Ilikuwa nyumbani kwa Hamza Mwapachu miezi ya mwanzo ya mwaka wa 1953.
Abdul Sykes akifuatana na Ali Mwinyi Tambwe katibu wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika alikwenda Nansio, Ukerewe kupata kauli ya mwisho ya Hamza kuhusu Julius Nyerere.
Abdul Sykes alitaka kupata kauli ya Hamza Mwapachu kuwa Julius Nyerere aingizwe kwenye uongozi wa juu wa TAA achaguliwe kuwa rais na mwaka unaofuatia 1954 TANU iundwe na Nyerere aongoze harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.
Hamza Mwapachu aliagiza kuwa Nyerere aingizwe kwenye uongozi wa TAA kama rais na mwaka 1954 TANU iundwe na Nyerere aongoze harakati za kudai uhuru.
View attachment 1286371
Kulia Abdulwahid Sykes na Hamza Mwapachu
View attachment 1286304
Ukumbi wa Arnautoglo ulipofanyika uchaguzi wa TAA tarehe 17 April 1953 ambako Nyerere na Abdul Sykes waligombea nafasi ya urais na Nyerere akashinda uchaguzi na kuwa Rais wa TAA na Abdu Sykes Makamu wa Rais
View attachment 1286311
Waasisi wa TANU mwaka wa 1954
View attachment 1286316
Baraza la Wazee wa TANU 1954
View attachment 1286283
Safari ya kwanza ya Julius Nyerere UNO February 1955
Wanachama wa mwanzo wa TANU wakimsindikiza Mwalimu Nyerere uwanja wa ndege.
Kulia ni Bi. Chiku bint Said Kisusa, Bi. Titi Mohamed, kushoto wa kwanza Bi. Tatu bint Mzee
View attachment 1286326
Waliomsindikiza Mwalimu Nyerere safari ya kwanza UNO
Kushoto Rashid Sisso, Robert Makange, Zuberi Mtemvu, Iddi Faiz Mafungo Mratibu wa safari wa Mwalimu Nyerere na Mweka Hazina wa TANU na Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika, Julius Nyerere, John Rupia na Bi. Titi Mohamed
View attachment 1286341
Kulia Ali Msham inaaminika ni katika wazalendo wa mwanzo kufungua tawi la TANU nyumbani kwake Magomeni Mapipa Mtaa wa Jaribu mwaka wa 1954/55 picha hii inamuonyesha akiwa kwenye tawi hilo la TANU siku alipomkaribisha Julius Nyerere tawini kumkabidhi samani kwa ajili ya ofisi kuu ya TANU New Street
View attachment 1286351
Uhuru Kamili 1961
Kulia ni Sheikh Issa Nasir wa Bagamoyo na pembeni yake ni Bi. Mgaya Nyang'ombe mama ya Julius Nyerere, nyuma yao ni Oscar Kambona na upande wa kulia wa Nyerere ni Rajab Diwani
Picha hizi ni chache na majina ya wazalendo waliomo katika picha hizi ni machache pia halikadhalika picha hizi haziwezi kuonyesha yale makubwa ambayo wazalendo hawa walifanya katika kuijenga TANU na kupigania uhuru wa Tanganyika.
Lakini ni nani anawajua wazalendo hawa na yale waliyofanya kuikomboa Tanganyika kutoka makucha ya ukoloni?
CHOZI LA MZEE KIMITI JINSI TANGANYIKA ILIVYOPATA UHURU
“Wakati bendera ya Tanganyika inapandishwa, baba alitoa machozi. Hakuwa na uhakika kama wazungu wakiondoka sisi tungeweza kuendesha nchi.
Baada ya kuona wote waliokuwapo walikuwa wazungu, akasema hawa wanaondoka sisi tutaweza kuendesha nchi?” Hii ni sehemu ya simulizi ya Paul Kimiti; mwanasiasa mkongwe aliyeaminiwa na marais wa awamu zote kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi serikalini.
Kimiti ambaye alizaliwa Januari 15, 1940 mkoani Rukwa, ametumika katika uongozi wakati wa serikali ya awamu ya kwanza baada ya mwaka 1982 Mwalimu Julius Nyerere kumteua kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu. Alianza kufanya kazi chini ya Waziri Mkuu Cleopa Msuya na kisha Edward Sokoine (marehemu). Mwaka 1984 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Mwaka 1989, Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi alimteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera hadi mwaka 1991 alipoteuliwa tena kuwa mkuu wa mkoa wa Mbeya. Macho ya viongozi wakuu wa nchi yaliendelea kumwona Kimiti kwani mwaka 1995, Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa alimteua kuwa Waziri wa Kilimo na mwaka 1998 akamteua kuwa Waziri wa Kazi na Vijana.
Kwa upande wa uwakilishi, mwaka 1980 alikuwa mbunge wa kuteuliwa na mwaka 1995 aliamua kwenda kugombea jimboni alikohudumu vipindi vitatu hadi mwaka 2010 alipotangaza kutogombea tena ubunge wa Sumbawanga Mjini. Serikali ya awamu ya tano pia imeendelea kumtumia mwanasiasa huyu mkongwe.
Oktoba 16 mwaka jana, Rais wa awamu ya tano, John Magufuli alimteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ranchi ya Taifa (NARCO). Kutokana na nyadhifa hizo mbalimbali alizoshika, Kimiti anayo mengi ya kulinganisha na hatimaye kuja na suluhisho kuhusu hatua ambayo nchi imepiga katika hii miaka 58 tangu uhuru. Lakini pia, licha ya kumulika kipindi baada ya uhuru, Kimiti ambaye alipata elimu ya msingi mkoani Rukwa na hatimaye mwaka 1954 kujiunga na shule ya sekondari ya Mzumbe, anazo kumbukumbu juu ya namna Tanganyika ilivyopata uhuru.
Baada ya kuhitimu sekondari, mwaka 1959 akiwa na umri wa miaka 19 aliajiriwa Wizara ya Kilimo kama ofisa kilimo (Extension Officer). Wakati nchi inapata uhuru, alijiunga na chuo cha kilimo Tengeru. Ndiyo maana anakumbuka namna ambavyo kipindi cha Watanganyika kuchukua madaraka kilivyokuwa kigumu kutokana na kutokuwapo watu wengi waliokuwa na ujuzi wa kushika madaraka.
Anakumbuka Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alivyopambana kuandaa watu wa kushika madaraka na wakati huo huo kuwaondolea Watanganyika mawazo ya kudhani kwamba bila wakoloni, nchi isingekwenda. Chozi la babake Kimiti anazungumzia hofu aliyokuwa nayo baba yake, Mzee Petro Kimiti mpaka akajikuta akitoa machozi baada ya bendera ya Waingereza kushushwa na kisha kupandishwa ya Tanganyika. Baba yake alikuwa dereva wa Mkuu wa Wilaya (DC) wa Sumbawanga wakati wa serikali ya kikoloni. Kimiti anasema mzazi wake huyo hakuwa na uhakika kabisa kama Watanganyika wangemudu kuendesha nchi baada ya Waingereza kuondoka.
“Wakati bendera ya Tanganyika inapandishwa, baba alitoa machozi. Hakuwa na uhakika kama wazungu wakiondoka sisi tutaendesha nchi. Baada ya kuona wote waliokuwapo walikuwa wazungu, akasema hawa wanaondoka sisi tutaweza kuendesha nchi,” anasema Kimiti.
Anaendelea kusema, “Baba hakuwa na imani… Wakati walipoanza kuteuliwa wengine, aliona hawafanani na hadhi ya viongozi wa kikoloni. Aliwaona ni waswahili anaowafahamu. Lakini baadaye alizoea akaendelea kuwatumikia hao hao.”
Kwa mujibu wa Kimiti, baba yake alikuwa askari polisi na baadaye ilipendekezwa ajifunze udereva ndipo akawa dereva wa Mkuu wa Wilaya tangu mwaka 1938 hadi 1972 alipostaafu wakati nchi ikiwa huru. Anasema mzazi wake huyo alikuwa dereva wa kwanza katika Sumbawanga nzima na hapakuwa na gari lolote katika eneo hilo zaidi ya alilokuwa akiendesha.
“Hapakuwa na gari lolote Ufipa (Sumbawanga) nzima. Gari la kwanza lililoonekana pale ni la mzee Petro.”
Kutokana na utumishi uliotukuka, mzee huyo aliongezewa muda wa kufanya kazi licha ya umri wa kustaafu kupita. Alikuwa akiendesha gari la wagonjwa la serikali. Mwaka 1954 baba yake alitunukiwa cheti cha utumishi bora uliotukuka kutoka kwa Malkia Elizabeth wa Pili. Alikabidhiwa cheti hicho na Gavana wa Kiingereza nchini Tanganyika, Edward Twining.
Uhuru bila wasomi Akizungumzia ugumu wa kipindi baada ya uhuru ambacho Watanganyika walichukua madaraka, Kimiti anasema ulitokana na kutokuwapo watu wengi waliofunzwa kushika madaraka. Hata hivyo, anasema Mwalimu Nyerere aliteua Watanganyika katika nafasi mbalimbali zilizokuwapo wakati wa ukoloni. Baadhi ya nyadhifa alizibadili majina kuondoa mawazo ya kuhusisha uongozi wa Watanganyika na utawala wa kikoloni.
Anatoa mfano wa nafasi ya Mkuu wa Wilaya (DC) kwamba aliibadili jina ikajulikana kama Area Commissioner. Vile vile wakati wa Tanganyika huru ndipo baadhi ya sare za mavazi ziliondolewa. Mathalani, Mkuu wa Mkoa (Province Commissioner) alivaa kaptula lakini baba wa taifa katika kufuta ukoloni vichwani mwa wananchi, aliwataka wavae kawaida. Vivyo hivyo kwa maofisa kilimo, Kimiti anasema, “tulivaa kaptula lakini baadaye ikabadilishwa.”
Mwanasiasa huyu mkongwe akiwa na umri wa miaka 19, Aprili Mosi, 1959 aliajiriwa kama Bwana Shamba bila kwenda kozi.
“Kipindi hicho tulivaa kaptula, bonge la koti limeandikwa agriculture na kofia. Tulitembea na note book kwa sababu lengo mojawapo ni kuangalia kama wakulima wanafuata masharti waliyopewa katika kilimo.” Baada ya kufanya kazi kwa miaka miwili, mwaka 1961 aliambiwa aende kwenye kozi Chuo cha Tengeru mkoani Arusha.
Anasema wakati wa Tanganyika kujitawala, watu wengi waliendelea kupata mafunzo na chuo walichokuwa wakitumia kilikuwa cha Mzumbe ambako walifundishwa masuala mbalimbali. Akielezea uongozi katika miaka ya awali ya uhuru, Kimiti anasema baadhi ya viongozi waliendesha nchi mithili ya wakoloni (kwa maana ya tabia) wakitaka kuendesha kwa mikiki kama ilivyokuwa wakati wa ukoloni.
Anasema wengi walitumia madaraka vibaya, wakiwaweka watu ndani kwa misingi ya kutaka kuendesha nchi inyooke.
“Mwingine unakutana naye klabu anaagiza mtieni huyu ndani. Kutia watu ndani ilikuwa ni kujenga nidhamu lakini wakatumia madaraka vibaya.”
Endelea kufuatilia mfululizo wa makala za mahojiano na mwanasiasa huyu mkongwe, Paul Kimiti akieleza serikali ilivyompeleka nje ya nchi kusoma; alivyokutana kwa mara ya kwanza na Mwalimu Nyerere na kumkabidhi kitita cha fedha zilizotokana na bendi ya muziki aliyoianzisha ughaibuni.