Enzi za mwalimu. Huwa najiuliza kati ya utamu wa kusoma kitabu au kutazama muvi ya kitabu nikikumbuka enzi hizo nadhani enzi ya vitabu utau ulikuwa mkubwa sana
"Oh! Tuliiarifu Interpol, lakini ilikuwa ni kazi bure. Kama nilivyosema, Kassim alikuwa hatulii mahali pamoja. Na inaaminika alukuwa na pasi kadhaa za bandia. Nilipoipokea telegram ya kutoka Kenya, nilishusha pumzi na kumshukuru Mungu. Nikalifunga faili lake."
"Unamaana ukikutana naye mitaani hutamkamata?" Bessy aliuliza.
"Huku nikijua anatuhumiwa kumgonga Dk. Makete?"
"Hapana kabla yake."
"Ningemfanya nini? Hivi sasa hata hao maafisa forodha na uhamiaji, na hao waliompa bidhaa hawataweza kupatikina kirahisi."
Dennis akauliza, "Ndio kusema inawezekana amerudi hapa nchini siku nyingi bila ya mtu yoyote kumjali?"
"Inawezekana kabisa kama kweli angali hai. Miaka zaidi ya ishirini ni muda mrefu Denny. Watu hubadilika. Watu husahau mengi. Mimi sidhani kama nitamtambua nikimwona. Isitoshe, bila shaka atakuwa amejipa jina jingine."
"Unazungumza kama vile unaamini kuwa upo uwezekano wa yeye kuwa angali hai?"
"Oh, upo kabisa. Siku hizi pesa zinaweza kufanya karibu chochote kile. Zinaweza kumfanya afisa wa polisi 'aokote' kitambulisho cha Kassim Hashir ndani ya gari lililopata ajali mbaya, na aamini kwa dhati kuwa marehemu ndiye Kassim Hashir. Hilo linaweza kutendeka kokote duniani, siyo hapa Afrika tu."
Baada ya kuukoleza mtemba kwa kuuvuta kwa nguvu, akamuuliza Bessy, "Umeshamfungulia faili?"
"Bado. Jina lake nimelipata muda mfupi tu uliopita."
"Nenda masjala ukamfungulie, kwa kosa la kijaribu kuua."
"Bessy akakibali kwa kichwa. "Nitafanya hivyo."
"Sidhani kama kuna lolote la kuongeza. Labda moja tu. Kuna mwandishi mmoja wa habari wa kujitegemea, Harold Chisimba, mbaye alisumbuliwa sana na Ibrahimu Mbelwa kwa sababu ya utafiti wake. Amekwishaandika kitabu....."
"Nimekisoma," alisema Bessy. "Nadhani ni mtu wa kumuona. Si tu anaweza kuwa na moja au mawili ya kuwaeleza kuhusu Kassim Hashir, bali anaweza kuwa hata na picha zake nzuri zaidi kuliko hii iliyomo ndani ya faili. Alikuwa mpiga picha mzuri sana."
"Tutampata wapi?"
"Anaishi Wazalendo Hotel, chumba namba nne.Ana hisa kubwa katika hoteli hiyo."
"Tutamtembelea." Alisema Bessy akiinuka. "Asante sana, Mzee Maliki."
"Karibuni tena." Wageni wake walipokuwa wakikaribia mlango akasema kwa kusita, "Bessy, una uhakika unaitaka kesi hii?"
"Una maana gani?"
"Naamini ni kesi ngumu na ya kutatanisha. Kassim Hashir...." Uso akiwa ameukunja, Bessy akamkatiza.
"Una hofu kuwa itanishinda?" Mzee Maliki akakubali kwa kichwa, macho chini.
"Kuna kesi yoyote ambayo imewahi kunishinda?" Bado akiangalia chini akatikisa kichwa.
"Hii ikinishinda," Bessy alisema kwa sauti kavu, "Nitajiuzulu."
************************************
Kembo aliliegesha gari lake karibu nusu kilomita mbali na Tupetupe Hotel, akateremke na kuelekea kwenye hoteli hiyo kwa mwendo wa taratibu, macho yake yakiangaza kijanja kila pembe kutazama kama palikuwa na ye yote mwenye shauku naye.
Tupe tupe ilikuwa ni hoteli yenye ghorofa nne, kukuu, iliyopendwa zaidi na wahuni. Mgahawa na baa na ukumbi wa dansi vilikuwa chini. Juu kulikuwa na vyumba vya kulala vya bei nafuu. Palikuwa na vyumba vya kitanda kimoja, vitanda viwili na hata vitanda vinne.
Kembo aliitembelea hoteli hiyo kwa nadra kadri alivyoweza. Na kila alipoitembelea alisita kwanza kabla ya kuingia ndani ya lifti yake iliyochakaa. Aliamini kwa dhati kuwa usingepita muda mrefu lifti hiyo ingeua. Lakini wakati mwingine wazo la kuhesabu ngazi hakuliafiki hata kidogo.
Lifti iliposimama salama na mlango kufunguka, Kembo alitoka na kwenda kwenye mlango wa chumba Namba 406. Akaugonga kwa kidole cha shahada na kusubiri kwa nukta tano. Kisha akagonga tena.
Mlango ukafunguliwa na kijana wa miaka thelathini mwenye nywele nyingi aliyebana sigara kwenye kona ya mdomo. Uso wake umepooza lakini alipomwona Kembo ukachanua.
"Za hapa, Chiko?"
"Safi, Bwana Kembo." Sauti yake alikwaruza, itakayo kooni. "Karibu." Kembo akaingia mlango ukafungwa.
Chumba hicho kilikuwa kimoja kati ya vyumba vizuri vya hoteli hiyo. Kilikuwa kidogo kipana chenye vitanda viwili, meza moja duara, viti viwili na kabati la nguo. Vijana wawili walikuwa wameketi vitini. Mmoja alikuwa mdogo kuliko Chiko, mwingine kigogo mkubwa. Mezani palikuwa na karata, pesa, chupa za pombe, paketi za sigara na kisahani cha kuwekea vishungi na majivu ya sigara. Chumba kizima kilijaa harufu ya moshi wa sigara, licha ya madirisha kuwa wazi na pangaboi juu kuzunguka.
Baada ya kuufunga mlango na kugeuka, Chiko akasema, "Fensy, Hoza, kutaneni na Bwana Kembo." Vijana hao waliitika kwa vichwa. Walikuwa na nyuso kavu kuliko umri wao.
Hoza aliekuwa mdogo, akainuka, akisema, "Karibu kiti Bwana Kembo." Yeye akaenda kuketi kitandani.
"Hapana, asante," Alisema Kembo, naye akijiwashia sigara. "Sina muda. Sitaketi." akapuliza moshi na kusema, "Chiko, umefanya kazi nzuri. "Umewezaje kupata habari kamili vile, tena katika muda mfupi tu?"
"Dadangu ni Nesi."
"Umesema hali yake ni mbaya, una maana hatapona?"
"Miriamu hakufafanu. Alichosema ni kwamba amefanyiwa operesheni ya hali ya juu ambayo hajapata kuiona."
Kembo akapuliza moshi. Akasema "Chiko, Dk. Makete ni adui yetu mkubwa. Akipona, tumekwisha. Lazima tuhakikishe haponi."
"Hiyo ni kazi ndogo kama kutafuna biskuti." Alisema Chiko. "Hata Hoza anaweza kuifanya."
"Anacho kibweka?"
"Kipo." Alijibu Hoza mwenyewe. Akainama na kuchomoa bastola kwenye soksi ya mguu wa kulia. Akaiweka mezani.
"Ina sailensa?" Hoza akatikisa kichwa. "Haina."
"Nitakupatia moja yenye sailensa." Kembo akatoa pochi nene na kulifungua. Akatoa kitita na kumkabidhi Chiko, akasema. "Utajua jinsi ya kugawa." Akamtazama kijana mdogo . "Hoza ukitenda kazi tuliyozungumza nitakupa milioni."
"Fanya milioni mbili, mzee." Akasema Hoza. "Si kazi ndogo kama anavyodhani Chiko."
"Ok. Lini?"
"Hata leo usiku."
"Good."
*******************************
Wazalendo Hoteli ilikuwa ghorofa moja, lakini ilichukua eneo kubwa. Ilikuwa Hoteli ya heshima. Harold Chisimba aliwakarisha wageni wake kwenye chumba alichokifanya sebule na ofisi yake, kilichopakana na chumba chake cha kulala.
"Mimi ni Luteni Dennis Makete, na huyu ni Kachero Inspekta Bessy. Tumeelekezwa kwako na Kamishna Msaidizi...."
"Nafahamu." Akamkatiza Chisimba. "Malik amenipigia simu na kuniarifu. Ameniambia niwape msaada wowote niwezao kuwapa kuhusu Kassim Hashir."
"Tushukuru sana Bwana Chisimba." Alisema Bessy.
"Sawa. Je niwapatie kiburudisho gani?"
Denny akasema haraka. "Hapana, hapana Bwana Chisimba. Asante sana."
Chisimba akainua mikono, kumaanisha 'mpendavyo.' Akasema, "Ni nini hasa mnachotaka kufahamu? Simuni Malik hakufafanua. Amesema mnaamini Kassim angali hai, na kwamba kuna mtu amemgonga na gari na kukimbia."
"Amemgonga babangu, Dk,Raymond Makete, leo asubuhi. Tunaamini amemgonga kusudi."
"Dk.Makete?" Chisimba akafinya uso kuwaza. Akasema, "Oh, ndiyo! Namkumbuka. Imekuwaje?"
"Hatujui chochote." Alijibu Bessy, "Mzee Makete aliondoka nyumbani kwake akiwa mzima kabisa. Aliaga anakwenda benki kuchukua pesa. Pesa asichukue. Kassim alimgonga wakati anatokea benki. Tena kamgonga kusudi."
"Mna hakika ni yeye aliemgonga."
"Mzee Makete mwenyewe alisema, alipozinduka kwa nukta chache."
"Ajali iliyomwua Kassim ilipotangazwa, niliwaambia watu kuwa ajali hiyo ni bandia, lakini wengi waliniona mpuuzi."
"Kwa hiyo uko pamoja nasi?" Dennis aliuliza. "Yaani katika kuamini Kassim angali hai?"
"Kabisa. Sikiliza. Laiti mimi ningekuwa ndiye Kassim ningefanya kama alivyofanya Kassim. Ningebuni ajali ya bandia."
Dennis na Bessy wakakubali kwa vichwa. "Lakini kwa nini atake kumwua babaangu?" Dennis aliuliza.
"Sijui." Alisema Chisimba, akajiwashia sigara, baada ya wageni wake kukataa karibisho lake la kuvuta. Kisha akasma ghafla, "Oh,subiri! Haiwezi kuwa kwa ajili ya lile tukio?"
"Tukio gani?" Denny na Bessy waliuliza kwa pamoja.
"Zaidi ya miaka ishirini na tano iliyopita, wakati wa utawala wa Mbelwa, Dk. Makete aliamini Kassim alimwua babake. Lakini hakuweza kufanya lolote kwa sababu Kassim na Mbelwa walikuwa marafiki. Akanieleza mimi, akidhani kuwa ningeweza kufanya lolote, kwa vile ni mwandishi. Nilipojaribu kufuatilia nikawekwa ndani."
Bessy aliwaza kidogo kisha akatikisa kichwa. "Hiyo haiwezi kuwa sababu ya kutaka kumwua mtu, tena kwa gari. Kwa nini asijaribu mapema? Hata hivyo nitalifuatilia tukio hilo. Ni nani wa kunisaidia ?"
"Dk. Makete mwenyewe." Alijibu Chisimba. "Au mkewe. Kwani yeye alikuwa nesi hapo hospitali wakati huo."
JamiiForums uses cookies to help personalise content, tailor your experience and to keep you logged in if you register.
By continuing to use this site, you are consenting to our use of cookies.