Posted Date::2/6/2008
Richmond chanzo cha kupanda bei ya umeme Tanzania
Na Waandishi Wetu
Mwananchi
KUPANDA kwa bei ya umeme kumebainika kuwa, pamoja na sababu nyingine, kumechangiwa na mkataba wa Kampuni Richmond Development Company LLC, iliyopewa kuzalisha umeme wa dharura.
Akiwasilisha taarifa ya Kamati Teule ya Bunge jana, Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge, Dk Harrison Mwakyembe alisema mkataba wa Richmond ni mzigo kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Dk Mwakyembe alisema mzigo huo unabebeshwa na watumiaji hatimaye walipa kodi na kuingiza hasara taifa kwa sababu ina vipengele vinavyoumiza Tanesco.
"Mkataba kati ya Tanesco na Richmond na sasa Dowans Holdings S.A, kama ilivyo mikataba kati ya Tanesco na IPTL, SONGAS, AGGREKO na Alstom Power Rentals, inatoa unafuu usiostahili kwa makampuni hayo ya umeme na kuiumiza Tanesco na hatimaye watumiaji na walipa kodi kimapato," alisema.
Alisema mikataba hiyo ina vipengele vya kuibana Tanesco kulipia kampuni hizo kodi zinazohusika na uendeshaji, matengenezo na marekebisho ya mara kwa mara ya mitambo, gharama za bima, ada za mawakili na washauri elekezi, gharama za mafuta na gesi ya kuendeshea mitambo na gharama za ukodishaji mitambo.
Dk Mwakyembe alisema, Tanesco kila mwezi hulipa sio chini ya wastani wa Sh2 bilioni kwa kila kampuni, izalishe au isizalishe umeme.
Januari 23, mwaka huu Tanesco ilitangaza kupanda kwa gharama za matumizi ya umeme kwa asilimia sita na kati ya 66 na 215 kwa ajili kuunganishi wateja wapya.
Ongezeko hilo lililoanza kutumika Februari Mosi, mwaka huu lililalamikiwa na watumiaji, lakini Tanesco ikidai kuwa gharama za uendeshaji zimepanda bila kuziainisha.
Kulingana na bei ya sasa uniti moja inauzwa kwa Sh40 badala ya Sh38, huku watumiaji wakubwa ikipanda kutoka Sh121 kwa 'unit' hadi Sh128.
Tanesco ilisema imelazimika kuongeza bei ya umeme kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kupanda kwa gharama za uzalishaji, kupanda kwa gharama ya mafuta, mfumko wa bei na ulinganisho wa bei zake na majirani.
Kamati Teule ya Bunge, ilitoa rai kwa serikali mikataba hiyo kupitiwa upya mapema iwezekanavyo kama ilivyofanya kwa ile ya mikataba ya madini.
"Bila kufanya hivyo, mzigo mkubwa wa gharama za umeme utawaelemea wananchi na kushindwa kufikia azma ya serikali ya maisha bora kwa kila Mtanzania," alisema Dk Mwakyembe.
Alisema kutokana na uchunguzi wa kina waliouainisha katika taarifa hiyo, kamati imejiridhisha na inatamka bayana kuwa mchakato wa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura wa MW 100, uliiwezesha Richmond kuteuliwa na baadaye kurithiwa na Dowans Holdings S.A, haukufuata taratibu.
"Uligubikwa na vitendo vya ukiukwaji taratibu, kanuni na sheria za nchi na hivyo kujenga kiwingu cha mashaka ya upendeleo, ubadhirifu na rushwa ambavyo vimechangia kumuongezea mwananchi mzigo wa gharama za umeme," alisema na kuongeza:
"Kamati Teule imethibitisha bila ya shaka lolote kuwa uteuzi wa Kampuni dhaifu kifedha, kiufundi na kiuzoefu na ambayo haina usajili Marekani wala Tanzania kama kampuni yenye ukomo wa hisa, yaani Richmond, ulitokana na kubebwa bila woga wala aibu na viongozi waandamizi wa Serikali".
Alisema kati ya Januari na Oktoba, 2007 Dowans Holdings S.A imewasilisha Tanesco hati za madai kwa malipo ya uwekezaji wa mitambo dola za Marekani 4,373,738.40 na uzalishaji umeme dola 16,487,495.46.
Dk Mwakyembe alisema hadi kufikia Desemba 2007, Dowans Holdings S.A inatamka kwamba Tanesco haijalipa madai yake kuanzia Januari 2007 hadi Novemba 2007, huku Benki ya CRDB Bank ikithibitisha kutofungua Barua ya Dhamana ya Benki nyingine baada ya ile ya awali ya dola za Marekani 30,696,598.
Alisema Novemba 28, 2007 Tanesco ilimwandikia Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini kuhusu mchakato wa kufidia madeni ya gharama za ucheleweshaji wa umeme dola za Marekani 10,000 kwa siku 243 za ucheleweshaji, sawa na dola 2,430,000 na marejesho ya malipo ya awali dola 1,279,026.
Mwakyembe alibainisha kuwa kampuni inatakiwa kulipwa zaidi ya Sh150 milioni kwa siku, hata kama haikuzalisha umeme gharama hizo zinabaki pale pale. Malipo yanaanza rasmi kuanzia Oktoba 4, 2007, siku ambayo uzinduzi wa mitambo ulifanyika.