“Mna hakika kuwa hamkumchukua mtu yoyote njiani?
“Hatujamchukua mtu yoyote kwani tunajua hata sheria za barabarani haz-
ituruhusu kufanya hivyo” yule dereva akaongea kwa msisitizo huku akioneka-
na kuwa mwenye mashaka.
Wale askari waliochepuka kuja kukagua nyuma ya lile tela walipekua kila
mahali huku wakifunua turubai lililokuwa limefunika ile mifuko ya sukari
hata hivyo hawakuwa watundu katika kufanya upekuzi hivyo hawakuyagun-
dua maficho yangu. Baadaye niliwaona wakiondoka na kuelekea kule mbele
na sikuweza kuwaona tena kwani walikuwa wamehamia upande mwingine.
Mimi niliendelea kujibanza mle ndani ya lile tela nikisikilizia huku bastola
yangu ikiwa tayari mkononi.
Haukupita muda mrefu mara niliwaona yule dereva wa lori na utingo wake
wakiingia ndani ya ile kibini ya lori kisha milango ikafungwa na haukupita
muda mrefu baada ya pale nikaanza kuisikia injini ya lile lori ikianza kuungu-
ruma. Muda mfupi baadaye lile lori lilianza kuondoka na kuingia tena baraba-
rani na hapo safari ikaanza tena.
Niliendelea kujibanza mle ndani ya tela hadi pale nilipohisi kuwa tuliku-
wa tumesafiri umbali mrefu wa safari yetu ndiyo nikaanza kutoka mle ndani
nikielekea kwenye ile kibini huku nikiwa makini kutazama nyuma kama lile
gari Nissan Patrol lilikuwa bado likitufuatilia. Sikuliona tena lile gari na hali
ile ilinipa furaha sana. Nilipofika kwenye ile kabini nikasimama juu ya lile
gunia la mkaa huku nikiufungua ule mlango mdogo wa dharura na baada ya
muda mfupi nikawa nimefanikiwa kurudi mle ndani ya kibini na kukaa ma-
hali pangu. Macho yenye hofu na mashaka ya utingo na yule dereva wa lori
yalinipokea bila kusema neno kisha yakageuka na kutazama mbele na hapo
nikafahamu kuwa ile hali ya urafiki ilishatoweka mle ndani na isingekuwa
rahisi kuirudisha haraka.
“Wale watu ni kama waliokuwa wakikutafuta wewe bwana kwani una shida
gani? yule dereva aliniuliza huku akionekana mwenye mashaka na mimi.
“Nilitarajia hivyo” nilimwambia yule dereva na jibu langu bila shaka lili-
washtua wote na hivyo kuwapelekea wageuke tena kunitazama kwa tuo kisha
wakageuka tena kutazama mbele.
“Kwa sababu gani unasema hivyo bwana? yule utingo aliniuliza
“Unajua kabla ya kuharibikiwa na basi letu kuna kituo kimoja cha njiani
nilisimamishwa na askari wa barabarani na hawakunikuta na kosa lolote hata
hivyo walikataa kuniruhusu eti mpaka niwape kitu kidogo. Sikuwapa pesa
yoyote na kwa hasira nikawasha gari na kuondoka nikiendelea na safari hivyo
nilijua tu askari wale wangenifuatilia. Nahisi watakuwa wameambiwa na wale
abiria kuwa mimi nimeelekea jijini Kigali kutafuta msaada hivyo wakaona
wanifuatilie na kunibana huku huku njiani wakiamini kuwa kwa vyovyote nina
pesa. Nimemkumbuka yule askari uliyeingia naye humu ndani kuwa alikuwa
miongoni mwa wale askari walionisimamisha kule njiani” nilimaliza kuongea
huku nikiupima uzito wa uwongo wangu kama ungekuwa rahisi kukubalika
hata hivyo sikuona kama uwongo wangu uliwaingia yule dereva na utingo
wake kwani nilikuwa ni kama ninayejiongelesha mwenyewe.
“Wanasema wewe ni mtu hatari unayesakwa kile pembe ya hii nchi” yule
utingo alidakia
“Toka lini mtu anayekataa kutoa rushwa akawa ni mtu hatari katika nchi?,
achana nao wale wana njaa zao. Ni kawaida kwa askari wa barabaani wa nchi
hii kudai rushwa hususani kwa madereva wasio wazawa” nilijaribu kujitetea
huku nikifahamu kuwa sikuwa na hoja ya msingi ya kujitetea lakini kukaa
kimya sikuona kama ingefaa, hata hivyo hakuna aliyeunga mkono utetezi
wangu.
“Ulikuwa umejificha wapi ?, nilikuwa na wasiwasi sana wakati yule askari
alipotaka kuingia humu ndani ili ajiridhishe kuwa hakukuwa na mtu tuliyem-
chukua” yule dereva aliniuuliza akiingiza gia na kukanyaga mafuta.
“Nilijua tu kuwa kwa vyovyote wale watu wangetaka kujiridhisha kwa ku-
fanya upekuzi humu ndani ndiyo maana niliwahi kutoka kwa kupitia mlango
wa dharura wa hii kibini na kwenda kujificha nyuma kwenye tela huku nikiji-
funika kwa ile mifuko ya sukari”
Niliendelea kuongea na wakati huu pia si utingo wala yule dereva aliyeo-
nekana kuvutiwa na maelezo yangu na hapo ukimya ukachukua nafasi yake
na mimi sikupenda tuendelee na maongezi yale. Niligeuka kutazama dirishani
nikaona kuwa kulikuwa na wingu zito limetanda angani na hapo nikajua kuwa
muda si mrefu mvua kubwa ingeanza kunyesha. Safari iliendelea na lile lori
lilikuwa likitimua mbio sana.
Mle ndani hakuna aliyekuwa na hamu ya maongezi yangu tena na mimi
nilipenda tuwahi kufika jijini Kigali ili kila mtu ashike hamsini zake. Nilitaka
kuuliza kuwa muda gani ungekuwa umesalia kabla ya kufika jijini Kigali la-
kini nilisita kufanya hivyo kwani huenda swali langu lingenifanya nionekane
kuwa sikuwa dereva niliyeifahamu vizuri barabara ile hivyo niliegemea siti
yangu vizuri nikawa nikitazama nje huku usingizi ukiwa mbali na mimi.
WALINISHUSHA PEMBENI YA KITUO kikubwa cha kujazia mafuta kili-
chokuwa katikati ya jiji la Kigali ikiwa tayari imekwishatimia saa kumi na
mbili jioni. Manyuyu hafifu ya mvua yalikuwa bado yakianguka toka angani
na giza nalo lilikuwa mbioni kushika hatamu. Niliwashukuru sana yule dereva
na utingo wa lile lori huku nikiwaahidi kuwa ningewatafuta baada ya kurudi
nchini Tanzania, na wakati nikiwaaga niliziona nyuso zao zikirudiwa na fura-
ha iliyotoweka kwa muda mrefu. Hapo nikajua furaha yao ilikuwa si kwa kwa
sababu walitaka tuonane tena hapo baadaye ila ni kwa sababu hawakupenda
kuwa na mimi na hilo halikunipa shida kwani mpaka pale walikuwa wameni-
saidia sana na sikuwa nahitaji msaada wao tena.
Baada ya kushuka kwenye lile lori na kuagana na yule dereva na utingo
wake nilisimama kando ya barabara ile nikiliacha lile lori likitoweka mbele
yangu kisha nikavuka barabara nikiwa mwenye tumaini jipya katika harakati
zangu. Sasa nilikuwa nimefika jijini Kigali.
Nikiwa na hakika kuwa hakuna mtu yeyote eneo lile aliyekuwa akizifuatilia
nyendo zangu tangu niliposhuka kwenye lile lori nilivuka barabara nyingine
upande wa kushoto na hapo nikaingia kwenye njia ya watembea kwa miguu.
Sikufahamu hasa ni wapi nilipaswa kuelekea ambapo ningeweza kutuliza
kwanza fikra zangu na kujipanga vizuri kabla ya kuanza tena harakati zangu
hata hivyo niliamini kuwa ingekuwa rahisi kupata jibu la swali hilo huku niki-
wa bado natembea kuliko nikiwa bado nimesimama eno lile.
Wakati nikiendelea kutembea nilijikuta nikifikiria kurudi kule chumbani
kwangu Hotel des Mille Colline hata hivyo nilipozidi kufikiria nilijikuta niki-
liweka wazo hilo kando kwanza kwani niliamini kuwa wale watu walioniteka
hadi wakati huu wangekuwa wakifahamu kila kitu kuhusu mimi ikiwemo ho-
teli niliyofikia na hata namba ya chumba changu na kwa kuwa nilikuwa nime-
watoroka kwa vyovyote sehemu ya kwanza ambayo wangenisubiri ingekuwa
ni kule chumbani kwangu hotelini. Hivyo sikuona kama ningekuwa nikifanya
uamuzi sahihi endapo ningeamua kufikia kule hotelini.
Nilifikiria niende kule Kigali Casino nikaonane na Mutesi hata hivyo wazo
hilo nalo pia sikuliona kuwa kama lingekuwa muafaka kwa kipindi kile hasa
nilipoanza kuhisi kuwa upo uwezekano kuwa huenda nisingemkuta Mutesi
wakati ule kwani nilikuwa sizifahamu vizuri ratiba zake na vilevile sikuwa na
hata pesa kidogo mfukoni ambayo ingeniwezesha kununua mzinga mmoja wa
pombe ambao ungetumika kuyasindikiza maongezi yetu. Hivyo wazo hilo pia
nililiweka kando huku nikifikiria mpango mwingine mzuri zaidi.
Wakati nikiendelea kufikiria nikajikuta nikiyakumbuka maelezo ya Ros-
ine wakati ule tulipokuwa pamoja kule kwenye ili nyumba katikati ya msitu.
Nikiwa nayakumbuka vizuri maelezo yake Rosine kuwa yeye na dada yake
aliyekuwa akiitwa Diane walikuwa wakiishi kwenye nyumba moja miongoni
mwa nyumba za shirika la nyumba la taifa la Rwanda eneo liitwalo Block C
nyumba namba 11 na nyumba hiyo ilikuwa ikimilikiwa na mume wa dada
yake aitwaye Jean Felix Akaga. Pia nilikumbuka kuwa huyo Diane na huyo
mumewe Jean Felix Akaga walikuwa wameuwawa hivyo katika familia hiyo
mtu pekee aliyesalia alikuwa Rosine. Na hadi wakati huu nilikuwa sifahamu
kuwa Rosine alikuwa wapi tangu tulipopoteana kule msituni, huenda angeku-
wa ametekwa na kuuwawa au labda angekuwa ametoroka, sikufahamu.
Kwa tathmini hiyo niliona kuwa sehemu salama ya kukimbilia kwanza in-
gekuwa ni huko Block C nyumba namba 11 na uamuzi wangu ukanipa faraja
kiasi huku nikiamini kuwa kama Rosine angekuwa amepata nafasi nzuri ku-
toroka toka kwa wale watu hatari kule msituni basi sehemu ya kwanza ambayo
angefikia ingekuwa ni kwenye hiyo nyumba. Na kwa maana nyingine hiyo
ingekuwa sehemu nzuri ya kuonana naye kwa mara nyingine huku tukiwa ni
wenye furaha na amani na mambo mengine yote yangefuatia baada ya hapo.
Mpango huu ukanipelekea nitabasamu na kuingiza mkono mmoja mfukoni
mwa suruali na sasa kilichobaki ilikuwa ni kupeleleza na kulijua hilo eneo la
Block C na sehemu ilipo nyumba namba11.
Niligeuka nyuma kutazama nikaona hakuna mtu yeyote aliyekuwa akini-
fuatilia kwani kila mtu alionekana kupita na hamsini zake hivyo nikaendelea
kufarijika huku nikizitupa hatua zangu ndefu kuifuata ile barabara ya watem-
bea kwa miguu. Nilifika mbele kidogo sehemu kulipokuwa na jengo dogo
la shirika la posta na hapo nikakunja kona na kuifuata barabara iyelekeayo
upande kushoto huku nikifurahishwa na namna jiji la Kigali lilivyojengwa
kwa mpangilio unaovutia. Kwa wakati huu kila sehemu ya jiji ilionekana
kuchangamka na watu walionekana kukusanyika katika baadhi ya sehemu
za starehe. Biashara ndogo ndogo za barabarani zilikuwa zikiendelea kama
kawaida na hata maduka makubwa yalikuwa wazi huku yamerembwa kwa
mabango makubwa ya taa za aina tofauti zinazopendeza. Jiji la Kigali lilikuwa
limechangamka na pilikapilika za watu zilikuwa mbioni kushamiri.
Niliendelea kutembea katika barabara ile huku nikipishana na watu wa aina
tofauti hata hivyo nilikuwa makini sana kuzichinguza nyuso za watu nili-
opishana nao. Nilipofika mwisho wa barabara ile nikawa nimetokezea kwenye
kituo cha mabasi madogo yanayoelekea maeneo tufauti ya jiji la Kigali. Ku
likuwa na kundi kubwa la abiria waliokuwa wakisubiri usafiri wa kuelekea
maeneo yao. Kufikia hapo nikakumbuka kuwa sikuwa na pesa yoyote mfukoni
na pia nilikuwa silifahamu hilo eneo la Block C lilikuwa wapi toka pale nili-
pokuwa.
Nilifika sehemu fulani na kusimama pale kwenye kituo cha mabasi madogo
huku nikijaribu kumtafuta mtu wa kumuuliza ambaye angekuwa tayari ku-
nielekeza. Baada ya kuchunguza chunguza nikawa nimemuona mzee moja
aliyeonekana kuwa muungwana na mwenye ufahamu mzuri wa jiji la Kigali
hivyo nikaaza kumsogelea lakini kabla sijamfikia nikapata wazo jingine baada
ya teksi fulani kuja na kusimama pembeni yangu.
Dereva wa teksi ile alikuwa kijana wa miaka ishirini na kitu hivi, aliposim-
amisha teksi pembeni yangu akatoa kichwa dirishani na kuniuliza kwa lugha
ya kinyarwada
“Amakuru? sikuweza kumjibu kwani nilikuwa siifahamu lugha ya kinyar-
wanda ingawaje nilikuwa nimehisi kuwa alikuwa akiniuliza “Habari za saa
hizi”. Nikamtumbulia macho kijana yule na nilipomuona kuwa hanielewi
nikaongea kwa lugha yangu mama ya kiswahili.
“Nipeleke eneo liitwalo Block C, unapafahamu?
“Ugiyehe? akaniuliza kwa kinyarwanda yaani “Unaenda wapi?” kama am-
baye hajanisikia vizuri.
“Block C” nikarudia kusema kwa sauti ya juu kidogo yenye msisitizo.
“Uri umushyits? akaniuliza akimaanisha “Wewe ni mgeni hapa?”
“Block C” nikasisitiza huku nikimwona ananichanganya na kinyarwanda
chake.
“Uri u mtanzania? akaniuliza tena yaani akimaanisha “Wewe ni mtanzania?”
“Ndiyo” nikamjibu “Nataka unipeleke eneo liitwalo Block C” nilimwambia
tena huku nikianza kukata tamaa.
“Ufite kibazoki? yule dereva wa teksi akatabasamu na kuniuliza tena
akimaanisha “Unashida gani?” Sikumjibu tena yule dereva wa teksi kwani
nilianza kumuona ni kama anayenipotezea muda wangu hivyo nikaacha kum-
tazama na kugeuka nikitazama upande mwingine huku nikijaribu kuchunguza
kama kulikuwa na teksi nyingine jirani na pale. Yule dereva wa teksi akawa
ameishtukia dhamira yangu hivyo haraka akapenyeza mkono wake kwa nyu-
ma na kufyatua kabari ya mlango.
“Ingia ndani my friend” yule kijana akaniambia kwa kiswanglish cha kin-
yarwanda, sikutaka kujivunga kwani sikupenda kuendelea kupoteza muda pale
na kuvuta macho ya watu. Nikafungua mlango na kuingia nyuma ya ile teksi
na muda uleule ile teksi ikaanza safari ikielekea sehemu ya kutokea magari ya
kituo kile cha mabasi madogo.
Tulipotoka nje ya kituo kile cha mabasi madogo tukaingia barabara ya
upande wa kulia na muda mfupi baadaye tukawa tukiuacha mtaa mmoja na
kuingia mwingine tukiendelea na safari yetu na mimi sikusahau wajibu wangu
hivyo kila mara nikawa nikigeuka nyuma kutazama kama kulikuwa na gari
lolote lililokuwa likitufungia mkia. Safari ilikuwa poa kwani sikuweza kuliona
gari lolote likitufungia mkia nyuma yetu na hivyo safari yetu iliendelea
Tuliwasili eneo la Block C dakika tano zikiwa mbele ya nusu saa kwa muji-
bu wa majira ya saa iliyokuwa kwenye dashibodi mle ndani ya gari. Tulikuwa
ndiyo tunaiingia eneo la Block C wakati nilipomtaka dereva asimame kando
ya barabara ile sehemu kulipokuwa na giza lilofanywa kwa vivuli vya miti ya
barabarani na teksi iliposimama tu nikafungua mlango na kushuka.
“Pesa yangu vipi ndugu? yule dereva aliniuliza kwa mshangao baada ya
kuniona nikishuka bila kumlipa. Sikumjibu badala yake nikaingiza mkono
wangu mfukoni na nilipoutoa nilikuwa nimeshika bastola, yule dereva alipoo-
na vile akawa naye ameshtuka na kunitazama kwa woga. Nikamsogelea karibu
na kumgusagusa shavuni kwa mtutu wa ile bastola na hapo akazidi kutetemeka
kwa hofu.
“Siku moja moja jifunze kujitolea”nilimuonya.
“Sawa ndugu” akanijibu kwa kihoro kama anayepigania roho yake usiuache
mwili.
“Potea!” nikamwambia na muda uleule akatia moto gari na kutokomea
mbele yangu. Nilitabasamu kidogo kisha nikairudisha bastola yangu mfukoni
na kupotelea kwenye vivuli vya miti iliyokuwa eneo lile na muda mfupi baa-
daye nikawa nimetokezea kwenye barabara ya mtaa wa pili.
Kulikuwa na bango kubwa katika barabara ile na bango hilo lilikuwa na
maandishi yaliyoandikwa kwa lugha ya kifaransa yakisomeka “Bien venu au
rendroir C” yaani “Karibu eneo la Block C” na hapo nikatabasamu taratibu
baada ya kuwa na hakika kuwa nilikuwa sijapotea. Sikuwa mgeni sana wa
lugha ya kifaransa kwani nilikuwa nimesoma kwenye shule ya sekondari ya
Milambo iliyopo mkoani Tabora nchini Tanzania. Shule hiyo ilikuwa ni mion-
goni mwa shule chache za serikali zilizokuwa zikifundisha somo la lugha ya
kifaransa nchini Tanzania ukiachilia mbali zile shule za watu binafsi ambazo
kwa idadi zilikuwa chache sana.
__________
ENEO LA BLOCK C LILIKUWA MIONGONI mwa maeneo yenye makazi
ya kisasa kabisa jijini Kigali, nyumba zake zilijengwa kwa mpangilio unaovu-
tia na barabara za lami zenye nguzo za taa pembeni. Wakatinikitembea katika
barabara ya mtaa ule nilihisi kama niliyekuwa nikionekana kwenye nyumba za
jirani hata hivyo suala hilo halikuyumbisha msimamo wangu.
Macho yangu yalizunguka kutazama kila nyumba ya mtaa ule na hadi nafika
mwisho wa ule mtaa geti la nyumba hiyo lilikuwa limeandikwa kwa lugha ya
kifaransa “Maison numero dix” yaani nyumba namba kumi, nikajua nyumba
namba kumi na moja ingekuwa ipo nyuma ya nyumba ile katika mtaa unao-
fuata. Hivyo nilikatisha kwenye uchochoro kuingia mtaa wa nyuma na safari
hii sikuhangaika kwani nyumba namba kumi na moja ilikuwa mbele. Hata
hivyo nilishangaa kuiona kuwa ilikuwa ni nyumba pekee eneo lile isiyokuwa
na uzio pia taa zake zilikuwa zimezimwa lakini hilo halikunishangaza kwani
nilifahamu kuwa wenyeji wa nyumba ile hawakuwepo.
Nilipofika nilizunguka nyumba ile nikaichunguza kama kulikuwa na dalili
za uwepo wa kiumbe chochote mle ndani. Niliporidhika kuwa mle ndani haku
wa na mtu yoyote nikazunguka nyuma na kuingia ndani kwa kupitia dirisha
la jikoni baada ya kukiharibu kitasa chake. Niliingia sehemu ya jikoni nika-
tokezea katika sebule ndogo yenye chumba cha kulia chakula pembeni yake.
Ile nyumba ilikuwa na samani za kisasa na hali hiyo ilinifahamisha kuwa
Jean Felix Akaga, mpelelezi wa kikosi maalumu kilichikuwa kikishughulika
na usalama wa rais wa Rwanda alikuwa ni mtu mwenye kipato cha kudhirisha.
IIikuwa ni nyumba yenye vyumba vitatu vya kulala, choo, maliwato, sebule
na sehemu ya jiko. Kwa muda mfupi nikawa nimeyazoea manzingira ya mle
ndani na kuridhika na usalama wake na hapo nikavua fulana yangu na kuitupa
sakafuni kisha nikaelekea vyumbani.
Nilianza kufanya upekuzi kwenye ile nyumba mle ndani na katika chumba
cha pili niligundua mle ndimo alimokuwa akiishi Rosine kwani mle ndani
nilifanikiwa kupata picha yake na zaidi ya hapo hapakuwa na kitu kingine cha
maana isipokuwa kabati moja liliyokuwa na nguo na lukuki ya vipodozi vya
kila namna. Chumba cha tatu na cha mwisho nilipowasha taa niligundua hara-
ka kuwa huenda kingekuwa ni chumba alichokuwa akiishi Jean Felix Akaga
na Diane. Ndani ya chumba kile sakafuni kulikuwa na zulia maridadi, kitanda
kipana na kizuri, makabati mawili ya nguo, seti moja ya runinga, meza ya
kusomea na kochi moja kubwa la sofa.
Niliyazungusha macho yangu mle ndani nikaziona picha mbili zilizokuwa
zimetundikwa ukutani, picha ya mwanamke na ya mwanaume. Nilianza kwa
kuitazama ile picha ya yule mwanamke na sikutaka kujiuliza kuwa yule aliku-
wa Diane yaani dada wa Rosine kwa namna walivyofanana. Kwa kweli Diane
alikuwa mzuri sana kama aliyokuwa mdogo wake, tabasamu lililochomoza
usoni mwake lilinifanya nijihisi ni kama ninayetazamana naye pale ukutani.
Niliitazama vizuri ile picha ya yule mwanaume nikaona ni kama niliyelinga-
na naye kwa umri, alikuwa amevaa suti nadhifu ya kijivu, shati jeupe na tai
shingoni.
Alikuwa mwanaume mwenye mvuto katika macho ya mwanamke yoyote
na sikuwa na mashaka kuwa ile picha ilikuwa ya Jean Felix Akaga. Kabla ya
kuendelea na udadisi zaidi niliyasogelea yale makabati na kulifungua mojawa-
po. Ndani ya kabati lile niliziona nguo za kiume zilizopangwa kwa unadhifu,
nilitabasamu kidogo baada ya kufikiria kuwa nilikuwa nimepata nguo za kuba-
dilisha. Nilisogea karibu na kioo cha kabati lile nikajitazama na kuridhika kwa
namna nywele na ndevu zangu zilivyokuwa na kuubadilisha kidogo ule mu-
onekano wangu wa wakati nilipokuwa nikiingia hapa jijini Kigali.
Kwa kitambo kidogo nilisimama mbele ya kioo kile nikijitazama bila akili
yangu kuwepo pale kwani mawazo juu ya Rosine yalikuwa yakianza kupita
upya kichwani mwangu na wakati huu nilianza kuhisi kupungukiwa na kitu
moyoni mwangu. Sijui ni kwanini nilikuwa nimetokea kumpenda sana Rosine
ingawa hapo nyuma niliwahi kukutana na wasichana wazuri wa kila sampuli
katika nchi tofauti tofauti nilizowahi kufika wakati nilipokuwa katika harakati
zangu za kijasusi.
Nilikumbuka wakati ule nilipokuwa na Rosine katika ile nyumba ya ma-
ficho kule msituni nikiwa nimelala juu ya kitanda kimoja na mrembo huyo
huku akiniruhusu kukitomasa tomasa kiuno chake na kuzifikicha chuchu zake
kifuani bila pingamizi lolote. Loh! kwa kweli hisia juu ya Rosine zilikuwa
zikinitafuna moyoni na sasa nilikuwa ndani ya nyumba hii bila yeye. Roho
iliniuma sana kwani sikufahamu kama Rosine alikuwa hai au mfu, na kama
alikuwa hai alikuwa wapi kwa wakati huu. Kwa kweli nilihisi upungufu wa
kitu fulani katika nafsi yangu.
Kwa muda wote ambao ningeendelea kuwepo nchini Rwanda nilikuwa
nimeazimia kuwa nyumba hii ingekuwa maskani yangu kwani sikuona sababu
ya kuingia gharama za kukaa kule hotelini, tena katika sehemu nisiyokuwa na
hakika ya usalama wake. Kitu cha kwanza nilichofikiria ilikuwa ni kuoga na
kubadilisha zile nguo zangu mwilini ambazo mpaka sasa zilikuwa chafu na
zinazonuka jasho. Hivyo nilivua nguo nikajifunga taulo nililolichukuwa mle
kabatini na kuingia bafuni.
Muda mfupi baadaye nilitoka bafuni na kujiandaa vizuri nikiwa na nguo
mpya na safi mwilini, nilipomaliza nilielekea kule jikoni na kufungua jokofu
lililokuwa na vyakula lakini vingi vikiwa vya kutoka kwenye maduka makub-
wa ya kisasa ama super market. Nikachukua pakiti mbili za soseji ya ng’ombe,
mayonaizi, vinega na karoti. Kulikuwa na trei moja ya mayai juu ya kabati la
vyombo lililokuwa mle jikoni hivyo nilichukuwa mayai mawili na kwa pamo-
ja nikatengeneza mlo kupitia jiko la gesi lilokuwa pale jikoni.
Ilikuwa imetimia saa nne kasoro usiku wakati nilipokuwa nimeketi mezani
kula. Nilijipatia mlo na kushiba vizuri kisha nikasukumia kwa mzinga mmoja
wa mvinyo mwekundu uliokuwa kwenye kabati la vinywaji lililokuwa mle
ndani pale sebuleni na wakati huo nilikuwa nimewasha runinga kubwa iliy-
okuwa pale ndani sebuleni nikitafuta stesheni inayorusha habari za nchi ya
Rwanda. Niligundua kuwa stesheni nyingi zilizokuwa zikipatikana kwenye
ile runinga zilikuwa zikirusha matangazo yake kwa lugha ya kifaransa huku
baadhi ya stesheni chache zikirusha matangazo yake kwa lugha ya kinyar-
wanda.
Hakukuwa na habari yeyote ya maana iliyonivutia katika stesheni niliyoi-
fungua isipokuwa stesheni moja tu iliyokuwa ikirusha habari kuwa rais wa
Rwanda Juvenal Habyarimana alikuwa amesafiri kwenda nchini Tanzania ku-
kutana na marais wengine wa nchi za ukanda wa maziwa makuu kuzungum-
zia masuala mbalimbali likiwemo suala la amani ya kudumu katika nchi ya
Rwanda na Burundi na masuala mengine ya kiuchumi. Taarifa zile ziliendelea
kueleza kuwa katika msafara huo wa rais kwenye ndege yake Falcon 50 Jet
angeambatana na mkuu wake wa majeshi Deogratias Nsabimana na mkuu wa
usalama wa rais Kanali Elie Sagatwa.
Nilipoitafakari taarifa ile nikajikuta nikifurahi kwa namna viongozi wetu
wa Afrika walivyokuwa wakishirikiana kama ndugu wa familia moja katika
kuziletea maendeleo nchi zao. Kisha vikafuatia vipindi vingine vya runinga
ambavyo havikuonekana kunivutia hivyo niliamua kuizima ile runinga pale
sebuleni. Nilihisi kuwa akili yangu ilikuwa imepata utulivu wa kutosha wa
kuweza kutafakari hili na lile na kutengeneza hoja zenye msingi na wakati nili-
pokuwa nikitafakari nikaikumbuka ile bahasha ya kaki niliyoichukua chini ya
godoro kwenye kile chumba cha mwenyeji wetu ndani ya ile nyumba iliyoku-
wa kule katikati ya ule msitu. Wazo hilo likanifanya ninyanyuke na kuelekea
kule chumbani nilipoiacha ile suruali yangu niliyotokanayo kule msituni am-
bamo ile bahasha ilikuwa ndani ya mfuko wa suruali hiyo.
Muda mfupi baadaye nikawa nimerudi na ile bahasha pale sebuleni na hapo
nikaketi kwenye kochi. Kabla ya kuifungua ile bahasha niliyapitisha macho
yangu nikiichunguza kwa juu hata hivyo sikufanikiwa kuona kitu chochote
mle ndani kwani ile bahasha ilifungwa kwa gundi kali na karatasi yake hai-
kuruhusu macho yangu kupenya na kuona ndani. Hivyo nikaichana ile baha-
sha kwa juu na kuchungulia ndani na hapo nikaiona karatasi yenye rangi ya
samawati. Mwanzoni nilipoichunguza ile karatasi haikuwa na maana yoyote
kwangu kwani sikuweza kuona chochote kilichoandikwa kwenye karatasi ile.
Hata hivyo mimi sikuwa mshamba wa karatasi za namna ile hasa pale nili-
pofikiria kuwa hakuna binadamu mwenye akili timamu ambaye angetumbuki-
za karatasi isiyo na kitu ndani ya bahasha na kuifunga kwa gundi kali namna
ile.
Baada ya kuigeuzageuza ile karatasi na kuichunguza vizuri nikajikuta niki-
tabasamu. Ilikuwa ni aina fulani ya karatasi inayotumiwa sana na majasusi ka-
tika kupashana habari. Karatasi ambayo ili kuweza kuyasoma maelezo ndani
yake nilihitajika niwe na kalamu ya grafati. Kupitia kalamu hiyo ningeilaza
ile karatasi juu ya meza au juu ya kitu chochote kilichonyooka vizuri halafu
baada ya hapo ningeanza kuichorachora ile karatasi huku nikiwa nimeilaza
kalamu hiyo ya grafiti katika pembe isiyozidi nyuzi ishirini na tano ili niweze
kupata taswira nzuri ya kilichoandikwa ndani ya karatasi husika. Kwa kawaida
karatasi ya namna hii zinapotumwa kwa mhusika hutumwa pamoja na kalamu
yake maalumu.
Kwa kulikumbuka hili nilizidi kuifungua ile bahasha na muda si marefu
kweli nikaiona kalamu ndogo ya grafiti iliyochongwa vizuri. Niliichukua ile
kalamu kisha nikachukua kitabu fulani kilichokuwa kwenye rafu pale sebuleni
na juu ya kitabu hicho nikailaza ile karatasi kisha nikaanza kuichorachora ile
karatasi kwa ule wino wa ile kalamu ya grafiti.
Mwanzoni nilidhani kuwa ile karatasi ingekuwa na mchoro fulani wa siri
ambao zingehitajika jitahada za kipekee katika kuutafsiri ili kuweza kuuele-
wa maana yake kwani mara nyingi karatasi za namna hii hutumika kupeleka
ujumbe kwa njia ya mchoro. Lakini kadiri nilivyokuwa nikizidi kuichorachora
karatasi ile nikawa naanza kuona herufi, nilipozidi kuchora zaidi herufi zile
zilianza kuunganika na kutengeneza sentensi fulani.
Niliendelea kuichora ile karatasi hadi mwisho na nilipomaliza nikaona mu-
unganiko wa sentensi kamili inayoleta maana ingawaje sentensi hiyo haikuwa
na maana kamili kwangu. Sentensi yote kwenye karatasi ile ilikuwa imeandik-
wa kwa lugha ya kifaransa ikisomeka,
“Mecred recontre avec elle en Halfmoon bar à 22:00hrs avant de nous com-
mencer, chaque chose est soyez bien”
Kwa kutuumia karatasi ileile nikaigeuza nyuma na kuanza kutafsiri neno
moja baada ya jingine kwa lugha yangu ya kiswahili na nilipomaliza nikawa
nimepata tafsiri kamili ya maneno yale ambayo yalimaanisha kuwa,
“Jumatano onana naye ndani ya Halfmoon bar saa nne usiku kabla hatu-
jaanza. Kila kitu kipo tayari”
Nilipomaliza kusoma sentensi hiyo moyo ulikuwa ukinienda mbio sana
na sikuweza kufahamu ni kwanini hali ile ilikuwa ikinitokea. Niliendelea
kuichunguza chunguza tena ile karatasi hata hivyo sikuweza kuliona jina la
mwandishi wala mtumiwaji wa ujumbe ule. Ila kwa kuwa nilikuwa nime-
ichukua ile bahasha toka chumbani kwa yule mwenyeji wetu aliyejinadi kwa
jina la Innocent Gahizi kwenye ile nyumba kule msituni hivyo niliamini kwa
vyovyote mtumiwaji angekuwa ni yeye.
Niliendelea kutafakari ujumbe ule kwenye ile karatasi bila kupata maana
yoyote kamili inayonipa picha ya nini kilichokuwa kikiendelea. Nilitembe-
za macho yangu kuitazama kalenda iliyokuwa imetundikwa pale sebuleni na
hapo moyo wangu ukapiga kite kwa nguvu kwani siku ile ilikuwa ni siku ya
jumatano kwa mujibu wa kalenda ile ilivyoonesha, yaani siku ambayo ujumbe
ule ilikusudiwa kufanyiwa kazi. Nikageuka kuitazama saa ya ukutani pale se-
buleni, tayari ilikwisha timia saa tatu na robo usiku hivyo zilikuwa zimesalia
dakika arobaini na tano tu kutimia saa nne usiku muda wa miadi.
Nikavuta pumzi nyingi na kuitoa taratibu huku nikianza kuhisi kuwa kuliku-
wa na hatari kubwa iliyo kuwa mbele yangu endapo ningeamua kujitumbukiza
katika mkasa huu usioeleweka. Hata hivyo kulikuwa na kitu kilichokuwa kiki-
nisukuma moyoni kuwa nisimame na kuanza kuitafuta Halfmoon Bar. Kingine
kilichonisukuma kutaka kufuatilia mkasa huu ni pale nilipowaza kuwa kwa
vyovyote mtu aliyekusudiwa kuupata ujumbe huu hadi wakati huu alikuwa
bado hajausoma na kuuelewa maana yake kwani mimi ndiye niliyekuwa mtu
wa kwanza.
Hivyo nilikuwa na hakika kuwa ndani ya hiyo Halfmoon Bar huo muda wa
saa nne usiku kungekuwa na mtu fulani anayemsubiri huyo mtu mwingine am-
baye bila shaka mtu huyo anayesubiriwa ndiye huyo ambaye ujumbe huu uli-
kusudiwa kwake. Na kwa kuwa mhusika huyo alikuwa bado hajaupata ujumbe
huu asingeweza kufika kwenye miadi na badala yake mimi ndiyo ningeitumia
nafasi hiyo. Niliendelea kuwaza nikapiga moyo konde na kusimama. Akili
yangu yote sasa ilikuwa ni wapi ambapo ningeipata hiyo Halfmoon Bar hapa
jijini Kigali.
__________