichwani! Maumivu ya safari hii ni makali zaidi kuliko ya mwanzoni.
Anagaragara, anajinyonganyonga.
"Vipi mheshimiwa, umeshindwa kabisa kujitetea ili nikumalize kabisa? Sema tu. Sitaki ushindi wangu uwe na makandokando. Nd'o sababu tumecheza mchezo wa wazi mbele ya watanzania. Watazame hata sasa wanatushuhudia!"
Masanja anajitahidi kugeuka kwa uchungu,
Kweli anawaona watu mamia kwa maelfu, wakizidisha shangwe. Lakini anagundua jambo moja la ajabu.
Hapo mwanzo walilitaja jina lake kwa bashasha. Lakini sauti zilizobeba jina lake, zinaanza kufifia na jina jipya linaanza kutajwa vinywani mwao.
"Zakaria shoka! Zakaria shoka!".
Rangi za bendera ya chama chake, chama tawala zinaanza kufifia na kushuka chini taratibu. Zile zilizochapishwa kwa sura yake, zinachanwa na kuraruriwa ovyoovyo.
Zinapanda bendera za chama kingine na sura mpya ya Mheshimiwa Zakaria, inaanza kuelea hewani. Sura inayotabasamu kwa ushindi.
"Nikumalize kabisa au nikuache?" Ni Zakaria anauliza, huku akilifuta shoka lake linalomweka kwa nuru inayoyaumiza macho yake. Liko tayari kuchinja.
Anainama na kukoroma kama mnyama aliyeelekea kibla tayari kwa kung'olewa shingo yake.
"Nasubiri jibu mzee..." Sauti ya Zakaria imebadilika na kubeba ukatili.
Zaidi ya yote, ati amemuita mzee! Sio tena mheshimiwa kama hapo mwanzo.
Sauti mpya kutoka kwenye kiti cha Urais inataja majina matatu mapya, Kamugisha Zakaria Stefano!
"Sina muda wa kupoteza!" Zakaria analinyanyua shoka lake juu kwa nguvu. Shoka linalisalimia anga, liking'aa maradufu. Sauti za watanzania zinazidi kuhanikiza kulichochea tukio hili. Mara shoka linashuka chini tayari kuipasua shingo ya Masanja. Hilo, hilo, hilo!
Paaaaa!


"Mamaaaa!!" Mheshimiwa anashtuka kwa nguvu na kujirusha juu.
Ni kama mtu aliyepagawa na mapepo.
"Daddy! Una nini tena?" Sauti tamu iliyojaa usingizi kutoka kwa mrembo aliyekuwa kifuani mwake usiku wote huu kabla ya kusukumwa kando baada ya mshtuko huu, inamuita.
Masanja anaangalia kulia na kushoto. Mara anasimama huku anahema kwa nguvu. Jasho linamtiririka kwa nguvu, kutokea kichwani mpaka kifuani. Anakikagua kitanda kile uvunguni. Anaelekea dirishani na kulipiga pazia kuchungulia nje gizani.
"Daddy?!" Binti yule aliyemuacha kitandani, anamuita katika namna ya kutomuelewa lakini sauti yake ni ileile ya nzuri, ya upole iliyojaa huruma. Amekificha kifua chake kwa kushikilia shuka jeupe.
Mheshimiwa Masanja anageuka na kumtazama. Anauegemea ukuta na kujiburuza kwa mgongo wake mpaka kwenye kigae cha sakafu ambapo anaketi mkono wake ukiwa kifuani.
"Frola! Tafadhali niambie kuwa nilikuwa naota!" Anashusha pumzi na kuhitaji udhibitisho kutoka kwa mrembo huyu aliyemuita kwa jina la Frola. Lakini mimi na wewe tunalifahamu jina lake la ziada. Bebe!

Frola, akatabasamu. Akaliachia shuka lile na kupiga hatua taratibu kutoka kwenye godoro lile laini na kumfuata mheshimiwa waziri mkuu, Brown Masanja pale sakafuni alipokuwa.
Hapo mwanzo, niliwaambia kuwa alijisitiri kwa shuka, na sasa halipo tena ameliacha kitandani. Mnaweza kukisia alikuwa kwenye hali gani, anapozihesabu hatua zake kumfuata huyu aliye sakafuni.
Ni mateso mpenzi msomaji.
Ni mateso!

Akamkaribia akiwa na kipande cha leso, akalipangusa jasho lile kwa ustaarabu na kimahaba. Huku mdomo wake ukiendelea kutamka maneno,
"Pole mpenzi wangu, pole!"
Katika namna ambayo hakuitarajia, moyo wa mheshimiwa ukapunguza kasi ya mapigo yake. Mapafu yakatii na kupunguza kasi yake ya upumuaji.
Bebe alipomaliza shughuli hii ya kulikausha jasho kwenye mwili wa waziri mkuu. Akaiviringisha mikono yake na kumkumbatia Mzee Masanja.
Masanja akakituliza kichwa chake kwenye kifua cha Bebe. Kifua kilichojazwa na muumba, kikajaa!

"Pole my wangu, sawa eh? Ni ndoto tu. Haina ukweli wowote ule!" Bebe akamlainisha.
"Asante baby, lakini ni ndoto mbaya sana hii. Una uhakika hakuna aliyeingia humu ndani kweli? Au bado nina-" Masanja akakatishwa kwa kidole cha Bebe kilichotulizwa kwa utulivu kwenye midomo yake.
"Shhhhhh! Tulia daddy. Humu ndani uko na mimi tu. Hakuna mwingine atakayeingia. Halafu hapo nje si kuna mabodyguard wako? Au umesahau kipenzi changu?" Bebe akaendelea kutema sumu zake.
"Ooh kidogo nisahau bwana! Duh, ama kweli nilikuwa naota! Lakini ilikuwa ndoto mbaya sana." Masanja akajiweka sawa.
"Mmh kweli?" Bee akamtuliza akimpapasa.
"Ni kuhusu mpinzani wangu, bwana Zakaria! Nimemuota yeye." Akatamka huku akimeza funda la mate kwa woga akilitaja jina la Zakaria.
"Achana na ndoto mbaya bwana! Haya bado tuna muda wa kutosha kuenjoy. Twende tukaote ndoto zetu nzuri!!"
Masanja akalainka kwa sumu ya Bebe.

Macho yake kayalegeza,
Makubwa meupe yanapendeza,
Tabasamu tamu kalikoleza,
Ngozi yake nyororo inateleza,
Umbo lake ni ngumu sana kulieleza,
Hata kwa tungo za kiingereza,
Mheshimiwa mheshimiwa mheshimiwa!
Huyu mtoto wa watu, utamuweza?!

Hili nd'o swali pekee ambalo ningemuuliza waziri mkuu, mheshimiwa Brown Masanja.
Katika kampeni zake, kuziomba kura za wananchi ili akikalie kiti cha uraisi, anajikuta amenasa kwenye mitego wa Bebe. Kahaba mzoefu, anayejifivha kwenye kivuli cha umaarufu wake wa utangazaji.
Haoooo, wakarejea kitandani,
Juu ya godoro laini,
Usingizi umetupwa kapuni,
Bebe akapewa upya usukani,
Yuko juu, mheshimiwa yuko chini,
Mambo haya si ya hadharani,
Hayawekwi wazi hufanywa sirini.

Zilikuwa dakika takribani thelathini za kuchoshana kwa mara nyingine, mpaka pale mheshimiwa alipokiri kuwa ameisahau ndoto yake.
Kila mmoja akajilegeza kivyake na kuukumbatia usingizi uliokuwa umesahaulika.
Yumkini, mheshimiwa alijiridhisha kuwa ni macho yao manne pekee yaliyokuwa pale chumbani.
Lakini kwenye kona ambazo hazijulikani, yalikuwepo macho mengine yanayoshuhudia kila kinachoendelea chumbani humu. Ni macho haya yaliyobeba taarifa ambayo ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa na mtu aliye nyuma ya kioo cha kompyuta yake mahala fulani.
Halali, usingizi aupate wapi wakati anahitaji pesa?
Na pesa aliyoiona ikimjia kwa wakati huu, aliikadiria kuwa nyingi zaidi. Nyingi kuliko hata kiasi alichokidai kwenye mitego yake mingine.
Giza likaendelea kulifunika anga la jiji hili la Mwanza.
Mwanza usiku!



Itaendelea....
 
Back
Top Bottom