KUITAFUTA BENKI YA ZANZIBAR MARINE jijini Dar es Salaam halikuwa
jambo jepesi hata kidogo kwa kuzingatia kuwa hii ilikuwa ni benki mpya kabisa kuwahi
kufanya shughuli zake jijini Dar es Salaam. Ni katika benki hii ndipo mtu mwenye jina
la Aden Mawala aliposemekana kufanya kazi kama meneja wa benki hiyo. Kupitia
barua yenye ujumbe mfupi ndani ya bahasha ndogo ya kaki ambayo Koplo Tsega
alikuwa ameiichukua kule nyumbani kwa Balimenya usiku ule baada ya kupambana
na wale wanausalama wawili na hatimaye kuwaangamiza. Maelekezo ndani ya barua
ile kutoka kwa mtu mmoja asiyefahamika jina lake yalikuwa yameweka bayana kuwa
meneja wa benki ya Zanzibar Marine tawi la jijini Dar es Salaam ndugu Aden Mawala
alikuwa amepewa maelekezo yote muhimu ya kuhakikisha kuwa kiasi fulani cha fedha
nyingi sana zilizoingizwa kwenye benki yake anazifanyia mgao sahihi kufuatana na
orodha ya majina yote ya watu waliokuwa wameorodheshwa katika barua ile kutokea
tarehe fulani. Maelezo yale yaliendelea kuelekeza kuwa watu hao wangefika kwenye
benki hiyo pamoja na vitambulisho vyao vya kazi huku wakiwa na hundi zao tayari
kulipwa mgao wao katika fedha hizo. Mtoa taarifa kupitia barua ile ambaye hakutaja
jina lake aliendelea kusisitiza kuwa shughuli yote ya mgao wa fedha hizo ilipaswa
kufanywa katika mazingira yenye usiri mkubwa sana ingawa hakueleza kuwa ni lini
mgao huo ulipaswa kufanyika.
Kupitia orodha ya majina ya watu waliokuwa katika barua ile Koplo Tsega alikuwa
ameongeza ziada nyingine katika utafiti wake. Jambo moja muhimu aliloligundua
ni kuwa majina yote yaliyokuwa katika zile hundi alizozikuta kwenye ile bahasha
nyumbani kwa Meja Khalid Makame yalikuwa pia kwenye ile barua aliyoikuta
nyumbani kwa Balimenya isipokuwa majina ya watu wanne tu ambao hakuwafahamu.
Pili, hundi zile alizozipata nyumbani kwa Meja Khalid Makame zilikuwa ni za benki
ya Zanzibar Marine. Hivyo kwa namna moja au nyingine ni kuwa meneja wa benki ya
Zanzibar Marine jijini Dar es Salaam ndugu Aden Mawala alikuwa akifahamu kila kitu
kilichokuwa kikiendelea akiwemo yule mtu aliyetoa maelekezo yale kwenye ile barua.
Zanzibar Marine Bank ilikuwa kando ya barabara kuu ya Bagamoyo upande
wa kulia umbali mfupi baada ya kuyapita makutano ya barabara ya Kawawa na ile
barabara ya Mwai Kibaki eneo la Morocco kando ya jengo refu la ghorofa la Drive
Inn Plaza. Baada ya safari ndefu ya kuzunguka katika vitongoji vingi vya jiji la Dar
es Salaam na ulizauliza ya hapa na pale hatimaye Koplo Tsega akawa ameyafumania
maficho makini ya benki hii change jijini Dar es Salaam.
Mchana huu foleni ya magari katika barabara ya Bagamoyo ilikuwa kubwa na yenye
kukera hivyo Koplo Tsega akaona kuwa lingekuwa ni jambo la usumbufu sana kusubiri
foleni ile hadi ipungue ili apate nafasi nzuri ya kuchepuka upande wa pili wa barabara
ilipokuwa ile benki hivyo badala yake akaingia upande wa kushoto na kuegesha gari
lake kwenye eneo la maegesho ya magari la mgahawa maarufu wa kichina uitwao
Seafoods kisha akafungua mlango na kushuka akiwa katika mwonekano mpya kabisa
wa kofia nyeusi ya Sombrero kichwani, miwani nyeusi ya jua machoni, blauzi nyeusi
ya pullneck aliyoitanguliza ndani ya shati zito la jeans la rangi ya bluu bahari. Chini
alikuwa amevaa suruali nyepesi ya jeans iliyolichora vyema umbo lake maridhawa la
kike na buti ngumu za rangi ya udongo aina ya Travolta. Kwa kukwepa aina yoyote ya
bahati mbaya pale ambapo rabsha zozote zingejitokeza mbele ya safari Koplo Tsega
alikuwa ameamua kushuka na begi lake la mgongoni jeusi, jembamba na refu lenye
zana zote muhimu za kazi ikiwemo Sniper Rifle 338 Lapua Magnum, bunduki maalum
kwa ajili ya kudungulia windo sumbufu la umbali wa masafa marefu.
Kulikuwa na watu wachache waliokuwa wameketi kwenye sehemu ya nje ya
mgahawa ule wakijipatia huduma. Wakati Koplo Tsega alipokuwa akishuka kwenye
gari watu wale waligeuka na kumtazama hata hivyo hakutoa nafasi yoyote ya kugeuka
kuvutia badala yake akafunga mlango haraka na kuvuka barabara akielekea upande wa
pili eneo lilipokuwa lile jengo la benki ya Zanzibar Marine huku akikatisha katikati ya
foleni ndefu ya magari katika barabara ile.
Akiwa na hakika kuwa hakuna mtu yeyote aliyekuwa akimfuatilia nyuma yake mara
tu alipomaliza kuvuka barabara ile Koplo Tsega akatembea kandokando ya barabara
ile akishika uelekeo wa upande wa kulia hadi pale alipokifikia kizuizi cha mbele cha
kuingia kwenye benki ile kando ya kibanda cha mlinzi kilichokuwa na askari polisi
wawili ambapo alipita pembeni ya kizuizi kile katika njia ya wazi ya watembea kwa
miguu iliyopakana na bustani nzuri ya nyasi za kijani kibichi na miti mirefu ya miashoki
iliyopandwa katika mstari mnyoofu wa kupendeza mbele ya jengo lile la benki.
Koplo Tsega akaendelea kutembea kwa utulivu akielekea kwenye ile benki huku
kumbukumbu zake zikimueleza kuwa kabla ya jengo lile kutumika na Zanzibar Marine
Bank hapo awali lilikuwa likitumika kama makao makuu ya shirika fulani la mtandao
wa mawasiliano ya simu. Tangu kutokea mauaji ya Sikawa kwenye kile chumba
namba 18 cha Hotel 92 Dar es Salaam eneo la Ubungo, Koplo Tsega alikuwa ameamua
kuhamishia makazi yake kwenye chumba kimoja alichokuwa akiishi Sikawa kati ya
vyumba vingi vya uani vya wapangaji katika nyumba moja iliyokuwa eneo la Mwenge
mtaa wa Mama Ngoma. Huku akirudi usiku wa manane wakati wapangaji wote
wakiwa usingizini na kuondoka mapema sana alfajiri kabla ya watu wote hawajaamka
katika kile chumba kidogo cha kijana wa mjini chenye kitanda kidogo cha futi tano
kwa sita, kabati dogo la nguo, seti moja ya runinga juu ya meza yenye deki moja ya ya
dvd, spika dhaifu za muziki wa gheto na ndoo nyingi za maji zilizokuwa kwenye kona
mojawapo ya chumba kile. Ili kumuenzi Sikawa, Koplo Tsega alikuwa amejiapiza
kulipa kisasi kwa wote walio husika na kifo chake.
Nje ya jengo lile la benki ya Zanzibar Marine kwenye eneo la maegesho ya magari
kulikuwa na magari machache yaliyokuwa yameegeshwa. Koplo Tsega alipochunguza
akajikuta akifurahi baada ya kugundua kuwa miongoni mwa magari yaliyokuwa katika
maegesho yale lilikuwepo gari moja aina ya Landcruiser jeupe lililokuwa limeegeshwa
katika sehemu maalum ya maegesho yenye utambulisho wa cheo cha meneja wa benki
ile. Uwepo wa lile gari eneo lile ikawa ni ishara tosha kuwa meneja wa benki ile ndugu
Aden Mawala alikuwepo ofisini kwake kama kawaida akiendelea na shughuli zake za
kiofisi kama ilivyo ada. Hata hivyo mandhari ya nje ya ile benki yalitosha kuthibitisha
kuwa benki ile haikuwa na msongamano mkubwa wa wateja kama zilivyokuwa benki
nyingine zenye umri mrefu jijini Dar es Salaam.
Koplo Tsega akaendelea kutembea kwa utulivu akikatisha kuelekea sehemu ya
mbele ya benki ile yenye baraza pana ya sakafu ya marumaru za kuvutia na juu yake
imefunikwa na paa zuri na imara ya zege iliyoezekwa kwa vigae na kushikiliwa na
nguzo mbili upande wa kushoto na kulia. Koplo Tsega alipozifikia ngazi za baraza ile
akazipanda kwa utulivu kisha baada ya safari ya hatua chache mbele yake akausukuma
mlango mkubwa wa kioo na kupotelea mle ndani.
Ndani ya benki ile kulikuwa na watu wachache ambao kwa idadi yao wengi wao
walikuwa ni wazanzibar kama siyo watu wenye asili ya bara la Asia. Mandhari ya benki
ile mle ndani yalikuwa tulivu na ya kisomi. Viyoyozi makini vya mle ndani vilikuwa
vikiendelea kusukuma hewa safi yenye baridi ya wastani. Mara baada ya kuingia mle
ndani upande wa kushoto kulikuwa na ngazi za kuelekea juu ghorofani kwenye ofisi
nyingine za idara tofauti za benki ile kama idara ya mikopo, idara za sera, mipango
na utawala na nyinginezo. Sehemu ya chini katikati ya jengo kulikuwa na nguzo mbili
kubwa za uviringo zilizoishikilia sehemu ya juu ya jengo lile na sakafu ya mle ndani
ilifunikwa kwa zulia zuri la rangi ya kijivu.
Mara baada ya kuingia mle ndani Koplo Tsega akasita kidogo na kusimama
akijitahidi kuyazoea mandhari ya mle ndani kwa kuyatembeza macho yake taratibu.
Upande wa kushoto kulikuwa na meza ya ukutani ambayo ilikuwa ikitumiwa na wateja
wa benki ile kwa ajili ya kuandikia au kujaza taarifa za benki kwenye slips zao. Mara
baada ya kuipita meza ile kulikuwa na viti vingi katika sehemu maalum ambapo wateja
wa benki ile wangeketi na kusubiri wakati shida zao zikishughulikiwa na maafisa wa
benki ile. Baada ya kuipita sehemu ile ya mangojeo mbele kidogo kulikuwa na dawati
kubwa lenye umbo la nusu mkate mbele ya msichana mrembo wa idara ya huduma
kwa wateja aliyevaa Hijabu.
Upande wa kulia mle ndani kulikuwa na vibanda vinne vya tellers wa benki
vilivyotengenezwa kwa mbao nyepesi ya mahogani sehemu za chini na kuta safi za
vioo vyenye matundu mbele yake. Ndani ya vile vibanda kulikuwa na wafanyakazi wa
benki ile waliokuwa wakiendelea kuwahudumia wateja wachache waliokuwa kwenye
foleni fupi kuelekea vibanda vile.
Akiwa ameridhishwa na tathmini ya mandhari yale taratibu Koplo Tsega akapiga
hatua zake kuelekea kwenye lile dawati la huduma kwa wateja ama customer care
alilokuwa ameketi yule dada mlimbwende aliyekuwa eneo lile akimuelekeza mteja
mmoja namna ya kujaza taarifa zake kwenye fomu maalum ya benki iliyokuwa juu
ya lile dawati. Wakati Koplo Tsega akifika sehemu ile yule dada mlimbwende wa
mapokezi alikuwa tayari amekwisha maliza kumuhudumia yule mteja hivyo haraka
akageuka na kumtazama Koplo Tsega katika uso wenye tabasamu la kibiashara.
“Karibu dada”
“Ahsante” Koplo Tsega akaitikia kisha kabla ya kusema neno akageuka kidogo
kuyatembeza macho yake makali yaliyojificha nyuma ya miwani kuchunguza eneo lile
na alipoona kuwa hali ilikuwa shwari akayarudisha tena macho yake kwa yule dada.
“Karibu tafadhali naomba nikusaidie dada yangu” yule mlimbwende akasisitiza
huku akimtazama Koplo Tsega katika uso wenye tabasamu jepesi. Koplo Tsega
akasogea vizuri karibu ya lile dawati na kuongea huku usoni akilazimisha tabasamu.
“Nahitaji kuonana na meneja wa benki”
“Una shida gani dada yangu labda huwenda nikakusaidia” yule dada akaongea
kiungwana
“Nahitaji mishahara yote ya wafanyakazi wa kampuni yetu ipitie kwenye benki
yenu” Koplo Tsega akaamua kudanganya kwa kutengeneza hoja yenye ushawishi
mkubwa ambayo kwa namna moja au nyingine aliamini kuwa ilikuwa nje ya uwezo
wa yule dada wa idara ya huduma kwa wateja.
“Ofisi ya meneja wa benki ipo mwisho wa hili jengo upande wa kushoto ukifika
utaona korido. Fuata korido hiyo ukifika mwisho utauona mlango”
“Ngoja nipige simu ofisini kwake kuuliza kama atakuwa na mgeni yeyote” yule
dada akaongea kwa utulivu na kabla Koplo Tsega hajatia neno kiwambo cha simu
ya mezani iliyokuwa juu ya meza fupi kando yake tayari ilikuwa sikioni. Baada ya
kubonyeza tarakimu kadhaa ile simu ikawa hewani na hapo kukafuatiwa na maongezi
mafupi baina yake na mtu wa upande wa pili wa ile simu kabla ya yule dada kukata
simu na kugeuka akimtazama Koplo Tsega katika uso wenye tabasamu la matumaini.
“Unaweza kwenda yupo ofisini kwake na hana mgeni yeyote”
“Nashukuru” Koplo Tsega akatoa shukrani zake huku tabasamu hafifu la
kutengeza likiumbika usoni mwake
“Karibu tena” yule dada akaitikia huku akijiandaa kumsikiliza mteja mwingine
aliyefika eneo lile. Bila kupoteza muda Koplo Tsega akaanza kuzitupa hatua zake
taratibu akikatisha eneo lile kuelekea mwisho wa lile jengo kama alivyoelekezwa na
wakati alipokuwa akitembea akagundua macho ya wanaume wote waliokuwa kwenye
vile vibanda vya tellers wa ile benki yalikuwa yakimtazama kwa uchu kupitia kuta safi
za vioo zilizowazunguka na hali ile ikampa faraja kidogo huku taratibu akizichezesha
malighafi muhimu za mwili wake.
Mara tu alipofika mwisho wa lile jengo upande wa kushoto akaiona korido fupi
kama alivyoelekezwa hivyo Koplo Tsega akaifuata korido ile. Ilikuwa ni korido fupi
iliyokuwa ikitazamana na milango mitatu. Mlango mmoja upande wa kushoto,mlango
mwingine upande wa kulia na mlango wa mwisho ulikuwa mwisho wa ile korido kwa
mbele. Wakati Koplo Tsega akiendelea kutembea akawa akiyatembeza macho yake
taratibu kuichunguza ile milango na kupitia vibao vidogo vyeusi vyenye maandishi
meupe akagundua kuwa mlango wa kwanza upande wa kushoto ulikuwa ni wa ofisi
ya Line manager wa kitengo cha Import and Export. Mlango uliyofuata upande wa
kulia ulikuwa ni wa ofisi inayoshughulikia miamala yenye kuhusisha kiasi kikubwa cha
fedha ama Bulk transaction na ule mlango uliyokuwa mbele mwisho wa ile korido
ndiyo uliyokuwa wa kuelekea kwenye ofisi ya meneja wa benki ile hali iliyompelekea
Koplo Tsega ajikute akitabasamu peke yake. Mandhari ya eneo lile yalikuwa tulivu
mno hata hivyo hali ile haikumaanisha kuwa ndani vyumba vile hapakuwa na shughuli
za kiofisi zilizokuwa zikiendelea.
Hatimaye Koplo Tsega akawa ameufikia ule umlango wa kuingia kwenye ile ofisi
ya meneja wa ile benki. Alipofika pale mlangoni akasimama kidogo akijipa utulivu na
kujitengeneza vizuri na baada ya kugeuka nyuma na kuhakikisha kuwa hapakuwa na
mtu yeyote mwingine eneo lile akausogelea mlango wa ile ofisi na kushika kitasa chake
huku akikisukuma taratibu. Tofauti na matarajio yake mlango ule mzito ukafunguka
taratibu na hapo Koplo Tsega akaingia mle ndani.
Kama zilivyokuwa ofisi nyingi za kisasa za zama hizi ofisi ile ilikuwa ya kisasa zaidi.
Sakafu yake ilifunikwa kwa zulia maridadi la rangi ya kijivu lenye michoro ya maua
meusi na meupe. Upande wa kushoto kulikuwa na dirisha kubwa lililofunikwa kwa
pazia jepesi. Kando ya dirisha lile kulikuwa na rafu nne kubwa ya chuma zenye droo
nyingi zilizosimama wima kama milima meza. Kabla ya kuzifikia rafu zile kulikuwa na
seti moja ya makochi laini meupe ya sofa yaliyoizunguka meza fupi ya kioo iliyokuwa
na majarida na vipeperushi vinavyohusiana na huduma zinazotolewa na ile benki.
Upande wa kulia wa yale makochi kulikuwa na jokofu kubwa la vinywaji baridi
na kupitia mlango wa kioo wa lile jokofu isingemuwia vigumu mtu yeyote kuona
kilichokuwa mle ndani. Kiyoyozi makini bado kilikuwa kazini kusambaza hewa safi
iliyokinzana na hali ya joto kali ya jiji la Dar es Salaam mle ndani.
Kama zilivyokuwa ofisi nyingi zinazotoa huduma kwa jamii na kuchangia pato la
taifa,katikati ya ofisi ile ukutani kulikuwa na picha mbili za marais zilizotundikwa. Rais
wa serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania na rais wa serikali ya mapinduzi ya
Zanzibar.
Koplo Tsega akasumbuka kidogo katika kutaka kufahamu ni wapi alipokuwa
mwenyeji wa ofisi ile mle ndani na hali ile ilitokana na namna ya mpangilio wa ofisi
ile ulivyokuwa. Baada ya kuufunga ule mlango na kusogea upande wa kulia akizipita
rafu nyingine mbili ndefu za chuma zilizopakana na rafu nyingine kubwa zenye
vitabu,mafaili na nyaraka nyingine za ofisi hatimaye Koplo Tsega akamuona meneja
wa benki ile akiwa ameketi kwenye kiti chake cha utukufu nyuma ya meza kubwa
ya ofisi yenye kompyuta kubwa ya mezani,tray ndogo yenye ngazi tano kwa ajili ya
kuwekea nyaraka nyepesi za ofisi,simu ya mezani,mhuri na kidau cha wino pamoja
na mlima wa mafaili mengi mbele yake. Upande wa kushoto eneo lile kulikuwa na
meza nyingine ndogo na fupi ya mbao na juu ya meza ile kulikuwa na mashine tatu za
ofisi printer,scanner na mashine ya kudurufu. Pembeni yake upande wa kulia wa ile
meza ya ofisi kulikuwa na rafu ndogo ya chuma ambayo isingemlazimu meneja yule
wa benki kusimama hadi kuifikia. Mbele ya ile meza kulikuwa na kiti kimoja kikubwa
cha ofisi.
“Karibu binti” mzee mfupi mwenye kipara cha afya njema,mnene mwenye kitambi
cha ukwasi na macho makubwa ya hila yaliyojificha nyuma ya miwani kubwa alikuwa
amesita kuendelea kufanya alichokuwa akikifanya na kisha kuiegemeza mikono yake
mezani kabla ya kumkaribisha Koplo Tsega. Uso wake wa duara na ndevu zilizokatiwa
vizuri kuuzunguka mdomo wake,umri wake usingekuwa zaidi ya miaka hamsini. Uso
wake ulituama kama maji ya mtungini pasina kuonesha tashwishwi yoyote usoni.
Koti lake la suti ya kijivu alikuwa amelitundika nyuma kwenye kiti chake cha ofisi
kinachoweza kuzunguka nyuzi mia tatu sitini na hivyo kuusanifu vizuri mwonekano
wake mpya wa shati jeusi la mikono mirefu bila tai shingoni hali iliyoupelekea mkufu
wake mkubwa wa dhahabu uliotia nanga shingoni mwake kuonekana kwa usahihi
kama mng’aro wa kito cha thamani katikati ya giza.
“Ahsante” Koplo Tsega akaitikia kwa nidhamu kama iwavyo kwa mtu yeyote
mgeni aingiapo katika ofisi nyeti za mijini kisha taratibu akapiga hatua zake za woga
wa kujifanyisha akikaribia kile kiti cha ofisi kilichokuwa kikitazamana na ile meza ya
ofisini ya yule meneja na alipokaribia akasita kidogo.
“Karibu uketi binti” yule mzee akaongea kwa mamlaka huku akimtazama Koplo
Tsega kwa utulivu kabla ya kujiegemeza taratibu kwenye foronya laini ya kiti chake
cha ofisini.
“Nashukuru” Koplo Tsega akaongea kwa utulivu kisha akasogea karibu na kile kiti
kabla ya kukisogeza nyuma na kuketi. Kibao kidogo chenye utambulisho wa jina na
cheo cha mhusika wa ofisi ile kikamtanabaisha Koplo Tsega kuwa yule mtu aliyeketi
mbele yake nyuma ya ile meza ya ofisini ndiye mwenye jina la Aden Mawala,meneja
wa benki ya Zanzibar Marine jijini Dar es Salaam na hapo akajikuta akimeza funda
kubwa la mate kuzimeza hisia zake moyoni. Kitambo kifupi cha ukimya kikafuata mle
ndani huku kila mmoja akiwaza lake kichwani kabla ya yule mzee meneja wa benki
kuegemeza tena mikono yake mezani na kuvunja ukimya.
“Nipo tayari kukusikiliza shida yako binti,nimebanwa na kazi na bahati mbaya
sana leo sina muda wa kutosha”
“Nahitaji kuonana na ndugu Aden Mawala meneja wa benki hii bila shaka ndiyo
wewe” Koplo Tsega akaongea kwa utulivu katika uso wa kazi huku akimtazama yule
mzee kwa makini.
“Hujakosea” yule meneja wa benki akaitikia kwa utulivu na Koplo Tsega alipozidi
kumchunguza moyoni akahitimisha kuwa alikuwa ni mtu mgeni kabisa machoni
mwake. Yule meneja wa benki kuona vile akapeleka mkono na kuvuta mtoto wa
meza kabla ya kutoa kabrasha fulani na kuliweka pale mezani.
“Nimeambiwa kuwa unahitaji mishahara ya wafanyakazi wa kampuni yenu ipitie
kwenye benki yetu. Unatokea kampuni gani hapa Dar es Salaam?” yule meneja wa
benki akauliza huku taratibu akianza kupekua karatasi za lile kabrasha aliloliweka
mezani.
“T.P.D.F” Koplo Tsega akavunja ukimya.
“Ndiyo kampuni gani hiyo mbona sijawahi kuisikia tangu nizaliwe” yule meneja
wa benki akaongea huku akipunguza kasi ya kupekua kurasa za lile kabrasha.
“Tanzania People Defense Force”
“Kampuni ya ulinzi?” yule meneja wa benki akauliza huku akiangua kicheko
hafifu chenye dharau ndani yake.
“Jeshi la wananchi wa Tanzania” Koplo Tsega akafafanua huku akionesha kuanza
kuchoshwa na dharau za kisomi. Maelezo ya Koplo Tsega yakampelekea yule meneja
wa benki asitishe ghafla kile alichokuwa akikifanya na kuyasimamisha macho yake
akimtazama Koplo Tsega kwa mashaka.
“Jeshi la wananchi wa Tanzania siyo kampuni nadhani kuna jambo lingine
lililokuleta humu ndani” yule meneja wa benki akaongea kwa jazba kidogo huku
akiendelea kumtazama Koplo Tsega kwa udadisi. Pasipo kutia neno Koplo Tsega
akaingiza mkono mfukoni kuchukua ile bahasha aliyoipata nyumbani kwa Balimenya.
Kisha akafungua ile bahasha na kutoa ile barua fupi iliyokuwa ndani ya ile bahasha na
kuitupa pale mezani karibu na yule meneja wa benki. Kuona vile yule meneja wa benki
akaichukua ile karatasi na kuanza kusoma maelezo yaliyokuwa ndani yake. Koplo
Tsega akiwa makini kuzitazama nyendo za yule meneja wa benki akashtukia kuwa
kadiri yule meneja wa benki alivyokuwa akizidi kuyapitia maelezo kwenye ile karatasi
ndivyo mikono yake ilivyokuwa ikizidi kutetemeka. Mwishowe yule meneja wa ile
benki akamaliza kuyapitia maelezo kwenye ile karatasi na kuiweka pale juu ya meza
huku uso wake ukiwa umepoteza utulivu kabisa sambamba na vitone vya jasho jepesi
vikichomoza kwenye paji la uso wake.
“Wewe ni nani?” yule meneja wa benki akajikaza na kumuuliza Koplo Tsega kwa
sauti iliyopwaya.
“Tiglis Tsega,Koplo na Komandoo wa daraja la kwanza,askari wa jeshi la wananchi
wa Tanzania” Koplo Tsega akajitambulisha kwa kujigamba huku akimtazama meneja
wa ile benki kwa udadisi.
“Nani aliyekupa hii barua?” yule meneja wa benki akauliza kwa hofu
“Nahitaji ushirikiano wako vinginevyo nisingetumia hila kufika humu ndani”
Koplo Tsega akaongea kwa utulivu huku akimtazama yule meneja wa benki kwa
makini. Kitambo kifupi cha ukimya kikafuata huku yule meneja wa benki akiachama
mdomo wake kwa mshangao wakati mawazo mengi yakipita kichwani mwake. Sasa
mshtuko alioupata meneja yule ulikuwa dhahiri usoni mwake huku akionekana kama
mtu aliyekuwa akifikiria kukurupuka ghafla na kuanza kutimua mbio ingawa mazingira
yakufanya vile hayakuwepo.
“Ushirikiano upi unaouhitaji kutoka kwangu?’’ baada ya kubabaika kidogo yule
meneja wa benki akajikaza na kuongea kwa sauti ya kupwaya.
“Nafahamu kuwa unatumika na watu wenye mamlaka zaidi juu yako na kutokana
na mazingira uliyonayo huwezi kukataa.Hata hivyo hiyo haimaanishi kuwa hufahamu
kinachoendelea na humfahamu kabisa mtu aliyetoa maagizo haya. Niko tayari
kukulinda wewe na maslahi yako kama utakuwa muwazi na kunipa ushirikiano wa
kutosha katika kumfichua mtu au watu waliopo nyuma ya mtandao huu mchafu”
Koplo Tsega akaongea kwa msisitizo huku macho yamemtoka na mishipa ya shingo
imemtuna hata hivyo kicheko cha mahoka kilichofuata kutoka kwa yule meneja wa
benki kikampelekea ashikwe na butwaa huku akimtazama yule meneja wa benki kama
kituko.
“Binti nadhani umechanganyikiwa bila shaka nani aliyekwambia kuwa mimi
nahitaji ulinzi kutoka kwako na huo mtandao mchafu unaozungumzia mbona
sikuelewi?” yule meneja wa benki akaongea kwa dharau huku akiendelea kuangua
kicheko
“Kwa hiyo unataka niamini kuwa hilo jina la kwenye hii barua siyo lako na hii siyo
benki ya Zanzibar Marine?’’Koplo Tsega akauliza kwa jazba huku akimkata jicho la
hasira yule meneja wa benki.
“Mimi sikatai kuwa Aden Mawala ni jina langu na hii ni benki ya Zanzibar Marine
lakini huu siyo ushahidi tosha wa kunifanya nikubaliane na kile unachokiamini binti.
Jiji hili la Dar es Salaam limejaa matapeli wa kila aina. Mimi ni mtu ninayefahamiana
na watu wengi kutokana na kazi yangu hivyo mtu yeyote mwenye hila mbaya anaweza
kulitumia jina langu kujipatia fedha kwa ujanjaujanja” yule meneja wa benki akajitetea.
“Sikiliza mzee usijaribu kuiondoa hoja yangu ya msingi kwenye mstari. Mimi
sijafika hapa kufuata pesa na wala sina haja na pesa zako badala yake ninachohitaji
kufahamu ni kuwa hizi fedha zilizoandikwa kwenye hii barua ambazo hadi wakati huu
naamini kuwa tayari zimeshaingizwa kwenye benki yako zimetoka kwa nani na ninani
aliyekupa maagizo haya”
“Hakuna pesa yoyote ya kiasi hicho iliyoingia kwenye benki yangu na hata kama
pesa hiyo ingekuwa imeingia taratibu za kibenki haziniruhusu kutoa taarifa za akaunti
ya mhusika kwa mtu mwingine isipokuwa kwa idhini ya mhusika tu” yule meneja wa
benki akaweka kituo huku akiunyanyua mkono wake kuitazama saa yake ya mkononi.
Kuona vile Koplo Tsega akaingiza tena mkono wake mfukoni na kuichukua ile
bahasha ya kaki aliyoipata kule nyumbani kwa Meja Khalid Makame ambayo ndani
yake ilikuwa na hundi nyingi zenye majina ya watu tofauti. Alipoitoa ile bahasha
mfukoni Koplo Tsega akaingiza mkono ndani yake na kuzitoa zile hundi kabla ya
kuzitupia pale mezani karibu na yule mzee meneja wa benki.
“Huwenda huo ukawa ni ushahidi tosha kwako kuwa mimi sijachanganyikiwa
kama unavyodhani na badala yake ninahakika na kile ninachokizungumza.
Ukichunguza kwa utulivu utagundua kuwa majina ya watu yaliyopo kwenye hundi
hizo ndiyo yale pia yaliyopo kwenye ile barua niliyokupa awali hivyo sijakosea njia”
Koplo Tsega akaongea kwa utulivu huku akijitahidi kuidhibiti hasira yake kifuani.
Yule meneja wa benki akainama kwa makini na kuanza kuzichunguza zile hundi pale
mezani huku akionekana kuingiwa na mshtuko kadiri alivyokuwa akimalizia kupitia
hundi moja na kuichukua nyingine. Hata hivyo yule meneja wa benki alikuwa mkaidi
kwani alipomaliza kuzipitia zile hundi akazikusanya kwa pamoja na kuzisogeza karibu
na Koplo Tsega pale mezani.
“Hizi ni taarifa nyepesi sana za kufoji binti na huwezi kunifungamanisha nazo
labda kama unashida nyingine za kibenki mbali na hii nitakusaidia ila kama huna hoja
za msingi utakuwa muungwana sana ukisimama na kuondoka uniache niendelee
na kazi zangu” yule meneja wa benki akaongea kwa dharau huku akiunyanyua tena
mkono wake na kuitazama saa yake mkononi. Koplo Tigls Tsega akazichukua zile
hundi na kuzirudishia kwenye ile bahasha kabla ya kuitia ile bahasha mfukoni pasipo
kuonesha tashwishwi yoyote usoni. Hata hivyo Koplo Tsega alikuwa makini kufuatilia
kwa hila nyendo za meneja yule wa benki hivyo wakati akijitia kuzama katika kuiweka
ile bahasha ya hundi mfukoni mwake alikuwa amemuona yule meneja wa benki jinsi
alivyokuwa akiupeleka mkono wake taratibu kuuvuta mtoto mmoja wa ile meza ya
ofisini.
Akiwa ameshaanza kuhisi nini maana ya tukio lile Koplo Tigils Tsega hakutaka
kusubiri hivyo kwa kasi ya ajabu akaisukuma ile meza ya ofisini kwa miguu yake
kumbana yule meneja wa benki kwenye kiti chake ukutani huku mkono wake mmoja
ukiwa tayari umezama mafichoni kuikamata vyema bastola yake. Yule meneja wa
benki alipotaka kufurukuta mahesabu yake yakagonga mwamba kwani mdomo wa
bastola ya Koplo Tsega ulikuwa tayari ukimtazama usoni. Kisha Koplo Tseakajitetea
karibu na yule meneja wa benki na kuupenyeza mkono wake katika ule mtoto wa
meza uliofunguliwa kwa hila na yule meneja wa benki na alipopapasa papasa bastola
aina ya 22 Caliber Revolver ikaenea vyema kwenye kiganja chake tukio lililompelekea
yule meneja wa benki ashikwe na kihoro baada ya kuona hila yake imeshtukiwa na
kugonga mwamba. Koplo Tsega alipoitoa ile bastola akaichomoa magazini yake na
kuitupa kando kabla ya kugeuka na kumtazama kwa utulivu yule meneja wa benki
ambaye wakati huu alikuwa amebanwa kwenye kile kiti na ile meza yake ya ofisini
huku macho yamemtoka kwa hofu.
“Sura yako inaonekana ni mtu msomi,mkarimu,mtulivu na mzalendo lakini
matendo yako ni ya kinyama kama walivyo wanamtandao wenzako wengine. Watu
kama nyinyi hamtakiwi kuundiwa tume ya uchunguzi huku mkiendelea na kazi kama
ilivyozoeleka badala yake mnastahili kifo cha aibu tena ikiwezekana hadharani ili vizazi
vijavyo visijifunze chochote kutoka kwenu’’Koplo Tsega akaongea kwa utulivu huku
akimzunguka yule meneja wa benki pale kwenye kiti.
“Unajidanganya bure binti hata ukiniua mimi huwezi kufika popote” yule meneja
wa benki akaongea kwa msisitizo huku akihisi kuzidiwa ujanja.
“Maelezo yako yanaonesha kuwa mtandao wenu ni mpana sana na una watu
wengi sana kiasi cha kujipa hakika kuwa hata nikikuua sitofika mbali” Koplo Tsega
akaongea kwa utulivu
“Huelewi unachokizungumza’’ yule meneja wa benki akaongea kwa kujiamini
“Niambie hizi fedha zilizoingia kwenye benki yako zimetoka kwa nani na huo
mtandao wenu unaongozwa na nani?’’
“Nimekwisha kwambia kuwa sifahamu chochote kuhusu hizo hundi wala hiyo
barua uliyokuja nayo. Ndiyo kwanza nimeviona kwako na hakuna kiasi cha pesa kama
hicho kilichoingizwa kwenye benki yangu” yule meneja wa benki akafoka kwa jazba.
“Unadhani ninaweza kukuamini kupitia maneno yako?. Huo ni uongo wa
mwisho usiokuwa na ushawishi niliowahi kuusikia kwa binadamu hapa duniani.
Nahitaji kuiona Cash flow ya hii benki inayoonesha miamala ya pesa zilizoingizwa
na kutolewa” Koplo Tsega akaongea kwa utulivu huku akimtazama yule meneja wa
benki kwa makini na alichokiona mbele yake ni mshtuko mkubwa uliojengeka usoni
kwa yule meneja wa benki.
“Nimekwisha kwambia kuwa taratibu zangu za kazi haziniruhusu kutoa taarifa
za namna hiyo kwa mtu asiyehusika” yule meneja wa benki akasisitiza huku akianza
kutokwa na kijasho chepesi usoni.
“Nahitaji kuona Cash flow statement ya hii benki ndugu Aden Mawala,usinipotezee
muda wangu” Koplo Tsega akasisitiza huku taratibu akikata kipande cha waya wa
simu ya pale mezani,yule meneja wa benki akashindwa kuelewa nini maana ya tukio
lile.
“Unataka kunifanya nini?” yule meneja wa benki akauliza kwa hofu baada ya
kumuona Koplo Tsega akimsogelea pale kwenye kiti na kipande cha waya wa ile simu
mkononi
“Cash flow statement…”
“What…?” yule meneja wa benki kabla hajamaliza kuongea kile kipande cha waya
tayari kilikuwa shingoni mwake na hapo Koplo Tsega akaanza kukikaza taratibu kwa
mikono yake. Yule meneja wa benki kuona vile akaanza kufurukuta katika kutaka
kujinasua huku akitupa mikono na miguu yake huku na kule huku mishipa ya kichwa
ikimchomoza na ulimi na macho vikimtoka. Jitihada zake za kujinasua hazikufua
dafu kwani hapakuwa na nafasi ya kuchomeka mikono yake kwenye ule waya
shingoni na kuuzuia usimkabe. Koplo Tsega akaendelea kuukaza ule waya hadi pale
alipomuona yule meneja wa benki akianza kuishiwa nguvu ndiyo akalegeza taratibu
hali iliyompelekea yule meneja wa benki aanze kukohoa ovyo akiurekebisha mfumo
wa upumuaji wake.
“Fungua kompyuta yako nahitaji kuona Cash flow statement ya hii benki” Koplo
Tsega akanong’ona kwa sauti tulivu sikioni mwa yule meneja wa benki.
“Okay…!” yule meneja wa benki akaitikia kwa shida huku hofu imemshika na
muda mfupi uliyofuata akaifungua ile kompyuta yake ya ofisini pale mezani huku
Koplo Tsega akiwa makini nyuma yake. Ile kompyuta ilipofunguka yule meneja wa
benki huku mikono ikimtetemeka akafungua mafaili kadhaa mle ndani ya kompyuta
hadi alipolifikia faili lenye rekodi za miamala ya pesa zilizoingia na kutoka kwenye ile
benki kufikia mwezi ule.
Kitambo kifupi cha ukimya kikapita mle ndani huku Koplo Tsega akijaribu
kuichunguza taarifa ile kwa maikini. Aliporidhikanayo akamwambia yule meneja wa
benki aiprint.Yule meneja wa benki akasita kidogo lakini macho yake yalipokutana
na macho ya Koplo Tsega hofu ikamuingia tena na hapo akalainika na kufanya vile
alivyoagizwa. Haraka akaiamuru ile kompyuta kuprint ile taarifa ya benki kwenye
printer iliyokuwa juu ya meza ndogo kando ya eneo lile.
Mara baada ya yule meneja wa benki kuprint ile taarifa ya benki Koplo Tsega
haraka akaichukua na kuanza kuipitia katika namna ya kuichunguza kama angeweza
kupata taarifa yoyote ya kumsaidia. Kupitia taarifa ile ya benki Koplo Tsega akagundua
kuwa kulikuwa na miamala mingi iliyofanywa kwenye ile benki kwa kipindi cha miezi
kadhaa iliyopita na alipozidi kuchunguza akagundua kuwa miamala mingi ilikuwa
imefanywa na kampuni nyingi zilizokuwa jijini Dar es Salaam ambazo kwa namna
moja au nyingine hazikupaswa kutiliwa mashaka kutokana na aina ya biashara
kampuni zile zilizokuwa zikifanya. Kulikuwa pia na miamala mingine iliyofanywa na
watu binafsi ambayo fedha zao zilikuwa za kawaida kwa vile benki ile ilikuwa imejikita
kwenye biashara ya uuzaji wa bidhaa nje ya nchi na uingizaji wa bidhaa ndani nchi.
Katika kuendelea kuchunguza Koplo Tsega akajikuta akivutiwa na akaunti moja
ambayo ilikuwa imetumika kufanya muamala wa pesa nyingi sana za kigeni kwa mara
moja. Akaunti ile ilikuwa na jina moja la Zanzibar Stone City Bazaar. Koplo Tsega
alipozidi kuchunguza akagundua kuwa kupitia rekodi zilizokuwa kwenye taarifa ile
ya benki akaunti ile ilikuwa ni mpya kabisa kwani hapakuonekana rekodi nyingine
zilizoonesha kuwa akaunti ile ilikuwa ikitumika huko siku za nyuma. Lilikuwa ni
jambo la kustaajabisha lakini vilevile linaloweza kuaminika.
Koplo Tsega alipozidi kuchunguza mashaka juu ya kile alichokuwa akikihisi
yakazidi kuongezeka. Muamala wa fedha nyingi uliofanywa kupitia akaunti ile ulikuwa
umefanyika siku chache baada ya wao kuondolewa kwenye ile tume ya udhibiti na
upambanaji wa biashara ya dawa za kulevya nchini na hatimaye kuingizwa kwenye
vikosi vya kijeshi vya kuimarisha amani ya kudumu-MONUSCO nchini jamhuri ya
kidemokrasia ya nchi ya Kongo. Lakini vile vile jina la akaunti ile lilifanana na jina
la akaunti iliyokuwa kwenye zile hundi alizozipata kule nyumbani kwa Meja Khalidi
Makame. Kwa sekunde kadhaa Koplo Tsega akajikuta ameganda kama nyamafu
huku akiendelea kuikodolea macho taarifa ile ya benki kwenye ile karatasi na mkono
wake mmoja ukiwa umeikamata bastola yake vyema mkononi na kuielekezea kifuani
kwa yule meneja wa benki ambaye mashaka yalionekana dhahiri usoni mwake.
“Nahitaji bank statement ya hii akaunti” Koplo Tsega akasogea karibu na
kumwambia yule meneja wa benki huku akimuelekeza kwa kidole chake kwenye ile
akaunti ya benki ya Zanzibar Stone City Bazaar. Yule meneja wa benki akaikodolea
macho ile akaunti kabla ya kusita huku akigeuka na kumtazama Koplo Tsega kwa
mashaka.
“Print…” Koplo Tsega akaongea kwa utulivu huku akifanya ishara ya kichwa
kumaanisha kile alichokuwa akikisema kisha akaihamisha bastola yake kichwani kwa
yule meneja wa benki. Yule meneja wa benki kuona vile akainama tena kwenye ile
kompyuta yake mezani na kuanza kushughulika nayo na baada ya muda mfupi ile
kompyuta ikaanza kuprint ile Bank statement ya akaunti ya Zanzibar Stone City Bazaar
ikionyesha kiasi cha pesa,mwaka,mwezi,siku,saa na tarehe ambayo muamala ule wa
fedha nyingi kwenye ile akaunti ulikuwa umefanyika.
Jambo moja la kushangaza ni kuwa fedha zilizoingizwa kwenye akaunti ile
zilionekana kuwa zilikuwa zimetokea kwenye benki mama iliyokuwa kisiwani
Zanzibar. Koplo Tsega akaendelea kuikodolea macho akaunti ile huku akishindwa
kuamini kile kilichokuwa kwenye ile karatasi.
“Kiongozi wa mtandao wenu anaitwa nani?’’ Koplo Tsega akavunja ukimya
akimuuliza yule meneja wa benki hata hivyo yule meneja wa benki hakuzungumza
neno badala yake akatikisa kichwa chake kuonesha kuwa alikuwa hafahamu chochote.
“Kukaa kimya haitakusaidia kitu ndugu Aden Mawala kwani ni vizuri ukawa
muwazi na kunieleza ni nani anayehusika na ugawaji wa mamilioni ya fedha nyingi
kiasi hiki huku akisisitiza mambo yenu yafanyike kwa usiri mkubwa’’
“Nimekwisha kukueleza kuwa mimi sifahamu chochote” yule meneja wa benki
akasisitiza hata hivyo kabla hajamaliza risasi moja kutoka kwenye bastola ya Koplo
Tsega yenye kiwambo cha kuzuia sauti ikapenya na kuuvunja mfupa wa paja lake.
Yule meneja wa benki akapiga yowe kali la maumivu huku akigugumia kwa maumivu
makali yaliyoambatana na jeraha linalovuja damu.
“Niambie Aden ni nani anayehusika na fedha hizi?” Koplo Tsega akauliza
“White…’’
“White ndiyo nani?” Koplo Tsega akauliza kwa shauku
“White Sugar…!” yule meneja wa benki akaongea huku akilalama kwa maumivu
makali ya jeraha la risasi pajani mwake.
“Niambie,huyo White Sugar ndiyo nani?’’ Koplo Tsega akauliza kwa utulivu.
“Meneja wa Zanzibar Stone City Bazaar”
“Anaishi wapi?’’
“Sifahamu na wala sijawahi kuonana naye” yule meneja wa benki akajitetea lakini
kitendo cha kumuona Koplo Tsega akiunyoosha mkono na kuelekezea bastola yake
kwenye paja la mguu wake mwingine akaingiwa na hofu.
“Duka lake lipo ndani ya Mlimani City Shopping Mall linatazamana na duka
kubwa la vinyago la African art craft” yule meneja wa benki akafafanua hata hivyo
mduwao mwingine ukamshika wakati alipouona mdomo wa ile bastola ya Koplo
Tsega ukielekezewa kwenye kifua chake.
“Tafadhali usiniue...!”
“Sikuui Aden nakupumzisha tu!’’ kabla yule meneja wa benki hajaongea neno
risasi mbili za bastola ya Koplo Tsega zikapenya kifuani mwake na kutengeneza
matundu makubwa mawili yanayovuja damu kwenye moyo na hapo yule meneja wa
benki akatikisika kidogo kwenye kile kiti chake cha ofisini kabla ya kutulia huku roho
yake ikiwa mbali na mwili.
Koplo Tsega hakutaka kuendelea kupoteza muda hivyo akaingiza mkono
mfukoni na kuchukua pipi ya kijiti na kuimenya kabla ya kuitia mdomoni. Kisha
haraka akachukua kilicho chake mle ndani na kuelekea kwenye mlango wa ile
ofisi. Alipoufungua mlango wa ile ofisi na kutoka nje pale mlangoni akakutana na
mwanaume mmoja aliyekuwa akielekea kwenye ile ofisi ya meneja wa benki.
“Subiri kidogo kuna mtu anazungumza na meneja” Koplo Tsega akamwambia
yule mwanaume wakati akipishananaye kwenye ile korido.
“Sawa!” yule mwanaume akaitikia huku akigeuza na kurudi kule alipotoka. Muda
mfupi uliofuata Koplo Tsega alikuwa akikatisha kando ya lile dawati la idara ya
huduma kwa wateja. Yule dada mlimbwende mfanyakazi wa idara ile alipomuona
Koplo Tsega akatabasamu na kumuuliza
“Vipi amekusikiliza haja yako?”
“Ndiyo nashukuru sana dada kwani amekwisha nielekeza cha kufanya. Nitarudi
tena mapema sana baada ya kukamilisha taratibu zote” Koplo Tsega akajinadi kwa
hila huku akijifanya ni mwenye haraka.
“Karibu tena”
“Ahsante na kazi njema” Koplo Tsega akashukuru na kuaga huku akielekea
kwenye mlango mkubwa wa kioo mbele ya lile jengo la benki ya Zanzibar Marine.
Alipofika akausukuma ule mlango na kutokomea nje huku macho ya yule dada
mlimbwende wa idara ya huduma kwa mteja yakimsindikiza kwa nyuma.