Rostam Aziz ajiuzulu, Mwananchi yatangazawa bodi mpya
Rostam Aziz, ambaye amejitoa katika bodi ya wakurugenzi wa Mwananchi Communication Ltd (MCL) baada ya kuuza hisa zake zote
Na Mwandishi Wetu
BODI ya wakurugenzi ya kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), ambaoni wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen, imetangaza uteuzi wa wakurugenzi huru wanne.
Wakurugenzi hao ni Profesa Palamagamba Kabudi, Zuhura Sinare Muro, Mohammed Rweyemamu na Abdulsultan Jamal. Wote wamejiunga na bodi ya MCL kuanzia jana na wote kwa ujumla historia yao kielimu inahusisha uandishi wa habari, uhandisi, rasilimali watu na masuala ya biashara.
Kuteuliwa kwao ni kutengeneza mfumo mpya wa kampuni baada kujiuzulu kwa Rostam Aziz na Balozi Ferdinand Ruhinda, ambao wameuza hisa zao kwa kampuni ya Nation Media Group.
Wengine ambao wamejiuzulu kwenye bodi ya MCL ni Wangethi Mwangi na James C. Kinyua wote wakitokea kampuni ya Nation Media Group.
Kampuni mama ya MCL ambayo ni kampuni tanzu ya Nation Media Group, inao wakurugenzi wawili katika bodi hiyo ambao ni Afisa Mtendaji Mkuu (CEO), Linus Gitahi na Mkurugenzi wa Fedha, Stephen Gitagama, kati ya wakurugenzi saba wa bodi ya MCL.
Akitangaza uteuzi huo jijini Dar es Salaam, mwenyekiti wa bodi ya MCL, Ali Mufuruki alisema: Tunafurahi kuwapata Watanzania waliojitolea kujiunga na bodi ya Mwananchi Communications. Limekuwa lengo letu kuunda bodi ya wakurugenzi ambayo ni yenye, uhuru, heshima na uwezo wa kimawazo, jinsia na historia yenye utaalamu.
Aliongeza kusema: Kuwa na Watanzania watano ambao ni wakurugenzi huru, ikiwa ni pamoja na mwenyekiti na wakurugenzi wawili kutoka Kenya, Mwananchi ina mrengo wa juu katika katika taaluma na biashara ya habari, kitu ambacho ni habari nzuri kwetu.
Prof. Kabudi, 51, ambaye ni mhadhiri mwandamizi wa kitivo cha sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ni mwandishi wa habari wa zamani ambaye pia ni mmoja wa wakurugenzi wa Bodi ya Baraza la Mazingira Tanzania (NEMC) na pia mjumbe wa bodi ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC). Ameandika zaidi ya vitabu 50 na taarifa za utafiti mbalimbali na ni mwenye ujuzi mkubwa katika ushauri.
Muro, 47, ana utaalamu wa uongozi wa rasilimali watu, na ni mwenye ujuzi mkubwa katika biashara za ndani, siasa ya jamii na uchumi wa mazingira kwa Tanzania na nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara.
Alikuwa mkuu wa kitengo cha uajiri cha kampuni ya simu ya Celtel, ambayo imebadilishwa jina na kuwa Zain, na pia ni mkurugenzi na katibu wa mfuko wa uongozi wa Afrika katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Rweyemamu, 50, ni mshauri wa masuala ya uhandisi wa kujitegemea na ana shahada ya uzamili ya sayansi ya uhandisi wa mitambo. Hivi sasa ni Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa kampuni za MEX ambazo zinashughulika na kukodisha vifaa vya ujenzi.
Mkurugenzi mpya wa nne ni Jamal, ambaye ni mfanyabiashara wa siku nyingi ambaye amehusika katika makampuni mbalimbali. Anahusika na biashara za samani, ujenzi wa nyumba na anahusika sana katika masuala ya jamii.
MCL ni kampuni dada ya Nation Media Group, ambayo makao makuu yake yako jijini Nairobi nchini Kenya.
source :
Mwananchi Tanzania News Paper