Riwaya: Mzalendo Kizimbani (Mwalimu Makoba)

Riwaya: Mzalendo Kizimbani (Mwalimu Makoba)

Sehemu ya 14

Hatimaye Mako alimaliza darasa la saba. Akaomba kusoma ‘pre-form one’ nje kidogo ya mji ambako kulikuwa na kituo cha masomo hayo tena kilichotoa huduma ya bweni. Alisema alitaka afurahie kukaa nje ya nyumbani kwa miezi japo mitatu ili ajifunze changamoto mpya. Kwa sababu Baba alimwamini kijana wake na alishampa mbinu mbili tatu za kukabiliana na dunia na mambo yake, alimruhusu.

Hatimaye ilifika siku ya mwisho ya mafunzo. Baba akafunga safari kwenda kumrejesha nyumbani kijana wake. Alipofika alielezwa kwamba mtoto yule aliandikishwa lakini alitoweka siku tatu tu baada ya masomo na hakuonekana tena. “Kwa nini hamkunijulisha. Atakuwa wapi sasa?” alihoji Baba aliyepatwa na mshituko.

“Hukutuachia namba ya simu.”

“Nilimpa awape.”

“Hakutupa.”

Baada ya mabishano ya muda, Baba aliamua kurudi nyumbani akiwa kachanganyikiwa. Alipofika alipitiliza katika ofisi yake, hakutaka kuongea na Mama aliyekuwa chumbani, hakuwa na jibu la swali lake.

Alipofungua mlango wa ofisi alitabasamu alipomuona kijana wa miaka 13 akiwa kakaa nyuma ya kompyuta, mikono kaweka kichwani naye anatabasamu.

“Umesoma wapi pre form one, hukuonekana shule miezi yote mitatu,” Baba aliuliza akivua kofia na kuiweka juu ya msumari katika pembe ya mlango.

“Password ya kompyuta ulibadili… nimeshindwa kufungua,” Mako aliuliza Akilikwepa swali la kwanza.

“Ulisoma wapi pre form one?” Aliuliza tena Baba, akiangaza huku na kule bila shaka akitafuta bakora yake, endapo angeikosa, yangetumika makofi.

“Kuna joto sana humu ndani… Oooooh… marafiki, nilinasa katika mtego wa marafiki. Marafiki zangu wote hawakuwa kituo kile, lakini wote walikuwa Bahari School. Hivyo nikaenda kusoma huko.”

“Ada tulilipa huku, kule ulilipa nini?”

“Hivi hujui kwamba Bahari School inamilikiwa na mama ya rafiki yangu Dan? Nilisoma bure.”

“Kwa nini hukunipa taarifa?”

“Vipi kama ungekataa, ilikuwa salama. Nilithubutu katika njia salama.”

“Nipe ushahidi kwamba umesoma.”

Mako alinyanyuka katika kiti. Akaelekea chumbani kwake na kurudi na begi. “Tazama hili, daftari la physics limeandikwa angalia na vema hizo. Hili la Mathematics, the study of number, hili la Biology, study of living things… hili la History, study of past, present and future events… angalia madaftari… unaona hii, hiki cheti cha heshima nimepewa, nimeongoza katika mitihani… angalia mitihani hiyo. Tisini, mia, sabini na nane… hilo ndiyo pekee nilianguka, zingine ni mia kwa tisini.”

Baba alikosa swali la kuuliza japo kichwani hakuwa na majibu. Aulize nini kama ushahidi upo mezani. Akamkaribisha kijana nyumbani.

Kuwa wa Kwanza Kupokea mwendelezo wa Riwaya hii Kwa kujiunga katika Group la bure WhatsApp. Kujiunga, Gusa Hapa

Tupate Wadhamini:

Soma: Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi

Soma: Jinsi ya Kuandika CV
 
Sehemu ya 15

Sekondari alisoma mbali na nyumbani. Shule ya serikali iliyokuwa mkoa wa mbali na ilikuwa ya bweni. Mara moja Baba alipata taarifa kuwa Mako kaonekana mjini, akapiga simu shule, akaambiwa kijana yupo na anasoma kwa bidii.

Baada ya kumaliza kidato cha nne, kidato cha tano na sita hakikuchukua muda, alimaliza na kwenda kulitumikia jeshi la kujenga taifa kwa miezi mitatu. Baadae alianza chuo kikuu akisomea shahada ya elimu. Mara tano Baba alienda chuo kumtafuta ili amjulie hali, hakumkuta, lakini alipewa taarifa mwanafunzi huyo yupo ila huonekana muda wa vipindi na haishi katika eneo la chuo. Baba alipomuuliza Mako, akajibu anaishi eneo la chuo na huonekana hapo muda wote. Hata hivyo akasisitiza Baba anapotaka kuja kumtembelea atoe taarifa kwani hujificha sehemu kujisomea na kufanya iwe ngumu kuonekana na watu wengine.

Alimaliza chuo, akakaa nyumbani wiki moja halafu akasema amepata shule kufundisha. Jina la shule alilotaja Baba alilitafuta hakulipata. Mako alishakuwa mtu mzima, alimuacha na maisha yake.

Mako aliondoka nyumbani akisema anafundisha katika shule yake isiyofikika. Muda mwingi hakuonana na Baba lakini waliwasiliana. Hata hivyo, huwezi kumpata Mako mpaka yeye akupigie. Ili kuwatoa hofu wazazi, Mako aliwapigia mara moja kila mwezi, akawaambia anaendelea vizuri na mambo yananyooka wasihofu!

Katika jiji kuu la Nchi Yetu, katika uwanja wa Uhuru watu wengi walifurika wakiwemo viongozi wa mataifa mbalimbali. Wote walifika kushuhudia tukio la kuapishwa kwa rais mpya wa Nchi Yetu, Mzee Mnyonge!

Baba alikuwa miongoni mwa watu waliokataa kupitwa na shughuli hii ya kihistoria. Alikaa uwanjani siti ya mbele akilitazama jukwaa alilopaswa kukaa Rais mpya, Mzee Mnyonge. Hata hivyo leo alionekana kuwa makini na asiyeamini alichokiona mbele yake. Alikaa katika mshangao ule kwa saa kadhaa mpaka Mzee Mnyonge alipoapishwa.

Sasa Mzee Mnyonge baada ya kuwa rais mpya, akakaa katika kigoda. Alivaa suruali ya mtumba nyeusi, shati jeupe lililovaliwa mara kadhaa na tai nyekundu ambayo inaonekana alilazimishwa kuivaa ili kuzingatia itifaki. Mkono wa kulia alishika mkuki, kushoto alikamata ngao iliyochorwa rangi za bendera ya Nchi Yetu. Baba aliendelea kumtazama mtu aliyemtazama kwa muda mrefu. Mtu huyo alisimama nyuma ya rais Mzee Mnyonge. Alivalia kofia ya askari, Koti jekundu lililotiwa nakshi za kijeshi kama kamba na mikufu iliyotambaa maeneo ya juu. Kijana huyu alikuwa mpambe wa rais, kwa jina la kimombo akiitwa ‘aide-de-camp’ lakini huko mtaani, watu humuita ‘bodigadi’ japo hiyo si kazi yake. Baba alimshangaa sana kijana huyo. Si kwamba alishangaa kijana wa umri mdogo kupewa jukumu hilo kubwa, au alishangaa mavazi aliyovalia la! Baba alimfahamu kijana huyo, alikuwa Mako!

Kuwa wa Kwanza Kupokea mwendelezo wa Riwaya hii Kwa kujiunga katika Group la bure WhatsApp. Kujiunga, Gusa Hapa

Tupate Wadhamini:

Soma: Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi

Soma: Jinsi ya Kuandika CV
 
Sehemu ya 15

Huku na huku huku na kule hatimaye purukushani ziliisha. Baba akanyanyuka kuelekea nyumbani mwenye mshangao. Baba mwenye akili nyingi alishagundua kuwa Mako alianza kujihusisha na watu wale miaka mingi iliyopita. Alichora matukio akilini mwake yakapangika vyema na sasa anautambua ukweli. Aliachia tabasamu pana. Alikuwa na uhakika wa kuyala matunda ya mwanae!

Utawala wa Mzee Mnyonge uliwavutia wengi pale alipoanza kazi. Mara tu baada ya kuapishwa, Mzee Mnyonge alianza kazi kwa kumteua mwanasheria mkuu wa Serikali. Katika siku zake hizo za mwanzo, alitumia mtindo wa kufanya ziara za kushtukiza katika taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na kukemea viongozi wazembe na wanaoendekeza ufisadi na rushwa serikalini.

Mtindo wake huo, ukatumiwa pia na watendaji wengine wa Serikali wakiwamo mawaziri na wakuu wa mikoa na wengine. Katika siku zake hizo za mwanzo, Mzee Mnyonge pia alifanya mabadiliko makubwa Ikulu kwa kufuta baadhi ya vitengo, kikiwamo cha lishe na benchi la wageni na kuagiza wananchi wote wenye matatizo waanzie ngazi za chini.

Halafu akafanya maamuzi magumu: akafuta safari za nje, ikafuata fukuzafukuza ya waliotuhumiwa kuwa wezi, akabana matumizi ya serikali na kujitangaza kuwa yeye ni Rais wa wanyonge kama lilivyo jina lake.

Wakati Mzee Mnyonge anaendelea na utawala wake, Mako alihudumu katika cheo chake kwa mwaka mmoja na miezi sita pekee. Ukaja ujumbe uliomtaka arejee kambi ya makomandoo ili akasaidie kuwapika makomandoo wazuri kama yeye. Kwa umri wake, elimu, kipaji na umahiri wake wa vita, ilionekana si vyema sana kuzurura na rais, cheo hicho ikaamuriwa apewe mtu mwingine. Mzee Mnyonge alisikitika waziwazi juu ya maamuzi hayo. Lakini hoja zilizidi mapenzi.

Mako alirejea haraka kambini na kuyaanza majukumu yake. Mpambe mpya aliwekwa, jina lake Ngosha Mbehi, Mzee Mnyonge akampenda Ngosha kama alivyompenda Mako.

Basi Mako akiendelea kufundisha Makomandoo huko kambini kwa miaka kadhaa, ndipo akapokea ujumbe uliomtaka kwenda kutetea amani huko katika nchi jirani ya Congo. Unakumbuka mkasa ulianza Mako akiwa vitani? Sasa nimekujuza, kabla ya vita alikuwa wapi!

inaendelea...

Wakati unaendelea kufuatilia riwaya hii, unaweza kununua riwaya zingine za mwalimu zilizokamilika. Fahamu zaidi kwa kugusa hapa.
 
Sehemu ya 16

Makomandoo walikuwa ndani ya gari baada ya kushuka katika dege la kivita lililowaacha katika jiji kuu la Nchi Yetu. Haikuchukua muda, gari ndogo ya kijeshi ilifika, Makomandoo yakaingia tayari kwa safari ya kuelekea kambi yao iliyokuwa mkoa jirani wa Maragara. Mako, Bwii na Ado walikaa nyuma; Moli alikaa mbele akiwa na dereva.

Gari ilianza kukimbia kwa mwendo wa wastani na umbali wa huko walikokwenda ilikuwa kilometa 194. Kila mmoja alikuwa kimya, pengine waliwaza namna watakavyopokelewa na wenzao huko kambini, namna watakavyoheshimiwa kwa kazi nzuri waliyofanya… na pengine labda, kupanda vyeo.

Katika barabara fulani kutaka kuingia barabara kuu, gari ilisimama kwa sababu ya foleni. Walikaa pale kwa zaidi ya dakika ishirini. Moli akavunja ukimya, “Kuna nini leo, mbona foleni inachukua muda.”

“Pengine kuna msafara wa kiongozi,” Mako alidakia.

“Ina maana hamna habari?” aliuliza dereva akigeuka nyuma kuwatazama abiria wake.

“Tujuze Komando,” alisema Moli akimtazama dereva.

“Imewezekanaje mkakosa taarifa, hata redio hamkusikiliza?”

“Redio tulisikiliza mara moja na hatukusikia lolote, nadhani unafahamu mambo ya uwanja wa vita, habari muhimu ni ile inayosema adui yupo wapi?” aliongeza Moli.

“Ndugu zangu…” alisema dereva akiinamisha kichwa chini. “Mzee Mnyonge amefariki! Atapitishwa barabara zote ili wananchi wamuage kwa mara ya mwisho.

inaendelea...

Wakati unaendelea kufuatilia riwaya hii, unaweza kununua riwaya zingine za mwalimu zilizokamilika. Fahamu zaidi kwa kugusa hapa.
 
Sehemu ya 17

Mako alifungua mlango wa gari akiwa kainamisha kichwa chake. Alitembea mpaka kunako barabara kuu akijipenyeza katikati ya watu waliokuwa wakisubiri kumuaga Mzee Mnyonge. Akiendelea kusubiri, akakumbuka yote aliyofanya akiwa mpambe wa Mzee.

“Egelaga aha nkwengwa,” alisema Mzee Mnyonge, Mako akasogea kumsikiliza.

“Nilitamani uendelee kuwa na mimi, lakini umewasikia wataalamu walivyosema? Mchango wako unahitajika kambini, unaondoka lakini sijataka na sijafurahi!”

Mako alijibu kwa kupiga saluti, halafu akasema taratibu, “ede na mhayo!”

“Dogo mana ibona lulu.” Alifunga mazungumzo Mzee Mnyonge.

Mako alitoka katika lindi la mawazo baada ya kusikia vilio vya watu pembezoni mwa barabara vikiongezeka. Akasogeza shingo yake, hapa akayaona magari yakija. Magari haya yalisheheni askari na viongozi mbalimbali. Halafu katikati lilikuwa gari maalumu jekundu, nyuma limebeba tela zuri lililobeba mwili wa Mzee Mnyonge. Gari ile ilitembea taratibu, watu wakaongezeka barabarani. Akina mama walitupa nguzo zao, machozi yakiwatoka.

“Tuendelee na safari Komando, Mzee Mnyonge hatupo naye tena,” alisisitiza Bwii akimshika mkono Mako kumrejesha garini tayari kuendelea na safari. Mako akaweka mkono usoni, alipoutoa, uliloa machozi, kumbe Makomandoo nayo hulia!

Waliendelea na safari Makomandoo wale. Katika muda wa saa zilizokadiriwa tatu, walifika kambini. Japo kulikuwa na msiba, walipokelewa kwa shamrashamra zilizoambatana na saluti nyingi.

Walikuta kambi imebadilika kidogo. Palikuwa na uongozi mpya na kiongozi huyu alikuwa mkali ajabu tena mwenye msimamo wake mwenyewe. Tena ilionekana kiongozi huyu hakuwafurahia Makomandoo hawa wanne waliokuwa gumzo kwa namna walivyowasambaratisha waasi katika nchi jirani. Aliwatazama kwa jicho baya na hakupenda kusikia habari zao.

Haukupita muda, Komandoo Moli alifukuzwa kazi kwa madai kwamba alihusika katika wizi wa mafuta. Akafuata Bwii ambaye alituhumiwa kuugua kichaa cha vita. Ilisemekana kwamba, Bwii hakusikiliza tena amri za wakubwa wake. Ado hakuchukua muda mrefu, ilisemekana kwamba alianza kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya, akafukuzwa.

Sasa alibaki Mako. Hakusubiri kufukuzwa, akaingia ofisini akiwa na heshima zote.

“Jambo afande!” alisalimia Mako kwa ukakamavu.

“Jambo!” Mkuu aliitika akimtazama Mako kwa dharau.

“Wenzangu wote umewafukuza kwa makosa ya kutunga. Nimebaki mimi ambaye najua sitachukua muda hapa. Nimekuja kukutaarifu kwamba, nimeacha kazi!”

“Nimekubali na kila la heri. Tena unabahati umewahi mapema, kesho ningekuletea mashtaka yako. Tuna ushahidi kwamba, unajihusisha na kundi la washirika wa Mzee Mnyonge kundi hili linataka kupindisha katiba, mtawala mpya asiwe yule anayetakiwa.”

Habari hizi zilikuwa mpya masikioni mwa Mako. Akamtazama Mkuu akitabasamu, halafu akatamka vyema, “Kwa heri ya kuonana!”

inaendelea...

Wakati unaendelea kufuatilia riwaya hii, unaweza kununua riwaya zingine za mwalimu zilizokamilika. Fahamu zaidi kwa kugusa hapa.
 
Back
Top Bottom