SEHEMU YA ISHIRINI NA TATU.
"Akh, huoni kuwa tunazungumza kama machizi wawili?" Sam Kembo aliuliza kwa karaha. Kassim Hashir akainua mabega. "Ni wewe uliyeleta kauli ya kutishana. Sijui jeuri hiyo umeitoa wapi?"
Akaliweka sigara lake mdomoni na kulivuta kidogo. Akaendelea, "Ukitaka tukubaliane na ukweli, ukweli ni kwamba mimi na wewe tunahitajiana. Mimi nakuhitaji wewe, na wewe unanihitaji mimi zaidi kuliko mimi ninavyokuhitaji wewe."
Kembo akajiwashia sigara nyingine. Akasema, "Ukweli ni kwamba sote tumo ndani ya lindi la choo, na ni wewe uliyenitumbukiza humo."
"Kwa ujira na ridhaa yako mwenyewe." Kembo akatahayari na kuyatazama maji ya bwawa yaliyong'arishwa na jua la asubuhi. "Jambo la busara kufanya sasa ni kujitoa katika lindi hili." Aliendelea Kassim. "Naamini tunaweza kufanya hivyo iwapo tutavitumia vizuri vichwa vyetu. Hebu tuangalie tatizo moja moja. La kwanza ni huyo Daktari mstaafu ambaye angali hai na analindwa masaa ishirini na nne."
"Ndiyo,lakini yuko taabani. Sidhani kama anaweza kusema lolote la maana leo au kesho. Na akisema amegongwa na Kassim Hashir sidhani kama watamsadiki. Kassim Hashir alifia huko Kenya miaka kadhaa iliyopita. Ulimgonga bure kabisa yule mzee."
"Nakwambia nakubali nilifanya kosa. Nakwambia nilitaharuki. Wewe hujawai kutaharuki? Na mahali penyewe palikuwa pazuri. Uchochoro ulikuwa mtupu kabisa. Na sikutazamia kama angepona. Laiti angekufa palepale mambo yengeishia pale pale. Hata wewe yasingekuhusu."
Kembo akatikisa kichwa. "Hapana, rafiki yangu, siyo kutaharuki kulikokufanya umpamie yule mzee. Wewe una asili ya ujahili. Wewe husikia raha kujerui, kuumiza, kutoa roho. Wapo watu wa aina hiyo. Wawili wengine niliotokea kuwafahamu walikuwa Hitler na Iddi Amin."
"Ah, ya Hitler na Idd Amin tuwaachie Hitler na Iddi Amin. Tuangalie yetu. Ya kwetu yanatutosha bila kujitwisha ya wengine."
"Enhe,tatizo la pili?"
"Tatizo letu la pili liko kwa huyo Fensy. Si umesema akibanwa na kutikiswa kidogo anaweza akayaleta mambwa hadi hapa?"
"Kwa nini usihame hapa?"Kembo aliuliza. "Kwa nini usiliuze jumba hili na kununua au kupanga mahali pengine?"
"Sam, wakati mwingine huwa unazungumza kama mtoto mdogo."
"Kwa nini?"
"Tatizo langu sio dogo kiasi hicho. Tatizo langu sio kujificha tu. Tatizo langu ni kungundulika mimi ni nani."
"Yaani kujulikana kuwa wewe ndiye Kassim Hashir?"
"Hapana, kujulika Habib Kessy ndiye nani."
"Mbona sikuelewe!"
"Unaijua kampuni iitwayo H.K. International?"
"Nani asiyeijua? Ni kampuni kubwa ya kimataifa inayouza magari ya Kijapani na bidhaa toka Ulaya." Akapiga pafu jingine refu la sigara kisha akaupuliza hewani moshi huku akiutazama unavyoyeyuka hewani, macho kayaminya. Kisha akaendelea, "Na inapeleka bidhaa Ulaya toka Afrika, kama vile pamba,buni, tumbaku na hata dhahabu na madini mbali mbali." Kembo alisema.
"Swadaktaa!" Kassim aliitikia na kuuliza, "Je, unamjua mwenye kampuni hiyo?"
"Hapana, simjui."
"Mwenyewe ni H.K." Kembo akabaki na sura ya kifal@fal@.
"Sam," Kessy akamwita, "Bado tu hujazibuka masikio?"
Ghafla Kembo akakunja uso. Akasema, "Kess - Habib, unataka kunambia, kunambia..." Kassim akakubali kwa kichwa.
"Mungu wangu - Ka!"
"Sawa kabisa. Hicho ndicho kizingiti chenyewe. Hata mwenyewe wakati mwingine hunitoka." Kembo akatikisa kichwa akisema, "Nilijua kuwa wewe una pesa, lakini kha! H.K. Habib Kessy! H.K.Internatioal! Nani angetegemea? Kha!
"Ibrahim Mbelwa alikuwa rafiki yangu mkubwa, pamoja na kunizidi umri kwa miaka kumi." Kassim alisimulia, "Ajabu yenyewe ni kwamba tulikutana dansini, wakati huo nikiwa ningali nasoma Chuo Kikuu,na yeye akiwa Sajini meja Jeshini. Alipenda sana wasichana warembo 'dogodogo' kama mimi, lakini yeye alikuwa hajui kutongoza, ambapo mimi nilikuwa kama sumaku kwa wasichana. Hivyo tukawa marafiki wakubwa.
"Mbelwa alipopora madaraka na kujitangaza Rais, hapakuwa na mtu mwingine aliyemwamini kuliko mimi. Akanifanya waziri nisiye na wizara maalumu. Kazi yangu kuu ilikuwa kutafuta fedha za kigeni kwa njia yoyote ile na kuzipeleka Ulaya. Kazi hiyo aliyonipa niliifanya vizuri sana." Kassim aliendelea "Katika miaka michachealiyotawala kimabavu nilitorosha mamilioni ya Dola, Pauni na kila pesa ya kigeni yenye kuthaminiwa kimataifa.
Na wala sikuziacha zitulie benki. Nikaanzisha H.K.International. Sikuwa na nia mbaya. Siku yoyote Ibrahim ingehitaji pesa ningempatia, na faida juu. Hata kwa kuiuza au kuiua hiyo kampuni, kama unavyojua, aliuwawa alipopinduliwa. Na kibunda chote kikawa changu peke yangu. Naam. Peke yangu kabisa."
Kembo akapumua kama aliyetua mzigo na kusema, "Una mwiko wa kutokunywa asubuhi? Kisa chako kimenikausha koo. Kha! Kuna mijitu yenye bahati duniani!"
Kassim akatabasamu. "Na wala si asubuhi tena." Akasema, akiitazama saa yake, Rolex ya dhahabu. "Inakaribia saa tano. Kinywaji changu cha saa hizi ni Gin na Tonic. Je, na wewe utatumia kinywaji gani?"
"Hiyohiyo Gin na Tonic itatosha."
Kassim akaita, "Kijana!" Mara mtumishi akatokea. "Jin na Tonik tafadhali." Kassim akamwambia.
Baada ya huyo mtumishi kuleta chupa ya Jin na chupa mbili za soda chungu na kuondoka, Kembo akauliza, "Sasa tatizo lako liko wapi?"
"Nyumba hii niliinunua kabla ya kurudi hapa nchini." Alijibu Kassim. "Aliinunua wakili wangu kwa niaba ya H.K.International. Hivyo, hata kama sipo, polisi wakiivamia watagundua kuwa nyumba hii ni mali ya kampuni hii."
"Kwa hiyo?"
"Sisemi kwamba polisi wetu wana mbongo zinazovuja masikioni. Lakini anaweza katokea chakaramu mmoja akaweka mbili na mbili na kupata jibu sahihi, yaani nyumba hii ni ya H.K.International. Na anayeishi hapa ni Habib Kessy."
"Kwani pana ubaya gani ikigunduluka Habib Kessy ndiye mmiliki wa H.K.International?"
"Lahaula! Sam, mpaka nikuchoree picha? Iwapo yule Daktari atasema kagongwa na Kassim Hashir, na kama polisi watagundua kuwa Kassim Hashir anaishi hapa, watagundua kuwa Habib Kessy ndiye Kassim Hashir. Na wakigundua kuwa Habib Kessy ndiye Kassim Hashir nimekwisha."
"Kivipi?"
"Kila kitu. Vile Kassim Hashir alikuwa akitafutwa na serikali ya nchi hii kwa kuhujumu uchumi na kutorosha fedha za kigeni na kuwa ndiye aliyesababisha vifo vya watu wawili watatu enzi zile - na sasa kuna shitaka jingine la kujaribu kuua kwa gari. Si tu kuwa nitakuwa na kesi mbaya ya kujibu hapa bali hata Interpol itaingilia kati jambo ambalo litasababisha kuchunguzwa kila tawi la kampuni yangu Afrika na kote duniani. Matokeo yake akaunta zangu zote popote ziliko zitapigwa tanchi. Hakuna cha kutoka, ila kuingia tu. Na mimi mwenyewe nitasakwa kila pembe ya dunia na hali nikiwa hohe hahe. Kwani kifedha, rafiki yangu mpendwa Sam, mimi na wewe tutakuwa hatuchekani."
"Gosh, Kessy, sikujua kuwa mambo yanaweza kuwa mabaya kiasi hicho."
"Sasa unaona kwa nini jana nikataharuki na kumgonga yule mzee? Picha ya kupatikana kwangu ilinijia mbele ya macho yangu. Ni miaka mitano sasa tangu nirejee nyumbani, baada ya kuhakikishiwa na watu kadhaa, mmojawapo akiwa bosi wako, kwamba nimeshasahauliwa kikamilifu. Kuwa asingetokea mtu mwenye shida na mimi. Sasa katokea mtu huyo.Basi ni dhahiri wapo wengine, isipokuwa wanaamini nimeshakufa. Wakizibuliwa masikio watajitokeza. Watataka wanikodolee macho na kunitoboa kwa madole yao ya shahada."
Baada ya kugida, Kassim akaendelea. "Nimekueleza yote hayo ili ujue hali halisi na msimamo ulivyo. Mimi ni mtu mhimu sana katika chama chenu na mstakabali wa taifa hili. Huwezi kuniongopea kuwa kuna mfadhili mwingine anayewasaidia au atakaeweza kuwasaidia kama ninavyowasaidia mimi. Hivyo nikiyoyoma ujue nchi imekwisha. Mmekwisha kabisa.Nyote kaputi."
*************************************
Baada ya kimya kifupi, kachero Inspekta Bessy akasema, "Tatizo lako Butu ni kuwa hujui kuongopa. Ni dhahiri kabisa kuwa wewe hukuondoka hapo kwa shangazi Suzy kwa sababu ya kujisikia ovyo. Inaelekea palitokea kutoelewana kati yako na Bob au na Kikoti. Au na huyo shangazi."
"Hataa..." Butu alijaribu kukanusha,akiangalia chini, lakini sauti yake ilikuwa ndogo na isiyo na nguvu.
"Je, Bessy akauliza, "Ni kuhusu hiyo chupa ya wisk ya wizi?"
Butu akakawia kujibu, Denny akasema, "Wewe ulijuaje kuwa chupa hiyo ni ya wizi, au Kikoti mwenyewe aliwaeleza hivyo, na hali mkiwa askari? Au hakujua kuwa ninyi ni askari?"
"Nadhani alijua."
"Hata hivyo bado akajigamba kuwa chupa hiyo kaiiba?"
"Yeye hakusema kaiiba, ila mimi nilishuku tu."
"Kwa nini?"
Butu hakujibu.
"Yeye alisema kaipata wapi?"
"Alisema kapewa."
"Na nani?"
"Na... na tajiri yake."
"Lakini wewe hukuamini?"
"Sikuamini."
"Kwa nini?"
Butu hakujibu.
"Kwani wisk ilikuwa ya aina gani?"
"Sijui, sikumbuki. Ni ya kutoka ng'ambo."
"Ghali?"
"Bob alisema ilikuwa ghali sana."
"Ilikuwa chupa ya ukubwa gani?"
"Ya wastani."
"Ilikuwa nzima, au ilikuwa imeshafunguliwa?"
"Ilikuwa imeshafunguliwa. Ilikuwa nusu chupa."
"Na wewe ukashuku kuwa kaiiba?"
"Ndiyo."
"Hicho ndicho kilichokuondoa hapo?" Denny aliuliza.
Butu akasita kisha akakubali kwa kichwa.
Bessy akatikisa kichwa. "Bado tuko mbali kabisa," Alisema akaita, "Butu, acha nikukumbushe tena Hii ni kesi ya mauaji. Sijui kama sababu iliyokuondoa hapo kwa shangazi Suzy ina uhusiano au haihusiani na kuuawa kwa Bob na Kikoti, lakini ni kazima nijue. Hivyo hutoki humu ndani mpaka umenieleza."
Ikapita dakika nzima ndipo tone la kwanza likamdondoka Butu, huku akisema, "Niliwakataza ! Naapa niliwakataza! Lakini hawakunisikia!"
Deny na Bessy wakatazamana na kuafikiana kwa macho. Wakampa Butu dakika tatu za kutanua mbavu, kupenga na kujifuta uso. Kisha Bessy akamwamuru, "Anza tangu mwanzo."
Lakini zikapita dakika tatu nyingine, ndipo Butu alipoweza kujizatiti kikamilifu. Akainuka, akasimama mbele ya meza ya Bessy na kupiga saluti ndefu. Kisha akaivua kofia na kuiweka mezani. Akauvua mkanda na kuuweka mezani. Akazivua V na kuziweka mezani, kisha akarudi kuketi na kuanza kuzungumza.
Itaendelea.