Kamati ya Richmond yakwamaa kumaliza kazi
* Muda wa kumaliza waisha jana
* Mwakyembe asema hawapati ushirikiano
* Wataka watu wengi wamejitokeza kutoa maoni
* Serikali yasema inasubiri kwa hamu ripoti hiyo
Na Tausi Mbowe
WAKATI muda wa Kamati Teule ya Bunge ya kuchunguza mchakato wa zabuni ya uzalishaji umeme wa kampuni ya Marekani ya Richmond Development (RDC) ukimalizika jana, kamati hiyo imeshindwa kumaliza kazi hiyo.
Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kyela (CCM), Dk Harrison Mwakyembe, ilipewa wiki tatu, kuanzia Novemba 13, mwaka huu kufanya kazi hiyo lakini hadi jana ilikuwa hadi jana ilikua hajamaliza.
Lakini Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Harrison Mwakyembe alimweleza mwandishi wa Mwananchi jana kuwa kamati hiyo imeshindwa kumaliza kazi yake kama ilivyopangwa kutokana na idadi ndogo ya wananchi kujitokeza kutoa ushahidi.
"Watanzania ni wepesi wa kuzungumza na kulaumu. Wengi hawapo tayari kujitokeza kutoa ushahidi. Tumekuwa tukikaa hapa kwa muda mrefu tukisubiri watu waje kutoa ushahidi wao, lakini wanaofika ni wachache," alisema Dk Mwakyembe.
Alisema kamati haiwezi kufanya kazi bila kuwa na ushahidi kutoka kwa wadau mbalimbali utakaowawezesha kutoa mapendekezo sahihi.
Kutokana na hali hiyo, Dk Mwakyembe aliwataka wananchi na waandishi wa habari kujitokeza kwa wingi kutoa ushahidi wao utakaowezesha kamati hiyo kukamilisha kazi yake.
Kamati hiyo iliundwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano na kutangazwa na Spika, Samwel Sitta katika Mkutano wa Tisa wa Bunge, uliofanyika mwezi uliopita mjini Dodoma.
Uamuzi wa kuundwa kwa kamati hiyo, ulitokana na taarifa ya Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Biashara, kutaka iundwe kamati hiyo ili kuondoa utata wa mkataba wa zabuni upatikanaji wa mwekezaji huyo uliotiwa saini kati ya kampuni hiyo na serikali.
Baada ya kuundwa kamati hiyo ilipewa muda wa wiki tatu ambao umemalizika jana na itatakiwa kutoa taarifa katika kikao kijacho cha bunge kinachotarajia kuketi Januari, mwakani.
Kamati hiyo imeundwa baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanya uchunguzi sakata hilo na kutoa taarifa za kuisafisha kampuni hiyo na wahusika katika mkataba wa uzalishaji umeme wa megawati 100 ambao ulipaswa kuingizwa katika gridi ya taifa mwaka 2006 kwa gharama ya Sh172 bilioni.
Mbali na Mwakyembe, wajumbe wengine katika kamati hiyo ni Mhandisi wa Umeme, Stella Manyanya, Habibu Mnyaa kutoka kambi ya upinzani, Lucas Selelii na Hurbet Mtangi.
Mapema akitangaza uamuzi huo, Sitta alisema hadidu za rejea za kamati hiyo ziko sita, mojawapo ikiwa ni kubainisha watu waliokuwamo katika kampuni ya Richmond ya Marekani na kuangalia uwezo wa Richmond katika uzalishaji umeme, kutathimini sheria, miiko na taratibu za mchakato mzima wa zabuni za kampuni hiyo.
Nyingine ni kuangalia mkataba kati ya Richmond na Shirika la Umeme (Tanesco) na kupitia taarifa zote zaidi ya zile za kijanai ambazo zimo katika ripoti ya Takukuru na za Mamlaka ya Zabuni ya Serikali (PPRA).
Miongoni mwa watu maarufu ambao kamati hiyo imeshawahoji hadi kufikia jana ni pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA).
Wengine ni Msajili wa Makampuni na Ofisa kutoka Kampuni ya Usajili katika Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko (BRELA).
Mbali na kamati hiyo Dk Mwakyembe, pia ni mjumbe wa kamati ya kuangalia upya mikataba ya uchimbaji madini nchini, inayoongozwa na Jaji Mark Bomani.
Katika hatua nyingine, Muhib Said anaripoti kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora, Philip Marmo amesema serikali inaisubiri kwa hamu kubwa ripoti ya Kamati Teule ya Bunge ya Kuchunguza mchakato wa zabuni ya uzalishaji wa umeme wa kampuni ya Marekani ya Richmond Development Corporation (RDC) kuona matokeo ya uchunguzi huo kama yataungana na ripoti ya kampuni hiyo au la.
Alisema hayo alipokuwa akijibu moja ya maswali aliyoulizwa na waandishi wa habari jana kwamba, serikali itakuwa tayari kukubaliana na ripoti ya uchunguzi wa kamati hiyo kwa RDC iwapo matokeo ya uchgunguzi huo yatatofautiana na ile ya Takukuru.
Pamoja na mambo mengine ripoti ya Takukuru ilitamka kwamba hakukuwa na utata wowote katika utiaji saini mkataba wa zabuni hiyo kati ya serikali na kampuni hiyo.
Waziri Marmo alisema tayari Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), imeshawalisha ripoti yake ya uchunguzi wa RDC kwa kamati hiyo kwa ajili ya kufanyiwa kazi na kamati hiyo.