Riziki Shahari Mngwali (ACT Wazalendo): Tunataka Wahadhiri waliokamatwa waachiwe huru mara moja

Riziki Shahari Mngwali (ACT Wazalendo): Tunataka Wahadhiri waliokamatwa waachiwe huru mara moja

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
5,352
Reaction score
15,876
WhatsApp Image 2026-07-21 at 11.18.14.jpeg


View: https://www.youtube.com/live/v5iSJl0zCvA?si=7kTwypJn-40quhtu
​

ACT Wazalendo imefuatilia kwa karibu matukio ya kukamatwa kwa wahadhiri wa vyuo vikuu mbalimbali nchini na inalaani hatua za kuwakamata wanataaluma hao katika mazingira yanayoibua maswali kuhusu uzingatiaji wa taratibu za kisheria na ulinzi wa uhuru wa taaluma nchini.

Pia soma, Maagizo kutoka juu, yamfanya Mhadhiri UDOM kusota mahabusu

Katika kipindi cha hivi karibuni, wahadhiri kadhaa wamekamatwa, kuhojiwa na kufunguliwa mashitaka kwa tuhuma zinazohusiana na kauli na maoni yao wanapotekeleza majukumu yao ya ufundishaji. Miongoni mwao ni Ndg. Melkzedeki Kaijage wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), pamoja na Ndg. Johaiven Revelian Bikongolo na Ndg. Titus Joseph Kituli wa Chuo Kikuu cha St. John Tanzania (SJUT), waliokamatwa tarehe 3 Julai 2026.
WhatsApp Image 2026-07-21 at 13.41.00.jpeg
WhatsApp Image 2026-07-21 at 13.40.59.jpeg
Kwa taarifa tulizonazo hadi sasa, wahadhiri hao walikamatwa bila kufuata taratibu zinazotakiwa za kuwashirikisha waajiri wao na wameendelea kushikiliwa kwa muda mrefu bila kuachiwa huru. Hali hii inaibua wasiwasi mkubwa kuhusu matumizi ya vyombo vya dola katika masuala ambayo yanapaswa pia kuzingatia mamlaka na taratibu za ndani za vyuo vikuu.

ACT Wazalendo inakumbusha kuwa vyuo vikuu vina mifumo yao ya kushughulikia masuala ya kitaaluma na kinidhamu kupitia idara, vitivo na Seneti. Pale ambapo kuna tuhuma zinazomhusu mhadhiri katika utekelezaji wa wajibu wake wa kitaaluma, ni muhimu taratibu hizo kuheshimiwa ili kulinda uhuru wa vyuo vikuu na wanataaluma.

Ikumbukwe kuwa wakati wa tukio la kukamatwa kwa Ndg. Melkzedeki Kaijage mwezi Disemba 2025, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda alisisitiza umuhimu wa kulinda uhuru wa wanataaluma na mamlaka za vyuo vikuu katika kushughulikia masuala yanayowahusu wahadhiri. Waziri Mkenda alinukuliwa akisema:

"Mhadhiri akiwa darasani yuko huru kufundisha. Kama kuna kitu kina ukakasi katika ufundishaji basi Polisi haina mamlaka ya kumkamata bali atachunguzwa na mamlaka ya chuo husika; Mkuu wa Idara, Mkuu wa Kitivo, Makamu Mkuu wa Chuo na Seneti."

Kauli hiyo ilikuwa na umuhimu mkubwa katika kulinda misingi ya uhuru wa kitaaluma na mamlaka ya vyuo vikuu. Hata hivyo, mwenendo unaoendelea wa kuwakamata wahadhiri bila kufuata taratibu hizo inaendelea kuonesha kuwa bado taifa letu linaendeshwa na mabavu ya dola ndio maana kauli hiyo, sherisa na taratibu zinaendelea kupuuzwa.

Hivyo, ACT Wazalendo tunataka wahadhiri wote waliokamatwa, Ndg. Melkzedeki Kaijage, Ndg. Johaiven Revelian Bikongolo na Ndg. Titus Joseph Kituli, waachiwe huru mara moja bila masharti. Endapo kuna masuala yoyote ya kitaaluma au kinidhamu, yashughulikiwe kwa mujibu wa taratibu za vyuo husika zinazolinda mamlaka na uhuru wa taasisi hizo.

Aidha, tunamtaka Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda kutoa maelezo hadharani kuhusu hatua ambazo serikali imechukua kuhakikisha kuwa matukio ya kuwakamata wahadhiri bila kuzingatia taratibu yanafikia mwisho na kwamba uhuru wa taaluma unalindwa nchini.

ACT Wazalendo inatoa wito kwa wadau wote wa elimu, taasisi za kiraia na wananchi kwa ujumla kusimama pamoja kulinda mazingira ambayo yanaruhusu wanataaluma kutekeleza wajibu wao kwa uhuru na kwa maslahi ya taifa.

Serikali inapaswa kufahamu kuwa maendeleo ya taifa hayawezi kujengwa kwa kuwanyamazisha wataalamu na kuzuia mijadala ya kitaaluma. Taifa linahitaji vyuo vikuu huru vinavyozalisha maarifa, tafiti na suluhisho kwa changamoto zinazolikabili.

Imetolewa na:
Ndg. Riziki Shari Mngwali
Waziri Kivuli wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
ACT Wazalendo
21 Julai 2026
 
Back
Top Bottom