Waziri aitetea Richmond si ya kigogo
Na Abdallah Bawazir
WAZIRI wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, amesema hakuna kigogo wala mtoto wa kigogo mwenye maslahi katika kampuni ya Richmond iliyopewa jukumu na serikali la kuleta mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura nchini .
Karamagi aliitisha mkutano wa waandishi wa habari jana kutoa maelezo hayo na kufafanua masuala mbalimbali yanayohusiana na kampuni hiyo, pamoja na mikakati ya serikali ya kukabiliana na tatizo la umeme nchini.
"Napenda kuwahakikishia kuwa hakuna kigogo wala mtoto wa kigogo kwenye kampuni ya Richmond," alisema Waziri huyo mwenye dhamana na masuala ya umeme, ambao kwa miezi takriban sita sasa unapatikana kwa mgawo.
Akielezea jinsi kampuni hiyo ilivyopata zabuni ya kuleta mitambo ya kufua megawati 100 za umeme, waziri huyo alisema ilipatikana kwa njia ya zabuni iliyotangazwa duniani kote.
Alisema makampuni manane ya ndani na nje ya nchi yalijitokeza kuwania zabuni hiyo na kampuni hiyo ilifanikiwa kushinda zabuni hiyo kutokana na kutimiza masharti na vigezo vilivyokuwa vimewekwa.
Alivitaja vigezo hivyo kuwa ni unafuu wa bei ya umeme na upatikanaji wa haraka wa vifaa.
Alisema baada ya makampuni hayo kujitokeza, serikali iliunda kamati ya kupitia na kuchambua maombi hayo kwa kila kampuni kabla ya kumtangaza mshindi.
Karamagi alisema katika makampuni yote manane yaliyojitokeza, Richmond ndiyo iliyofikia vigezo hivyo na kupewa zabuni ya kuleta mitambo hiyo.
Aliyataja makampuni mengine yaliyoomba zabuni hiyo na bei zake kwa dola za Marekani kuwa ni Upagum (senti 4.5), Aggreko (senti 6.79), Globalake (senti 5.8), Richmond (senti 4.99), Renko (senti 10), Onetus (dola 1.11), Reo Ernegy ya Kenya na Gapco ya Tanzania.
Alisema kutokana na Richmond kuonekana kuwa na umeme wa bei na nafuu, ilichaguliwa kutoka miongoni mwa makampuni hayo. Alisema wakati ikiomba zabuni hiyo, ilikuwa ikishirikiana na kampuni nyingine kubwa ya kutengeneza injini za ndege, jambo ambalo pia liliisaidia kushinda zabuni hiyo.
Kwa upande mwingine Karamagi alisema kampuni hiyo ya Richmond tayari imeshapata mitambo mingine iliyobaki, yenye uwezo wa kuzalishamegawati 80 za umeme.
Alisema mitambo hiyo imepatikana nchini Afrika Kusini na kwamba kutokana na nchi hiyo kutokuwa mbali sana na Tanzania, inatarajiwa kuwasili nchini wakati wowote kwa ajili ya kufungwa na kuzalisha umeme kabla mwisho wa Desemba.
Hata hivyo, alisema mitambo hiyo inaweza isiletwe yote kwa mkupuo bali kwa awamu, lakini akasisitiza kuwa hadi mwishoni mwa Desemba itakuwa yote imeshawasili na kuanza kuzalisha umeme kama ilivyokusudiwa.
Waziri huyo aliongeza kuwa makampuni yote yaliyopewa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura nchini, yamepewa mikataba ya miaka miwili na baada ya hapo serikali itakuwa imeshajiweka tayari kwa ajili ya kuwa na vyanzo vyake yenyewe vya kuzalisha nishati hiyo.
Pamoja na Richmond, kampuni nyingine iliyopewa zabuni hiyo ya miaka miwili ni ya Aggreko ambayo inazalisha wamegawati 40 za umeme. Kampuni hizo zimepewa mkataba wa miaka miwili, lakini haikuelezwa bayana baada ya muda huo mitambo hiyo itapelekwa wapi.
Akieleza mipango ya muda mrefu ya serikaliya kuwa na mitambo yake yenyewe ya kuzalisha umeme, Karamagi alisema ni pamoja na kununua mitambo aina ya Wartsilla yenye uwezo wa kuzalisha megawati 100.
Alisema mitambo hiyo yenye thamani ya Euro 58.2 milioni itafungwa eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam na hadi kufikia Agosti mwakani itakuwa tayari imeanza kuzalisha umeme.
Alisema mikakati mingine ni kufunga mtambo mwingine aina ya Oret katika eneo la Tegeta ambao utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 45 na kwamba mtambo huo utakuwa tayari kwa matumizi mwishoni mwa mwaka 2007 au mwanzoni mwa 2008.
Alisema pia kuna mkakati wa kuingia mkataba wa kuzalisha umeme wa megawati 200 ambao mitambo yake itajengwa katika awamu tatu, ya kwanza ikianza Julai mwakani kwa kuzalisha megawati 50. Aliongeza kuwa mtambo mwingine wa kuzalisha megawati 100 utafungwa mwishoni mwa mwaka huo na uliobaki wa megawati 50 utafungwa mwanzoni mwa mwaka 2008.
Alisema mitambo yote hiyo itakapofungwa, itakuwa na uwezo wa kuzalisha jumla ya megawati 475 za umeme ambazo zitatosheleza na kumaliza kabisa tatizo la mgao wa umeme nchini.
http://www.mwananchi.co.tz/mwananchisite/Mwananchi/Habari/Habari0.asp