SEHEMU YA KUMI NA TISA.
Kembo alikuwa anatoka bafuni kuoga, kengele ya simu ilipolia sebuleni. Akajifunga taulo vizuri na kuokota mkono wa simu. Akasema, "Yees?"
"Mzee, mimi ni chiko."
"Kitu gani asubuhi yote hii?" Kembo aliuliza kwa ikirahi, akijua ni masula ya pesa tu.
"Mzee, lazima nikuone. Mambo si mazuri." Alijibu chiko.
"Unamaana gani?"
"Hoza amekufa. Na Dikwe ameliwa na fisi baada ya kutekelezwa Uwanja wa Gofu. Bila ya shaka alihojiwa."
"Ndiye nani huyo Dikwe?"
"Rafiki yake Hoza." Alijibu Chiko, akipumua kwa nguvu. "Jana usiku polisi walikwenda Tupetupe Hotel. Wakakipekua chumba cha Hoza na kuwahoji mapusha na maguberi kadhaa. Sisi hatukulala tupetupe, kwa kuhofia wanaweza kurudi."
"Uko wapi sasa hivi?"
"Karibu na soko kuu."
"Umeshafungua kinywa?"
"Bado."
"Nenda Pundamilia Inn, kijichumba namba nane, agiza utakacho. Muhudum akikwambia hicho ni kijichumba maalumu, nitaje mimi."
"Sawa mzee."
"Nitakuwa nawe baada ya dakika kumi au kumi na tano." Alisema Kembo na kuikata simu.
Akabonyeza namba aliyoizoea. Sauti nzito ya Kassim Hashir ikasema, "Yees?"
"Bwana Kessy, ni Kembo hapa."
"Unasemaje?"
"Unatazamia kutoka asubuhi hii?"
"Siyo kabla ya saa nne. Kwani vipi?"
"Kijana wangu mmoja amenipigia simu sasa hivi. Anashuku mambo si mazuri."
"Mabaya kiasi gani?"
"Siwezi kusema mpaka nikutane na kuzungumza naye. Nitamwona baada ya robo saa hivi."
"Unanishauri vipi? Niyeyuka?"
"Hapana , ni mapema mno kwa hatua kama hiyo. Haitatokea haja ya kuchukua hatua kama hiyo. Sioni kwa nini nishindwe kuyadhibiti mambo. Pengine Chiko anataka kutaharuki bure. Pengine anataka kunifanya fal@ anipune kuliko tulivyopatana."
"Sasa unanishauri nini?"
"Tulia. Nitakuja mara tu baada ya kuzungumza na huyu kijana."
"Vizuri"
*************************************
Miezi mitatu au minne ikapita. Kisa cha roba karne kikaendelea. Ndipo Bwana na Bibi Makete walipomona tena yule msichana. Na ndipo walipolijua jina lake Asha Rajabu.
Safari hii hakwenda hapo hospitalini kwa miguu yake, bali kwa ambulance, na kukimbizwa thieta kwa machela, akiwa na majeraha mawili mabaya kwenye tumbo lake lililo fura.
Siku hiyo Dr. Makete na mkewe walipangiwa shughuli za thieta. Wao na msichana huyo walikuwa kama waliopangiwa na Mungu mara hizo mbili.
Mambo yakawa haraka haraka. Wataalamu wa vyombo vya upasuaji, Dk.Makete, mkewe... kila mmoja alikuwa kama cherehani cha umeme.
Ni wakati akimwandaa kwenye meza ya upasuaji ndipo Bi. Makete akamtambua yule msichana. Akaguta, "Ray! Ray! Ni yule msichana wa Kassim Hashir!"
"Ndyo." Akakubali yule msichana kwa sauti dhaifu.
"Ndiye mimi Asha Rajabu."
Kila jozi ya macho ikaenda mezani. Dk. Makete akajongea kando ya meza, huku akiendelea kuvaa glovu za kupasulia. Akasema, "Gosh! Ni yeye!" Kisha akameuliza , "Imekuwaje tena mama?"
"Kassim kanipiga kisu." Alijibu Asha.
"My God! Nilikwambia usirudi kwake!"
"Baba kanifukuza nyumbani. Nilihitaji nauli niende kwa mjomba." Alisita akikusanya pumzi, kisha akaendelea. "Mimi sijali kufa. Lakini mwanangu... angali hai. Tafadhali..."
"Nitahitaji kuwaokoa nyote."
Bi mkumbwa akashusha pumzi na kuendelea. "Operation ikaanza. Ilikuwa ngumu kuliko tulivyotazamia. Ray akapambana nayo kwa karibu masaa mawili mazima."
Akatikisa kichwa. "ilikuwa kazi bure. Wote tuliokuwa humo ndani tulijua kazi bure. Kisu kilikata sehemu mbili nyeti sana. Afadhali ingekuwa sehemu moja. Lakini sehemu mbili , ilikuwa ni operesheni tata ajabu. Lakini Ray hakukubali kushindwa. Wote alitushangaza. Alifanya kazi isivyo kawaida, huku akivujwa jasho usoni. Mungu peke yake ndiye anyefahamu idadi ya vitambaa nilivyovitumia kumfutia jasho."
Bi mkubwa akatikisa tena kichwa. "Ilikuwa kazi bure. Mtu wa kwenye mashine ya mapigo ya moyo aliita mara tatu. 'Dokta... Dokta ... Dokta ...lakini aliendelea tu kushughulika. Kakata hiki, kaunga hiki, katoa hiki, kasafisha hiki... Ikanibidi nimshike bega na kumwambia, 'Ray, it's all over. She is gone! She is dead.'
'God! Ooh Lord! It is horrible!' Ray aliduwaa kama asiyeyaamini macho yake. Msichana yule alikuwa kama ... kama mtu anayemhusu - anaetuhusu kwa karibu sana.
Kwa mara ya kwanza na ya pekee - nikamwona Ray akitokwa machozi, tena hadharani. Sikuweza kujizuia. Hakuna alieweza kujizuia humo chumbani."
Bi mkubwa akatoa leso na kupenga .
Denny akauliza kwa sauti kavu, "Huyo mnyama hakufanywa chochote?"
"Jesus, Denny!" Bessy akaguta. "Badala ya kuuliza habari za yule mtoto!"
"Habari za yule mtoto nazifahamu."
"Are you joking?"
"No, I am bloody not."
Bi mkubwa, kama vile vijana hao hawakusema lolote, akasema, "Kassim Hashir afanywe nini? Nani kati yetu athubutu kushitaki? Na hata kama tungeshitaki, asingefanywa lolote, alikuwa kama nusu - Mungu. Tungejitafutia matatizo ya bure tu."
"Mama," Bessy akauliza kwa sauti ndogo, "Nini matokeo ya mtoto wa Asha, alinusurika au nae alikufa pia?"
"Hapana, yeye alinusurika, mtoto wa kiume mwenye afya nzuri. Kisu kilimkata begani na takoni. Tukamshona na kumfunga. Hadi leo anayo makovu hayo. Atakufa nayo."
Mabega ya Bi mkubwa yakaanza kucheza kabla ya sauti kusikika. "Atakufa nayo." Alirudia. "Atakufa nayo."
Denny akaenda kumshika bega.
"Mama umesema mwenyewe kipindi cha machozi kimepita."
Itaendelea