Riwaya Mpya: Mpelelezi Ray Shaba katika

Tupo pamoja mzeee
 
Mzee mwanakijiji asante,ila ucpotee sana
 
SURA YA 12
(Inaendelea)

TANGU MAPEMA ASUBUHI siku ile ya Jumatatu watu walianza kutiririka taratibu kuelekea Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza wakitokea katika viunga mbalimbali vya jiji hilo. Kina mama na watoto wao migongoni, huku wengine wakishikwa mikononi, wazee na fimbo zao za kutembelea na vijana na baskeli zao huku wengine wakitembea kwa miguu kila mmoja na simu mkononi walielekea Kirumba. Milango ya uwanja wa Kirumba ilifunguliwa tangu saa kumi na mbili asubuhi na watu walianza kuingia toka mida hiyo na ilipofika saa nne asubuhi, mzunguko wa uwanja ulikuwa tayari umejaa.

Watu waliruhusiwa siyo tu kukaa kwenye mzunguko bali pia kukaa katikati kabisa kwenye eneo la kuchezea mpira ambapo viti kwa maelfu vimepangwa vizuri kabisa kuelekea upande mmoja wa goli katika uwanja huo wa kabumbu. Upande ule ambapo viti vilielekezwa ndiko jukwaa kubwa lilikuwa limejengwa. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa mkutano mkubwa wa Injili kama ule kuruhusiwa kufanyika ndani ya uwanja wa CCM Kirumba. Uwanja ule ulichaguliwa kwa sababu ndio ulikuwa na eneo kubwa la kuweza kuchukua maelfu ya watu kwa wakati mmoja katika mazingira salama pale jijini Mwanza.

Watu walitoka nje ya Jiji la Mwanza kutoka mikoa ya Shinyanga, Mara, Geita, na Simiyu walikuwa wameingia mjini, wengi siku moja kabla. Kwa wakazi wa Mwanza ujio wa mkutano mkubwa wa Injili wa Askofu Mkuu Ndondo ulikuwa ni neema kubwa kwa wenye mahoteli, nyumba za kulala wageni, na biashara mbalimbali. Mkutano wa Kanisa la Mavuno ulileta mavuno ya neema kwa kila mtu mwenye akili ya kuchakarika.

Wale waliofika siku moja au mbili kabla waliweka kambi nje ya uwanja kama watu wanavyofanya huko Marekani wanaposubiria simu mpya za Iphone au kuwahi kufanya manunuzi yenye punguzo kubwa la bei wakati wa Krismasi. Polisi kutoka mikoa mitano jirani waliletwa jijini Mwanza kuongeza nguvu. Harufu ya ujio wa Nabii na Mtume Damien Ndondo ilikuwa imetanda kwa siku kadhaa katika anga zima la jiji la Mwanza, lenye maji baridi na samaki watamu waliosifiwa na Dkt. Remmy Ongala. Mkutano huo haukuvutia wenyeji tu bali hata raia wa kigeni ambao walikuwa wanatembelea Tanzania. Wageni wengi waliamua kutumia muda Jijini Mwanza kushuhudia mkutano huo mkubwa kama sehemu ya utalii pia.

Malori makubwa kumi ya aina ya Fuso Fighter yalikuwa yametangulia wiki moja kabla yakiwa na vifaa na vyombo vyote vitakavyohitajika kufanikisha mkutano. Malori yote yalikuwa yameandikwa pembeni kwa maandishi makubwa “Huduma ya Mavuno”. Magari mengine madogo yalibeba wafanyakazi mbalimbali na wahudumu wengine ambao jukumu lao ilikuwa ni kusimamia maandalizi ya mkutano, wote wakitoka makao makuu Dar-es-Salaam. Jukumu kubwa la timu hiyo iliyotangulia ilikuwa kuhakikisha kuwa dakika ambayo Askofu Mkuu, Nabii na Mtumishi wa Mungu Damien Ndondo anasimama jukwaani kila kitu kinaenda kwa ufanisi wa hali yajuu. Hakuna kitu ambacho Ndondo hakukipenda wala kukizoea kama watu kufanya kazi bila ufanisi wa hali ya juu. Kuanzia sauti, eneo, umeme na kila kitu ambacho kilihitajika kifanye kazi yake basi ilikuwa ni jukumu la timu hiyo kuhakikisha kinafanya hivyo. Wao walikuwa ni kwanza kufika na ni wa mwisho kuondoka.

Mazoezi ya vyombo na mitambo yote pamoja na kwaya zote yalifanyika siku ya Jumamosi siku moja kabla ya kuanza kwa mkutano. Pamoja na kuwa na genereta zao wenyewe kusimamia mifumo mikubwa ya utangazaji, huduma ya Ndondo ilitumia pia umeme wa nguvu za jua hasa kwenye matumizi ya taa pale uwanjani ambazo ziliongezwa kwani uwanja wa CCM Kirumba haukuwa na taa za kutosha za kisasa kuweza kumulika ndani na nje ya uwanja. Hii ilisaidia kupunguza kutegemea huduma ya umeme wa Tanesco na hawakutaka kutumia umeme huo sana kwani kama wangetumia basi kungekuwa na upungufu wa umeme kwa Jiji la Mwanza.

Uamuzi wa kuja na mtambo wao za kuzalisha umeme ulisaidia pia kuishawishi serikali kuruhusu kutumiwa kwa uwanja huo maarufu ambao huwa unatumiwa na timu za Pamba na Toto African za Jijini humo. Umeme wa ziada uliozalishwa uliingizwa kwenye maduka ya eneo lile na kuleta afueni kwa muda wa wiki nzima mkutano ulikuwa unafanyika. Hakuna mtu aliyetaka kupitwa na ujio wa Askofu Mkuu Ndondo. Kwa wakazi wa Mwanza iliwakumbushia ujio wa Mtakatifu Papa Yohani Paulo II mwaka 1990 kwenye kilima cha Kawekamo upande wa Magharibi wa jiji hilo kuelekea Uwanja wa Ndege. Wakatoliki kwa Wapentekoste, Walutheri kwa Waangalikana, Waislamu kwa Wahindu wote walitaka angalau kumuona mtu ambaye alitajwa kuwa ni miongoni mwa wachungaji maarufu zaidi katika Bara la Afrika lakini pia akiwa ni miongoni mwa wachungaji matajiri zaidi katika Afrika.

Ilipofika saa nane mchana hakukuwa na mahali pa kukaa pale uwanjani. Huduma ya Ndondo hata hivyo ilikuwa imejiandaa. Kulikuwa na TV kubwa zilizowekwa kuzunguka uwanja wa Kirumba kwa ajili ya watu waliokuwa nje ya eneo lile. Vile vile TV nyingine ziliwekwa kwenye viwanja vya Furahisha, pamoja na viwanja vya shule za Nyamanoro na Nyakabungo ambapo maelfu ya watu ambao hawakupata nafasi ya kwenda Kirumba walisubiria kufuatilia moja kwa moja mahubiri ya Askofu Ndondo. Mamilioni ya Watanzania wengine yalisubiri kwa hamu mahubiri kupitia televisheni ya ITV ambayo ilikuwa imenunua haki za kurusha matangazo yale moja kwa moja. Baadhi ya TV za Kenya na DRC maeneo ya Katanga.

Saa tisa kamili juu ya alama uwanja wa CCM Kirumba ulilipuka kwa shangwe baada ya helikopta iliyombeba Askofu Damien Ndondo kuibukia upande wa Magharibi wa uwanja ikitokea maeneo ya Pasiansi kiliko kiwanja cha ndege. Kelele na vigelele vilivyolipuka uwanjani hapo havikuweza kuzuia sauti ya ngurumo ya helikopta ile ambayo ilitumia dakika kadhaa kuuzunguka uwanja huku Askofu Ndondo.

Baada ya dakika chache za kuzunguka angani helikopta ya Askofu ilianza kushuka taratibu na kuchukua usawa wa sehemu iliyoandaliwa kwa ajili ya kutua. Sehemu ile ilikuwa imezungukwa na walinzi wa kanisa lake wakiwa katika sare zao nadhifu. Walinzi wale wapatao hamsini walikuwa wanahakikisha mtu hasogei karibu na sehemu ya helikopta kutua. Sehemu ile iliachwa wazi huku herufi kubwa ya “H” iliyoandikwa kwa chokaa ikionekana. Ilimaanisha ni eneo la kutulia helikopta.

Ngurumo ilibadilika na kuashilia taratibu za kuizima zimeanza. Baada ya mapangaboi kutulia mlango wa helikopta ulifunguliwa na wa kwanza kutoka alikuwa ni mpambe wa Askofu Mkuu Ndondo ambaye alikuwa kama yule askari wa Jeshi la Wananchi ambaye huwa anafuatana na Rais mahali popote anapokwenda. Mpambe wa Ndondo alikuwa amevaa sare za kampuni yake ya ulinzi ambayo ilikuwa ni ya rangi nyeupe, huku akivaa kofia kama ya kiaskari ikiwa na nembo yenye msalaba na maua. Alikuwa na nyota nne mabegani ziking’ara. Walifuatia walinzi wengine wawili kasha First Lady Grace na ndipo Askofu Ndondo mwenyewe aliteremka. Mpiga video wa kanisa ambaye alikuwa anarusha moja kwa moja safari ya Askofu Ndondo kuanzia wakiwa uwanja wa ndege. Alitua jijini Mwanza na ndege yake ya Gulfstream na kuchukua helikopta kuelekea uwanjani.

Sauti za vigelegele na shangwe za vijana zilizizima pale uwanjani wakati Askofu Mkuu Ndondo aliposimama na kupunga mikono. Askofu Ndondo alikuwa amevalia suti nyeupe, huku ndani akiwa amevaa shati la Kiaskofu la rangi nyekundu, msalaba wake haukuwa kifuani bali ulichomekwa kwenye mfuko wake wa kushoto wa shati lake. Mke wa Askofu Grace Ndondo naye alikuwa amevaa gauni zuri la rangi ya zambarau lililombana mwili kiasi. Mabinti wawili wa kanisa waliovalia suti za kike walikuwa ni wapambe maalum wa Grace Ndondo; wao walikuwa wanawasubiria pale uwanjani. Waliwapungia mkono watu na taratibu wakiongozwa na wapambe wao huku wakifuatiwa na ujumbe wao waliteremka jukwaa lile maalum la kutua helikopta. Viongozi wengine wa mkoa na wa makanisa mbalimbali walikuwepo pale kumpokea Askofu Mkuu Ndondo. Kiongozi pekee ambaye hakuweza kuhudhuria alikuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Mwanza, Mhashamu Yuda Ruwa’ichi O.F.M. Cap.

Alipomaliza kusalimiana nao tu aliingia kwenye gari la wazi la Bentley Bentayga la rangi nyeusi. Gari hilo lilikuwa ni miongoni mwa magari magari ya kifahari na ghali zaidi duniani. Mara baada ya Askofu, Grace na Mpambe wa Askofu kuingia kwenye gari lile, pikipiki kumi na mbili zilikuwa tayari kuanza msafara wa kuzunguka ndani ya uwanja kusalimia maelfu na makumi ya elfu ya watu waliojaa pale uwanjani. Pamoja na msafara wa pikipiki na magari mawili yaliyotangulia mbili Askofu alikuwa kama Rais akiwa tayari kuhudhuria sherehe za kitaifa. Alizunguka taratibu huku kwaya ikiendelea kupiga nyimbo mbalimbali za sifa kwenye jukwaa kuu. Ilichukua kama dakika kumi na tano kwa Askofu Ndondo kukamilisha mzunguko na alipofika pale walipoegesha Helikopta waliteremka na Askofu alitembea katikati ya uwanja akipita kama Musa alivyopita na wana wa Israeli kwenye bahari ya Shamu.

Wamama walirusha kanga zao kuzitandika chini wakati Askofu, mke wake na wapambe walipotembea kuelekea mwisho mwingine wa uwanja ambapo Jukwaa kuu kubwa lilikuwa limejengwa likitazama upande wa Magharibi. Watu walijaribu kumgusa, na wengine wakiomba baraka mbalimbali huku wakimpa vitu aviguse ili vipate upako wake. Alipofika jukwaa kuu viongozi wote na wageni waalikwa walisimama kumkaribisha tena na walikuwa tayari kwa ajili ya mkutano mkubwa kabisa wa Injili Tanzania.

Baada ya taratibu zote za kukaribishwa na kutambulisha wageni mbalimbali, kwaya mbalimbali zilianza kuhudumu huku watu wakiendelea kusubiri kwa hamu muda ufike Askofu Mkuu Ndondo apande jukwaani. Kulikuwa na upako wa aina ya pekee. Upako ambao maelfu ya watu waliamini upo, upako ambao hakuna aliyetaka kuukosa na wale ambao waliwahi kuupata hawakutaka kukosa upako mara mbili.

Saa kumi na moja na nusu Mtumishi wa Mungu, Askofu na Mjumbe wa Nyakati za Mwisho, Nabii na Balozi wa Serikali ya Mbinguni kama alivyokuwa ameanza kujiita wiki chache kabla alikuwa anapanda jukwaani. Alipopewa tu kipaza sauti na kukishika mkononi taa kubwa za uwanja ule zote ziliwashwa kama ishara kuwa mambo pale uwanjani yalikuwa yameiva. Hakuna aliyetaka kupitwa na lolote.

Askofu Ndondo aliuangalia umati ule, alinyosha mkono wake juu kuubariki, aliongoza kuimba wimbo maarufu wa Baba wa Mbinguni Nyosha Mkono Wako huku kwaya ikimsindikiza kwa muziki murua ukiwa na tarumbeta na magitaa yakicharazwa kiufundi. Umati uliitikia kwa shangwe kwani wimbo huo uliweza kuimbwa kwa lugha mbalimbali. Na walipoimba kwa Kisukuma vigelegele na kelele za shangwe zilipaa tena. Kwaya ambayo ilikuwa inaongoza ilikuwa ni ile ya Mavuno ikishirikiana na Bendi ya Hossana Life Ministry ya kutoka Entebbe Uganda ikiwa na mwimbaji Leona Mukasa.

Ujumbe wa Askofu Mkuu wiki ile ulijengwa kutoka kitabu cha Ufunuo wa Yohana 22:17 ambapo imeandikwa “Na Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure”.

Mahubiri yalikuwa motomoto, Askofu alikuwa ni kama mwigizaji mahiri aliyeweza kumudu jukwaa lake vilivyo. Aliweza kupaza sauti na kuishusha kwa mbwembwe. Mifano yake iliendana na vichekesho na kila baada ya muda aliwahimiza watu wamshangilie Mfalme wa Serikali ya Mbinguni, huku akiwauliza watu waseme Amina, na kuwaambia warudie tena kusema Amina. Maelfu ya watu walifuatilia mahubiri yale, huku wakijihisi wanabarikiwa kwa kila namna. Michango ya watu kwenye kurasa za Facebook na Instagram zilikuwa zikitoa maneno mengi ya shukrani na kuonesha kuguswa na ujumbe.

Mtu pekee ambaye hakutaka kusikia habari za maji ya uzima wala chupa yake wala kuyaona yana rangi gani hakutaka kuwepo mahali popote alipo Askofu Ndondo. Mtu huyo alitoa udhuru wa kutokuweza kuongoza ibada licha ya kuahidiwa mamilioni ya shilingi na kuombwa kusahau yaliyotokea kwa sababu yalikuwa ni madhaifu ya kibinadamu. Jina la Askofu Ndondo kwake lilikuwa ni kama ubini wa shetani. Mtu huyo hakuwa tayari kuona watu wengine wanaingia kwenye mikono ya Askofu Ndondo. Alitambua kuwa Askofu alikuwa ni mtu hatari. Mtu huyo alikuwa ameapa kwa maisha yake kumuangusha Askofu Ndondo haraka iwezekanavyo, kwa namna yeyote inavyowezekana, na mahali popote itakapowezekana. Aliamini Askofu Ndondo alikuwa ni Mjumbe wa Shetani.

(Itaendelea)
 
Twaisubir mkuu
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…