RIWAYA: KITISHO
MTUNZI: richard MWAMBE
“Haya nataka password ya hii kompyuta!” ile sauti ya kihindi ikaendelea. Alipoichukua ile kompyuta kutoka kwa kijana mmoja ndipo Chiba alipoiona kwa uvunguni na kugundua kuwa kompyuta ile si yenyewe, akamtazama Madam S, akajikohoza mara tatu kwa mtindo wa pekee, Madam akaelewa kuwa ule ni wito akamtazama Chiba, Chiba akayazungusha macho yake kwa namna ya ajabu huku akibana na kuachia kope zake, Madam S akaelewa anachoambiwa kuwa kompyuta ile ni feki.
Akawatajia password ya hiyo kompyuta, wale jamaa wakaanza kuifungua, ilipoanza kufunguka wakafurahi sana na kuondoka zao.
“Tunarudi muda si mrefu kuwaua!” mmoja wao akasema.
Wakaondoka zao.
SEHEMU YA 06
KITUO CHA POLISI KATI –saa 11 alfajiri.
KIPIGO alichokipata Ravi Kumar kutoka katika mikono ya vijana wataalam wa kazi hiyo alitapika kila alichokijua juu ya sakata hilo, ingawaje alionekana vingi hafahamu lakini alimtaja mshirika wake mkubwa aliyekuwa akimpa maagizo ya kupeleka Gerezani au kuchukua na kuleta kwake, huyu hakuwa mwingine ni Pancho Panchilio.
“Kwa hiyo Pancho ndiye alikuwa anakutuma?” kamanda akauliza.
“Ndiyo kabisa yaani, ni jeje huyo, lakini mimi sijui nini alikuwa anaadika,” akajieleza.
“Pancho anaishi wapi?” akauliza Kamanda.
“Mimi mtaniua, sijui naishi wapi najua ofisi yake tu,” Ravi akajibu huku akilia na damu zikimtoka kinywani na puani.
“Na huyu Mke wa Mahmoud umemjuaje?” kamanda akauliza.
“Huyu manamuke bana, nilikutanishwa na jeje tu,” akaeleza.
“Sasa yuko wapi?” swali linguine.
“Aliniaga anaenda Zanzibar na atarudi jumamosi hii,” akajibu.
“Zanziba sehemu gani?”
“Mimi hapana jua jamani, mambo ya familia hayo!” akaanza kulia.
Kamanda Amata akaanza kupekuwa simu moja baada ya nyingine za wale wafanyakazi, ndipo katika simu ya msichana wa kazi alipokuta ujumbe mfupi wenye maagizo Fulani kuwa mtu yeyote akiuliza aseme mama huyo kaenda Zanzibar lakini alipochunguza haraka kwa makampuni ya simu aliambiwa namba hiyo mara ya mwisho ilikuwa ikisoma eneo la Laskazoni Tanga.
Kamanda Amata akaagiza kwa Inspekta Simbeye kuwa huyo mama akamatwe mara moja, simu ikapigwa Tanga, kituo kikuucha polisi, masako wa panya wa kimya kimya ukaanza.
“Kamanda Amata,” Simbeye akaita, kisha akampa ishara ya mkono kumwita pembeni.
“Vijana wangu wawili wameuawa eneo la Klabu ya Mbowe! Masaa matatu yaliyopita,” akamnong’oneza.
“Pole sana Inspekta, walikuwa kazini, wamekufa kishujaa, na muuaji atapatikana tu!” kamanda Amata akajibu na kutoka kituoni hapo.
4
JOKI alitulia mezani kupokea taarifa zote za vikosi kazi walivyovituma kuwasaka watu hao, vikosi vinavyoongozwa na wapiganaji hodari kuanzia makabiliano ya ana kwa ana na hata yale ya silaha za kila aina. Alishangaa tu kuwa muda unakwenda lakini hapati jibu lolote juu ya kupatikana au kuonekana kwa Kamanda Amata ambaye nguvu zote walikuwa wameelekeza kwake, isitoshe ilikwisha amuriwa kuwa akipatikana wala haina haja kumleta na uhai wake bali ni kumuua kwa vyovyote vile.
Aliitazama saa yake, pambazuko lilikuwa kwenye miimo ya mlango ulio mbele yake. Wamepatwa nini hawa? Mbona muda umetutupa mkono! Alijisemea kwa sauti ndogo iliyotosha kujisikia yeye mwenyewe. Kichwa kilikuwa kikimzunguka kila mara alitamanai kuinua simu awapigie kuliza lakini alikumbuka kuwa makubaliano yao hayakuwa hivyo bai wao wakikamilisha kazi watampigia simu kama walivyofanya kwa wengine wote.
Akiwa katika kuwaza, simu yake iliita, akaiinua na kuiweka sikioni akiwa na shauku ya kujua nini kimetokea katika msakao huo.
“JoKi !” sauti iliita kisha ikakata.
“Sema, mmekamlisha kazi?” akauliza.
“Hapana JoKi, muda tulioupanga kukamilisha kazi umepita, lakini hatujafanikiwa kumpata Yule hayawani, tufanyeje?” Mkuu wa kikosi cha kwanza akajieleza.
JoKi akatulia kimya kwa fungu la sekunde, akashusha pumzi na kuitoa simu sikioni; tayari alikuwa amesahau anaongea na nani, akakumbuka, akajicheka na kurudisha simu sikioni.
“Subiri kidogo, nitakupa jibu,” JoKi akajibu. Akaitua simu chini na kuhisi kuchanganyikiwa, akabofya namba Fulani na kusikiliza. Naima alikuwa upande wa pili.
“Yes JoKi!” akaitikia.
“Niambie mmefikia wapi na harakati?” JoKi akauliza.
“Bad! Very bad! Huyu jamaa kwanza keshaua mtu mmoja, nimepambana naye lakini Polisi wameharibu muvi, kanitoroka,” akaeleza.
JoKi akapiga ngumi mezani baada ya kujua uwa keshapoteza watu wane katika harakati zake.
“Shiit!” akang’aka, “Unamwonaje?” akauliza.
“Mtepetevu, simshindwi hata kidogo, nab ado namsaka kwani amenijeruhi,” Naima akajigamba. Baada ya kuongea na Naima akapigia kikosi cha tatu nacho majibu ni yaleyale kuwa mtu huyo hajaonekana. Ni Naima peke yake aliweza kumwona na kupambana naye japo kwa sekunde chache. JoKi akatoa maagizo kuwa vikosi viwili vibaki kazini na kikosi kimoja kirudi kambini kwa ajili ya kutekeleza majukumu mengine. Kati ya vikosi viwili vilivyobaki kumsaka Amata kikosi cha Naima nacho kilikuwamo.
Tayari giza lilianza kuuachia mwanga nafasi ya utawala, kwa pande zote mbili huo haukuwa muda rafiki kufanya makeke yoyote lakini haikuwa na jinsi. Pande zote mbili zilikuwa kazini kwa umakini zaidi.
JoKi aliwapanga watu wake vyema katika jiji la Dar es salaam kuwa popote watakapomuona Kamanda Amata wasifanye lolote bali waitaarifu ofisi nayo itajua nini cha kufanya ili kumaliza kijana huyo shababi.
§§§§§
KATIKATI YA JIJI LA DAR ES SALAAM-saa 1:02 asubuhi.
MITEGO MIWILI ilitegwa mahsusi kwa ajili ya Kamanda Amata, wakati huu wa jua hawakutakiwa kumuua ila walipewa amri moja tu ya kutoa taarifa kwamba kaonekana sehemu Fulani kisha kazi ya kummaliza ifanyike bila tabu.
Kikosi cha kwanza chenye watu wane kilikuwa jirani kabisa na jingo la JM Mall ambapo ndani yake, juu; ghorofa ya sita kuna ofisi ya AGI Investiment inayomilikiwa na Kamanda Amata kama Mkurugenza huku Gina akiwa kama Katibu wake, hapo ndipo hupangia mipango yote migumu na kuigeuza kuwa myepesi, nani afe na nani hasife, nani aokolewe na nani atoswe yote yalijadiliwa hapo kwa usiri mkubwa wakati leseni ya kampuni hiyo ni ya ufaulishaji mizigo bandarini.
Watu waliaanza kulijaza jiji, mishemishe za hapa na pale zilianza kuzikumba kona za jiji la Dar es salaam, jua nalo lilipanda angani taratibu likitokea pande zile za Kigamboni. Naima alikuwa ametulia katika moja ya mbao za magazeti akitazama habari nzito iliyobeba magazeti mengi ya siku hiyo.
…Mbunge wa Miroroso auawa kikatili nyumbani kwake Msasani…
Moja ya gazeti liliandika hivyo kwa wino mzito, watu walijazana kusoma habari hiyo, kila kona ya jiji liliongelewa hilo.
“Washamuua huyo! Nchi hii utaiweza!” mmoja wa madereva Tax aliropoka
“Ndiyo hivyo, hii nchi ya wenyewe hii, alikuwa anaongea sana huyu, washamtengeneza!” mwingine alidakia.
“Badala msikitike wapigania haki wanapotezwa nyie mnashabikia kwa maneno ya ajabu,” mara hii mshona viatu alimalizia.
Mazungumzo juu ya hilo yakatawala kila kona ya eneo lile, kufumba na kufumbua gazeti la Mbiu ya Mnyonge likapotea mbaoni, likaisha kabisa kwa kuwa liliandika vizuri habari hiyo.
Naima alisikiliza yote hayo, akakitazama kidole chake cha shahada cha mkono wa kuume akatabasamu na kusogea pembeni ya eneo hilo, aliwatazama vijana wake wawili aliobaki nao katika kikosi chake akawapa ishara kuwa mambo yako sawa.
Kamanda Amata alikuwa akisubiriwa katika maeneo yake muhimu ya kujidai, yeye hakuwa na habari ya lolote katika kuwindwa huko. Asubuhi hiyo alirudi nyumbani kwake japo kujiweka sawa na kuanza awamu mpya ya mapambano ya mchana, muda ulimpiga kikumbo, alipenda kuibuka kidedea kabla ya jogoo kuwika lakini akajikuta akikabiliwa na mambo mengi ya kiupelelzi ili kuwajua adui zake walivyo, lakini hakujuwa bado wamejipanga vipi, kitu kilichompa ujasiri siku hiyo, ni kule kuwa peke yake katika uwanja wa mapambano, kumbe hakuhitaji kutumia akili ya pili kumlinda mwingine; lakini pia alijua wazi kuwa nalo ni hatari ubwa kwani macho ya adui yake yatakuwa na kazi moja tu ya kumtazama yeye kila anaponyanyua wayo wa mguu wake. Aliegesha pikipiki lake mahala pake na kulizima, akatulia kusikiliza lolote kama lipo, ukimya ulitawala, hakuna jipya, akavua kofia lake na kulipachika juu ya kioo cha pikipiki hilo kisha yeye kujitoma ndani huku mkono mmoja ukiwa ndani ya jaketi lake.
Alipohakikisha kila kitu ni salama, akaingia chumbani mwake na kujiweka sawa kivingine.
Alipotoka ndani; alikuwa ndani ya suti ya kijivu iliyotanguliwa na shati la buluu bahari, akalielekea jokofu na kuchukua dumu la maziwa, akamimina kwenye kikombe kikubwa, soseji tatu nene pamoja na slesi kadhaa za mkate, vikapashwa kwa microwave na toaster.
Nje ya nyumba ya Amata kulikuwa na pub ya kisasa ambayo iliendesha shughuli zake saa saa ishirini na nne, asubuhi hiyo iliyokuwa na hali ya mawingu, bado watu wachache walionekana kuwapo eneo hilo ama wakiongea hiki na kile au wakipata supu ya kongolo. Hilo halikuwa tatizo kwa Amata, aliitoa gari yake nje na kuiweka sawa tayari kwa safari, akafunga geti lake kwa kutumia rimoti maalum kwa kazi hiyo.
Huku macho yake yakifanya kazi ya ziada ya kuatzama huku na kule akili yake ilipisha uamuzi wa kuhamisha tiba za Gina na Scoba kwenda shamba ili kuepusha lolote ambalo adui yake anaweza kulifanya, kwa maana kama ni watu aliyoawategemea basi ni hao tu. Aliingia kwenye gari yake aina ya Volks Wagen, au wengi mngependa kuiita Golf, akashusha kioo taratibu na kumtazama binti aliyekuwa akipita mbele ya gari yake. “Duniani kuna viumbe mwe!” akajisemea na kisha akaingiza gia namba moja na kuondoka taratibu, alipoumaliza wigo wa ile Pub, akatupa jicho kutazama kijia kile alichoingilia Yule mwanadada, akalisanifu umbo la msichana huyo kwa nyuma, lo; akashindwa afanye nini, akaodoa gari yake na kuikamata barabara ya KInondoni kuelekea daraja la Salenda, alipoikanyaga tu barabara ile na kwenda mwendo wa mita kama 200 hivi, akatazama kioo chake cha ndani na kuona gari nyingine nyeupe ikiingia barabarani kutokea njia ileile. Hakuitilia shaka lakini alitaka kupata uhakika kama gari hiyo ana nasaba nayo au la.
Kabla hajafika kwenye makutano, akakunja kulia na kuingia ofisi za ubalozi wa Uswizz, akaweka gari katika maegesho yake, hakushuka. Akaiona ile gari ikipitiliza, hapo nay eye akatoa gari yake na kurudi barabarani, alipokunja kulia hakuiona ile gari, akajua hisia zake hazikuwa sawasawa, akaingia barabarani na kuifuata barabara ya Bagamoyo mpaka Salenda na kukunja kushoto kuingia barabara ya Ocean kisha akaegesha gari yake kwa mbele kidogo akitazama kama kunayeyote anayefuatilia nyendo hizo. Alipohakikisha hakuna jipya, akakodi Tax na kuelekea Sea View.
“Nishushe hapa!” akamwamuru dereva Tax kisha akamtupia not ya 5000 na kutokomea zake.
§§§§§
DR. KHADRAI ALIKUWA BIZE NA MGONJWA WAKE, kama Mzuka Kamanda Amata akasimama katika mlango wa chumba hicho.
“Karibu Amata,” akamkaribisha kitini.
“Asante nimekaribia, anaendeleaje huyo?” akauliza mara baada ya kuketi kitini.
“Anaendelea vyema, ameamka ila bado fahamu hazijamrudia, lakini si muda mrefu atakuwa sawa, lakini, Amata, huyu atatakiwa kupumzika kama miezi mitatu hivi asifanye shughuli za mikiki mikiki,” akaeleza.
“Ok, umeeleweka kabisa. Sasa Khadrai ipo hivi, hali ya kiusalama sio nzuri sana, na nimekuja hapa kwa jambo moja tu,” Kamanda akainuka kitini, na kuliendea dirisha kubwa la aluminium na kuchungulia nje, akaiona ile gari ikiegeshwa mahala Fulani jirani kabisa na lile jumba la Khadrai, akarudi na kusimama karibu kabisa na daktari huyo, “Sikiliza, wewe na huyu Gina nitawapeleka Safe House, leo hii, kila kitu kipo kule utatumia ofisi ya Dr. Jasmine”.
“Ni wapi huko?” Khadrai akauliza.
“We jua ni Safe House, iko wapi hilo sio swali kwa sasa, haya mwandae mgonjwa wako kwa safari, ukiwa tayari unambie, nitatumia gari yako pia,” akamwambia huku akitokea sebuleni, ukimya wa jumba hilo ulibaki hivyo hivyo, akatzama huku na huko, akachomoa bastola yake ndogo kabisa na kuiweka sawa, akavuta hatua kuuelekea mlango wa kutokea nje, akabana dirishani kutazama.
Mlinzi wa geti aliliendea kufungua baada ya kusikia mbisho, Kamanda akatulia palepale akitazama huku bastola yake ikiwa tayari kutekeleza itakaloamuriwa. Yule mlinzi akafungua geti, mtu mmoja akaingia ndani akifuatiwa na wengine wawili, alikuwa amevalia suti nyeupe kabisa na wale wenzake vivyo hivyo, hakuwa Mtanzania, wala hakuwa Mwafrika, kutoka pale dirishani Kamanda Amata akajihisi kupata ubaridi wa ghafla.
“Smart Killer!” akajisemea, kisha akarudi ndani kwa Daktari Khadrai.
“Kaeni humu, msitoke nje wala kuchungulia,” akarudi sebuleni, na kukuta wageni wake wakiujia mlango mkubwa wa nyumba ilhali mlinzi anagalagala chini pale getini.
“Haina haja ya kutukaribisha,” Yule mtu aliongea kwa Kifaransa safi huku wale wenzake wakiwa kimya na mikono yao wameifumbata ndani ya makoti yao, Yule bwana mkubwa alijishika kiuno na kuyaachia mabastola yake waziwazi yakining’inia.
“Karibuni, karibuni viti,” akawakaribisha huku yeye akikiendea kimoja ya viti hivyo.
“Hatuna haja ya kukaa! Tumeshakaa sana kwenye ndege tuliyokuja nayo!” tunataka kitu kimoja tu hapa na tunaondoka na ndege ya saa tano,” Yule bwana akajibu kijeuri huku akichomoa bastola moja na kuifunga kiwambo cha sauti.
“Kitu gani?” Amata akauliza.
“Roho, roho yako inayokutia ujeuri ndiyo tunayoitaka sisi!” Yule bwana akaeleza, huku akiwa tayari kainua bastola yake na kuielekezea katika paji la uso la Amata. Uongo wa Amata ulikuwa ukifanya kazi kwa kasi ya ajabu kuliko kawaida yake akitazama huku na kule kwa kuzungusha macho, akiwatazama wote watatu na kuuona kwa haraka haraka uhatari wa viumbe hao waliovalia sare mpaka mtindo wa viatu vyao ulikuwa wa kipiganaji kabisa. “Kazi ipo, hapa ni kufa nakupona,” Kamanda akawaza.
§§§§§
5
KANAYO O. KANAYO ALIKETI KATIKA NUSU UKUTA akiangali mechi ya mpira wa miguu kati ya afungwa mashabiki wa Yanga na Simba. Nywele zilianza kupoteza mng’ao wake, ndevu zilizokosa mnyoaji mzuri anayeijua kazi yake nazo zilikuwa hoi, uzee ulinyemelea mwili huo ambao ulikuwa wa kupendeza kwa mafuta na unyunyu wa gharama. Akiwa ametingwa katika kutazama mechi hiyo ambayo upande wa Yanga ulishinda 3-0 kama kawaida, alihisi kitu kikipenyeshwa kwenye kiganja cha mkono wake.
Ilikuwa kijikaratasi kidogo, akamtazama huyo aliyeifanya kazi hiyo, akamwona na kumbania jicho kisha akaifungua ile karatasi na kuisoma, alipomaliza, akaikunja na kuondoka zake.
Ndani ya chumba chao cha kulala chake cha kulala kilichokuwa na kitanda kimoja kidogo chenye tandiko tu bila godoro, aliketi kwa utulivu na kuingiza mkono uvunguni akachomoa bahasha ndogo na kuifungua ndani.
“…Kazi imeanza mtaani, tumekamata watatu, tumewaweka kwenye hali mbaya wawili, bado mmoja, Kamanda Amata.
Tumeleta Smart Killer kama mlivyoagiza, tukimmaliza yeye ndipo tutafanya plan B, kaa tayari kwa taarifa ya mapinduzi.
Mafisadi; kama wanavyotuita, tutaendelea kuwapo tu na tutaiburuza nchi kwa noti zetu.
Cheers!...”
Akaikunja ile karatasi na kuitia kinywani huku akitabasamu.
§§§§§
MAHMOUD ZEBAKI alitema karatasi iliyokuwa kinywani mwake na kuipachika uvunguni mwa kitanda chake, akatabasamu kwa tabasamu pana. Ijapokua ngozi yake ilikuwa kavu kwa kukosa japo Vaseline lakini bado ilionesha afya kwa mbali, jela ni jela tu. “Hawatuwezi hawa, tutaendelea kutafuna pesa tu, fisadi sio peke yangu kuna Magurubembe huko nje hawayajui, na kesi yetu tutashinda,” akajipa moyo huku akisimama na kutembea hapa na pale.
Kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na pesa za umma waliyoshitakiwa Mahmoud Zebaki, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Uswizz na Kanayo O. Kanayo aliyekuwa Waziri katia Wizara nyeti ya Serikali ilikuwa ikiunguruma katika Mahakama ya Kisutu, kila mara iliposomwa iliahirishwa na watu hao kurudisha lumande. Wananchi wengi walilalamika kwani hawakuelewa kwanini kesi hiyo inapigwa danadana kiasi hicho, wakati Wananchi wakilalama kuwa watu hao ‘wasulibiwe’, walioshika mpini wanasema ‘uchunguzi unaendelea’.
§§§§§§
Kama kuna kitu kilimuuzi Pancho Panchilio alipokuwa ofisini kwake ni kitendo cha kudanganywa juu ya ile kompyuta, alipoifungua akiwa ofisini mwake ilifunguka na kumuonesha picha moja tu ya fuvu lenye ujumbe chini yake ‘Ni zamu yako kufa’. “Kama wao ni wajanja basi mimi ni zaidi, na ile kompyuta lazima niipate leo hii,” akajiwazia huku mwili wake ukitetemeka kwa hasira. Aliinuka na kuliendea dirisha kubwa la kioo na kuitazama mandhari ya jiji la Dar es salaam, akasonya na kuichomoa bastola yake, alipogeuka alifyatua na kuisambaratisha ile kompyuta pale mezani, akairudisha bastola yake na kurudi kitini. “Fanya nililokuagiza, kumbuka sisi ndiyo tunaokulinda hapa nchini na hata nchi yako haijui kama upo hapa kutokana na makosa uliyoyafanya huko,” aliyakumbuka maneno ya Kanayo O. kanayo siku alipokwenda kumtembelea gerezani.
“Lazima ufe leo Kamanda,” akajisemea na kujibwaga kitini. Aliinamisha kichwa chake mezani huku mikono yake ikizitimua nywele zake za Kihindi kama anayetafuta kitu Fulani humo, kisha akakiinua ghafla na kutazama mlangoni. Akapiga ngumi mezani, akanyanyuka na kuibeba briefcase yake, akatoka mpaka kwenye ofisi ndogo ya katibu wake.
“Boss, mbona mapema?” Yule binti akauliza.
“Usijali, natoka, kuna kazi naenda kuifanya, nitarudi hapa kesho, aaah no hapana, naweza kuchukua hata siku mbili nje ya ofisi, nitakupigia baadaye,” alikuwa akiongea huku akibabaika hapa na pale. Akatoka ofisini na kuiendea gari yake kabla hajapotelea mjini.
KITUO CHA POLISI CHA KATI- muda huohuo
INSPEKTA SIMBEYE hakujua nini la kufanya asubuhi hiyo, wingu jeusi lilikuwa limekigubika kichwa chake, alijua la kufanya lakini alishindwa kulifanya. Hapo ndipo moyo wake uliporudisha uamuzi wa kustahafu kazi hiyo, uamuzi ambao ulikataliwa pindi ulipowafikia wakubwa, ulikataliwa kwa sababu ya utendaji kazi wa kiumbe huyo alijulikana kwa cheo kama jina, Inspekta. Aliipenda kazi yake sana, hata baadaye akafanya kazi nyingi kwa kushirikiana na Idara nyeti za Usalama wa Taifa, alikuwa mpole, mnyeyekevu, msiri, mwenye huruma, lakini makini katika kazi na hakufanya makosa. Hakupenda kukumbatia ujinga wala upumbavu. Alikuwa mkufunzi wa mafunzo ya polisi wapya pale CCP na ndipo alipokuatana na Kijana Amata alipoingia mafunzoni.
Mara kwa mara alikuwa akimtazama kijana huyo mchangamfu kwa jicho la pekee, “Anafaa,” alijisemea huku akitikisa kichwa alipokuwa akishuhudia shabaha ya aina yake iliyokuwa ikilengwa mazoezini, wepesi wa kufanya michezo ya karate na kungfu, alivutiwa. Alimjua vema, vema sana na alimwamini kuliko unavyofikiria.
Alijiinua kichwa chake na kuitazama picha kubwa ya Mwl. Nyerere iliyokuwa imening’inia ukutani, “Tutakumbatia waovu mpaka lini ilhali wanajulikana walipo?” alijikuta akiiuliza ile picha bila kujua kuwa haiwezi kumjibu, akatikisa kichwa. “Usifanye lolote juu ya mtu huyo! Mwache kama alivyo mpaka oda ya juu itakapotoka,” aliikumbuka sauti hiyo iliyomfikia kupitia simu yake ya ofisini pale alipoomba kumkamata bwanyenye huyo aliyezaliwa India na kutarajia kufia Tanganyika.
Akasonya, akaisogeza kofia yake pembeni na kuinyanyua simu yake, akabofya zile namba unazozifahamu, akaiweka sikioni, tayari moyo wake ulipitisha maamuzi, kifua chake kilikuwa kikipanda na kushuka, “Nitajua la kumfanya!” alijiambia.
§§§§§
ITAENDELEA....