UTEUZI wa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kumpendekeza Dkt. Willibrod Slaa kuwania urais utezidi kuvuta umma wa Watanzania na hadi jana watu 48,000 walikuwa wamejitokeza kumdhamini katika Wialaya ya Karatu pekee.
Tangu alipoingia katika wilayani Karatu kuomba ridhaa ya wapiga kura wake kwenda kuwania urais, Dkt. Slaa amekuwa kivutio na mikutano yake aliyotumia kuwaaga wananchi ilijaa mashabiki, ambapo wengi walijitokeza kujaza fimu zake kumdhamini na wengine kumchangia fedha kufanikisha harakati zake kwenda Ikulu.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika jana katika viwanja vya Mbulu Mjini, Mwenyekiti wa CHADEMA mkoani Kagera, Bw. Wilfred Lwakatare ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama hicho, alisema idadi hiyo imetokana na watu waliojitokeza kwa siku tatu katika maeneo mbalimbali wilayani humo na wanatarajia idadi kubwa zaidi katika mikoa mingine atakapopeleka fomu hizo.
Katika hatua nyingine, chama hicho leo kinazindua mpango wa Saidia Slaa Ashinde (SASA) katika mkutano utakaofanyika mjini Arusha. Akitangaza mpango huo, Bw. Lwakatare alisema jana kuwa mkakati huo ni maalumu kwa ajili ya kumpeleka Dkt. Slaa Ikulu kuwakomboa Watanzania. "Mabadiliko ya nchi ni SASA, maendeleo ya nchi ni SASA, kumpeleka Slaa ikulu ni SASA," alisema Bw. Lwakatare.
Alifafanua kuwa chama hicho kitatumia SASA kufungua akaunti maalumu kwa ajili ya kuchangisha fedha za kumsaidia mgombe wao.
Akihutubia mkutano wa kuwaaga wapigakura wake wa Jimbo la Karatu juzi katika Uwanja wa Barazani, Kijiji cha Mang'ola, Tarafa ya Eyasi, Dkt. Slaa aliwaomba wananchi wamwombee ili aweze kutimiza kile ambacho Mungu anakusudia kutoka kwake.
Katika mkutano huo ambao pia ulikuwa wa nne katika kusaka wadhamini wa fomu yake ya kuwania urais, Dkt. Slaa alisema: "Kwa desturi za Kiiraq, kijana yeyote akitaka kuoa au kuolewa huja kwa wazazi kuomba baraka zao, nisingeweza kwenda kabla wananchi wangu mlionilea hamjatoa kibali, nilitegemea mtaniokoa lakini nanyi mmekubali niende...niombeeni ili nikafanye kile Mungu anachotaka kufanya kupitia kwangu."
Dk. Slaa aliyekuwa anafafanua jinsi alivyopata wakati mgumu kukubali uteuzi huo wa kuwania madaraka ya juu kabisa nchini, aliongeza: "...Nilikuwa namuomba Mwenyezi Mungu ikiwezekana kikombe hiki kinipite mbali, yanayoendelea moyoni mwangu si rahisi kuwaelezea, ikulu si mahali pa kukimbilia, nayakumbuka maneno ya Mwalimu Nyerere aliyesema kuwa mwogopeni kama ukoma anayekimbilia ikulu.
"Nilipotafakari sana, nilipata jibu kuwa sauti ya watu ni sauti ya Mungu, nilikumbuka Mungu alivyomteua mtu dhaifu sana awavushe watu wake kutoka Misri kwenda nchi ya neema, nikatafakari mimi ni nani hata nikatae kauli ya Mungu kupitia kwa watu.
Dkt. Slaa alisema kuwa siku zote Mungu hawezi kumuacha mtu anayesikiliza ujumbe aliotoa kupitia kwa watu wake, vile vile wananchi hawataweza kumuacha.
Aliongeza kuwa pamoja na kupewa taarifa kisha kuombwa rasmi na Kamati Kuu, bado aliona ipo haja ya kupata ridhaa ya watu wake wa Karatu na ndio maana amekwenda kuomba ridhaa yao.
Alisema sababu zilizomfanya akubali kugombea urais zimezidi kuongezeka kutoka nane za awali, ikiwamo hali ya matabaka inayoongezeka nchini. Alisema amesikia kilio cha Watanzania walio wengi kuwa taifa linakwenda kubaya, limemomonyolewa na viongozi walioko madarakani hadi kusababisha nchi kugawanyika katika matabaka makubwa mawili ya matajairi wakubwa na maskini wa kutupwa.
"Hali hii niliisema bungeni mwaka 2006 nchi inakwenda kubaya, taifa linamomonyoka, linamomonyolewa na viongozi wa CCM na serikali yake, taifa limegawanywa katika matabaka makubwa, nchi inameguka, taifa linateketea, hatutafika miaka 20 taifa litakwisha.
"Wakati ule nilitumia mfano wa mishahara ya wabunge ilivyo mikubwa nikamwambia spika kuwa nchi hii tunayoifurahia inajengwa na wakulima na wafanyakazi lakini hakuna anayewajali, haiwezekani mbunge anayepiga porojo tu amzidi mshahara askari polisi, tofauti hizi ni kubwa iko siku nchi italipuka," alisema Dkt. Slaa.
Akizungumzia suala la mrithi wa Dkt. Slaa katika kuwania ubunge Jimbo la Karatu kwa kupitia tiketi ya CHADEMA, Mwenyekiti wa taifa wa chama hicho, Bw. Freeman Mbowe alisema kuwa wameamua kutumia njia ya maridhiano kumpata.
Akirudia maneno aliyotumia juzi Mjini Karatu, Bw. Mbowe alisema "Tutatumia njia ya political consesus yaani maridhiano ya kisiasa ndani ya chama, kwa sababu tunataka kuepuka mgawanyiko na kuzua makundi ndani ya chama wakati huu, mafisadi wanaweza kutumia njia kuingilia na kutuvuruga hapo.
"Hivyo mkisharidhika ninyi tutakaa ndani ya chama na kuteua jina la mtu mmoja kwa makubaliano ili agombee kiti cha ubunge Karatu na tunawahakikishia kuwa atakuwa chini ya uangalizi wa chama kutoka makao makuu na Dkt. Slaa mwenyewe, msihofu na lazima atashinda na Karatu haiendi CCM," alisema Bw. Mbowe.
Aliongezea kuwa mstakabali wa nchi ya Tanzania na wananchi wake uko mikononi mwa Watanzania wenyewe, ambapo aliwataka kuacha kugombana kwa sababu ya vyama vya siasa bali watafakari mstakabali wa maisha yao na kizazi kijacho.
"Kila mtanzania bila kujali dini yake, rangi wala itikadi ya chama ajadili tumetoka wapi, tuko wapi na tunakwenda wapi. Dkt. Slaa kwa vipimo vyote vya uongozi ndani ya bunge na ndani ya chama anafaa kuwa rais wa nchi hii," alisema Bw. Mbowe.