WAKALA WA SIRI Episode 07
Mtunzi; Robert Heriel
WhatsApp 0693322300
EPISODE 07
ILIPOISHIA...
“ Wakanipiga sana kabla, kisha baadae wakanitwanga risasi ya Bega, hapo nikadhani nimekufa kwani sikujua kilichotokea, kumbe nilikuwa nimepoteza tuu fahamu, na hayo yote Mzee Mpole aliniambia kuwa alinikuta Ufukweni nimetelekezwa nikiwa nimepoteza fahamu huku jeraha la risasi likitoa damu. Hivyo ndivyo ilivyokuwa ndugu yangu” Fernanda akamaliza kusimulia kisa cha uongo chenye hitimisho lenye ukweli, basi huyo Belinda alikuwa akitoa machozi wakati akisimuliwa, akamkumbatia na wote wakafarijiana, wote walikuwa wameichoka siku ile, hawakuta iendelee hivyo usingizi ukawachukua, wakalala.
ENDELEA
Usiku ulizidi kunawiri kadiri masaa yalivyokuwa yanaenda, yapata saa nane giza likiwa linanguvu usoni pa nchi, hakuna aliyekuwa macho, kila mmoja alikuwa katika ndoto yake, hali ya mawingu ilizidi kuongeza sehemu ya giza katika usiku ule, usiku wenye kutisha huwa na vibweka, haukuwa usiku mzuri kwa Fernanda, alikuwa akihangaika kwa kujigeuza upande huu na upande huu kama mtu mwenye kuota ndoto mbaya, labda ni jeraha lake lilikuwa likimsumbua, baridi iliyokuwa ikiingia ikamfanya Fernanda aamke, maumivu kwenye bega lake la kulia ya lile jeraha la risasi aliyopigwa yalikuwa yakimsumbua, akaamka; bado Belinda alikuwa amelala, Fernanda akaamka na kuketi kitandani, kisha akajifunga kanga akatoka kwani alikuwa amebanwa na haja ndogo pia; akiwa amefika sebuleni alishtushwa na minong’ono iliyokuwa kwa nje kwenye dirisha la sebule, zilikuwa sauti za wanaume wawili waliokuwa wakizungumza kwa sauti ya chini kabisa, Akajongea polepole mpaka lilipokuwa dirisha, akafungua pazia kwa tahadhari. Alipigwa na butwaa alipomuona Mzee Mpole akiwa na wanaume wawili wenye miili mikakamavu; Fernanda akajua ni wale watu wanaomtafuta Sajenti; akawasikia wakisema;
“ Lakini mzee mwanzangu nawe unamakosa bhana! Unawezaje kupokea mtu aliyejeruhiwa kwa bastola ukamuweka ndani kwako, huoni hilo ni kosa” Mzee Mchonga akasema, lakini akakatishwa na mwanaume mmoja aliyekuja naye,
“ Hatutaki kukudhuru, ndio maana tumekuja na Mzee Mchonga hapa, ndiye aliyetuonyesha kwako, gari yao waliiacha kwenye Gereji yake, kama sio ile gari wala tusingejua kwa urahisi alikimbia huku kigamboni, samahani kwa usumbufu, amelala chumba kipi?” Yule mwanaume akasema, akiwa anamuambia Mzee Mpole.
“ Sawa nimewaelewa, kwa hiyo mnataka nifanyaje?” Mzee Mpole akasema, Fernanda aliposikia hivyo akasonya; “ Huyu mze ni mnafiki sana, kumbe katusaliti” Fernanda akawaza huku akisonga upesiupesi kuufuata mlango wa chumba cha Sajenti, taa zote zilikuwa zimezimwa hivyo kulikuwa na giza ingawaje taa za nje nuru yake ilifanya mule ndani kuwa na nuru angalau, Fernanda akamuamsha Sajenti, kisha wakatoka sajenti akiwa anafunga vifungo vya shati lake, bastola ikiwa kiunoni, walinyata mpaka sebuleni na kulifikia lile dirisha alipokuwa amesimama Fernanda hapo kabla, lakini walipochungua nje hawakuona mtu; Sajenti akamuambia Fernanda “ Labda ulikuwa kwenye ndoto” Lakini Fernanda akasisitiza kuwa yeye hakuwa anaota, mambo hayo yote waliyafanya kimya kimya bila kuharibu utulivu wa eneo lile.
Sajenti akiwa dirishani bado wanajibishana, akashtuka kuona kitu kama kivuli kwa nje kikipita kule ilipo miti ya mihogo, hapo akamtuliza Fernanda, akaangalia nje akiwa anachungulia kwenye pazia la lile dirisha lakini hakuona kitu, hata hivyo asingejiongopea kuwa macho yake hayakuona kitu, wakati akiwa anatafakari ghafla upande wa chini kabisa akaona wanaume wawili wenye silaha wakiwa wamejificha, kufikia hapo Sajenti akajua kuwa watu wabaya wamewafikia,
“ Tuondoke sasa hivi” Sajenti akasema huku akimshika mkono Fernanda akimvuta, mkono mwingine ukiitoa bastola yake mafichoni na kuikamata vizuri,
“ Sasa tunaenda wapi, mlango wakutokea ni huu tuu” Fernanda akasema, angalia akisema ghafla mlango ukafunguliwa na bila akili yao kujua chakufanya punde akatokea Mzee Mpole akifuatiwa na wanaume wawili wakiwa na silaha, Sajenti hakutaka kupoteza muda akawapiga wale wanaume risasi wakaanguka chini, Mzee Mpole akabaki amesimama kwa hofu akitetemeka,
“ Nisameheni! Tafadhalini msiniue! Sikuwa na namna!” Mzee mpole akawa anajitetea, lakini kabla hajamaliza wanaume wengine wawili walitokea, kitendo cha wanaume wale kuona wenzao wamekufa wakajificha na milio ya risasi ikarindima, vita imeanza. Mzee Mpole akapigwa risasi ya ubavu akaanguka chini, Sajenti na Fernanda walijua nini chakufanya kwenye mazingira kama hayo, kama mtu mmoja waliruka sarakasi na kujiviringa kama Gunzi la mhindi na kujificha huku wakijibu mapigo, Fernanda alikuwa amechukua Bastola ya moja ya wale wanaume wa mwanzoni waliouawa na Sajenti, milio ya risasi iliwaita wale majahili wengine waliokuwa wapo mbali, risasi zilirindima mpaka Mke wa Mzee Mpole na Belinda wakaamka, baada ya majibizano ya risasi kwa zaidi ya nusu saa, wale wanaume waliuawa na kutoa upenyo wa Sajenti na Fernanda kuwakimbia. Walipotelea kwenye miti ya mihogo na kutokomea kwenye giza wakiacha nyumba ya Mzee Mpole ikiwa imevamiwa na shetani mwenye kiu ya damu.
“ No! No! Hapana! Turudi!” Fernanda akasema, akiwa amesimama huku akitaka kurudi,
“ Unawazimu!” Sajenti akasema,
“ Kuna kitu muhimu nimesahau, ingekuwa bora ningekufa kuliko kukiacha kitu hicho”
“ Kitu gani hicho” Sajenti akasema, akiwa amemkatisha Fernanda
“ Simu!” Fernanda akajibu,
“ Simu gani nawe, embu twende, simu tutanunua mbele kwa mbele” Sajenti akasema,
‘ Utainunua simu ya Meja Venance?”
“ Umesemaje Fernanda?”
“ Nimeiacha simu ya Meja Venance” Fernanda akasema, na wote wakaanza kupiga hatua kurudi, hawakuchukua muda kwani hawakuwa wamefika mbali,
“ Wewe baki hapa, mimi ngoja nikaichukue, uliiweka wapi” Sajenti akasema,
“ Hapana, twende wote tuu, ni hatari wewe kwenda mwenyewe”
“ Embu nisikilize ninachokuambia” Sajenti akasema kwa sauti ya hasira,
“ Unaijua hata hiyo simu ilivyo, acha ubishi Otieno” Basi wakaenda wote, walipofika eneo bado lilikuwa kimya lenye kutisha, miili mitatu ilikuwa ipo nje kabisa ya nyumba, miwili ilikuwa mlangoni, wakafika mlangoni ghafla wakasikia sauti ya mwanaume akiwa anafoka, na mwanamke akiwa analia, wakajua aliyekuwa analia ni Belinda kutokana na sauti yake, wakaingia, kumbe walikuwa wanaume wawili wakiwa wamewaweka chini ya ulinzi Belinda pamoja na mke wa mzee mpole, piga nikupige zikaanza, adui wawili wakajificha katika chumba alichokuwa amelazwa Fernanda mchana ambacho ndicho chenye simu ya Meja Venance, mwingine akauawa palepale.
Kisha wale wanaume wakawa wanaongea na simu wakiwa wamejifungia kwenye kile chumba, walikuwa wakitoa maelekezo ya wapi walipo na wapo katika mapigano makali na Sajenti warioba, mazungumzo yao yaliwatahadharisha Sajenti na Fernanda kuwa muda mfupi ujao kikosi kingine kitawasili pale hivyo itawapasa wafanye upesi, Sajenti akawa anafikiria cha kufanya, muda nao ulikuwa ukienda,
“ Hutotukimbia Sajenti, mwisho wako umefika, umechokoza nyuki kwenye mzinga wake, sasa subiri kung’atwa” Mwanaume mmoja akasema akiwa chumbani,
“ Nilisema mauti imekuja mume wangu hukunisikia” Mke wa mzee Mpole alikuwa pale chini akiongea na Mume wake aliyekuwa anakoroma nusu ya kufa,
“ Sajenti! Wewe Sajenti unajifanya haunisikii, hahahah! Subiri tutazibua hayo masikio yako, wewe ni adui wa taifa, Iko wapi kadava, ipo wapi chipu na sampo ya uchunguzi?” Yule mwanaume akaendelea kusema,
“ Ssa tutafanyaje Otieno, tutaendelea kumsikiliza huyo mwehu akisema hayo, au tunawasubiri hao wanaokuja kutukamata?” Fernanda akasema, punde Sajenti akakumbuka jambo, akaingiza mkono mfukoni akatoa dawa Fulani kama panadol kisha akatoa kibiriti cha gesi na kuichoma ile dawa ilipoanza kuwa na kutoa moshi akairusha ndani ya kile chumba cha wale wanaume walikojificha, wale wanaume wakaanza kukohoa huku mmoja akijaribu kuzima ile dawa kwa kuikanyaga, kisha baada ya dakika tano kukatokea ukimya, Sajenti akauvunja ule mlango akaingia ndani na kuwakuta wale wanaume wamelala wanakoroma, ilikuwa dawa ya kulevya ya usingizi, Wakaichukua ile simu ya Meja Venance wakatoka wakiwa pamoja na Belinda,
Lakini kabla hawajafika mbali wakiwa wanapotelea kwenye miti ya mihogo, ndivyo huitwa mkisamvu, wale maadui walikuwa wameshafika na kuwakabila, tena wakati mmoja alipokuwa akimpiga risasi Sajenti ili amuue, ndipo Belinda akajitokeza na kukaa mbele ya Sajenti kama ngao na ile risasi ikampata yeye kifua badala ya Sajenti, papohapo Belinda akaanguka na kufa, lilikuwa tukio lenye kutisha na lililomsononesha sana Sajenti, Fernanda alimvuta Sajenti na kumwambia waondoke kwani Belinda ndio ameshakufa, wakaondoka wakikimbia huku midomo ya risasi yenye uchu ikiachama kuwameza, walitokea kwenye korongo ambapo ndani yake kulikuwa na mto mdogo wenye maji machache huku kukiwa na miti mikubwa na vichaka, walikuwa wakirusha risasi huku wakikimbia na kujificha kwenye miti kulifuata lile korongo, wakapandisha mpaka wakatokea kwenye muinuko ambao juu yake ilikuwepo uzio wa senyenge, wakavuta ile senyenge kwa chini wakapita na kuzama ndani ya lile eneo ambalo halikuwa na nyumba yoyote isipokuwa shamba kubwa lenye mihogo na minazi, Fernanda alikuwa amekimbia akawa amechoka, jeraha lake alikuwa amelichokoza, maumivu makali yalizidi kumpa kero, hata hivyo hakuwa na chaguo zaidi ya kuchagua kuyapuuza, lakini hakuweza kupuuza kuchoka kwake, pumzi ilikuwa imemuishia, walikuwa wamekimbia umbali mrefu sana,
SURA YA 7
“ Ninakupongeza sana Mr. Daniel kwa kazi nzuri unayoendelea kuifanya, sikukosea kukuweka katika nafasi hiyo, njia yetu ni nyeupe lakini inatupasa kuendelea kuhakikisha hakuna wakuvuruga mipango yetu, propaganda zinazoendelea mitandaoni, kwenye vyombo vya habari vinatuweka kwenye hatua nzuri zaidi, wafanyabiashara wakubwa karibu wote tumewaweka kwenye mbawa zetu, watu mashuhuri kama wanamuziki, waigizaji, pamoja na viongozi wakubwa wa kidini wapo upande wetu, kazi iliyobaki ni kufuatilia asitokee msaliti miongoni mwetu akatusaliti, mnajua adhabu ya wasaliti, nitamuua kwa mikono yangu mwenyewe” akameza mate kisha akaendelea “ Kuna mtu mwenye swali au neno lolote la kuongeza” Kisha mwanaume mwingine aliyekuwa kwenye kile Kikao cha siri akanyosha mkono, akaruhusiwa kuzungumza;
“ Mhe. Rais, nashukuru kwa kunipa hii nafasi, sikuwa na jambo kubwa la kusema isipokuwa ni huyu Askofu Joshua Kalima” Yule mtu akasema, Rais akamkatisha,
“ Askofu Joshua Dawa yake inachemka, nafikiri wiki hii tutakuwa tumemalizana, ingawaje nimemtuma mtu amshawishi kwa mara ya mwisho kuwa upande wetu kisha amchunguze yupo na akina nani,akikataa kuwa upande wetu basi hatutakuwa na namna itabidi kumuangamiza” Rais akasema,
“ Lakini Mhe. Rais unafahamu kabisa Askofu Joshua anawafuasi wengi, mbali na hivyo pia mashirika na taasisi kubwa za kimataifa hasa nchi za magharibi wapo nyuma yake, naona itakuwa hatari sana kama tukimmaliza, inaweza kutuletea shida katika kuiongoza serikali” Mr. Gombe akasema, huku watu wengine waliokuwa kwenye kile kikao wakionekana kukubaliana na asemacho,
“ Sikiliza Gombe, Askofu Joshua hana Dola sisi ndio wenye Dola, huna haja ya kumhofia, tunakila nyenzo ya kukabiliana naye, hawezi kututisha na kuwa kikwazo katika kutimiza mipango yetu, kama hatutamuua tupe pendekezo, tumfanye nini akae kimya” Rais akasema, Kilikuwa kikao cha siri chenye watu saba ambao wote walikuwa wanaume, kati yao alikuwepo mzee mmoja mwenye umri upatao miaka sitini na saba hivi, mzee huyu muda wote alikuwa kimya pasipo kusema jambo lolote, baada ya mjadala wa namna ya kukabiliana na Askofu Joshua kila mmoja akitoa wazo lake, yule mzee akakohoa kidogo kisha watu wote wakakaa kimya, na kumtazama,
“ Kuhusu Askofu Joshua niachieni mimi, ndani ya siku tatu nitaleta ripoti hapa, tunaweza kujadili agenda zingine” Yule mzee akasema, watu wote wakatabasamu huku Mhe. Rais akimtania Mzee yule, baada ya kukubaliana kuwa suala la Askofu Joshua litashughuliwa na Yule mzee, Mhe. Rais akaendelea kusema,
“ Mr. Gombe hakikisha mambo yote yanayoendelea kwenye kikundi cha Ambagon unanipa taarifa, zipo taarifa kuwa yule mwanamke komando kutoka taasisi zetu za siri za usalama, aitwaye Fernanda, aliyekuwa ametekwa na kikundi cha Ambagon akatoroka aliokotwa ufukweni huko kigamboni, taarifa zinasema kuwa anasimu ya Meja Venance ambayo aliitoa katika nyumba ya Meja Venance, Kundi la Ambagon linaitaka hiyo simu kwa hali na mali, kama mjuavyo Meja Venance kumbe alikuwa msaliti wetu akitoa siri zetu kwa kundi la Ambagon, baada ya kundi lao kugundua kuwa tumeshajua kuwa Meja Venance anatusaliti, ndipo akauawa” wakati anaongea hayo Mr. Gombe alikuwa kwenye lindi la mawazo, kichwani zilimjia kumbukumbu za siku ile Meja Venance alivyouawa, akakumbuka;
“ Hello Venance kwema” Mr. Gombe alikuwa anaongea na simu na Meja Venance kwenye simu, akiwa ndani ya gari,
“ Kwema Kaka, usalama upo maana simu za usiku sio kawaida” Meja Venance akasema akiwa simuni,
“ Sio kwema kaka, nipo njiani nakuja, dakika kama kumi nitakuwa hapo Mkuu”
“ Kivipi kaka, kuna tatizo gani?” Meja Venance akasema,
“ Nipo njiani, vumilia dakika chache nitakuwa hapo” Mr. Gombe akasema,
“ Wamegundua?”
“ Ungeniambia mapema kuwa nawe ni mshirika wa siri wa Ambagon, subiri nakuja” Mr. Gombe akasema. Akikatisha kwenye barabara inayoingia katika mtaa aliokuwa anaishi Meja Venance, ulikuwa usiku wa saa tano kuelekea saa sita za usiku.
“ Daah! Sasa itakuwaje Ndugu yangu, nimekwisha mimi Kaka” Meja Venance akasema,
“ Hakuna kitakachoharibika usihofu, mimi ni kama ndugu yako, urafiki wetu niwa kufa kupona, ndio maana nikakuambia subiri nipo hapa ndio nakatiza hii kona kuingia kwenye barabara ambayo ipo nyumba yenu.”
“ Subiri kidogo,” Meja Venance akasema akiwa amemkatisha Mr. Gombe,
“ Meja! Venance! Venance!” Mr. Gombe alikuwa akiita kwenye simu lakini hakuitikiwa, alishtuka kusikia milio ya risasi Kupitia simu yake, kisha akasikia na vishindo vya watu wakipigana, kwa haraka akaongeza mwendo wa gari na kwa vile hapakuwa mbali tokea pale alipokuwa haikumchukua dakika moja alikuwa amesimamisha gari mbele ya geti la nyumba ya Meja Venance. Akatoa bastola yake na kuishika mkononi akiwa kajiandaa, alafu akatoka ndani ya gari, akafungua geti akakuta lipo wazi, alipoingia ndani akakuta walinzi wawili waliokuwa kwenye sare wamekufa, akazidisha umakini zaidi, akasonga mpaka kwenye mlango wa ile nyumba, akasikilizia akakuta kuko kimya, akagusa kitasa polepole, mlango pia ulikuwa upo wazi, akaingia, sebule ilikuwa inagiza, akapita kuifuata korido ya kuelekea kwenye vyumba, akiwa ananyata akashtushwa na kelele za mwanamke anayejitahidi kupiga kelele lakini mdomo wake unazuiwa kisha akasikia sauti ya mwanaume ikifoka kumtisha na kumnyamazisha yule mwanamke, Mr. Gombe akajua huyo ni mke wa Venance aliyekuwa analia, upesiupesi kwa tahadhari akakaribia kwenye mlango wa chumba zilipokuwa zinatokea zile kelele, akaufungua polepole huku bastola ikiwa tayari mkononi mwake, akafungua mlango akapokelewa na chumba chenye mwanga ambacho kwa mbele ulikuwepo mlango mdogo kama wa choo na bafu, kisha mkono wa kulia kulikuwa na mlango wa chumba kingine, bado alikuwa anasikia kelele za mwanamke anayefumbwa mdomo, huku mikikimikiki ikiendelea, hiyo ilimuambia kuwa tukio la ubakaji lilikuwa linaendelea; akafungua mlango kwa upesi kama umeme kisha akapokelewa na taswira ya mwanaume mmoja aliyemlalia kwa juu mwanamke, akakimbia na kumpiga kichwani yule mwanaume na kitako cha bastola, muda wote alikuwa kavaa Gloves mikononi, Yule mwanaume akasimama lakini kabla hajafanya chochote akapigwa ngumi ya uso akapepesuka, Mr. Gombe akamtazama yule mwanaume akamtambua ni mtu kutoka kundi la Ambagon, akampiga risasi ya kichwa kabla hajaongea jambo lolote maana alikuwa anataka kuropoka, Mr. Gombe hakutaka Mke wa Meja Venance ayasikie maneno ya yule Mwanaume.
Mr. Gombe akiwa amesimama akipumua kama bata dume, akashtuka alipouona mwili wa Meja Venance ukiwa umelala sakafuni ukitoa damu nyingi zilizotapakaa karibu chumba kizima, huku akiwa na majeraha makubwa ya risasi, Mke wa Meja Venance akiwa amenusurika kubakwa alimkimbilia Mr. Gombe na kumkumbatia akiwa na kinguo chake kilaini cha kulalia. Akawa analia akiwa amekumbatiana na Gombe. Baada ya kumfariji sana, ndipo Gombe akamwambia Mke wa Meja;
“ Hapa sio salama tena, tuondoke nikupeleke kwangu. Mtoto yupo wapi?”
“ Yupo chumbani kwake” Mkewe Meja Akajibu,
“ Vaa tukamchukue tuondoke”
“ Usiku huu huu jamani!”
“ Sio usiku huuhuu, namaanisha sasa hivi” Gombe akasema, Basi Mkewe Venance akavaa kisha akaenda kumuamsha mtoto chumba kingine, mtoto alikuwa akimuuliza mama yake maswali lakini Mama yake alikuwa akimdanganya huku akijizuia asilie na kuficha huzuni usoni mwake, hata alipoulizwa alipo Baba yake, ndiye Meja Venance akadanganya pia kuwa ametoka ameitwa kazini, kutokana na kazi ya baba yake ilikuwa ni kawaida Baba yake kuondoka hata usiku hivyo hilo halikumpa wasiwasi mtoto.
Wakatoka nje lakini Gombe akawaomba wamsubiri aingie ndani kwani kuna jambo amesahau kulifanya, Gombe akaingia ndani, akaufuata mwili wa yule mwanaume muuaji, akampekua katika mifuko yake ya suruali, akakuta namba anayoijua fika ni ya kiongozi wa Ambagon, akaandika ujumbe usemao “ fanyeni haraka nimezidiwa, ingawa nimemuua” kisha akaituma. Baada ya hapo akatoka, akawachukua mke wa Meja Venance na binti yake, wakaingia ndani ya Gari la Mr. Gombe alilokuwa ameliegesha nje ya Geti la nyumba ya Meja Venance, wakaondoka.
Wakiwa njiani wakapishana na Gari ambayo Gombe alikuwa akiifahamu, alijua kabisa gari lile linaelekea kwa Meja Venance, kumbukumbu hizo za Mr. Gombe alizokuwa akiziwaza zilikatishwa na sauti ya Mhe. Rais katika kikao kile;
“ Mr. Gombe unawaza nini?” Mhe. Rais akasema,
“ ooh! Tupo pamoja Mkuu” Gombe akajibu.
“ Tuweni makini, hatutaki uzembe wowote katika shughuli zetu, mwezi ujao ni uchaguzi, nyote mnajua kuwa kushinda kwangu ni kushinda kwenu, kuanguka kwangu ni kuanguka kwenu, kama hamnielewi vizuri, jaribuni kufikiria miradi yenu mlioianzisha ambayo kama sio mimi kuwalinda ingekuwa imeshajifia, hamlipi kodi, na karibu tenda zote zile kubwa tunawapa ninyi na washirika wenu, Kwa mfano Mzee kibangu, kampuni lako la Ukandarasi na Uhandisi tumelipatia mara nyingi tenda ambazo zimekufanya kuwa na pesa nyingi mpaka kufikia hatua umeanzisha biashara za hoteli nchi za ulaya, sijui kama tunaelewana lakini” Mhe. Rais akasema,
“ Mbona tunaelewa sana Mkuu, wewe toa shaka, utashinda kwa kishindo awamu hii, hakuna aliyetayari kuwa masikini, tumeshaonja maji ya maiti hatutaki tena kuyaacha, utashinda, hapa tunachojadili sio kushinda kwako Mhe. Rais kwani hata washindani wetu wanajua wewe ndio utakayeshinda, tunachojadili hapa ni namna ya kuwashughulikia maadui zetu yasijetokea yale ya Meja Venance” Mzee Kibangu akasema, ndiye yule aliyesema aachiwe amshughulie Askofu Joshua.
“ Kesho nitakutana na Vyama vya upinzani mamluki kusudi watoe tamko kutuunga mkono, kuhusu vyombo vya habari wote wanaogopa hawawezi kutangaza habari za mahasimu wetu isipokuwa habari mbaya tuu” Mr. Danieli alisema,
“ Kuhusu masuala ya ulinzi na usalama kila kitu kipo sawa, adui zetu hawana mbinu za maana za kukushinda Mhe. Rais, tunachohangaika ni kuhakikisha tunamkamata Huyo mwanamke aliyekimbia na simu ya Meja Venance bila shaka simu hiyo itakuwa muhimu sana kwetu, maana ile siku tulikagua nyumba yote tukakuta simu moja tuu, hatukujua kuwa kuna simu nyingine sirini, lakini bado nina mashaka sana Mkuu, kuna kitu hakiko sawa!” Mkurugenzi wa idara ya usalama wa taifa alisema,
“ Kitu gani hiko” watu wote kama mtu mmoja wakasema,
“ Unajua ile picha ya tukio la ile siku bado kiusalama bado inaacha maswali mengi, embu fikiria tulipanga wote hapa sisi watu saba kasoro mmoja ambaye ndiye Meja Venance, tulipanga kwenda kumteka Meja Venance na kumhoji juu ya usaliti wake kisha tungemuua, lakini chakushangaza siku ile tumefika nyumbani kwa Meja tukakuta miili miwili ikiwa imeuawa kwa kupigwa risasi, Meja Venance akiwemo, maganda ya risasi yanaashiria zilitumika bastola tatu ingawaje miili ilikuwa miwili pale chini, baada ya uchunguzi ripoti ilipotoka yale maganda ya risasi yalionyesha kuwa bastola iliyotumika niya yule Mwanaume na nyingine bastola ya Meja ambazo zote tulizikuta palepale eneo la tukio, bastola ya tatu iliyotumika haikujulikana ipo wapi hii ilimaanisha alikuwepo mtu wa tatu” Akameza mate kisha akaendelea,
“ Jambo jingine ni kutojulikana alipo mke wa Meja Venance na binti yake, wazo la kusema yeye, yaani mke wa meja ndiye aliyefanya tukio lile la kikatili akaamua kutoroka, nakataa, nina wazo la kuwa ametekwa na mtu asiyejulikana, kwa sababu zifuatazo, eneo lile katika kile chumba kulikuwa na nyayo za viatu zilizokanyaga damu ambazo zilikuwa tofauti kabisa na viatu vya yule mwanaume aliyeuawa pamoja na Meja Venance, vipimo vyake vilikuwa inchi kumi na moja kasoro hii ilimaanisha alikuwa mwanaume mwenye urefu wa kati, pia tulipoishika ile simu ya yule mwanaume ambayo ilikuwa kifuani mwake jambo hilo lilitupa picha kwamba, kuna mtu aliyemuweka ile simu kifuani, isingewezekana simu kukaa kifuani kwa jinsi alivyokuwa amelala, yaani apigwe risasi ya kichwa aanguke chini alafu simu ikae kifuani, hapana kijasusi hiyo inaashiria kuwa kuna mtu alimuwekea simu hiyo kifuani, kama hiyo haitoshi;” Akakohoa kidogo kisha akaendelea;
“ Ile simu tulipoifungua tulikuta ujumbe uliotoka kuandikwa dakika chache tuu zilizopita tangu tulipofika pale, muuaji wa yule mwanaume bila shaka hakumuua Meja Venance, ila inaonyesha yule mwanaume ndiye aliyemuua Meja Venance kisha baadaye akataka kumbaka Mke wa Meja kutokana na namna kitanda tulivyokikuta kilikuwa kimevurugika sana, na mashuka yake yaliyokuwa na nyayo za damu za yule mwanaume, pia mashuka yalikuwa na harufu ya manukato ya yule Mwanaume iliyochanganyikana na marashi ya mwanamke, hata tulivyonusa nguo za yule mwanaume aliyeuawa alikuwa akinukia marashi ya kike yanayofanana na marashi ya kwenye mashuka ambayo bila shaka ni marashi ya mke wa Meja, kisha aliyemuua yule mwanaume akatokea na kumuua yule mwanaume, alafu baada ya kumuua ndio wakaamua kuandika ujumbe kisha kumuweka simu juu yake, Muuaji aliyemuua mwanaume aliyemuua Meja Venance lazima atakuwa anajua kundi hilo la Ambagon au ni mwanachama wa kikundi hicho, lakini najiuliza, kama ni mwanachama wa kikundi hicho iweje wamuue mwenzao? Na kama sio mwanachama, alijuaje namba zile ambazo hata sisi tunazijua nizakiongozi wa Ambagon ambaye mpaka leo tunahangaika kumtafuta?” Hapo akanyamaza, wote walikuwa wakitafakari maneno hayo, Mr. Gombe alikuwa kimya huku hofu ikitembea katika mishipa yake ya damu, yeye ndiye aliyeshuhudia tukio lile, naye ndiye aliyeichukua familia ya Meja Venance na kuihifadhi nyumbani kwake.
“ Nguo ya kulalia ya Mke wa Venance tuliikuta juu ya kitanda, hii ilimaanisha alibadili ndio akaondoka kutokana na kuwa ilikuwa juu ya zile nyayo za damu za viatu vya yule mwanaume. Jambo la mwisho ni kuhusu Marashi na manukato ya ile simu, tulipoinusa ile simu ilikuwa na marashi yenye harufu tofauti na harufu ya Yule mwanaume aliyeuawa, pia ilikuwa tofauti na harufu ya marashi ya Meja Venance pamoja na harufu za marashi ya mke wa meja kwani tuliangalia vipodozi vyake hatukuona hata kipodozi kimoja chenye harufu kama ile, harufu ya manukato yale hutumiwa na wanaume zaidi hasa watu wazima wa kuanzia miaka arobaini wenye vipato vikubwa, hii ni kusema muuaji wa Meja Venance hakuwa kijana mdogo au mtu mwenye uchumi wa kawaida au uchumi wa chini, lazima atakuwa mtu mzima mwenye kipato kinachoeleweka. Huyu aliyemteka mke wa Meja Venance ndiye ananipa mashaka, lazima mkewe Venance atakuwa anafahamiana naye, wasiwasi wangu isijekuwa yupo kati yetu hapa” Mkurugenzi wa Idara ya Taifa akanyamaza, kisha akawa anawaangalia wanakikao kwa zamu, alipofika kwenye uso wa Mr. Gombe akatulia kwa kitambo, jambo ambalo Gombe lilimshtua sana ingawaje alijikaza kuficha hila yake ili asigundulike kuwa ndiye yeye aliyefanya hayo, “ Sikuwa mjinga, nilibadili kutumia marashi na mafuta yale tangu nilipofanya tukio lile, nilijua kuwa haya yangeweza kutokea” Mr. Gombe akawaza. Lakini akiwa anawaza ghafla moyo wake uliingia baridi baada ya Mkurugenzi wa Idara ya usalama wa taifa kusema;
“ Yale marashi niliwahi kuyasikia kwenye vikao vyetu, sikumbuki vizuri ni nani alikuwa anayatumia, ila nina mashaka makubwa mtumiaji wa marashi yale anaukaribu wa kile kilichotokea siku ile”
“ Rafiki yake Meja Venance ni nani hapa kama sio Mr. Gombe?’ Mwanaume mmoja mfupi mwenye upara na kitambi akasema, hapo kila mtu akamtazama Mr. Gombe, lakini Mhe. Rais akamtetea, Mhe. Rais alikuwa akimuamini sana Mr. Gombe kutokana na mishemishe alizokuwa anafanya naye.
“ Tuachana na jambo hilo, hiyo simu ya Meja Venance hakikisha inapatikana, kumbukeni yeye ndiye aliyekuwa katibu na muweka kumbukumbu za vikao vyetu hapa, huyo mwanamke akamatwe ndani ya masaa arobaini na nane, na huyo Sajenti, lakini Mr. Lusingi hawa si vijana wako kabisa, iweje watusumbue hivi?” Rais akasema,
“ Mhe. Rais ni kweli kabisa hawa ni vijana wangu, wote ni wanakitengo katika usalama wa Taifa letu, tatizo lao wao wanapenda sana haki, kimsingi wao ni wanauzalendo uliopitiliza kwa taifa lao” Mr. Lusingi ambaye ndiye Mkurugenzi wa Idara ya usalama wa Taifa akasema, hapohapo akakatishwa,
“ Unamaanisha sisi sio wazalendo?” Mhe. Rais akasema, kisha wote wakacheka,
“ Mhe. Rais, wala hatuna haja ya kujadiliana na mambo hayo, kila mmoja anajua ukweli moyoni mwake kuwa sisi ni wazalendo au wachumia tumbo tukilinyonya taifa hili, tutahangaika kuwatafuta hawa watu, hawawezi kutukimbia, ingawaje jambo hili tunalifanya kwa siri kwa sababu wanausalama wengine wanawajua Sajenti na Fernanda kama Wazalendo, hivyo hatutawahusisha kwa lolote, hatutaki pia waangukie katika mikono ya Polisi, ni bora wakamatwe na hilo kundi la Ambagon, jambo moja la uhakika ni kuwa Sajenti Warioba anaujuzi na uzoefu mkubwa sana wa kijeshi, kiulinzi na kijasusi, hivyo lazima tuwe makini” Mr. Lusingi akasema,
“ Hahahaha! Serikali haiwezi ogopa kinyago ilichokichonga yenyewe, huyo Sajenti ni Mende tuu kwenye kinyesi” Mhe. Rais akasema,
“ Lakini Mhe. Rais, Bwana, Kinyunumba tambua tunachokifanya watu wengi hawakijui, na kama siku wakijua kuwa tupo kwa ajili ya maslahi yetu na wala sio maslahi ya taifa, hawatatuunga mkono, fikiria wafanyakazi wa umma mishahara yao ilivyomidogo, jeshi la polisi watumishi wake nao hivyohivyo, makazi yao duni, mishahara ya bei ya mkaa, hata hilo jeshi halitatusapoti Mhe. Rais, kusema Sajenti hawezi kushindana na Serikali tutakuwa tunajidanganya, yeye hashindani na serikali bali anashindana na wahujumu uchumi na wachumia matumbo” Mr. Lusingi akasema,
“ Kwa hiyo unataka kusema nini, au upo pamoja naye? Unabishana na mimi?” Rais Kinyunumba akasema,
“ Hapana Mkuu, sibishani na wala sina ubavu wakukuzuilia neno lolote”
“ Basi nawataka hao wadudu ndani ya masaa ishirini na nne. Wawe hapa ima wangali hao au mizoga yao, kikao kimefungwa” Rais Kinyunumba akasema, akiwa ameghadhibika,
Kikao cha Siri kiliisha, wanakikao wakaondoka kila mmoja akipanda gari lake kuelekea nyumbani kwake, huku Rais akirejea Ikulu.
INAENDELEA
Kitabu kipo Tayari, lIPIA Tsh, 15,000/= UJIPATIE NAKALA YAKO
0693322300
Robert Heriel
Airtelmoney