SEHEMU YA NANE
Jua hilohilo lilikuwa mgongoni kwa Reacher aliyekuwa akielekea yalipo maegesho ya taxi baada ya kushuka kwenye ndege. Alipanda Taxi moja na kumwelekeza dereva ampeleke Roosevelt Square, Manhattan. Walipofika Reacher alitulia kama anayetafakari jambo. Alikuwa anawaza ni wapi atapata hoteli ya gharama nafuu, lakini iwe na huduma ya kupiga simu. Na iwe na kitabu cha namba ya simu. Jibu moja lilikuwa wazi: Asingepata hoteli yenye sifa zote hizo tatu. Hata hivyo alishuka na kimlipa dereva wa Taxi. Alikuwa ameamua atatembea kwa safari iliyobaki.
Wanaume wengine wawili waliokuwa wamevalia suti zao vizuri walisubiri hadi Chester Stone alipoondoka ndipo wakaingia ofisi ya ndani na kusimama mbele ya meza. Hobie aliinua kichwa kuwatazama. Bila kusema jambo alifungua droo yake na kuweka lile faili jekundu pamoja na mkataba. Halafu akatoa kikaratasi kingine cha njano.
"Nawasikiliza." Alisema.
"Tumefika muda huu." Mwanaume wa kwanza aliongea.
"Mmepata taarifa niliyowatuma?" Hobie aliuliza.
Mwanaume wa pili alitikisa kichwa kukubali halafu akaketi kwenye sofa na kuongea, "Costello alikuwa anamtafuta mtu anaitwa Jack Reacher."
Hobie aliandika lile jina kwenye kile kikaratasi cha njano.
"Huyo Jack Reacher ni nani?"
"Hatufahamu." Yule mwanaume aliyekuwa amesimama alijibu.
Hobie alitikisa kichwa, "Na huyo Costello alikuwa ametumwa na nani kwenda huko?"
Ukapita ukimya kidogo.
"Hatufahamu pia." Yule mwanaume aliyekuwa amesimama alijibu tena.
"Hayo ni maswali ambayo yapo wazi kabisa," Hobie alisema. "Inamaana hamkumuuliza Costello hata moja wapo."
Yule mwanaume aliyekuwa amekaa akajibu, "Tulimuuliza, mkuu."
"Lakini?"
"Hakutujibu."
"Hakuwajibu?"
"Alifariki kwa mshtuko," Yule mwanaume aliyekuwa amekaa alijibu na kuongeza. "Tusamehe sana, boss."
Hobie alitikisa kichwa chake taratibu. "Kuna uwezekano pengine mwili wake ukagundulika alikuwa nani?"
"Hapana," Yule jamaa aliyekuwa amesimama alijibu. "Tumehakikisha huo uwezekano unakuwa ni mdogo."
"Na kisu kipo wapi?"
"Tumekitupa baharini." Yule mwanaume aliyekuwa amekaa alijibu.
Hobie alitembeza mkono wake kuipapasa chuma yake. Alikuwa anafikiria kabla hajasema jambo.
"Basi sawa." Aliwaambia. "Sio kosa lenu, ni kosa la moyo wake mbovu. Lakini mmefikiria cha kufanya?"
Yule mwanaume aliyekuwa amesimama alipungukiwa wasiwasi akaenda kukaa kwenye sofa. Alikuwa ameponea chupuchupu!
"Tunatakiwa kumpata aliyemtuma Costello huko."Hobie alisema.
Wale wanaume wawili walitikisa vichwa vyao kukubali.
"Costello lazima alikuwa na katibu mhtasi, sio?" Hobie alijiuliza kwa sauti. "Basi huyo ndiye atatupeleka kwa tunayemtafuta. Hakikisha mnamleta huyu katibu muhtasi."
Hawakujibu kitu na walibaki wamekaa kwenye sofa.
"Hamkunisikia?" Hobie aliuliza.
"Tatizo ni huyu Jack Reacher," Yule mwanaume wa kwanza kuketi alisema. "Tuliambiwa jamaa ana mwili mkubwa na anafanya kazi baa - Costello pia alisema hivyohivyo. Tulivyoenda baa tulimkuta lakini alisema hilo sio jina lake."
"Kwahivyo?"
"Tulipofika uwanja wa ndege kulikuwa na ndege ya moja kwa moja kuja New York na ndege inayopitia Delta, Atlanta hadi New York."
"Na?"
"Tulimuona Jack Reacher akiwa anakata tiketi kwenye dirisha la ndege ya pili."
"Una uhakika?"
"Kwa zaidi ya asilimia tisini na tisa, mkuu. Ni kweli tulikwa mbalimbali, lakini nina uhakika yule alikuwa ni yeye."
Hobie alianza kugusagusa chuma yake akiwa kwenye dimbwi la mawazo.
"OK, Anaitwa Reacher." Alisema. "Baada ya kutafutwa anaamua kukimbilia New York, sio?
Yule mwanaume wa kwanza kuketi alijibu, "Ndiyo. Ila ni kama hajashukia Delta au Atlanta na basi lazima atakuwa yupo New York."
"Kwanini?" Hobie aliuliza na kuongeza, "Mmekwishafahamu yeye ana shughuli gani?"
Hakuna aliyejibu. Alitafakari kwa muda na kujijibu swali lake mwenyewe.
"Katibu muhtasi wa Costello atatuambia mteja wao alikuwa ni nani, sio?"
Halafu akatabasamu tena.
"Huyo mteja atatuambia Reacher ni nani na Reacher atatuambia anashughulika na nini."
Wale wanaume wawili walitikisa vichwa vyao kwa pamoja kukubaliana na Hobie. Halafu wakanyanyuka kutona nje ya ile ofisi.
Reacher alikuwa anatembea kusini mwa barabara ya mitaa ya Manhattan. Alikuwa anajaribu kuwaza ugumu na ukubwa wa shughuli iliyokuwa mbele yake. Mambo mawili yalikuwa wazi. Kwanza alikuwa yupo sehemu sahihi na kwa muda sahihi. Lakini New York ni jiji kubwa lenye idadi ya watu wengi. Watu zaidi ya milioni saba na nusu kwa mjini. Ukijumlisha na kijijini unaongelea watu zaidi ya milioni kumi na nane. Hisia zake zilimuwambia pia Costello alikuwa mtu wa Manhattan lakini mteja wake hakuwa mtu wa Manhattan. Kama wewe ni mwanamke na unataka mpelelezi wa kujitegemea sehemu pekee ya kumpata ni kwenye kitabu cha namba za makampuni na watoa huduma mbalimbali.
Aliamua hatoanzia kwenye hoteli. Hakuwa na muda wa kupoteza. Hivyo alihitaji apate kitabu cha namba za simu. Lakini pia hakuwa tayari kulipa gharama kubwa wanazotoza wenye mahoteli kwaajili ya kupiga simu. Kazi ya kuchimba mabwawa haikuwa imemfanya tajiri.
Kwahivyo alianza kutafuta maktaba kuu ya mji. Ambayo duniani ni maktaba ya kwanza kwa ukubwa. Labda ndiyo au labda hapana, hakuwa na uhakika. Lakini aliamini itakuwa kubwa kiasi cha kutosha kumpatia vitabu kadhaa vya namba za simu. Alitumia mwendo wa lisaa limoja hadi kufika hapo maktaba. Kilichofanya atumue muda mwingi ni pale aliposimama kununua kalamu na kidaftari kidogo.
Aliyekuwa ameingia kwenye ofisi ya Hobie muda huu alikuwa ni yule mwanaume wa mapokezi. Aliingia ndani na kuufunga mlango kwa funguo. Alitembea na kwenda kukaa kwenye sofa karibu kabisa na Hobie. Hapo alimtazama machoni.
"Nini?" Hobie aliuliza.
"Unatakiwa uondoke," Yule mwanaume wa mapokezi alisema. "Ni hatari sana wewe kuendelea kukaa hapa."
Hobie hakujibu. Alikuwa anaishikashika chuma yake kwa vidole vya mkono wa kushoto.
"Huo ndiyo ulikuwa mpango wetu," Yule mwanaume alisema tena. "Na uliniahidi sasa nashangaa imekuwaje?"
Hobie aliinua mabega juu na kuguna bila kusema kitu.
"Makubaliano ilikuwa kama tukipata dokezo kutoka Hawaai utaondoka."
"Costello hakufika Hawaai," Hobie alijitetea. "Ushahidi tunao."
"Na hicho ndicho kinafanya nikuambie mambo hayako sawa. Kama Costello hakufika inamaana kuna mtu mwingine anafuatilia pia."
"Umesahau mipango yetu," Hobie alijitetea tena. "Hebu fikiria kwanini upande wa pili hawajasema kitu chochote? Kama taarifa itatoka huko pia ndiyo tutaingia hatua inayofuata."
"Lakini uliniahidi..." Yule mwanaume wa mapokezi alisema tena.
"Bado ni mapema," Hobie alijitetea tena. "Hebu fikiria. Ni kama umemuona mtu amenunua bunduki na boksi la risasi halafu akakuweka chini ya ulinzi, utaogopa?"
"Ndiyo nitaogopa."
"Mimi siataogopa," Hobie alianza kueleza. "Sitaogopa kwasababu huyo mtu hajaweka risasi kwenye hiyo bunduki yake. Alinunua bunduki na boksi la risasi, lakini hakuweka risasi. Kwahivyo hadi tusikie kutoka upande wa pili ndipo tukae kwenye mpango. Vinginevyo dokezo la Hawaai ni kama bunduki isiyokuwa na risasi."
Yule mwanaume aliegemea sofa na kuinua kichwa kutazama dari.
"Kwanini unafanya huu ujinga?" Aliuliza.
Hobie alifungua kabati lake na kutoa kabrasha la Chester. Akautoa ule mkata uliosaniwa na kumuonesha yule mwanaume., "Nahitaji wiki sita tu."
Yule mwanaume wa mapokezi akaguna, "Wiki sita za nini?"
"Hii ndiyo nafasi yangu ya dhahabu," Hobie alianza kueleza. "Chester amenipa kampuni yake burebure. Kazi ya vizazi vyake vitatu naipata kiulaini sana."
"Mimi naona kama umepoteza dola milioni moja nukta moja kwaajili ya makaratasi tu."
Hobie alitabasamu. Nusu ya uso wake mmoja ilikuwa imenunua kama sanamu.
"Acha nikuambie ninachofikiria," Hobie alianza kuongea. "Chester anamiliki kiwanda kikubwa cha uzalishaji na jumba kubwa tu la kifahari. Kiwanda chake kina eneo kubwa sana na takribani nyumba mia tano."
"Hizo nyumba sio zake." Yule mwanaume aliingilia.
"Ni za kwake lakini zipo kwenye dhamana."
"Kwahiyo?"
"Hebu fikiria nini kitatokea kama nikiingiza hisa anazonipa sokoni."
"Hautopata kitu kwa sababu hazina thamani kwa sasa hivi."
"Ni kweli. Na ndiyo maana akaja kwangu. Hataki benki zilizomkopesha zijue hilo. Sasa waza benki zikijua hicho kitu?"
"Watahaha." Yule mwanaume alijibu.
"Safi," Hobie alisema na kuendelea, "Watahaha. Halafu watakurupuka kunifuata mimi ambaye tayari nitakuwa nazimiliki kwahivyo nitawalipi senti ishirini kwa kila dola wanayomdai Chester."
"Watakubali."
"Kwanini wakatae. Ni bora wapate kidogo kuliko kukosa kabisa." Hobie alisema huku akitabasamu.
"Na kuhusu hizo nyumba... Utazifanyia nini?"
"Kwakuwa nitakuwa mmiliki kamili nitakifunga kiwanda kufanya marekebisho. Hapo nitakodisha magari ya kuja kusawazisha eneo lote libaki wazi. Tutapata zaidi ya hekari elfu tatu. Jumlisha jumba lake?
Pengine gharama nitakazotumia zitafika dola milioni sita, lakini faida itakuwa ni lukuki. Zaidi ya dola milioni mia."
Yule mwanaume wa mapokezi alikuwa anamshangaa Hobie. "Ndiyo maana unahitaji wiki sita?"
Hobie alitikisa kichwa kukubali halafu chumba kikaingiwa ukimya kidogo.
"Hauwezi kufanikiwa." Yule mwanaume wa mapokezi alisema na kuongeza, "Hiyo ni biashara ya familia. Lazima kuna hisa ambazo Chester hajaziweka dhamana. Kwahivyo umiliki wako wa kampuni hautakuwa asilimia mia moja."
Hobie alitikisa kichwa kupinga, "Ataniuzia kila kitu chake. Subiria uone."
"Hawezi kufanya hivyo hata iwe vipi!"
"Ninao mpango. Niamini mimi ataniuzia kila kitu chake."
SEHEMU YA TISA