Riwaya: Msako wa Hayawani

Riwaya: Msako wa Hayawani

SEHEMU YA ISHIRINI NA NNE



"Ninachohitaji ni muda." Kassim Hashir aliendelea. Muda wa kubadili kila kitu. Kumuua Habib Kessy na kampuni yake na kuibuka mtu mpya na kampuni mpya yenye shughuli tofauti kabisa na shughuli za H.K.International."
"Utaweza kufanya hivyo?" Kembo akauliza.
"Kwa nini nisiweze. Iwapo kwanza nilikumuua Kassim Hashir? Ninachohitaji ni muda tu."
"Muda gani?"
"Mimi kugeuka mtu mwigine si tatizo. Nina paspoti nyingine maalum kwa dharura kama hii. Lakini kuuza na kufungua kampuni nyingine kubwa kama H.K.International na akaunta zake kutachukua muda."
"Ndiyo. Muda gani?"
"Kwa vyovyote vile siyo chini ya mwezi mmoja, pengine miwili."



"Jesus!"
"Jambo hili limetokea wakati mbaya sana. Tatizo ni kwamba kwa sasa ninabidhaa nyingi kuliko fedha taslimu. Na bidhaa nyingine ziko njiani. Kuna meli nzima ya makontena toka Ulaya bado haijawasili. Kuna meli nyingine ina magari zaidi ya miambili kutoka Japani iko njiani. Meli nyingine mbili zina malighafi toka Afrika bado hazijatia nanga Ulaya. Vitu vyote hivyo vina thamani ya mamilioni kwa mamilioni kama si mabilioni ya pesa za kigeni. Na sina ujanja hadi vifike vinakokwenda. Kama ni Mungu amepanga jambo hili litokee wakati huu ni yeye pekee anayejua. Nahitaji muda vibaya sana."


"Mambo yakituchachia," Kembo akasema. "Hapatakuwa na muda wowote."
"Hayawezi kutuchachia iwapo tutavitumia vichwa vyetu wenyewe vizuri. Wa kuwashughulikia ni wawili tu. Fensy na huyo Daktari mstaafu."
"Umemsahau mtu wa tatu."
"Mtu wa tatu?" Kassim aliuliza.
"Ndiyo. Huyo kijana X aliyempeleka Dikwe Uwanja wa Gofu."
"Oh!"
"Lakini yeye si tishio. Kamuonea Dikwe kwa sababu Dikwe alikuwa pusha wa kawaida tu, tena mwanafunzi aliyetegemea kisu. Hakuwa katika daraja la Chiko na Fensy."
"Kwa hiyo?"
"Ni moja kati ya mawili kwa kijana huyo. Anunuliwe au alipuliwe chaguo ni lake."
"Kwa hiyo tatizo liko kwa Dokta Makete ?" Kassim aliuliza.
"Hapana. Tatizo lipo kwa Fensy. Ni kweli akishikwa mambo yanaweza kuwa mabaya."
"Kwa nini asifikwe na 'ajali'?"
"Nitafikiria. Kwa sasa atapiga mbizi. Sitaki kupoteza wangu ovyo. Nilipo nina pengo la mmoja."
"Hoza."
"Ndiyo."


Baada ya kupuliza moshi angani, Kassim akasema, "Umesema huyo Dk .Mstaafu si tatizo?"
"Si tatizo. Nilifanya kosa pale mwanzo kumtuma Hoza aende hospitalini na kibweka. Nilipaswa kumpeleka Daktari wa bandia."
"Na sindano ya sumu?"
"Yes."
"Good. I'll fix you up with BMV - Black Mamba Venom. Hutumiwa na Vets [Madaktari wa wanyama] kuwaulia mbwa,farasi n.k. wenye maumivu makali ambao hawana matumaini ya kupona. Ni safi sana. Sekunde thelathini, garantii."


*****************************


Kwa sauti madhubuti kabisa Butu akasema, "Humo chumbani mwa shangazi mna radio. Katika taarifa ya habari ya saa kumi ilitangazwa ajali ya Dk.Makete. Ikatangazwa ile zawadi ya milioni moja kwa yeyote atakayemtaja mtu aliyemgonga Dokta huyo. Kikoti akapandwa na jazba, akidai anamfahamu mtu huyo. Na kuwa ndiye mwajiri wake. Akatuomba tumsaidie kuipata hiyo zawadi."


Bessy na Dennis wakatazamana, macho ya msichana huyo yakiwaka moto kwa ghadhabu. Dennis akarudisha macho kwa Butu na kumwambia, "Endelea."
"Bob akaingiwa na tamaa. Akataka kujua kama huyo mwajiri wake alikuwa tajiri wa kuweza kutoa milioni mbili au tatu za kufumba mdomo. Kikoti akamhakikishia kuwa ni tajiri sana, na kwamba angeweza kutoa hata zaidi. Bob akasema basi ya nini kudai milioni ikiwa wanaweza kupata milioni mbili au tatu.
"Nikajaribu kuwakataza." Butu akaendelea, "Naapa niliwakataza, lakini hawakukubali. Bob akanambia niachane nao na nisimwambie mtu yeyote. Nikaondoka na kuwaacha."


Bessy akatikisa kichwa. "Butu, Butu, Butu! Na ukabaki kimya kweli!"
"Ningefanyeje, afande? Bob alikuwa rafiki yangu mkubwa. Nisingeweza kumsaliti. Lakini baada ya kuwaza usiku kucha nilipania kumlazimisha aje kukuona asubuhi. Angekataa, mimi ningekuja kuripoti. Lakini asubuhi hakuwepo nyumbani kwake. Na nilipofika hapa kituoni nikapata habari kuwa kauwawa. Nikapapatika, nisijue la kufanya."
"Unajua ni lazima nikuweke ndani na kukufungulia shitaka la kuficha siri za uhalifu?" Butu hakujibu. "Kwa vyovyote vile" Bessy akaendelea, "Umeshakwishapoteza kazi yako. Hustahili kuwa askari."


Denny akauliza, "Ni nani huyo mwajiri wa Kikoti?"
"Simjui." Butu akajibu kinyonge. "Kikoti alimwita Bwana Kessy. Jina hilo moja tu."
"Kwa hiyo uliongopa uliposema hakuwa na kazi maalumu?" Bessy akauliza.
"Hapana hata kwa huyo Bwana Kessy nadhani alikuwa kibarua tu. Hakuwa na muda mrefu hapa jijini."
"Alikuwa anafanya kazi gani kwa huyo Kessy?"
"Nadhani alikuwa mtumishi wa nyumbani."
"Sehemu gani hiyo?"
"Nadhani itakuwa Buffalo Hill."
"Nadhani. Nadhani. Nadhani. Ni msaada mkubwa kweli kweli !" Bessy alifoka. Akaongeza, "Na alipokuwa akiishi Kikoti hukujui?"
Butu akatikisa kichwa.
"Ona sasa! Katika kuogopa kumsaliti ndugu yako, umeyaponza maisha yake!"
"Najuta sana, afande, najuta sana."
"Majuto ni mkuu." Bessy alisema kwa ghadhabu.
"Hayasaidii chochote. Angalia ulivyoboronga! Tulikuwa na nafasi ya kuwabamba wote. Huyo aliyemgonga Dk.Makete, hao wauaji, huyo Bob pamoja na Kikoti wake. Na sasa tuko wapi? Pale pale tulipoanzia!"


"Butu," Denny aliita kwa sauti tulivu kabisa. "Unadhani kitu gani kilitokea pale kwa shangazi Suzy baada ya wewe kuondoka?"
"Sijui,Luteni."
"Hukuisikia mipango ya Bob na Kikoti?"
"Hata kidogo. Sikutaka kujihusisha na mipango ya kifumba mdomo."
"Afadhali ungesuburi uisikie mipango yao pengine tungejua anapoishi huyo mlaaniwa!" Bessy alilalama.


Kama vile msichana hakuwa amesemalolote, Denny akaendelea kwa sauti yake tulivu. "Tunafahamu kuwa mtu aliyemgonga ni Kassim Hashir, lakini anatumia jina jingine. Jina Kassim Hashir lilishakufa siku nyingi. Umenielewa Butu?"
"Ndiyo, Luteni."
"Sasa, kama mwajiri wa Kikoti ndiye aliyemgonga babangu na naamini ndiye, ama sivyo Bob na Kikoti wasingeuwawa. Na kama mwajiri wa Kikoti anaitwa Kessy,basi ndiye Kassim Hashir. Sawa Butu?"
"Sawa, Luteni."
"Ni jambo linalofahamika dhahiri kuwa Kassim Hashir, kwa jina jingine Kessy ni mtu mbaya kweli kweli. Ni mnyama. Na anawakora wauaji. Watatu tunawafahamu. Chiko,Fensy na Hoza. Huyo wa tatu sasa ni marehemu. Inspekta Bessy akamuwahi. Je, haikujii akilini mwako kuwa waliowaua Bob na Kikoti ni Chiko na Fensy?"
"Inawezekana kabisa." Alikubali Butu.


Denny akamtazama Bessy na kumwambia, "Tafadhali uliza chumba cha kumbukumbu kama wana faili la Fensy" Bessy akainua simu na kuzungumza na masijala. Kisha akaurudisha chini mkono wa simu,akitikisa kichwa. "Hawana."
"Si kitu." Alisema Denny. "Waambie makachero wako waanze kuwasaka Chiko na Fensy."
Bessy akainua tena mkono wa simu.


Itaendelea
 
Hapa nisimama nataka kwenda polisi wangapi mtakuwa mashahidi wangu kuwa idawa anatucheleweshea story halafu akileta analeta kidogo? Upo juu mkuu
 
Hapa nisimama nataka kwenda polisi wangapi mtakuwa mashahidi wangu kuwa idawa anatucheleweshea story halafu akileta analeta kidogo? Upo juu mkuu

Hahahaha! Usimpeleke bhn! Aliyotupa leo si haba!
 
Hapa nisimama nataka kwenda polisi wangapi mtakuwa mashahidi wangu kuwa idawa anatucheleweshea story halafu akileta analeta kidogo? Upo juu mkuu

Episode inayofuata hadi wkend ijayo
 
Muheshimiwa idawa itanipa wakati mgumu sana kama leo hii story haitaendelea kwakweli maana sio vyema
 
Hahahaha! Mwenzenu mi nishazowea! Nikikuta hamna kitu nachomoka zangu mdg mdg!
 
SEHEMU YA ISHIRINI NA TANO.



Walikuwemo watu watatu katika gari la Kembo. Yeye Kembo mwenyewe, akiendesha na Chiko aliyeketi kando yake, na Fensy aliyeketi kiti cha nyuma.
"Tumejadili kwa kirefu swala hili na Bwana Kessy." Alisema Kembo, "Na kufikia maamuzi kadhaa. Jambo mhimu ni kwamba ni lazima mjihadhari. Kama Dikwe amewataja, mnaweza kuwa mnatafutwa na polisi."

"No sweat." Alisema Chiko. "Haitakuwa mara yao ya kwanza kunitafuta. Na kunikosa."
"Hata hivyo ni lazima mjihadhari." Alisisitiza Kembo. "Msizurure ovyo. Chiko, bila shaka picha yako wanayo. Fensy je?" Fensy akatikisa kichwa, akasema, "Hawana."
"Good. Jambo la pili ni kuhusu yule kijana aliyempeleka Dikwe kule Uwanja wa Gofu. Angali ananitia wasiwasi."
Chiko akasema, "Vile n'na imani kuwa atarejea pale Tupetupe, kuna wazo lililonijia."
"Wazo gani?"
"Unajua, lile jengo linalotazamana na Tupetupe Hotel, lina vyumba vya kukodi ghorofani. Panaitwa Flamingo. Nataka nichukue chumba kimoja cha mbele. Kisha nitamchukua Chox akae dirishani na kusubiri. Kijana huyo akitokea nataka anionyeshe. Kumjua adui ni nusu ya kushinda vita."


"Sawa. Lakini akikubali kununuliwa ni bora tumnunue."
"Ok."
"Sasa kuhusu yule Daktari mstaafu," alisema Kembo. "Bwana Kessy amenipatia sindano na kichupa cha black mamba venom. Kifo katika nukta thelethini tu. Haiogopi wala haikopeshi. Tunachokihitaji ni Daktari wa bandia tu."
"Chox anatosha. Hakuna wa kumpata kwa kugeresha. Kuna wakati hujifanya askari na kuwashika askari wa kweli kweli."


************************************


Dennis na Bessy, baada kuelekezwa vizuri na Butu, hawakupa shida kupapata kwa shangazi Suzy. Bessy alilitengua wazo lake la awali la kumvamia na kumpekua kwa kuhofia kukosa ushirikiano na msaada wake. Hivyo wakamwendea kirafiki.
Wakamkuta chumbani mwake, ndiyo kwanza amalize mlo ambao kwake ulikuwa mchanganyiko wa staftahi na chakula cha mchana. Kipolo cha wali na mchuzi wa samaki, vitumbua, chapati, mayai ya kukaanga na chai.


Wakabisha hodi, na walipokaribishwa wakaingia. Alikuwa peke yake humo ndani, "Shikamoo, Shangazi,"
"Marahaba." Sauti yake haikulingana na umbo lake kubwa. "Karibuni." Aliwakaribisha, bila ya shaka akiwadhania ni wateja.
"Asante." Alisema Bessy, akiufungua mkoba wake na kutoa kitambulisho chake. "Mimi ni Kachero Inspekta Bessy na mwenzangu ni Luteni Dennis Makete."


Shangazi akataka kuinuka kama vile mto wa sofa ulishika moto ghafla. Bessy akamzuia kwa kumshika bega kirafiki.
"Hapana Shangazi, keti tu. Tumekuja kuhusu kifo cha Bob." Alisema, naye aliketi akimfanyia Denny ishara Denny afanye hivyohivyo.
Denny akaketi
Bessy akauliza, "Unayo habari kuwa Bob na Kikoti wameuawa?"
"Ndiyo." Alijibu shangazi. "Butu alipitia hapa alipotoka hospitalini kuziona maiti."
Denny akauliza, "Alitaka nini?"
"Sijui. Kunitaarifu, bila shaka. Lakini alikuwa na wasiwasi na akibabaika kama-kama..."
"Kama aliyeona jini?" Bessy alimsaidia.
"Naam, kama aliyeona jini." Shangazi alikubali.


"Hakuuliza chochote?" Denny aliuliza.
"Alitaka kujua ilikuwakuwaje kama vile mimi nilikuwa pamoja nao katika matembezi yao. Alikuwa akibabaika, akilalamika na akilaani. Hata sikuwa namwelewa. Bila shaka lilikuwa pigo kubwa sana kwake."
"Hilo limeshatokea. Kilichotuleta ni kutaka msaada wako."
"Abee?" Shangazi hakumwelewa.


"Ni kisa kirefu, lakini kwa kuwa tunahitaji msaada wako, ni bora ukifahamu angalau kifupi. Ni hivi. Kuna mtu mmoja tajiri sana na wa hatari sana ambaye anatafutwa na polisi. Yeyete atakaewezesha mtu huyo akamatwe atapata zawadi ya milioni moja. Kikoti akagundua kuwa mtu huyo si mwingine bali ndiye mwajiri wake. Kwa vile yeye ni mbumbumbu akawataka Bob na Butu wamsaidie kuipata zawadi hiyo. Sijui unanielewa?"
"Nakuelewa vizuri sana."

"Bob," Bessy akaendelea, "Akaiona milioni moja ni ndogo. Akawashauri wenzake wamdai huyo tajiri kifumba mdomo. Kikoti akaafiki, lakini Butu akakataa. Akajaribu kuwakataza wenzake lakini walimpuuza. Akakasirika na kuondoka."
"Hivyo ndiyo maana jana aliondoka mapema?" Shangazi aliuliza.
"Ndyo." Bessy akakubali. "Kudai kifumba mdomo ni kosa la jinai, hata kama huyo anayedaiwa ni mhalifu. Na adhabu yake ni kali. Hivyo Butu hakutaka kushiriki. Lakini ni kosa la jinai pia kuficha siri ya uhalifu. Ukiwa askari kosa hilo huwa kubwa zaidi. Ndiyo maana ukamwona Butu akihaha."
"Maskini! Sasa yuko wapi?"
"Yuko ndani. Nimemfungulia shitaka la kuficha siri ya uhalifu. Ilimpasa awaripoti Bob na Kikoti mara moja."
"Maskini, asingeweza. Bob ni - maskini! - Alikuwa rafiki yake mkubwa."


"Nafahamu, lakini amekula kiapo cha kipolisi kabla ya kukabidhiwa madaraka, tunaapa kuwa tutatekeleza wajibu wetu ipasavyo hata kama mhalifu ni baba au mama mzazi. Yeye hakutekeleza wajibu wake. Na sasa ona matokeo yake - kapoteza maisha ya Bob na huyo Kikoti."
Shangazi akatisa kichwa na kuliza ulimi kwa majonzi.
Denny akamuuliza, "Ni wateja wako wakubwa?"
"Sana."
"Hata kikoti?"
"Hapana. Yeye anamiezi michache tu hapa."
"Ni lazima tumpate huyo mwajiri wake, ndiye aliyewatuma wakora wawauwe Bob na Kikoti. Humjui ni nani na anaishi wapi?"
"Mwenyewe husema - hasa anapolewa na kutaka mkopo - anafanya kazi sehemu za Buffalo Hill, kwa Bwana Kessy."


"Hayo tunayafahamu, katueleza Butu, lakini ni msaada mdogo sana. Buffalo Hill ni eneo kubwa sana. Lina maelfu, kama si malaki ya wakazi. Na jina la Kessy ni la kawaida kabisa. Linatumiwa na watu mbali mbali, waislamu, wakristo na hata wapagani. Bessy akadakia, "Kikoti hakuwai kusema huyo Kessy yukoje. Anakaa mtaa gani, nyumba yake ikoje - chochote kile cha kutusaidia kumpata?"


Shangazi aliwaza kidogo kisha akasema, "Alewapo aliropoka mengi lakini hakuna aliyemtia maanani. Wakati mwingine mazungumzo yake yaliwakera Bob na But."
"Jaribu kukumbuka chochote alichoropoka kuhusu huyo mwajiri wake."
"Mengi ya kipuuzi. Kama vile huyo Bwana Kessy kakaa kizungu zungu, tajiri sana, hubadili magari kama mashati, jumba ni la kifahari lenye bwawa la kuogelea."
"Hakuwahi kusema lipo mtaa gani?"
"Nadhani aliwahi kusema lakini sikutia maanani. Ilikuwa ni lugha ya kukopea, kama vile huyo tajiri yake ndiye mdhamini wake."


"Kama utakumbuka mtaa huo , piga simu Kituo Kikuu uniarifu. Kama sipo acha ujumbe. Jina langu, kama nilivyokwambia, ni Bessy."
Denny akasema, "Je, kazi ya huyo Kessy, Kikoti hakuwai kuitaja?"
"Alikuwa akijigamba kuwa bosi wake ni mfanyabiashara wa kimataifa, anasafiri mara kwa mara, hasa nchi za Ulaya. Na wageni wake ni watu wakubwa wakubwa, ikiwa ni pamoja na vigogo wa vyama vya siasa na serikali."
"Sasa." Alisema Bessy. "Hebu tueleze yote yaliyotokea hapa kwako jana jioni, yaani kati ya Bob na Kikoti."


"Bob na Butu walitangulia kufika. Bob akaketi hapa na Butu akaketi hapo. Wakaagiza bia. Punde Kikoti naye akaingia. Alikuja na chupa ya wiski. Wakaniomba glasi tupu, nikawapatia. Wakaendelea kunywa. Walinikaribisha nikakataa. Mimi na wiski tuko mbalimbali. Nikaenda uani kuwahudumia wateja wengine. Niliporudi Butu hakuwepo, na Bob alikuwa akiandika namba alizokuwa akipewa na Kikoti."
"Bila shaka zitakuwa namba za simu ya Kessy." Alisema Denny, "Huwezi kuzikumbuka?"
"Siwezi. Yalikuwa ni maongezi ya wawili na sikutilia maanani hata chembe."


"Hukuwauliza Butu kaenda wapi?"
"Sikuwauliza. Nilijua katoka kidogo. Kaenda kujisaidia au kununua sigara."
"Enhe, kisha ikawaje?"
"Bob naye akatoka, akisema atarudi punde tu. Na kweli baada ya muda mfupi akarudi."
"Alikwenda kumpigia simu Kessy." Alisema Bessy. "Sasa jaribu kuwa makini na mazungumzo yako."
"Lakini sikuyatilia maanani sana. Na nilikuwa situlii, mara niko ndani, mara niko nje."
"Haidhuru, jaribu kadri ya uwezo wako."


"Bob aliporudi akasema, 'Tayari, keshanasa mshenzi. Milioni saba! Hayo nayakumbuka vizuri, kwani ndio maneno aliyoingia nayo. Na uso wake ulijaa furaha."
"Hakuna kingine chochote unachokumbuka?"
Shangazi alitikisa kichwa alisema, akitafakari. "Bob alisema kitu kama wameukata."
"Kisha ikawaje?"
"Wakaendelea kunywa. Kwa mara ya kwanza nikamuona Bob akimnunulia bia Kikoti, huku akimwambia wasilewe sana,kuna kazi muhimu inayowasuburi. Bob alimshauri Kikoti asiendelee kunywa wiski."
"Kisha?"
"Kwenye saa nne hivi Bob akatoka tena. Vile vile hakuchelewa kurudi."
"Safari hii akasemaje?"
"Alisema tutakabidhiwa mzigo wetu saa sita kamili karibu na daraja la Singisa. Akampa mkono Kikoti. Nilidhani wamelewa, kumbe wanapeana mkono wa buriani!"


Itaendelea
 
Asanteeee:thumbup::thumbup::thumbup::thumbup::thumbup::thumbup::thumbup::thumbup::thumbup::thumbup::thumbup::thumbup::thumbup::thumbup::thumbup:: tulisubiri sana tupe hata ep mbili leo mkuu
 
Sikuiona hii ngoja nianze kuanzia mwanzo.
 
Back
Top Bottom