RIWAYA

RIWAYA

godlovalez360

Member
Joined
Oct 4, 2023
Posts
13
Reaction score
17
SHAMBA LA HELA
Imetungwa na Godlove Kabati.
WhatsApp 0763204351.

SEHEMU YA KWANZA;

FEROOUZ HAIR CUTS


Bukoba, Kagera
Jumamosi, saa kumi jioni.


KITENDO cha kukatika kwa umeme kiliuzika uchangamfu na kufufua hali ya kupooza kwenye genge la mtaa huu.
Hii sio hali ya kawaida kabisa,
Yaani kwenye genge la mtaa huu wa Buyekera mida kama hii ya jioni kuwa kimya namna hii?
Kwa kawaida, imezoeleka hali ya uchangamfu wa anga linalotetemeshwa kwa kelele za hapa na pale.
Duka lile utasikia midundo ya muziki murua wenye ladha ya Amapiano. Mara pale kwenye maduka ya kanda za video utasikia namna spika zinavyoshindana kupaza sauti za watafsiri wa filamu mbalimbali kutoka n'gambo.
Kule utasikia vipaza sauti vya wapiga minada kusifia upungufu wa bei za bidhaa zao. Na vibanda-umiza navyo havikutaka kuachwa nyuma, hupaza sauti za watangazaji mbalimbali wa mechi.
Ni kelele mtindo moja, ili mradi tu kila mfanyabiashara, biashara yake isikike vyema zaidi ya mwingine.
Genge hili kubwa hugeuka kuwa gulio dogo. Leo mambo ni tofauti kabisa. Genge limepoa!

Kupooza huku kumefifisha hata idadi ya wanunuzi na wachuuzi mahali hapa. Kwa kawaida ardhi hii hukusanya watu wengi sana muda kama huu. Ardhi hupata suluba sana kuzibeba nyayo za viumbe hai wanaotembea juu yake. Lakini leo hali ni tofauti kidogo, genge limepoa sana. Ni kama watu wamelisaliti genge la mtaa huu.

Hakukuwa na tangazo lolote lile juu ya kukatwa kwa umeme kwa muda mrefu namna hii. Wakazi wa eneo lile walikubali kukosa umeme kwa siku moja, wakaukosa siku ya pili na sasa hii ilikuwa siku ya tatu. Siku tatu bila umeme!
Maswali na lawama vikawa vingi kwa serikali yao, lakini majibu waliyopewa yalikuwa yaleyale waliyozoea kuyasikia siku zote,

"Kuna matatizo ya kiufundi. Ambayo yanafanyiwa kazi" . Walijibiwa hivyo.

Adha hii imeyumbisha biashara za wale waliotegemea sana umeme ili kuuza bidhaa au ujuzi wao.
Tatizo hili likawa kama ngumi ya pua kwa wale wafanyabishara wasioweza kumiliki majenereta ya umeme, na shughuli zao zilitegemea umeme ili wapate kipato.

******

Nje ya jengo dogo mfano wa kibanda, kilichonakshiwa kwa rangi na mchoro mkubwa wa aliyekuwa msanii maarufu wa marekani, Tupac Shakur.
Maneno makubwa yanasomeka pale juu ya mlango wa banda hili la mbao,
FEROOUZ HAIR CUTS.

Kijana mmoja wa kiume anaonekana kuketi umbali wa hatua nne hadi tano nje kidogo kutoka kwenye banda hili. Yeye pia akiwa mmoja miongoni mwa wahanga wa tatizo hili la kukatwa kwa umeme. Ikiwa ni siku ya tatu hii amefungua saluni yake bila kutoa huduma yoyote ile.
Amekaa juu ya benchi, ameegemea ukuta wa nyumba iliyokuwa mkabala na saluni yake.

Ameketi kuuelekea mlango wa ofisi yake hii uliokuwa wazi. Ni mtulivu ameifumbata mikono yake, macho mbele ameitazama taa ndani ya saluni yake.
Alikuwa amewasha swichi akitarajia kuwa taa ile itawaka mara tu umeme utakaporudi kutoka huko ulikokuwa umeenda kutalii. Lakini taa ikabaki kimya ikinin'ginia juu ya dari.

"Aah kudadek!", ilimtoka kinywani mwake.
"Wana nini hawa?". Haikujulikana kama anajiuliza swali au alikuwa analalamika.
"Hivi wanataka tule mchanga? Au wanataka tule mwanga wa jua kama Jadu. Yaani siku ya tatu hii wamekaa kimya tu. Sema ngoja! Wata-", hakuimaliza sentensi yake.
Aligundua kuwa hata akilalamika vipi, hatakuwa na namna yoyote ile ya kuiumiza serikali.
Kwani ni matatizo mangapi yamewahi kulalamikiwa na bado wakaishi humohumo?
Alibaki kufyonza tu.
Lilikuwa sawa na dua la kuku, lisiloweza kumpata mwewe.

Anasimama na kupiga hatua tano kuingia ndani ya banda hili. Amefika ndani na kunyanyua chupa yake kubwa ya maji ambayo ilikuwa na maji nusu ya ujazo wake kamili. Anazungusha mfuniko wake kulifungua lakini anakatishwa baada ya kusikia sauti ya muito wa simu mfukoni mwake.

Anaachana na chupa la maji, anachukua simu yake na kutazama jina la aliyempigia. Mara anaishusha chini simu yake akiwa amekunja ndita usoni kwa hasira. Akaiacha iendelee kuita, huenda huyu aliyempigia amemuudhi au hakutaka kuongea naye kwa muda huo...

"Huyu demu naye atakuwa anataka hela tu sa'hivi , sijui kwa nini nilimuahidi?"
Akajisemea peke yake,
"Sipokei simu yake!"
Akaamua kupiga mafunda kadhaa ya maji kutoka kwenye chupa lile.

Mara ikasikika sauti ya mtetemo wa pikipiki ambayo ilikuwa ikijongea kuelekea jengo lake la saluni lilipo. Mtetemo ule ukazimika ghafla, karibu zaidi na saluni yake. Hii ikamjulisha kuwa kuna mtu yupo nje ya saluni.

Akajaribu kuchungulia nje kupitia dirisha lake dogo, ili aone ni nani huyu aliyesimama nje ya saluni yake, huenda akawa mteja ambaye hakumtarajia kuwa pale muda kama huu.
Alichokiona kilimfanya atabasamu.
"Kijana Mtemi Moringo...naona mambo sio mabaya sana!" Feruzi akapaza sauti yake, ambayo ilimfikia yule mtu pale nje, aliyejulikana kwa jina la Mtemi. Na yeye akatabasamu.
Mtemi akapaki pikipiki yake vizuri kisha akaanza kujongea kuingia ndani ya saluni.

"Oyaaae kijana Feruzi niaje hapa!" Akasalimiwa na huyu mgeni.
"Aah kaka, jau jau tu." Kijana huyu aliyejulikana kwa jina la Feruzi akamjibu kwa sauti iliyotangaza unyonge.

Mtemi akavua koti lake kubwa na kulitundika juu ya msumari mmojawapo uliochomoza kwenye ubao. Akaweka helmeti yake kwenye kiti kilichokuwepo pale ndani.
Kisha akajongea moja kwa moja mpaka mbele ya kioo kipana kilichokuwepo pale ndani, akachagua chanuo kubwa la nywele miongoni mwa vingi vilivyokuwepo pale kwenye shubaka. Akaanza kuchana nywele zake nyingi kichwani, zilizokuwa kwenye mtindo wa Afro, huku akijitazama kwenye kioo.

"Umeme bado hujarudi tu?!" Akatupa swali huku akiendelea kugeuzageuza kichwa chake mbele ya kioo.

"Yaani acha tu bro, siku ya tatu leo...wanataka tuwalambe miguu yao sijui?" Feruzi akatamka huku na yeye pia muda huu akiwa amekigeukia kioo akiitazama taswira yake...ambayo ilimkasirikia kama alivyokuwa amekasirika yeye.

"Lakini nasikia kuna nguzo imeanguka kule juu maeneo ya Kibeta! Huenda nd'o wanashughulika nayo muda huu" , akasema Mtemi.
"Nguzo? Ina maana muda wote huu tangu juzi wameshindwa kubadilisha? Hawajui kuwa watu huku tunakula upepo?" Feruzi, akaongea tena kwa makasiriko.

"Nd'o serikali yetu hio... siku zote mwenye shibe hamjui mwenye njaa."

"Aah hata kama bhana...unaona hapa mwanangu, leo tumbo langu halijasalimiwa na chakula chochote kile. Na sioni hata hela ya kununua hicho chakula napata wapi." Feruzi akaanza kuangusha malalamiko yake.

"Eboo! Kumbe nd'o maana una hasira. Hii yote ni kwa sababu ya njaa!" Mtemi akayasindikiza maneno yake kwa kicheko dhaifu, kilichoudhibitisha utani uliokuwepo tangu siku nyingi baina ya marafiki hawa wawili.
Maneno yake yakamfanya Feruzi ashindwe kujizuia na yeye akacheka. Japo kicheko chake kilionyesha wazi kuwa amechoka na ana njaa!

"Nimezoea muda kama huu tena wikendi! Wateja kibao sana, halafu nikifika huwa unanifukuza we fala!" Mtemi akatupa kauli nyingine ya utani.

"Duh! Hapa mwanangu unanionea! Lini nimekufukuza wewe. Wakati humu umepafanya kama sebule yako, tena huwa nakunyoa bure kabisa!" Feruzi akajitetea.

"Aah wapi we mshikaji huwa unatukataa wahuni. Sema hamna mbaya, ngoja nenge ikunyooshe kwanza! Hahaha"

Feruzi akasogea karibu na koti lililokuwa limetundikwa pale kwenye ubao.
Akalichukua na kuanza kulivaa kabla Mtemi hajamshitua,
"Oyah wee, namna gani tena? Wapi na koti langu tena"
Feruzi akalivaa koti kimya, kisha akasogelea helmeti iliokuwepo pale juu ya kiti. Akiokota na kuivaa kichwani mwake.
Muda huu wote Mtemi amemtumbulia macho akimshangaa, hajui ni nini rafiki yake amepanga kufanya.

Feruzi akamaliza kuvaa akiwa kimya. Halafu akamsogelea Mtemi na kunyoosha mkono wake,
"Em nipe funguo hapo chap, nikatafute chochote kitu."
Mtemi akaa kimya kwa sekunde tatu kisha akaangua kicheko.
"Kwa hio umeamua kuwa Sekido!" Akatamka Mtemi huku kicheko kikiendelea kumyumbisha.

(Sekido ni jina rejesta itumikayo katika jamii za wahaya, kumaanisha dereva pikipiki au bodaboda kama ilivyozoeleka na wengi)

"We leta hio kii, nikabebe wateja wawili watatu. Nipate chochote kitu." Feruzi akaendelea kusisitiza.
Ghafla simu yake ikaita tena, wote wakageuza shingo zao kutazama ni nani huyo aliyepiga.
Simu ikiwa juu ya shubaka, wakasoma jina 'Alinda'.
Wote wakatazamana na vicheko vikalipuka tena kutoka vinywani mwao.
"Unaona? Demu huyo hapo kanipigia tena, hii mara ya pili. Nilimuahidi afu tano tu ya kusuka ndo ananidai utadhani kanikopesha!" . Kwa utulivu Feruzi akajongea na kuikata simu ile, kisha akabonyeza kitufe chake kimojawapo ili aizime kabisa. Ikazimika!

"Khaa! Ndo unazima simu kabisa?" Mtemi akatoa kauli ya mshangao, bado yumo katika hali ya kicheko.
"Yaani mi sijui leo nitakula nini....halafu nimpatie demu hela ya kujiremba?! Au anadhai mi nitakula nywele zake." Akajibu Feruzi.
"Mademu zenu hao; mkiwa mnawaita gheto kuwakamia wakiwaomba hela msiwanyime! Hata hivyo ahadi ni deni."
"Eeh bwana ee...we nipe funguo nisepe bhana. Masuala ya mademu zetu tuachie sisi wenyewe!" Kwa kukasirika kidogo, Feruzi akadai funguo isiyokuwa yake ili mradi tu abadilishe mada.
Bila kusita Mtemi akachomoa funguo kutoka kwenye mkanda wa suruali lake na akampatia Feruzi huku tabasamu likiupamba uso wake.

"Kwani nina baya basi mzee? Chukua funguo hizi hapa. Nenda ukashindane na upepo sasa, tutakuokota ukiwa mifupa!!"
"Aweee tulia bhana, fundi mimi. Haya mambo madogo madogo."
"Umezoea kushevu watu tu hapa...unapindisha mashine huku na huku, kazi simpo sana hizi. Nenda kafanye kazi za wanaume barabarani mdogo wangu!" Mtemi akatamba.

"Kazi simpo eh au sio? We nikikuacha hapa hata kwa masaa mawili tu. Utatoka umevimba mikono." Feruzi akamjibu huku akipokea ufunguo ule uliokuwa umeunganishwa barabara kwenye ringi ambayo ilikusanya jumla ya funguo nne, zilizoshindana kupiga kelele kila zilipogongana.
Feruzi akatoka nje akimuacha Mtemi ndani ya saluni.

"Kwa hiyo unarudi saa ngapi sasa?",.Mtemi akapaza sauti.
"Tulia bhana....sichelewi!" Akajibiwa.
"Angalia basi usinipaki humu ndani." Akapaza sauti yake tena akilalamika japo hakuwa na hasira.
Hakujibiwa!
Alichokisikia zaidi, ni muungurumo wa ghafla na mtetemo wa sauti ambavyo vilitosha kumjulisha kabisa kuwa pikipiki imewashwa. Halafu akasikia tena sauti ile ya mtetemo ikiishia, Feruzi aliondoka na pikipiki yake.

Akachungulia dirishani kumsindikiza kwa macho mpaka alipopotea kwenye upeo wa mwisho wa macho yake. Kisha akatabasamu!
Tabasamu lake daima liliupamba uso wake, lilikuwa tabasamu ambalo halikueleweka kama lilitafsiri furaha au huzuni moyoni mwake.

Akatoka dirishani, akaketi kwenye kiti kikubwa ambacho hukaliwa na wateja wanaponyolewa.
Akastarehe kwa kuegemeza mwili wake huku akijizungusha huku na huku. Macho yake yakilikagua dari la saluni ile.
Akawaza mambo mengi sana, kuhusu yeye na rafiki yake.

Alimuamini sana na rafiki yake,
Ni mambo mengi wamesaidiana na wameyafanya pamoja tangu walipokutana hapa mjini wote wakiwa katika utafutaji. Yeye akiwa kama dereva bodaboda na Feruzi akiwa kama kinyozi. Namna yao ya kukutana ilikuwa ya ajabu, ajabu sana!
Alipotaka kuikumbuka tu,
WAAH!

Mwanga mweupe wa taa kubwa ukammulika usoni mwake. Akafumba macho yake kuukwepa. Umeme ulirudi!
Ghafla! Ndani ya sekunde chache tu, mziki mzito ukaanza kuunguruma ndani ya saluni ile.

"Aaargh, huyu naye alikuwa hajazima spika yake!" Akasimama kuelekea ilipo spika ili afanye alichotaka kufanya ambacho mimi na wewe hatukijui.
Labda alitaka kubadilisha mziki ule au kupunguza sauti au kuzima kabisa. Tumshangae tu!

Kabla hajamaliza hatua yake ya pili tu, saluni ikapata ugeni mpya. Watu wawili wakaingia wakihitaji kunyolewa. Mtemi hakupata nafasi ya kusema lolote la kuikana saluni hata kidogo, wakaongezeka watoto watatu walioonekana kuwa wa shule ya msingi .
Ikawa ni kama watu walikuwa karibu na salumi ile wakisubiri umeme useme wiiii na wao waitikie waaa, waingie ndani yake.
Tayari ulikuwa umesema wiiii na sasa wamo ndani.

Mtemi akakasirika lakini hakuwa na namna. Ilibidi amsaidie kazi rafiki yake ambaye kaenda kutafuta pia. Ilibidi wabadilishane kazi kwa muda kidogo.
Hakuwa mgeni katika kazi hii ya kunyoa watu, alikuwa na ujuzi kidogo wa kucheza na mashine ile ya kunyolea. Akavaa aproni akawasha mashine na kuanza kusuguasugua vichwa vya wateja kuondoa nywele zao.

Alikuwa na ujuzi japo hakuwa na uzoefu. Mkono ukaanza kumuuma akajizuia sana asitetemeke kuharibu vichwa vya wateja hasa wale walioonekana wanazijali sana nywele zao kuliko vichwa vyenyewe.
Kazi aliioiita 'simpo' ikamfanya avuje jasho apate na mafua ambayo hakuwa nayo dakika kumi tu zilizopita.

Tukutane wakati ujao....
Kujua ni nini kitajiri.
490d008a.jpg
 
490d008a.jpg
SHAMBA LA HELA,

SEHEMU YA PILI;
ABIRIA MWENYE MABEGI MEUSI
----------------------

MKUKUMKUKU,
aliivamia barabara akiendesha pikipiki yake kwa kasi sana.
Alivuta gia kwa fujo, akiiungurumisha pikipiki ile kwa mbwembwe .Ili mradi tu kila mtu ajue kuwa anafahamu kuendesha pikipiki.

"Vijana wa siku hizi bhana! Hapo akisababisha ajali anaelaumiwa ni shetani. Utasikia mara ooh , shetani kanipitia!"
Mzee mmoja aliyekuwa anakunywa kahawa alitamka,
"Unadhani changamoto ni nini sasa pale kama sio bhange na mirungi?"
Mwingine akaongezea hoja yake. Wote wakimshuhudia Feruzi akiwa juu ya pikipiki, nusu ardhini nusu hewani...kwa kasi aliyochomoza nayo pale kando ya kijiwe cha kahawa.

Kwa upande wake yeye, ilikuwa ni kama faraja. Alikuwa na muda mrefu sana tangu ameendesha pikipiki, kwa maana hio alitaka afidie hamu yake.
Lakini utupu wa mifuko yake na njaa ya tumbo lake vikamkumbusha kuwa ana muda mchache sana wa kutafuta abiria.
Akasimamisha pikipiki yake kando kidogo ya barabara na akaangaza huku na huko.
Hakukuwa na dalili yoyote ile ya watembea kwa miguu.
"Aah huu mtaa jau sana. Ngoja niingie hapo tauni kati. Hata hivyo hakuna nabii anayekubalika kwao."
Akaichochea tena pikipiki yake na kuendesha kuelekea mjini. Ambako alitarajia kupata abiria kwa urahisi kuliko mtaani kwake.

Akakata upepo kwa kasi kidogo kuelekea mjini. Na alipokuwa njiani kichwa chake kilikuwa bize kikikagua huki na huku.
Mara akamwona mwanamke mmoja kwa mbali aliyevaa mavazi mazuri namkoba ukining'inia kwenye bega lake la kushoto. Mwendo wake ulioenesha wazi kuwa amechoka sana.
" Enhe kichwa hiki hapo ngoja nikakile!" Akaongeza kasi kuelekea kwa mwanamke yule mwenye umri wa makamo na alipomkaribia tu akapunguza kasi na kumpigia honi,
"Mamaah! Twendeeeee?!"

Mwanamke yule hakutoa jibu la moja kwa moja badala yake alisimama akaisogelea pikipiki na kuketi,
"Kashai matopeni!"
Feruzi akatabasamu na kuchochea tena pikipiki ile ya mkopo,
Akaanza tena kukata upepo kuutafuta mtaa huu wa Kashai matopeni. Tayari akili yake imeshapiga hesabu kali juu ya shilingi kadhaa ambazo angezipata kulingana na umbali ambao angemsafirisha abiria yule.
Dakika sita pekee zilitosha kumfikisha mtaani hapo.

Yule mama alishuka na kupekua mkoba wake taratibu kwa mkono wake wa kulia. Mkono wake ukaibuka na noti ya shilingi elfu moja. Akampatia Feruzi,
"Hii hapa nashukuru!"
Feruzi hakuamini alichokuwa amekipokea mkononi mwake. Mikono yake ilitetemeka kidogo,

"Eer mamaaa...samahani nadhaniii, umenipa pesa pungufu kidogo. Eeer ni buku jero mama, buku jero mpaka huku."
Akajaribu kutetea ujira wake.

Mama yule akapigwa na butwaa,
"Khee! Tangu lini tena...Yaani mpaka hapa elfu moja mia tano?"
"Eeh mama ni hiohio"
"Mmepandisha nauli kuanzia lini? Juzi tu hapa nimelipa elfu moja! Leo hii unaniambia ni elfu moja na mia tano?"

Feruzi akakumbwa na wasiwasi. Hakuwa akijua bei za nauli kwa maeneo mbalimbali, alikuwa akibahatisha tu. Na ili msala huu uishe kwa amani, akaamua kukubaliana na mama yule haraka sana maana hata wapita njia walikuwa wameanza kuvutiwa na maongezi yao.
Akawasha pikipiki yake na kuondoka!

Akaendelea kufanya msako wa abiria wengine...muda ukizidi kupotea, hakufanikiwa.
Abiria wengine aliokuwa akiwapigia honi kufahamu kama wanahitaji usafiri walimpungia mikono yao kuonesha kuwa hawahitaji usafiri. Na wengine hawakumjibu chochote, walimkalia kimya alishindwa kutafsiri kama ni dharau au hawako tayari kutumia usafiri wake.
Akazunguka mpaka akachoka, akatafuta kivuli akapaki pikipiki yake na kupumzika. Tumbo liliendelea kuunguruma kwa fujo likimdai chakula...akahisi ni kama utumbo wake ulikuwa ukitetemeka.
Akajipapasa mfukoni mwake na kuitazama noti yake ya shilingi elfu moja aliyokuwa ameipata baada ya kumsafirisha abiria mmoja tu.
Akakadiria bei za vyakula ambavyo angeweza kununua kwa fedha ile, akakunja sura yake baada ya kugundua kuwa fedha ile bado haitoshi.
"Mbona Mtemi aliwahi kusema kuwa yeye hawezi kukosa elfu kumi kwa siku? Hao abiria anawanunua au?", akajiuliza yeye mwenyewe.
"Yaani hadi sa hivi nina buku tu? Aah kudadek. Inabidi nikaze sana nipate angalau wawili wengine."
Akapanda tena pikipiki yake,
"Ngoja niende kule maeneo ya Tan-point, pale siwezi kukosa vichwa pale".
Akabadilisha uelekeo.

Akiwa njiani kwa mbalii akamuona mwanaume mfupi aliyekuwa katika mchakato wa kuvuka barabara.
Mwili wake ulifunikwa gubigubi kwa koti kubwa jeusi na kofia kichwani kwake ilipambana kuuficha uso wake. Haikuwa rahisi kuiona sura yake.
Mgongo wake ulibeba begi kubwa jeusi na mikono yake ilipakata mabegi makubwa ya wastani meusi pia, mabegi haya hayakuonekana kuwa na kitu chochote kile ndani yake.
Uso wake ulionyesha wasiwasi alipokuwa akikagua barabara huku na huko.
Haikujulikana kama ana haraka au ana hofu ya kupokonywa mabegi yake ambayo aliyashikilia barabara..

"Kichwa kile pale!"
Feruzi akakata kona kuelekea alipokuwa yule mwanaume mwenye mabegi.
Kwa mbaaali akamuona mwanaume mwingine amesimama kimya kaegemea mti

"Faza tuondokeee?! Hii hapa faza wapi hio?" Alianza kupaza sauti yake kabla hata hajamfikia.
Yule bwana akageuza shingo yake na kumtazama Feruzi kwa sekunde kadhaa, hakumjibu chochote.
Feruzi hakukata tamaa akaikokota pikipiki yake karibu zaidi,
Ikambidi atumie lugha ya kistaarabu labda angeushinda uamuzi wa huyu bwana.
"Baba yangu vipi nikupeleke?"

Bado bwana yule hakujibu kwa maneno, akatikisa kichwa chake kuashiria kwamba hakuitaji usafiri. Kimya! Na kwa utulivu mkubwa sana.
Akaendelea kutazama pande zote za barabara kwa hofu. Ilikuwa ni kama anasubiria usafiri wake binafsi ufike pale na kumchukua. Lakini jambo ambalo liliuvutia umakini wa Feruzi, ni ile wasiwasi yake usoni.
Na mbaya zaidi jasho lilianza kuulowanisha uso wake.

Feruzi, wakati huu akiwa amemkaribia kwa ukaribu zaidi. Akamtazama bwana yule vizuri.
Akawaza,
'Dah! Huyu faza, jamaa kavaa koti kubwa tena jeusi...halafu ana mabegi matatu meusi. Huyu anaenda wapi sa'hivi huyu?.
Lakini hawa nd'o huwa wana hela hawa. Em ngoja nimtongoze kwanza huyu dingi. Nalinusa buku tano hapa kabisa nje nje.'

"Baba yangu!",
Kwa upole na adabu zaidi Feruzi akajaribu kutumia maongezi yaliyotangaza heshima, huenda angeweza kumvutia huyu 'faza' awe abiria wake.
"Hapo ulipo nakuona kabisa umechoka baba yangu, au nakosea?"
Hakujibiwa. Lakini hata yeye hakusubiri jibu akaendelea,
"Una mizigo mingi mzee wangu, naomba basi kama hutojali. Nikusaidie tu kukufikisha huko unapoenda! Maana, sio jambo jema kwa mzee kama wewe kukosa usafiri na kijana kama mimi nipo. Ni kweli natafuta, lakini kwako wewe ngoja nikufanyie kama msaada tu baba yangu!"
Bwana huyu mfupi alimsikiliza Feruzi kwa umakini sana. Kisha kwa taabu sana akajipekua kwenye mfuko wa suruali lake akipambana na ukinzani wa koti alilokuwa amevaa na mzigo wake mkononi.
Feruzi akanyoosha mkono wake kumpokea begi,
"Ngoja nikusaidie begi mzee wangu".
Kitendo cha mkono wa Feruzi kulifikia begi lile tu, kwa kasi ya ajabu mzee yule akapakata begi lake kwapani kwa nguvu zaidi. Hakutaka kupokelewa mzigo ule.
Jambo lililomshangaza Feruzi.

"Ni sawa tu baba yangu, kama hutotaka nikupokee." Akajitetea Feruzi huku moyoni mwake akiwaza
'Ina maana faza anadhani mi ni kibaka au?'.
Mkono wa mzee yule ukaibuka na simu ndogo kutoka mfukoni. Huku akitetemeka, akaibofyabofya kisha akaiweka sikioni mwake,

"Haloooo! Eeeh njalii njaa...njali a Bukoba, m" Akakaa kimya.
Mshtuko kwa Feruzi, hii lugha hakuielewa kabisa.
'Lugha gani tena hii?'

Mzee akaendelea, tena kwa wakati huu woga ulimuongezeka mara dufu zaidi. Jasho likimiminika kama maji usoni mwake, midomo ikimtetemeka. Na mkono ulioshikilia simu ukitetemeka pia.
"Jibooookaa! Jibooooka!.....Kyamuneeene...ano ano. Suruyuuuwe."
Akakata simu ile. Akaangalia kwa mara nyingine tena barabarani huku na kule. Kisha akamtazama Feruzi,
"Kyamunene!...Turatiaaa...Kyamunene!"
Akatamka huku amemtazama Feruzi.

Feruzi akiwa bado kwenye ganzi ya butwaa, alipatwa na kigugumizi kumjibu huyu bwana. Hakujua kama alitajiwa sehemu ya kumpeleka au alikuwa anafundishwa hii lugha asiyoifahamu.
Alichokifahamu pekee ni mahali hapo alipopataja huyu bwana, Kyamunene.

Lilikuwa ni eneo la kitalii lililokuwa ndani ya pori kubwa lililojulikana kama Rubare. Lilipambwa kwa maporomoko ya maji na mapango makubwa.
'Hili ni eneo la kitalii, huyu faza anaenda kufanya nini na mabegi yote haya?' Feruzi alijiuliza.
Lakini aliamua kutojisumbua baada ya kugundua kuwa yeye ni dereva pikipiki na hapa alikuwa na kazi moja tu, kubeba abiria.
Masuala ya kujua abiria huyu anafuata nini kule, hayakumuhusu.

Sasa ikambidi Feruzi akubali kwa kutikisa kichwa pia na yeye akatamka,
"Kyamunene! Twende Kyamunene!" Akaongezea na ishara ya mkono kumuashiria yule bwana apande juu ya pikipiki yake, ameshatambua kuwa mtu anayezungumza naye haelewi kiswahili.

Kwa haraka sana, huyu mwanaume akaruka juu ya pikipiki na kuketi. Bado ameyakumbata mabegi yake kwa nguvu.
Feruzi akawasha pikipiki yake na kuanza kuelekea huko misitu ya Kyamunene.

Njiani, hakukuwa na mazungumzo baina yao. Feruzi alikipa kichwa chake maswali kibao ambayo majibu yake yalichelewa sana.
Alishindwa kabisa kumuelewa huyu abiria ambaye amempandisha kwenye chombo chake.
Lugha yake, mavazi yake na hofu iliyokuwa imemvaa. Vyote vilimchanganya.
Hata huyu abiria huku nyuma alionekana kama anacheleweshwa kule anakoenda. Jasho jingi lilimvuja.

Safari yao iliyodumu kwa takribani dakika 7 kwenye barabarani ya lami, halafu ghafla huyu abiria akaanza kutoa maelekezo.
Kwa lugha yake ileile isoyoeleweka;
"Anuu anuu!"
Alitumia maneno na vitendo kwa mkono wake.
Feruzi akakunja kona na kuhamia kwenye barabara ya vumbi iliokuwa korofi kwa mwendo wao.

Wakaanza kuingia katika barabara yenye kona nyingi zilizofichwa kwa majani marefu na vichaka, halafu wakaingia ndani ya msitu na wakati huu wakaiacha barabara iliyoonekana kama ilikuwa ikikanyagwa na watu.
Feruzi akaanza kupatwa na wasiwasi.
'Huyu Bushman anataka kuniingiza wapi tena? Mbona ananipeleka ndichi? Au hawa ndo wale wanaoiba pikipiki nini? Huyu hanijui huyu...' akawaza.
Walikuwa wanaingia kwenye vichaka vikubwa na hakukuonekana kuwa na usalama katika sehemu walipokuwa wakielekea. Hakuweza kuuliza wanapoenda angeuliza nini sasa wakati mtu mwenyewe aliongea lugha asiyoifahamu,
Ni kikongo, kinaijeria, kiyoruba...hakujua! Kwa hio yeye alimchukulia kama mzigo ambao anaupeleka mahali maalumu kwa maelekezo maalumu.
Alichokiwaza pekee kwa wakati huu ni hela. Hela tu basi!

Wakaendelea kuingia kwenye vichaka,
"Jadhulaaa, anooo anoooo!"
Yule mtu akampigapiga begabi kama kuashiria asimamishe pikipiki yake. Akasimama.

Yule bwana akashuka. Lakini kabla hajapekua mifuko ya suruali lake kutoa fedha ili amlipe, ghafla wakaibuka wanaume wawili kutoka vichakani ambao walikuwa wamevaa makoti makubwa meusi sawa na alivyokuwa amevaa yule mwanaume mfupi aliyeletwa na Feruzi.
Miili yao ilikuwa mikubwa. Mmoja akiwa amebeba koleo na panga kubwa lenye kutu. Na mwingine akiwa na shoka kubwa ambalo lilionyesha waziwazi kuwa linaweza kupasua kitu chochote kwa wakati wowote. Na wote miguuni mwao walivaa buti kubwa zilizochafuliwa kwa udongo mbichi wa mfinyazi, jambo lililowatambulisha kuwa walikuwa kazini!

Feruzi akawatazama usoni...nyuso zao hazikuonyesha dalili yoyote ile kuwa ziliwahi hata kufikiria kutabasamu tangu wazaliwe. Jambo lililowafanya waonekane kama madude ya kutisha!
Mmoja wa majitu yale ya kutisha akasogea haraka mpaka alipokuwa yule mwanaume aliyeletwa pale na Feruzi ambaye naye alionekana kuwa haelewi ni kitu gani kinaendelea. Likatupa panga lake lenye kutu chini.
"Unuyuuu? Ambi likijaaa mbanuu? Enhe?!!!" Likamuuliza huku limemnyooshea kidole Feruzi.
Liliongea kwa sauti nzito na hasira huku ndevu zake nyingi mithili ya stiliwaya zikipanda na kushuka kadri alivyotamka kwa sauti ile ya kutisha.
'Eboo?! Kumbe wanafahamiana hawa?' Feruzi akazidi kustaajabu.

Yule abiria akashusha mabegi yake chini, yungali anatetemeka...anaonekana anataka kujibu swali lile japo kigugumizi na woga vinamzuia.
Kofi kali likatua juu ya uso wake, likamfanya apepesuke kutafuta mhimili ili arejee kusimama wima tena.
"Ambiii likija mbanuu? Ambiiii?!!" Lile jitu likaendelea kumuuliza kwa hasira huku likilalamika. Bado mkono umenyoosha kidole chake kwa Feruzi. Feruzi amebaki akitazama tu huku mapigo ya moyo wake yakibadilisha kasi, yakaamua yaanze kwenda mbio. Ameshagundua kuwa yuko sehemu ambayo hakuitajika!

Ghafla! Jitu lilitumia sekunde mbili tu kumchota yule mwanaume kwa mtama mkali, ambao ulimuacha hewani kwa nusu sekunde na kabla hajatua ardhini akapigwa ngumi kali ya kifua.
Ngumi ambayo kama haikuuhamisha moyo kutoka sehemu yake basi ilinuia kumpasua kifua chake.
"Aaargh!" Akapiga kelele na kutua chini PUUH! Kama mzigo.
Akalala chali chini huku akiunguruma taratibu. Amekufa kwa kupasuka kifua? Amezirai? hata hatujui.
Halafu jitu lile likamgeukia Feruzi ambaye alikuwa bado juu ya pikipiki akisubiria malipo yake.

Ndugu msomaji,
Hebu mshauri Feruzi afanye nini baada ya kuona madhara yaliyomkuta abiria wake. Aendelee kusubiri nauli yake? Au arudi tu town aendelee kusaka wateja? Eti jamani...tumshauri ndugu yetu Feruzi Kinyozi.

Unaweza kukisia hofu ambayo Feruzi alikuwa kwa wakati huo. Kipigo alichopokea abiria wake, kikamuacha na maswali mengi zaidi ya kumuogofya!
Feruzi akawaza mambo mengi sana, akilini.
'Hawa ni majambazi wanaofahamiana au ni kina nani hawa?'
Hata mwili wake ukashtuka, ikawa ni kama vipepeo vinarukaruka tumboni, koo likakauka na miguu ikamuishia nguvu.
Kama yule wanayefahamiana naye wamemfanya vile, itakuwaje kwake yeye wasiyemfahamu?

Lile Jitu likaokota panga na likamsogelea Feruzi huku pumzi zikipishana kwa nguvu kwenye pua zake kwa hasira. Na macho yake yakageuka kuwa kama ya mnyama wa kutisha kuashiria kuwa linaenda kumtenganisha vipandevipande.
Ni msituni! Apige kelele kwa nani kuuita msaada? Labda wewe msomaji unayemuona kwa fikra zako. Atauwa na haya majitu na hatojulikana ni wapi alipo. Hakuna namna ambayo angalau vipande vyake vitaokotwa na kuzikwa.
Alikiona kifo na hakuwa na namna ya kujitetea!

Itaendelea
 

Attachments

  • 490d008a.jpg
    490d008a.jpg
    1.7 MB · Views: 1
SHAMBA LA HELA
SEHEMU YA TATU;

MTEKAJI-MTANASHATI

MWILI wake ulizizima!
Ardhi iliitikia kwa kutoa mtetemo kwa kila hatua ambayo jitu lile lilikanyaga juu yake. Ilikuwa ni kama inalalamika juu ya uzito wa mwili wake yule bwana.
Mkono wake wa kuume uliobeba lile panga kubwa lenye kutu ulikuwa imara, na tambo la mwili wake lilikuwa la kutisha sana.

Feruzi alikosa cha kufanya. Cha maana zaidi alichokifanya ni kuzima pikipiki yake na kusubiri kuona yule bwana amenuia kumfanya nini. Mana kama ni kumuua, asingeweza kujitetea kwa lolote dhidi ya majitu haya mawili yanayotisha tena katikati kwenye pori hili kubwa.
Akiwa anatetemeka akajikuta anapambana sana kuuzuia mkojo wake lakini hata mfumo wa utoaji taka mwili nao haukumuacha salama! Akajikojolea..

"Shikaa..shikamooo!", akajikuta akitoa salamu ya kwanza tangu afike katika eneo hili ambalo kwa sasa lilimuonesha waziwazi kuwa ni ardhi ambayo atazikwa.

Lile jitu likamkaribia zaidi...
"Marahaba!". Likaijibu salamu kwa maneno kisha likafuatisha kwa vitendo huku likiutumia mkono wake wa kushoto kuushika ukosi wa koti la Feruzi na kuubana kiasi kwamba shingo yake nayo ikahusika kwenye mbano huu.
Kwa kutumia nguvu kiasi likamnyanyua juu na kumuondoa kwenye pikipiki yake kisha likamtupa ardhini huku pikipiki nayo ikianguka.

Yule mtu mkubwa aliyefanania na jitu akamtazama Feruzi pale chini huku akihema kwa hasira...macho yake yakimpa maswali magumu Feruzi ambayo asingeweza kuyajibu.

"Aah wewe ni nani? Na umefuata nini huku?!" Likamuuliza.
"Mi...mimi ni bodaboda tu mkuu, nime...nimeml..nimemleta abiria yule pale...!"
Feruzi akajibu kwa sauti iliyochanganyikana na kigugumizi, hofu na vikohozi vya nukta. Akitarajia kuwa huenda ataonekana kuwa hausiki na ataachiwa huru aende zake.
Lile jitu likageuza kichwa na kumtazama mwenzake ambaye alikuwa kimya akiwatazama tu, kisha likamrudia tena Feruzi ambaye alikuwa akitetemeka kwa woga pale chini.
Likabonyea chini na kupiga goti moja, kisha likaikita ncha ya panga lake ardhini na panga likanata kwa kutulia. Ukimya wa kutisha ukatawala!
Kwa kuliegemea kidogo panga lile likamkaribia Feruzi na kumuuliza,
"Una muda gani kwenye tasnia ya maigizo?"

Sauti yake haikuwa na dalili yoyote ya utani au kicheko...alikuwa makini na alimaanisha alichokizungumza. Lakini kauli hii iliwasha taa ya hatari kwa Feruzi, kuwa haaminiki.

"Hapana bro! Hapana mimi siigizi kweli kabisa...nime...nime nimemleta baba yule pale..kanambia nimelete huku misitu ya Kyamunene... sa'ndo njiani akanielekeza mpaka hapa!" Feruzi akajitetea kwa sauti yenye machozi, kisha akaendelea.

"Tafadhali msiniue...naomba sana mkuu, mimi..mimi sina lengo baya sijui chochote..ni bodaboda tu.."

"Ni nani amekuambia anataka kukuua?" Jitu likamtupia swali.
Feruzi akatoa macho, hakuwa na jibu. Akashuhudia jitu lile likichomoa panga lile kutoka ardhini na kulinyoosha kwa Feruzi.

"Tungetaka kukuua tungekuwa tumeshafanya hivyo mapema sana...sekunde kumi zilizopita."
Likaweka kituo na kumtazama Feruzi.
Ukimya huu ukawa ni kama muendelezo wa hofu tu kwa Feruzi, kisha likaendelea,

"Lakini hilo halimaanishi kwamba hatutakuchinja hapana...tutakuua dakika chache tu zijazo, endapo tunachokifikiria juu yako kitakuwa kweli!". Likakaa kimya tena.

Ukimya huu ukawa ni kama umempasia kipaza yule mwenzie aliyekuwa amesimama kando. Yeye akakohoa kidogo kisha akasema,
"Tumekusikia ukimshawishi huyu mzee kwa nguvu sana, na ukambeba mpaka hapa!
Haya sasa tuambie haraka wewe ni nani? Na ni nani amekutuma!"

Sauti zao nzito na za kutisha zilifanana, na zote mbili hazikuwa na masihara kabisa. Feruzi akawa mdogo, akanywea na kuwa mpole. Akatambua kuwa yuko katikati ya wauaji. Madirisha ya macho yake yakafunguka na mifereji ya machozi ikaanza kumtiririka,
Taratibu akapiga magoti kwa unyonge, akaifumbata mikono yake kama mtu anayejiandaa kusali kisha akatamka,
"Jamani...mimi sihusiki kwa lolote. Mimi ni bodaboda wa kawaida kabisa! Sekido masikini kabisa. Niacheni tu niende. Nihurumieni jamani!"

Watu wale wawili bado wako kimya...sura zao komavu ziliendelea kumtazama tu na angalau basi zingempa matumaini kuwa ataonewa huruma, lakini zikamkatisha tamaa.
Hazikuonyesha kuwa zina tabia ya kuvaa vazi lolote lile lililoshonwa kwa nyuzi za huruma wala msamaha.
Kwanza sura zao zilikuwa na makovu, ambayo yalionyesha kuwa hata wao dunia haijawahi kuwahurumia. Sasa ni huruma gani aliitaka Feruzi?

"Yaani tumekusikia unamwambia mzee wetu kuwaa..unataka kumfanyia hisani ya bure tu...umelete hapa bure! Halafu unasema we ni bodaboda masikini? Umasikini gani huo ambao unakupa utu wa kuwapa lifti abiria usiowafahamu na kuwasafirisha maili nyingi mpaka huku kwenye mapori ya kutisha! Mmh? Nijibu..."

Ndugu msomaji, kama umewahi kupatwa na msisimko wa ghafla ambao ulikudai maji ili kupoza koo lako, basi mfikirie ndugu yetu Feruzi kidogo.
Alibaa!
Koo likamkauka! Akashindwa kujibu chochote kile.

"Halafu ulivyo fala! Njiani ukawa unasema etii...huyu faza hanijui! Ngoja nitamuonyesha! Haya ulitaka kumwonyesha nini huyu mzee? Eeh tuambie...ulitaka kumwonyesha nini?
Au ni kwa vile haelewi Kiswahili...ukaona unaweza kutumia fursa? Eeh?"
Akazidi kupangiliwa orodha ya maswali ambayo yalimuwia magumu mno kujibu.
Swali moja tu lililokuwa kichwani mwake,
'Wamejuaje hawa?'
Kwa mara ya kwanza maishani mwake, Feruzi akakubaliana na ule msemo unaosema
"MDOMO ULIKIPONZA KICHWA!"
Angejibu nini?

Lile jitu lililokuwa karibu yake likashusha pumzi. Kisha likamtazama mwenzie,
"Nadhani tumpeleke kwa mkuu yeye atajua tumfanye nini."
Yule mwingine akatikisa kichwa kukubali.

"Haya simama!" Hii ilikuwa amri ambayo kabla hata haijamalizika tayari Feruzi alikuwa kasimama haraka.
Bwana yule akatoa kamba kubwa na kuifunga barabara mikono ya Feruzi. Kisha akachukua mfuko mkubwa mweusi akamvalisha Feruzi kichwani, asione anakokwenda.

Yule mwingine akajipa jukumu la kujitwika mwili wa yule mzee aliyekuwa amezimia. Wote wakashika ujia mdogo ulioingia katikati ya pori lile. Feruzi akiongozwa njia kwa kuburuzwa na kupigwa na ubapa wa panga ili asipoteze muda.
Mwendo wa mateka!

**********

Ulikuwa mwendo wa dakika ishirini za kujikwaa kwenye visiki, kuanguka na kuamka, kupigwa makofi mazito ya mgongo na kusukumwa ili mradi tu Feruzi aongeze mwendo.
Hatimaye wakafika sehemu ambayo aliambiwa asimame. Akasimama na ule mfuko mweusi ukatolewa kichwani mwake haraka...
Mwanga ukayaumiza macho yake yaliyokuwa yamelizoea giza kwa dakika zote hizo, akayafumba ili kupunguza maumivu yale.

"Kaa chini!"
Akapewa amri ambayo ilisindikizwa kwa kofi zito lililotua juu ya mgongo wake. Kofi lililomkohoza kidogo. Akakaa chini bado mikono yake imefungwa kwa nyuma.

Macho yake yalipouzoea mwanga kidogo, akajaribu kuitazama sehemu ile kwa umakini. Macho hayakumfanyia ajizi, yakamtaarifu kuwa yuko katikati ya msitu mkubwa asioufahamu na yuko na watekaji ambao wanaweza kuiondoa roho yake mara moja kama tu watataka kufanya hivyo. Akaogopa!

Lakini macho yake yakavutiwa sana na mandhari ya eneo lile alipokuwepo. Ndio, ni kweli alikuwa katikati ya msitu! Lakini hapa palikuwa pa kitofauti kidogo.
Lilikuwa eneo kubwa lililo wazi limezungukwa na miti mikubwa, kiasi cha kutengeneza kiwanja kikubwa cha kadri chenye umbo la duara mahali pale.
Ardhi ya eneo hilo ilikuwa imetifuliwatifuliwa na ilionesha kuwa ni aidha imetoka kuchimbwa mda sio mrefu au ina imeshazoea kuchimbwa na kutifuliwatifuliwa mara kwa mara.
'Mungu wangu! Hawa majambazi wataniua halafu watanizika hapa!!' Mawazo ya hofu yakamkumbusha hatari iliyokuwa mbele yake. Akashindwa kujizuia...akaanza kulia. Lakini alipotazama vizuri mbele yake akakutana na kiwiliwili cha mtu ambaye alikuwa amesimama na ameweka mikono yake nyuma akajitahidi kumtazama.

"Unaitwa nani wewe? Na ni kwa nini unatufatilia?!". Sauti tulivu ya mamlaka ikasikika kutoka kwenye kiwilkwili kile. Hii ilikuwa sauti ngeni kabisa, masikio yake hayakuwa yamewahi kuisikia.

Akamuona na mwanaume mtanashati aliyevaa suti nzuri nyeusi ya gharama. Miwani nyeusi ikiyaficha macho usoni mwake. Ni mtulivu na mikono yake akiwa ameifumbata nyuma, ni kama ambaye alikuwa ameficha kitu.

"Eeh? Mimi ni bodaboda wa kawaida jamani, kiongozi naomba mniache tafadhali! Niache niende tu. Sihusiki kwa lolote" Feruzi akaendelea kutamka sentensi zilezile zenye kilio. Tena kwa wakati huu alipomuona huyu bwana mtanashati akategemea labda huyu atamuhurumia kuliko yale majitu ya kutisha yenye miili mikubwa.
Yule bwana akakohoa kidogo kisha akatamka,
"Unaitwa nani? Na ni kwa nini unatufatilia!" Sauti yake ni tulivu sana, anaongea kwa mamlaka na inaonesha kuwa yeye sio muumini wa maongezi marefu yasiyo na mantiki.
Kwa kigugumizi kilichochanganyikana na hofu Feruzi akajibu,
"Feruzi anko!...Naitwa Feruzi! Mimi ni kinyozi kuleeee Buyekera kulee" akataja jina lake, akataja na wadhifa wake kwenye jamii. Bado anaitafuta batani ya huruma kwenye moyo wa huyu bwana ambaye hivi sasa angemuita mtekaji-mtanashati.

Sekunde mbili tu baada ya kumaliza sentensi yake, akashuhudia jitu mojawapo limemrukia na kushusha kofi zito usoni mwake ambalo lilimfanya apepesuke na kuona nyota zenye rangi tofauti tofauti.
"Kwani we ni mbwa?! Eeh? We una jina moja umekuwa mbwa?"
Jitu lile likabweka kwa hasira, mzuzu wa ndevu zake chafu ukicheza huku na huko kumuuliza Feruzi ambaye bado alikuwa anajiuliza kama amepigwa na kofi, radi au shoti ya umeme. Bado alikuwa hajielewi.

"Dubu!! Muache....achana naye" yule bwana akamuamuru lile jitu liachane na Feruzi. Likatii likiwa bado linahema kwa hasira, limetoa macho linaonyesha waziwazi kuwa limezoea shari...na anayefanyiwa shari yupo hapa.

"Naitwa Adam Feruzi Adam." Feruzi akajibu kwa sauti chovu, bado akili yake haijakaa sawa, baada ya kupokea pigo kwenye kiganja cha lile jitu, lililojulikana kama Dubu.

Yule bwana akapiga hatua tano mpaka mbele ya Feruzi aliyekuwa ameketi chini bado,kwa kila hatua aliyoipiga alitumia msaada wa fimbo iliyompa mhimili. Alikuwa akichechemea kidogo. Feruzi akaendelea kumtazama tu. Akili yake ikamkumbusha zile filamu za vikundi vya magaidi na wauaji. Na wale mafia aliowahi kuwasikia kwenye simulizi na filamu mbalimbali.

Yule bwana akachuchumaa kwa msaada wa fimbo yake akamtazama Feruzi akashusha pumzi kisha akatamka,
"Nisikilize Adam! Kazi yako wewe ni ipi? Dereva bodaboda au kinyozi? Eeh niambie kazi yako we ni ipi?"...sauti yake ikaanza kubadilika kutoka kwenye utulivu ikaanza kunukia hasira na jaziba.
Lakini hayo hayakumfikirisha Feruzi hata kidogo, alichokifikira muda huu ni kosa lake jingine la kuchanganya majibu yake yeye mwenyewe,
Kawaambia ni dereva bodaboda halafu tena kajitambulisha kama kinyozi. Kafanya makosa mbele ya watu wabaya! Akajua kuwa kwa namna yoyote ile hawawezi kumuacha.
Machozi yaliyokuwa yamemkauka yakachukua nafasi yake tena, akarejea tena kwenye kitendo cha kulia.

"Miongoni mwa vitu ambavyo navichukia sana ni kuona machozi ya kinafiki! Tena kwa dume kama wewe uliyekomaa." Kauli hii ikakiyeyusha kilio cha Feruzi, kikapotea na sura yake ikavaa ukimya. Ukimya uliopambwa kwa wasiwasi.
"Mkuu, mimi ni kinyozi pale mtaani kwetu. Lakini nimeazima pikipiki ya rafiki yangu ili nipate walau hela kidogo mkuu! Hivyo tu."

Yule bwana akainamisha kichwa chake kwa huzuni kisha akasema,
"Hela! Unatafuta hela! Ooh Adam. Hela! Hela! Hela!" Akatoa miwani yake usoni kisha akamtazama tena Feruzi.
Uso wake haukuwa wa kawaida, ulitisha!
Alikuwa chongo, kovu kubwa lilipita katikati ya jicho lake la kulia na kuliharibu vibaya sana, lilikuwa ni kama linalotoa machozi muda wote. Uso wake pia ulionesha kuwa hata yeye amepitia mateso na adha mbalimbali katika maisha. Jambo lililozidi kumkatisha tamaa Feruzi kuwa asitegemee aina yoyote ile ya msamaha jioni hii ya leo.

Yule bwana akatazama ardhini na kuanza kutamka peke yake,
"Tulikukosea nini fedha?! Ni kwa nini unatutesa namna hii? Watu wanakutafuta kila kukicha na bado unaishia kuwaingiza shimoni. Kwa nini lakini? Hela! "
Akakaa kimya kisha akatoa leso kwennye mfuko wa koti lake na kulifuta chozi kwenye jicho lake lenye chongo.
Kisha akamtazama tena Feruzi kwa sura yenye udadisi.
Wakati huo Feruzi akawa amepagawa kwa maneno ya huyu bwana ambaye anailaumu fedha ambayo hata haioni na hata haiwezi kumsikia.

"Adam Feruzi Adam! Jina zuri sana... wewe ni kijana mwema sana, nadhani hata kama nikikuua, mbingu zitafurahi sana kukupokea. Eti Adam au nakosea?"
Maneno 'hata kama nikikuua, mbingu zitafurahi sana kukupokea' yakamtisha sana Feruzi. Akajua kuwa sasa hana muda mwingi sana pale porini atakufa!

"Si huwa mnasema kuwa Mungu amempenda zaidi marehemu? Sasa kama Mungu anakupenda unafanya nini hapa duniani. Dunia mbaya ambayo imechafuliwa kwa shetani anayeitwa fedha! Hela!" Yule bwana akazidi kutamka kwa sauti tulivu lakini iliyotangaza hasira.

Feruzi bado yupo kwenye mshangao, hakujua kama hawa viumbe watatu waliomzunguka wana akili timamu au la! Alianza kumvua vyeo vya heshima huyu bwana mwenye suti, maana aliyoyaongea na muonekano wake havikufanana hata kidogo.
Ni mtu gani ambaye anaweza kuilaumu hela? Tena kama vile anaongea nayo tu uso kwa uso. Feruzi akajihakikishia kuwa hakika huyu bwana ni punguani.

"Lakini wewe leo umekosea njia Adam Feruzi, umekosea njia mdogo wangu. Na wala sikulaumu kwa hilo! Lakini huyo jamaa mrugaruga nd'o amekupoteza njia." Akamnyooshea kidole yule bwana mfupi, abiria aliyeletwa pale porini. Alikuwa ameamka tayari japo anaonekana amedhoofu kutokana na pigo kali alilopokea nusu saa tu iliopita. Mtekaji-mtanashati akaendelea,
"Najua kuwa huoni kama utaokoka leo, na ni kweli hutaokoka. Hii siku itayabadilisha maisha yako Adam. Unatafuta hela?!
Hujui kuwa hela inasababisha kifo? Eeh...hujui Adam? Hela inaua.." Akamuuliza.

Sasa Feruzi akapigia mstari imani yake juu ya kifo chake, akaona ni kama wanampa nafasi ya kutoa neno lake la mwisho kabla ya mauti.
"Makusudio yangu juu yako yamekuwa tofauti. Lakini ngoja nikupe darasa kidogo Adam, em tazama hela inavyoweza kuua. Ngoja Adam em tazama tazama ninachokifanya!"
Akasimama kwa taabu akijitahidi kujiegemeza kwa ile fimbo yake...

Fimbo ambayo ilikuwa na sanamu la kichwa cha simba kwenye mshikio wake, ishara nyingine ya kuwa huyu bwana sio mtu wa kawaida!
Akamsogelea taratibu huku akichechemea, mwanaume yule pale chini akamtazama huku macho yake yakidai huruma. Yule bwana mwenye suti akamtamkia maneno fulani ya lugha ileile ambayo ilikuwa ya kikabila. Lugha ambayo inaonekana wanaifahamu wao tu, isipokuwa Feruzi.
Yule bwana akamjibu kwa lugha ile ile, machozi yakiulowanisha uso wake. Yule mtekaji-mtanashati akanyanyua fimbo yake na kuivuta kama anaifuta, akachomoa upanga uliokuwa ndani ya fimbo ile halafu bila kusita kama utani tu.

Akauvurumisha upanga ule hewani kama mtu anayejiandaa kufyeka kitu. Kisha akaushusha chini kwa nguvu juu ya kichwa cha yule bwana abiria. Kufumba na kufumbua, damu ziliruka hewani kama maji ya bomba lililopasuliwa.

Kiwiliwili cha mwili kikadondoka upande wa kulia na kichwa kikadondoka upande mwingine. Lilikuwa tukio lililochukua sekunde tatu tu. Yule abiria aliyeletwa pale akawa tayari amekuwa historia!
Akauawa kwa upanga. Ilikuwa kama utani tu!
Feruzi anashuhudia kwa mauaji mubashara kwa mara ya kwanza kwenye maisha yake.

Mauaji ambayo alizoea kuyaona kwenye filamu tu. Lakini leo hii akayaona kwa macho yake ya nyama.

ITAENDELEA....
 
Back
Top Bottom