ULIKUWA NI MUDA WA KATI YA SAA KUMI NA SAA KUMI NA MOJA
ALFAJIRI ya siku iliyofuata na nilikuwa sijatongoa hata lepe moja la usingizi
wakati niliposikia makelele ya makufuli ya ule mlango wa pango yakifunguliwa kwa nje. Ghafla moyo wangu ulianza kuingiwa na wasiwasi mwingi,
nikageuka kuwatazama wenzangu mle pangoni nikagundua kuwa nao walikuwa wameshtuka na kuamka toka usingizini na sasa walikuwa wamegeuka
kuutazama ule mlango wa pango huku nyuso zao zikiwa na mashaka.
Mara baada ya Ikirezi kushtuka toka usingizini aligeuka kuutazama ule
mlango kisha akageuka kunitazama mimi na hapo niliusoma uso wake namna
alivyokata tamaa, nikamuonesha ishara ya kumtuliza huku nikimtaka kuwa
asiwe na wasiwasi ingawaje hata mimi binafsi nilifahamu kuwa ujio ule wa
alfajiri haukuwa ule wa kutuletea chakula bali kulikuwa na jambo fulani lisilo la kawaida. Jérome Muganza aligeuka kunitazama na hapo nikayaona machozi yakianza taratibu kushuka mashavuni mwake.
“Wanakuja kutuchukua na kama siyo wewe basi nitakuwa mimi” Jérome
Muganza aliniambia huku sauti yake imejaa kitetemeshi cha hofu.
“Usijali wala hakuna baya lolote litakalotokea” niliongea kama mpumbavu
huku nikijitahidi kumfariji Jérome Muganza ingawaje kwa kiasi fulani nilifahamu kuwa alichokuwa akikizungumza kilikuwa kweli. Nilimuona Jérome
Muganza akiangua kicheko hafifu na nilipogeuka kumtazama nikagundua
kuwa kicheko chake hakikuwa cha furaha bali kicheko cha hofu na kukata
tamaa huku machozi yakimtoka.
“Usinifariji rafiki yangu kwani usiku wa leo sikutapa usingizi vizuri, nilifahamu fika kuwa leo ni mwisho wangu na muda si mrefu ninaenda kufa na labda huenda tutakufa pamoja, mimi na wewe” nilimuona Jérome Muganza kama
ambaye alikuwa akitapatapa kwa hofu, nikamvuta haraka na kumwambia
“Hautakufa rafiki jipe moyo na Mungu wako atakusaidia”
Muda si mrefu ule mlango ulifunguliwa na hapo tukawaona wale wanajeshi wawili waliotuletea chakula siku ya jana wakiwa wamesimama mlangoni
pale, hata hivyo wakati huu hawakuwa na sufuria ya ugali wala ndoo ya maji
na hapo nikahisi baridi kali ya hofu ikipita nyuma ya shingo yangu.
Niliwatazama usoni wanajeshi wale nikazidi kukata tamaa nilipoliona
lile tabasamu la kinyama likianza kuumbika nyusoni mwao na sasa walikuwa wamesimama pale mlangoni huku wakiyazungusha macho yao taratibu
kumtazama mtu mmoja baada ya mwingine mle pangoni. Watu wote wakawa wameinamisha vichwa vyao chini wakikwepa kuonesha sura zao siziwe
kivutio katika macho ya wanajeshi wale. Moyo wangu ukapigwa na taharuki
kwa sekunde chache pale nilipoyaona macho ya askari wale yakiweka kituo
kwa Jérome Muganza na hapo nikaliona tena lile tabasamu la kinyama likizidi
kuchanua kwenye nyuso zao.
“Wewe! simama juu” askari mmoja alifoka huku akimtazama Jérome
Muganza na hapo nilimuona Jérome Muganza akisita kusimama kama ambaye
amri ile haikumhusu.
“Unajifanya hukunisikia siyo? yule askari alifoka kwa hasira na kuanza kuiandaa bunduki yake waziwazi na hapo nikawa napiga mahesabu ya harakaharaka ya namna ya kuweza kuwavamia kwa hila wanajeshi wale. Lakini katika mahesabu yangu niligundua kuwa namna yoyote ya hila katika mazingira
yale ingenipelekea karibu na kifo kwani hakukuwa na mwanya wa kutosha wa
kuweza kufanya hila yeyote kwa sababu wale wanajeshi walikuwa mbali sana
kutoka pale nilipokuwa nimeketi hivyo hadi kuwafikia risasi siyo chini ya sita
zingekuwa tayari zimepenya mwilini mwangu na kuniacha nikiwa marehemu.
Hivyo nilijionya na kutulia huku nikimuomba Mungu.
Nilipogeuka tena hapo nikakutana na macho yaliyokata tamaa ya Jérome
Muganza yakinitazama kana kwamba mimi ndiye niliyekuwa na mamlaka
ya kuwapa amri wanajeshi wale wamwache. Nikamuonea huruma sana hata
hivyo nilimfanyia ishara ya kichwa kuwa asimame juu maana nilijua endapo
angeendelea kukaa pale chini na kupuuza amri ya wanajeshi wale ingekuwa
ni sawa na kukigongea hodi kifo. Jérome Muganza akanielewa na kusimama
kama nilivyomtaka hata hivyo nilipomtazama niligundua kuwa alikuwa akitetemeka sana kwa hofu.
“Sogea mbele!” yule mwanajeshi akafoka na hapo Jérome Muganza akafanya kama alivyoambiwa, akaanza kusogea taratibu kuelekea ile sehemu ya
katikati ya pango. Tukio hili likanifanya niikumbuke siku ya jana ambayo Dr.
Francois Trezor alipigwa risasi humu pangoni baada ya kutimiza amri zinazofanana na hizi anazopewa Jérome Muganza. Ghafla koo langu likaanza
kukauka kwa hofu.
“Simama hapo hapo” yule mwanajeshi alifoka tena wakati Jérome Muganza alipofika sehemu ya katikati ya pango, Jérome Muganza akasimama kama
alivyoamrishwa huku akigeuka tena kunitazama. Nilimuonea huruma sana
hata hivyo sikuwa na la kufanya nikabaki nikimtazama tu. Mara tu Jérome
Muganza aliposimama wale wanajeshi wakaanza kumsogelea taratibu na walipomfikia niliwaona wakitaka kumshika mikono na hapo nilimuona Jérome
Muganza akipingana na tukio lile kwa kuinyanyua mikono yake hewani ili isishikwe.
Wale wanajeshi wakajaribu kutaka kumdhibiti hata hivyo walionekana
kuelekea kushindwa ndipo mmoja wao akamuwahi kwa kumgonga na kitako
cha bunduki kichwani. Lilikuwa ni pigo moja la nguvu kiasi kwamba niliweza kusikia mngongano wa kitako cha bunduki ya askari yule na kichwa
cha Jérome Muganza na muda ule ule niliiona damu ikiruka hewani kutoka
kwenye jeraha kichwani mwa Jérome Muganza huku yeye akipiga yowe kali
la maumivu.
Hata hivyo sauti yake haikwenda mbali sana mle pangoni kwani taratibu ilififia na hapo nikamuona Jérome Muganza akianguka chini huku fahamu zikiwa zimemtoka, hata hivyo wale wanajeshi walimuwahi kabla hajafika chini
wakamdaka huku mmoja akiuweka mkono wake mmoja begani na yule askari
mwingine akafanya vivohivyo kwa ule mkono uliosalia hali iliyompelekea
Jérome Muganza abaki akibembea katikati yao kisha wakaanza kumburuta
wakielekea nje ya pango. Na mara tu baada ya kutoka nje ule mlango wa
pango ulifungwa hivyo wakawa wameendoka na Jérome Muganza, nikabaki
nimeduwaa nisijue la kufanya.
Kwa kweli nilijihisi kuchanganyikiwa kwani nilijua hata kama nafasi ya
kutoroka mle pangoni ingepatikana bado swala la kutoka salama nje mapango
haya lingebaki kuwa ni kitendawili pasipo uwepo wa Jérome Muganza, kwani
ni yeye ndiye aliyekuwa akivifahamu vizuri vichochoro vya mapango haya
na vinginevyo tungejikuta tukizunguka mle ndani na si ajabu sana tungejikuta
tunarudi kule kule tulipotoka.
Bila kujielewa nikajikuta nikigongesha kwa nguvu ngumi yangu ya mkono wa kulia kwenye kiganja changu cha mkono wa kushoto huku tusi zito
likiniponyoka mdomoni, nikainamisha kichwa chini huku nikijihisi kuishiwa nguvu na kukata tamaa. Nilipoinua kichwa nikashtuka kumuona Ikirezi
na Jean Pierre Umugwaneza wakiwa pembeni yangu hata hivyo hakuna aliyenisemesha ingawaje nilipowatazama niligundua kuwa walikuwa wamenuia
kunifariji hasa baada ya fahamu kuwa mtu ambaye angefuatia kuchukuliwa
mle pangoni nilikuwa mimi. Nikatabasamu kidogo kuwatia moyo huku nikiwaonesha kuwa sikuwa nimekata tamaa sana na hali ile.
__________
SIKU NZIMA ILIYOSALIA MLE PANGONI hali ilikuwa imebadilika
sana, yale maongezi ya kirafiki na hali ya matumaini niliyokuwa nimejitahidi kuirejesha ilikuwa imetoweka na wakati wote mle pangoni kulikuwa na
ukimya na vilio hafifu vya hapa na pale vilivyokuwa vikija na kuondoka kama
upepo. Hata hivyo nilishangazwa sana na Ikirezi kwani wakati huo wote hakuwa akilia badala yake alionekana ni mtu mwenye mawazo sana. Mchana kutwa ulipita na hatimaye ukaingia usiku bila ule mlango wa pango kufunguliwa
tena na hivyo tulishinda siku nzima bila kuletewa chakula. Usiku ulipoingia
nikajua siku ile ndiyo ilikuwa imepita kimya kimya na suala la chakula lingekuwa ni mpaka kesho.
Sikuwa na mashaka kuwa ningeweza kuvumilia njaa hata kwa muda wa siku tatu hadi nne kutokana na mazoezi ya kikomandoo na mafunzo ya kijeshi
ambayo yalikuwa yamenikolea vizuri mwilini isipokuwa nilikuwa nikiwahofia wenzangu mle pangoni ambao afya zao zilikuwa zimedhoofika sana.
Usiku ule ulikuwa mgumu sana kwangu pengine katika kipindi chote cha
maisha yangu hapa duniani. Akili yangu haikuweza kutulia kabisa kwani mara
kwa mara nilijikuta nikizungumza peke yangu kama mwehu. Wakati wote
mle ndani ya pango nilikuwa nikimuwaza Jérome Muganza, nikawa kama
ninayemuona akiwa katika mateso makali ya kinyama mbele ya wanajeshi
wale katili waliomchukua, nikabaki nikimuombea kwa Mungu amukoe na
kadhia hiyo.
Niliyaona masaa yalikuwa yakienda haraka sana kupita kiasi na siku ya pili
ilikuwa ikikaribia sana. Nikaanza kuhisi kuwa wale wanajeshi ni kama waliokuwa wakiusogelea ule mlango wa pango taratibu kuja kunichukua. Sikuwa
nikiogopa kuja kuchukuliwa mle ndani ila kilichokuwa kikinitia hofu ni kuwa
kitu gani kingefuata baada ya kuchukuliwa mle pangoni. Ulipofika usiku wa
manane watu wote mle pangoni walilala nikabaki macho peke yangu nikiendelea kutafakari juu ya hatima yangu.
__________
ALFAJIRI YA SIKU ILIYOFUATA iliingia katika utaratibu kama ule uliozoeleka wa siku zote mle pangoni ingawaje mimi binafsi niliiona ile siku ilikuwa imewahi sana, hata hivyo nilikuwa na nguvu na tumaini jipya, tumaini
ambalo sikuweza kufahamu lilitokea wapi. Uso wangu ulijawa na furaha sana
hali aliyowafanya watu wote mle pangoni wanishangae. Watu wote mle pangoni walikuwa wakiniaga na kunitia moyo kwani walikuwa wakijua kuwa
muda wowote ningekuja kuchukuliwa na wale wanajeshi.
Nilizipokea faraja zao na kuwatia moyo kuwa wasiwe na wasiwasi na mimi
na kuwa hakuna baya lolote ambalo lingenitokea ingawaje moyoni nilikuwa
na hofu sana. Baadhi yao walilia sana hata hivyo nilijitahidi kuwatuliza ingawaje moyoni nilifahamu kuwa mwanzo wa safari yangu ya kifo ulikuwa
umewadia. Nilitarajia kuwaona wale wanajeshi wakija kunichukua mapema
mle pangoni lakini haikuwa hivyo kwani masaa yaliendelea kusonga na hapo
nikajikuta nikianza kuingiwa na wasiwasi.
Kitendo cha kutomuona Jérome Muganza akirudishwa tena mle pangoni
kikazidi kuniongezea hofu moyoni huku nikiwaza kuwa pengine angekuwa
ameuwawa na wale wanajeshi. Muda wote nikiwa ndani ya lile pango nilikuwa nikiwafariji Ikirezi na Jean Pierre Umugwaneza kuwa wasiwe na wasiwasi
na badala yake waendelee kumuomba Mungu atuokoe na kadhia ile.
__________
HAIKUWA MPAKA ILIPOFIKA MCHANA ndipo nilipoyasikia makufuli
ya ule mlango wa pango lile yakifunguliwa kwa nje. Watu wote mle pangoni
wakawa wameshtuka na kugeuka wakinitazama katika namna ya kuniambia
buriani hata hivyo mimi nilibaki nikiutazama ule mlango wa pango. Baada ya
muda mfupi niliuona ule mlango ukifunguliwa na hapo niliwaona wanajeshi wanne wakiingia mle ndani, nikafahamu kuwa ulinzi ulikuwa umeongezwa
na hiyo ilitokana na kuwa walikuwa wakija kumchukua mtu hatari aliyekuwa
akizifahamu mbinu zote za kijeshi ambaye mtu huyo ni mimi.
Niliwatazama wale wanajeshi huku nikiwakumbuka wawili miongoni
mwao kuwa walikuwa ni wale waliomchukua Jérome Muganza siku ya jana.
Wale wengine sura zao zilikuwa ngeni machoni mwangu na wote walikuwa ni
wanajeshi wenye afya nzuri, warefu na wenye miili iliyojengeka vizuri kimazoezi na wote walikuwa na bunduki zao mikononi. Nilipowachunguza usoni
nikaziona nyuso zao kuwa hazikuwa na mzaha hata kidogo.
Mara baada ya mlango wa pango kufunguliwa wale wanajeshi wawili wageni machoni mwangu waliingia ndani na kusogea mbele zaidi wakiwaacha
wale wenzao kiasi cha hatua kama nne nyuma yao kisha wakasimama na
kuanza kumtazama mtu mmoja baada ya mwingine mle pangoni. Mimi sikuificha sura yangu kwani nilifahamu kuwa kwa vyovyote walikuwa wamenifuata
mimi na hata kama ningejificha wangenipata tu.
Hivyo nilibaki nikiwatazama wale wanajeshi huku wenyewe wakiendelea
kuwachunguza watu mle pangoni, lakini hatimaye wakaweka kituo kunitazama mimi na hapo nikahisi kama niliyemwagiwa maji ya baridi.
“Luteni Venus Jaka wa jeshi la wananchi wa Tanzania leo ni zamu yako
kamanda” mwanajeshi mmoja kati ya wale wawili aliongea kwa dharau huku
akinitazama.
“Zamu yangu kufanya nini? niliwauliza na hapo wote wakaangua kicheko
“Kwa hiyo unataka kuendelea kukaa humu ndani uchi namna hiyo? mwenzake alidakia huku akiendelea kucheka.
“Kamanda wetu anataka kukuona na bila shaka utakuwa na majibu ya maswali yake” yule mwanajeshi mwingine aliendelea
“Maswali gani? niliwauliza huku nikinuia kuwakoroga akili zao.
“Utajua kila kitu pale utakapoonana naye” mmoja alinijibu na hapo nikageuka kuwatazama wanajeshi wawili waliokuwa wamesimama pale mlangoni
ambao ndiyo wale waliomchukua Jérome Muganza siku ya jana.
“Jérome Muganza yuko wapi? niliwauliza wale wanajeshi kwa hasira.
“Huu ni wakati wa kuyawazia maisha yako Luteni na si maisha ya Jérome
Muganza” mmoja alinijibu kwa dharau.
“Mnafichaficha nini kwanini msizungumze kama wanaume waliotahiriwa
jandoni au mmemuua? niliwauliza na hapo nikajikuta nikitandikwa ngumi nne
tumboni hali iliyonipelekea nimtapikie usoni yule mwanajeshi aliyekuwa akinipiga huku nikihisi maumivu makali sana tumboni.
Yule mwanajeshi alighadhibika sana kwa yale matapishi yangu akazidi kunishushia kipigo cha nguvu lakini mwenzake aliwahi kumkataza kuwa aniache
kwani hali yangu ingezidi kuwa mbaya zaidi. Yule mwanajeshi alisitisha kunipiga huku akionekana kufura kwa hasira ya kukatishwa adhma yake na muda
uleule ikachukuliwa kamba kisha nikaanza kufungwa miguuni na mikononi
kama ng’ombe anayeandaliwa kuchinjwa.
Nilijaribu kufurukuta lakini haikunisaidia kitu kwani yule mwanajeshi
alinidhibiti kikamilifu nikabaki nikihema tu kwa hasira. Alipomaliza kunifunga ile kamba wale wanajeshi waliomchukua Jérome Muganza walikuja
na kunibeba begani kama gogo wakinitoa mle pangoni na wale wanajeshi
wengine wakatufuata kwa nyuma huku mitutu yao ya bunduki ikiwa tayari
muda wowote kufanya shambulizi pale ambapo ningejidai kuleta ujanja.
Mara baada ya kutoka nje ya lile pango ule mlango ukafungwa na wale wanajeshi walionibeba waliniweka chini na hapo mmoja alinimbia
“Hatuna utaratibu wa kumbeba mtu luteni utabidi utembee mwenyewe”
Niliitazama miguu na mikono yangu nakaiona kuwa ilikuwa bado imefungwa kamba kwa umadhubuti wa hali ya juu na hapo nikashindwa kumuelewa
yule mwanajeshi alimaanisha nini kuniambia nitembee mwenyewe wakati mikono na miguu yangu ilikuwa bado imefungwa. Wakati nikiendelea
kushangaa nilishtukia nikipigwa mtama na hapo nikaanguka chini mzimamzima na kujipigiza bila mhimili wowote, nikasikia maumivu makali mno.
Mara nikamuona mwanajeshi mmoja akitoa ule mnyororo uliokuwa ukitumika kuniburuta hapo awali wakati nilipokuwa nikiletwa mle pangoni na hapo
nikafahamu kuwa yule mwanajeshi alimaanisha nini wakati aliponiambia
kuwa “Hatuna utaratibu wa kumbeba mtu Luteni utabidi utembee mwenyewe”
Bila ya kufunguliwa zile kamba nilimuona mwanajeshi mmoja akiufunga
ule mnyororo miguuni kwangu na hapo hofu ikanishika kwani nilifahamu
kuwa kutembea kwenyewe kulikozungumziwa kulikuwa ni kule kuburutwa
kama ule utaratibu uliotumika wakati nilipokuwa nikiletwa mle pangoni.
Zoezi la kunifunga ule mnyororo lilipokamilika safari ilianza, mwanajeshi
mmoja alitangulia mbele yangu akiuvuta ule mnyororo niliofungwa miguuni
na mwingine alitembea sambamba na mimi pembeni yangu. Nyuma yangu
walinifuata wanajeshi wawili waliosalia na bunduki zao mikononi. Kwa kweli
nilisikia maumivu makali mno huku nikipiga mayowe bila msaada wowote
kwani wale wanajeshi walikuwa wakinicheka tu na wakati fuani niliwasikia
wakibadilishana maneno kwa lugha ya kinyarwanda ambayo mimi nilikuwa
siifahamu kabisa.
Wakati nikiendelea kuburutwa kwenye sakafu ile mbaya ya mapango yale
nilihisi vile vidonda vikubwa vya michubuko mgongoni mwangu vilivyokuwa
vimeanza kukauka vilikuwa vikitoneshwa upya huku nikiendelea kuchunika
vibaya sehemu za nyuma za mwili wangu. Nilisikia maumivu makali sana ambayo sikuwahi kuyapata katika maisha yangu hata hivyo sikuwa na jinsi nilibaki kumwomba Mungu anisaidie na hapo nikaanza kupoteza fahamu taratibu
ingawaje niliweza kuzihisi njia tulizokuwa tukizipita mle pangoni japokuwa
kulikuwa na giza zito mno lisiloruhusu kumuona hata mtu wa pembeni yangu.
Wakati tukiendelea na safari yetu mle pangoni niligundua kuwa baadhi ya
sehemu za mapango yale zilikuwa na majimaji yaliyokuwa yakitiririka kwenye
mifereji hafifu ya mle ndani. Pia niliweza kuzisikia sauti za popo waliokuwa
wakipiga makelele sehemu fulani fulani na hapo nikayakumbuka maneno ya
Jérome Muganza juu ya popo na chatu wakali waliokuwa ndani ya mapango haya. Nikajikuta nikimuomba Mungu atuepushe tusije tukakumbanana na
mashambulizi ya viumbe hao huku mimi nikiwa bado nimefungwa mikono na
miguu yangu. Tulisafiri kiasi cha umbali wa kama mita mia mbili hivi huku tukizipita kona
nane za mapango yale ambazo nilikuwa makini sana kuzihesabu huku nikijaribu kuyazoea mazingira yake. Baada ya kusafiri kwa umbali ule hatimaye safari yetu ilikuja kuhitimika mbele ya mlango mmoja uliokuwa sehemu fulani
katika mapango yake.
Tulipofika hapo wale wanajeshi walisimama na mmoja wapo akaenda kugonga kwenye mlango ule, baada ya kugonga kidogo nilimuona mtu fulani
ndani ya chumba kile akifungua dirisha dogo lililokuwa juu ya mlango ule
na kuchungulia. Alipofungua akatazama tazama kisha sura yake ilitoweka na
lile dirisha kikafungwa halafu muda ule ule niliuona ule mlango wenye dirisha ukifunguliwa. Mlango ulipofunguliwa yule askari aliyekuwa mbele yangu
akaanza tena kuniburuta kuelekea ndani ya chumba kile cha pango huku wale
wenzake wakitufuata kwa nyuma.
Tulipoingia tu mle ndani ule mlango ulifungwa nyuma yetu na tukawa tumetokezea kwenye korido nyingine ya pango ambapo tuliendelea na safari
nyingine yenye urefu wa kama mita ishirini hivi. Tulipofika hapo tukakunja kona upande wa kushoto na hapo mbele yetu niliuona mlango mwingine
mkumbwa zaidi ya ule wa awali na kulikuwa na miale hafifu ya mwanga iliyokuwa ukipenya kutoka ndani ya chumba kile. Tulipofika tulisimama na mwanajeshi mmoja alienda kugonga mlangoni pale kama alivyokuwa amefanya
kwenye ule mlango wa awali.
Kulikuwa na dirisha jingine dogo kama lile lililokuwa kwenye ule mlango
wa awali ambapo mara baada ya yule mwanajeshi kugonga lile dirisha lilifunguliwa kisha mtu fulani alichungulia. Sikuweza kuiona vizuri sura ya mtu
yule na mara baada ya mtu yule kuchungulia lile dirisha lilifungwa kisha ule
mlango ukafunguliwa na yule mwanajeshi akaanza kuniburuta kuelekea ndani
ya chumba kile.
__________
TULIPOINGIA TU MLE NDANI ule mlango ulifungwa nyuma yetu na
hapo nikajua kuwa tulikuwa tumefika mwisho wa safari yetu. Tulipoingia tu
niliweza kumuoa yule mtu aliyetufungulia mlango akiwa amesimama pembeni ya mlango ule. Niligeuka kutazamatazama upande huu na ule mle ndani na
hapo nikakikumbuka vizuri kile chumba kuwa kilikuwa ni kile chumba nilichokuwa nimeletwa siku ya kwanza baada ya kutekwa kule njiani.
Mbele ya chumba kile nyuma ya meza kubwa idadi ya watu ilikuwa imeongezeka na kulikuwa na makamanda watano wa jeshi. Watatu walikuwa ni
wale niliowaona siku ile ya kwanza nilipofikishwa ndani ya mapango haya
yaani Kanali Bosco Rutaganda na wenzake wawili. Wengine walikuwa ni
makamanda na maafisa wa kizungu wa jeshi la umoja wa mataifa la kulinda
amani nchini Rwanda. Maafisa hao wawili wa kizungu walikuwa ni wa jeshi la
Ufaransa, niliweza kuwatambua kutokana na mavazi yao ya kijeshi hata hivyo
nilishindwa kuelewa ni kwanini maafisa wale wa jeshi la umoja wa mataifa
walikuwa mle ndani.
Wakati huo yule mwanajeshi aliyekuwa akiniburuta alikuja na kuniketisha kwenye kiti kilichokuwa kikitazamana na ile meza ya maafisa wa kijeshi
waliokuwa kiasi cha umbali wa hatua nne mbele yangu na hapo nilijikuta nikitazamana na meza ile huku Kanali Bosco Rutaganda akiwa katikati yao.
Nilijihisi mfadhaiko kwa kuketi uchi mbele ya wanaume wenzangu hata
hivyo sikuwa na namna nikabaki nikitazamana na Kanali Bosco Rutaganda
na hapo nikaliona tabasamu lake la dhihaka likichanua usoni mwake. Nilipokichunguza chumba kile cha pango nikagundua kuwa sehemu kubwa ya
chumba kile ilitawaliwa na giza zito. Mwanga mdogo wa taa ya kandili iliyokuwa juu ya meza ya maafisa wale ndiyo iliyoleta nuru kidogo mle ndani.
Baada ya kuketishwa vizuri na kufungwa kamba kwenye kiti kile wale wanajeshi wawili yaani yule aliyekuwa akiniburuta na yule mwenzake waliyekuwa wakiongozana kutuletea chakula kule pangoni walipiga saluti kwa pamoja
wakaaga na kuondoka hivyo mle ndani tulibaki jumla ya watu tisa. Yaani wale
maafisa wa jeshi watano waliokuwa wameketi nyuma ya ile meza, mimi na
wanajeshi wengine watatu, wawili wakiwa ni wale waliokuwa wakinilinda
kwa nyuma wakati nilipokuwa nikiburutwa kuja humu ndani na mmoja alikuwa ni yule aliyetufungulia mlango wa chumba hiki cha pango.
Wanajeshi wale wawili walikuwa wamesimama nyuma yangu na yule
mmoja alisimama pale mlangoni wote wakinitazama na sasa chumba kilikuwa
kimetulia na hakuna sauti yoyote iliyokuwa ikisikika mle pangoni. Niliyazungusha macho yangu taratibu kukikagua vizuri kile chumba na watu wale, juu
ya ile meza ya maafisa wa kijeshi kulikuwa na bastola moja ambayo sikuelewa
nini hasa lilikuwa dhumuni la kuiweka bastola ile pale mezani. Wale wanajeshi wawili waliokuwa nyuma yangu sikuweza kugeuka na kuwatazama kutokana na namna kamba zile nilizofungwa zilivyokuwa zimenikaba.
Nilipogeuka kumtazama yule mwanajeshi aliyesimama pale mlangoni
nikaiona kurunzi ndefu ikiwa imening’inia kiunoni mwake na bunduki yake
mkononi tayari kunishambulia pale ambapo ningethubutu kufurukuta. Nikayarudisha tena macho yangu kuwatazama wale maafisa wa kijeshi mbele yangu.
“Habari yako Luteni” Kanali Bosco Rutaganda akaanza kwa kunisalimia
huku akitabasamu nikajua tu alikuwa akinisanifu hata hivyo nilimuitikia kwa
utulivu.
“Si nzuri”
“Kwa nini? aliniuliza huku akiiegemeza mikono yake mezani.
“Nina njaa kali naomba mnisaidie chakula kwanza” niliwaambia hapo wote
wakaangua kicheko.
“Mara hii tu unahitaji chakula wakati hata kazi yetu bado hujaifanya? Kanali Bosco Rutaganda akaniuliza huku akiendelea kuangua kicheko hafifu.
“Nahitaji chakula kwanza ndiyo nitaweza kuwafanyika hicho mnachokihitaji” nilisisitiza
“Usilete hila Luteni kwani huu si wakati wake” Kanali Bosco Rutaganda
alikatisha kicheko chake na kuniamba huku akinikazia macho.
“Hila gani nitakayoileta hapa katika hali ya kufungwa kama hii?, nina njaa
kali nahitaji chakula kwanza” nilimwambia huku nimeshikwa na hasira na hapo nikamwona Kanali Bosco Rutaganda akimfanyia ishara fulani yule mwanajeshi aliyesimama pale mlangoni na hapo nilimuona yule mwanajeshi akifungua mlango na kutoka nje ya lile pango.
Ulipopita muda wa dakika kama kumi yule mwanajeshi alirudi akiwa na sahani moja iliyojaa wali na nyama ya kuku, mkono mwingine alishika gudulia
la maji ya kunywa na kikombe. Nilistaajabu sana kukiona chakula cha namna ile mle pangoni huku nikijiuliza kilikuwa kimeletwa au kulikuwa na watu
fulani mle pangoni waliokuwa wakipika, kwa kweli sikutapa majibu. Yule
mwanajeshi aliyerudi na chakula alikuja na kusimama pembeni yangu huku
akiitazama ile meza ya Kanali Bosco Rutaganda, nikajua alikuwa akisubiri
amri kutoka kwa bosi wake.
“Nifungue mikono wewe bwege sasa unadhani nitakulaje, vitu vingine siyo
mpaka usubiri maelekezo ya mumeo” nilimwambia yule mwanajeshi na hapo
nilimuona alivyobadilika na kufura kwa hasira ingawaje hakunifanya kitu chochote mbele ya mabosi wake.
“Mfungue” Kanali Bosco Rutaganda akamwambia na hapo nikamuona yule
mwanajeshi akianza kunifungua zile kamba nilizofungwa kifuani na mikononi,
hata hivyo niligundua kuwa alikuwa akinifungua kwa jazba kwa vile nilikuwa
nimemtukana. Hali ile ikanifanya nianze kuwaza kuwa endapo wale maafisa
wa kijeshi wasingekuwepo mle ndani mwanajeshi yule angeweza kuitumia
nafasi hiyo kuzimalizia hasira zake zote kwangu, hata hivyo sikumuacha na
wakati alipokuwa akinifungua zile kamba nilimnong’oneza
“Mbona unakuwa na hasira hivyo utadhani mwanamke mwenye mimba
changa? nilimwambia na hapo akanitandika ngumi mbili mgongoni za kiujanjaujanja ambazo hakuna mtu yeyote aliyemuona mle ndani na hapo nikahisi
maumivu makali mgongoni.
“Leo ndiyo mwisho wako wewe mwanaharamu na usifikiri kwamba utapata
nafasi ya kuponyokwa tena na maneno yako machafu mdomoni” yule mwanajeshi alininong’oneza kwa hasira bila ya mtu yeyote mwingine kumsikia
mle ndani kwani wale maafisa wa kijeshi walikuwa wakiteta jambo fulani
hivyo hawakuwa wakitutazama kwa wakati ule.
Nilitabasamu kidogo huku nikiyatafakari maneno ya mwanajeshi yule, sasa
nilifahamu kuwa nilikuwa nikiandaliwa mazingira ili niuwawe. Nikaushukuru uchokozi wangu kwani ulikuwa umenipelekea kuzisikia habari zile nyeti
ingawaje yule mwanajeshi yeye alidhani kuwa alikuwa akiniambia vile kwa
kunikomoa kumbe badala yake alikuwa amenipa habari za kunitahadharisha.
Niliwatazama tena wale maafisa wa kijeshi mbele yangu, upande wa kushoto wa Kanali Bosco Rutaganda alikaa mzungu mmoja ambaye nilimtambua
kwa cheo chake cha kijeshi cha Meja Theodole Nicholous na kulia kwake
alikaa Luteni Kanali Jean Petit wote wakiwa na beji maalum vifuani mwao
kwenye sare zao za kijeshi, beji hizo zikieleza majina na vyeo vyao.
“Hawa ni akina nani? nilimuuliza Kanali Bosco Rutaganda huku nikiwakodolea macho wale maafisa wa kijeshi wazungu
“Hawa ni marafiki zetu wanaotusaidia kulinda amani hapa nchini Rwanda”
Kanali Bosco Rutaganda alinijibu kwa utulivu
“Kwanini wako hapa?
“Wanataka kukusikia wewe”
“Wanisikie nini?
“Chochote unachokifahamu kuhusiana na hali ya usalama ya hapa Rwanda
kwani pengine taarifa zako zikawasaidia wazidi kudumisha usalama” Kanali
Bosco Rutaganda alinijibu huku akinitazama na hapo nikauona uso wake namna ulivyobadilika na kuwa wa kinyama.
“Kitu gani?
“Usilete mchezo na mimi luteni, usidhani kuwa nimekuja hapa kufungisha
ndoa, kumbuka ulituambia kuwa una njaa kali na usingeweza kuifanya kazi
yetu hadi upewe chakula. Umepewa chakula sasa ni wakati wa kujibu maswali
yetu kwa unyoofu na si kutuletea ubabaishaji” Kanali Bosco Rutaganda alinifokea kwa hasira kisha akakohoa kidogo na kuendelea
“Tuambie, ulitumwa hapa Rwanda kufanya nini na kipi ulichokipata mpaka
sasa?
“Mimi sikutumwa na mtu bwana nani aliyekuambia mimi nimetumwa?
“Kama hujatumwa ni sawa, basi tueleze ni kipi kilichokuleta hapa Rwanda”
“Nilikuja kupumzika na kustarehe tu niifurahie likizo yangu”
“Na hili jina la Patrick Zambi umelipata wapi?
“Nimepewa na wazazi wangu”
“Kwa hiyo wewe una majina mawili?
“Matatu” nilimkatisha huku nikipandwa na hasira kwa kuulizwa maswali ya
kipuuzi na mwanafunzi wangu wa kijeshi.
“Majina matatu?
“Ndiyo, moja ni la kikabila” niliongea na hapo nikamuona Kanali Bosco
Rutaganda akicheka kwa dharau.
“Usitudanganye luteni mtu mmoja hawezi kuwa na majina matatu huo ni
utapeli, mara hii uitwe Venus Jaka mara hii uitwe Patrick Zambi na wakati
huohuo uitwe sijui nani huko, hebu kuwa mkweli na utuambie umefuata nini
hapa Rwanda”
“Si nimeishakueleza kuwa nimekuja hapa Rwanda kupumzika na kustarehe,
nipo likizo kwa kipindi cha mwezi mmoja”
“Usijifariji kuwa unaweza kutudanganya danganya kirahisi luteni”
“Sasa mnataka nisemeje? nilimuuliza.
“Sema ukweli wako kwani ni ukweli tu ndiyo utakaokusaidia vinginevyo
hatutoivumilia janja yako” Kanali Bosco Rutaganda aliniambia halafu akaweka kituo kidogo kama anayefikiria jambo kabla ya kuendelea tena
“Bila shaka upo hapa nchini Rwanda kwa ajili ya uchunguzi wa kifo cha
mwandishi wa habari Tobias Moyo, hizo ndizo habari tulizonazo na wewe si
mwandishi wa habari wa kujitegemea uitwae Patrick Zambi kama unavyopenda watu wa hapa Rwanda wakufahamu. Wewe ni mpelelezi tena wa jeshi la
wananchi wa Tanzania mwenye cheo cha luteni. Tunachotaka kufahamu ni
yapi mafanikio ya kazi yako tangu ulipofika hapa Rwanda”
Niliinua macho yangu kumtazama Kanali Bosco Rutaganda huku nikiwa na
donge la chuki kooni baada ya kuifahamu vizuri hila yake. Yule mwanajeshi alimaliza kunifungua zile kamba katika muda mfupi tu na hapo nikahisi ahueni, nikaipokea ile sahani ya wali na kuipakata mapajani kisha nikaanza kula
taratibu bila kujali kuwa wale watu mle ndani walikuwa wakinitazama.
Wakati nikiendelea kula nikajikuta nikimuwaza Jérome Muganza huku nikijiuliza kama alikuwa tayari amekwisha uwawa au bado alikuwa hai, na kama
alikuwa hai alikuwa wapi kwa wakati huu. Niliendelea kula taratibu huku nikitafakari ulinzi imara uliokuwa mle ndani, kwa kweli nilikata tamaa sana kwani
sikuona udhaifu wowote ambao ningeweza kuutumia katika kujiokoa. Wale
wanajeshi hawakuyaondoa macho yao kwangu kwani kila mmoja alionekana
kuzifuatilia vizuri nyendo zangu na hali hiyo ilinikatisha tamaa sana.
Nilikumbuka namna safari yangu ilivyokuwa nzuri wakati nilipokuwa nikitoka jijini Dar es Salaam kuja hapa Rwanda na kwa kweli sikuwa nimetarajia
kukutana na kadhia hii tena mapema kiasi hiki. Sasa nilijiona kuwa nilikuwa
nikielekea kufa tena kifo cha aibu kisicholingana kabisa na hadhi yangu. Kufa
nikiwa uchi wa mnyama na pengine maiti yangu kutupwa sehemu fulani mle
pangoni na taarifa zangu kupotelea kusikojulikana.
Kwa mara nyingine nilijikuta nikimkumbuka Brigedia Masaki Kambona,
mratibu wa safari zangu za kijasusi na hapo nikaanza kumhisi ni kama aliyekuwa akiujua mwisho wa maisha yangu mahali pale, kwa kweli nilihisi
kuchanganyikiwa.
“Luteni fanya haraka utueleze mpaka sasa umefikia wapi katika harakati
zako hapa Rwanda kwani wageni wangu wanataka kuondoka na wanahitaji
kusikia toka kwako” Kanali Bosco Rutaganda aliyakatisha mawazo yangu na
kuyarudisha mle pangoni na hapo nikabaki nikimtazama tu.
“Tafadhali tueleze luteni hatuna muda wa kuendelea kukusubiri zaidi”
Kanali Bosco Rutaganda aliendelea na hapo nikamuona ni kama aliyekuwa
akiharakisha kifo changu huku nikiingiwa na hofu kwani sikujua ni kitu gani
kingetokea pale ambapo kile walichokitarajia kutoka kwangu wangekikosa.
Nilipokuwa nikimaliza tonge la mwisho la chakula kwa maana nyingine
nilijiona ni kama niliyekuwa nikigongelea msumari wa mwisho kwenye jeneza langu mwenyewe, nikaiweka ile sahani chini kisha nikajimiminia maji na
kugida bilauri mbili za chapuchapu. Kilikuwa chakula kizuri na kitamu na
nilipomaliza kula nikahisi hali ya nguvu ya mwili wangu ilikuwa imerudi sehemu yake.
Nilikuwa nimeshiba vizuri hivyo nilitulia kwenye kile kiti nikisubiri kifuatacho. Kanali Bosco Rutaganda alinitazama na kukenua meno yake meusi
yenye ukungu wa moshi wa sigara huku akitabasamu. Hata hivyo tabasamu
lake halikuwa na maana yoyote kwangu kwani nilibaki nikimtazama kwa hasira.
“Bila shaka umeshiba vizuri luteni na sasa upo tayari kutueleza” Kanali Bosco Rutaganda aliniambia huku akiendelea kutabasamu kwa dhihaka.
“Nilikuwa na njaa sana”
“Haya tueleze”
“Sasa mnataka niwaeleze nini ambacho hamkijui? nilimuuliza huku nikijichokoa meno kutoa mabaki ya vipande vya nyama vilivyonasa.
“Tunachokijua sisi ni sehemu ndogo tu ya ulichonacho ndiyo maana upo
hapa utueleze hiyo sehemu iliyosalia”
“Mna hakika gani kwamba mimi nina hiyo sehemu iliyosalia? niliwaambia
na hapo nikawaona wakigeuka kutazamana huku kila mmoja akionesha kukasirishwa na maneno yangu
“Luteni si unafahamu kuwa kufanya ujasusi kwenye nchi yoyote ni kosa
kubwa lisilostahili kusameheka, kwani hiyo ni sawa na kuzichunguza siri za
nchi husika na kuzitumia kwa maslahi ya nchi yako. Kosa hilo huwa halina
msamaha na msamaha pekee unaoweza kujitokeza ni kwa kushirikiana na sisi
vizuri kwa kutupatia taarifa tunazozihitaji”
“Mimi sina taarifa zozote vinginevyo si mngeziona katika ile kamera yangu
mliyoichukua”
“Usitufanye sisi ni watoto luteni! ile kamera ni mpya na wala haina kitu
chochote tumeisha ichunguza”
“Si ndiyo nilikuwa nataka nianze kazi yangu nyie mkanikamata”
“Ulikuwa ukitaka kuanzia wapi hiyo kazi yako?
“Bado nilikuwa sijaamua nianzie wapi ila mpaka kufikia usiku wa siku ile
ningepata wazo la wapi pa kuanzia. Hivi hufahamu kuwa kazi yangu nyingine
ni uandishi wa habari? nilimuuliza Kanali Bosco Rutaganda na hapo niliona
uso wa chuki kali ukiumbika taratibu usoni mwake.
“Tukitaka tunaweza kukulazimisha utuambie kila kitu lakini sidhani kama
utapenda tufike huko, hata hivyo uvumilivu wetu huwa una kikomo”
Kanali Bosco Rutaganda aliniambia huku uso wake umefura kwa hasira. Nilipomtazama nikagundua kuwa alikuwa akimaanisha alichokuwa akikiongea
lakini hali hiyo haikunishawishi nitake kumueleza juu ya safari yangu ya kuja
hapa Rwanda. Nilimkumbuka mwalimu wangu wa mafunzo ya kijeshi wakati
nilipokuwa mafunzoni pale alipokuwa akisema “Unapokamatwa mateka katika uwanja wa kivita usidhani kuwa ukisema ukweli ndiyo utakuwa salama,
hiyo haitakusaidia kitu kwani hata kama ukizungumza ukweli adhabu yako
bado itabaki palepale kwani wewe bado ni mateka tu”. Na katika pango hili
nilifahamu kuwa nikiwa kama jasusi adhabu pakee niliyostahili ingekuwa ni
kifo tena bila shaka kifo cha kinyama chenye maumivu makali mno, hivyo
niliona ni bora nife na siri zangu moyoni kuliko kuwaambia kwani hiyo isingenifaa chochote.
Niliwatazama wale wazungu wawili wafaransa maafisa wa jeshi la umoja
wa mataifa (UN) ambao walikuwa hapa nchini Rwanda kama walinzi wa
amani huku nikishindwa kuwaelewa walikuwa ni walinzi wa amani wa namna
gani wanaoshirikiana na mtu muuaji kama Kanali Bosco Rutaganda, na walikuwa wamekuja mle pangoni kusikia nini kutoka kwangu?.
Nilikumbuka kuwa Kanali Bosco Rutaganda alinitaka nimueleze nilipofikia
katika upelelezi wangu juu ya kifo cha mwandishi Tobias Moyo lakini nilishindwa kuelewa ni kwanini alinitaka nimueleze mambo yangu mbele ya
maafisa wale. Nikabaki nimeinamisha kichwa changu chini huku nikimuomba
Mungu.
Nikiwa bado natafakari nilimsikia Kanali Bosco Rutaganda akiteta jambo fulani na wale maafisa wa jeshi wazungu katika lugha ya kifaransa kisha
nikamuona Kanali Bosco Rutaganda akigeuka kunitazama.
“Luteni!, au labda nikuoneshe ni kitu gani ninachomaanisha” Kanali Bosco
Rutaganda aliniambia na hapo nilimuona yule mwanajeshi aliyesimama pale
mlangoni akiiwasha ile kurunzi yake iliyokuwa ikining’inia kiunoni halafu
akamulika upande wa kushoto wa pango lile sehemu kulikokuwa na giza, ikabidi na mimi nigeuke kuutazama ule mwanga wa ile kurunzi mahali ulipokuwa ukimulika, loh! nilijikuta nikishikwa na taharuki.
Kulikuwa na miili ya watu wawili iliyokuwa imefungwa kamba miguu juu
kichwa chini huku ikining’inia toka sehemu ya juu ya pango lile, umbali mfupi
toka pale nilipoketi. Miili hiyo ilikuwa ikibembea taratibu juu ya paa la pango lile na nilipoitazama nikajikuta nikikata tamaa sana ya maisha yangu. Ule
mwili wa mtu wa kwanza ulikuwa umetapakaa damu kila mahali na nilipoutazama vizuri nikaona kuwa ulikuwa na majeraha ya mapanga karibu kila eneo,
vilevile damu nyingi ilikuwa imejikusanya chini ya mwili ule na sikuwa na
shaka kuwa mtu yule alikwishakufa ingawaje matone ya damu yake yalikuwa
bado yakiendelea kuchuruzika taratibu pale chini sakafuni.
Ule mwili wa mtu wa pili ulionesha uhai hafifu kwa kiasi fulani ingawaje
nao ulikuwa na majeraha katika baadhi ya sehemu na ulikuwa ukiendelea kuchuruzika damu taratibu. Niliutazama mwili wa mtu yule na hapo nikajikuta
nikimkumbuka Jérome Muganza na kwa kweli hofu ilinishika sana hasa pale
nilipowaza kuwa pengine angekuwa yupo miongoni mwa watu wale wawili.
Wakati nikiendelea kuwaza ghafla ile kurunzi ilizimwa na kunifanya nigeuke kutazama kwenye ile meza ya maafisa wa kijeshi na hapo nikajikuta nikitazamana na Kanali Bosco Rutaganda huku lile tabasamu lake la kinyama likichanua usoni mwake. Kisha nikamuona akifikicha macho kwa vidole vyake
na alipomaliza aliiweka tena mikono yake pale mezani.
“Tuambie luteni umefikia wapi katika upelelezi wako?
“Nikwambie nini tena?, na hawa maafisa wa jeshi la kulinda amani la umoja
wa mataifa wapo hapa kwa sababu gani?
“Hawa ni marafiki zetu wanaotusaidia sana kulinda amani hapa nchini na
wamekuja humu ndani kututembelea na kusikia kutoka kwako” Kanali Bosco
Rutaganda aliniambia huku akicheka kwa kebehi.
“Wanawasaidia nini?
“Hiyo si kazi uliyotumwa hapa Rwanda tafadhali tuambie umefikia wapi
kwenye huo uchunguzi wa kifo cha Tobias Moyo na usitupotezee muda wetu
luteni” Kanali Bosco Rutaganda alipiga mikono yake juu ya meza na kufoka.
“Mbona mnaning’ang’aniza niwape majibu kwa kazi ambayo hamjanituma?
niliwaambia lakini kabla sijaamaliza kuongea ghafla nilishangaa nikichotwa
pale nilipoketi kwa wepesi wa kushangaza na muda uleule nikapandishwa juu
na kugeuzwa kichwa chini miguu juu, nikawa nikining’inia hewani na kile kiti
nilichokuwa nimekikalia nikawa nakiona kwa chini yangu.
Nikagundua kuwa kile kiti kilikuwa kimewekewa mtego wa kamba unaoweza kumchukua hewani mtu yoyote pale anapokikalia baada ya kufyatuliwa kwa siri. Wale watu wote mle ndani wakaangua kicheko cha dhihaka. Kwa kweli nilijiona kama bwege kwa kuchezewa akili yangu bila kupenda na hapo
tusi zito likaniponyoka nikiwatukana watu wote mle ndani.
“Hakuna aliyewahi kuingia kwenye pango hili akabaki na siri zake moyoni
luteni, hivyo hata wewe tunaamini kuwa utatuambia tu” Kanali Bosco Rutaganda aliniambia na muda huohuo nilimuona akiinama na kuvuta droo mojawapo ya ile meza aliyoketi na mikono yake iliporudi mezani ilikuwa imeshika misumari na nyundo. Hofu ikazidi kunishika, nikajikuta nikifumba macho
na kumuomba Mungu kwani nilifahamu kitu gani kilichokuwa kikifuatia. Nilipofumbua macho nikamuona yule mwanajeshi aliyekuwa amasimama pale
mlangoni akifungua mlango na kutoka, nikajua alikua ameagizwa kitu fulani.
Muda mfupi baadaye yule mwanajeshi alirudi huku akiwa amebeba jiko
la mkaa uliokolea vizuri, nilishtuka sana kuliona lile jiko na nilipotazama
vizuri nikaviona vipande vya nyaya ngumu kama zile zitumikazo kubanikia
mishikaki zikiwa zimepata moto kisawasawa na kuwa nyekundu na hapo nikajua kuwa nilikuwa nikiandaliwa mimi, kwa kweli nilikata tamaa sana. Yule
mwanajeshi alitoka tena na aliporudi alikuwa na betri kubwa ya gari aina ya
Yuasa iliyokuwa imefungwa nyaya katika temino zake. Kisha vitu vyote vile
vikasogezwa karibu yangu na hapo nilimuona yule mwanajeshi akiijaribu ile
nguvu ya betri kwa kuzigusanisha zile nyaya mbili ambapo zilipiga shoti kubwa na kutoa cheche.
Nilimuona yule mwanajeshi akifurahi kisha akaenda kuichukua ile nyundo
na ile misumari iliyokuwa pale juu ya meza ya Kanali Bosco Rutaganda na
aliporudi wale wanajeshi wawili walinishika na kunidhibiti vizuri nikawa siwezi hata kujitikisa. Muda huo huo yule mwanajeshi wa mlangoni akazunguka
nyuma yangu na kunishika na mara nikaanza kuhisi maumivu makali huku
nikipiga mayowe lakini hakuna aliyeonekana kushtushwa na hali ile.
Walikuwa wakinigongelea msumari mgongoni mwangu na ule msumari
ulipoingia nusu ya sehemu yake wakaanza kugongelea msumari mwingine
kwenye paja langu la mguu wa kushoto na walipomaliza wakafanya hivyohivyo kwenye paja la mguu wangu wa kulia. Walipomaliza wakahamia na
mikononi ambako walinigongelea misumari miwili mingine, mmoja mkono
wa kushoto na mwingine mkono wa kulia.
Nilihisi maumivu makali mno ambayo sikuwahi kuyapata tangu nizaliwe.
Damu nyingi ilikuwa ikinitoka toka katika majeraha yale ya misumari lakini
hakuna aliyeonekana kujali.
“Luteni! utatusamehe sana kwani hatukupenda tufikishane huku ila ni wewe
ndiye uliyetulazimisha kufanya hivi, hata hivyo muda wa kujiokoa bado
upo. Unaweza kujiokoa kwa kutuambia ukweli kuwa ulikuwa umefikia wapi
kwenye upelelezi wako hapa Rwanda na ulikuwa ukishirikiana na nani kwani
bado hujachelewa sana” Kanali Bosco Rutaganda aliniambia.
Sikumjibu neno kwani hasira ilikuwa imenishika mno na badala yake nikakusanya mate mdomoni na kumtemea usoni. Nilikuwa nimemlenga vizuri na
mate yale yalimpata vizuri usoni pale alipoketi na hapo akajipangusa kwa kiganja chake huku akiwa amefura kwa hasira. Akanyanyuka na kunifuata pale
nilipoketi na hapo akaanza kunitandika ngumi mwilini. Aliendelea kunishushia kipigo hadi pale alipochoka huku wale wanajeshi
wengine wakiwa wakiwa wamenishikilia kikakamavu ili nisifurukute. Damu
ilianza kunitoka mdomoni na puani nikawa nikihema hovyo kuitafuta hewa ya
oksijeni iliyoonekana adimu sana kwa wakati ule.
“Wakati mwingine jifunze kuwa na adabu Luteni kwani jeuri haitakusaidia
kitu hapa” Kanali Bosco Rutaganda alifoka baada ya kusitisha kipigo kile kisha nilimuona akigeuka kuwatazama wale wanajeshi.
“Endeleeni na kazi” hatimaye aliwaambia wale wanajeshi na muda huohuo
nikamuona mwanajeshi mmoja akizichukua zile nyaya za umeme zilizounganishwa kwenye ile betri ya gari na hapo nikajua kuwa walikuwa wamepanga
kunipa mateso kwa kunipiga shoti ya umeme kwani ulikuwa ni mtindo wa
mateso niliokua nikiufahamu vizuri.
Ulikua ni mtindo wa mateso wenye maumivu makali mno yasioelezeka.
Zile nyaya zilipounganishwa kwenye ile misumari iliyogongelewa mwilini
nikaanza kupigwa shoti kali nikitetemeshwa mwili mzima, nilihisi maumivu
makali sana nikapiga mayowe ya hofu huku nikitokwa na jasho jingi.
Hali yangu ilipoanza kuwa mbaya wakaondoa zile nyaya kwenye ile misumari na hapo nikahisi auheni kidogo hata hivyo nilijihisi kizunguzungu huku
nikihisi kutaka kutapika.
“Mwacheni” Kanali Bosco Rutaganda aliwaambia wale wanajeshi “Bila ya
shaka sasa yupo tayari kutuambia”
Mimi nikabaki nikiwatumbulia macho.
“Luteni swali letu si unalifahamu, tunasubiri jibu lako”
“Mimi sifahamu chochote” niliwaabia huku nikiwatazama wale wazungu na
hapa nikawaona wakitabasamu.
“Endeleeni na kazi” Kanali Bosco Rutaganda akawaambia wale wanajeshi
na zile nyaya zikaunganishwa tena kwenye ile misumari. Nikapiga tena yowe
la maumivu huku nikiwasihi waniache kwani hali yangu ilikuwa mbaya sana
lakini hakuna aliyesikiliza ombi langu. Yale mateso yaliendelea zaidi hadi pale
nilipoonekana kuishiwa na nguvu ndipo waliponiacha. Kanali Bosco Rutaganda akasimama na kuja kuninong’oneza sikioni.
“Afadhali utuambie Luteni, tupo tayari kukubadilishia starehe endapo hii
itaonekana haikufai”
“Mimi sifahamu chochote” nilimwambia
“Unafahamu kila kitu Luteni usitudanganye”
“Ningekuwa nafahamu ningewaambia”
“Endeleeni na kazi” akawaambia wale wanajeshi baada ya kuona naendelea
kukaidi na safari hii Kanali Basco Rutaganda aliongea kwa hasira akiwaambia
wale wanajeshi, na zile nyaya zilipounganishwa kwenye ile misumari mwilini
ziliachwa kwa muda mrefu zaidi.
Nilihisi maumivu makali sana nikapiga mayowe nikiwasihi waniache na
wakati huo nikawa nikiisikia sauti yangu namna ilivyokuwa ikisafiri na kutengeneza mwangwi kwenye kona za pango lile. Niliendelea kupiga mayowe
huku kile kizunguzungu kichwani kikizidi kuongezeka na hatimaye nikaacha
kupiga mayowe kwani nilihisi kuishiwa nguvu.
“Tuambie Luteni” nilisikia tena sauti ya Kanali Bosco Rutaganda ikininong’oneza tena sikioni
“Mimi sifahamu chochote mtaniua bure tu” nilimjibu huku nikifumbua macho kumtazama na hapo nilimuona akiwa ameshika waya uliokuwa kwenye
lile jiko la mkaa ambao wakati huu ulikuwa umepata moto kiasi cha kuwa
umebadilika rangi na kuwa mwekundu. Ule waya sasa ulikuwa sentimita
chache mbele ya macho yangu na nilipomtazama Kanali Bosco Rutaganda
nikamuona akitabasamu.
“Tunakubadilishia starehe Luteni utatusamehe kidogo” Kanali Bosco Rutaganda aliniambia huku akicheka na muda uleule wale wanajeshi wakanikamata vizuri kiasi kwamba sikupata nafasi ya kujitingisha na ule waya uliopata
moto vizuri ukawekwa juu ya jicho langu la kulia. Maumivu niliyoyasikia
hayaelezeki kwani nilikuwa nikiungua taratibu na nikawa nikinusa harufu ya
nyama mbichi iliyokuwa ikiungua pembeni ya jicho langu, harufu ya mchomo
wa nyama iliyoambatana na moshi hafifu. Maumivu niliyoyasikia niliomba
ardhi ipasuke nitumbukie ili niwe mbali na kadhia ile.
Nikaachama mdomo wangu ili nipige mayowe kuomba msaada lakini sauti
haikutoka. Kwa kweli nilijisikia vibaya sana kama niliyekuwa mbioni kukata
roho.
“Haya tuambie Luteni” Kanali Bosco Rutaganda alininong’oneza hata
hivyo sikuweza kumjibu kwani hali yangu ilikuwa mbaya sana.
“Endeleeni na kazi” nilimsikia akiwaambia tena wale wanajeshi na hapo
nilianza tena kuchomwa na zile nyaya kila sehemu mwilini nikilazimishwa
kuongea. Zoezi hili liliendelea huku nikihisi maumivu makali mno mwilini
hata hivyo niliendelea kushikilia msimamo wangu wa kutowaeleza chochote.
Waliendelea kunipa mateso yale na mengine zaidi kwa muda mrefu na walipoona sielekei kuwaambia chochote cha maana Kanali Bosco Rutaganda
akawaambia wale wanajeshi waniache.
“Naona umedhamiria kufa kiume Luteni, wala usijali tunayo njia nyingine
itakayokulazimisha kuongea” Kanali Bosco Rutaganda aliniambia na muda
huo nikamuona akichomoa kisu chake kiunoni.
“Mkamateni vizuri” akawaambia wale wanajeshi
“Unataka kunifanya nini? nilimuuliza kwa hofu
“Usiwe na haraka subiri utaona tu” Kanali Bosco Rutaganda aliniambia
na hapo nikawaona wale wanajeshi wakinishika vizuri, hofu ikaniingia sana
kwani sikujua ni nini walichotaka kunifanyia. Nilijitahidi kufurukuta hata
hivyo sikufanikiwa kwani nilikuwa nimeshikwa kisawasawa na hapo Kanali Bosco Rutaganda akaushika mkono wangu halafu kwa kutumia kile kisu
chake mkononi akaanza kunikata kidole changu cha mwisho kiganjani. Nilisikia maumivu makali sana huku damu nyingi ikinitoka kwenye lile jereha
mkononi, nilijitahidi kupiga mayowe lakini sikufanikiwa sana nikaambulia
kipigo.
Hatimaye kizunguzungu kilinizidi nikawa siwezi tena kuwaona watu waliokuwa mbele yangu mle ndani. Nikaanza kuhisi kuwa hali yangu ilikuwa
ikizidi kuwa mbaya zaidi mle pangoni, damu iliendelea kunitoka kwenye lile jeraha mkononi na nikahisi kuwa uzito wote wa mwili wangu ulikuwa ni kama
unaokielemea kichwa changu.
Nikiwa bado nimening’inia hewani nilijitahidi tena kufumbua macho yangu
bila mafanikio, nikawa nikiona giza tu mbele yangu na kwa mbali niliisikia
sauti ya Kanali Bosco Rutaganda ikiniambia.
“Tuambie Luteni vinginevyo tutaendelea na zoezi hili kwenye vidole
vingine vilivyosalia”
Nilijitahidi tena kufumbua mdomo wangu ili nimjibu hata hivyo sikufanikiwa kwani fahamu zilikuwa mbioni kunitoka. Mwili wangu ulizidiwa na
maumivu makali yasiyoelezeka na sasa nikatambua kuwa mwisho wangu ulikuwa umefika.
Kwa mbali niliweza kuhisi kuwa ile mikono ya wale wanajeshi walionishika
ilikuwa ikiniachia taratibu na mwili wangu sasa ulianza kuwa mwepesi ingawaje ule uzito wa kichwa na maumivu mwilini bado nilikuwa navyo. Halafu
ghafla nikawa siwezi tena kuhisi chochote mle pangoni. Fahamu zikawa zimenitoka.
*************
NILIJIHISI NI KAMA NILIYEKUWA umbali mrefu sana angani nikianguka kwa kasi sana kuelekea ardhini huku nikiwa nimetanguliza kichwa chini.
Picha kamili ya eneo lile nililokuwa nikielekea sikuweza kuiona na kichwa
changu kilikuwa kizito mno kama niliyefungiwa jiwe kubwa.
Mwanga hafifu uliokuwa ukipenya katikati ya kope za macho yangu niliyokuwa nimeyafumbua kidogo ndiyo ulionishawishi kufumbua macho yangu taratibu nikiyazungusha huku na kule bila ya kufanya ishara ya mjongeo
wowote. Mbele yangu nikaona taa ya kandili iliyokuwa juu ya meza pana
yenye viti vitano vitupu nyuma yake ingawaje meza na viti hivyo niliviona ni
kama vilivyokuwa vimegeuzwa juu chini. Nikagundua kuwa fahamu zilikuwa
zikinirudia huku ile picha ya kabla sijapoteza fahamu ikianza taratibu kujikumbusha katika fikra zangu.
Nilikumbuka kuwa nyuma ya meza ile walikuwa wameketi maafisa wa jeshi
ambao wakati huu hawakuwepo mle ndani kwani vile viti vilikuwa wazi. Nilikumbuka pia juu ya meza ile kulikuwa na bastola ambayo nayo wakati huu
haikuwepo na badala yake kulikuwa na kisu kilichokuwa kimetapakaa damu.
Nikakitazama kile kisu na kukumbuka kuwa kilikuwa ni kile kisu cha Kanali
Bosco Rutaganda ambacho ndiyo kilichotumika katika kukikata kidole changu mkononi. Loh! nikahema taratibu huku nikijiuliza maafisa wale wa jeshi
pamoja na Kanali Bosco Rutaganda walikuwa wameenda wapi.
Nikiwa bado ninaendelea kuning’inia hewani huku miguu yangu na mikono ikiwa imefungwa kamba, nilibembea taratibu nikijizungusha nyuma yangu
ili kukagua kama kulikuwa na mtu yeyote aliyekuwa mle ndani lakini katika
mjongeo ambao usingeweza kumshtua mtu yeyote wa karibu. Ile kamba iliyokuwa imenining’iniza ilijizungusha taratibu kwa jitihada nilizozifanya kiasi
kwamba mtu yeyote ambaye angenitazama angeweza kudhani kuwa ulikuwa
ni mjongeo wa kawaida tu. Wakati nikijizunguka niliyatupa macho yangu
kukikagua vizuri kile chumba cha pango na hapo nikagundua kuwa kulikuwa na mwanajeshi mmoja tu mle pangoni ambaye ndiye yule aliyekuwa amesimama katika ule mlango wa kuingilia mle pangoni.
Wale wanajeshi waliokuwa wakinilinda nyuma yangu hawakuwepo na hapo
nikajua kuwa hata wao walikuwa wametoka. Sasa nilibaki nikimtazama yule
mwanajeshi mmoja aliyebakia mle ndani ambaye wakati huu alikuwa amezama katika kuvuta sigara kiasi cha umbali wa hatua zisizopungua tano toka
pale nilipokuwa. Bunduki yake alikuwa ameining’iniza begani huku akitembea taratibu kulizunguka pango lile.
Nilifikiri na kuona kuwa hii ingekuwa nafasi pekee ninayoweza kuitumia kujiokoa kabla ya wale wanajeshi wangine hawajarudi mle ndani au vinginevyo
isingejitokeza bahati nyingine kama hii. Nilijitahidi kuupima mwili wangu
kama ulikuwa na nguvu za kutosha na nikajiridhisha kuwa bado nilikuwa na
uwezo mzuri wa kupambana. Kitu pekee kilichonitia mashaka ni namna gani
ningeweza kupambana huku mikono na miguu yangu ikiwa bado imefungwa
namna ile hata hivyo sikukata tamaa.
Nikawa sasa napanga mahesabu yangu kichwani namna ya kuanza hata
hivyo nilifahamu fika kuwa kujiokoa kwangu kungetokana na kupungua kwa
umbali kati yangu na yule mwanajeshi aliyebaki mle ndani. Kilipita kitambo
kifupi mle pangoni huku nikimsubiri kwa hamu yule mwanajeshi anikaribie
pale nilipo lakini haikutokea hivyo kwani bado aliendelea kuvuta sigara yake
huku akizunguka mle pangoni taratibu katika umbali usiokuwa na msaada
wowote kwangu.
Nilipoona muda unazidi kusonga bila ya yeye kusogea karibu yangu
nikaamua nijitikise kidogo ili kumshtua. Jaribio langu likazaa matunda kwani
yule mwanajeshi akawa kama ameshtushwa na mtikisiko wangu hivyo alisimama na kunitazama huku akiwa ameitoa sigara mdomoni na mimi nikatulia
bila kujitikisa tena. Yule mwanajeshi aliendelea kunitazama kwa udadisi kama
anayejishauri kitu halafu mara nikamuona akipiga hatua kuelekea mlangoni.
Nikajikuta nikikasirishwa na tukio lile kwani nilijua yule mwanajeshi alikuwa akienda kuwaita wenzake, niliaani sana tukio lile nikafura kwa hasira. Yule
mwanajeshi alipofika mlangoni akageuka tena kunitazama na hapo nikamuona ni kama aliyejishauri kwamba aidha atoke akawaite wenzake au alitakiwa
athibitishe kwanza kuwa nimerudiwa na fahamu.
Nilimuona akiufungua ule mlango kidogo huku akinitazama halafu mara
nikamuona akiufunga tena ule mlango na kuanza kunifuata. Nikajikuta nikifurahi kupata nafasi niliyokuwa nikiisubiri kwa hamu. Sasa nilikuwa na hakika
kuwa yule mwanajeshi alikuwa akija kunichuguza kwa ukaribu ili ajiridhishe
kabla ya kwenda kuwaita wenzake nami nikajiandaa kufanya shambulizi la
uhakika.
Alikuwa amebakisha umbali wa hatua moja tu kunifikia pale nilipojirusha
hewani kumrukia akawa kama aliyeshtushwa na tukio lile hivyo akataka
ageuke nyuma na kunikimbia. Chupuchupu nimkose lakini alikwisha chelewa kwani nilikilengesha kichwa chake vizuri ili kipite katikati ya mikono
yangu miwili iliyofungwa kwamba kwa pamoja. Mahesabu yangu yalifanikiwa kwani kichwa chake kiliingia katikati ya mikono yangu akataka akitoe kwa kutumia mikono yake lakini mbinu hiyo haikumsaidia kwani nilikuwa
nimefanikiwa kumbana vizuri kwa kubari moja timamu isiyoruhusu hata kasi
kidogo cha hewa kupenya kwenye kolomelo lake. Akajitahidi kufurukuta na
kutupatupa miguu huku na kule hata hivyo sikumuacha ingawaje alikuwa ni
mwenye nguvu mno.
Alipoona sina mpango wa kumuachia akaanza kunitupia ngumi usoni,
chache zikanipata nyingine nilifanikiwa kuzikwepa hata hivyo niliona endapo
hali ile ingeendelea pengine bahati ingeangukia upande wake na kufanikiwa
kuniponyoka hivyo nilikusanya nguvu tena na kujitupa naye upande mwingine
bila ya kuilegeza ile kabari na tulipojitupa upande ule nikafanikiwa kuivunja
shingo yake, kichwa chake kikalegea na hapo akaishusha chini mikono yake
taratibu huku nikiwa bado nimembana kikamilifu ili asipate nafasi ya kupiga
yowe la kuomba msaada na wakati huo nilikuwa namuomba Mungu kuwa
wale wenzake wasije wakarudi mapema mle ndani na kunikuta nikiwa bado
katika hali ile ya kuning’inia hewani kama nyama buchani.
Yule mwanajeshi alirusha miguu na mikono na hatimaye akatulia na hapo
nikajua nilikwisha maliza kazi, nikamuacha akijibwaga chini kama gunia na
mimi nikabaki nikibembea hewani taratibu. Sasa mawazo yangu yalihamia
kwenye kile kisu kilichokuwa pale juu mezani. Niliupima kwa macho urefu
wa ile kamba iliyokuwa imenining’iniza mle pangoni huku nikijiuliza kama
ingeweza kunifikisha pale juu ya meza kwenye kile kisu.
Sikuwa na uhakika sana na makadirio yangu hata hivyo sikuwa na njia
nyingine mbadala hivyo nikaanza kupunguza ule urefu kati yangu na ile meza
yenye kile kisu kwa kubembea taratibu kutoka upande huu kwenda ule. Mwendo ulipochanganya vizuri nikagundua kuwa ile kamba ilikuwa fupi kidogo
hivyo palihitajika jitihada nyingine kukifikia kile kisu juu ya meza. Niliendelea kuchochea mwendo kasi wa ile kamba na hatimaye nikawa nimekikaribia
kile kisu hivyo nikawa nikienda na kukigusagusa pasipo kupata nafasi nzuri
ya kukichukua. Zoezi hili likaanza kunikatisha tamaa kwani kile kisu nilikuwa
nikikigusa pasipo kupata nafasi nzuri ya kukichukua kiasi kwamba kilikuwa
kikisogea mbele zaidi. Nilirudiarudia zoezi lile bila ya mafanikio na hatimaye
nikapata wazo jipya.
Nilipoenda kwa mara nyingine sikujishughulisha na kile kisu badala yake
niliishika pembe ya meza ile na kuivuta kidogo ile meza hivyo nikawa nikienda kwa kupunguza umbali wakati huo huo nikiomba ile sauti hafifu ya mburuto wa meza isije ikasikika. Mwishowe nikafanikiwa kuisogeza ile meza karibu
na kukichukua kile kisu mezani, nikakishika kwa kiganja changu cha mkono
wa kulia na kuanza kuzikata haraka zile kamba za mikononi. Nilipomaliza nikajipinda na kuishika ile kamba iliyoning’iniza miguu yangu na hapo nikaanza
kuikata kwa haraka huku mara kwa mara nikigeuka kuutazama ule mlango
wa pango ili kujua kama kulikuwa na mtu yeyote aliyekuwa akija. Hali bado
ilikuwa poa tu na hapakuwa na mtu yeyote.
Nyuzi ya mwisho ya kamba ile nilipoikata ilinifanya nianguke ardhini kama
fuko la maembe hata hivyo nilikuwa makini sana nikitua kama paka pasipo
kutoa sauti yoyote ya kishindo. Nilikuwa kama niliyepata nguvu na roho mpya huku nikiyapuuza yale maumivu makali mwilini mwangu. Niliichomoa ile
misumari niliyogongelewa mwilini na hapo nikasikia maumivu makali sana
huku damu nyingi ikinitoka kwenye majeraha yale.
Nilipojaribu kupiga hatua kutembea mara ya kwanza nilishindwa na kupiga
mweleka hata hivyo niliposimama tena nikahisi nguvu mpya mwilini na kile
kizunguzungu kilikuwa kimeanza kupungua ingawaje kichwa bado kilikuwa
kizito na kikiuma sana.
Nilimsogelea yule mwanajeshi kwa tahadhari na nilipomfikia nikajua
asingeweza kuamka tena hivyo nikaichukua ile bunduki yake na ile kurunzi
aliyokuwa akiibeba kiunoni mwake, nilipompekua nikazipata funguo za ule
mlango wa kutokea nje ya pango. Nilipata wazo kuwa isingefaa kuondoka
mle ndani pasipo kuzikagua zile droo za ile meza hivyo nilikatisha katikati ya
kile chumba kuiendea ile meza na nilipofika nikaanza kuzifungua zile droo na
kuanza kupekua, mara nikawa nimeipata ile bastola ambayo ilikuwa juu ya
meza pamoja na kitabu kidogo ndani ya droo zile.
Ni wakati huu nilipogutuka kuwa nilikuwa uchi nikawaza kuwa nisingeweza
kutoka mle ndani nikiwa katika hali ile hivyo nikamkumbuka yule mwanajeshi
niliyemuua mle ndani. Sikutaka kupoteza muda haraka nikamrudia na kumvua
nguo zake ambazo nilizivaa kwa haraka isiyoelezeka ili nisije nikachelewa
na kukutwa mle ndani. Urefu wake na wangu ulikuwa ukilingana hivyo magwanda yake yalinienea vizuri na nilipomaliza nilimvua na buti zake miguuni
na kuzivaa. Sasa nilijihisi kuwa nilikuwa tayari kutoka mle pangoni ingawaje
wasiwasi bado nilikuwa nao juu ya zile njia za kutokea nje ya mapango haya
ambazo zilikuwa ni zenye kona na makutano mengi kiasi kwamba kwa mtu
yeyote mgeni angejikuta akizunguka na kurudi alipotoka bila kujijua.
Nilikuwa tayari nimekwishaufikia mlango wa kutoka nje ya chumba kile
cha pango wakati niliposikia sauti hafifu ikiita nyuma yangu.
“Patrick…Patrick, usiniache” ile sauti ilirudia tena kusisitiza nikatazama
nyuma na kugundua kuwa ilikuwa akitokea kwenye ile sehemu ya pango iliyokuwa na giza.
“Wewe ni nani? niliuliza kwa hofu huku nikiona kero kwa mtu yule kwani
ni kama aliyekuwa akinichelewesha kuondoka mle pangoni.
“Ni mimi Jérome,…Jérome Muganza tafadhali usiniache”. Ile sauti ilisisitiza na hapo nikajikuta nikiikumbuka ile miili ya wale watu wawili iliyokuwa
imening’inizwa kwenye lile eneo lenye giza mle pangoni. Nikaiwasha ile kurunzi kumulika na hapo nilikutana na sura ya mtu iliyotaabika ikinitazama kwa
matumaini. Kama si kuikumbuka vizuri ile sura yake nisingeweza kujiridhisha kirahisi kuwa mtu yule alikuwa ndiye yule Jérome Muganza, mmiliki wa
magazeti la République na mateka mwenzangu niliyekuwa naye kule pangoni
kwani mwili wake wote ulikuwa umetapakaa damu.
“J’erome!, ni wewe? nilimuuliza kwa furaha huku nikishindwa kuamini macho yangu.
“Ni mimi Patrick njoo uniokoe haraka watarudi sasa hivi na kutukuta humu
ndani” yule mtu alinisisitiza na sikutaka kupoteza muda tena nikamfuata na
kuikata ile kamba iliyokuwa imemning’iniza juu kisha nikamshusha chini taratibu na kuzikata zile kamba nyingine alizofungwa miguuni na mikononi
kwa msaada wa kile kisu nilichokichukua juu ya ile meza iliyokuwa mle
ndani. Nilipomchunguza vizuri nikagundua kwa alikuwa na majeraha makubwa ya mapanga mwilini isipokuwa sehemu za kichwani tu na hilo likanitia
moyo kuwa angekuwa na unafuu kidogo ingawaje alikuwa amepoteza damu
nyingi sana.
“Utaweza kutembea? nilimuuliza.
“Ndiyo” alinijibu ingawaje nilipomchunguza vizuri nilifahamu kuwa
isingekuwa rahisi kwake kutembea kama alivyodhani.
“Nilidhani ungekuwa umeuwawa Jérome”
“Ndiyo bila shaka ningekuwa nimeuwawa kwani nilipowaona wanazidi
kunichabanga mapanga ikabidi nijidai nimekufa, nafikiri hicho ndicho kilichowafanya waniache”
“Kwa hiyo uliniona wakati nilipokuwa nikiletwa humu ndani na kuteswa?
“Nilikuona na kwa kweli nilikata tamaa sana kwani sote mle pangoni tulikuwa na imani kuwa ni wewe tu ndiye ambaye ungeweza kutuokoa. Nilikuwa
nikiona kila kitu ulichokuwa unafanyiwa humu ndani hata hivyo sikutaka hata
kujitingisha kwani kwa kufanya hivyo wangenishtukia kuwa bado mzima na
hivyo wangenimalizia kabisa” Jérome Muganza alikuwa akiongea huku akitweta kwa hofu.
“Usijali rafiki yangu sasa upo salama Mungu wako amekuokoa. Na huyu ni
nani? nilimuuliza huku nikiumulika ule mwili wa yule mtu mwingine pembeni
yake.
“Simfahamu, nilimkuta humu ndani akiwa katika hali hiyohiyo bila shaka
atakuwa amekufa”
Nilimsogelea yule mtu na kumtingishatingisha hata hivyo hakuonesha ishara yoyote ya uhai, nikamchunguza vizuri na kugundua kuwa alikuwa tayari
amekufa.
“Tuondoke humu ndani Patrick wale watu watarudi sasa hivi” Jéremo
Muganza alinisisitiza
“Wameenda wapi? nilimuuliza
“Nilimsikia yule afisa aliyekuwa akikuhoji wewe akiwaaga wale wanajeshi
wengine kuwa alikuwa akiwasindikiza wale maafisa wa jeshi wa kizungu na
kuwa angerudi muda si mrefu ili aendelee kukuhoji wewe mpaka hapo utakapozungumza kile anachokihitaji kwako”
Niligeuka kumtazama Jérome Muganza kisha nikatabasamu huku nikiyaamini maneno yake kwani wakati wale maafisa walipokuwa wakiondoka
mimi nilikuwa bado nimepoteza fahamu. Muda uleule nikaunyanyua mkono
mmoja wa Jérome Muganza na kuuweka begani nikimsaidia kutembea, sasa
tukawa tukielekea kwenye ule mlango wa kutokea nje ya kile chumba cha
pango. Moyoni nilikuwa nimefurahi sana kukutana tena na Jérome Muganza
akiwa hai kwani bado angekuwa msaada mkubwa kwangu katika kutoroka
katika mapango haya kwa kuzingatia kuwa ni yeye tu ndiye aliyekuwa akizifahamu vizuri njia zote za mle ndani.
“Nashukuru sana Patrick” aliniambia nami nikatikisa kichwa kukubali shukrani zake nikiendelea kumkokota huku mkono wangu wa kushoto ambao ndiyo niliokuwa nimemuegemeza Jérome Muganza ukiwa ameshika ile
kurunzi na mkono wangu wa kulia akiwa umeishika vema ile bunduki niliyopora kwa yule askari niliyemuua huku nikiwa tayari kufanya shambulizi lolote mbele yangu. Tulipoufikia ule mlango wa kile chumba nilipachika funguo
kwenye kitasa na kuufungua na hapo niligeuka kumtazama Jérome Muganza,
nikamuona ni kama aliyekuwa akisita kuendelea na safari.
“Vipi? nilimuuliza
“Kuna watu wanakuja” aliniambia na hapo nikayatega masikio yangu
kusikiliza vizuri, kwa mbali nilisikia mwangwi hafifu wa sauti za watu waliokuwa wakija upande wetu, nikajua kwa vyovyote wangekuwa ni wale wanajeshi wakirudi mle ndani. Nikapiga mahesabu ya haraka haraka na kuona kuwa
tusingeweza kufika mbali kabla ya watu wale hawajatufikia endapo tungeamua kutoka mle ndani kwani zile njia za pango zilikuwa nyembamba sana
na ingekuwa rahisi sana kwetu kushambuliwa. Hivyo nikafanya maamuzi ya
haraka ya kurudi mle ndani ya pango ingawaje Jérome Muganza hakuonekana
kuafikiana haraka na wazo langu.
Tulirudi ndani ya pango lile haraka sana huku nikimkokota Jérome Muganza na kwenda kumficha kule sehemu yenye giza mle pangoni. Sauti za wale
watu zilizidi kusikika na kabla hawajafika mle ndani nilikimbia haraka na
kwenda kuiburuta ile maiti ya yule mwanajeshi niliyemuua mle pangoni na
kwenda kuificha nyuma ya ile meza ya mle ndani kisha nikabanisha nikisubiri.
Zile sauti ya maongezi ya wale watu sasa ilikuwa imeongezeka ijapokuwa sikuweza kufahamu walikuwa wakizungumzia nini kutokana na lugha
yenyewe ya kinyarwanda waliyokuwa wakiizungumza ambayo mimi nilikuwa
siifahamu. Muda mfupi uliofuata niliuona ule mlango wa pango ukifunguliwa
kisha mwanajeshi mmoja mrefu mwenye mwili uliojengeka vizuri alisimama
pale mlangoni halafu akawa ni kama anayesita kuingia baada ya kushtukia
mabadiliko ya hali fulani ya mle ndani.
Toka kwenye maficho yangu mle ndani nilimchunguza vizuri mtu yule
nikamkumbuka kuwa alikuwa miongoni mwa wale wanajeshi wawili waliokuwa wakinilinda nyuma yangu kipindi kile nilipokuwa nikihojiwa na Kanali
Bosco Rutaganda.
“Vipi? mwenzake alimuuliza kwa nyuma alipomuona anasita kuingia mle
ndani
“Subiri kwanza”
“Kwani kuna nini? mwenzake aliuliza tena huku akijipenyeza pembeni yake
kutazama mle ndani.
“Wakati ulipokuwa ukitoka humu ndani ulimuacha Koplo Karazama? yule
mwanajeshi wa kwanza kuingia alimuuliza mwenzake huku akionesha mashaka.
“Ndiyo, niliwaacha yeye na yule mateka” mwenzake alijibu kwa wasiwasi
huku akikikagua vizuri kile chumba kwa taharuki.
“Sasa mbona hayupo na yule mateka mbona simuoni?, una hakika ulimuacha humu ndani wewe?
“Kwani si tuliondoka pamoja japokuwa mimi ndiye niliyefunga mlango”
“Acha upumbavu wewe sasa mbona watu wote hawapo? mwenzake alifoka
huku akiendelea kutazama mle ndani. Ukimya kidogo ukafuatia na hapo nikafahamu kuwa walikuwa wakifanya tathmini ya hali ya mle ndani huku macho
yao yakizunguka kutazama kila mahali
“Au pengine atakuwa amemhamishia kwenye kile chumba kingine”
“Labda lakini kwa sababu gani?
“Hebu nenda katazame” yule mwanajeshi mmoja alipoondoka nilimuona
yule mwanajeshi aliyebaki akinyata taratibu kuiendea ile kamba iliyokuwa ikining’inia ambayo hapo awali nilikuwa nimening’inizwa mimi kwa juu. Wakati
akielekea ilipo ile kamba yule mwanajeshi akaichomoa bastola yake kiunoni.
Alipofika pale ilipokuwa ile kamba akaanza kuchunguzachunguza, namna ya
ile kamba kuonekana imekatwa kwa juu bila shaka ilimshtua sana kwani muda
uleule yule mwanajeshi akageuka kutazama juu ya ile meza ambayo mimi
nilikuwa nimejificha kwa nyuma na ile maiti ya yule kwa majeshi mwingine,
nikajua pengine alikuwa akikikumbuka kile kisu kilichokuwa juu ya meza ile.
Mimi sikumkawiza kwani alikuwa akija kwenye uelekeo mzuri nilioutaka, nilikuwa nimejiandaa vizuri na toka pale nilipojificha nilikichukua kile kisu ambacho wakati huu nilikuwa nimekichomeka katika mkanda wa suruali yangu.
Mchezo wa shabaha ya visu ulikuwa ni mchezo niliyoupenda na kuucheza vizuri wakati wote nilipokuwa jeshini hivyo ilikuwa ni kazi rahisi sana
kwangu. Nilikishika vizuri kile kisu upande wa makali kisha nikakizungusha
mkononi mara tatu kabla ya kukifyatua hewani. Ilikuwa ni shabaha nzuri sana
kwani kile kisu kilipenya na kuzama katikati ya shingo ya yule mwanajeshi na
sehemu ya mpini tu ikabaki kwa nje. Nikamuona namna alivyoshikwa na taharuki na macho yamemtoka huku mkono wake wa kushoto ukiwa umeushika
ule mpini wa kisu ambao sasa ulikuwa umetapakaa damu kila mahali akijaribu
kukichomoa kisu kile bila mafanikio.
Alikuwa tayari ameniona hivyo ule mkono wake ulioshika bastola
akaunyanyua na kuulekezea kwangu hata hivyo hakufanikiwa kunilenga
kwani nilikuwa tayari nimekwishamfikia. Nikaupiga teke ule mkono wake
na ile bastola aliyoishika ikapaa hewani lakini kwa bahati mbaya sana ule
mtikisiko ukapelekea risasi kufyatuka na kuchimba ardhini hata hivyo niliwahi kuidaka ile bastola kabla haijafika chini. Hata hivyo nilikuwa na wasiwasi
sana kwani ule mlio wa risasi ungeweza kumshtua mtu yeyote ambaye angekuwa jirani na eneo lile na mimi sikupenda hilo litokee kwani siri yetu ya
kutoroka ingeweza kugundulika mapema. Wakati haya yakiendelea nilifahamu fika kuwa macho ya Jérome Muganza yalikuwa kule gizani yakinitazama
na sikufahamu alikuwa akiichukuliaje hali ile.
Yule mwanajeshi alianguka chini kama gunia nikamuwahi kumziba mdomo
huku nikimkandamiza chini kwa mikono yangu na hapo akafurukuta kidogo
na kutulia. Muda uleule nikamburuta na kumficha kule nyuma ya ile meza kisha nikabanisha gizani na kisikilizia. Sekunde chache baadaye yule mwenzake
alirudi na kuingia mle ndani huku akitweta kwa hofu, akaanza kuita
“Afande Nzeymana!”
Yule mtu aliendelea kuita kwa muda mrefu na alipoona kuwa haitikiwi akasimama na kuanza kutazama mle ndani na hapo niliweza kuusoma uso wake
namna ulivyokuwa umejawa na hofu na wasiwasi mwingi. Aliendelea kumuita
mwenzake kisha akaweka kituo kabla ya kuendelea “Afande Nzeymana!...”
aliendelea kuita halafu bila kusikiliza kuwa alikuwa akiitikiwa au lah! kisha
niliyaona macho yake yakitazama mle ndani sakafuni.
Niliyazungusha macho yangu kutazama pale alipokuwa akitazama nikagundua kuwa alikuwa akiitazama ile damu ya mwenzake ambaye nilikuwa nimeishamalizanaye muda mfupi uliyopita. Ile damu kutoka kwenye lile jeraha
la kile kisu la yule mwenzake ilikuwa imesambaa kidogo pale chini hivyo
nilimuona akiikamata vizuri bunduki yake mkononi huku akinyata taratibu
kuisogolea vizuri ile damu. Alipoifikia karibu ile damu akaichunguza kidogo
na kuanza kuzitupa hatua zake hafifu kuifuatilia kule ilipoelekea hata hivyo
hakufika mbali pale alipoinua macho yake na kujikuta akitazamana na mtutu
wa bastola yangu, loh! niliweza kuiona taharuki usoni mwake.
“Weka chini bunduki yako” nilimwambia huku akiwa bado haamini macho
yake na kwa msisitizo zaidi nikavuta kilimi cha bastola yangu na kuiruhusu risasi moja kukaa kwenye foleni tayari kufyatuka. Kusikia vile tu jamaa
akaiangusha chini bunduki yake bila kupenda.
“Rudi nyuma hatua tatu” nilimwambia tena na bila ubishi akafanya kama
nilivyomuagiza. Sasa nikawa nimepata nafasi ya kuiokota ile bunduki yake
na kusimama
“Kanali Bosco Rutaganda yupo wapi? nilimuuliza kwa hasira
“Amewasindikiza wageni”
“Atarudi muda gani?
“Hakutuambia” alinijibu katika sauti iliyojaa hofu na kitetemeshi
“Mko wangapi humu ndani?
“Wengi tu ila hatuonani kwani kila mmoja anashughuli yake aliyopangiwa”
“Nani aliyetoa amri ya kukamatwa kwa watu na kuja kufichwa humu pangoni?
“Sijui ila sisi huwa tunapokea amri zote toka kwa Kanali Bosco Rutaganda”
“Wale wazungu wanamahusiano gani na Kanali Bosco Rutaganda?
“Ni marafiki zake” yule mwanajeshi alinijibu hata hivyo nilipomtazama
nilimshtukia kuwa alikuwa akiichomoa bastola yake aliyokuwa ameisunda
nyuma kiunoni na sikumpa nafasi kwani muda uleule nikabonyeza kilimi cha
bastola yangu na risasi moja iliyotoka ikamzoa na kukifumua vibaya kichwa
chake alipotua chini alitulia kimya na mimi nikageuka kule gizani na kuanza
kuita.
“Jerome…Jerome…!” muda uleule nikamuona Jérome Muganza akitoka
kule mafichoni huku akiwa anashindwa kuamini mambo yaliyotokea mle
ndani. Bila shaka alikuwa amepumbazika kwa kunishangaa mimi namna
nilivyokuwa nimeyasawazisha mambo kiulaini na kwa muda mfupi. Nilimwambia Jérome Muganza amvue maiti mmoja nguo zake na azivae naye akafanya haraka kama nilivyomuagiza na wakati akivaa zile nguo mimi nilikuwa
nikizikusanya zile silaha zote mle ndani pamoja na kukichomoa kile kisu toka shingoni mwa yule mwanajeshi. Katika muda mfupi tu tukawa tupo tayari
kikitoroka chumba kile na zile silaha zote nilizibeba kwani sikuwa nafahamu
kuwa hali ya huko mbele ingekuwaje.
__________
TULITOKA NJE YA CHUMBA KILE NA KUKIFUNGA, niliutazama ule
uelekeo tuliokuja nao hapo awali na sikutaka turudi tena na njia ile kwani
tungeweza kukutana na hatari yoyote. Jérome Muganza alinionesha njia
nyingine ambayo tungeweza kuitumia ijapokuwa ilikuwa imeachwa kutumika
kwa muda mrefu kutokana na kujawa na majani mengi mle ndani, nikaafikiananaye kwani yeye ndiye aliyekuwa akivielewa vizuri vichororo vya mle
ndani.
Tuliambaa na korido fupi ya pango lile na mbele kidogo tulikutana na njia
nyingine iliyokatisha mbele yetu, tukaifuata njia hiyo kwa upande wa kushoto
huku Jérome Muganza akiwa ametangulia mbele na mimi nyuma yake. Nilimuuliza kama alikuwa akifahamu kutumia silaha akaniambia kuwa alikuwa hafahamu nikaona angekuwa mzigo kwangu kwani kwa rika lake vijana wengi
wa nchini Tanzania walikuwa wakifahamu kutumia silaha kutokana na kupitia mafunzo ya mgambo ambayo yalikuwa ni lazima kwa mfanyakazi yeyote
kuyapitia kabla ya kuajiriwa hata hivyo sikuwa na jinsi.
Tuliendelea na safari yetu taratibu na kwa tahadhari huku mara kwa mara
nikigeuka nyuma kutazama kama tulikuwa tukifuatiliwa au lah!, wakati fulani nilimsimamisha Jérome Muganza pale nilipohisi kuwa tulitapaswa kulichunguza kwa tahadhari eneo tulilokuwa tukilipita. Tulikutana na kona nyingi
sana mle pangoni lakini nilishangaa kumuona Jérome Muganza akizifahamu
vizuri kona zote mle pangoni na mwishowe tukawa tumefika sehemu fulani
kulipokuwa na jabali kubwa. Tulipofika hapo niliweza kusikia sauti ya maji
yaliyokuwa yakipita sehemu ya chini ya eneo lile.
Tulikuwa ndiyo tunalikaribia vizuri lile jabali pale nilipoona kivuli cha
mtu kikitujia mbele yetu, nikawahi kuizima ile kurunzi na kumtaka Jérome
Muganza atulie. Mpaka wakati huu tulikuwa tumechoka sana kwani zile njia
za mle pangoni kwa sehemu kubwa zilikuwa nyembamba sana zinazoruhusu
mtu mmoja tu kupenya kwa kulalia tumbo katika umbali tofauti. Nilimuona
Jérome Mugaza kama aliyekuwa ameanza kubabaika baada ya kumuona yule
mtu mbele yetu akija nikawahi kumbana kwa nguvu mkono wake kuwa atulie.
Akanisikia na kubanisha pembeni yangu ingawaje niliyasikia mapigo ya moyo
wake namna yalivyokuwa yakihangaika hovyo na hapo nikamshika kifuani na
kumtuliza. Muda huohuo yule mtu alitupita karibu bila ya kutushtukia huku
akiwa na bunduki yake begani na ndoo ya maji mkononi nikajua kuwa alikuwa
akitoka kuteka maji kule chini ya jabali.
Tuliendelea kujibaza ile sehemu mpaka yule mtu alipopotea kwenye kona
nyingine iliyokuwa nyuma yetu upande wa kulia na hapo nikampa ishara
Jérome Muganza kuwa tuendelee na safari yetu. Sasa tulikuwa tukienda kwa
tahadhari kubwa sana kwani tulifahamu kuwa tulikuwa tupo karibu sana na makazi ya askari wa Kanali Bosco Rutaganda. Na wakati tukiendelea na safari
mimi bado akili yangu ilikuwa ikiwaza kule nyuma tulipotoka kuwa ungepita
muda gani mpaka kushtukiwa kutoroka kwetu, na Kanali Bosco Rutaganda
angetaharuki vipi pale ambapo angeambiwa kuwa mateka wake wametoroka.
Nilifahamu fika kuwa Kanali Bosco Rutaganda asingekubali kushindwa kirahisi hivyo kwa vyovyote angewapanga wanajeshi wake katika kila
kona ya mapango haya akihakikisha kuwa hatufanikiwi kutoroka na tunakamatwa mapema na kurudishwa tena kwenye himaya yake. Hata hivyo hilo
nisingekubaliana nalo asilani kwani nilifahamu kuwa endapo tungekamatwa
tena adhabu yetu ingekuwa kifo na kuliko kuuwawa kinyama na Kanali Bosco Rutaganda ingekuwa ni afadhali nijiue mimi mwenyewe lakini pia kabla
ya kufikia hatua hiyo ningemuonesha Kanali Bosco Rutaganda kuwa mimi si
mwanafunzi bali bado nilikuwa mwalimu wake wa kijeshi tena niliyehitimu
vizuri katika medani za kijasusi, iwe porini au mjini, mapangoni au jangwani.
Kila mara Jérome Muganza alikuwa akigeuka nyuma kunitazama bila ya
kusema neno ingawaje tulikuwa hatuonani vizuri kutokana na giza zito la
mle pangoni. Zile kelele za maporomoko hafifu ya maji nilikuwa nikiendelea kuzisikia ingawaje bado sikuweza kujua kuwa yale maji yalikuwa eneo
gani katika ile sehemu. Tulifika mbele eneo fulani tukaingia katika uchochoro
mwembamba wenye mwamba wa chokaa, tukawa tukipita kiubavu ubavu na
pale tulipoona panatatiza niliwasha kurunzi kidogo kumulika na kisha kuizima
na safari ikaendelea, sikutaka kuitumia sana ile kurunzi japokuwa mle ndani
kulikuwa na giza zito.
Tulipoupita ule mwamba wa chokaa tukawa tumetokezea eneo lililokuwa na
makutano ya njia tatu za pango, njia moja upande wa kushoto ya pili upande
wa kulia na ya tatu mbele yetu. Tulipofika pale nilimuona Jérome Muganza
akisita kidogo na hapo nikajua kuwa kwa vyovyote alikuwa akijaribu kuzikumbuka vizuri njia zile nami sikutaka kumuingilia kwenye maamuzi yake
hivyo nikamuacha aitulize vizuri akili yake na kufikiri vizuri ili aweze kuichagua njia iliyo sahihi. Baada ya muda mfupi akawa amekumbuka vizuri,
nikamuonna tena akigeuka kunitazama, safari hii alinitazama kwa muda kidogo kisha akaanza kuifuata ile njia ya upande wa kulia nami ikabidi nimfuate
kwa nyuma ingawaje nilianza kupatwa na wasiwasi juu ya namna Jérome
Muganza alivyokuwa akigeukageuka nyuma kunitazama.
Tulitembea kidogo kwa kuinamainama na baada ya kitambo kirefu cha safari yetu tukatokezea kwenye njia pana zaidi lakini iliyokuwa na vipango vingi
vidogovidogo vyenye ncha kali lakini hatukupata shida sana kutokana na zile
buti ngumu za kijeshi tulizovaa miguuni. Tulipofika mbele kidogo tukatokezea
kwenye uchochoro mwingine mwembamba ulituhitaji kupita katika mtindo wa
kulala chini na kutambaa. Uchochoro huo ulikuwa unaelekea sehemu ya chini
zaidi ya mapango yale na kwa mbali niliweza kuyasikia tena yale makelele ya
maji yaliyokuwa yakitiririka sehemu fulani katika eneo lile.
Lakini kabla ya kuanza safari katika kichochoro kile nilimuona Jérome
Muganza akigeuka tena nyuma kunitazama kama alivyokuwa akifanya kule
nyuma. Kwa kweli nilishindwa kumuelewa kuwa alikuwa akimaanisha nini kufanya vile wakati mle ndani kulikuwa giza zito na tulikuwa hatuonani hata
hivyo nilipiga moyo konde na kumpuuza huku tukiendelea na safari yetu. Tulishuka chini ya mapango yale kwa namna ileile ya kutambaa kisha tukapinda kona kushoto na hapo tukawa tumetokezea eneo kama lile lakini kwenye
pango jingine lililokuwa chini lakini fupi sana lisilomruhusu mtu kupita akiwa
anatembea na yenye matope mazito. Tuliserereka na kuingia kwenye lile tope
na kuzama nusu ya kiwiliwili na hapo niliyasikia vizuri yale makelele ya maji
kuwa yalikuwa karibu sana na pale tulipokuwa.
Na kwa mara ya kwanza nilimsikia Jérome Muganza akiniambia kuwa eneo
lile lilikuwa na popo wakubwa na wakali mno wajulikanao kwa lugha ya kitaalamu kama hysignathus Monstrosus hivyo alinitaka niwe makini sana nami
nikatingisha kichwa kumuonesha kuwa nilikuwa nimemuelewa na hapo akageuka kunitazama tena kisha akageuka mbele na hapo tukaanza tena kuendelea na safari yetu. Nilikuwa nimemwambia Jérome Muganza kuwa tulitakiwa
kurudi kwanza kule pangoni walipofungwa wenzetu ili tukawaokoe halafu
baada ya hapo ndiyo tungetoroka kwa pamoja. Hivyo kwa mujibu wa maelezo
yake njia ile ndiyo iliyokuwa njia rahisi na ya kificho ya kuweza kutufikisha
kule pangoni walipofungwa wenzetu.
Ile sehemu ya chini ya pango tulikotokezea ilikuwa na matope mazito
yenye utelezi mkali ya udongo mfinyanzi na ilikuwa ni shida sana kutembea hivyo mwendo wetu ulikuwa umepungua sana na kama ingetokea kuwa
Jérome Muganza angeniacha pale angekuwa ameniweza sana kwani nilikuwa
nimeshapoteza ramani yote ya kule tulipotoka na sikuwa na ramani ya kule
tunapokwenda na pale tulipokuwa sikufahamu tulikuwa eneo gani japokuwa
Jérome Muganza alikuwa ameniambia kuwa tulikuwa tumeukaribia mrefeji mkubwa wa maji uliokuwa mle pangoni. Na kwa mujibu wa maelezo ya
Jérome Muganza ni kuwa kwa kuutumia mfereji huo ndiyo ambao ungetusafirisha moja kwa moja hadi karibu na lile pango walikofungwa wale wenzetu huku akidai kuwa mfereji huo ulikuwa ni miongoni mwa mifereji mingi
inayotoka kwenye chemi chemi za mapango haya kuelekea bonde la ufa la
Albertine.
Sikuwa na saa yangu ya mkononi lakini niliweza kukisia kuwa tulikuwa
tumetembea katika lile tope zito katika muda usiopungua nusu saa na wakati
huo miguu na viungo vyote mwilini vilikuwa vimeanza kuchoka kutokana na
kutumia nguvu nyingi katika kutembea katika matope yale mazito. Kona moja
tu ilikuwa imesalia mbele yetu kabla ya kuufikia ule mfereji mkubwa wa maji
pale nilipomuona Jérome Muganza mbele yangu akisita kuendelea na safari na
mara hii hakugeuka tena kunitazama kama alivyokuwa akifanya kule nyuma
isipokuwa nilimuona akisimama kwa ghafla sana huku akiangalia kule mbele.
Nikashikwa na wasiwasi na kumuuliza
“Mbona umesimama, kuna nini?
“Kuna kitu fulani pale mbele” alinong’ona na hapo nikasogea vizuri kutazama kule mbele hata hivyo sikuona chochote.
“Mbona sioni kitu”
“Tazama vizuri pale mbele upande wa kushoto” aliniambia kwa sauti ya kunong’ona na hapo nikayakaza vizuri macho yangu kutazama kwa makini
kule mbele hata hivyo bado sikuona chochote.
“Sioni chochote” nilimwambia Jérome Muganza huku nikigeuka kumtazama hata hivyo Jérome Muganza hakunijibu kitu badala yake aliendelea kusimama huku akitazama kule mbele katika namna ya hofu na wasiwasi. Nilipomchunguza vizuri nikajua kuwa alikuwa ameanza kutetemeka kwa hofu na
hapo nikaanza kushikwa na wasiwasi. Niliacha kumtazama Jérome Muganza
nikageuka tena kutazama kule mbele alipokuwa akitazama na mara hii niliweza kuona alichokuwa akikitazama.
Kiasi cha umbali mfupi tu toka pale tulipokuwa mbele yetu, kiumbe kikubwa cha ajabu chenye upana unaofanana na ule wa gogo la mti kubwa lenye
urefu usiojulikana kilikuwa kimegeuka kututazama au pengine kutushangaa
kama sisi tulivyokuwa tukikishangaa. Tofauti iliyokuwepo baina yetu na kiumbe kile ni kuwa sisi tulikuwa hatujiwezi kwa hofu wakati chenyewe ni
kama kilikuwa kikitabasamu lakini vilevile kikijuliza kama tulikuwa tumekosea njia au tulikuwa tumedhamiria kupita pale alipokuwepo. Na hapo nikafahamu nini kwani Jérome Muganza alikuwa akitetemeka vile.
Lilikuwa joka kubwa sana ambalo sikupata kuwahi kuliona sehemu yoyote duniani wala kwenye picha yoyote. Katika muda wa sekunde moja tu
tangu nilione joka lile mbele yetu nilihisi damu yangu ilikuwa ikichemka
isivyokawaida mwilini, jasho nalo lilikuwa limeanza kunitoka kila sehemu
mwilini ingawaje mle ndani ya pango kulikuwa na baridi kali. Mate yalikuwa
yakinikauka haraka mdomoni na ni kama mapigo elfu moja ya moyo wangu
yaliyokuwa yamesafiri katika nukta moja tu ya sekunde.
Lile joka lilikuwa limetuona na lilikuwa likijizungusha taratibu kututazama vizuri, sikuweza kuliona vizuri lakini ukubwa wa kichwa chake ulikuwa
ukifanana na ukubwa wa kichwa cha simba dume na kichwa chake kilikuwa chenye umbo bapa na chenye mifupa imara ya taya lake. Nilikuwa nikiwafahamu vizuri nyoka wengi jamii ya chatu kwani niliwahi kukutana nao
maporini katika harakati zangu lakini nilikataa kulifananisha joka lile na chatu
kutokana na umbo la kichwa chake lilivyokuwa kama jeneza, rangi ya ngozi,
umbo na macho yake.
Nyoka wote wasiokuwa na sumu nilikuwa nikiwafahamu vizuri kwa tabia
moja tu kubwa, macho yao yalikuwa na kiini chenye umbo la uviringo katikati
na wenye tabia ya kulizuia na kulirukia windo lao kwa kulibana mpaka pale
linapoishiwa pumzi ndiyo huanza kulimeza taratibu, lakini joka hili halikuwa
na tabia za awali zilizokuwa zikifanana na hizo. Nililitazama joka lile nikayaona macho yake makubwa na makali yalivyokuwa yakimeremeta katika namna
ya ajabu na hapo nikagundua kuwa lilikuwa ni aina ya joka lenye sumu kali
sana kwani macho yake hayakuwa na kiini chenye umbo la uviringo kama
wale nyoka wengine wasio na sumu bali macho yake katikati yalikuwa na kiini
chenye umbo linalofanana na ile alama ya kisu iliyopo kwenye karata.
Matundu ya pua yake yalikuwa makubwa kama matundu ya pua ya binadamu na sehemu ya mbele ya mdomo wake ilikuwa pana na iliyogawanyika
katika mafungu ya sehemu kuu nne. Rangi ya ngozi yake ilikuwa na mabakamabaka kama ya kombati ya jeshi na rangi hiyo ilikuwa na mstari mpana
wa rangi ya njano uliyoizunguka shingo yake kama ushanga. Sehemu ya kiwiliwili chake ilikuwa imebakia kwenye upande mwingine wa pango. Sasa joka
lile kubwa la ajabu linalotisha lilikuwa likijisogeza taratibu kututuzama huku
likifoka na kutoatoa nje ulimi wake mkubwa na mrefu uliotengeneza pacha
sehemu yake ya mbele.
Sikutaka kugeuka nyuma kwani nilifahamu fika kuwa kwa kufanya hivyo
kungeweza kulishawishi lile joka lifanye maamuzi ya haraka ya kutushambulia hivyo niliyazungusha macho yangu taratibu na kumtazama Jérome Muganza aliyekuwa pembeni yangu na hapo nikamuona kuwa alikuwa amefikia
kwenye kiwango chake cha mwisho cha hofu. Roho yake ni kama ilikuwa
tayari imekwishajitenga na mwili na hivyo alikuwa tayari chochote kitokee
kwani hakuwa na tumaini jengine la kutoka na ushindi mbele ya joka lile
lililoonekana kutokuwa na mazoea hata kidogo na binadamu.
Kwa sekunde chache ni kama akili yangu ilikuwa imepigwa na ugonjwa wa
kiharusi na kushidwa kufanya kazi yake kwa usahihi. Niliona ni kheri ningepambana na Kanali Bosco Rutaganda ambaye ni binadamu kama mimi kuliko
kupambana na kiumbe kile. Nilikatishwa tamaa na mambo makubwa mawili
katika kutaka kupata ushindi kwa joka lile. Kwanza, tulikuwa tupo katikati ya
tope zito mno na linaloteleza hivyo kwa vyovyote isingekuwa rahisi kwetu
kukimbia. Pili, nilifahamu kuwa lile lilikuwa joka mkubwa tena lenye sumu
kali hivyo endapo tungelipa mwanya wa pigo moja tu la kutuuma na kutukamulia sumu yake tusingefika mbali na sumu yake kali ingetukausha haraka
na hicho ndicho kilichonikatisha tamaa.
Lile joka sasa lilikuwa limetulia likitutazama kama linalotuvizia tujitikise tu
ili tuzijutie nafsi zetu. Nikazikumbuka zile bunduki nilizozichukua kule pangoni tulipotoroka kuwa bado nilikuwanazo mwilini hata hivyo kwa wakati huu
nilifahamu kuwa zisingetufaa kitu kwani toka kuzichukua hadi kujiweka sawa
lile joka lingekuwa tayari limekwishatushambulia.
Niliacha kumtazama Jérome Muganza ambaye alikuwa ameganda kama
sanamu pembeni yangu nikayapeleka macho yangu kulitazama tena lile joka
huku akili yangu ikionekana kuzidiwa uwezo wa kufanya kazi. Nilipoendelea kulitazama vizuri lile joka nikagundua kuwa lilikuwa likijiandaa taratibu
kutushambulia hivyo nikajua tusingekuwa na muda mrefu wa kuendelea kujishauri nini cha kufanya. Nikaikamata vizuri ile kurunzi niliyoichukua kule
pangoni huku mkono wangu mwingine nikiuzungusha taratibu kiunoni mwangu kukichukuwa kile kisu na wakati huo wote macho yangu hayakuhama kwa
lile joka.
Niliweza kuyasikia mapigo ya moyo wangu namna yalivyokuwa yakihangaika ovyo hata hivyo niliyapuuza. Lile joka sasa lilikuwa likijigeuza taratibu kunitazama na hapo nikajua kuwa lilikuwa limenishtukia nilichokuwa
nikikifanya, mara nikaanza kuliona likijiandaa kufanya shambulizi makini la
kushtukiza. Sasa nilifahamu kuwa nilipaswa kufanya maamuzi makini na ya
haraka bila ya kuchelewa zaidi vinginevyo lingeniwahi na kunifanya kafara.
Lile joka sasa nililiona kuwa lilikuwa tayari kunishambulia ikabidi niwahi kulipotezea shabaha yake hivyo haraka nikaiwasha ile kurunzi na hapo mwanga mkali ukaangaza kisha nikamulika upande mwingine wa lile pango na hapo
lile joka likageuka haraka sana kuutazama ule mwanga kule ulipomulika.
Jaribio langu la kwanza likawa limefaulu vizuri na hapo nikajikuta nikimsifu
Mungu kwa kunipa binadamu akili nyingi kuliko viumbe vingine wote, lakini
kwa namna nyingine mambo yaliharibika.
Lile eneo lilikuwa na popo wakubwa wenye mbwawa pana kama Mwewe.
Popo hao wengi kumbe walikuwa wamening’inia juu ya paa la pango lile
hivyo ule mwanga wa kurunzi ukawa umewaharibia starehe yao na kuwafanya
wachanguke kila mahali na kuanza kuzungukazunguka hovyo mle ndani huku
wakitoa sauti mbaya zinayoumiza masikio.
Nilimuona Jérome Muganza akiwahi kujilaza chini na kujifunika kichwa
chake kwa mikono ili wale popo wasimuume hata hivyo mimi sikushughulika
nao sana kwani macho yangu bado yalikuwa kwa lile joka. Wale popo walikuja na kuanza kunipiga usoni na kichwani kwa mbwawa zao ngumu kama
waliokuwa wakinitaka niizime ile kurunzi, nikawaputa kwa mkono wangu lakini wakati huohuo nikiendelea kulitazama vizuri lile joka mbele yangu ambalo wakati huu lilionekana kutusahau kwa muda likibabaishwa na ule mwanga
kurunzi ukutani, wale popo na makelele yao.
Niliuhamisha ule mwanga wa kurunzi na kumulika sehemu nyingine ili lile
joka ligeuke tena kuutazama ule mwanga na wakati huo niweze kuliona vizuri.
Lile joka likafanya kama nilivyotaka, likageuka na kuutazama ule mwanga na
hapo nikakibana vizuri kile kisu changu mkononi na kuanza kukizungusha na
kilipokoleavizuri nikakifyatua na kukirusha usawa wa kichwa cha lile joka.
Ilikuwa ni shabaha nzuri sana kwani kile kisu kilipenya vizuri katikati ya jicho
lake la upande wa kulia na kuiacha sehemu ya mpini tu kubaki kwa nje.
Muda uleule lile joka likaanza kuyumbayumba likijipigizapigiza kichwa
chake ukutani huku likitoa sauti kali na mbaya ambayo iliniogopesha sana
kiasi kwamba hata wale popo walihofia usalama wao wakatoka mle pangoni
na kukimbia. Lile joka liliendelea kujipigiza pigiza ukutani kwa hasira huku
likijinyonganyonga hivyo likawa linapasua kuta za lile pango kama mchezo.
Vumbi kali likatimka mle ndani na baadhi ya udongo ukawa ukiporomoka
toka juu ya lile pango. Nikaanza kuhisi kuwa mwangwi wa sauti kali ya lile
joka ulikuwa ukisafiri na kupenya katika kila kona ya mapango yale.
Wakati likiendelea kujipigiza na kujinyonganyonga ndiyo nikakiona kile
kiwiliwili chake kwa sehemu tu, urefu wa kiwiliwili chake ulikuwa sawa na
urefu wa mti mrefu wa mnazi. Mkia wake ulikuwa una nguvu sana, ulinipiga
nikaukwepa hivyo ukaenda kupasua sehemu ya ukuta wa pango lile hata hivyo
upepo wake tu ulifanikiwa kuniyumbisha. Ile sehemu ya ukuta wa pango iliyovunjika chini yake ndiyo kulikuwa na ule mfereji mkubwa wa maji tuliokuwa tukiufuata hivyo lile joka likawa limeturahisishia kazi. Sikuona sababu ya
kuendelea kupambana tena na lile joka kubwa lenye hasira kwani nilifahamu
hatari ambayo ingenikabili hasa ukichukulia kuwa nilikuwa tayari nimelijeruhi jicho moja. Nililicha liendelee kujipigizapigiza hovyo kisha nikamshika
Jérome Muganza mkono na kuanza kumvuta kuwa tuondoke. Jérome Muganza hakuweza hata kuongea kwani hofu ilikuwa bado imemshika na alikuwaakiyaona mambo yote yaliyokuwa yakitokea mle pangoni ni
kama ilivyokuwa sinema ya kutengeneza.
Tulisota juu ya tope lile mpaka tukafika ukingoni kwenye ule ukuta wa pango uliovunjika ambako chini yake kulikuwa na ule mrefeji wa maji na hapo
nikamshika mkono Jérome Muganza na kijirusha naye kwenye ule mfereji.
Ulikuwa ni mfereji mkubwa kiasi na wenye maji baridi sana. Nilimuuliza
Jérome Muganza kama alikuwa fundi wa kuogelea akaniambia kuwa nisiwe
na wasiwasi huku akiwa bado haamini macho yake.
Safari nyingine ikaanza tena yeye akitangulia mbele na mimi nikimfuata
kwa nyuma huku silaha zangu nikizinyanyua juu kwa mkono mmoja ili zisiloane kwenye yale maji wakati tukiogelea. Tukaanza kuogelea taratibu kuufuata uelekeo wa ule mfereji. Yale maji ya ule mfereji yalikuwa ya baridi mno
na yalikuwa yakiendelea kutusafisha yale matope yaliyokuwa yametuganda
mwilini. Kwa kweli hata mimi nilikuwa siamini kuwa tulikuwa tumeponyoka
toka katika domo la lile joka kali na la kutisha tena muda mfupi tu uliyopita.
__________
TULIENDELEA KUOGELEA TARATIBU NA KWA UTULIVU huku
tukiwa tumeongozana kuufuata uelekeo wa ule mfereji. Ile kurunzi nilikuwa
nimeizima na kuishikilia mkononi na macho yangu yote yalikuwa kwa Jérome
Muganza nikizifuatilia kwa ukaribu nyendo zake. Nilimshangaa sana Jérome
Muganza kuwa alikuwa ni mwogeleaji stadi mno akiyakata maji kama samaki,
ule mfereji ulitusafirisha na tukawa tukikunja kona moja na kuingia nyingine.
Nilikuwa nikizihesabu vizuri zile kona na hadi wakati huu tulikuwa tumeziacha kona nane nyuma yetu na bado tulikuwa tukiendelea kuogelea katikati ya
giza zito.
Tulifika sehemu moja kwenye kona fulani ambako ule mfereji ulikuwa
umekunja kona kuelekea sehemu ya chini zaidi ya pango lile. Tukaogelea na
kwenda kusimama kwenye ile kona sehemu iliyokuwa na mchanga mwepesi
na laini kama wa ufukweni na safari yetu ikaishia hapo.
Tulitoka mle mferejini na kuketi kwenye ufukwe ule mdogo uliojaa mchanga
huku kila mmoja akionekana kuzama katika fikra zake. Nilimtazama Jérome
Muganza na kumuona kuwa alikuwa bado akitweta kwa hofu na hakuna aliyemsemesha mwenzake ingawaje niligundua kuwa Jérome Muganza alikuwa
akinitazama kwa jicho la wiziwizi tukio ambalo liliendelea kunipa wasiwasi.
Wakati Jérome Muganza akipumzika mimi nilikuwa nikizikagua vizuri zile
silaha nilizoziiba kwa wale askari wa Kanali Bosco Rutaganda na kuziweka
sawa kukabiliana na chochote ambacho kingetokea mbele ya safari yetu. Nilipomaliza kuziweka vizuri zile silaha nilijilaza pale mchangani kuupa mwili na
akili yangu utulivu kidogo na hapo nikajihisi ni kama niliyeutua mzigo mzito
mno ulikuwa ukinielemea kwa kipindi kirefu mwilini kwani nilikuwa sijapata
nafasi ya kupumzika tangu nilipotekwa na kuletwa mle pangoni hata hivyo
yale maumivu ya majeraha mwilini nilikuwa bado nikiyasikia.
Nikiwa bado nimelala pale mchangani huku nikitazama sehemu ya juu ya pango lile niligundua kuwa Jérome Muganza alikuwa amegeuka kwa siri
kunitazama tena na alikuwa akinipiga jicho la wizi taratibu katika mtazamo
usioeleweka kana kwamba mimi nilikuwa kiumbe cha ajabu mbele yake. Kwa
kweli moyo wangu ulianza kushikwa na wasiwasi sana juu ya tabia yake ile
na sikufahamu ni kwanini alikuwa akinitazama namna ile kila mara, vilevile
sikufahamu alikuwa akiniwazia nini kichwani.
Nilianza kuhisi kama kengele ya tahadhari ilikuwa ikianza kugonga
kichwani mwangu ikinitahadharisha kuwa niwe makini na mtu ninayeongozana naye hata hivyo nilijikuta nikiyapuuza mawazo yangu kwani sikuona
dalili yoyote ya hatari kwa wakati ule. Sikutana Jérome Muganza aendelee
kunitazama vile hivyo niligeuka na kumuuliza
“Bado tupo mbali sana na lile pango? nilimuuliza na hapo akaacha kunitazama na kutazama pembeni.
“Siyo mbali sana kutoka hapa” alinijibu kivivuvivu huku akiendelea kutazama pembeni.
“Inaweza ikatuchukua muda gani?
“Muda wa kama dakika kumi na tano unaweza kututosha” Jérome Muganza
aliniambia na nilipogeuka vizuri kumtazama nikamuona ni kama aliyekuwa
amezama katika fikra fulani hali iliyompeleka mawazo yake yasiwe pale.
“Vipi kuhusu gazeti lako?, utaendelea na kazi yako endapo tutafanikiwa kutoka humu pangoni salama?
“Kwa sasa siwezi kufahamu kwani bado hatujatoka”
“Gazeti lako bado ni muhimu sana katika kuieleza dunia juu ya unyama
unaofanyika humu ndani” nilimchombeza kidogo Jérome Muganza huku uso
wangu ukiumba tabasamu hafifu na hapo nikamuona akigeuka kunitazama
hata hivyo nilishangazwa kidogo na uso wake kwani haukuonesha tashwishwi
yoyote. Baadaye nilimuona akitabasamu kidogo kabla ya tabasamu lake kufifia taratibu na hatimaye kukoma.
__________
NILIHISI KUWA TULIKUWA TUMEPUMZIKA kwa muda wa kutosha
pale ufukweni kiasi cha kuipa utulivu wa kiasi miili na akili zetu hivyo toka
pale nilipolala nilisimama taratibu na hapo nikajihisi kama niliyekuwa nimepata nguvu mpya.
“Simama twende hatuna muda zaidi wa kuendelea kukaa hapa” nilimwambia Jérome Muganza huku nikimtazama usoni na hapo nilimuona ni kama
anayesita kuendelea na safari lakini hatimaye alisimama kivivuvivu na hapo
safari yetu ilianza tena. Kama ilivyokuwa kawaida yetu Jérome Muganza alitangulia mbele kwa kuwa yeye ndiye aliyekuwa akizifahamu vizuri njia za
mapango yale.
Wakati tukiondoka eneo lile nyuma yetu nilikuwa nikiyasikia yale makelele
ya maji yaliyokuwa yakisafiri mferejini. Tuliingia kwenye uchochoro
mwingine wa pango lile ambao ulikuwa mwembamba na mfupi kwa kwenda
juu hivyo tukawa tunatembea kwa kuinama inama. Nilipotaka kuwasha ile
kurunzi Jérome Muganza alinitahadharisha kuwa nisiiwashe kwani eneo lile lilikuwa na popo wengi ambao wangeweza kutushambulia endapo wangeuona
mwanga wa ile kurunzi, hivyo tuliendelea kutembea gizani. Kiasi cha umbali
wa mita kama thelathini mbele yetu tulifika katika eneo lilioonekana kama njia
panda yenye makutano ya vichochoro vinne.
Tulipofika pale Jérome Muganza alisita kidogo na hapo nikajua kuwa alikuwa akijaribu kuyakumbuka vizuri mazingira yale. Baada ya muda mfupi
nilimuona Jérome Muganza ikipinda kona kuingia uchochoro wa upande wa
kulia nami nikamfuata kwa nyuma. Tukawa tumeingia kwenye uchochoro
mwingine ulioonekana kama uliokuwa ukiturudisha kule tulipokuwa tukitoka
lakini tulipofika mbele kidogo tulichepuka na kuingia upande wa kushoto. Ulikuwa ni uchochoro mwembamba sana uliofanana na tundu dogo linaloelekea
mgodini hivyo tulijongea kwa kulalia tumbo.
Ulikuwa ni uchochoro wenye joto kali hivyo nilihisi zile gwanda za jeshi
nilizozivaa zilikuwa mbioni kulowana kwa jasho. Tulipovuka uchochoro ule
tukatokezea kwenye pango jingine lililokuwa likielekea sehemu ya chini zaidi.
Lilikuwa ni pango lililokuwa linafanana na lile pango tulilokutana na lile joka
hatari hivyo nilihisi damu yangu ikianza kuchemka taratibu kwenye pango
lile. Wakati tukishuka kule chini ile hali ya joto ilikuwa ikipungua taratibu na
sehemu yake kuchukuliwa na baridi kali, Jérome Muganza akaniambia kuwa
tulikuwa tumelikaribia lile pango walilofungwa wenzetu.
Sasa tulikuwa tukitembea kwa tahadhari sana katikati ya pango lile lenye
giza kote. Tukawa tunatembea kwa kupapasapapasa. Sehemu ya chini ya pango lile kulikuwa na mawe yaliyochongoka sana hata hivyo kwa kuwa tulikuwa
tumevaa zile buti za kijeshi hatukuweza kupata adha yoyote. Tulitembea kwa
tahadhari sana na wakati huu niliyasikia tena yale makelele ya maji, nikajua
kuwa hatukuwa mbali sana ule mfereji. Tulifika sehemu fulani katikati ya lile
pango kulikokuwa na uchochoro na hapo tukaanza kupanda juu kwa kushikilia
mawe yaliyochongoka yaliyokuwa pembeni ya kuta za uchororo ule.