SURA YA KUMI NA MOJA (Inaendelea)
ZILIPITA WIKI KADHAA tangu Ray na Sofia waende kwa Padre Kiko kule Agape Center kutafuta ushauri katika matatizo yao ya ndoa. Siku ile ya Ijumaa Ray aliona kama ni ndefu isiyoisha; lakini hakuwa na haraka ya kurudi nyumbani kwani Sofia alipafanya nyumbani kuwa pachungu. Alijiuliza wanaume wangapi wako kwenye hali kama yake ambao hutafuta visingizio vya kutokwenda nyumbani mara moja ili kukwepa ugomvi.
Siku ile ilikuwa ni ya kawaida tu. Baada ya mazoezi yake ya asubuhi alijiandaa kuwahi kazini kama ilivyokuwa kawaida yake. Alipofika ofisini alikuta kuna ujumbe uliomtaka aende moja kwa moja ofisini kwa RPC. Aliingia ofisini kwake kwa dakika chache tu kuvua koti lake na kubaki na tai na moja kwa moja alielekea ofisini kwa RPC. Kufika huko alikuta ametanguliwa na maafisa wengine wa vikosi maalum vya jeshi hilo katika Kanda ya Dar na alikuwepo mmoja kutoka Makao Makuu ya Jeshi hilo.
Siku ilianzia hapo na kufika jioni Ray alikuwa hoi bin taabani. Tangu alipoingia ofisini kwa RPC hadi jioni alipotoka kazini Ray na wenzake walikuwa katika jukumu kubwa la kufuatilia kundi la majambazi ambalo lilidaiwa kuwa limeingia nchini Kenya. Taarifa za inteligensia ambazo zilipatikana kutoka Jeshi la Polisi la Kenya ni kuwa kundi hilo lilikuwa na lengo la kufanya matukio kadhaa ya ujambazi katika jiji la Dar-es-Salaam na Mwanza. Kutwa nzima siku ile Ray alikuwa na kazi ya kuratibu wapelelezi wa pale mkoani na wa mikoani katika kujiweka tayari kufuatilia kundi hilo na kuhakikisha taarifa zozote zinawasilishwa mara moja Jijini Dar. Kila mpelelezi aliviweka vyanzo vyake tayari tayari kwa fununu au tetesi zozote watakazozisikia.
Vyanzo vya wapelelezi hao vilikuwa ni vingi na hakuna aliyejua; walikuwepo wapiga kiwi viatu, wauza magazeti, madereva wa bajaji, dalala na hata vijana wanaoshinda vijiweni. Polisi waliwatumia watu hao kupata taarifa nyingi za siri na siyo wao tu hata watu wa Usalama wa Taifa nao walikuwa na watu kama hao nchi nzima. Mitego mbalimbali ya kipolisi ilianza kuwekwa sehemu mbalimbali nchini. Pamoja na juhudi zote za kutwa nzima kundi hilo la majambazi lilikuwa kama limegeuka upepo mara tu baada ya kuingia Tanzania.
Haikujulikana wamepotelea wapi, kwani magari mawili ambayo ilidaiwa walikuwa wameyatumia wakati wanatoka Kenya yalitoweka vile vile na hayakuonekana kwenye barabara yoyote ama kuelekea Moshi au mji mwingine. Jeshi la Upolisi lilikuwa na kamera kwenye baadhi ya barabara kuu ambazo zilikuwa zinarekodi magari yote yanayopita kila siku. Hisia ya viongozi wa polisi ni kuwa majambazi hayo yalikuwa yametulia mahali na kujificha kwa kimya kidogo kabla hawajaendelea. Hii ilimaanisha kuwa walikuwa na washirika wengine Tanzania ambao waliwapa hifadhi na labda hata usafiri mwingine.
Ilikuwa ni agizo la IGP kuhakikisha kuwa watu hao wanapatikana kwa namna yoyote na kwa mbinu yoyote kwani kiwango cha silaha ambazo kundi hilo lilidaiwa kuwa nacho lilimaanisha hawakuingia nchini kufanya ujambazi au uhalifu mdogo. Polisi na watu wa Usalama wa Taifa walitambua mara moja kuwa kundi hilo lilikuwa ni zaidi ya majambazi. Hivyo, kwa Ray ilikuwa ni siku ndefu kwani hakuweza hata kupata nafasi ya kula chakula cha mchana zaidi ya kunywa maji na juisi tu pale pale ofisini. Kutokana na kutokuwa na mafanikio makubwa siku hiyo Ray alitakiwa kuondoka na kuongoza kundi la wapelelezi waandamizi kuelekea Arusha mapema asubuhi kuongeza nguvu.
Alipokuwa akitafakari hayo alikuwa anaingia kwenye geti la nyumba yake funguo ya gari lake mkononi na mkoba uliobeba kompyuta na nyaraka mbalimbali mkono mwingine. Bastola yake ilikuwa upande wa kulia wa mkanda wake. Geti lilifunguliwa na mlinzi wake na taa za nje ndizo zilitoa mwanga pekee pale. Aliingia ndani lakini alikuta taa zote zilikuwa zimezimwa. Aliwasha taa ya pale sebuleni kwa kutumia mkono wenye bastola. Walinzi wake wawili walikuwa bado hawajafika, kwani kawaida walikuwa wanafika pale kwenye majira ya saa tatu hivi za usiku na kupishana na mlinzi wa mchana. Mara nyingi kama Ray yupo nyumbani huwa anamruhusu mlinzi wa mchana kuondoka mapema.
“Sofia!” Ray aliita kwa sauti kubwa. Hakukuwa na kuitikiwa. Alikuwa na uhakika kuwa alipoingia aliliona gari la Sofia likiwa limeegeshwa pembeni ya kibanda cha walinzi. Aliwasha taa ya kuelekea chumbani, na akaangalia jikoni ambako aliwasha taa pia na hakukuwa na mtu. Alienda moja kwa moja chumbani kwake akidhania labda Sofia alikuwa amelala. Hakukuwa na mtu. Kitanda kilikuwa kimetandikwa vizuri. Alianza kuingia na wasiwasi, akakumbuka bado ameshikilia mkoba na funguo yake, akarudi sebuleni na kuviweka juu ya meza. Akaenda bafuni, huko nako hakukuwa na mtu. Ray alikuwa na uhakika kuwa kuna kitu hakiko sawa.
Alirudi tena hadi sebuleni na kuangalia kila kitu kimepangwa vizuri, na inaonekana nyumba nzima ilikuwa imesafishwa vizuri. Hilo halikumshangaza sana kwani ndivyo alivyopenda sana nyumba yake kuonekana. Hata ofisini kwake kila kitu kilikuwa kinapangwa vizuri hadi kalamu za mezani. Kati ya vitu ambavyo hakuwa anavipenda sana ni kukuta vitu vyake vimevurugwa. Marafiki zake walikuwa wanamtania toka zamani kuwa kupenda kwake usafi na kupanga vitu vizuri kulitokana na malezi yake ya seminari. Alipoingia jikoni mara hii ya pili ndio aliona karatasi imebandikwa kwa gundi kwenye mlango wa friji lake kubwa la GE. Ilikuwa imekunjwa mara mbili tu.
Ray aliichukua na kuifungua. Alijikuta amemeza mate kwa ghafla yakampalia na kuanza kukohoa mfululizo kwa sekunde kadhaa. Aliamua kuchukua chupa ya maji ndani ya friji na kufungua na kunywa na mara kukohoa kukatulia. Pale pale jikoni akiwa amesimama bila kuegemea popote alianza kusoma karatasi ile akiwa ameishika kwa mikono miwili kama ilikuwa nzito mkononi.
Mpendwa Ray,
Naomba usishtuke sana kukuta nyumba imekupokea kwa ubaridi na upweke. Baada ya miaka yote ya kuishi nawe na maisha yote tuliyopitia pamoja nimejikuta sina ujasiri wa kuzungumza nawe ana kwa ana na najua mwisho wa siku tungeishia kugombana na tusizungumze kwa siku kadhaa kama ilivyo kawaida miezi hii mingi sasa.
Matamanio yangu yote tangu unioe ni kuwa ningeweza kupata mtoto na hata watoto wengi. Unajua jinsi gani kiu yangu hiyo imeshindwa kutulizwa katika maisha haya tuliyoishi pamoja. Miaka inaenda kwangu na sioni kama mwenzangu una kiu kama yangu kwani ni wazi umeamua kuweka kazi yako kwanza. Mazungumzo yote tuliyoyafanya inaonekana hatuendi popote zaidi ya kukosoana na kukosana.
Ni kwa sababu hiyo nimeamua kuondoka niende kutafuta maisha mahali pengine na Mungu akinijalia niweze kutimiza kiu yangu hiyo. Naomba usihuzunike sana na wala usinitafutea. Nitakuwa tayari kuzungumza nawe mara moja tu kwa simu kukuondoa hofu. Nakutakia mafanikio na maisha mema huko mbeleni.
Sofia.
Chini ya barua kulikuwa na sahihi ya sofia na tarehe ya siku ile. Ray Shaba, hakutaka kuamini kuwa ndoa yake ilikuwa imefikia kikomo kwa namna na mtindo ule. Alijihisi hasira zaidi kuliko uchungu. Lakini kitu kingine kilikuwa kimemshika moyoni nayo ni hisia ya hatia na kujiona kama mtu aliyeshindwa maisha. Hakutaka kuamini maisha ya useminari yalimshinda na sasa ndoa nayo imemshinda. Alijaribu kutafakari jinsi gani walifika hadi kuachana kwa namna ile hakuamini. Sofia alikuwa ni mpenzi wake wa pili lakini katika mapenzi ndiye alikuwa wa kwanza aliyemuingiza katika ulimwengu wa mapenzi na kumpagawisha. Hakuwahi kudhania kuwa maisha yake yangefikia mahali hapo, na kwa vile alikuwa ni Mkatoliki alijua hawezi tena kuoa mwanamke mwingine na wazo la kuishi kinyumba tu hivi hivi hakutaka hata kulipa nafasi.
Alichukua simu yake na kutaka kumpigia Sofia saa ile ile lakini alijikuta anajiuliza mara mbilimbili kama ampigie au vipi. Upande mmoja alitaka kuhakikisha kuwa yuko salama na ajaribu kumbembeleza kurudi lakini upande mwingine alikuwa na hasira na kiburi. Hata hivyo aliamua kukishinda kiburi chake.
“Hi Ray” Sofia alijibu mara baada tu ya simu kuita mara moja.
“Sofia, uko wapi?” Ray aliuliza huku sauti yake ikiwa kama ya mtu anayenong’ona lakini si kwa sababu ya kutaka kuficha jambo bali kutotaka kufichua hasira iliyokuwa inachemka kwenye damu yake.
“Ray usianze, umeisoma barua yangu?” Sofia alimjibu sauti yake ikiwa thabiti kabisa na isiyoonesha unyonge au huzuni au woga fulani mbele ya Ray.
“Ndio nimeisoma, kwanini usije tuzungumze Sofia?”
“Muda wa kuzungumza umepita Ray, tumezungumza sana na kwa kweli mimi ndio nimezungumza sana lakini sioni namna nyingine” Sofia alianza kutoa ya moyoni.
“Sasa kwanini usije unieleze vizuri mke wangu” Ray alijikuta anabembeleza. Hakujua kama anabembeleza kwa sababu kweli anataka arudi au anabembeleza kwa sababu alikuwa anatarajiwa kubembeleza. Sofia hakusogea hata nchi mmoja wala kuonesha dalili ya kumsikia Ray. Alikuwa ni mwanamke anayejua anachotaka na akishaamua kukipata hakukuwa na kitu cha kumbadilisha. Kwa dakika kama tano bila kumpa nafasi Ray kuzungumza Sofia alieleza tena aliyoyasema kwenye barua yake na kusema kuwa anaenda kukata simu na atabadilisha namba yake. Alichomuambia Ray ni kuwa tu asimtafute ampe muda kama atajikuta anataka kurudi basi atarudi mwenyewe. Alimuomba sana Ray asiwasumbue wazazi wake yeye Sofia kwani haendi kwao wala haendi kwa ndugu yeyote ambaye Ray anaweza kumpata.
Ray alijikuta hana la kusema zaidi ya kumwambia Sofia kuwa ule ulikuwa ni uamuzi wake na kuwa kama akitaka kurudi nyumba ile ni yake na ni pake na anaweza kurudi wakati wowote kwa sababu yeye hakumfukuza.
Walikata simu bila ya kwaheri wala kutakiana heri.
Aliamua saa ile ile kama kweli Sofia ameamua kuondoka basi hatokuja kuoa tena kwani hakutaka tena kuhangaika na wanawake. Aliona kuwa kama ndoa zipo duniani basi kwake ndoa yake pekee iliyobakia ni kazi na kazi peke yake. Aliamua kwenda tena kwenye friji safari hii hakutaka maji tena, alichukua chupa ya rangi ya dhahabu ya kinywaji kikali cha whiski ya Fyfe. Alichukua madonge matatu ya barafu na kuyaweka kwenye glasi na kumimina whiski ile hadi karibu ya kujaa. Bila kupumua aliiweka mdomoni na kuibugia kwa mafundo kama maji. Ray Shaba hakuwa mnywaji sana wa whiski lakini huwa anakunywa kwa mtindo huo kila anapokuwa katika msongo mkubwa wa mawazo na hisia kama ilivyokuwa usiku ule. Hakutaka hata kula.
Alielekea moja kwa moja chumbani, alibadilisha nguo zake za kutwa na kuvaa nguo za kulalia. Alitoka nje mara moja kuhakikisha walinzi wameshafika na aliwakuta hakuwaambia kitu aliwatakia tu usiku mwema yeye mwenyewe akarudi ndani. Alielekea moja kwa moja kulala kwani kesho yake kulikuwa na kazi ya kuwatafuta wale washukiwa walioingia nchini kutokea Kenya.
Hakutaka kumsikia Sofia, wala kumfikiria wala kuulizia mambo ya Sofia. Alitaka kujilalia tu; mambo ya Sofia aliamua kumuachia Sofia. Wakati anajiandaa kuzima taa kwenye meza ndogo ya pembeni ndio macho yake yakagongana na pete ya ndoa ambayo Sofia aliiacha pale. Aliiangalia kwa muda bila kutaka kuigusa kama kwa kuiangalia kule kungeifanya itoweke. Alijigeuza upande mwingine.
(Itaendelea)