3
FAHAMU ZILIPONIRUDIA nilijikuta nimeketi kwenye kiti huku miguu na
mikono yangu imefungwa kamba ndani ya chumba kilichofanana na pango
dogo. Nilikua nimevuliwa nguo zote na kubaki uchi wa mnyama, baridi kali ilikuwa ikinitafuna mwilini na nilipojaribu kufumbua macho kwa shida sikuweza kuona kitu chochote mbele yangu kwani nilikua bado nimefunikwa na ule
mfuko mweusi. Hisia zangu zilinieleza kuwa mle ndani kulikuwa na watu hata
hivyo sikuweza kuwaona kutokana na kichwa changu kufunikwa. Ni kama
watu wale walinihisi kuwa nilikua nimerudiwa na fahamu kwani nilisikia sauti
nzito ya kiume ikitoa amri mbele yangu.
“Muondoe kitambaa anarejewa na fahamu huyo” muda uleule mara nikasikia sauti ya hatua za mtu ikinijia kwa nyuma, moyo ukaanza kunienda
mbio huku nikijiuliza pale nilikuwa wapi, nikifanya nini na watu wale waliosemeshana walikua ni akina nani.
Ile sauti ya hatua za yule mtu ilikuja na kuishia kando yangu na hapo nikasikia ule mfuko mweusi niliokuwa nimefunikwa kichwani ukivutwa kwa
juu na hapo nikabaki nikitumbua macho huku nikihisi kizunguzungu kikipita
kichwani mwangu. Nikaanza kuzungusha macho yangu mle pangoni na hapo
nikawaona watu wanne mle ndani, watatu walikua wameketi kwenye viti nyuma ya meza kubwa iliyokuwa mbele yao huku juu ya meza hiyo kukiwa na
taa moja ya kandili iliyokua imewashwa na kutoa mwanga hafifu na sehemu
nyingine zote za chumba kile zilikuwa na giza.
Niliwatazama wale watu mbele yangu na sikuweza kumtambua hata mmoja wao, zilikuwa sura ngeni kabisa na miongoni mwao hakuwepo hata mmoja
kati ya wale wanajeshi walioniteka kule porini. Hata hivyo walikuwa ni maafisa wa ngazi za juu wa jeshi la wananchi wa Rwanda, niliwatambua kutokana
na mavazi yao ya kiafisa wa jeshi kwa namna yalivyokuwa yamechafuka vyeo
vya kila namna isipokuwa mmoja wao ambaye alionekana kuwa ni mwanajeshi mwenye cheo cha chini sana yaani kuruta ambaye ndiye aliyekuwa akitumikishwa mle ndani. Wakati nikiendelea kutafakari ile hali ya mle ndani nikajikuta nikimwagiwa maji ya baridi kichwani na yule askari mwenye cheo cha kuruta na hapo
nikawaona wale maafisa wa jeshi mbele yangu wakitabasamu. Wakaniacha
nijitikisetikise kuyaondoa yale maji usoni mwangu kwani nilikuwa nimefungwa na nilipotulia afisa yule alieketi mbele yangu katikati ya wenzake akaanza
kunisemesha baada ya kunywa funda moja la kahawa iliyokuwa kwenye kikombe juu ya meza ile mbele yake. Uso wake haukuonesha hata chembe ya
mzaha.
“Una bahati sana kuwa mpaka sasa upo hai tena bila ya kutuhonga chochote
ndugu Patrick Zambi ingawa mimi nitaendelea kukuita Luteni Venus Jaka,
mwanajeshi wa jeshi la wananchi wa Tanzania”
Nilishtuka sana kusikia jina langu halisi likitajwa na afisa yule wa jeshi,
moyo wangu ukawa kama uliopigwa shoti kali ya umeme wenye nguvu za
ajabu hali iliyonifanya nijihisi kama niliyeugua maradhi ya kiharusi. Kwa
sekunde kadhaa nilihisi akili yangu ilikuwa imevurugika kabisa, nilipotulia
nikabaki nikimtazama afisa yule kwa makini huku kurasa za kitabu changu
cha kumbukumbu zikianza kufunuka moja baada ya nyingine kichwani. Muda
mfupi baadaye nilijikuta nikishusha pumzi taratibu na kuishiwa nguvu, nikaachama mdogo wazi kwa mshangao kwani sikuamini macho yangu.
“Kanali Bosco Rutaganda...” nilijikuta nikinong’ona kwa sauti ya chini
huku nikishindwa kuamini macho yangu. Ukweli ni kwamba mara ya mwisho
kuonana na kanali Bosco Rutaganda ilikuwa ni miaka minne iliyopita mkoani
Arusha Tanzania katika chuo cha mafunzo ya kijeshi cha Tanzania Military
Academy (T.M.A) Monduli. Wakati huo mimi nikiwa ni mmoja wa wakufunzi
wa chuo hicho kwa wanafunzi waliokuwa wakisomea mafunzo ya uafisa wa
jeshi kutoka nchi kumi na moja za bara la Afrika. Nchi hizo zikiwemo D.R
Congo, Kenya, Malawi, Uganda, Botswana, Zimbabwe, Msumbiji, Tanzania, Djibout, Burundi na Rwanda. Naam! sasa nilimkumbuka vizuri kanali
Bosco Rutaganda kipindi hicho akiwa miongoni mwa wanafunzi wangu, na
hapa nilimtazama akiwa katika suti yake nadhifu iliyokitambulisha vizuri cheo
chake cha kanali.
“Luteni Venus Jaka! kweli milima haikutani lakini binadamu tunakutana na
bahati mbaya sana ni kuwa maisha huwa yanabadilikabadilika ndiyo maana
leo upo uchi mbele yangu kama mchawi. Niliposikia kuwa ni wewe ndiye
uliyetumwa hapa Rwanda nilijikuta nikifurahi sana kwani nilijua hii ndiyo
ingekuwa nafasi nzuri ya kuonana kwetu tangu tulipopoteana miaka minne
iliyopita rafiki yangu”
“Mbona sikuelewi unachoongea” nilimkatisha kwa hasira “Nyinyi ni akina
nani na mnashida gani na mimi?
“Usijidanganye kuwa nimekusahau Luteni hukumbuki kuwa miaka minne
iliyopita ulishiriki kikamilifu katika jopo la maafisa wa kijeshi kutoa hukumu
dhidi yangu nchini Tanzania. Eti kuwa nifukuzwe kwenye mafunzo yale ya
kijeshi kisha nikamatwe na kufunguliwa mashtaka ya uhaini kwa kuwa nilikuwa kwenye orodha ya watu waliokuwa wakipanga njama ya kumpindua
Rais wa Rwanda.Mlijitahidi sana lakini bahati mbaya hamkufanikiwa kwani nilikuwa mjanja
zaidi yenu nikawaacha kwenye mataa, viongozi wa kijeshi wa jeshi la Rwanda
wanaufahamu vizuri mchango wangu katika nchi hii, nawashukuru tu kwa
kuwa hawakunitupa na ndiyo maana hadi leo hii bado nipo jeshini naitumikia
nchi yangu nikiisubiri ile siku ya mapinduzi ya kweli na bila shaka dunia
itafahamu nini kinachoendelea katika nchi hii” Kanali Bosco Rutaganda alizungumza kwa hisia huku akinitazama.
“Mbona unaongea kama unayetaka kulia kanali?, ni mapinduzi ya namna
gani hayo ambayo utaweza kuyafanya mtu mwoga kama wewe unayejificha
kwenye pango hili kama Popo?
“Ndiyo maana sikupenda uuwawe mapema kwani ningeweza kufanya hivyo
ila niliamua kuichelewesha safari yako ya kifo nikitaka siku ile ya mapinduzi
ikukute ukiwa hai, ujionee mwenyewe mambo yatakavyokuwa halafu baada
ya hapo nitajua namna ya kukufanya”
“Ni mapinduzi gani hayo unayozungumzia?
“Mapinduzi ya kuwarudishia uhuru wazawa wa nchi hii, uhuru wao waliopokonywa na kupewa kundi dogo la watu wachache ambao kimsingi wao ni
wavamizi tu”
“Mimi sikuelewi ni uhuru gani huo unaouzungumzia. Ninavyofahamu ni
kuwa nchi zote za Afrika zimekwisha pata uhuru wake toka kwa wakoloni sasa
huo uhuru unaozungumzia wewe ni upi?
Nilimuuliza Kanali Bosco Rutaganda na hapo nikamuona yeye na wale
wenziwe wakicheka, sikufahamu kitu kilichokuwa kikiwachekesha nikabaki
nikiwatazama kwa hasira. Kanali Bosco Rutaganda akachukua kile kikombe
cha kahawa pale mezani na kunywa mafunda kadhaa alipokirudisha mezani
aliendelea
“Nani aliyekudanganya kuwa nchi zote za Afrika zimepata uhuru Luteni?,
kama zimepata uhuru mbona bado haziwezi kujiendesha zenyewe?, huo unaosema wewe si uhuru bali ni kubadilisha aina nyingine ya mfumo wa ukoloni
na mbaya zaidi wakoloni wa sasa ni waafrika kama sisi wanaozijua vizuri
shida za nchi hizi”
“Mbona sikuelewi Bosco kwa nini usiniweke wazi badala yake unajiongelesha kama baamedi aliyenunuliwa bia na basha wake” nilimuuliza Kanali
Bosco Rutaganda huku nikimtazama kwa hasira hata hivyo sikumuona kama
alikuwa akifanya jitihada zozote za kutaka kujibu swali langu badala yake
nilimuona akigongeshagongesha vidole vyake juu ya meza huku akinitazama
bila kuzungumza neno kisha akavunja ukimya
“Tuambie Luteni ni kitu gani kilichokuleta hapa Rwanda? aliniuliza huku
chuki ikionekana dhahiri machoni mwake.
“Kwani mimi siruhusiwi kuingia hapa Rwanda? nilimuuliza huku nikimtazama.
“Jibu swali kama ulivyoulizwa siyo unauliza swali” yule kamanda aliyekuwa upande wa kulia wa Kanali Bosco Rutaganda alinifokea.
“Nilikuja kutembea”
“Kwa nini ukajiita Patrick Zambi wakati wewe ni Luteni Venus Jaka?
kwanini hukutaka kutumia jina lako?
“Tatizo ni mimi kuwa na majina mawili au tatizo ni mimi kuja hapa Rwanda? Niliuliza na hapo nikamuona Kanali Bosco Rutaganda akimtazama
yule askari kuruta aliekuwa karibu yangu. Muda uleule nikaanza kupewa
mkong’oto wa nguvu wa makofi ya kichwani na ngumi za tumbo, kwa kweli
nilisikia maumivu makali sana na damu ikaanza kunitoka puani na mdomoni.
Yule askari hakuacha kunishushia kibano na alikuwa akifanya kwa sifa ili kuwaridhisha wakubwa zake. Walipoona kichapo kile kimenikolea wakamwambia yule askari aniache.
Kwa kweli askari yule alikuwa amebobea katika kutoa mkong’oto maana
kichapo kile kiliniingia sana nikachanika mdomoni na kutapakaa damu mwili
mzima. Aliponiacha nikabaki nikihema hovyo na hapo nilimuona Kanali Bosco Rutaganda akikichukua tena kile kikombe cha kahawa mezani na kuvuta
funda moja alipokirudisha mezani alibaki akitabasamu.
“Hata kama ukiendelea kutuficha tunajua kwa hakika kuwa umetumwa
hapa Rwanda na kwa taarifa yako habari zako tulizipata mapema sana Luteni” Kanali Bosco Rutaganda aliendelea kuongea na hapo nikainua macho
kumtazama, nikagundua kuwa alikuwa akimaanisha alichokua akikisema.
Moyo wangu ukapiga kite kwa nguvu “Ina maana nilikuwa nimeuzwa!” nilijisemea moyoni huku nikiwaza ni nani ambaye angeweza kutoa taarifa zangu
kwa watu hawa na hapo nikajikuta nikumkumbuka Brigedia Masaki Kambona
ambaye ndiye aliyekuwa mratibu mkuu wa safari zangu za kijasusi kutoka
jijini Dar es Salaam. Hata hivyo akili yangu ilishindwa kabisa kumuhusisha
na sakata hili kwani Bregedia Masaki Kambona alikuwa si tu bosi wangu
mwenye cheo kikubwa cha kijeshi ila pia rafiki yangu wa karibu sana pamoja
na utofauti mkubwa wa vyeo uliotutenganisha.
Vilevile sikuona sababu yoyote ya yeye kuniuza kwani hapakuwa na sababu
yoyote ambayo ingempelekea kufanya hivyo, istoshe hii haikuwa operesheni
yangu ya kwanza ya kijasusi kuifanya nikiwa chini yake. Kwa kweli nilijisikia
kuishiwa nguvu huku nikijihisi kuchanganyikiwa na kukata tamaa.
“Nani aliyewapa taarifa zangu? niliwauliza hatimaye na hapo wakaanza
tena kuangua kicheko cha kejeli, nikabaki nikiwatazama huku hasira zimenipanda. Nilijitahidi kufurukuta pale kwenye kiti bila mafanikio badala yake
nilitulizwa na ngumi mbili za puani toka kwa yule askari kuruta aliyekuwa
amesimama pembeni yangu. Nikapiga yowe la maumivu huku damu ikianza
kunitoka puani, nikawa najisikia kutaka kutapika.
“Tulia wewe kenge” yule askari Kuruta alinionya na hapo nikakumbuka
kuitazama ile saa yangu ya mkononi hata hivyo nilijikuta nikikata tamaa pale
nilipokumbuka kuwa nilikua uchi na vitu vyangu vyote nilikuwa nimevuliwa. Giza zito la mle ndani halikuweza kabisa kunifanya niweze kukisia kuwa
muda ule ulikuwa ni saa ngapi hivyo nilijikuta nikimkumbuka Mutesi huku
nikijiuliza kuwa angefanya nini endapo angefika kule Hotel des Mille Collines na kunikosa?, na vipi kama ingetokea Niyonkuru angenitafuta kupitia zile
namba za simu nilizompa na kunikosa?. Bila shaka ningekuwa nimepoteza
hatua muhimu sana katika harakati zangu.
Loh! Kwa nini nilikubali kukamatwa na watu hawa hatari na hapa ni wapi?
nitabahatika kweli kutoka nikiwa salama? niliendelea kujiuliza bila kupata majibu. Halafu wakati nilipokua nikiendelea kuwaza wazo la Jean Pierre
Umugwaneza likatumbukia katika fikra zangu, Jean Pierre Umugwaneza
alikuwa wapi na kipi kilikuwa kimemsibu hadi asiweze kupatikana kwenye
simu? mpaka kufikia hapa nilijihisi kuchanganyikiwa.
“Luteni!” Kanali Bosco Rutaganda aliniita na hapo nikayakatisha mawazo
yangu na kuinua macho kumtazama.
“Wewe ni kiongozi mkubwa wa jeshi na bila shaka unafahamu vizuri hukumu aipatayo mtu pale anapokamatwa akifanya shughuli za kijasusi katika
nchi nyingine tena mbaya zaidi kwa manufaa ya nchi yake” aliniuliza na hapo
nikabaki nikimtazama katika hali ya kukata tamaa.
“Adhabu yake huwa ni kifo. Kifo tu ndiyo malipo stahili ya kazi kama hiyo
na bila shaka uliingia hapa nchini Rwanda ukiwa unaifahamu vizuri adhabu
hiyo” Kanali Bosco Rutaganda aliendelea kuongea huku akimalizia kunywa
funda la mwisho la kahawa iliyobakia kwenye kile kikombe mezani halafu
akasimama na hapo niliwaona wale wenzake nao wakisimama.
“Endelea kufikiria nini cha kutueleza vizuri tukakuelewa ili tutakapokutana
tena uwe na majibu yaliyonyooka” Kanali Bosco Rutaganda akaniambia kisha
akageuka tena na kumtazama yule askari Kuruta aliyekua amesimama pembeni yangu na hapo hofu ikaniingia kwani nilikuwa nafahamu ni tukio gani ambalo lingefuatia. Mara ghafla nikasikia kitu kizito kikinipiga nyuma ya kichwa
changu, nikapiga yowe kali la maumivu hata hivyo ni kama sauti ile ya yowe
nilikua nikiisikia peke yangu mle ndani kwani hakuna aliyeshtuka.
Muda uleule nikaanza kuona giza huku viungo vyangu mwilini vikiishiwa
nguvu, macho yangu yakafumba na sikusikia tena kilichokuwa kikiendelea,
fahamu zikanitoka.
_________
NILIPOFUMBUA MACHO nilihisi maumivu makali sana nyuma ya
kichwa na mgongoni kwangu, mikono yangu ilikuwa bado imefungwa hivyo
sikuweza hata kupapasa eneo lile ambalo wakati huu lilikuwa limeshatawaliwa na giza zito. Niliyatega vizuri masikio yangu lakini hata hivyo sikuweza kusikia sauti ya kitu chochote eneo lile hata pale nilipoituliza vizuri akili
yangu. Hata hivyo nilikumbuka kuwa fahamu zilikuwa zimenitoka baada ya
kupigwa na kitu kizito mara tu sehemu ya kwanza ya mahojiano yangu na
Kanali Bosco Rutaganda ilipomalizika kwenye lile pango dogo na baada ya
hapo sikufahamu kilichoendela.
Fahamu ziliponirudia vizuri nilihisi maumivu ya mgongoni yaliyokuwa yakiongezeka kadiri muda ulivyokuwa ukienda, nilipotuliza vizuri akili yangu
nikashtuka kuwa nilikuwa nikiburutwa katika sakafu ya eneo lile. Miguu yangu ilikuwa imefungwa minyororo na mvutaji alikuwa mbele yangu akiendelea
kuniburuza hivyo nikaelewa kuwa yale maumivu ya mgongo yalitokana na
machibuko niliokuwa nikiyapata katokana na kule kuburuzwa. Nilijitahidi kujitetea bila mafanikio kwani yule mvutaji bado alikuwa akiendelea kuburuta minyororo ile iliyonifunga miguuni.
Matundu ya pua yangu yaliweza kupitisha harufu mbaya ya uvundo iliyokuwa eneo lile hali iliyonifanya nijisikie kutaka kutapika hata hivyo sikuweza
kutapika kwani tumboni hakukuwa na kitu chochote. Nilihisi njaa kali sana,
njaa iliyoambatana na hali ya homa pengine kutokana na ile baridi kali ya mle
ndani. Maumivu ya mgongo yalikuwa makali mno kiasi kwamba nilianza
kuhisi kuwa nilikuwa nikichubuka nyama zangu za mgongoni kutokana na
mburuzo ule sakafuni.
Mara ghafla tulisimama eneo fulani ambalo nilisikia ukimya wa kupita kiasi halafu mara nikasikia kelele za kitu kama funguo zilizokuwa zikifungua
kwenye kitasa mlangoni huku mfunguaji akionekana kutokuwa na uhakika
wa funguo halisi. Muda uleule mara nikaona mlango fulani wa eneo lile ukifunguliwa na hapo nikaona mwanga hafifu toka ndani ya mlango ule ukipenya
nje, muda huohuo nikasikia kelele za minong’ono hafifu toka ndani ya chumba kile. Hofu ilinishika sana kwani sikufahamu watu wale walikuwa ni akina
nani.
Yule mtu aliyekuwa akiniburuta sasa alikuwa amesimama pale mlangoni
akitazama mle ndani ya kile chumba. Nilipomtazama kwa makini mtu yule
nikamkumbuka kuwa alikuwa ni yule askari kuruta aliekuwa kule pangoni
na wale maafisa wengine wa jeshi la Rwanda akiwemo Kanali Bosco Rutaganda. Japokuwa sikuweza kumuona vizuri lakini nilimtambua kutokana na
umbo lake, urefu na magwanda ya jeshi aliyoyavaa. Alipomaliza kutazama
mle ndani ya kile chumba akageuka kunitazama na hapo nikahisi kama niliyekuwa nikitazamwa na mnyama mkali mwenye njaa. Muda uleule yule mtu
akaishika ile minyororo na kuanza kunivutia pale aliposimama, nilipomfikia
akanifungua ile minyororo miguuni na kunisimamisha huku akinitazama na
kuangua kicheko hafifu cha dharau.
“Wewe ndiye Luteni? Luteni nani sijui huko, Luteni gani unakuwa na tabia
za kishogashoga za kuingilia mambo yasiyokuhusu. Utakaa humu ndani na
wenzako mpaka hapo hukumu yako itakaposomwa” yule Kuruta aliniambia
kwa dharau na muda uleule nami nikakusanya mate mdomoni na kumtemea
usoni.
Akanitazama kwa hasira usoni kisha kwa kutumia kitambaa cha gwanda
lake mkononi akajifuta yale mate na hapo akageuka na kuanza kinishushia
kichapo cha nguvu cha ngumi na mateke ya tumbo. Nilihisi maumivu makali
mno ambayo sikuwahi kuyasikia hapo kabla. Aliporidhika na kichapo alichonitandika akanisukumiza ndani ya chumba kile kwa pigo la teke la mgongoni. Nikaingia ndani mzimamzima na kuanguka chini kisha nilisikia ule
mlango ukifungwa nyuma yangu.
__________
NIKIWA NIMEKATA TAMAA sana pale chini niliinua macho yangu kutazama mbele yangu, mwanga hafifu wa taa ndogo ya kandili iliyokuwa katikati
ya chumba kile mfano wa pango kama lile la awali uliniwezesha kuwaona
watu waliokuwa mle ndani na hapo nilishikwa na mshangao nikisikitishwa na afya za watu wale kwani walikuwa wamekondeana sana kiasi cha sehemu za
mifupa ya miili yao kuchomoza. Walikuwa wamekonda haswa hata vichwa
vyao vilionekana kama mafuvu, meno yao yalichomoza nje na macho yao yalikuwa yameingia ndani ya vishimo na kuwafanya watishe sana kuwatazama.
Harufu kali ya uvundo iliyokuwa mle ndani ilinifanya nijihisi kutaka kutapika. Mbaya zaidi watu wale walichanganywa kwa pamoja wanawake kwa
wanaume wote wakiwa uchi “Balaa gani hili? nilijisemea. Wakati nikiendelea kutazama mle ndani mara nikasikia mkono wa mtu ukinigusa begani na
hapo nikageuka taratibu kumtazama yule mtu aliyenigusa. Nilishangaa sana
nilipomwona Jean Pierre Umugwaneza nyuma yangu na hapo tukabaki tukitazamana kwa mshangao.
“Pole sana Patrick” Jean Pierre Umugwaneza aliniambia huku akinisaidia
kuninyanyua pale chini, niliposimama niliendelea kumtazama nikishindwa
kuamini macho yangu.
“Jean... ni wewe?” nilimuuliza.
“Ni mimi, sikutegemea kukuona humu ndani Patrick imekuaje? aliniuliza
kwa mshangao.
“Ni hadithi ndefu Jean hata mimi sikutarajia kukuona hapa, nilikuwa na hisia mbaya nikidhani pengine ulikuwa umeuwawa baada ya kukutafuta kwenye
simu na kukukosa”
“Oh! Patrick nilijua tu kuwa ungenitafuta lakini waliwahi kunikamata hivyo
nikabaki nikimwomba Mungu atukutanishe tena” Jean aliendelea kuongea
huku machozi yakimtelemka mashavuni, nikampigapiga kidogo kifuani kumtia moyo.
“Usijali Jean tupo pamoja, sisi ni marafiki sasa lazima tuimalize safari yetu
pamoja kama tulivyoianza” nilimwambia na hapo nikaiona sura yake ikirudiwa na tumaini, akanivuta na kunikumbatia kwa sekunde kadhaa kabla ya
kuniachia kisha niligeuka kuwatazama wale watu wengine waliokuwa mle
pangoni.
Wote walikuwa wakitutazama na baadhi walikuwa wakilia. Nilisimama
taratibu nikiwatazama watu wale ambao walikuwa wa rika tofauti wanawake
kwa wanaume wote wakiwa uchi bila ya nguo kama mimi. Aibu aliniingia hata
hivyo sikuona sababu ya kuziba utupu wangu kwani watu wote mle ndani ni
kama tulifanana tu ingawaje nilihuzunishwa sana na baadhi yao kwani afya
zao zikionekana kudhoofika sana.
Harufu mbaya ya uvundo ilikuwa imesambaa kila kona mle ndani na cha
kustaajabisha sikumuona hata mmoja miongoni mwa watu wale aliyeonekana
kutaabishwa na harufu ile mbaya. Nikageuka kutazama sehemu za wazi iliyoonekana kutengwa na wale watu mle ndani na hapo nilishtuka sana kuuona
mwili wa mtu fulani ukiwa umelala sakafuni sehemu ile.
Nikapiga hatua taratibu kuuendea ule mwili na nilipoufikia nilishtuka kuwa
ile ilikuwa ni maiti ya mwanamke yenye majeraha ya kutisha. Mwili wa mwanamke yule ulikuwa umeanza kuharibika na baadhi ya nyama za mwili wake
zilikuwa zimeanza kupukutika. Macho yake yaliingia ndani na kuacha vishimo, mifupa ya mashavuni ilikuwa imechomoza nje na mdomo wake ulikuwa wazi huku amekenua meno. “Mungu wangu!” nilijisemea huku nikiuziba
mdomo na pua yangu kwa kiganja changu kupambana na harufu ile kali ya
uvundo.
Nilisimama nikiitazama maiti ile iliyokuwa imeharibika vibaya pale chini huku ikitoa harufu mbaya na hapo nikajua kwa nini watu wale mle ndani
walikuwa wamejitenga na kujikusanya sehemu moja ingawaje lile pango lilikuwa dogo na lisilokuwa na hata tundu dogo la kupitishia hewa safi. Ile maiti ilikuwa ikitoa funza wakubwa waliokuwa wakisambaa kuizunguka. “Loh!
unyama gani huu binadamu anaweza kumfanyia mwenzake? Nilijisemea huku
machozi yakinilengalenga nikachuchumaa chini na kuanza kuangua kilio hafifu hata hivyo Jean alinifuata akaninyanyua na kunirudisha taratibu kule tulipokuwa mwanzo, sikupenda tena kugeuka na kutazama upande ule ilipokuwa
imelala ile maiti.
Pango lilikuwa dogo kulingana na idadi ya watu waliokuwa mle ndani hali
iliyopelekea ongezeko kubwa la joto. Niligeuka kulichunguza pango lile dogo
na kwenye kona moja nikaona galoni ya kijeshi, juu ya galoni ile kulikuwa na
kikombe na hapo nikajua kuwa galoni ile ilikuwa na maji ya kunywa.
Jean akanitambulisha kwa watu wote waliokuwa mle ndani na alipomaliza akaanza kuwatambulisha wale watu kwangu. Nikawapa pole wale watu
na kuwatia moyo kisha tulitafuta eneo la pembeni ya ukuta wa pango lile na
kuketi. Ile njaa na yale maumivu makali niliyokuwa nikiyasikia hapo awali
yalikwishatoweka kutokana na ile hali niliyokutana nayo mle ndani. Baada ya
kutulia chini na kuanza kumchunguza kila mtu mle ndani niligundua kuwa ni
watu watano tu ndiyo tuliokuwa na afya nzuri, yaani mimi, Jean, mzee mmoja
wa makamo, msichana mmoja na kijana mmoja.
Tulipoketi nilimtaka Jean anisimulie masaibu yaliyomkuta mpaka mimi
kumkuta mle pangoni akiwa mateka. Jean alianza kunielezea namna alivyotekwa, kuwa mara baada ya kuniwekea nafasi ya chumba kule Hotel Des Milles
Collines aliamua kurudi nyumbani kwake Avenue de la Justice nyumba namba
13 kupumzika kwa vile siku ile alikuwa amepata pesa ya kutosha hivyo hakuona sababu ya kurudi tena kule uwanja wa ndege wa Kigali kusubiri tena abiria
usiku ule. Akaendelea kunisimulia kuwa mara baada ya kufika na kuegesha
taksi yake nje ya nyumba aliingia ndani ambapo alipokelewa vizuri na mkewe
huku mtoto wao akiwa tayari amekwisha lala. Akaniambia kwa vile alikuwa
na uchovu sana aliamua kwenda kwanza bafuni kuoga alipotoka alirudi mezani na kula ambapo baadaye alipomaliza alielekea chumbani kulala. Ikawa
ilipofika saa tisa usiku ndipo aliposhtuliwa usingizini na mkewe akimwambia
kuwa mlango wa mbele wa nyumba yao ulikuwa ukigongwa.
“Nilishtushwa sana na ugongaji ule kwani mgongaji alikuwa akigonga
mlango kwa fujo mno, si kutaka kabisa kumfungulia nikwamwambia mke
wangu tumpuuze mgongaji hata hivyo haikuwa rahisi kwani tusingeweza kulala tena. Mgongaji aliendelea kugonga kwa fujo hali iliyomfanya mtoto wetu
atoke chumbani kwake na kukimbilia chumbani kwetu akiogopa. Makalele ya
mgongaji yalipozidi mke wangu alinishawishi nikafungue mlango nimsikilize
mgongaji akidhani pengine alikuwa ni mmoja wa majirani zetu aliyepatwa na shida.
Nilipingana sana na hoja ya mke wangu hata hivyo baadaye nilizidiwa na
kelele za mgongaji hivyo nikaamua nikamfungulie na kumsikiliza ili kuondoa kelele zile. Loh!...” Jean alishindwa kuendelea kunisimulia badala yake
machozi yalianza kumtoka na ili kujihimili akainama chini na kuanza kuchorachora sakafuni. Nilimtazama na kumuonea huruma sana huku nikifahamu fika
kuwa maelezo ambayo yangefuatia baada ya pale yasingependeza kuyasikia.
“Pole sana Jean, nafahamu..., nafahamu...” nilimpigapiga mgongoni huku
nami nikijizuia nisitokwe na machozi.
“Nini kilifuatia baada ya hapo? nilimuuliza baada ya kitambo kifupi cha
ukimya kupita na hapo akageuka na kunitazama uso wake ukiwa umesawajika
huku machozi yakimtoka kama mtoto mdogo. Akarudia tena kutazama chini huku akichorachora sakafuni, nilimpigapiga mgongoni kumtia moyo kisha
nikamuacha kidogo aweze kutulia. Alipotulia aliendelea
“Nilipofungua mlango nikawaona wanajeshi wawili wakiwa na bunduki
zao mikononi, nilitaka kuwahi kufunga mlango hata hivyo nilichelewa. Askari
mmoja aliupiga teke mlango ule mlango ukafunguka na hapo askari wale
wakaingia ndani, nikajitahidi kuwazuia hata hivyo sikufanikiwa kwani askari
mmoja alinipiga korodani zangu kwa kitako cha bunduki yake. Nikapiga yowe
kali la maumivu hali iliyowapelekea mke wangu na mtoto waje kuniangalia
lakini...” Jean alishindwa tena kuendelea kunisimulia na safari hii akaangua
kilio hafifu. Nikamwacha alie kidogo kupunguza simanzi aliyokuwanayo baadaye alipotulia nikambembeleza nikimshawishi aendelea kunisimulia.
“Niliwauliza wale wanajeshi kuwa walikuwa na shida gani hadi wanivamimi vile, wakasema niwapeleke sehemu nilipompeleka abiria niliekuwa
nimembeba ambaye ni wewe. Sikutaka kuwaeleza mahali ulipokuwa kwani
nilijua kulikuwa na jambo la hatari”
“Sasa uliwaambiaje?
“Walipozidi kunibana nikawaambia mimi nilikushusha nje ya Top Tower
Hotel ukanilipa pesa yangu nami nikaondoka na baada ya hapo sikufahamu ulipoelekea. Niliwaambia vile nikiamini kuwa mpaka wao kunipeleleza
hadi kunifuata pale nyumbani walikua tayari wamekukosa na kama muda ule
wangeamua kurudi tena kule Top Tower Hotel niliamini kuwa wasingekukuta kwani ulikuwa ukifahamu fika kuwa ulikuwa ukifuatiliwa hivyo niliamini
kuwa wasingekupata” Maelezo ya Jean yalinifanya nimshangae kwa namna
alivyokuwa mwelevu.
“Sasa ikawaje baada ya hapo? nilimuuliza tena na hapo akageuka kunitazama huku machozi yakimlengalenga tena ingawaje alifanikiwa kuyadhibiti,
akajifuta machozi kwa kiganja chake na kutazama tena chini na hapo alianza
tena kusimulia.
“Hawakutaka kunielewa, wakang’ang’ania tu msimamo wao kuwa lazima
niwaonesha ulipo huku wakinionya kuwa endapo ningeendelea kushikilia
msimamo wangu wangenionesha cha mtema kuni. Mimi bado niliendelea kushikilia msimamo wangu wa kuwa sijui mahali ulipokuwa na kuwa mawasiliano yangu na wewe yalimalizika pale nilipokushusha nje ya Top Tower Hotel na baada ya hapo sikujua ulipoelekea. Walipoona kuwa naendelea na msimamo
wangu hawakutaka tena kunilazimisha, wakawashika mke wangu na mtoto”
kufikia hapa Jean alianza tena kulia, nikamwambia ajikaze kiume huku taratibu nikimpigapiga tena mgongoni.
“Nini kilichoendelea niambie Jean?
“Walimuua mtoto wangu kwa kumfyatulia risasi mbele ya macho yangu
mimi nikiwa siwezi kutoa msaada wowote kwani nilikuwa nimepigwa sana
kiasi cha kushindwa kusimama”
“Pole sana Jean” nilimfariji huku nami nikitokwa na machoni kwa huzuni,
Jean akafuta machozi na kuendelea
“Mke wangu walimbaka palepale sebuleni kwenye kochi na walipomaliza
wakamuua kwa risasi. Nilishindwa kuvumilia na nafikiri nilipoteza fahamu
kwani baada ya pale sikuona kilichoendelea na nilipozinduka nilijikuta ndani
ya pango hili na mpaka sasa sijui hatima yangu” Jean alimaliza kunisimulia
huku akigeuka kunitazama nikajua alikuwa akisubiri na mimi nimsimulie
mkasa wangu. Nikamtazama huku nikamuonea huruma kwa namna alivyojitolea kupoteza mke na mtoto wake ili ayaokoe maisha yangu. Kwa kweli
sikuwahi kuona upendo wa namna ile na sijui ningemlipa nini kama sehemu
ya shukrani yangu.
Nilimsubiri atulie na hapo nikaanza kumsimulia mkasa wangu huku nikiamua kumueleza wazi kuwa mimi sikuwa nikiitwa Patrick Zambi kama
nilivyojitambulisha kwake hapo awali. Bali mimi nilikuwa mwanajeshi komandoo na mpelelezi kutoka jeshi la wananchi wa Tanzania na nilikuwa na
cheo cha Luteni na jina langu halisi lilikuwa Venus Jaka na nilikuwa nimekuja pale Kigali Rwanda kuchunguza juu ya kifo cha mwandishi wa habari
wa ubalozi wa Tanzania nchini Rwanda na vilevile mwandishi wa habari wa
gazeti la Afrika mashariki aitwae Tobias Moyo aliyeuwawa katika mazingira
ya kutatanisha.
Nimlimsihi asimueleze mtu yeyote mwingine kuwa mimi ni nani ili kama
ingetokea mimi ningekufa mle ndani na yeye akabahatika kuachiwa huru au
kutoroka aende akatoe taarifa kwenye ofisi za ubalozi wangu ijapokuwa nilikuwa nikikiuka maadili ya kazi yangu kwa kumueleza kuwa mimi ni nani.
Hata hivyo sikuona sababu ya kumficha kwa kuzingatia kuwa sikuwa na tumaini lolote la kutoka salama mle ndani istoshe alikwishapoteza mke na mtoto
wake ili kuyaokoa maisha yangu.
Vilevile niliwaza kuwa kama nisingepata muujiza wa kutoroka mle pangoni
nilifahamu fika kuwa adhabu iliyokuwa ikinisubiri ilikuwa ni kifo tu kwani
Kanali Bosco Rutaganda alikuwa tayari amenifahamisha kuhusu hilo. Hivyo
kwa kuzingatia haya yote sikuona kama nilikuwa nikifanya makosa kumueleza Jean Pierre Umugwaneza kuwa mimi ni nani. Nikampa namba yangu ya
simu na anwani ya posta ya mtu ambaye angewasiliana nae aliyeko nchini
Tanzania na kumjulisha yaliyonikuta endapo mimi ningeuwawa na yeye Jean
kufanikiwa kutoka salama mle pangoni.
Baada ya hapo nilianza kumueleza Jean mambo yalivyokuwa mpaka mimi kufikishwa mle pangoni. Jean alistaajabu sana akabaki akinitazama kwa
mshangao, mshangao wa kukutana na komandoo mzoefu kwenye uwanja wa
mapambano ndani ya pango lile nikiwa mbali kabisa na ule mwonekano wangu wa awali wa suti ya ghali aina ya Kenzo, kofia yangu nadhifu aina ya pama,
saa ya dhahabu mkononi aina ya Alpha GMT-Dead Ringer, sunduku langu
mkononi na yale marashi yangu ya gharama niliyojipulizia yenye harufu nzuri,
thamani yake ikilingana na mshahara mmoja wa kima cha chini wa mfanyakazi wa serikali, huku nikijibatiza kwa jina la Patrick Zambi, mwandishi wa
habari wa kujitegemea.
“Loh! kweli sikudhani kabisa kuwa wewe ni mwanajeshi tena komandoo”
Jean aliniambia mara tu nilipomaliza kumsimulia mkasa wangu nikabaki nikitabasamu tu huku akili yangu ikiwa mbioni kuanza kufanya kazi nyingine.
Kazi ya kuanza kufikiri namna ya kutoroka mle pangoni ingawaje sikuona
matumaini yoyote kwani mlango wa pango lile ulikuwa wa chuma nao ulikuwa ikifungwa kwa nje na zaidi ya hapo hapakuwa na dirisha lolote isipokuwa
uwazi mdogo uliokuwa chini ya mlango ule ambao ulitumika kupitisha hewa
kidogo iliyotuwezesha kuishi mle ndani.
Niliyazungusha macho yangu kukipeleleza vizuri kile chumba kidogo cha
pango na hapo nikajikuta nikipoteza tumaini la kutoka mle ndani salama. Niligeuka kumtazama Jean nikamuona kuwa alikuwa amezama katika simanzi na
hapo nikajua kuwa alikuwa akiiwaza familia yake kisha nikaanza kumtazama
kila mtu aliyekuwa mle ndani. Wanawake waliyakwepesha macho yao pale
nilipowatazama, bila shaka waliona aibu namna walivyokuwa uchi bila nguo
yoyote ya kujisitiri. Hasira zilinishika huku nikiulaani uvunjifu huu mkubwa
na udhalilishaji wa haki za binadamu.
“Hapa ni wapi? niligeuka na kumuuliza Jean aliyekuwa ameegemea ukuta
pembeni yangu.
“Sipajui wala sijawahi kufika ila nafahamu kuwa bado tupo Rwanda na si
nchi yoyote ya jirani”
“Unaweza kufahamu huu ni muda wa saa ngapi?
“Nani anaefahamu? pango lote hili ni giza si mchana si usiku kweli hii ni
sehemu hatari”
“Wale askari huwa wanabadilishana zamu kuja humu ndani? nilimuuliza
Jean huku nikimtazama
“Siwezi kujua, kama nilivyokueleza kuwa mimi fahamu ziliponirudia nilijikuta nipo humu ndani nikiwa sifahamu nimefikajefikaje” Jean alinijibu na
wakati huo nilimuona kijana mmoja aliekuwa jirani yetu akijisogeza pale tulipokaa huku akionekana kutaka kujiunga na maongezi yetu. Jean akazungumzanae kwa lugha ya kinyarwanda ambayo mimi nilikuwa siifahamu kabisa
kisha nilimuona yule kijana akigeuka kunitazama na hapo nikasikia Jean akiniambia.
“Muulize huyu anasema anayafahamu vizuri mapango haya” nikageuka
kumtazama vizuri yule kijana na hata kabla sijamsemesha akafungua maongezi
“Habari yako” alinisalimia huku akinipa mkono na hapo nikajua kuwa Jean alikuwa amemwambia kuwa mimi ni mtanzania na nilikuwa siifahamu lugha
ya kinyarwanda.
“Nzuri” nilimjibu na kushikana nae mkono.
“Nimeambiwa na huyu bwana kuwa wewe ni Mtanzania”
“Ndiyo, nimekuja hapa Rwanda kikazi bahati mbaya nimejikuta humu”
“Pole sana, mimi nimewahi kukaa Dar es Salaam”
“Dar es Salaam! ulikuwa ukifanya nini? nilimuuliza huku nikimtazama
“Nimesoma chuo kikuu cha Dar es Salaam wakati nilipokuwa nikichukua
shahada yangu ya pili ya Akiolojia na wakati nikisoma nilikuwa nimepanga
chumba eneo la Kijitonyama” yule kijana aliniambia na hapo tumaini dogo
lilifufuka moyoni mwangu. Kusikia kijana yule alikuwa amesomea Akiolojia yaani taaluma ya mambo ya kale na ugunduzi wa vitu kama mapango na
utamaduni na hapo nikajua kuwa kwa vyovyote angeweza kuwa na msaada
kwangu.
“Mimi naishi Tegeta ndipo nilipojenga”
“Umeoa? yule kijana aliniuliza huku nikishindwa kuelewa dhamuni la swali
lake
“Sijaoa ila naishi na mwanamke nimezaanae mtoto mmoja” nilimdanganya
“Hongera na afadhali yako wewe umeoa na una mtoto mimi ndiyo nilikuwa
nikijiandaa kufunga ndoa ndiyo haya yakanikuta sasa siitamani tena hiyo ndoa
na endapo nikifanikiwa kutoka nikiwa hai humu ndani nitaitoroka hii nchi”
“Kwa nini? nilimuuliza
“Hakuna haki!, mimi ni mwandishi wa habari na mhariri wa gazeti la hapa
Rwanda liitwalo République ukweli wangu ndiyo ulioniponza na sasa nipo
humu pangoni nasubiri kifo tu” kijana yule aliongea kwa majuto na nilipomtazama nikauona uso wake namna ulivyokata tamaa
“Jina lako nani? nilimuuliza
“Jérome Muganza”
“Unaweza kufahamu hapo tulipo ni wapi?
“Napafahamu, nimefanya kazi miaka minne ndani ya mapango haya kama
mtunzaji mkuu hifadhi ya mapango yote ya hapa nchini Rwanda na vivutio
vingine vya kale kabla ya kuacha kazi hiyo na kujiunga na gezeti la République nikiwa kama mwandishi wa habari na mhariri mkuu. Haya ni mapango ya Musanze yapo jimbo la kaskazini mwa nchi ya Rwanda ama Northern
Province” Jérome Muganza aliniambia na maelezo yake yakanifanya nigeuke
na kuketi vizuri nikimsikiliza.
“Kwa hiyo hapa tupo Northern Province?
“Bila shaka hata hivyo si mbali sana na jiji la Kigali”
“Mapango haya yapoje?
“Una maana gani? aliniuliza
“Yaani namna yalivyo, njia zake, ukubwa wa eneo lake na endapo kuna
makazi yoyote ya watu eneo la jirani”
“Oh! sasa nimekuelewa, haya ni mapango yanayotokana na miamba mikubwa ya kivolkano iitwayo Cenozoic, mfano kuna mwamba wa Manjari wenye
urefu wa zaidi ya mita moja na nusu na mwingine uitwao Nyiraghina wenye urefu wa mita moja.
Jumla ya mapango yaliyogunduliwa eneo hili yapo hamsini na mbili na
yenye jumla ya njia zenye urefu wa kilometa kumi na tano. Lakini hili bila
shaka ni pango la Musanze, urefu wake ni kilometa mbili kwa njia zake za
chini. Njia hizo zimepita juu ya matabaka ya uji wa volkano ulioganda kwa
zaidi ya miaka sitini iliyopita. Matabaka hayo sasa yametengeneza bonde kubwa mbele ya mapango haya liitwalo Albertine Rift Valley. Mapango haya yana
njia za kuingilia zipatazo thelathini na moja lakini mengine sehemu zake juu
zimemong’onyoka, haya ni mapango marefu zaidi kwa hapa Rwanda na yanapatikana popo wakubwa wenye midomo mirefu na wakali na nyoka wakubwa
aina ya chatu.
Bado watafiti wanaendelea kuyachunguza vizuri mapango haya ili kuyaingiza kwenye vivutio rasmi vya utalii vya hapa Rwanda.
“Kuna makazi yoyote ya watu karibu na mapango haya? nilimuuliza
“Yapo, kiasi cha urefu wa maili zaidi ya kumi mashariki mwa mapango
haya” Jérome Muganza aliniambia na hapo nikajikuta nikianza kuwawaza
chatu na hao popo wakali waliosemekana kuwapo ndani ya mapango haya.
Nilimtazama Je’rome Muganza huku nikifarijika kwa maelezo yake.
“Umesema ulikuwa ukifanya kazi kwenye gazeti la République la hapa
Rwanda kama mhariri na ukaniambia kuwa ukweli wako ndiyo uliokuponza,
ni ukweli gani huo? nilimuuliza huku nikimtazama.
“Ndiyo, hata sasa hiyo ndiyo kazi yangu na hilo gazeti la République mmiliki wake ni mimi. Baada ya kufanya kazi kwa muda mrefu kidogo mimi
nikiwa kama mtunzaji wa mwangalizi mkuu wa hifadhi za mapango yote ya
hapa Rwanda hatimaye niliomba kustaafu mapema kabla ya umri wangu.
Nilipolipwa mafao yangu nikaamua kuanzisha hilo gazeti lengo lake kubwa
likiwa ni kuionya serikali juu ya hali tete ya amani katika nchi hii na hali ya
kisiasa ilivyo kwa ujumla. Naweza kusema nilifanikiwa kwa kiasi kikubwa
kwani gazeti hilo liliondokea kupendwa sana hapa nchini na hata mauzo yake
yalikuwa ya kuridhisha na hii ilitokana na gazeti langu kujikita zaidi katika
kuzungumzia ukweli juu ya mambo yanayoisibu nchi hii”
“Unaweza kuniambia kuwa ni sababu gani hasa iliyopelekea wewe kukamatwa na kuletwa humu ndani? nilimuuliza
“Ni kutokana na ukweli wa gazeti langu, nahisi nilikuwa nikiyagusa maslahi
ya baadhi ya viongozi wakubwa wa kisiasa wa hapa nchini. Kabla ya kukamatwa niliwahi kupewa vitisho vya hapa na pale juu ya kugusa maslahi ya viongozi hao, nilitoa taarifa kwenye vyombo vya usalama lakini sikuona juhudi
zozote za vyombo hivyo vya usalama katika kuzifanyia kazi taarifa zangu”
“Umesema habari zako zilikuwa zikigusa maslahi ya baadhi ya viongozi,
kwa vipi?
“Wiki mbili zilizopita nilichapisha habari iliyokuwa ikieleza juu ya matukio
ya mauji ya chini chini yaliyokuwa yakiendelea sehemu mbalimbali hapa
nchini. Katika habari hiyo niliandika juu ya majina ya washukiwa wakuu wa
mauaji hayo huku nikiishauri serikali iingilie kati hali hiyo kwani maisha ya
watu wasio na hatia yalikuwa yakipotea kila kukicha. Habari ile ilipokelewa vizuri na wasomaji wengi hasa kwa kuwa ilikuwa
ikiongelea hali halisi ya hapa nchini hata hivyo siyo wote ambao walifurahia ukweli ule kwani siku mbili tu baada ya kuchapisha habari ile nilianza
kupokea vitisho kutoka kwa watu nisiowajua. Nikatoa taarifa kwenye vyombo
vya usalama juu ya vitisho hivyo ila sikupata msaada wowote kwani ni kama
taarifa zangu ziliishia kwenye mafaili yao.
Ilikuwa ni baada ya muda wa siku nne kupita tangu nilipochapisha habari
zile gazetini ndiyo nilipokutana na mkasa huu ulionifikisha humu ndani nikiwa
sina fahamu” Jérome Muganza aliweka kituo kidogo akimeza funda la mate
nami nikavuta pumzi kubwa na kuishusha taratibu kisha nikageuka pembeni
yangu kumtazama Jean Pierre Umugwaneza ambaye nae alikuwa akiyasikiliza
kwa makini maongezi yale halafu nikarudia tena kumtazama Jérome Muganza na hapo akaendelea
“Ndiyo nakumbuka kuwa ilikuwa imetimia saa tano na nusu usiku na nilikuwa ni mtu wa mwisho kufunga ofisi yangu iliyopo Masaka Avenue katikati ya
jiji la Kigali ambako nilikuwa nimemaliza kuhariri habari ambazo zingetoka
kwenye gazeti la asubuhi inayofuata. Baada ya kumaliza kuhariri nilizipeleka habari zile chumba cha pili tayari kuchapishwa na mara baada ya kutoka
na kufunga ofisi ile nilihisi uchovu mwilini hivyo sikuona sababu ya kuanza
mizunguko mingine, nikaamua kuwasha gari langu na kuelekea nyumbani kupumzika.
Wakati nilipokuwa njiani kuelekea nyumbani ndipo nilipopigiwa simu na
mtu nisiyemfahamu akiniambia kuwa kulikuwa na tukio la mauaji lililokuwa
limetokea muda ule kwenye jengo moja la shirika la nyumba la hapa Rwanda
lililokuwa katikati ya jiji la Kigali. Nilikuwa nimechoka mno kwa wakati ule
na sikupenda kujishughulisha na kitu chochote zaidi ya kwenda kupumzika lakini nilijikuta nikihisi habari zile huenda zingekuwa na umuhimu wake kama
ningeweza kuziwahi na kuzitoa kwenye gazeti la asubuhi ya siku iliyofuata
hivyo hatimaye niliamua kubadilisha uelekeo na kuelekea mjini ilipo nyumba
ile.
Sikufika mbali sana wakati nilipogundua kuwa nyuma yangu kulikuwa na
gari fulani lililokuwa likinifuatilia, nilishikwa na wasiwasi sana nikaamua
kupiga simu polisi lakini simu ile iliita muda mrefu bila kupokelewa na ilipopokelewa hakuna aliyenipa msaada. Lile gari nyuma yangu lilinifikia na
kunisimamisha kwa mbele, nakumbuka walishuka watu sita kwenye gari lile
wakiwa na mapanga mikononi. Wakanishusha kwenye gari langu na kuanza
kunipiga bila ya kuniambia chochote, nilisikia maumivu makali sana nikawasihi waniache lakini hakuna aliyenisikiliza. Maumivu ya kipigo kile yalikuwa
makali mno hivyo nikapoteza fahamu na nilipozinduka nilijikuta nipo ndani
ya pango hili” J’erome Muganza alimalizia simulizi lile fupi huku akionesha
kusikitika sana.
“Pole sana” nilimtia moyo
“Ahsante”
“Sasa nini hatima yetu humu ndani? Jean aliuliza huku akionekana mwenye
hofu.
“Watatuua tu, mmoja baada ya mwingine na inavyosemekana ni kuwa sisi si
watu wa kwanza kufichwa ndani ya mapango haya. Nilikuja kufahamu kuwa
wapigania haki wengi wa nchi hii waliokuwa wakipotea katika mazingira ya
kutatanisha walikuwa wakitekwa na kuletwa hapa kabla ya baadaye kuuwawa
na taarifa zao kupotelea kusikojulikana” Jérome Muganza alikuwa akiongea
huku akionekana kuwa ni mwenye hakika na maelezo yake.
Sote tulibaki tukimtazama Jérome Muganza huku kila mmoja akitafakari
lake moyoni. Nilifahamu sasakuwa nilikuwa nimetumbukia kwenye shimo la
kifo na kujinasua kwake isingekuwa kazi rahisi. Niliyazungusha macho yangu
kulitazama tena lile pango ambalo sasa lilionekana kama kaburi la kuzikia
watu hai na sikuona tumaini lolote la kutoka mle ndani nikiwa hai na hapo
nikayarudisha macho yangu kumtazama tena Jérome Muganza.
“Sasa tumewekwa humu ndani nini hatima yetu? niliuliza katika namna ya
kukata tamaa.
“Huwa wanakuja kumchukua mtu mmoja baada ya mwingine wakidai wanaenda kufanya nae mahojiano lakini pindi mtu huyo anapochukuliwa hatumuoni akirudi tena na hicho ndiyo kitu kinachonifanya niamini kuwa watu hao
huwa wanaenda kuuwawa” Jérome aliendelea kutueleza.
“Ulituambia kuwa wapigania haki za binadamu wengi katika nchi hii waliosemekana kupotea katika mazingira ya kutatanisha ulikuja kugundua kuwa
walikuwa wakitekwa na kuletwa humu kabla ya baadaye kuuwawa, umejuaje?
nilimuuliza.
“Ni kupitia uchunguzi nilioufanya ndani ya pango hili mara tu baada ya
kujikuta nipo humu ndani”
“Uchunguzi upi huo? Jean aliuliza na hapo nilimuona Jérome Muganza akigeuka kutazama sehemu fulani ya ukutani mle pangoni. Wote tukawa tumegeuka kutazama kule alipokuwa akitazama Jérome Muganza
“Pale kuna majina ya watu ninaowafahamu ambao hapo siku za nyuma walitoweka katika mazingira ya kutatanisha na hakuna aliyekuwa akifahamu taarifa zao. Nilikuja kufahamu kuwa watu hao walitekwa na kuletwa humu baada
ya kukuta majina yao yameandikwa ndani ya pango hili na nina kila hakika ni
wao wenyewe ndiyo walioandika majina yale”
Huku tukiwa tumeshikwa na mshangao wote tuligeuka vizuri na kuanza
kutazama kwa makini pale ukutani na hapo tukayaona majina mbalimbali
ya watu yakiwa yameandikwa pale ukutani. J’erome Muganza alituonesha
baadhi ya majina ya watu aliokuwa akiwafahamu na hata wengine ambao waliwahi kuwa marafiki zake wa karibu. Miongoni mwa majina yale lilikuwepo
jina la Théoneste Egide ambaye alikuwa mkurugenzi mkuu wa shirika la haki
za binadamu duniani yaani Human Right Watch nchini Rwanda na alikuwa
ametoweka katika mazingira ya kutatanisha sana zaidi ya miaka mitatu iliyopita wakati alipokuwa akiingoza tume ya kuchunguza vifo vya watu ishirini
na moja waliouwawa kwa kukatwa mapanga katika eneo moja nchini Rwanda
liitwalo Nyarugenge.
Miongoni mwa majina yale pia lilikuwepo jina la mama Magdeline Mukasano aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari wanawake cha nchini Rwanda ambaye nae pia ilisadikika kuwa alikuwa ametoweka miaka miwili iliyopita wakati usiku mmoja alipokuwa akirudi nyumbnai kutoka
ofisini kwake na baadaye gari lake lilikutwa eneo fulani porini likiwa limetelekezwa na baadhi ya matundu ya risasi yaligundulika katika mlango mmoja
wa gari hilo.
Nilimuuliza Jérome Muganza kuwa ni sababu gani aliyokuwa akiidhani
kuwa pengine ilikuwa imepelekea kutekwa na kuuwawa kwa mama Magdeline Mukasano naye akaniambia kuwa kifo chake kilitokana na harakati zake
za kupigania haki na kutetea wanyonge kwa njia ya uhandishi wa habari kama
yeye, na pia katika maelezo yake Jérome Muganza alitueleza kuwa mama
Magdeline Mukasano alikuwa na urafiki sana na jaji mmoja maarufu nchini
Rwanda aliyekuwa akijulikana kwa jina la Jaji Makesa ambaye naye alitoweka muda mfupi baada ya kupotea kwa mama Magdaline Mukasano.
Jérome aliendelea kutueleza kuwa alikuwa ametarajia pia kuliona jina la Jaji
Makesa katika orodha ile ya majina yaliyoandikwa katika ukuta ule wa pango
lile kwa kuwa alikuwa akiamini kuwa hata jaji Makesa nae alikuwa ametweka
lakini alishangaa sana kuona katika orodha ile ya majina jina la Jaji Makesa
halikuwepo.
Mimi na Jean Pierre Umugwaneza tulikuwa kama tulioshikwa na bumbuwazi wakati tulipokuwa tukiyasikiliza maelezo ya Jérome Muganza mle pangoni. Kila mtu akajikuta amezama katika fikra fulani juu ya maelezo yale hata
hivyo nilipomtazama Jean niligundua namna alivyokuwa na hofu na hata uso
wake ulijieleza.
Nilijihisi kuanza kuyazoea mazingira ya mle ndani ingawaje hata mimi
nilikuwa na wasiwasi mwingi juu ya hatima ya maisha yangu na wale watu
waliokuwa mle ndani. Nikayahamishia tena macho yangu kuyasoma yale majina yaliyokuwa yameandikwa kwenye ule ukuta wa pango. Yalikuwa ni zaidi
ya majina ya watu thelatini na baadhi ya majina yale yalikuwa ni ya watu
mashuhuri sana niliowahi kuwasikia wa nchini Rwanda. Majina mengine hayakuwa na maana sana kwangu hata hivyo majina yote niliyapa heshima kwa
kufa kishujaa katika harakati za kutetea haki za binaadamu na usawa na vilevile kuwasaidia wanyonge sambamba na kuwakosoa baadhi ya viongozi wa
serikali.
Nikiwa naamini sasa kuwa yule majina ya watu yaliyoandikwa mle pangoni
sasa watu hao walikuwa marehemu nikajikuta na mimi nikipata hisia za kuandika jina langu na kuwashawishi wengine kujiandika katika orodha ile huku
nikiamini kuwa hata kama watu wote tungekufa mle ndani ipo siku moja dunia
ingekuja kuufahamu kweli wa mambo kupitia orodha ya majina yetu.
Kwa kweli lilikuwa ni jambo la kushangaza sana kwa namna majina yale
yalivyokuwa yameandikwa kwa kuchongwa kiustadi katika ukuta wa mwamba mgumu wa pango lile. Nikajikuta nikiwaza kuwa bila ya shaka ilimchukua
mtu mmoja kwa zaidi ya siku mbili hadi kufanikiwa kuandika jina lake katika
ukuta ule kwa kutumia kipande cha ncha kali ya jiwe lililochongoka. Nilimtazama Jérome Muganza na kumuona kuwa alikuwa ni mtu msomi na mwelevu
sana hadi kuweza kupeleleza na kugundua orodha ile ya majina yaliyoandikwa mle ukutani. Kwa kweli nilipoyatazama yale majina nilijisikia faraja sana
kuwa hatukuwa peke yetu kwani japokuwa watu wale walikwishakufa lakini
nilikuwa ni kama ninaewaona huku nyuso zao zikiwa zimejawa na tumaini la
kufa kishujaa. Nikiwa naendelea kuiwaza hali ile nikaanza kuhisi kuwa mbegu
ya ujasiri ilikuwa ikianza kuchipua taratibu moyoni mwangu huku nikijiapia
kuwa kabla ya kifo changu ingefaa na mimi kufanya kitendo tofauti cha ujasiri
ili nife nikiwa na amani moyoni.
Bila shaka muda ulikuwa umesonga sana ingawaje sikuweza kufahamu
wakati ule ulikuwa ni muda wa saa ngapi kutokana na giza zito lililokuwa
limetanda mle pangoni. Niligeuka kumtazama Jérome Muganza pembeni
yangu nikagundua kuwa alikuwa ameanza kusinzia ingawaje nilimuona kuwa
alikuwa akijitahidi sana kupambana na hali ile ya usingizi. Nikageuka kumtazama Jean Pierre Umugwaneza ambaye naye alikuwa ameketi pembeni yangu
na hapo nikagundua kuwa japokuwa nae alionekana kunitazama lakini macho
yake hayakuonesha mjongeo wa namna yoyote.
Alikuwa ameachama mdomo wazi na sauti hafifu ya mkoromo wa uchovu
ilikuwa ikipenya kinywani mwake. Kichwa chake kiliegemea bega lake upande wa kushoto huku yeye mwenyewe akiwa ameegemea ule ukuta wa pango.
Sikutaka kuendelea kuwasemesha nikawaacha waendelee kupumzika na hapo
nikayazungusha tena macho yangu kutazama mle pangoni, nikagundua kuwa
watu wote mle ndani walikuwa wamelala.
Baadhi ya wanawake walikuwa wamelala pale sakafuni pasipo kuonesha jitihada zozote za kuficha tupu zao, baadhi yao walikuwa na majeraha makubwa
katika sehemu zao za matiti, migongoni, tumboni na kwenye makalio. Roho
iliniuma sana nilipoyatazama majeraha yao na kuanza kuvuta picha juu ya
mateso waliopitia kabla ya kuletwa mle pangoni.
Wote walikuwa wamejilaza sakafuni kila mmoja akiwa amelala katika
namna yake aliyodhani ingemfaa bila ya kujali mbu wakali waliokuwa mle
pangoni. Wengi walikuwa ni wanawake warefu wenye maumbo na sura nzuri
za kuyavutia macho ya mwanaume yoyote kuwatazama, na kutokana na muonekano wao sikuwa na shaka kuwa wengi wao walitoka katika mazingira ya
ukwasi kama siyo kwenye kazi zenye vipato vya kuridhisha.
Niliwatazama wote mmoja baada ya mwingine kwa zamu huku nikiwaza
hatima yangu mle pangoni na wakati nilipokuwa nikiendelea na zoezi hilo
ghafla nilijikuta nikitazamana na msichana mmoja mrembo aliyekuwa amejikunyata katikati ya kundi lile la wanawake waliolala pale chini sakafuni.
Macho yangu yalipogongana na macho ya msichana yule nikagundua kuwa
hata yeye alikuwa akinitaza kwa muda mrefu. Niligundua pia kuwa yeye ndiye
aliyekuwa mwanamke pekee aliyekuwa bado hajalala mle pangoni hadi wakati huu. Nilishangaa kumuona msichana yule akitabasamu usoni pindi macho
yetu yalipogongana na japokuwa tabasamu lake lilichanua vizuri usoni lakini
niligundua kuwa tabasamu lile halikufanikiwa kuitowesha sura yake ya hofu
na mashaka iliyokuwa nyuma ya tabasamu lile.
Sura ya mashaka yenye alama za mifereji ya machozi yaliyokauka baada ya
kulia kwa muda mrefu bila matumaini. Nilibaki nikimtazama msichana yule mrembo kwa muda mrefu huku nikiwa nimepumbazika kwa uzuri wake na
hapo nikajikuta nikizisahau kwa muda shida zote za mle pangoni. Msichana
yule alikuwa mzuri sana, mrefu na mweusi mwenye nywele nyeusi na laini
ingawaje nywele hizo zilikuwa zimesukwa mabutu.
Alikuwa ameketi chini kwenye sakafu ya pango lile huku ameikunja miguu
yake kifuani katika mtindo wa kujikunyata, mikono yake alikuwa ameigemeza
juu ya magoti yake. Nilipomchunguza niligundua kuwa alikuwa ameishiwa
nguvu kwa kulia muda mrefu.
“Kwanini hulali mrembo? nilimuuliza huku nikiendelea kulimudu tabasamu
langu. Hakunijibu kitu badala yake alitikisa kichwa chake upande huu na ule
kuonesha kukataa kisha aliinama chini na hapo nikayaona machozi yakianza
safari ya kushuka kwenye mashavu yake. Huzuni ilinishika moyoni wakati
nilipokuwa nikiendelea kumtazama nami nikajikuta nikipambana kuyazuia
machozi yasinitoke.
“Jina lako nani? nilijikaza nikamuuliza tena na hapo akanyanyua macho
yake kunitazama, tulitazamana tena huku nikipumbazika kwa uzuri wake.
“Ikirezi” hatimaye alinijibu kwa upole
“Ikirezi!” nilirudia kulitamka jina lake “Lina maana gani jina lako?
“Sifahamu mimi nilipewa tu na wazazi wangu”
“Una muda gani tangu uletwe humu ndani ya pango hili?
“Wiki moja na siku mbili”
“Pole sana” nilimfariji kwa sauti ya upole na hapo akatikisa kichwa akionesha kuikubali pole yangu pasipo kuzungumza kisha ukimya kidogo ukapita
kabla hajaniuliza
“Unaitwa nani?
“Naitwa Patrick Zambi, mimi ni Mtanzania”
“Mtanzania? alionesha mshangao kidogo “Imekuwaje ukaletwa humu
ndani?
“Ni kama wewe tu bila shaka hukupenda kuwepo humu ndani ila imetokea
tu na ukajikuta umeletwa humu ndani” niliongea huku nikimtazama.
“Una ndugu yako yoyote anaefahamu kuwa wewe upo humu ndani? aliniuliza
“Hapana, sikupata nafasi ya kumueleza yoyote kwani kutekwa kwangu kulikuwa ni kwa ghafla sana”
Ikirezi alinitazama kwa kitambo kifupi kama mtu anayetafakari jambo fulani kisha akavunja ukimya
“Unadhani kuna uwezekano wowote wa kutoroka ndani ya pango hili?
“Mh! bado sioni tumaini lolote kwa sasa labda itokee miujiza” nilimwambia
Ikirezi huku nikijaribu kuyasoma mawazo yake na hapo nilimuona namna
alivyokata tamaa kwa ghafla.
“Kama sitofanikiwa kutoroka humu pangoni ndani ya muda wa wiki moja
kuanzia sasa nitauwawa” Ikirezi aliniambia huku machozi hafifu yakianza
tena kumtoka.
“Nani aliyekuambia kuwa utauwawa? nilimuuliza kwa udadisi.
“Watakuja kunichukua nikahojiwe kwani zamu yangu imekaribia na najua tu kuwa mara baada ya mahojiano hayo nitauwawa kwa sababu hakuna mtu
hata mmoja aliyechukuliwa humu ndani kwa mahojiano hayo na baadaye kurudishwa. Wote wanaochukuliwa humu ndani huwa hawarudi”
“Wanataka kukuhoji kuhusu nini na kipi kilichopelekea wewe kuletwa
humu ndani?
“Wanataka niwaeleze mahali alipo mume wangu”
Nilimtazama msichana yule huku nikikilaani sana kitendo hicho cha yeye
kuolewa na mwanaume mwingine na siyo mimi kwani ukweli ni kwamba
nilishaanza kumpenda ingawaje mapenzi yetu yasingekuwa na maana yoyote
ndani ya shimo hili la kifo.
“Mume wako amefanya nini hadi wamtafute?
“Kwa kweli mpaka muda huu sifahamu”
“Mume wako yuko wapi? nilimuuliza na hapo nikamuona namna alivyonitazama kwa jicho la hasira.
“Sifahamu na hata kama ningekuwa nafahamu sehemu alipo nisingekueleza” akanijibu kwa hasira.
“Kwanini unasema hivyo huoni kuwa sisi sote humu ndani ni mateka na
pengine tukasaidiana kwa namna moja au nyingine endapo tukafanikiwa kutoka humu ndani salama”
“Lakini si umeniambia kuwa uwezekano wa kutoroka humu ndani ni mdogo
na labda itokee miujiza sasa ni vipi unipe matumaini hewa?
“Ni kweli lakini sikusema kwamba miujiza imeisha” nilimwambia na hapo
nikaona tabasamu hafifu likiumbika usoni mwake.
“Unadhani kuna uwezekano wa kutoroka humu ndani kabla ya muda wa
wiki moja haujatimia? aliniuliza
“Sina hakika ila itategemeana na hali ilivyo”
“Itategemeana na nini?
“Hali yenyewe itakavyokuwa mfano namna ya ulinzi ulivyo eneo hili na
kama hiyo nafasi ya kutoroka itapatikana” nilimwambia huku nikijaribu
kuyatafakari mawazo yake. Kitambo cha ukimya kilipita huku kila mmoja
akionekana kutafakari, ukimya huo ulipokuwa mbioni kushika hatamu nikaanzisha tena maongezi
“Mume wako anafanya kazi gani? nilimuuliza na hapo akanitazama tena
kabla ya kunijibu
“Ni afisa wa jeshi la wananchi wa Rwanda”
“Ana cheo gani?
“Meja”
“Anaitwa meja nani?
“Meja Faustine Bagasora”
“Mumeo aliwahi kukueleza juu ya hali yoyote ya kutoelewana na mtu au
watu fulani hapo kabla?
“Hakuwahi kunieleza chochote ingawaje hizi siku za karibuni nilimuona
akiwa ni mwenye wasiwasi na mashaka”
“Kwa vipi?
“Alikuwa akirudi usiku wa manane na haikuwa kawaida ya mume wangu”
Ikirezi aliongea huku akijizuia asitokwe na machozi.
“Ulipokuwa ukimuuliza alikuwa akisemaje?
“Hakutaka kunieleza chochote ingawaje nilifahamu kuwa hakuwa katika
hali ya kawaida”
“Pole sana” nilimfariji huku nikimtamza “Sasa ilikuwaje mpaka ukaletwa
humu ndani? nilimuuliza na hapo alinitazama kisha akayapangusa machozi
na kuendelea
“Ilikuwa usiku wa saa mbili pale simu ya sebuleni ilipoanza kuita, nilipoipokea simu ile ndiyo nilipogundua kuwa nilikuwa nikiongea na mume
wangu. Alikuwa ni mtu anaeongea kwa wasiwasi na kwa haraka sana kama
mtu anayekimbizwa na hatari”
“Alikuambiaje?
“Aliniambia kuwa alikuwa kwenye hatari”
“Hatari gani?
“Hakuweza kunieleza ni jambo gani badala yake alinitaka nijiandae haraka
na nichukue vitu vyote muhimu vikiwemo nguo na pesa zote ambazo tulikuwa tumezihifadhi pale nyumbani na kisha nimchukue mtoto wetu mchanga
halafu niondoke na gari mpaka mzunguko wa barabara wa katikati ya jiji la
Kigali ambapo ningemkuta akinisubiri”
“Alikwambia baada ya hapo mngeenda wapi?
“Rusumo, mpakani mwa Tanzania na Rwanda na baada ya hapo tungevuka
mpaka na kuingia nchini Tanzania”
“Ulimuuliza ni kwa sababu gani alilazimika kufanya vile”
“Hakutaka kunieleza badala yake alinisisitiza tu kuwa nifanye haraka sana
kwani kulikuwa na hatari mbele yetu” Ikirezi aliendelea kunielezea na safari
hii machozi yakimtoka.
“Pole sana jipe moyo” nilimfariji kisha nikamuacha atulie kabla ya kumuuliza tena
“Sasa ilikuwaje?
“Nilifanya kama alivyoniagiza mume wangu lakini bahati mbaya sikufanikiwa”
“Nini kilitokea?
Nilikuwa nipo mbioni kumalizia kupanga nguo kwenye sanduku toka
kwenye kabati lililokuwa chumbani wakati niliposikia mlango wa mbele wa
nyumba ukigongwa usike ule. Wasiwasi ulinishika sana nikaanza kuhisi hatari
ikinikaribia nikaacha kupanga nguo huku nikijishauri nimchukue mtoto wangu mchanga na kutoroka kupitia mlango wa nyuma wa nyumba hata hivyo
nilijikuta nikipingana na wazo lile pale nilipofikiria kuwa kama wengekuwa
wameizunguka ile nyumba wangeweza kunikamata tu”
“Sasa ulifanyaje?
“Sikuwa na jinsi kwani nilifahamu kuwa kama watu wale wangekuwa na
nia mbaya wangenikamata tu hivyo nilimchukua mtoto wangu na kumficha
kabatini, nikamuacha na chupa ya maziwa” Ikirezi akafuta machozi na kuendelea “Mlango wa mbele wa nyumba ulivunjwa kabla ya mimi sijaufikia na
hapo nililiona kundi la wanajeshi wakiingia, walipoingia ndani wakaniuliza kama mume wangu alikuwa mle ndani nikawaambia alikuwa bado hajarudi
kutoka kazini. Wakaniuliza kama mle ndani nilikuwa peke yangu nikawajibu
ndiyo hata hivyo hawakuniamini wakaanza kufanya upekuzi mle ndani na ninachoshukuru ni kuwa hawakulifikia lile kabati nililomficha mwanangu”
“Baada ya kumkosa Meja Bagasora walifanya nini?
“Waliniambia kuwa badala yake wangenichukua mimi na kwa kweli sikuamini macho yangu” Ikirezi aliniambia huku akitokwa na machozi
“Pole sana nini kilifuatia baada ya hapo?
“Walinishika na kuanza kunibaka kwa zamu nilisikia maumivu makali
sana nikapiga malele kuomba msaada hata hivyo ilikuwa kazi bure kwani hawakunionea huruma. Alipomaliza mmoja aliingia mwingine na mwisho nguvu
ziliniishia kabisa nikapoteza fahamu na sikufahamu tena kilichoendelea.
Niliporudiwa na fahamu ndiyo nikajikuta nipo humu ndani nikiwa nimevuliwa nguo zangu zote kama hivi unavyoniona” Ikirezi alimaliza kunisimulia
huku akiangua kilio hafifu nami nilibaki nikimtazama tu msichana yule mrembo ambaye sasa urembo wake haukuwa na thamani tena ndani ya pango
hili. Nikakunja ngumi kwa hasira huku nikimeza funda kubwa la mate kooni
kuyazuia machozi yasinitoke.
“Pole sana kwa masaibu yaliyokukuta” hatimaye nilimwambia kwa sauti
ya upole
“Ahsante” akanijibu huku akijipangusa machozi na nilipomtazama nikakumbuka kumuuliza
“Mtoto wako yuko wapi?
“Nilimuacha amelala kabatini” alinijibu huku akizidisha kilio na hapo nikajisogeza karibu yake na kuanza kumbembeleza. Kwa kweli nilijisikia kukata
tamaa sana baada ya kusikia mikasa ya watu wa mle pangoni kwani ni kama
kila mtu mle ndani alikuwa na mkasa wake wenye kutisha na kuhuzunisha
sana na vilevile niligundua kuwa kila mtu mle pangoni alikuwa na sababu zake
za kuletwa mle ndani. Kitendo cha ubakaji alichofanyiwa Ikirezi kilinifanya
niyahamishe tena macho yangu kuwatazama wale wanawake waliolala pale
chini sakafuni na hapo nikajikuta nikiwaza kuwa miongoni mwao kama si
wote basi wangekuwepo waliobakwa kama Ikirezi.
Nikiwa nimeanza kupata utulivu wa akili yangu nilijikuta nikianza tena
kuikumbuka safari yangu tangu kutoka Dar es Salaam mpaka jijini Kigali,
nikamkumbuka yule msichana aitwaye Marceline wa kule kiwanja cha ndege
cha Kigali huku nikijiuliza ni kwa nini alitaka tuonane siku ile ya kwanza
tulipofahamiana, na hapo nikakumbuka kuwa alikuwa amenipa business card
yenye namba zake za simu.
Nikakumbuka kuwa sikuwa nimemtafuta kwani ile kadi yenye namba zake
za simu ilikuwa kwenye waleti yangu ambayo nilikuwa nimeitupa kule porini
muda mfupi kabla sijatekwa, kwa kweli bado sikuweza kufahamu ni kwa nini
Marceline alitaka tuonane. Nilijikuta pia nikimkumbua Mutesi, yule msichana
niliyekutana naye ndani ya Kigali Casino na kumpa kazi ya kumchunguza na
kuniletea taarifa juu ya yule mtu aliyekuwa akinifuatilia toka kule kiwanja cha
ndege cha Kigali. Nikawaza kuwa Mutesi angenifikiriaje baada ya kufika kule Hotel Des Mille Collines na kunikosa? Niliendelea kujiuliza huku pia nikiwaza juu ya taarifa alizokuwa ameahidi kuniletea kuhusu mtu yule aliyekuwa
akinifuatilia kule Casino.
Halafu nikamkumbuka Niyonkuru, yule msichana aliyekuwa mpenzi wa
marehemu Tobias Moyo, nikakumbuka namna nilivyopewa makaribisho
yenye utata siku ile nilipoenda kumtembelea nyumbani kwake na hapo nilijikuta nikimuwaza yule mwanaume aliyekuwa mle ndani ambaye mimi sikumuona. Nikaanza kujiuliza kuwa mtu yule alikuwa nani na kwanini alijificha pindi
nilipofika. Niliendelea kujiuliza bila ya kupata majibu.
Nikiwa bado naendelea kutafakari niliyakumbuka tena maneno ya Kanali
Bosco Rutaganda, mwanafunzi wangu wa kijeshi miaka minne iliyopita ambaye sasa nilikuwa uchi wa mnyama ndani ya himaya yake. Niliyakumbuka
maneno ya Kanali Bosco Rutaganda juu ya mapinduzi aliyokuwa akiyasubiri
kwa hamu muda mfupi ujao, kwa kweli sikufahamu alikuwa akimaanisha ni
mapinduzi ya namna gani, eti mapinduzi ya kuwarudishia uhuru watu wa nchi
ya Rwanda ambao ulipokonywa kwao na kundi dogo la wavamizi, ni kundi
gani hilo mbona sikuwahi kulisikia hapo kabla kwani kama ni uhuru nchi ya
Rwanda ilikwishapata uhuru wake toka kwa wakoloni kama zilivyokuwa nchi
nyingine zote za bara la Afrika.
Nikakumbuka kuwa Kanali Bosco Rutaganda aliniambia kuwa alikuwa
amefurahi sana aliposikia kuwa mimi ndiye niliyekuwa nimetumwa kuja hapa
Rwanda kwani hii ndiyo ingekuwa nafasi nzuri ya yeye kuonana tena na mimi.
Nilijiuliza kuwa ni nani aliyekuwa amempa taarifa hizo za kuja kwangu hapa
Rwanda na sikuweza kupata majibu badala yake nikabaki nikimuwaza Brigedia Masaki Kambona ambaye ndiye aliyekuwa mratibu mkuu wa safari yangu
ya kuja hapa Kigali na vilevile mkuu wa operesheni za siri za kijeshi. Lakini
bado akili yangu alikataa kabisa kumuhusisha na uvujaji huu wa siri za safari
yangu kwani sikuona sababu ambayo ingempelekea kufanya hivyo. Sasa mtu
huyo angekuwa nani na kwa sababu gani afanye hivyo?.
Niliendelea kujiuliza bila kupata mwanga wowote katika kuwaza kwangu
na maswali pekee yaliyozidi kunichanganya ni kuwa Kanali Bosco Rutaganda
na wenzake walikuwa na agenda gani ya kuwateka watu na hatimaye kuwaua
humu mapangoni, na sababu ipi ilikuwa imepelekea kifo cha mwandishi Tobias Moyo. Tobias Moyo alikuwa ameona nini hadi jitihada za kumfumba mdomo mapema zikatumika?.
Wakati mawazo haya na mengine yakiendelea kupita kichwani mwangu
nilikuwa nikijihisi kuchanganyikiwa kwa msongo mkubwa wa mawazo. Niligeuka tena kuitazama ile maiti iliyokuwa imelala kwenye kona ya pango huku
nikiwa nimekata tamaa sana na maisha ya mle ndani. Nikageuka tena kumtazama Ikirezi na hapo nilijikuta nikimhurumia juu ya mtoto wake mchanga
aliyemficha ndani ya kabati nyumbani kwake. Nilihuzunika zaidi baada ya
kuwaza kuwa kama isingetokea mtu yeyote wa kumfikia mtoto huyo mpaka
kufikia wakati huu basi mtoto huyo angekuwa tayari amekufa. Loh! hasira
zilizidi kunipanda nikameza funda kubwa la mate kupambana nayo. Ikirezi
alikuwa bado amejikunyata pale chini huku akiendelea kunitazama ingawaje nilifahamu fika kuwa akili yake haikuwa mle pangoni.
“Unaishi wapi hapa Rwanda? nilimuuliza tena
“Zion Temple nyumba namba 6, unadhani itakusaidia chochote? sisi sote ni
kama wafu tu humu ndani” alinijibu akionekana kukata tamaa.
“Bado hatujakufa kabisa” nilimjibu kwa mkato huku akili yangu ikienda
mbali zaidi kufikiri.
“Umesema tangu uletwe humu ndani una muda wa wiki moja na siku mbili
unaweza kuniambia ni baada ya muda gani mtu wa humu ndani huja kuchukuliwa?
“Siku mbili au tatu”
“Na utaribu wake upoje, huwa wanaita majina au humchukua mtu yeyote
tu?
“Wanaita jina hata hivyo inavyoonekana ni kama huwa wanamfahamu mtu
wanayemfuata kwa siku hiyo kwani pamoja na kumuita jina lake humfuata na
kumchukua kwa nguvu”
“Huwa wanakuwa askari wangapi?
“Wawili na wote huwa na silaha zao mabegani”
“Leo ni zamu ya kuchukuliwa kwa mtu mwingine?
“Ilitakiwa iwe hivyo ila nafikiri ratiba yao imebadilika kwani mpaka sasa
hawajamchukua mtu mwingine isipokuwa ni wewe tu uliyeletwa” Ikirezi
alinijibu huku akinitazama tena.
“Chakula na maliwato kwa ajili ya mateka wa humu ndani utaratibu wake
upoje?
“Wote tunajisaidia kwenye ile kona” Ikirezi aliniambia huku akinionesha
kona ya pango lile iliyokuwa na giza “Na wakati wanapokuja kumchukua mtu
wao ndiyo muda huo huo huleta na chakula huku wakitusimamia tule”
“Kwa hiyo watu wa humu ndani hula chakula baada ya siku mbili?
“Ndiyo, na ndiyo maana afya za watu humu ndani zimedhoofika sana”
“Maneno ya Ikirezi yalinifanya nimtazame huku nikifikiria juu ya mambo
yote ya mle pangoni hata hivyo ni wakati huu nilipojihisi mwenye uchovu
sana mwilini. Kwa mbali nilianza kuhisi hata usingizi ulikuwa ukininyemelea,
kichwa nacho kilikuwa kikipwitapwita kutokana na yale maumivu ya mgongo
ambayo niliyahisi kuwa yalikuwa yakiongezeka taratibu kwa kadiri baridi ilivyokuwa ikipenya taratibu kwenye majereha yangu. Nilimtazama tena Ikirezi
na kumuona kuwa alikuwa bado amejiinamia na machozi yalikuwa yakiendelea kushuka taratibu mashavuni mwake. Huzuni ilinishika sana nikamuonea
huruma ingawaje sikuona namna yoyote ya kumsaidia.
“Unahitaji kupumzika sasa” nilimwambia
“Sina usingizi”
“Pumzika Ikirezi tutatoroka tu wala usijali” nilimwambia huku nikiumba
tabasamu hafifu usoni mwangu na hapo nilimuona akiinua macho yake kunitazama tena na kwa mara ya kwanza nikaliona tabasamu jepesi likichanua
usoni mwake.
“Unaniahidi kweli kuwa tutatoroka? akaniuliza kwa sauti ya upole
“Nakuahidi ondoa shaka na utamkuta mtoto wako akiwa salama” nilimfariji ingawaje moyoni sikuona tumaini lolote la kutoroka mle pangoni.
Tulibaki tukitazamana kwa kitambo hata hivyo sikuona dalili yoyote kwa
Ikirezi ya kutaka kulala. Uchovu uliponizidi nikajisogeza taratibu na kujiegemeza vizuri kwenye ukuta wa pango lile huku nikijikunyata kisha nikaikunja
na kuiegemeza mikono yangu juu ya magoti. Nilipoinua macho yangu kumtazama tena Ikirezi nikamuona kuwa alikuwa bado akiendelea kunitazama,
nikamuaga kwa tabasamu langu jepesi kisha nikainamisha kichwa katikati ya
mapaja yangu na hapo uzingizi ulinichukua taratibu na sikufahamu tena kilichokuwa kikiendelea mle pangoni.
NILIKUWA WA KWANZA KUAMKA alfajiri ya siku ya pili ingawaje mle
pangoni bado kulitawaliwa na giza kila mahali, ile taa ya kandili iliyokuwa ikiangaza katikati ya pango lile ilikuwa mbioni kuishiwa mafuta kwani mwanga
wake ulikuwa ukififia taratibu. Mara baada ya kuamkanilikimbilia kutazama
upande ule aliokuwa ameketi Ikirezi, nikamuona kuwa alikuwa amepitiwa na
usingizi ingawaje bado alikuwa ameketi katika mtindo ule ule niliyomuacha
nao kabla sijalala. Baridi ilikuwa kali mno ikipenya na kuitafuna mifupa yangu taratibu, nilihisi njaa kali sana tumboni hali hiyo ilinitia hofu huku nikiwaza
kuwa endapo hali ile ingeendelea kuwa vile afya yangu ingedhoofika.
Baada ya muda mfupi uliofuata mtu mmoja baada ya mwingine aliamka
mle pangoni. Watu wote walipoamka tuligundua kuwa mwenzetu mmoja alikuwa bado amelala pale sakafuni. Alikuwa ni miongoni mwa watu waliokuwa
wamedhoofika sana mle pangoni, mzee wa makamo mwenye umri kati ya miaka hamsini na tano mpaka sitini.
Nilimsogelea mzee yule na kumchunguza vizuri kama alikuwa yupo katika
hali ya uzingizi wa kawaida au alikuwa amezidiwa na ugonjwa. Nilipomfikia
nilimtingisha taratibu lakini sikumuona akionesha dalili zozote za kuamka,
hali yake ilinitia mashaka sana nikamgeuza na kumchunguza vizuri. Kwa taaluma yangu ya kikomandoo na kama askari niliyefuzu vizuri katika medani za kivita ilinichukua muda mfupi tu kujiridhisha kuwa mtu yule alikuwa
amekufa na hapo nilizivuta pumzi zangu kwa mkupuo na kuzishusha taratibu
kisha nikainua macho yangu kuwatazama watu waliokuwa mle ndani, nikagundua kuwa watu wote walikuwa wakinitazama kwa shauku kama ndugu wa
mgonjwa wanapomtazama daktari aliyetoka kwenye chumba cha wagonjwa
mahututi.
Macho yangu yakawaeleza nini kilichokuwa kimemsibu mtu yule na hapo
vilio hafifu vya wanawake vilifuatia, wanaume waliinamisha vichwa vyao chini kwa masikitiko sana. Kwa mikono yangu miwili niliubeba mwili wa mtu
yule aliyekufa toka pale chini sakafuni na kwenda kumlaza sehemu ya pembeni mwisho wa pango lile kisha nikarudi na kuketi mahali pangu. Mle ndani
harufu ya uvundo ilikuwa kali mno na ilikuwa ikiongezeka taritibu kutokana
na kuharibika vibaya kwa ule mwili wa yule mtu wa mwanzo. Kwa kweli
nilijisikia kutaka kutapika hata hivyo sikuweza kutokana na tumbo langu kwa
tupu.
Hadi ilipofika mchana wa siku ile nilijikuta nimefahamiana na watu wote
wa mle pangoni na kuifahamu mikasa iliyowasibu lakini wakati huohuo pia
nilikuwa nimewahamasisha watu wale kwa kiasi cha kutosha juu ya kuandika
majina yao kwenye ile orodha ya majina iliyokuwa mle pangoni na hoja yangu
ilionekana kufanikiwa kwa kiasi kikubwa sana. Baada ya kufanya uchunguzi
wa kina mle pangoni nilikuwa nimegundua kuwa karibia watu wote waliokuwa mle ndani walikuwa wasomi na wenye taaluma tofauti tofauti na hivyo
askari pekee aliyekuwa mle pangoni nilikuwa ni mimi peke yangu. Hili lilinitia mashaka sana kwani nilifahamu kuwa adhabu yangu ingekuwa tofauti na
wenzangu hata hivyo sikukata tamaa huku nikijipa moyo kuwa kama ni kufa
hapa duniani kila mtu atakufa suala lilikuwa ni nani aanze na yupi amalizie na
vilevile katika mtindo gani wa kifo.
Mpaka wakati huu nilikuwa nimekubaliana na hali halisi ya mle pangoni
vilevile nilikuwa tayari kufa pale ambapo ingenibidi kufanya hivyo lakini
nilipanga kutokufa kifo cha kondoo anayechinjwa huku ameinamisha kichwa
chini. Vilevile wakati huo wote nilikuwa nikiifikiria ile hoja ya Ikerezi ya juu
ya kutoroka mle pangoni, nilikuwa nimeafikiana naye kuwa lilikuwa wazo
zuri lakini kwa upande mwingine nilifahamu kuwa utekelezaji wake ulikuwa
mgumu. Nilimkumbuka mwalimu wangu wa kijeshi alipokuwa akinifundisha
kuwa unapokamatwa na adui kutoroka huwa ni hatua ya awali kabisa ya kufikiria kabla ile ya kujiua hasa pale unapoona kuwa suala la kutoroka limeshindikana kabisa. Hata hivyo alikuwa amenionya kuwa kabla ya kutoroka ilikuwa
ni muhimu sana kuwa na picha kamili ya mazingira husika uliyopo na si kufanya papara bila ya kuyaelewa vizuri mazingira hayo kwani kwa kufanya hivyo
ilikuwa ni kuichezea kamari roho yako.
Katika hali kama ile nilifamu fika kuwa ingenipasa kukaa mle pangoni zaidi
ya siku mbili au tatu ili kuweza kuyasoma vizuri mazingira ya pango lile na
kupeleleza vitu fulanifulani kwa kufanya mahojiano na watu waliotangulia kuletwa mle pangoni kwa kupitia mbinu zangu. Kwa kipindi kifupi nilichokuwa
mle ndani nilifanikiwa kurudisha matumaini katika mioyo ya watu mle pangoni kwa kuwafanya watambuane, kuzungumza, kujadili na kupeana moyo huku
nikisisitiza kuwa kila mmoja alipaswa kumuomba Mungu wake ili atunusuru
na kadhia ile.
Mchana wa siku ile ulipita kimya bila mlango wa pango lile kufunguliwa,
mtu yeyote kuletwa mle ndani wala askari kutuletea chakula. Hali ya tumbo
langu ilikuwa mbaya sana na nilianza kuhisi udhaifu kwa kuwa sikuwa nimetia kitu chochote tumboni hata hivyo nilijikaza na kutumia muda ule kujadili suala hili na lile na akina Jerome Muganza na Jean Pierre Umugwaneza.
Ikirezi yeye alikuwa pembeni akitusikiliza na mara kwa mara nilipomtazama
niligundua kuwa alikuwa amezama katika fikra za kuiwaza familia yake na yule mtoto wake mchanga aliyemficha kabatini kule chumbani kwake.
Ni katika maongezi yale ya kufarijiana ndipo nilipopata bahati ya kufahamiana na mzee mmoja wa kizungu mwenye umri wa miaka sitini na kitu hivi
ambaye pia ndiye alikuwa mzungu pekee mle pangoni. Alikuwa ni raia wa
ufaransa na jina lake aliitwa Dr. Francois Trezor. Yeye alikuwa ni daktari wa
kujitolea kutoka nchini ufaransa na alikuwa akifanya kazi katika hospitali kuu
ya jiji la Kigali kama daktari bingwa wa mifupa.
Daktari huyo mkongwe akiongea katika lugha ya kiingereza cha kubabaisha
alinieleza kuwa alikuwa akifanya kazi katika hospitali hiyo kwa muda wa miaka sita tangu afike nchini Rwanda yeye na daktari mwenzake wa kike aitwaye
Lisa Olivier. Katika maongezi yetu nilimuuliza ni kipi hasa kilichokuwa kimemsibu mpaka kuletwa mle ndani na hapo ndipo nilipopata fununu za taarifa
nilizokuwa nikizihitaji. Daktati yule alinitazama huku uso wake ukishindwa
kuonesha tashishwi yoyote machoni kwangu pindi nilipomtupia swali lile.
“Jaji Makesa!, unamfahamu? aliniuliza
“Nimewahi kumsikia tu” nilimjibu huku nikiyakumbuka maelezo ya Jérome
Muganza aliyonigusia juu ya jaji Makesa.
“Yeye ndiye aliyenifanya niwepo humu”
“Ilikuwaje? nilimuuliza.
“Ilikuwa ni siku ya ijumaa pale nilipokuwa naingia zamu ya usiku hospitalini wakati nilipowapokea majeruhi wawili mwanaume na mwanamke ambao niliwahisi kuwa walikuwa ni mtu na mkewe. Walikuwa wamejeruhiwa
vibaya kwa shambulizi la mapanga. Sehemu kubwa za majeraha hayo zilikuwa vichwani hata hivyo yule mwanamke yeye alikuwa amejeruhiwa zaidi.
Nikiwa ndiyo daktari wa zamu wa usiku ule niliwapokea majeruhi wale na
kuwapelekea moja kwa moja kwenye chumba cha wagonjwa mahututi.
Huku nikishirikiana na jopo la madaktari wenzangu tulijitahidi kufanya kila
lililowezekana kuokoa maisha yao lakini bahati mbaya sana yule mwanamke
alifariki tulipokuwa kwenye jitihada hizo. Kifo chake kilichangiwa kwa kiasi
kikubwa na kupungukiwa damu nyingi kutokana na yale majeraha hata hivyo
pamoja na majeraha yale kuwa mengi lakini hayakuwa yameuathiri ubongo
wake”
“Nani aliyewaleta majeruhi hao hapo hospitalini? nilimuuliza.
“Mtu mmoja ambaye alijitambulisha kama msamaria mwema huku akisema kuwa aliwaokota majeruhi wale wakiwa wametelekezwa barabarani usiku
ule”
Nilimtazama mzungu yule daktari wa kifaransa kwa makini huku nikiyapima maelezo yake hata hivyo bado sikuweza kupata picha yoyote.
“Na huyo majeruhi mwingine mwanaume aliyesalia mliweza kumfahamu
kuwa ni nani?
“Baadhi ya madaktari wenyeji walimtambua na kuniambia kuwa alikuwa ni
jaji maarufu sana wa hapa nchini Rwanda”
“Alikufa? nilimuuliza kwa shauku.
“Hapana! nafikiri mpaka sasa anaweza kuwa hai japo sina hakika sana” Dr.
Francois Trezor aliniambia na hapo nikashikwa na butwaa.
“Kwanini huna hakika?
“Bila shaka alitoroshwa na mtu au watu fulani pale hospitali”
“Kwa vipi?
“Zilikuwa tayari zimepita siku nne tangu tulipompokea Jaji Makesa pale
hospitali na hali yake ilikuwa ikionesha matumaini japo bado alikuwa hawezi
kuzungumza wala kufumbua macho. Siku ile tulikuwa madaktari wanne tu
kwenye chumba kile cha wagonjwa mahututi na tulikuwa tumetumia muda wa
saa nane kuwashughulika wagonjwa watatu mahututi akiwemo jaji Makesa.
Ilipofika saa kumi jioni mimi na madaktari wenzangu tuliamua kutoka
kwenye chumba kile na kwenda kupata mlo kwa kuwa tangu tulipoingia saa
mbili asubuhi ya siku ile hatukuwa tumetoka. Tulitumia muda wa robo saa tu
kupata mlo ule kwa kuwa tulikuwa na kazi iliyokuwa ikitusubiri na tulipomaliza kula tulirudi haraka kule wodini na hapo ndipo tuliposhangaa kukikuta
kile kitanda tulichomlaza Jaji Makesa kikiwa kitupu. Wote tulitaharuki sana
na kushikwa na wasiwasi hivyo tukaamua kwenda kutoa taarifa kwa uongozi
wa hospitali ile”
“Baada ya hapo ni hatua gani zilichukuliwa?
“Kwa kweli sikuona hatua zozote za muhimu zikichukuliwa, mwanzoni nilidhani labda pengine ile ni tabia za waafrika kutokuwa na umakini kwenye
mambo yao lakini nilipofuatilia vizuri niligundua kuwa ile haikuwa hali ya
kawaida ila kulikuwa na jambo fulani nyuma ya pazia”
“Hali gani?
“Nilipokuwa nikijaribu kufuatilia kwenye uongozi ule wa hospitali juu
ya kupotea kwa Jaji Makesa niliambiwa kuwa lile halikuwa jukumu langu,
maadamu nilikuwa nimeshatoa taarifa nilitakiwa kuendelea na kazi yangu
na suala lile lilikuwa ni jukumu la uongozi kufuatilia juu ya tukio lile. Mimi
sikuridhishwa na majibu yao hivyo usiku ule nilipotoka hospitali nikaamua
kuitafuta nyumba aliyokuwa akiishi Jaji Makesa.
Baada ya kuulizauliza kwa wenyeji hatimaye nikaelekezwa. Nyumba yake
ilikuwa kando kidogo ya jiji la Kigali. Nilifanikiwa kuipata nyumba ile na
kuingia ndani. Ilikuwa ni nyumba yenye uzio wa ukuta na geti kwa mbele.
Nilipogonga hodi kijana wa kiume wa miaka ishirini na kitu hivi alikuja
kunifungulia, nilihisi kuwa kijana yule alikuwa miongoni mwa watoto wa Jaji
Makesa kwa namna alivyofanana na wazazi wake.
Kijana yule alinikaribisha ndani hata hivyo alikuwa akisitasita kufanya vile.
Wakati tukielekea ndani ya nyumba ile nilimuuliza kama pale kulikuwa ndiyo
nyumbani kwa Jaji Makesa akaniambia ndiyo penyewe na nilikuwa sijakosea.
Nikamuuliza kama Jaji Makesa alikuwa mle ndani muda ule akaniambia kuwa
baba yake na mama yake walikuwa wameondoka tangu asubuhi ya siku ile
na walikuwa bado hawajarudi. Nilimuuliza kuwa walikuwa wameenda wapi
akanijibu kuwa kulikuwa na taarifa fulani walizokuwa wakizifuatilia juu ya
kifo cha mwandishi wa habari Mtanzania aitwaye Tobias Moyo hivyo siku ile
wangechelewa kurudi kidogo.
Ni wakati tulipokuwa tukiukaribia mlango wa kuingilia sebule ya nyumba
ile hapo ndipo niliposhtukia nikipigwa na kitu kizito kichwani na hapo fahamu zikanipotea na nilipozinduka nikajikuta humu ndani” Dr. Francois Trezor alimaliza kunieleze huku akinitazama usoni. Nikabaki nikimtazama kwa shauku
bila ya yeye kufahamu kuwa maelezo yake yalikuwa yamenigusa mno maana
nami nilikuwa nimetumwa hapa Rwanda ili kupeleleza juu ya kifo cha mwandishi wa habari wa Tanzania aitwaye Tobias Moyo aliyekuwa ameuwawa
katika mazingira yenye utata, ambaye ndiye huyo Jaji Makesa naye alikuwa
akifuatilia taarifa zake. Loh! nilishusha pumzi taratibu huku mate yakinikauka
kooni moyo wangu ukawa ukinienda mbio.
__________
MUDA ULE ULE TULISIKIA MLANGO WA PANGO lile ukifunguliwa
na wote takageuka kutazama huku hofu ikiwa imetushika. Mlango wa lile pango ulipofunguliwa askari wawili walisimama mlangoni wakiwa wamebeba sufuria kubwa mikononi mwao huku bunduki zao zikiwa begani. Ghafla ukimya
ukachukua nafasi mle ndani wote tukabaki tukiwatazama wale askari kama
waumini waliogeuka nyuma kumtazama shetani wakati akiingia kanisani.
“Wale askari walisimama wakiyazungusha macho yao kututazama mle pangoni mmoja baada ya mwingine kama waliokuwa wakituhesabu na walipofika
kwangu waliweka kituo kunitazama na hapo moyo wangu ukapiga kite kwa
nguvu huku mwili ukifa ganzi kwa sekunde kadhaa.
“Luteni!” Mmoja aliita huku akiangua kicheko cha kejeli.
“Sema unachotaka kusema siyo unachekacheka tu kama mwanamke malaya” nilimwambia kwa hasira.
“Sisi na wewe nani ni malaya? huoni kuwa malaya ni wewe uliyewekwa
kinyumba na wanaume wenzako ndani ya pango hili la wafu bila nguo hata
moja” yule askari aliyekuwa akicheka hapo awali aliongea na kuangua kicheko
cha dhihaka na mwenzake naye akaungana naye katika kucheka. Wakati huo
watu wote mle pangoni walikuwa wamegeuka kunitazama mimi hata hivyo
sikujali kitu nikabaki nimepandwa na hasira tu kama mbogo aliyejeruhiwa.
Wale wanajeshi wakalilitua lile sufuria chini na kulisukuma kwetu kwa buti
zao za kijeshi miguuni na hapo wote tukanyanyuka na kuanza kulikimbilia lile
sufuria kugombea chakula. Kuona vile wale askari wakaanza kucheka tena.
Kwenye lile sufuria kulikuwa na ugali uliochanganywa na maharage na
vyote vilikuwa vibichi hata hivyo hakuna aliyethubutu kususia kile chakula
kwani sote tulikula kwa kugombea kama mbwa. Wakati huohuo nilimuona
askari mmoja akiiendea ile taa ya kandili iliyokuwa imefifia kiasi cha kuelekea
kuzimika mle pangoni. Alipoifikia ile taa ya kandili akainama na kukifungua
kibuyu cha maji kitumiwacho na wanajeshi vitani ambacho alikuwa amekining’iniza kiunoni. Alipokifungua akaanza kumimina kitu fulani kwenye ile
taa ya kandili na hapo nikagundua kuwa alikuwa akiongeza mafuta ya taa
kwenye ile taa.
Kwa macho ya wizi nilizisoma vizuri nyendo za wanajeshi wale huku nikianza kutengeneza mipango yangu kichwani. Walikuwa ni wanajeshi wenye
maumbo wakubwa na warefu wakionekana kuzingatia vizuri ratiba zao za
mazoezi. Niliwachunguza namna walivyokuwa wamezishika bunduki zao na hapo nikagundua kitu fulani ambacho kilizidi kunivutia katika harakati zangu.
Tulimaliza kula ndani ya muda mfupi sana huku tukiwa hatujashiba vizuri
na tulipomaliza kula askari mmoja alikuja na kulichukua lile sufuria huku
akitutazama na kucheka. Nilimkodolea jicho la hasira yule askari hata hivyo
nilijizuia kufanya lolote. Wakati huohuo niliwaona wale askari wakiacha kunitazama badala yake wakayahamishia macho yao kumtazama yule mzee wa
kizungu, daktari wa kifaransa niliyekuwa nikizungumza naye yaani Dr. Francois Trezor. Na hapo waliweka kituo kumtazama na hali ile ikapelekea watu
wote mle pangoni nao wageuke kumtazana Dr. Francois Trezor.
Nilipowatazama askari wale usoni nilishtuka sana kuziona sura zao zikiwa zimebadilika ghafla na kuvaa tabasamu la kinyama, moyo wangu ukaanza kwenda mbio, nikaanza pia kuhisi jasho jepesi lilikuwa likinitoka sehemu
mbalimbali za mwili wangu huku koo langu likikauka taratibu kwa hofu. Sikufahamu kwanini hali ile ilikuwa ikinitokea hata hivyo nilihisi kufikwa na
kitu kibaya kilichokuwa kikielekea kutokea mle pangoni kwani hisia zangu
ziliniambia hivyo.
“Simama juu Dr. Francois Trezor!” yule askari aliyekuwa amesimama mlangoni wakati mwenzake alipokuwa akimimina mafuta kwenye ile taa ya kundili alifoka huku tabasamu la dhidhaka likimponyoka taratibu usoni mwake.
Nikamuona Dr. Francois Trezor akigeuka taratibu kunitazama huku uso wake
ukionekana kugubikwa na hofu isiyoelezeka, kisha akaanza kunisogelea taratibu. Kwa kweli nilihisi kama mzimu wa mtu ulikuwa ukinisogelea hata hivyo
nikapiga moyo konde na kutulia, watu wote mle pangoni wakawa wanatutazama.
Dr. Francois Trezor aliponifikia akaishika shingo yangu na kunivuta karibu yake na hapo nikajua kulikuwa na jambo alilotaka kunieleza, hata hivyo
niligundua kuwa mikono yake haikuwa na nguvu na alikuwa akitetemeka
mwili mzima. Aliponishika shingoni nilihisi ni kama niliyeshikwa na vijiti
vyembamba vya mti mteke kutokana na nyama kidogo zilizokuwa zimesalia
kwenye vidole vyake vilivyokonda.
“Wewe ni askari sivyo? aliniuliza baada ya kukisogeza kichwa changu karibu na mdomo wake na hapo nikageuka na kumtazama kwa mshangao.
“Ndiyo, wewe ni askari tena Luteni wa jeshi na hata kabla hawajakuita nilikufahamu tu kwa muonekano wako tangu siku ya kwanza ulipoletwa humu
ndani” aliendelea kuniambia nami nikabaki nikimtazama.
“Usiogope kijana mimi pia ni askari mwanajeshi lakini ni askari mzee aliyekongoroka wa jeshi la ufaransa na kabla ya kuja hapa Rwanda nilitokea
nchini Sierra Leone na baadaye nchini Angola na safari yangu ilikuwa iishie
nchini D.R Congo lakini sioni tumaini tena” Aliweka kituo na hapo nilimuona
akimeza funda kubwa la mate kwa uchungu, macho yake ni kama yalikuwa
yakijikamua kutoa machozi lakini hakufanikiwa kwani alikuwa amekonda
sana.
“D.R Congo ulikuwa ikienda kufanya nini? nilimuuliza kwa shauku ya kutaka kujua hata hivyo hakunijibu badala yake niliuona uso wake ukiumba tabasamu hafifu lenye uchungu mkubwa ndani yake.
“Wewe ni mwanajeshi wa kweli na siyo mimi, a true soldier will never
die” aliendelea kuninong’oneza sikioni hata hivyo maneno yake hayakuwa na
maana yoyote kwangu badala yake nilimuona ni kama anayetapatapa baada ya
kuhisi kuwa roho yake ilikuwa inakikaribia kifo. Lakini nilishangaa kuuona
uso wake ulikuwa ukimaanisha alichokuwa akikiongea na hakuwa akiongea
kama mtu anayeogopa kifo. Akaendelea
“Askari wa kweli hakubali kufa kirahisi kama mimi, najua kuwa utatoka
ndani ya kaburi hili la watu hai, ukitoka mtafute Dr. Lisa Olivier mwambie
yote yaliyonisibu humu pangoni. Mwambie kuwa nimekufa na asihangaike
kunitafuta kwani ni tamaa yangu mwenyewe imeniponza”. Akaweka kituo na
kumeza funda la mate na alipoanza kuongea tena niligundua kuwa alikuwa
akizidi kutetemeka
“Usiishie hapo tu bali nenda ukaieleze dunia juu ya unyama huu unaotendeka humu pangoni, nenda na wala usigeuke nyuma, nenda kaitahadharishe dunia na kuionya juu ya tukio baya litakaloikumba nchi hii” alipomaliza kuongea
nilimuona Dr. Francois Trezor akiangua kicheko hafifu cha kukata tamaa na
dunia kisha akaendelea tena
“Nilikudanganya soldier naomba unisamehe sana na ukitoka humu ndani
nenda kamtafute Dr. Lisa Olivier atakuonesha mahali alipo Jaji Makesa
kwani huyo ndiye mtu pekee atakayekusaidia” Dr. Francois Trezor alimaliza
kwa kunivuta karibu na kunibusu kichwani kisha akaniambia kwa sauti ya
kunong’ona “It is time for me to die” kisha akanipigia saluti hafifu na mimi
nikamuonesha heshima kwa kumpigia saluti na hapo akaniacha taratibu huku
akitabasamu. Watu wote mle ndani walikuwa bado wakitutazama wakati nilipogeuka kuyazungusha macho yangu na hapo nikaziona nyuso zilizojawa na
huzuni, nyingine zikitoa machozi na kilio hafifu cha kwikwi.
“Sogea katikati daktari” yule askari aliongea katika sauti ya kiafande na
hapo nilimuona Dr. Francois Trezor akisogea taratibu. Miguu yake ilikuwa
ikitetemeka sana kwa kadili alivyokuwa akizitupa hatua zake kutembea hali
iliyomfanya aonekane kama anayeogopa kukanyaga ardhi. Wakati huu ukimya
ulichukua tena nafasi yake mle pangoni.
“Simama!” yule askari alifoka alipomuona Dr. Francois Trezor amefika katikati ya pango lile, Dr. Francois Trezor akasimama.
“Huna taarifa zozote za maana za kuweza kutufaa daktari, hatuwezi kuendelea kutengeneza bajeti ya chakula kwa ajili yako” mara baada ya askari yule
kumaliza kuongea nilimuona Dr. Francois Trezor akifanya ishara ya msalaba kisha akageuka kunitazama huku lile tabasamu la uchungu likiwa usoni
mwake.
Huzuni ilinishika sana toka pale chini nilipoketi nilitaka nisimame niwafuate wale askari nikawatie adabu hata hivyo nilizuiliwa kikamilifu na mikono
ya Jérome Muganza na Jean Pierre Umugwaneza waliokuwa pembeni yangu
na wakati wakifanya vile muda ule ule nikasikia mlio mkali wa risasi. Nikataharuki kumuona Dr. Francois Trezor akisombwa na kutupwa hewani. Nguvu ya risasi zile zilizofyatuliwa toka katika bunduki za askari wale ilikuwa
imemsomba na kumrusha kasi kiasi cha umbali wa mita mbili nyuma toka pale alipokuwa amesimama.
Akarushwa hewani na kutua pembeni mwa ile miili miwili huku kichwa
chake kikiwa kimesambaratika na ubongo wake ukitawanyika angani na
mwingine ukiturukia sisi watu tuliokuwa karibunae, na huo ndiyo ukawa
mwisho wa Dr. Francois Trezor. Alipotua chini kiwiliwili chake kilirukaruka kidogo na kutulia. Kila mtu mle ndani akawa ameshikwa na kihoro kwa
kushuhudia kifo kile cha kinyama. Wale askari wakayahamisha macho yao
kunitazama tena na hapo nikahisi kama walikuwa wakiuona moyo wangu kifuani kwa namna ulivyokuwa ukihangaika kwa hofu.
“Luteni Venus Jaka! na wewe jiandae kesho kamanda wetu atakuja na atahitaji kuongea na wewe” askari mmoja aliniambia na hapo nikahisi kama mwili
wangu ulikuwa mbioni kufa ganzi kwa hofu, nikavuta pumzi nyingi kifuani na
kuishusha taratibu huku nikijiona kama mfu. Sikuweza kuongea chochote na
wale askari wakayahamishia macho yao kumtazama Jérome Muganza.
“Na wewe jiandae, bila shaka utakuwa tayari kuyajibu maswali yetu” askari
yule alifoka kwa kiburi kisha akalichukua lile sufuria na kuanza kuelekea nje
ya lile pango, yule mwenzake akamfuata kwa nyuma.
__________
UKIMYA WA HALI YA JUU ULIKUWA UMETAWALA MLE NDANI na
watu wote sasa walikuwa wamegeuka kututazama sisi huku wakiwa na hakika kuwa kwa vyovyote mimi na Jérome Muganza ndiyo tuliokuwa tukifuatia
kwenye orodha ya watu waliopaswa kuuwawa mle pangoni. Ule mlango wa
pango ulipofungwa tulisikia makelele ya makufuli mawili moja juu na jingine
chini ya mlango ule yakifungwa kwa nje kisha yale makelele yalipotoweka
wote tulibaki tukiutazama ule mlango kwa hofu.
Vilio vya chinichini vya wanawake na baadhi ya wanaume mle pangoni
vikaanza kusikika. Niliacha kuutazama ule mlango nikageuka kuitazama ile
maiti ya Dr Fracois Trezor pale chini ilipolala na wakati nikiitazama ile maiti
nikahisi kuwa yale maneno aliyokuwa akiniambia daktari yule ni kama yalikuwa yakijirudiarudia kichwani mwangu. “A true soldier will never die” nikajisemea huku nikihisi kutetemeka kwa hasira.
Nilipogeuka kumtazama Ikirezi nikagundua kuwa alikuwa akilia kwa hofu
huku akiwa amejikunyata vilevile na hapo akainua macho yake kunitazama
bila kusema neno. Huruma ilinishika mno na sikuweza kumtazama nikayakwepesha macho yangu pembeni. Nilipoyarudisha macho yangu kumtazama
tena nikashtukia kuwa alikwishanifikia pale nilipokuwa akanishika bega langu
na kunitazama.
“Kumbe wewe ni askari, tafadhali naomba uniokoe kwani nami zamu yangu ya kuuwawa inakaribia” Ikirezi alikuwa akinitingisha kama mwehu huku
akilia kama mtoto
“Tafadhali niokoe nitakupa chochote utakacho mtoto wangu anakufa kule
kabatini, nisaidie tafadhali nakuomba” kihoro kilikuwa kimemshika Ikerezi na
alikuwa akibwabwaja maneno kama mtoto.
Nikaishika shingo yake na kuivutia kwangu bila pingamizi akanilalia begani na hapo hisia kali za mapenzi zikaanza kutembea mwilini mwangu kama
umeme wa radi, joto lake la mwili na matiti yake laini vikanitia faraja nami
nikapitisha mkono wangu na kumbembeleza mgongoni mwake taratibu mpaka pale alipotulia na kuacha kulia bila ya kujali kuwa macho ya watu yalikuwa
yakitutazama mle pangoni.
__________
USIKU WA SIKU ILE ULIKUWA MFUPI sana mle pangoni na kila mtu
alionekana akiwa kwenye tafakari nzito juu ya lile tukio la kifo cha kinyama
cha Dr Francois Trezor. Jérome Muganza na Ikirezi walikuwa wakiendelea
kulia na nilikuwa nikijitahidi sana kuwabembeleza bila ya mafanikio. Ikirezi
alikuwa akilia kila mara alipojikuta akimkumbuka mtoto wake aliyemficha
kule nyumbani kwake kabatini, Jérome Muganza yeye alikuwa akilia juu ya
hofu ya kifo baada ya kuwa ameambiwa ajiandae na wale askari waliomuua
Dr. Francois Trezor. Pia kulikuwa na wanawake wengine watatu waliokuwa
wakilia kwa sauti za kwikwi za chini chini.
Mimi fikra zangu zilikuwa mbali zaidi na mawazo mengi yalikuwa yakipita
kichwani mwangu hata hivyo miongoni mwa mawazo hayo sikuwa na wazo
hata moja la hofu ya kifo. Mpaka kufikia wakati huu nilifahamu kuwa kifo
lilikuwa jambo la kawaida tu katika pango lile nipende au nisipende, na dawa
yake ilikuwa si kukiogopa na kulia usiku mzima la hasha! kwani hali hiyo isingenisaidia kitu na badala yake nilipaswa kufikiria na kujipanga vizuri namna
ya kukabiliana na hicho kifo pale ambapo ningehitajika kukabiliana nacho.
Na hali hiyo ndiyo ilikuwa imenifanya nijikunyate kimya mle pangoni nikitafakari.
Wakati fulani nilipokuwa nikiendelea kutafakari hali hiyo yale maneno ya
Dr. Frencois Trezor yalikuwa yakipita taratibu kichwani mwangu na kwa kweli sikuwa nimeyachukulia kama maneno ayatamkayo mtu anayetapatapa katika mdomo wa tundu la kifo, bali kwangu yalikuwa na maana tofauti kabisa na
hiyo. Yalikuwa ni maneno yenye maana fulani na yaliyozungumzwa na mtu
mwenye ufahamu na akili timamu bila shinikizo la hali yeyote. Nilimuwaza
huyo Dr. Lisa Olivier ambaye kwa mujibu wa maelezo ya marehemu Dr. Francois Trezor yeye ndiye aliyekuwa akifahamu wapi alipokuwa Jaji Makesa hata
hivyo sikufahamu Dr. Francois Trezor alimaanisha nini pale aliposema “Nilikudanganya soldier nisemehe sana soldier”, kwa kweli sikumuelewa alikuwa
akimaanisha nini katika maneno yale.
Niliendelea kutafakari na kujiuliza kuwa Dr. Francois Trezor alimaanisha
nini wakati aliponiambia kuwa tamaa yake ndiyo iliyomponza na kuwa alikuwa ametoka nchini Sierra Lione, Angola na alikuwa akielekea nchini RD Congo, alikuwa akifanya nini kwenye nchi hizo?, nilijiuliza bila kupata majibu.
Niliyakumbuka maneno ya Kanali Bosco Rutaganda kuwa nilikuwa
nimewekwa pale ili niyashuhudie mapinduzi kwanza kisha ndiyo baadaye
hukumu yangu ifanyike na hapo nikayakumbuka na maneno ya Dr. Francois
Trezor kuwa endapo ningefanikiwa kutoka salama kwenye pango hili alinitaka
nikaitahadharishe na kuionya dunia juu ya tukio litakalokuja kutokea katika nchi hii.
Nilijitahidi sana kuyatafakari maneno yale bila ya kupata picha yoyote juu
ya tukio hilo na wakati nikiendelea kutakari nilifahamu fika kuwa isingekuwa
rahisi kuyajibu maswali yangu nikiwa bado nipo ndani ya pango hili dogo nililolifananisha na kaburi la watu hai, na hapo ndipo wazo la kutoroka lilipoanza
kujengeka upya kichwani mwangu.
Niligeuka na kuwatazama watu wote waliokuwa mle ndani na hapo
nikawaona namna walivyokuwa wametaabika na kukata tamaa. Nilimuona
Ikirezi wakati huu akiwa ameacha kulia na alikuwa amejikunyata huku akinitazama ingawaje nilipomchunguza nilijua mawazo yake hayakuwa mle ndani
ya pango. Jean Pierre Umugwaneza yeye alikuwa ameshapitiwa na usingizi na
sasa alikuwa amelala huku amejiegemeza kwenye ukuta wa pango.
Nilimtamzama Jérome Muganza nikamuona kuwa naye alikwishaacha
kulia na sasa alikuwa ametulia akiitazama ile orodha ya majina yaliyokuwa yameandikwa kwenye ule ukuta wa pango. Sikumsemesha neno badala
yake nikamuacha aendelee kutafakari yaliyokuwa kichwani mwake na mimi
nikawa nikiendelea kutafakari hatima yangu kutika pango lile. Nilihisi kuwa
kichwa kilikuwa kikiniuma sana na viungo vyangu vyote mwilini vilikuwa hoi
kwa uchovu, tumbo langu lilikuwa likiunguruma pengine kutokana na ugeni
wa chakula kile kibovu na kibichi nilichokula.
Vile vidonda vya michubuko mikali vilivyokuwa mgongoni mwangu nilianza kuvihisi kuwa vilikuwa vimeanza kukauka hata hivyo bado nilikuwa
nikihisi maumivu makali sana mgongoni. Niligeuka kumtazama tena Ikirezi
pembeni yangu na hapo nilikutana na tabasamu lake.
“Pumzika kidogo” aliniambia huku akitabasamu
“Sina usingizi mpenzi” nilimwambia na hapo akaangua kicheko hafifu huku
akiendelea kunitazama. Niligundua kuwa hisia za mapenzi juu ya msichana
yule zilikuwa zikijengeka taratibu kichwani mwangu kila nilipokuwa nikimtazama lakini nilipokumbuka kuwa alikuwa mke wa mtu tena mwenye mtoto
nilizipuuza hisia zangu na vilevile sikuona kama ule ulikuwa wakati muafaka
kuziruhusu hisia za mapenzi kichwani mwangu.
Bado nilikuwa nikiwaza juu ya hatima ya maisha yangu na watu wote tuliokuwa mle pangoni, nilijikuta nikimuwaza tena Jérome Muganza kuwa endapo
ingetokea kuwa tumefanikiwa kutoroka salama mle pangoni yeye ndiye angekuwa mtu muhimu sana katika kutuongoza kutoka nje ya mapango haya
kwa kuwa alikuwa akivifahamu vizuri vichochoro vyote ndani ya mapango
haya.
Niliwawaza popo wakali na chatu ambao Jérome Muganza hapo awali alikuwa amenieleza kuwa walikuwa wamezagaa ovyo katika kila kona ya mapango
haya na hapo nikaanza kuutathmini ugumu wa kupambana na viumbe hao pale
ambapo tungefanikiwa kutoroka kwani bila shaka nao pia wangekuwa wakimvizia adui yeyote akatishe mbele yao wamshambulie.
Hata hivyo kwangu niliona kuwa ilikuwa ni rahisi zaidi kupambana na viumbe hao kuliko kuendelea kubaki ndani ya pango lili la wafu hai. Fikra hizi
zilinifanya nigeuke tena kuutazama ule mlango imara wa kuingilia mle pangoni huku nikiufananisha na jiwe kubwa lenye uzito wa ajabu lililokuwa limefunikwa kwenye kaburi la wafu hai. Niliendelea kuutazama mlango ule huku
akili yangu ikiendelea kufikiri.