Samahani kwa kutoka nje ya mada...Lakini nitaeleza ni kwanini.
Hiyo hotuba hapo chini...Mtanzania kama atakumbuka niliyasema maneno yote hayo hapo chini kwenye mjadala mmoja juzi kama sikosei pale nilipogusia kuhusu AGOA.
Kuhusu sisi kuuza raw materials na pia kutotumia mpango wa AGOA na EPZ.
Sasa ndugu zangu ni kweli huyu mtu hana washauri!
Haya anayoyasema hapo chini ni mambo ambayo wasaidizi wake wangetakiwa kuyafanya...Lakini badala yake wanamwachia yeye kila kitu? Tena hata kuwaambia wananchi kuhusu opportunities zilizoko?
Sasa kama kweli wangekuwa wanafanya kazi zao vizuri...Mipango hiyo ingeshatekelezwa na si kusubiri rais awakumbushe kila siku majukumu yao!
Hawa watu hadi Ngurdoto kwenye seminar lakini hawakuingiza AKILI!
Sasa na hii mikataba waliyosaini badala ya kuwachungulisha dili wananchi wao wako kwenye maslahi yao na ndio maana ni NOMA!
Kwenye highlights ndipo haswa palipogusiwa PAMOJA NA MENGINE KAMA NILIVYOSEMA KWENYE MJADALA ULE WA VIWANDA KUWA KINACHOTUKWAMISHA NAMBA MOJA NI UMEME.
JK: Wafanyabiashara msiuze bidhaa ghafi, ziongezeeni thamani
2008-07-14 09:31:31
Na Joseph Mwendapole
Rais Jakaya Kikwete, amewataka wafanyabiashara Watanzania, kuziongezea thamani bidhaa wanazozalisha badala ya kuziuza zikiwa ghafi.
Aliyasema hayo jana wakati wa kutoa tuzo ya Rais ya wazalishaji bora wa mwaka 2008, iliyoandaliwa na Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini (CTI).
Alisema tabia ya kuuza bidhaa zikiwa ghafi, ndiyo inaifanya Tanzania kuendelea kuwa maskini na wanaonunua bidhaa hizo ghafi kutajirika baada ya kuziongezea thamani.
Rais Kikwete alitoa mfano wa watu wanaouza pamba nje wanawanufaisha zaidi wanaonunua kwani hutengeneza bidhaa na kuzirejesha tena nchini ambapo huuzwa kwa bei kubwa.
``Badala ya kuuza pamba nje kwa nini usiuze nguo, maana kilo moja ya pamba inaweza kutengeneza mashati mawili, tanzanite ghafi yenye thamani ya Sh. milioni 20 wenzetu wanaiongezea thamani na wanapata zaidi ya Sh. milioni 300,`` alisema.
Aliwataka pia wafanyabiashara kutangaza bidhaa zao nje ya nchi kwani kwa kufanya hivyo watapata masoko mengi na aliwashauri wasiogope gharama za kujitangaza.
``Tuache tabia ya kunung`unika bila sababu na tufanye mambo, kujitangaza wengine wanasema ni ghali sasa hakuna cha bure, na mkiendekeza vya bure nawaambia hamtakua, mtabaki hivyo hivyo,`` alisisitiza Rais Kikwete.
Aliwataka pia kufanya mambo yao kwa malengo na kwamba bila kufanya hivyo wanaweza kudhani wamefanikiwa kumbe hakuna walichopata.
Aliwashauri wajitahidi kuongeza mauzo ya bidhaa zao nje ya nchi angalau kwa asilimia kumi kila mwaka na kuongeza kuwa nchi zote zilizoendelea uchumi wake umekua kutokana na kuuza zaidi nje ya nchi.
Alisema hata soko la Afrika Mashariki ni kubwa la wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa zao hawatozwi ushuru na kwamba hata vikwzo vilivyokuwepo awali vimeshaondolewa.
``Masoko yapo jamani, Ulaya, Marekani wametupa fursa kupitia mpango wa Agoa tunaingiza bidhaa zaidi ya 5,000 bila ushuru, kinachotakiwa tuongeze thamani bidhaa zetu tuzitangaze na tuache tabia ya kunung`unika nung`unika haitatusaidia chochote,`` alisema.
Aidha, aliongeza kuwa, serikali inatambua kero ya miundombinu ya barabara na umeme na kwamba inajitahidi kuhakikisha inaiboresha ili wenye viwanda wafanye biashara zao katika mazingira mazuri.
Alisema anatambua kuwa umeme ni kilio kikubwa kwa wenye viwanda nchini na serikali itajitahidi kutumia rasilimali zilizopo kuhakikisha umeme unazalishwa kwa bei nafuu.
``Hii Sheria mpya ya umeme italeta ushindani mkubwa katika uzalishaji umeme, wawekezaji watakuwa na uwezo wa kuzalisha, kusambaza na kuuza umeme hivyo ni dhahiri gharama zitashuka,`` alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda CTI, Bw. Reginald Mengi, naye alizungumzia umuhimu wa wafanyabiashara Watanzania kuongezea thamani bidhaa zao badala ya kuziuza zikiwa ghafi, ambapo hupata bei ya chini.
Bw. Mengi alisema alitoa mfano kuwa bei ya kilo moja ya kahawa ambayo haijaongezewa thamani ni Dola za Marekani 1.5 , wakati ile iliyoongezewa thamani inaweza kuuzwa hadi Dola 15 za Marekani.
Alimshukuru kipekee Rais Kikwete kutokana na busara na hekina anazotumia kutatua changamoto mbali za kisiasa na kiuchumi ambazo zimekuwa zikitokea hapa nchini na hata nje ya nchi.
``Mheshimiwa Rais sisi wafanyabiashara hatuna wasiwasi na wewe hata kidogo, kutokana na busara ulizonazo tunaamini utaendelea kutuongoza vizuri na utatuvusha,`` alisema Bw. Mengi ambaye pia ni Mwenyekiti Mtendaji wa IPP.
Mkurugenzi Mkuu wa NBC, ambayo ni mmoja wa wafadhili wa tuzo hiyo, Bw. Christo De Vries, aliipongeza CTI kwa maandalizi mazuri ya utoaji wa tuzo hiyo na aliahidi kuwa benki yake itaendelea kushirikisha na shirikisho hilo.
``Kama Mheshimiwa Rais ulivyosema sekta binafsi ndiyo injini ya ukuaji wa uchumi, injini haiwezi kwenda bila mafuta kwa hiyo mafuta ya injini ni NBC nyote mnakaribishwa kufungua akaunti,`` alisema na kuwafanya wageni waalikwa kuangua kicheko.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Celtel, ambao nao walifadhili utoaji wa tuzo hiyo, Bw. Chirui Walingo, alisema lengo la kampuni hiyo ni kuyafanya maisha ya watanzania kuwa mazuri kwa kuhakikisha mawasiliano yanakuwa mazuri nchini kote.
Alitoa mfano kuwa mteja wa Celtel anaweza kupiga simu akiwa Kenya, Uganda na nchi zingine 15 za Afrika kwa kiwango kile kile cha fedha anachotozwa akiwa hapa nchini.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Utawala ya CTI, Bw. Yogesh Manek, alisema CTI imepokea changamoto zilizotolewa na Rais Kikwete na watazifanyia kazi ili kusaidia jitihada za kuondokana na umaskini.
Alisema watafanya kila linalowezekana kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa hapa nchini zinaongezewa thamani ili wafanyabiashara wapate fedha zaidi.
Mshindi wa jumla alikuwa kampuni ya bia Tanzania TBL.
Makampuni mengine yaliyopatiwa tuzo ya uzalishaji bora ni Allieance Insurance , Alaf Ltd, Simba Plastics Ltd, Shely Pharmaceuticals, 21 Century textiles Ltd, Said Salim Bakhresa and Company, DPI Simba Ltd na Nyanza mine Ltd.