3
Kilomita 18, kutoka kijiji cha Chiro, Abbas Jembe alikoroma kitandani mwake kwenye jumba lake la kifahari, jijini Arusha.
Chumba kilikuwa kipana mno, vitanda 12 vya sita kwa sita vingeenea endapo vingepangwa sambamba. Kushoto mwa kitanda chake, kulikopaswa kuweko ukuta wa nne, kulikuwepo kioo kikubwa kilichotoka kwenye paa hadi sakafu. Hili ndilo lilipaswa kuwa dirisha. Vitu vingi vya kifahari vilitapakaa kwenye meza pana ya kioo iliyokuwa mkabala na kitanda, karibu na dirisha lile kubwa la kioo. Saa tatu za dhahabu, kompyuta mpakato aina ya Apple Macbook Pro, na simu kadhaa za gharama vilitandazwa bila mpangilio kwenye meza ile. Kwa juu, feni ilizunguka kwa kasi ya wastani.
'NGO NGO NGO' NGO' mtu alibisha hodi. Ila hakujibiwa.
'NGO NGO NGO' NGO' Alirudia tena. Bado kulikuwa kimya.
'NGO NGO NG...'
"Arrgh!" Abbas alizinduka kutoka usingizini. " Nini? Nani? Aki ya nan kama...."
"Ni James, mkuu," mtu yule alijibu kwa upande wa pili.
"Oh," Abbas ambaye bado alikuwa amejikunyata kwenye kitanda alijibu. Aliamka na hapo hapo alitumia mkono wake kuyakinga macho yake kutokana na mwanga wa jua uliokuwa ukipita kwa urahisi na kwa wingi kwenye dirisha lake kubwa. Alijipa muda na kuyafunua macho yake taratibu.
"Ingia," alisema na kunyanyuka kutoka pale kitandani, na kusimama kwenye ukuta ule wa kioo, dirisha. Kwa njee aliweza kuona mandhari ya nyuma ya jengo lake yaliyovutia. Kulikuweko na bustani nzuri ya maua, na bwawa la kisasa la kuogelea. Magali manne ya kifahali yalipaki kushoto kwenye sehemu maalumu iliyokuwa imejengwa kwa ajili ya matumizi hayo. Chumba chake kilikuwa kwenye horofa ya tatu kwenye jengo lake la horofa tano, hivyo yote aliweza kuyaona kutoka juu. Kwa mbali kidogo aliweza kuziona horofa nyingine za jiji la Arusha, na alivutiwa na mandhari nzima.
Mwanaume, mwenye umri wa miaka therathini hivi, akiwa amevaa suti, tai , na viatu vyeusi, shati tu likwa jeupe, aliingia chumbani humo huku akiwa ameshikilia faili jeusi mkononi. Kwa jinsi alivyotembea---wima, huku kichwa chake kikiwa kama cha mwanajeshi kwenye gwaride---mtu angesema alikuwa roboti.
"Saa ngapi sa hivi?" Abbas ambaye bado alikuwa akitazama nje, aliuliza.
"Saba na dakika tano, mkuu, " James alijibu.
"Shit," Abbas alitamka kimya kimya na kumgeukia James, "Kikao...nlikuwa na kikao!"
"Ndio, mkuu."
"Enhe?"
"Ulikiwa na vikao viwili, mkuu. Cha saa mbili na cha saa nne, nlijaribu kukuamsha, hukuamka, mkuu. Gloria amekuwakilisha." James alijibu kwa unyenyekevu.
Abbas alimtazama James kwa muda, na bila kusema neno aliugeukia ukuta ule wa kioo...na kundelea kutazama nje. Ukimya ulipita kwa sekunde kadhaa. Nae aliruhusu, uendeelee kutawala kwa sekunde zilizofuata.
"Kuna kitu?" Mwishowe aliuliza.
"Ndio, waandishi wa habari wamefika sio muda na wamesisitiza kuonana na..."
"Mimi."
"Ndio, mkuu."
'Pumbavu zao,' aliwaza.
"Sawa, kawaambie nafika, ndani ya dakika kumi kama wataweza subiri."
"Ndio, mkuu," James alijibu. Na kuweka faili lile jeusi kwenye ile meza ya kioo."Maafikiano, kwenye vikao vyote viwili, leo."
"Ntapitia baadae," Abbas alisema, na kupiga muayo. "Vipi, mipango iko kama ilivyopangwa?"
"Ndio, mkuu," James alijibu.
"Vizuri, Gloria asifahamu kitu. Hakikisha kila kitu kinaenda sambamba."
"Ndio, mkuu."
"Nakuaminia, " alisema Abbas na kurudi kuketi kwenye kitanda chake kikubwa. Alisema hivyo kila alipo maliza maongezi na mtu wake wa ndani, na hivyo James, kama alivyoingia, alitoka na kufunga mlango.
Abbas, alihema na kupitisha mikono yake kichwani.
'Saa saba!' Aliwaza. Kwenye mambo ambayo hakuwa akiamini ni kuwa angeweza kulala fofo hadi saa saba mchana. Haijakaa sawa hii, alifikiri. Alijinyoosha na kisha kuelekea bafuni.
Abbas, alikuwa wa urefu wa wastani mwenye mwili imara kwa mtu mwenye miaka hamsini na sita. Mikunjo kwenye sura yake ambayo ilianza kuonesha uzee, ilimfanya kila mtu aliyemuona kwa mara ya kwanza kuwaza kama aliwahi kucheka maishani mwake. Na wengi hawakuwahi kufanikiwa kumuona akifanya hivyo.
Siku hii ilikuwa ya muhimu kwake naye alikuwa ameikosa. Baada ya kujiingiza kwenye siasa na kujaribu kugombea u 'meya' wa jiji la Arusha, alianza kuchoka haraka kutokana na kamepeni alizofanya kwenye wilaya na vimiji kadhaa mkoani humo, hali iliyompelekea kulala sana.
Ndani ya dakika chache aliweza kutoka bafuni, na kubofya kijirimoti kilichokuwa pale mezani, ukuta mmoja wapo, taratibu ulifunuka kuonesha chumba cha siri kilichokuwa na makabati makubwa matatu na sehemu ya manukato.
Alifungua kabati la kwanza---lilikouwa na nguo za kila aina---na kutoa suruali gumu, la kahawia, fulana pamoja na shati jeupe la mikono mirefu. Hakutumia muda kuvaa, na baada ya kuhakikisha alipenda muonekano wake, alifungua kabati lile la pili. Hili lilikuwa la viatu. Kulikuwemo kila aina ya viatu, ilimchukua sekunde therathini hivi kuamua angevaa vipi. Baada ya kuwaza kwa makini lichukua raba, nyeupe na kujivalia. Alijipuliza manukato yake pendwa, na kabla hajatoka kwenye chumba kile, alifikiria kidogo na kufungua kabati lile la tatu. Silaha na bunduki za aina mbali mbali zilitandazwa humo kwa umakini. Alichukua 'Glock 20 SD' kutoka sehemu iliyokuwa na aina kumi hivi za bastora na kisha kufunga kabati lile. Kwa umakini aliichomeka kwenye suruali yake kwa nyuma, na kufungua kabati lile na nguo. Alitoa mkoti wa kahawia na kuvalia kwa juu. Hakuwa na uhakika kwanini alichukua bastora ile, ila hakuirudisha. Alitoka kwenye chumba kile, na kubofya namba kadhaa alizojua yeye, nao ukuta ulijifunga. Kama ulivyokuwa awali, mtu asinge dhani kulikuwa na chumba hicho cha siri nyuma ya ukuta huo.
****
Horofa ya kwanza, kwenye jumba hili la kifahari, lilitumika kama sebule. Masofa marefu ya kuvutia yalipangwa kiupekee huku meza kadhaa za kioo zikifidia ile nafasi iliyobaki kati kati. Kwenye kuta moja wapo, Runinga ya inchi sabini na sita ilitundikwa kwa makini huku mfumo wa sauti ukiwa umeundwa kiumakini kumfanya mtazamaji ahisi sauti ilitoka chini ya sofa alilo kalia.
Siku hii, waandishi wa habari kutoka makampuni mbali mbali walikusanyika humu, kila mtu na peni pamoja na karatasi yake, baadhi wakiwa na 'tepu rekoda' tayari kumhoji Abbas, na kupata cha kuandika kwenye mageziti yao.
Dakika therathini na nane zilikuwa zimepita toka mtu aje na kuwaambia kuwa Abbas angefika ndani ya dakika kumi. Waliendelea kungonjea kwa hamu, huku baadhi wakitazama saa zao za mikononi kila baada ya muda fulani.
"Hellow!" Alisema Abbas, aliyetokea kwenye ngazi zilizokuwa zikielekea kwenye horofa ya pili. Hatimaye alikuwa amefika, na kila nyuso ya muandishi wa habari iliwaka, na furaha isiyofichika.
"Mtaniwia radhi, haikuwa kwenye ratiba yangu kuwa mchana wa Ijumaa hii, ningetembelewa na wanamiyeyusho," alisema kwa mitani huku akiketi. Baadhi walitabasamu, baadhi tu.
Wapiga picha walianza kupiga picha.
"Er...niko tayari kuwasikiliza, natumai mtakuwa na maswali," Alisema Abbas huku akijituliza vizuri kwenye sofa,"...ntajaribu kujibu kadri muda utakavyo ruhusu....saa nane na nusu nina 'interview' pale ShaniTV, hivyo....yap, tuanze!"
Kama ilivyokuwa makubaliano, wanahabari walinyoosha mikono yao, na yeye angechagua nani aulize swali.
Baada ya kuwaangaza kwa muda, alimchagua mmama mmoja aliyekuwa akituliza miwani yake usoni.
"Ahsante," yule mama alisimama na kusema. "Watu wa jiji la Arusha, na watanzania kwa ujumla wangetaka kufahamu, billionea kama wewe, kwanini utake kuwa meya, kwanini sasa hivi baada ya miaka yote hii?"
Abbas alikooa kabla ya kuendelea kuzungumza, na kila mtu alikuwa tayari kuandika.
"Kiufupi, kila mtu ana ndoto, nami nilikuwa na ndoto za kuwa mwanasiasa toka udogoni, nimeipata nafasi hii ambapo mkoa wetu unahitaji mabadiliko, kwanini nisijaribu?"
Wanahabari walimalizia kuandika, kila mtu kwa nafasi yake na mikono ilirushwa tena hewani. Abbas alimchagua mkaka mmoja aliyekuwa na kinasa sauti.
"Shukrani, boss wangu," Kijana yule alianza. "Unazumziaje matukio ya kinyama ambayo yamekuwa yakitokea mkoani Arusha kwa miezi sita mfurulizo?"
"Er," Abbas aliwaza kwa makini kabla ya kujibu. "Hizi ni nyakati mbaya, na haya matukio ya utekaji wa ndugu zetu yanaendelea kwa kuwa vyombo husika havifanyi wajibu wake kiustahiki. Kwa kuwa Meya wa Jiji la Arusha amefumbia macho, yeye na viongozi wengine wa jiji hili, hata na viongozi wa mkoa. Na hii ndio sababu moja wapo nimeamua kugombea ili Kuleta ukomo katika swala hili."
Kulikuwepo minon'gono kadhaa, na baada ya muda, mikono ilirushwa tena juu. Kabla hajachagua, James aliingia na kumnong'oneza kitu sikioni na kisha kuondoka.
"Er....rafiki zangu, muda sio rafiki, ntaruhusu swali la mwisho...ummm..." Aliwaza kwa muda akiwatazama. "....Wewe," alimnyooshea kidole mdada mmoja aliyekuwa kanyoa nywele zake na kuziwekea rangi nyeupe, zile zilizobaki.
"Umm, Ahsante. Kwanini kwa miaka yote hii ya umaarufu wako, hukuwahi kuonekana na mke...au kuwa na mahusiano, Bwana Abbas? Huyu Gloria, tetesi zinasema ni binti yako, je ni binti yako wa..."
"Kumzaa, kuokota au kununua?" Abbas alimalizia swali kuwafanya baadhi wacheke. "Nadhani mtu akimtazama Gloria na kunitazama, jibu analo. Samahani, huko sintogusia." Abbas alisema na kisha kuamka pale alipoketi.
"Bwana Abbas! Bwana Abbas!" Wanahabari walianza kuita....wakirusha mikono yao, maswali mawili matatu hayakuwa yamefidia muda wote waliobaki pale wakimsubiri.
Abbas aliruhusu mbaba mmoja wa makamo, kuuliza swali, alipofika kwenye lango la nyuma.
"Er...tunaweza kufahamu mikakati ya kuanza mradi wako wa 'Mabastania' uliko fikia....na...na...kama ugomvi wako na meya Patel unachangia..kwa ucheleweshaji?"
Mabastania, mnafahamu...nliropoka au?, aliwaza kwenye ukimya uliofuata. Hakuwahi kukumbuka kutamka hadharani kuhusu mradi huo.
"Mimi na Meya Patel, hatuna ugomvi. Ni misuguano ya ki..ya kisiasa, na siwezi muhusisha na kuchelewa kwa 'Mabastania'. Nadhani nliwahi kuwaambia(kama niliwahi) kuwa...huu utakuwa mradi mkubwa utakao tatua tatizo la ukosefu wa ajira kwa maelfu nchini. Unahitaji maandalizi marefu, hivyo ningewataka muwe na subira."
Kulikuwa na minong'ono kadhaa na mikono ilirushwa tena hewani. Bwana Abbas alitazama saa yake, ilikuwa saa nane dakika tisa. Muda sio rafiki, hivyo aliwakimbia.
Alipitia mlango wa nyuma, huku akiacha wanahabari wakimuita na kumwambia asubiri. Muda hakuwa nao. Hivyo hakuwasikiliza. Kwa nje, alikuta gari likimsubiri, na kijakazi aliyekuwa kasimama pembeni ya mlango alimfungulia mlango wa siti ya nyuma kwa heshima.
"Habari, Rashid," Abbas alisalimia na kuingia kwenye gari lile la kifahali aina ya Ferrari GT 32X. Rashid, kwa nje alifunga mlando na dereva wake bila kusubiri amri yoyote, aliwasha ingini na hao walipepea kupitia kwenye geti pana lililojifungua lenyewe na baada ya muda, walikuwa kwenye barabara kuu kuelekea jijini.
Kwenye gari, Abbas alivuta tray nyuma ya siti ya dereva, na kijifriji kidogo kilifunguka, humo kulikuwemo na aina mbali mbali za vilevi, na vinywaji baridi. Alichukua chupa ya mvinyo na glass na kujimwagia mpaka glass ilipotishia kujaa. Kwa umakini, alikifunga kiji friji kile, na kupiga pafu refu la mvinyo, na kutabasamu. Alihisi ubongo wake ulianza kuchangamka.
Ilimchukua sekunde kadhaa, na tumbo lake lililalama njaa. Ilikuwa saa nane nae hakuwa ameweka kitu tumboni. Alivuta tena tray kwenye siti ile pembeni na ya dereva na kijokofu kidogo kilitokea. Humo alichukua vipande kadhaa vya pizza, na kuanza kula.
"Ben...nna njaa," Abbas alimwambia dereva wake akiwa akijaribu kutafuta pande kubwa la pizza mdomoni, "Sikupipo asee!" Alisema kwa matani.
Ben, ambaye alikuwa makini kwenye uskani alitabasamu, na hakusema kitu.
"Hawa waandishi, watakuja kuniua bure, kila vijisiku viwili, washakutembela na vimaswali vile vile, tu kuuliza tofauti ya walivyo fanya mwanzo," Abbas alilalama akibugia kipande kingine cha pizza. "Uchumi ama kweli mbaya, mpaka wanasahau hadhi yao kwa taifa."
"Hadhi yao kwa taifa, mkuu?" Ben ambaye alikuwa kimya mda wote aliuliza. Kwenye mambo ambayo hakuwahi kudhani ni kuwa mwandishi wa habari angeonwa mwenye hadhi yoyote na billionea kama Abbas.
"Acha tu," alisema Abbas ambaye alikuwa amefungua jokofu na kutoa pizza nyingine. Ben alijitahidi kutoangua kicheko, "Usicheke Ben...sijala toka asubuhi na ni saa nane....nlikuwa...nlikuwa," aling'ata kipande cha piza na kufikiria.
"Yes...nlikuwa naongelea hawa wana habari. Enzi zetu kipindi ninakuwa, hawakuwa wakisukumwa na hela, bali mapenzi kwa kazi yao. Kupata interview kwenye TV, au gazeti...ilikuwa mziki kweli kweli,"
"Oh," alisema Ben, bila kutoa macho yake kwenye barabara.
"Enhe...nawashangaa hawa, wanakufuata wenyewe, maswali yale yale, nadhan ukiwapa hongo kidogo wanaweza andika uongo wowote kukuhusu!" Alisema Abbas, huku akimalizia glass yake ya pili ya mvinyo.
Alipenda kuongelea mambo kama haya alipokuwa anakula au ameshiba. Ben alilitambua hili, hivyo alibaki kimya.
Kwa mbali kidogo waliweza ona, horofa ndefu za jiji la Arusha, kwa kushoto, horofa ndefu kuliko zote ndiko waliko paswa kuwa. Lilikuwa jengo la Shani Media PLC, na muwasilishaji wa kipindi cha BiasharaLeo aliomba kupata nafasi hii na Abbas.
Ilikuwa Jumatano, na karani wa Abbas alipiga kumuambia kuwa ilikuwepo simu, kutoka ShaniTV kumhusu. Aliipokea nae aliulizwa kama alikuwa na muda kuhudhuria kipindi cha BiasharaLeo kilichoruka kuanzia saa nane na nusu mchana hadi saa kumi na mbili kamili jioni. Abbas hakukataa.
Walifika kwenye sehemu ya kuegeshea magari, nae Ben kwa umakini aliegesha gari, kwenye nafasi iliyokuwa wazi.
"Tumefika, mkuu," Alisema na kuizima injini.
"Vizuri, Ben," alisema Abbas aliyekuwa akinywa kinywaji maalumu kwa ajili ya kuondoa harufu mbaya mdomoni. Alifanya hivyo ili kuondoa harufu ya mvinyo. Wananchi hawakuwa wakijua kuwa alikuwa akitumia vilevi, naye hakutaka wajue. "Waweza kuendelea na shughuli zako, ila saa kumi na moja dakika arobaini uwe hapa...nataka nikawahi nyumbani."
"Ndio, mkuu."
Baada ya kuyasema hayo, Abbas alitoka nje na hapo hapo, alipokewa na mhudumu wa pale ShaniMedia tayari kumpeleka kwenye studio husika.
Kwa nyuma, Ben, ali ungurumisha gari na kutoweka.
ITAENDELEA