INGAWA MUDA ULIKUWA UMEENDA SANA lakini kwa
M.D.Kunzugala,mkurugenzi mkuu wa usalama wa taifa suala lile halikuwa na
maana yoyote kwake kwani asingeweza kurudi nyumbani kwake na kupumzika
huku bado akiwa hajaona mafanikio yoyote katika kazi yake.
M.D.Kunzugala wakati huu alikuwa amejiegemeza kwenye kiti chake cha ofisini
chenye foronya laini huku chupa tupu kubwa ya maji ya kunywa na bilauri vikimtazama
mezani mbele yake. Chupa ya nne ya maji ilikuwa mbioni kuteketea mwilini mwake
kitu ambacho hakikuwa cha kawaida tangu alipoteuliwa na rais kushika wadhifa huu.
Kwa muda wa masaa matatu yaliyopita simu nyingi zilikuwa zimemiminika ofisini
kwake kutoka kwa watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali na vijana wake wa
kazi. Watu hao wakidodosa juu ya mafanikio yaliyokuwa yamefikiwa katika kazi yake
na wengine wakitoa ripoti kwake juu ya wapi walipokuwa wamefikia katika harakati za
kumnasa yule mtu aliyewatoroka maafisa wake chini ya jengo la ghorofa lililopo eneo
la posta kuu jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo hadi kufikia wakati huu bado alikuwa hajapokea hata simu moja
ya kuashiria kuwa kulikuwa na mwelekeo wa matumaini hali iliyompelekea mara
kwa mara aizime na kuiwasha simu yake ya mezani kwa kuhofia kuwa simu hiyo
ingempelekea ugonjwa mpya wa msukumo mkubwa wa damu mwilini.
Sulle Kiganga alikuwa bado akiongoza vijana wake kufanya msako makini katika
kona zote za jiji la Dar es Saalam katika kuhakikisha kuwa yule mtu aliyewatoroka
kwenye lile jengo la ghorofa anapatika haraka kabla hajaendelea kuendeleza maafa
zaidi. Hata hivyo uchunguzi kutoka kwa kamati yake ya usalama iliyokuwa ikiongozwa
na Sulle Kiganja ulikuwa umemletea majibu yenye kumshangaza na kuziyumbisha
vibaya fikra zake. Uchunguzi huo ulikuwa ukieleza kuwa yule mtu aliyewatoroka
maafisa wake kwenye lile jengo la ghorofa lililopo eneo la posta mchana ule alikuwa ni
komandoo na askari wa jeshi la wananchi wa Tanzania aliyeacha kazi miezi michache
iliyopita akifahamika kwa jina la Chaz Siga. Hivyo kitendo cha kufahamu kuwa mtu
waliyekuwa wakishughulikanaye alikuwa ni askari komandoo kilikuwa kimezidi
kuzamisha matumaini yake ya kumtia mikononi kiulaini.
Pia kulikuwa na taarifa nyingine zilizozidi kumtia mashaka. Taarifa hizo
zikitanabaisha kuwa shambulizi dhidi ya afisa wake mmoja wa usalama aliyeuwawa
kwa risasi kwenye lile jengo la ghorofa la posta akifahamika kwa jina la Balimenya
lilikuwa limetokana na risasi kutoka kwa mtu mwingine na siyo Chaz Siga.
Dhana hiyo ikawa imeongeza hisia nyingine mbaya kwa M.D Kunzugala kuwa
adui hakuwa mmoja kama yeye na wanausalama wenzake walivyodhani hapo awali na
hali hiyo ikawa imeongeza hisia nyingine tofauti katika kushughulika na matukio ya
mauaji yaliyokuwa yakiendelea jijini Dar es Salaam.
Saa ya ukutani ofisini kwake ilikuwa ikionesha kuwa ilikuwa ikielekea kutimia saa
tano usiku na kupitia madirisha ya vioo vya ofisini kwake katika jengo lile la ghorofa
M.D.Kunzugala aliweza kuyaona manyunyu ya mvua nyepesi iliyokuwa ikiendelea
kunyesha. Bado alikuwa kazini kusubiri ripoti kutoka kwa watendaji wake waliokuwa
mitaani kumsaka Chaz Siga na mtu mwingine aliyeshukiwa kufanya shambulizi la kifo
dhidi ya afisa wake wa usalama.
__________
TEKSI NILIYOIKODI ILINISHUSHA NYUMA YA JENGO LA Barracuda
Plaza mtaa wa tatu kabla ya sehemu lilipokuwa kanisa kubwa la The Last Days
Gospel Ministry . Kwa kuwa mvua ilikuwa imeanza kunyesha tena ikanibidi nitembee
kandokando ya baraza za majengo marefu ya ghorofa ya eneo lile la posta ili kujikinga
na manyunyu hayo.
Nilikuwa na hakika kuwa bado nilikuwa nikitafutwa na wale watu walionikimbiza
mchana uliopita. Hivyo wakati huu nilikuwa makini zaidi na nyendo zangu kwa
kuchunguza magari na watu wote niliyokuwa nikipishana nao barabarani.
Nilikuwa nimemaliza kikao cha siri cha masaa matatu na mzee James Risasi
katika hoteli moja iliyopo eneo la Magomeni nikimpa ripoti ya harakati zangu hadi
pale nilipofikia. Mzee James Risasi alikuwa ameipokea ripoti yangu na kuridhishwa na
hatua niliyokuwa nimefikia katika harakati zangu.
Mbali na hayo mzee James Risasi alikuwa amenipa mrejesho juu ya kile
kilichokuwa kikiendelea baada ya mkutano wa maafisa usalama uliyofanyika alfajiri
ile huku akinitahadharisha juu ya hatua zilizokuwa zimechukuliwa. Mzee James Risasi
akaendelea kunieleza kuwa tayari taarifa zangu zilikuwa zimeifikia ofisi kuu ya idara
ya usalama wa taifa na idara hiyo ilikuwa imejipanga vizuri na maafisa wake katika
kuhakikisha kuwa ninakamatwa mapema iwezekanavyo. Nilikuwa nimejipanga vizuri
na kamwe sikutaka kutoa nafasi kwa adui zangu.
Nilimaliza kuipita barabara ya mtaa wa kwanza kisha nikaingia barabara ya mtaa
wa pili na nilipoingia barabara ya mtaa wa tatu nikakumbuka kuitazama saa yangu
ya mkononi na hapo nikagundua kuwa zilikuwa zimesalia dakika chache kufika saa
sita usiku. Njiani nilipishana na jozi tofautia za wapenzi waliokuwa wakitoka kwenye
kumbi za starehe na walevi waliokuwa wakiyumba ovyo barabarani.
Nililipita jengo la benki ya maendeleo ya Afrika na nilipomaliza kuipita ofisi
ya magazeti upande wa kushoto nikaliona kanisa la The Last Days Gospel Ministry.
Niliyatazama mandhari ya kanisa lile na sehemu ya wazi ya kanisa lile upande wa
kushoto nikaliona gari moja dogo aina ya Toyota Starlet nyeupe. Kuliona gari lile
nje ya kanisa kukanipa matumaini kuwa mtu niliyekuwa nikimhitaji alikuwa bado
hajaondoka.
Niligeuka nyuma kuchunguza kama kulikuwa na mtu yeyote aliyekuwa akiniufatilia
na nilipoona hali bado ilikuwa shwari nikasubiri gari moja lililokuwa likija mbele yangu
lipite kisha nikavuka barabara na kuelekea kwenye lile kanisa. Nilitembea kwa utulivu
na wakati nikikaribia eneo lile nikagundua kuwa taa za ndani ya kanisa lile zilikuwa
zikiwaka. Hatimaye niliufikia mlango wa kuingia kwenye kanisa lile na kuusukuma
ndani huku nikivikagua vivuli vya miti ya mikungu vilivyokuwa nje ya kanisa lile.
Mara baada ya kuingia ndani ya kanisa lile kwa utulivu nikaurudishia ule mlango
nyuma yangu. Huwenda uwepo wangu mle ndani ya kanisa ulinifanya nijihisi kuwa
ni mwenye dhambi nyingi kwani sikuweza kukumbuka kuwa kwa mara yangu ya
mwisho kuhudhuria ibada kanisani ilikuwa lini. Viongozi wa dini ambao husema
binadamu humkumbuka Mungu nyakati za shida huwenda hawakuwa wamekosea
kwani kama isingekuwa shida sina hakika kama ningekuwa eneo lile.
Mara baada ya kuingia mle ndani nikasimama kidogo huku nikiyatazama kwa
utulivu mabenchi mengi ya kanisa yaliyopangwa katika pande mbili kushoto na kulia
yakiacha nafasi ya kupita katikati. Wakati huu mabenchi yale hayakuwa na mtu hata
mmoja na hivyo kupelekea kanisa lote litawaliwe na ukimya wa aina yake.
Kupitia madirisha makubwa ya kanisa lile ambayo baadhi yalikuwa wazi niliweza
kuyaona mapazia mepesi yakipepea kutokana na upepo hafifu uliosababishwa na
mvua iliyokuwa ikinyesha nje na upepo ule sasa ulikuwa ukiisukasuka mishumaa
michache iliyokuwa ikiwaka mbele ya madhabahu ya kanisa lile.
“Karibu sana kijana” sauti tulivu ya kizee ilisikika kutoka mbele ya madhabahu ya
kanisa lile na hapo nikashtuka kuwa kumbe mle ndani sikuwa peke yangu.
“Ahsante!” niliitikia pasipo kumuona yule mtu aliyenikaribisha huku nikianza
kutembea taratibu nikielekea mbele ya kanisa lile na baada ya kuyatembeza macho
yangu kule mbele ya kanisa nikamuona mzee mmoja akiwa ameketi kwenye kiti
nyuma ya meza fupi iliyofunikwa kwa vitambaa vyeupe vyenye alama za misalaba
iliyodariziwa vizuri huku akiwa amevaa mavazi meupe. Nilipomchunguza vizuri mzee
yule nikatambua kuwa umri wake ulikuwa ni miaka sabini na ushei. Mzee yule alikuwa
amejiegemeza vizuri kwenye kiti chake cha utukufu huku mikono yake ikiwa imeshika
Biblia ambayo haraka aliwahi kuiweka mezani baada ya kuniona.
“Shikamoo mzee!” nikamsalimia yule mzee
“Marahaba kijana karibu sana!” mzee yule akaniitikia huku akinitazama kwa
shauku.
“Ahsante sana” nikamwitikia huku nikitafuta nafasi nzuri kwenye benchi la mbele
la kanisa lile na kuketi. Yule mzee aliupisha utulivu kidogo huku akinitazama hadi
pale nilipoketi na yeye ndiyo akasimama na kuanza kutembea akija pale nilipokuwa
nimeketi. Yule mzee mchungaji wa kanisa lile aliponifikia pale nilipoketi nikasimama
na kusalimiana naye kisha wote tukaketi. Hata hivyo aliendelea kunitazama kwa
utulivu na hapo nikajua kuwa bila shaka alikuwa ameshangazwa na ugeni wangu.
“Jina langu naitwa Chaz Siga”
“Pastor Romanus Mugonzibwa” yule mzee akajitambulisha huku akinitazama
kwa makini kisha akaitoa miwani yake usoni na kufikicha macho yake kidogo na
alipomaliza akairudishia ile miwani yake machoni na kuongea
“Karibu sana nyumbani kwa Bwana”
“Nina shida Pastor au labda nisema nahitaji elimu ya kiroho” maelezo yangu
yakampelekea Pastor Romanus atabasamu kidogo na kupelekea makunyanzi ya uzee
yazidi kujitokeza usoni mwake.
“Umefanya jambo jema kuja kanisani kwani ni vijana wachache wa zama hizi
wanaoenda kwenye nyumba za ibada kutafuta elimu ya kiroho” Pastor Romanus
akakohoa kidogo kusafisha koo lake kisha akaniuliza.
“Shida gani kijana?”
“Nahitaji kufahamu kama kuna uhusiano wowote wa mambo ya kiroho na namba
666” niliongea kwa utulivu huku nikimtazama Pastor Romanus. Kilichonipelekea
kufika kwenye kanisa hili ni umaarufu alikuwanao Pastor Romanus katika kufafanua
masuala mbalimbali ya kiroho. Siku fulani za huko nyuma vipindi vyake vya ufafanuzi
wa masuala mbalimbali ya kiroho vilikuwa vikirushwa hewani na vyombo mbalimbali
vya habari vya jijini Dar es Saalm na hivyo kumjengea umaarufu mkubwa. Pastor
Romanus akanitazama kama aliyeshangazwa na shida yangu au pengine lile halikuwa
swali alilolitarajia kutoka kwangu.
“Hiyo ni namba ya chapa ya mnyama” Pastor Romanus akaongea kwa utulivu
akiweka kituo kisha akaendelea
“Kama wewe ni msomaji mzuri wa maandiko matakatifu ya Biblia huwenda
ukafahamu ninachozungumza” Pastor Romanus akaongea huku akionekana
kutafakari kisha akaniambia kwa utulivu
“Hebu subiri kidogo” kisha nikamuona Pastor Romanus akisimama na kuanza
kutembea kizeezee akielekea kwenye ile madhabahu ya kanisa na muda mfupi
iliofuata nikamuona akipotelea kwenye mlango fulani uliokuwa upande wa kushoto
wa madhabahu ile.
Niliendelea kuketi pale kwenye benchi huku nikimsubiri Pastor Romanus na
baada ya kitambo kirefu mara nikamuona akirejea na kitabu fulani kikubwa mikononi
ambacho hapo awali sikuwahi kukiona katika harakati zangu. Nilikitazama kitabu
kile mikononi mwake huku nikishangazwa na ukubwa wake. Kurasa za kitabu kile
zilikuwa chakavu mno zikiashiria kuwa kitabu kile kilikuwa kimetumika kwa miaka
mingi.
Pastor Romanus akaja na kuketi kando yangu kisha akafunua kurasa kadhaa za
kile kitabu na kuweka kituo akiyapitia maelezo fulani kama anayetafakari baadaye
nilimuona akigeuka na kunitazama.
Kwenye maandiko ya Textus receptus katika agano jipya la Biblia kitabu cha Ufunuo
wa Yohana 13:16-18 maandiko yanaihusisha namba 666 na chapa ya mnyama ama
The Beast ambaye ndiye shetani. Namba hii imeanza kusambazwa na inaendelea
kusambazwa kwa vizazi vya dunia hii vinavyoshikama na matendo ya kishetani. Lengo
kubwa hasa ni shetani kuhakikisha kuwa anaongeza idadi ya binadamu wengi zaidi
katika ufalme wake ambao atahukumiwa nao wakati utakapofika” Pastor Romanus
aliweka kituo na kukohoa kidogo na hapo nikapata swali la kumuuliza
“Kwa hiyo hao washirika wa shetani ni lazima wawe na hii chapa 666?”
“Ni utambulisho kwa watu wake ingawa maandiko yanaeleza kuwa mara baada
ya unyakuo wa wacha Mungu kufanyika chapa hii 666 itaingia kwenye matumizi
rasmi kwa walioachwa kwenye unyakuo huo ambao ndiyo washirika wa huyo shetani.
Watu hao watakaoachwa baada ya unyakuo huo ambao ni watu wa aina zote;wadogo
kwa wakubwa,matajiri kwa maskini,watumwa na walio huru watatiwa chapa katika
mikono yao ya kuume au katika vipaji vya nyuso zao ili kwamba mtu yeyote asiweze
kununua wala kuuza isipokuwa mwenye chapa hiyo tu”
“Kwa nini itakuwa hivyo?” nikamuuliza Pastor Romanus kwa utulivu.
“Maandiko yatimie lakini vilevile tambua kuwa mara baada ya unyakuo huo
wapo baadhi ya binadamu watakaoachwa ambao watashtukia kuwa wamedanganywa
na shetani. Sasa kitu kitakachowaokoa watu wa namna hiyo ni kuhakikisha kuwa
hawatiwi chapa ya huyu mnyama jambo ambalo naweza kusema siyo rahisi hata kwa
kulisikia” Pastor Romanus akaweka kituo na kuyapeleka macho yake tena kwenye
kile kitabu na hapo nikapata nafasi ya kutafakari huku nikiyakumbuka mambo yote
niliyoyaona ndani ya ule mlango mweusi kwenye lile jengo la ghorofa lililopo eneo la
posta jijini Dar es Salaam.
Mvua bado ilikuwa ikiendelea kunyesha na kwa mbali niliisikia ikianguka kwenye
paa la kanisa lile huku upepo uliokuwa ukipenya kupitia madirishani ukiendelea
kuisukasuka ile mishumaa iliyokuwa ikiwaka pale madhabahuni mle kanisani.
“Huu ulimwengu sasa unaelekea wapi?” nikajiuliza huku nikitafakari na hapo
Pastor Romanus akageuka na kunitazama kwa udadisi.
“Huu ndiyo muda wa binadamu kutubu na kuacha dhambi wakimkimbilia
Mungu kwani baada ya hapa hakutakuwa na neema hii” Pastor Romanus akaongea
kwa masikitiko huku akionekana kufikiria jambo kisha akaendelea.
“Watu wa zama hizi hawamwogopi Mungu kabisa na ndiyo maana unaweza
kuwasikia baadhi ya wasanii,wanasiasa na wanamichezo wakijinadi kuwa eti wao ni
marafiki wa shetani lakini hawafahamu kuwa shetani huwa hana urafiki na kiumbe
chochote cha Mungu”
“Kwa hiyo wale watu wasiokuwa na hiyo chapa 666 ya mnyama wapo salama?”
nikauliza kwa udadisi.
“Hapana!” Pastor Romanus akaongea kwa msisitizo ”Kwanza ni lazima ufahamu
kuwa hii chapa ya mnyama ninayoizungumzia hapa siyo lazima sana ukaiona kwa
macho ikiwa imeandikwa katika hizo sehemu za miili ya wanadamu nilizozitaja hapo
awali. Lakini ukichunguza utagundua kuwa mfumo wa namna hii tayari umeanza
kutumika katika baadhi ya nchi zilizoendelea kiuchumi na baadaye mfumo huu
utasambaa dunia nzima.
Kwa mfano katika chapisho la mwandishi mmoja anayeitwa Mac Slavo wa huko
nchini Marekani amezungumzia vizuri juu ya seli ndogo zilizoanza kupandikizwa
katika miili ya binadamu huko Marekani. Teknolojia iitwayo Human-implanted microships
ambayo kwa siku za usoni itakuwa siyo jambo la kushangaza tena hapa duniani.
Ingawa maendeleo ya teknolojia katika dunia ya sasa siyo jambo la kupinga kwani
ni utabili wa maneno ya Mungu hata hivyo ni vizuri kuwa na maarifa ya kuweza
kuelewa kama maendeleo hayo yanavunja taratibu za Mungu au yapo katika makusudi
yake.
Watafiti wa maandiko matakatifu wanasema kuwa dunia hii tuliyonayo inaelekea
kwenye mfumo wa kishetani uitwao New World Order ambapo chapa 666 inatoa ishara
tosha katika utimilifu wa mifumo yote ya maisha ya binadamu ambayo imetengana na
Mungu na vilevile ipo kwenye nguvu ya msukumo mkubwa wa shetani na washirika
wake” Pastor Romanus akaweka kituo na kukohoa kidogo akilisafisha koo lake na
hapo nikageuka na kumtazama huku nikiendelea kuyatafakari maelezo yake. Kwa
kweli bado nilikuwa bado sijamuelewa vizuri.
“New World Order ni nini?” hatimaye nikamuuliza kwa udadisi.
“New world order ni Conspiracy theory au mikakati ya siri iliyoandaliwa kwa usiri
mkubwa na jamii ya wapinga Mungu na watu wenye nguvu kubwa za kishetani
ambao lengo lao kuu ni kuitawala dunia hii kwa kusimamisha utawala wa dunia
wenye serikali moja ambayo haitokuwa na uvumilivu kwa watu au vikundi vyovyote
vya watu watakaokuwa na mtazamo tofauti na wao au utawala wa kidikteta katika
sehemu zote za mfumo wa binadamu Authoritarian world government. Hivyo mataifa
yote huru ya dunia hii ama Sovereign nation-states yatamezwa na mfumo huu” Pastor
Romanus akatulia kidogo akiutumia wakati ule kuyapitia maelezo fulani kwenye kile
kitabu chake na mara hii nikajisikia faraja kuwa nilikuwa sijapoteza muda wangu kuja
pale na kutafuta msaada wake” Baada ya kitambo kifupi cha ukimya Pastor Romanus
akavunja ukimya na kuendelea.
“Mapema sana kabla ya miaka ya 1990 nadharia ya mkakati wa siri wa New World
Order ilikuwa ikifuatwa na makundi mawili makubwa ya huko Marekani. Kundi la
kwanza lilikuwa ni lile lililokuwa likipinga sheria za serikali ama Militantly anti-government
right na kundi la pili lilikuwa ni lile la Fundamentalist christianity ama kundi la wakristo
wenye msimamo mkali. Lakini sasa hata wewe ni shahidi kuwa huu msimamo mkali
unaendelea kuenea kwa kasi hata katika baadhi ya imani nyingine duniani”
“Kwa kweli nilikuwa sifahamu kabisa kuhusu haya mambo” nikaongea kwa
utulivu huku nikitafakari.
“Bado naendelea kutoa elimu hii kwa sababu watu wengi bado hawaelewi kile
kinachoendelea. Hata hivyo kizazi hiki ni kizazi cha ukaidi na hakina tofauti kabisa na
kizazi cha Nuhu. Muda uliobaki ni mfupi sana kuliko unavyodhani kabla ya mambo
haya kutimia. Amani inayoendelea kumomonyoka katika maeneo mbalimbali ya hapa
duniani ni ishara tosha.
Bado kuna mifano mingi ya kukuthibitishia juu ya hiki ninachokizingumza. Mifano
mizuri ya hizo Conspiracy theories ni ule wa End Time Conspiracy theory iliyoandikwa
na John Nelson Darby ikielezea nadharia ya New World Order kwa kuchambua vizuri
maandiko matakatifu kutoka katika vitabu vya Biblia kama kitabu cha Ezekieli,kitabu
cha Danieli na kile cha Ufunuo wa Yohana ambapo vimeelezea kwa kina kuwa watu
wengi wamemkana Mungu na kumkimbilia shetani ili wapate utajiri na nguvu za
kishetani zenye utatu usiyo wa kitakatifu. Utatu unaoundwa na shetani,mpinga kristo
na mitume wa uongo walioenea kila kona ambao lengo lao kuu bado ni lilelile la
kuitawala dunia kwa misingi ya kishetani.
Conspirancy theory nyingine ni ile ya jumuiya ya freemasonry iliyoanzishwa mwishoni
mwa karne ya 16 na mapema sana mwanzoni mwa karne ya 17. Kwa muda wa miaka
mingi jamii hii yenye mikakati ya siri ya kuitawala dunia kinyume na mipango ya
Mungu imekuwa ikishutumiwa kwa kuingiza ajenda za kisiasa katika serikali za hapa
duniani ile hatimaye dunia itawalike kwa kufuata misingi yao.
Katika miaka ya 1890 mwandishi wa kifaransa akifahamika kwa jina la Léo Taxil
aliandika msururu wa machapisho na vitabu vinavyoelezea freemasonry kama jamii ya
kishetani ikizituhumu nyumba zao za kulala wageni au Lodges kuwa zilikuwa zikitumika
kumuabudu lusifa ambaye ndiye shetani kuwa ndiye mwenye nguvu na mamlaka yote
na ndiye mjenzi mkuu wa hii dunia.
Conspiracy theory nyingine ni ile ya illuminati ambayo ni jamii nyingine yenye
mikakati ya kisiri iliyoanzishwa na profesa wa chuo kikuu akifahamika kwa jina
Adam Weishaupt tarehe moja mwezi wa tano mwaka 1776 katika eneo la Upper
Bavaria huko nchini Ujerumani. Misingi ya jamii hii ni kuamini katika uhuru wa
mawazo,liberalism,republicanism,secularism na usawa wa kijinsia huku akiwa amepata
elimu hiyo kutoka kwenye Lodges za freemasonry vitu ambavyo ni tofauti kabisa na
misingi ya Mungu.
Conspiracy theory nyingine ni ile ya itifaki ya kiyahudi ifahamikayo kwa jina la The
Protocols of the Elders of Zion iliyoandikwa nchini Urusi mwaka 1903 ikiwa na misingi
ileile ya kuitawala dunia. Vidokezo kutoka kwenye mkutano ya siri wa cabal wa baadhi
ya viongozi wa kiyahudi ambao waliamua kushirikiana na jamii ya freemasonry katika
kupanga mipango kwa niaba ya wayahudi kuitawala dunia kwa kuamini kuwa wao
ndiyo waliochaguliwa na Mungu.
Kwenye Conspirancy theory nyingine ni ile ya Round Table iliyoanzishwa kwenye
karne ya mfumo wa Imperialism katikati ya mwaka 1815 na mwaka 1914 na mzungu
mmoja aliyezaliwa Afrika ya kusini,mfanyabiashara,mchimba madini na mwanasiasa
akifahamika kwa jina la Cecil Rhodes ambapo alitengeza mkakati wa kuifanya dola ya
Uingereza kuunda serikali yenye utawala wa shirikisho ambayo itakuwa na nguvu na
kuimiliki amani ya dunia.
Katika muswada wake ulioandikwa mwaka 1877 akiwa na umri wa miaka 23 tu
Cecil Rhodes alieleza kuwa alikuwa amenuia kuimwagia pesa jamii ya siri au Secret Society
inayojulikana kama Society of the Elect ambayo ndiyo ingetekeleza malengo yake. Mwaka
1902 gazeti la New York Times liliandika kwamba kufuatia muswada wake wa mwaka
1877,Cecil Rhodes katika mwaka 1890 alitia msisitizo wa muswada wake huku akisisitiza
kuwa malengo ya jamii ya siri ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na mkakati wa taratibu
wa kushikilia utajiri wote wa dunia.
Open conspiracy theory ya mwaka 1928 iliyoandikwa na mwandishi wa Uingereza
na mwanamitazamo maarufu aitwaye H.G.Wells. Yeye aliupa nguvu na msukumo
mkubwa mfumo wa Cosmopolitanism kisha akatoa mwongozo wa mapinduzi ya dunia
na mhimili wa dunia kwa kuanzisha dunia yenye utawala wa teknolojia ya viwango vya
juu na mipango ya kiuchumi ambapo dhana hiyo ameilezea vizuri katika kitabu chake
cha mwaka 1940 kiitwacho The New World Order” Pastor Romanus akaweka kituo
kama anayetafakari na hapo nikaweka kituo nikimtazama kwa makini na kushangazwa
sana na utashi wake katika masuala yale yaliyofichika.
“Cosmopolitanism ni nini?” nilimuuliza.
“Cosmopolitanism ni nadharia ambayo inasema kuwa matabaka ya jamii zote duniani
yanatokana na jamii moja” Pastor Romanus akanijibu huku akinitazama na hapo
nikatikisa kichwa kumuonesha kuwa nimemuelewa na baada ya kukohoa kidogo
akaendelea
“Conspiracy theory nyingine ni ile ya Population Control. Wanatheolojia wa nadharia
hii wanaamini katika New World Order ambayo itaingizwa katika mfumo wa maisha
ya binadamu kwa kudhibiti ongezeko la idadi ya watu duniani ili iwe rahisi kwao
kusimamia na kudhibiti harakati za mtu mmoja mmoja. Hii ni tofauti na mipango
ya Mungu kwani ukisoma katika kitabu cha Mwanzo 1:28 ambapo Mungu anawataka
binadamu wazaane na kuongezeka hapa duniani.
Kwa mujibu wa maelezo ya nadharia hii ni kuwa udhibiti wa ongezeko la idadi ya
watu utafanyika kupitia afya ya uzazi ambapo mikakati ya uzazi wa mpango ambayo
itawafanya watu wasizaane,watumie vidonge vya kuzuia mimba au utoaji wa mimba
au kupungua idadi kubwa ya watu duniani kwa majanga ya mara moja mfano mauaji
ya kimbari kwa kuanzisha vita visivyo na sababu za msingi. Kueneza magonjwa
hatari ya kuambukiza yasiyokuwa na tiba au pengine tiba zake ni za gharama sana au
kusababisha majanga ya mazingira kwa kuwa na mfumo wa kudhibiti hali ya hewa“
Pastor Romanus akaweka kituo kisha akakohoa kidogo na kunitazama kabla ya
kuendelea
“Mind Control ni conspiracy theory nyingine ambapo jamii inaituhumu
serikali,mashirikisho na vyombo vya habari kwa kuwa mstari wa mbele katika
kuhakikisha kuwa kunakuwa na aina fulani ya umoja usiokuwa na maana kwa watu
wake na kupandikiza utamaduni wa kuogopa utawala ambao utapelekea jamii ya
kishetani iendelee kushikilia madaraka ya serikali na hivyo mfumo wa New Word Order
kujiingiza kirahisi duniani” Pastor Romanus akaweka kituo kidogo na kunitazama
kisha akaniambia
“Kijana!,pengine ukaona kama ninayekupotezea muda wako mwingi kwa
kukueleza haya yote lakini nafanya hivi kwa sababu maelezo haya ni sehemu ya majibu
ya swali lako”
“Ondoa shaka Pastor mimi nipo tayari kukusikiliza” nikaongea kwa utulivu na
hapo Pastor Romanus akatabasamu kidogo na kuyapelekea mapengo yake mawili
yaonekane vizuri bila kificho kisha tabasamu lake lilipofifia na kutoweka akaendekea
“Conspiracy theory nyingine ni ile ya Mass Survaillance. Katika nadharia hii
wanatheolojia wanaamini kuwa utawala wa New Word Order umeanza kuingizwa
duniani au utaingizwa kupitia mapinduzi makubwa ya akili za binadamu katika
masuala ya teknolojia ambayo matumizi yake yanaunganisha jamii kubwa ya watu.
Kwa mfano utumiaji wa teknolojia ya Barcode katika bidhaa za viwandani. Alama
fulani katika bidhaa zinazotumika au kusambazwa duniani mfano teknolojia ya RFID
tagging inayotumia seli ndogo zilizopandwa kwenye bidhaa. Matumizi ya mifumo
ya mikusanyiko ya taarifa mbalimbali za watu ama Database systems katika maeneo
mbalimbali” Pastor Romanus akaweka kituo tena na kunitazama kama aliyetaka
kupata hakika kuwa nilikuwa nikimsikiliza au lah!. Kitendo cha kuniona nikimtazama
kikampelekea aendelee na mada yake.
“Coup d’état ni conspiracy theory nyingine ambapo wanatheolojia wanaamini kuwa
mfumo wa kishetani wa utawala wa dunia yaani New World Order utaingizwa katika
utawala wa serikali za dunia kwa kufanya mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali
zisizotaka kukubaliana na mfumo wa aina hii. Mara baada ya mapinduzi hayo utawala
wa kishetani utasimika viongozi wanaowataka ambao watakuwa tayari kukubaliana na
mfumo huu wa New World Order ambao dalili zinaonesha kuwa utakuwa ukisimamiwa
na jumuiya ya umoja wa mataifa.
Mifano bado ni mingi sana kwa mfano wanatheolojia katika Gradualism conspiracy
theory wao wanaamini kuwa utawala wa New World Order taratibu umeshaanza
kuingizwa katika mifumo ya utendaji ya mashirikisho makubwa ya kimatifa. Mfano
katika shirika la nchini Marekani la Federal Reserve System mwaka 1913. The League of
Nations mwaka 1919. Shirika la fedha duniani International Monetary Fund mwaka 1944.
The United Nations mwaka 1945. Benki ya dunia mwaka 1945. Shirika la afya duniani
WHO mwaka 1993. Shirika la biashara duniani WTO mwaka 1998. Umoja wa nchi za
Afrika mwaka 2002 na katika muungano wa mataifa ya kusini mwa bara la Marekani
mwaka 2008.
Mifano bado ni mingi sana ni bahati mbaya tu kuwa sina muda wa kuelezea mambo
yote kwa sasa japokuwa napenda ujue hali ya dunia hii kule inapoelekea. Nitakapopata
muda wa kutosha nitakueleza conspiracy theories nyingine za New World Order kama ile ya
Occultism,Fourth Reich,Brave New World na ile ya viumbe wa ajabu katoka sayari ya mbali
wanaotabiriwa kuja kuivamia hii dunia iitwayo Alien invansion conspirancy theory” Pastor
Romanus akamaliza kunieleza kisha akafunika ukurasa wa kile kitabu na kuupisha
utulivu huku akiangalia mbele ya lile kanisa kama anayefikiria jambo fulani.
“Lakini Pastor huoni kuwa haya mambo yamekaa katika mtazamo wa kidini?”
hatimaye nikavunja ukimya na kumuuliza.
“Hapo ndiyo ugumu wa watu kuelewa ulipo. Watu wengi hudhani kuwa kwa
kuwa mambo haya yanazungumzwa na mtu wa imani tofauti basi wao ambao hawapo
kwenye imani hiyo mambo haya hayawahusu. Hii dunia ni ya kwetu sote na janga
linapokuja huwa halichagui dini ya mtu na vilevile mambo haya yana ushahidi ingawa
bado kwa mtu asiyetaka kuelewa anaweza kuyachukulia mambo haya katika mtazamo
ya kidini. Viongozi wa dini tuliyobahatika kuyafahamu mambo haya tunakesha katika
kuwafahamisha watu lakini siyo busara kumlazimisha mtu atuelewe. Kila binadamu
atakuja kuelewa pale nafsi yake itakapokuwa tayari” Pastor Romanus akaongea kwa
masikitiko.
“Wewe unavyodhani huu mfumo wa New World Order umeshaanza kujipenyeza
barani Afrika?” nilimuuliza Pastor Romanus na hapo akageuka taratibu na kunitazama
kwa mshangao kisha nikamuona akitabasamu.
“Siku zote waumini wazuri wa dini huwa hawajitangazi!” maneno ya Pastor
Romanus yakinipelekea nitabasamu kidogo na kabla sijatia neno akaendelea
“Viongozi wengi wa nchi za Afrika na kwengineko duniani wameshaukubali
mfumo huu aidha kwa kuutaka,kwa kujua au kwa kutokujua. Viongozi wa hizi nchi
zetu za Afrika wao ndiyo wako kwenye mtego mkubwa kwani kutokana na umasikini
uliokithiri katika nchi zao na tamaa za kupata utajiri mkubwa na kupenda kung’ang’ania
madarakani. Hivyo wanajikuta wakikubali kila kitu kutoka kwa viongozi wa mataifa
makubwa yaliyoendelea kiuchumi ambao ndiyo wadua wakubwa wa mfumo huu wa
New World Order.
Baadhi ya viongozi wetu wa Afrika wamekuwa kama msichana mwenye nuksi
ya kuolewa ambaye kuolewa kwake imekuwa ndoto ya kuisikilizia kwenye bomba.
Hivyo anapotokea mwanaume yoyote wa kumuoa hata kama hana vigezo vyake yeye
humkubalia tu ili ndoto yake itimie hata kama hiyo ndoa ni batili.
Kwa mfano chama cha kimataifa cha wanaume mashoga na wanawake wasagaji
kiitwacho International Gay and Lesbian Association katika taarifa zake za kongamano
la dunia kimetoa makadirio ya takwimu kwa kusema kuwa suala la ushoga angalau
limejadiliwa kwa namna tofauti katika nchi 38 za barani Afrika. Hivyo ukitoa idadi
hiyo kutoka katika jumla ya idadi ya nchi za Afrika ambazo ni 54 utagundua kuwa ni
nchi 16 tu ambazo hazijaruhusu mijadala ya ushoga na usagaji kufanyika. Na katika
majadiliano hayo nchi 13 za barani Afrika zimeonekana kuwa baadhi yao zimepitisha
sheria za kuruhusu vitendo vya ushoga na usagaji na nyingine hazikuruhusu au kutoa
tamko la kupitisha. Hivyo ukichunguza vizuri utagundua kuwa hata hizi nchi ambazo
hazikutoa tamko lolote kwa maana nyingine ni kuwa hazina shida ya moja kwa moja
na suala hili.
Taarifa za chama hicho zimeeleza kuwa angalau vitendo vya kujamiana kwa watu
wa jinsia moja bado havijatambulika rasmi kuwa ni kosa katika baadhi ya nchi za Afrika
kama Burkina Faso,Central African Republic,Chad,Republic of Congo,Côte d’Ivoire,Democratic
Republic of Congo,Gabon,Madagascar,Mali,Niger na Rwanda.
Tangu mwaka 2011 baadhi ya nchi za dunia ya kwanza zimeanza mchakato wa
kuzuia na nyingine zimepitisha sheria ambazo zinaruhusu kusitisha mgao wa pesa za
bajeti au kupunguza mgao huo kwa serikali za nchi za Afrika ambazo bado zinapingana
vikali na masuala ya ushoga na usagaji. Ingawa baadhi ya nchi hizi za Afrika zinapinga
vikali masuala ya ushoga na usagaji kwa kudai kuwa ni vitendo visivyoendana na mila
na dini za bara la Afrika.
Katika nchi za Mauritania,Sudan na kaskazini mwa nchi ya Nigeria adhabu ya
kushiriki vitendo vya ushoga na usagaji ni kifo. Katika nchi ya Uganda,Tanzania na
Sierra Leone washiriki wa vitendo vya ushoga na usagaji adhabu yake huwa ni kifungo
cha maisha. Lakini ni kweli kuwa hapa nchini kuna mtu yeyote aliyefungwa kifungo
cha maisha kwa ajili ya kushiriki vitendo vya namna hii?. Jibu unalo mwenyewe.
Katika nchi ya Afrika ya kusini katiba ya nchi hiyo kwa kiasi kikubwa inatoa mwanya
wa haki za mashoga,wasagaji na kuunga mkono ndoa za jinsia moja” Pastor Romanus
akaweka kituo kisha akakohoa kidogo kulilainisha koo lake.
“Sasa nimeanza kupata picha kamili ya mambo yalivyo,kuwa hii chapa 666 ni
mpango wa shetani na ina nafasi kubwa katika hii mikakati ya siri ya kusimamisha
serikani ya dunia yenye nguvu kubwa za kifedha na kishetani” niliongea kwa utulivu
huku nikihisi kuwa nilikuwa nimepata ufahamu mzuri wa masuala ya hii dunia. Pastor
Romanus akafurahi huku akizipangusa kingo za mdomo wake kwa ulimi kabla ya
kuongea kwa utulivu
“Idadi ya wacha Mungu katika hii dunia ni ndogo sana kama kipande cha ubao
moja kwenye safina ya Nuhu. Sisi kama watumishi wa Mungu kazi yetu ni kuwahubiria
watu waache dhambi na kumwabudu Mungu kwani yeye ndiye mwenye milki ya
vitu vyote hapa duniani na mbinguni. Baadhi ya watu wametusikia na kutuelewa na
wamebadilika kwani katika zama hizi kumuona mchawi anaacha kula nyama za watu
na kukimbilia mishkaki ni jambo la kumshukuru sana Mungu”
Niliangua kicheko hafifu na kumtazama Pastor Romanus kwa umakini na hapo
akanitupia swali
“Unaweza kuniambia hasa ni kitu gani kilichokupelekea ufunge safari kutoka
huko utokako na kuja hapa kanisani usiku huu kuuliza juu ya hiyo namba 666?” swali
la Pastor Romanus lilikuwa la kushtukiza na kwa kiasi fulani liliyahamisha mawazo
yangu kichwani hata hivyo huwenda ningemshangaa sana endapo asingeniuliza swali
lile hadi ukomo wa maongezi yetu. Hivyo niliviminyaminya vidole vyangu mikononi
huku nikitafakari kisha nikageuka na kumtazama Pastor Romanus na macho yetu
yalipokutana nikaanza kujieleza kuwa mimi na nani,nafanya kazi gani na kwanini
nilikuwa nimefika pale. Maelezo yangu yalikuwa yamenyooka na hivyo wakati
nikimalizia kutoa utambulisho wangu Pastor Romanus alinipa mkono na kunipongeza
japokuwa niliona mashaka kidogo katika uso wake.
“Wewe ni mpelelezi?” hatimaye Pastor Romanus akaniuliza huku akinitazama
usoni na kwa hakika swali lake lilinishangaza sana. Nilishikwa na mduwao kidogo na
fikra zangu zilipopata utulivu nikamjibu
“Ndiyo!,mimi ni mpelelezi” nikaongea kwa utulivu
“Nilikufahamu tangu wakati ulipokuwa anaingia humu ndani. Nimewahi kukutana
na wapelelezi mara kadhaa baadhi yao wakitaka kunipeleleza juu ya huduma yangu”
Pastor Romanus akaongea kwa utulivu huku akigeuka tena na kunitazama.
“Napeleleza juu ya kupotea kwa mpelelezi mwenzangu”
“Anaitwa nani?”
“Gabbi Masebo”
Mara tu nilipomaliza kuongea Pastor Romanus akanitazama kwa mshangao.
“Gabbi Masebo!...” Pastor Romanus akaongea kwa utulivu huku akitafakari.
“Hakuna anayefahamu Gabbi Masebo alipo. Muda mfupi baada ya kufunga ndoa
miaka kumi iliyopita alichana na mkewe na baada ya hapo Gabbi Masebo anasemekana
kutoweka kusikojulikana” nikaongea kwa utulivu huku nikiichukua ile picha ya Gabbi
Masebo kutoka mfukoni na kumuonesha Pastor Romanus. Baada ya kitambo kifupi
cha ukimya huku Pastor Romanus akiitazama ile picha mara nikamuona akigeuka na
kunitazama
“Unamfahamu?” nikawahi kumuuliza.
“Gabbi Masebo alikuwa rafiki yangu” Pastor Romanus akaongea kwa utulivu
halafu kama niliyeshtushwa na maelezo yake nikageuka haraka na kumtazama kwa
shauku. Nilimuona Pastor Romanus akiacha kuitazama ile picha mkononi mwangu na
badala yake akayahamishia macho yake kutazama mbele ya ile madhabahu ya kanisa.
Nilipomtazama vizuri nikatambua kuwa fikra zake hazikuwa pale. Mvua kubwa bado
ilikuwa ikiendelea kunyesha kwani niliweza kuisikia vizuri namna iliyokuwa ikianguka
juu ya paa la kanisa lile.
“Alikuwa akifika hapa kanisani mara kwa mara lakini hakuwahi kuniambia kuwa
yeye ni mpelelezi ingawa baadaye nilianza kuhisi kuwa alikuwa akichunguza jambo
fulani ambalo mimi sikulifahamu”
“Unafahamu kuwa alifunga ndoa?”
“Nilipata habari tu na sikumbuki habari hizo nilizipata kutoka kwa nani lakini
ndoa yake hakuifungia hapa” Pastor Romanus akaongea kwa hakika.
“Uliwahi kusikia tetesi zozote juu ya mkewe?” nilimuuliza Pastor Romanus huku
nikimtazama usoni kuyapima maelezo yake.
“Niliambiwa kuwa huyo msichana aliyemuoa alikuwa muumini wa hapa lakini
kwa sasa simkumbiki na huwenda Gabbi Masebo alikuwa akifika hapa katika harakati
za kumnasa huyo msichana japo sina hakika”
“Unadhani ni kwanini hawakufungia ndoa yao hapa kanisani kwako?”
“Sifahamu ingawa mara nyingi wasichana wengi wanapopata wanaume wa
kuolewa suala la wapi wakafungie ndoa yao huwa ni la mwanaume. Wasichana hufuata
maamuzi ya makanisa yale ambayo waume zao watarajiwa ndiyo wanapoamini na
huwenda hilo ndiyo lililotokea”
“Wewe kama kiongozi wa kanisa huwa hupewi taarifa juu ya wapi ndoa za
waumini wako zinapofungiwa?”
“Baadhi huona kuwa ni sahihi kuniambia na mimi huwaombea baraka zote lakini
wengine huamua kufanya mambo yao kimyakimya hivyo ni vigumu kufahamu”
Pastor Romanus akaongea kwa utulivu huku akiyatafakari maelezo yangu.
“Kwa hiyo mke wa Gabbi Masebo alikuwa muumini wa kanisa lako?” nilimuuliza
Pastor Romanus huku nikimtazama.
“Ni vigumu sana kumfahamu kila muumini wa hapa kanisani hususani katika jiji
lenye watu wengi kama hili la Dar es Salaam. Kama nilivyokuambia hapo awali taarifa
hizo nilizipata kwa waumini ambapo sasa siwakumbuki” Pastor Romanus akaongea
kwa msisitizo na nilipomtathmini vizuri nikatambua kuwa kulikuwa na ukweli katika
maneno yake. Nilitulia kidogo nikiupisha utulivu kichwani mwangu kwani maelezo ya
Pastor Romanus yalikuwa yametowesha ukungu kidogo katika fikra zangu.
“Nahitaji msaada wako Pastor” hatimaye nilivunja ukimya huku nikimtazama
Pastor Romanus kwa makini.
“Msaada upi?” Pastor Romanus akaniuliza kwa shauku
“Nahitaji kupata taarifa zinazojitosheleza juu ya Gabbi Masebo na huyo msichana
aliyefunga naye ndoa. Nina hisia kubwa kuwa huwenda kupotea kwa Gabbi
Masebo,msichana aliyefunganaye ndoa na hawa watu wasioeleweka kwenye lile jengo
la ghorofa la kule posta nililokuelezea hapo awali kwenye maongezi yangu kuwa kuna
uhusiano wa namna fulani”
“Sasa mimi nitakusaidiaje?” Pastor Romanus akaniuliza kwa utulivu
“Nahitaji kufahamu ni wapi hiyo ndoa ya Gabbi Masebo na huyo binti
anayesadikika kuwa alikuwa ni muumini wako ilipofungwa. Nahitaji pia unitafutie jina
la huyo msichana aliyefunga ndoa na Gabbi Masebo”
“Unadhani ni jambo rahisi?. Makanisa ni mengi sana hapa jijini Dar es Salaam”
Pastor Romanus akaongea kwa msisitizo.
“Najua siyo jambo rahisi lakini kwa uzoefu na mamlaka uliyonayo kupata taarifa
za namna hiyo naamini inawezekana” nilimwambia Pastor Romanus na hapo ukimya
ukafuatia hivyo nikajua kuwa kwa vyovyote alikuwa akitafakari ombi langu.
“Nitajaribu lakini hili siyo jambo la kukupa sana matumaini. Hata hivyo ningependa
kwanza kufahamu kwanini unazihitaji taarifa hizi” ombi la Pastor Romanus
likanipelekea nitabasamu kidogo kisha nikayafikicha macho yangu na kupiga mwayo
hafifu wa uchovu.
“Nafanya upelelezi kutaka kufahamu ukweli kama Gabbi Masebo yupo hai au
amekufa na kama amekufa nifahamu kuwa amezikwa wapi na nini chanzo cha kifo
chake”
“Baada ya kufahamu je?”
“Ndugu zake watafahamishwa na hapo kazi yangu itakuwa imefika ukomo”
niliongea kwa msisitizo na hapo Pastor Romanus akanitazama kwa makini kabla ya
kuvunja ukimya.
“Nafahamu nini kinachoendelea hata hivyo hili ni jambo hatari linaloweza
kugharimu uhai wa mtu” Pastor Romanus akaongea kwa utulivu huku maelezo
yake yakiibua shauku ya aina yake usoni mwangu hali iliyonipelekea niketi vizuri na
kumtazama kwa makini.
“Unafahamu nini?” hatimaye nikamuuliza kwa udadisi na hapo Pastor Romanus
akanitazama kwa utulivu kabla ya kuvunja ukimya.
“Nahisi lipo jambo kubwa lililofichika nyuma ya kutoweka kwa Gabbi Masebo
ambalo huwenda likawa kwa namna moja au nyingine lina maslahi makubwa kwa
serikali kama siyo baadhi ya maafisa wake”
“Kwanini unasema hivyo?” nilimuuliza Pastor Romanus kwa shauku
“Mara kwa mara nimekuwa nikiitwa na vyombo vya usalama na kuhojiwa juu
ya Gabbi Masebo kwa kigezo kuwa alikuwa muumini wangu” nilimtazama Pastor
Romanus na kuvutika na maelezo yake na hapo nikamuuliza
“Walikuwa wakikuhoji nini?”
“Kama nilikuwa nikifahamu taarifa zake zozote kuhusu yeye”
“Unadhani kwanini wanataka kufahamu alipo?”
“Kwa kweli sifahamu ingawa nahisi huwenda Gabbi Masebo alikuwa ni mtu
hatari sana kuliko nilivyokuwa nikimdhania”
“Mahojiano hayo yalianza lini?”
“Hizi siku za karibuni” Pastor Romanus akaongea kwa msisitizo
“Sasa naanza kuhisi kuwa kuna jambo fulani hatari limefichika nyuma ya Gabbi
Masebo na jambo hilo linapiganiwa kufa na kupona ili lisiweze kuwekwa hadharani.
Hata hivyo muda siyo mrefu ukweli wa mambo utafahamika” niliongea kwa hakika
huku nikiupisha utulivu kichwani mwangu.
“Dar es Salaam limekuwa jiji la matukio ya ajabu sana kwa zama hizi. Kila mtu
anakimbizana na utajiri wa hii dunia na umaarufu wake na kwa kufanya hivyo watu
wengi wamejikuta wakijitumbukiza kwenye dini na ibada za kishetani ili mambo yao
yawanyookee kama wanavyodhani. Lakini mafanikio ya shetani huwa ni ya muda
mfupi sana na ya ghafla mno na yanapozimika huzimika kama mshumaa kwenye
upepo wa jangwani.
Chapa 666 uliyoiona katika hilo jengo ni kiashiria cha uwepo wa dini ya kishetani
iliyoanza kuzoa maelfu ya wanasiasa,wasanii,wanamichezo na hata baadhi ya viongozi
wakubwa wa kidini hapa jijini Dar es Salaam. Mafanikio ya watu hawa huambatana
na utoaji mkubwa wa kafara ya damu nyingi za watu wasio na hatia. Watoto wengi
wanaopotea kila kukicha hapa jijini Dar es Salaam ni sehemu ya ibada za kishetani
zinazofanyika ili kuwapa watu utajiri wa muda mfupi” Pastor Romanus alimaliza
kuongea na maelezo yake yakawa yamenizindua fikra zangu.
Niliikumbuka ile chapa 666 kwenye ule mlango wa lile jengo la ghorofa kule
posta kisha nikakumbuka zile sauti za vicheko vya wanawake na zile kelele za vilio
vya watoto wadogo waliokuwa wakilia mle ndani.Halafu nikakumbuka wale watu
waliokuwa wameketi kwenye ule ukumbi. Kwa kweli nilihisi kuishiwa nguvu hata
hivyo niliupisha utulivu kichwani mwangu.
“Nitapata vipi majibu ya kazi yangu?” hatimaye nilimuuliza Pastor Romanus
“Njoo nyumbani kwangu kesho jioni nyumba namba 14 mtaa wa Azikiwe”
“Nitashukuru sana” nilimwambia Pastor Romanus huku nikitabasamu kabla
hajavunja ukimya.
“Huwezi kupambana na shetani kama huna Mungu”
“Nahitaji msaada wako” nikamwambia Pastor Romanus na hapo nikamuona
akisimama na kunisogelea pale nilipoketi.
“Fumba macho” aliponifikia akaniambia nami nikafanya kama alivyotaka na hapo
akanifanyika sala fupi ya kuniombea ulinzi. Alipomaliza akanipa mkono wa baraka.
“Nitajitahidi kulifanyia kazi ombi lako” Pastor Romanus akaongea kwa utulivu
huku akiuweka mkono wake begani kwangu. Nilitabasamu kidogo kisha nikaingiza
mkono mfukoni kuchukua kadi yangu ndogo ya mawasiliano ambayo nilimpa Pastor
Romanus.
“Tafadhali! naomba tuwasiliane kupitia kadi hii” nikamwambia wakati akiipokea
kadi ile kisha akavuta mkono wa vazi lake mkononi na kuitazama saa yake.
“Bila shaka na muda nao umetutupa mkono” Pastor Romanus akaniambia
“Nashukuru sana kwa kunipa muda wako” nikamwambia huku nikisimama
“Tuonane kesho!”
Hatimaye tulishikana mkono na kuagana kisha nikaelekea sehemu ya mbele ya
madhabahu ya lile kanisa ambapo nilitumbukiza noti mbili za shilingi elfu kumi kwenye
kapu la sadaka kama shukrani yangu kisha nikaanza kukatisha katikati ya lile kanisa
katika uchochoro mpana uliofanywa baina ya mabenchi ya lile kanisa yaliyokuwa
upande wa kushoto na kulia. Pamoja na kelele za manyunyu ya mvua yaliyokuwa
yakianguka juu ya lile paa la kanisa hata hivyo bado niliweza kuzisikia hatua zangu
sakafuni wakati nikiyoyoma kuelekea nje ya lile kanisa huku nikiwa na hakika kuwa
macho ya Pastor Romanus yalikuwa yakinisindikiza kwa nyuma.
Mara tu nilipotoka nje ya lile kanisa nikasimama kwenye ngazi za pale mlangoni
huku nikiyapeleleza vizuri mandhari ya nje ya lile kanisa yenye vivuli vingi vya miti ya
mikungu. Hali ilikuwa tulivu kwani sikuona kitu chochote cha kukitilia mashaka. Mvua
kubwa iliyokuwa ikinyesha haikunizuia nisiendelee na safari yangu hivyo nikafyatua
kofia ya koti langu jeusi na refu la kijasusi ama Trench coat na kujifunika vizuri kichwani
kisha nikashuka ngazi nikitokomea mbali na ile kanisa.
Kutembea bila gari langu yalikuwa ni maisha mapya kabisa ambayo kwa kweli
sikuwa na budi kukabiliana nayo kwa wakati huu. Niliitazama saa yangu ya mkononi
na kugundua kuwa muda ulikuwa umesonga sana kwani ilikuwa ikielekea kutimia
saa saba na nusu usiku. Wakati huu barabara nyingi za jiji la Dar es Salaam zilikuwa
zimekaukiwa na pilika za watu na magari na hali ile ikanipelekea nijihisi kuwa ni kama